Wednesday 28 July 2010

63 wapigana vikumbo viti maalum wanawake

Na Mwanajuma Abdi
IDADI kubwa wanawake wamejitokeza katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi za wasomi, wafanyakazi, walemavu, ubunge, uwakilishi, kupitia viti vya wanawake katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Katibu wa Mkoa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Asia Juma Khamis aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili jana, katika mkutano mkuu wa UWT Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wa kuwapigia kura wagombea wa CCM wanawake watakaoingia katika vyombo vya kutunga sheria baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu utaofanyika Oktoba 31, ulifanyika Amani mjini hapa.

Alisema wanawake 63 wamejitokeza katika kuwania nafasi hizo ili kuweza kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT kwa kuongeza idadi ya washiriki katika vyombo vya maamuzi na kufikia asilimia 50 iliyoongezwa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Alieleza kwa upande wa viti maalum katika Baraza la Wawakilishi wamejitokeza wagombea 23 kati ya hao watano ndio watakaochaguliwa, Ubunge wamejitokeza 22 ambao nao pia wanatakiwa watano, wasomi watakaoingia katika Baraza la Wawakilishi wamejitokeza watano anahitajika mmoja na msomi mmoja amejitokeza kuingia katika Bunge hivyo hatakuwa ana mpinzani.

Aidha nafasi nyengine zilizojitokeza wagombea ni pamoja na viti vya ulemavu, nafasi za wafanyakazi na muakilishi wa Jumuia za kiraia (NGOs).

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Yussuf Mohammed alisema akinamama katika uchaguzi wa mwaka huu wamehamasika kuchukuwa fomu kwa wingi katika ngazi za udiwani, uwakilishi na ubunge ndani ya viti maalum na majimboni.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kuchagua viongozi wenye sifa ambao watawasaidia kuwatetea wanawake na sio wanaojali maslahi yao.

Mwenyekiti huyo, alitoa wito kwa wagombea watakaoshindwa wasinune wala wasijiweke makundi kwani kufanya hivyo ni athari kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi katika kipindi hiki cha kuelekea chaguzi mkuu.

Nae Makamo Mwenyekiti wa UWT Taifa, Asha Bakar akitoa shukurani kwa Mwenyekiti Yussuf, alimuahidi mkutano huo utafanyika kwa amani na utulivu, sambamba na kuwapata wagombe wake watakaoingia katika vyombo vya maamuzi.

Aidha aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo uchaguzi unapomalizika watu wote warudi wawe wamoja katika kudumisha mashirikiano yao katika kuhakikisha CCM inashinda katika uchaguzi mkuu.

Shamuhuna akifungua mkutano

Naibu Waziri kiongozi na Waziri wa Habari na Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna akifungua mkutano wa UWT Mkoa wa Kaskazini.(Picha na Zanzibar Leo).

Mchakato wa uchaguzi usidhoofishe CCM- Shamuhuna

Na Abdi Shamnah
WAJUMBE wa Mkutano mkuu wa UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, unaowachagua Wawakilishi na Wabunge kupitia viti maalum, wametakiwa kuhakikisha mchakato wa uchaguzi kupitia kura za maoni, hauwagawi na kudhoofisha nguvu za CCM katika kukiletea ushindi chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Changamoto jiyo imetolewa jana na Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na michezo Zanzibar, Ali Juma Shamuhuna wakati alipofungua mkutano huo katika ukumbi wa Chuo cha Amali Mkokotoni.

Shamuhuna amesema CCM imeweka utaratibu maalum wa kuwapata viongozi wake kwa lengo la kukijengea nguvu chama hicho kukabiliana na na mikikimikiki ya vyama vya upinzani katika chaguzi mbali mbali.

Aliwataka wanaoshiriki katika kinyang'anyiro hicho kukubali matokeo yatakayojiri na hatimae kujenga nguvu na ushirikiano wa kukiimarisha chama kiweze kufanya vyema katika uchaguzi ujao.

Alisema Jumuia ya wanawake nchini ina mtandao mpana kwa kuhusisha asilimia kubwa ya wananchi wote, hivyo, aliwataka kuitumia vyema fursa hiyo kuongeza wingi wa viongozi kupitia nafasi mbali mbali.

Alisema mafanikio ya CCM na vyama vilivyotangulia kabla yake yanatokana na umoja na harakati za akinamama,hivyo

aliwataka kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za kuchaguliwa badala ya kungojea nafasi za upendeleo kwani hazitoi tafsiri nzuri ya uwezo walionao.

Katika hatua nyingine, aliwakumbusha wajumbe hao umuhimu wa kushiriki katika kura ya maoni itakayoamua fumo upi umafaa utumike uundwaji wa Serikali baada ya Uhaguzi mkuu.
 
Alisema kuingia katika Serikali ya Umoja wa kitaifa haina maana ya kupoteza uongozi wa Taifa bali ni kujenga ushirikiano na vyama vya upinzani ili kuendesha nchi kwa amani na utulivu.

Alisema ili CCM iweze kupata mafanikio ya kweli ni muhimu kuchagua 'viongozi bora' watakaoweza kutekeleza kikamilifu sera za chama hicho.

Alisema pale wana CCM watakapochagua 'bora viongozi' watakuwa wamechaguwa wasikilizaji tu katika mikutano na kamwe hawatoweza kukitetea chama hicho.

Jumla ay wajumbe watano kutoka nafasi za Uwakilishi na Ubunge wanahitajika kuwakilisha mkoa huo kupitia viti maalum.aikufahamika mara mja wangapi wamejitokeza kuwaia nafasi hizo maalum.

Asiyekuwa na kitambulisho cha kupigia kura hatapiga ya maoni

Na Bakari Mussa, Pemba
Mdhamini wa Tume ya Uchaguzi ZEC, kisiwani Pemba, Ali Moh’d Dadi amesema matayarisho kwajili ya kpigaji wa kura ya Mmoni inayotarajiwa kufanyika tarehe 31 mwezi huu yamekamilika.
 
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko katika Afisi ya Tume ya Uchaguzi Pemba, harakati za matayarisho hayo zilikuwa ni pamoja na lisema matayarisho hayo ni pamoja na kupewa mafunzo kwa watendaji wa ngazi zote kuanzia ngazi ya vituo hadi majimbo.

Alisema Tume imepeleka vifaa vyote vinavyohusika katika ofisi za wilaya kwa ajili ya kura hiyo na inasubiri siku ifike wakamilishe taratibu nyengine ili kuhakikisha uchaguzi huo umekwenda kama ilivyopangwa.
 
Afisa huyo, alieleza kuwa vituo vya kupigia kura vitakuwa wazi kuanzia saa 2.00, asubuhi hadi saa 10.00 jioni , kwa hiyo kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura na kama amejiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kutakiwa kufika mapema kwa ajili ya kutimiza demokrasia ya kupiga kura yake ya maoni.

Aidha , Dadi, amewataka wananchi Kisiwani Pemba, ambao walibahatika kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na bado hawajachukua vitambulisho vyao vya kupigia kura hadi sasa kwenda katika Ofisi zao za Tume ya Uchaguzi za wilaya kwenda kuvichukua kwa haraka.

Alisema kuwa mtu yeyote ambae hajakichukua kitambulisho chake cha kupigia kura akumbuke hatakuwa na haki ya kupiga kura katika kura ya maoni wiki ijayo.
 
"Ni lazima wananchi kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 30/7 mwaka huu kila mmoja awe na kitambulisho chake cha kupigia kura ili apate haki yake hiyo", alisema.

Tuesday 27 July 2010

Moto wasababisha kizaa zaa Darajani, vifaa vya mamilioni vyaangamia

Na Ramadhan Makame
MOTO uliozuka jana majira ya saa 4:30 asubuhi katika eneo la Darajani mjini hapa umeteketeza maduka matatu yaliyosheni bidhaa mbali mbali.

Moto huo uliosababisha msongamano wa watu kwenye eneo hilo la kibiashra hakuathiri maisha ya mtu yeyote mbali ya kuteketeza mali za wafanyabishara zilizokuwemo ndani ya maduka.

Mmoja wa wafanyabiasha ambaye duka lake limeathirika kwenye tukio hilo Mahir Mohammed, alidai chanzo cha mto huo inawezekana kinatokana na mafundi waliokuwa wakifanya matengenezo ya kuchoma 'walding'.
 
Mahir ambaye ni mfanyabishara wa rangi na vifaa vya ujenzi alisema pembeni ya duka lake kulikuwa kukifanywa matengenezo ya kuchoma kwa 'walding' hali iliyosababisha kuzuka kwa moshi mwingi na baadae moto kusambaa kwenye duka hilo na maduka ya jirani.
 
"Sisi tulikuwa dukani kama kawaida yetu ghafla tunauona moshi mwingi na baadae kufuatia moto, walijaribu kuuzima kwa udongo lakini ulishindikana na kusababisha maafa haya",alisema Mahir.

Naye mfanyabishara mwengine katika eneo hilo, Juma Abdulla Hassan alisema chanzo cha moto huo inawezekana matengenenzo ya "welding" yaliyokuwa yakiendelea kwenye duka la jirani.
 
"Tumekaa mara tukasikia mdato mkubwa moshi mwingi na baadae kufuatiwa na moto, tulichofanya ni kujaribu kuokoa mali zilizomoko madukani",alisema mfanyabishara huyo.
 
Naibu Kamishna wa Kikosi za Zimamoto na Uokozi Gora Haji Gora, alisema kikosi chake kiliarifiwa kuzuka kwa moto huo na kilichukua muda mfupi kuwasilisi kwenye eneo hilo.

Alisema kikosi hicho kilifika kwenye eneo hilo huku moto huo ukiwa umeshika kasi kabla ya kuanza kuudhibiti.
 
"Tulijipanga vizuri baada ya kupokea taarifa na ndio maana vijana wangu wamefanikiwa kuudhibiti",alisema Gora.
 
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Abdulla Mwinyi Khamis ambaye alifika kwenye eneo hilo alisisitiza kazi za ufundi wa umeme wapewe mafundi wafanyakazi wa shirika la Umeme (ZECO) na wafanyabishara waweke vifaa maalum vya kuzimia umeme kwenye maeneo yao ya biashara.
 
"Umeme usiungwe kiholela kazi hiyo wapewe mafundi na wafanyabishara wanamali za mamilioni kwenye maduka kwanini hawanunui vifaa vya kuzimia umeme?".
 
Mkuu wa Operesheni kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Hamdan Omar Makame alisema jeshi lake lililazimika kufanya kazi ya ziada kuzuia wale waliokuwa na tamaa ya kukwapua vitu wakati uokozi ukiwendelea.

"Tumechukua nafasi yetu, kwa mazingira kama haya unapaswa uwadhibiti wale wanaowania ngawira badala ya kutoa msaada",alisema Kamishna Hamdan.
 
Kamanada wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Aziz Juma alisema ni mapema mno kutahmini hasara iliyopatikana pamoja na chanzo cha moto huo.
 
"Ndio kwanza tupo kwenye eneo hili siwezi kuwaambia nini chanzo na harasa ipo imepatikana hadi hapo tutakapopitisha uchunguzi",alisema Kamanda Aziz.
 
Katika harakati za uokoza wa mali kwenye maduka hayo pamoja na ulinzi mkali imeripotiwa vibaka nao kuchukua nafasi yao kwa kupora baadhi ya vitu vikiwemo vitambaa.
 
Maduka yaliyoathirika kwenye tukio hilo yanauza bidhaa za vyakula, vitambaa, vifaa vya ujenzi na mapambo.

Vyakula vyaungua moto Darajani

 
Duka linalotoa huduma za vyakula lilioko eneo la Darajani ambalo limeathirika kwa moto.(Picha na Zanzibar Leo).

Kujenga nyumba ya watoto Mazizini kumezingatia ufinyu Forodhani-Mama Shadya

Na Mwanajuma Abdi
MWENYEKITI wa Jumuia ya ZAYEDESA, ambae pia ni Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Shadya Karume amesema kujengwa nyumba ya watoto yatima Mazizini inalenga kuwaekea mazingira mazuri ya makaazi, kutokana na nyumba ya Forodhani kuwa finyu.

Hayo aliyasema jana, wakati akizungumza na Rais wa Jumuiya ya Maendeleo ya Elimu na Upasuaji wa Mishipa ya Kichwa na Mgongo ya Spain, Dk. Jose Piguer, huko Ikulu ya Migombani mjini hapa.
 
Alisema nyumba ya watoto yatima Forodhani ilianza kutumika baada ya Mapinduzi, 1964, ambapo kutokana kuongezeka kwa watoto na kukua kwa shughuli mbali mbali katika Mji Mkongwe wa Zanzibar kumekuwa na ufinyu wa nafasi katika nyumba hiyo, hali iliosababisha ZAYEDESA kujenga nyumba mpya ya kisasa katika eneo la Mazizini.
 
Mama Shadya Karume alimshukuru Dk. Jose kwa kuamua kusaidia vifaa mbali mbali kwa ajili ya nyumba ya watoto yatima ya Mazizini, ambayo ipo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha mambo madogo madogo kwa ajili ya kuhamia watoto wanaoishi katika nyumba ya kulelea watoto Forodhan, ambao wapo chini ya hifadhi ya Serikali.
 
Alifahamisha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuwatunza watoto hao kwa kuwapatia huduma mbali mbali pamoja na elimu, ambapo misaada kama hiyo inasaidia kuongezea nguvu katika kuwapatia makaazi bora watoto yatima wajione kama wanawazazi kamili.

Nae, Dk. Jose Piguer alisema jumuia hiyo licha ya kuwa ya Hispania lakini inafanyakazi zake zaidi Bara la Afrika.

Alisema mbali ya kusaidia huduma za afya lakini hivi sasa imeguswa katika kusaidia watoto yatima wa Zanzibar.

Aidha alimpongeza Mama Shadya Karume kwa kusimamia vizuri Jumuia anayoingoza ya ZAYEDESA, katika kuwasaidia vijana, wanawake katika kuwakomboa na umasikini, sambamba na uhifadhi wa mazingira na kuwajengea nyumba ya kisasa watoto yatima katika kuwapatia makaazi bora.

Zimamoto na Uokozi

Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi wakizima moto kwenye maduka ya darajani. (Picha na Zanzibar Leo). 

Mkaazi Mtemani ajinyonga

Na Zuhra Msabah, Pemba
SIKU saba baada ya tukio la kuinyonga Suleiman Hamad (65), mkaazi wa Wete, kijana mwengine mwenye umri wa miaka 23 mkaazi wa Mtemani naye juzi alijinyonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kaskazini Pemba,Yahya Rashid Bugi alimtaja kijana huyo aliyejiondoshea uhai ni Farouk Ali Mahadhi.

Kamanda Bugi alisema kijana huyo alikutikana keshajitia kitanzi kwa kutumia kamba ya nailoni kwenye mlango wa chumba anachoishi kwenye nyumba za maendeleao Matemani.

Alisema tukio la kujinyonga kwa Farouk liliripotiwa na mwenziwe anayeishi naye nyumba Salum Khamis ambaye baada ya kuukuta mwili wa wake ukining'inia alitoa ripoti ambao walifika kuuchukua mwili ho na kuupeleka hospitali kwa uchunguzi.

"Baada ya upekuzi kwenye chumba cha marehemu tuliikuta sumu ya panya iliyokorogwa ndani ya kikombe ambayo haijawahi kuywewa", alisema kamanda Bugi.

Alisema chanzo cha kujinyonga kwa kujana huyo bado hakijajulikana na uchunguzi umeanza ambapo jana mwili huo ulikabidhiwa kwa jamaa zake kwa mazishi.

Wiki iliyopita katika kijiji cha Selem, mzee Suleiman Hamad alijinyonga kwa kutumia seruni akidaiwa mgonjwa wa akili.

Tunakoa mali isiathirike na moto


Wananchi wakiokoa bidhaa mbali mbali kutoka madukani ili kuzisalimisha na moto uliozuka Darajani.(Picha na Zanzibar Leo).

Saturday 17 July 2010

Nataka Uwakilishi nafasi za Wanawake

Najma Muntaza Giga, akitangaza kuwania nafasi ya viti maalum wanawake katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo. (Picha na Zanzibar Leo).

Natawania Ubunge Mpendae

MUANDISHI Muandamizi wa Shirika la Magazeti ya Serikali, Omar Said Ameir akitangaza nia ya kutaka kuwania Ubunge katika jimbo la Mpendae mbele ya waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo.(Picha na Zanzibar Leo).

Huyu ndo! Dk. Bilal mmemuona

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi akimnadi Dk. Mohamed Gharib Bilal huko Pemba. (Picha na Zanzibar Leo).

Rais Karume awanadi Dk.Shein, Dk. Bilan

Na Bakari Mussa, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya kufanikisha zoezi la upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Alisema mazingira hayo ni pamoja na kutengeneza kadi za kupigia kura za kisasa pamoja na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, ambavyo vina hadhi bora kuliko vya nchi yeyote katika ukanda wa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Dk. Karume aliwataka wananchi wa Zanzibar, kuvitumia vitumbulisho hivyo pale vitakapohitajika ikiwa ni pamoja na Julai 31 mwaka huu, kwenye zoezi la upigaji wa kura ya maoni kuamua juu ya muelekeo mpya wa serikali baada ya uchaguzi mkuu.

Rais Karume aliyasema hayo jana katika Kiwanja cha Gombani Kongwe Chake Chake Pemba, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba, katika hafla ya kumtambulisha mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Ali Mohammed Shein na mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal.

Dk. Karume alifahamisha kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta zote muhimu za kijamii ambapo hilo limewezeshwa kutokana na kuwepo umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari wote.

Aliwataka wananchi kuendeleza kasi hiyo ya mshikamano miongoni mwao iliyooneshwa kwenye awamu ya sita na kwamba maendeleo zaidi yatapatikana kwa kuendelezwa yale yaliyoasisiwa na awamu hiyo.

Dk. Karume aliwataka wananchi wa mikoa miwili ya Pemba na Zanzibar kwa ujumla kuwaunga mkono wagombea CCM, kwani Dk. Shein na Dk. Bilal ni watu mahiri na wenye uwezo wa kuongoza Taifa.



Alisema Uamuzi wa CCM kuwateuwa Wagombea hao ni wa busara, hekima na demokrasia, kwani wote walikuwa wanafaa nafasi walioomba lakini mtu mmoja tu, ndie anaetakiwa, hivyo kila mgombea aliyekuwa na kundi ni vyema na ni lazima kuvunjwa na hatimae kumuunga mkono Dk. Shein kwa lengo la kukipatia Ushindi CCM.

Aidha, Mgombea Urais Zanzibar, kupitia tiketi ya CCM ambae pia ni Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, aliwashukuru wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba,kwa mapokezi yao makubwa waliyoyaonesha kwake na kwa Dk. Bilal kwamba mapokezi hayo yameonesha Ishara ya Upendo kwao na Chama cha Mapinduzi kwa ujumla.

Aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano, miongoni mwao ili kujenga historia yao ya upendo.

Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekitiwa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amefanya mambo mengi makubwa ya maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar, pamoja na changamoto mbali mbali alizokuwa nazo lakini Umoja waliokuwa nao wananchi kwake na Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar inajivunia maendeleo hayo.

“Mafanikio ya maendeleo yalioletwa na Rais Karume, yanaonekana na yanaendelea na yataendelezwa hatua kwa hatua wakati utakapowadia wa kunadi Sera za CCM,” alisema Dk. Shein.

“Rais Amani, amefanya kazi kubwa na isiyo kifani kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar jambo ambalo kila mmoja anafurahia”alieleza mgombea huyo.

Dk. Shein, alimpongeza Rais Karume, kwa kufanya mazungumzo ya maridhiano na Katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, yenye lengo la kuleta umoja na mshikamano ndani ya nchi hii, hivyo alisema mazungumzo hayo yatakuwa endelevu iwapo wananchi watapiga kura ya ndio katika kura ya maoni ifikapo tarehe 31 .7 mwaka huu.

Nae Mgombea mwenza wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alikipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kumlea na kumtunza na kumpa heshima kubwa ya kuwa mgombea mwenza wa Jamhuri ya Muungano jambo ambalo hatalisahau katika maisha yake yote.

Aliendelea kusema kuwa katika mbio za kuwania Urais wa Zanzibar walikuwa wengi na ndio Demokrasia ndani ya CCM, lakini yule alieshinda amechaguliwa na WanaCCM, wenyewe hivyo kama kulikuwa na makundi ndani ya Chama sasa yamekwisha ni kuungana na Dk. Shein, lengo likiwa ni Ushindi ndani ya CCM.

“Bila ya CCM, hakuna maendeleo, hakuna Demokrasia, wala maelewano wala sheria, na yote yaliojitokeza Dodoma ni ya Kisheria na Kidemokrasia” alieleza Dk. Bilal.

Alieleza kuwa uongozi wa Dk. Karume, umefanya mengi mazuri kwa wananchi wa Zanzibar, hivyo Wazanzibari hawana budi kuungana pamoja na kuyaendeleza yale yote ambayo Rais Karume aliyafanya katika uongozi wake huo.

Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kupata kura 99.16% na kuwa Mgombea pekee kwa Chama cha Mapinduzi ili aweze kuendelea kuipeperusha Bendera ya CCM, kwa mara nyengine tena na kuiongoza Tanzania.

Nao WanaCCM na wananchi wa mikoa miwili ya Pemba, katika risala yao wameeleza kuridhishwa na maendeleo makubwa yaliofikiwa Zanzibar chini ya Uongozi wa Rais Karume, na kueleza imani yao kwa Mgombea alieteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar Dk. Shein kuwa na uwezo wa kuyaendeleza maendeleo yaliofikiwa nchini.

Walieleza kuwa hawatasahau maendeleo yaliopatikana katika Uongozi wa awamu ya sita na wataendelea kuyathamini maendeleo hayo ili yawe endelevu kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Maelfu ya wananchi na WanaCCM wa mikoa miwili ya Pemba walihudhuria kwa furaha kubwa katika kuwapokea na kuwaona wagombea wao kuanzia kiwanja cha Ndege cha Karume Pemba, hadi kiwanja cha Gombani ya kale ambapo palifanyika hafla hiyo iliyoambatana na burdani mbali mbali.

Wagombea wetu hawa, mmewaona!


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume akiwatambulisha wagombe wa CCM, Urais wa Zanzibar Ali Mohammed Shein (kushoto), Dk. Mohammed Gharib Bilal.(Picha na Zanzibar Leo).
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume akiwa na wagombe wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein mgombe wa Urais wa Zanzibar na Dk. Mohammed Gharib Bilal mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Picha na Zanzibar Leo).

Viongozi wa dini waelimishe Serikali ya umoja wa kitaifa

Na Ramadhan Makame
ENDAPO wananchi wataridhia kura ya maoni itakayopigwa mwishoni mwa mwezi huu, serikali ya umoja wa kitaifa itakayoundwa itazingatia sera za pamoja zinazojali kuindeleza Zanzibar.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya watu sita ya Baraza la Wawakilishi yenye madhumuni ya kusimamia hoja ya baraza hilo ya kufanyika kwa kura ya maoni, Abubakar Khamis Bakary, aliwaeleza viongozi wa dini kwenye mkutano maalum uliofanyika katika ukumbi wa baraza hilo.

Abubakar ambaye pia ni mkuu wa kambi ya upinzani katika baraza hilo, alisema vyama vya siasa vilivyopo Zanzibar, havitofautiani kwenye sera zao, tofauti yao ni namna ya utekelezaji wa sera hizo kwa maendeleo ya wananchi.

"Sera za CCM na CUF zinafanana na zina lengo moja, nalo ni kuwaletea maendeleo wananchi, kuwapatia amani, ustawi wa maisha yao", alisema Makamo huyo.

Alifahamisha kuwa msingi wa kutekelezwa sera ya pamoja (minimum policy) katika serikali ijayo unatokana na utekelezwaji wa malengo ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.

"Hakuna baya hata moja kwenye malengo ya Mapinduzi, hayo ndiyo yatakayotekelezwa kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoundwa kwa maslahi ya wananchi wetu wote",Makamo huyo aliwaeleza viongozi hao wa dini.

Abubakar, aliwataka viongozi hao kuchukua nafasi yao kwa kuwaelimisha wafuasi wao, juu ya umuhimu wa zoezi hilo na hatima nzuri ya baadae ya Zanzibar na Wazanzibari.

Alisema wajumbe wa baraza hilo, wameridhia kupelekwa suala la kura ya maoni likaamuliwe na wananchi kutokana na uzito wake na umuhimu kushirikishwa wananchi katika maamuzi yanayohusu mustakbali wa taifa lao.

"Sisi wawakilishi tumepitisha azimio kutokana na kuweka maslahi ya taifa mbele, kuondosha mifarakano na migogoro inayojitokeza kila baada ya uhchaguzi".

Aidha alisema serikali itaheshimu matokeo yeyote yatakayotoka kwa wananchi kwenye upigaji wa kura hiyo.

Kwa upande wao viongozi hao wa dini, waliahidi kulifikisha suala hilo kwa waumini wao huku wakitahadharisha juu ya vyombo vya dola kuja kuwatimua kwenye viriri kwa hisia za kuchanganya dini na siasa.

"Ni vyema kwanza mkazungumza na vyombo vya dola, kwa sababu itaonekana haramu kuzungumza dini na siasa na hivyo viongozi wa dini tutaingia kwenye hatia",alisema mmoja wa mashekh aliyehudhuria mkutano huo.

Naye mchungaji wa KKKT, Maloda Shukuru alisema uwepo umakini kwenye uundwaji wa serikali kwani uzoefu unaonyesha kuwa matatizo hujitokeza wakati wa kugawana zile zinazoitwa wizara nyeti.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, sheikh Khalid Mohammed Mrisho aliwataka viongozi wa dini walifikishe jukumu hilo kwa kuwafikishia waumini wao kwani viongozi wa siasa wamelifikisha kwa kuogopa kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Wednesday 14 July 2010

Meli ya Mv Viona iliyofunga gati jana na kushusha makontena 250 ya wafanyabishara wa Zanzibar.

Kamati ya Baraza serikali ya umoja wa kitaifa yaanza kazi

Na Mwanajuma Abdi
KAMATI ya watu sita ya kusimamia utekelezaji wa azimio la Baraza la Wawakilishi kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeanza kazi ya kuwaelimisha wananchi wa Unguja na Pemba juu ya upigaji wa kura ya maoni itayofanyika Julai 31 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ali Mzee Ali, alisema kamati hiyo inawajumuisha watu sita imeanza kazi rasmi kwa kuwaelimisha wananchi kwa kupitia njia mbali mbali ikiwemo kuvitumia ipasavyo vyombo vya habari.

"Kamati imeundwa kwa mujibu wa kifungu namba 11 cha maazimio ya Baraza kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya hoja ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo inawajumuisha wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na CUF akiwemo Makamo Mwenyekiti Abubakar Khamis Bakary (CUF), wajumbe ni Ali Abdalla Ali (CCM), Haji Omar Kheir (CCM), Nasso Ahmed Mazrui (CUF), Zakiya Omar Juma (CUF) na yeye ni Mwenyekiti", alisema Ali Mzee.

Alieleza licha ya kubakia kwa muda mchache wa wiki mbili, lakini kamati hiyo itafanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa umma kuhusiana na suala la kura ya maoni, ambapo alisisitiza kwamba waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuifikisha sauti ya kamati hiyo kwa wananchi.
 
Alifahamisha kuwa, wananchi walio wengi wakiunga mkono juu ya uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kikao cha Baraza la Wawakilishi kitaitishwa mwezi ujao kwa ajili ya mabadiliko ya katiba ya Zanzibar.
 
"Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinatarajiwa kufikia tamati yake Ijumaa, lakini bado wajumbe wake wataendelea kuwa wawakilishi hadi Oktoba 31 siku ya uchaguzi mkuu ndio watapoteza sifa hiyo, hivyo watakuwa na uwezo wa kuitisha kikao cha dharura baada ya kumaliza mkutano wa 20 wa Baraza hilo.
 
Mwenyekiti huyo, alifahamisha kuwa, katika chaguzi mbali mbali zilizofanyika ya vyama vingi vya siasa Zanzibar kuanzia mwaka 1995, mwaka 2000 na mwaka 2005 zilikuwa zikifanyika kwa mazingira ya chuki na uhasama mkubwa ulijengeka wa kisiasa na Chama cha Wananchi (CUF) kilikataa matokeo, sambamba na kuvunjika kwa muafaka.

Alisema muafaka wa kwanza ulikuwa mwaka 1999 chini ya uongozi wa Dk. Salmin Amour haukutekelezwa hata kidogo, muafaka wa pili ulikuwa 2001 chini Dk. Amani Abeid Karume ulitekelezwa kidogo kwa kufanywa marekebisho a katiba ya Zanzibar mwaka 1984 (marekebisho ya nane 2002 na marekebisho ya tisa 2003).
 
Hata hivyo alifafanua kuwa, siasa za chuki na hasama ziliejea na kujitokeza tena katika uchaguzi mkuu wa 2005 na muafaka wa tatu ulifuuka Navemba 2009 baada ya mazungumzo ya Navombe 5, mwaka jana baina ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shaif Hamad.
 
Akimnukuu Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake aliyoitoa Disemba 30, 2005 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alionyesha nia ya dhati ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar unaojitokeza kila mara baada ya uchaguzi mkuu katika kutekeleza azma ake hiyo, kamati ya pamoja ya CCM na CUF iliundwa.
Na Ramadhan Makame
MELI inayomilikiwa na Emirates Shipping Lines, Mv Viona jana ilitia nanga katika bandari ya Malindi na kushusha makontena 250 yenye bidhaa zilizoagiziwa na wafanyabiashara wa Zanzibar.

Mkurugenzi wa Operesheni katika shirika la Bandari, Mohammed Salum 'Shilton', alisema meli hiyo imetokea Dubai na ilitarajiwa kushusha makontena hayo yote kwa siku moja.

Shilton alisema hii ni mara ya kwanza meli ya kampuni ya Emirates Shipping Lines, meli yake kufunga gati katika banadari hiyo, huku akiieleza kuwa meli hiyo ina urefu wa mita 178.

Mkurugenzi huyo alisema meli hiyo imesajiliwa Monrovia nchini Liberia na imekuwa na kawaida ya kuchukua makontena kwenye bandari za Mashariki ya Kati na barani Asia.
 
Aidha alifahamisha kuwa kabla ya meli hiyo kufunga nanga muwakilishi wa Emirates Shipping Lines, alifika kuonana na uongozi wa shirika hilo na kulipongeza kutokana na kuimarisha huduma zake hasa za upakuzi wa makontena.
 
"Muwakilishi wa kampuni hiyo ameridhika na huduma zetu za kushusha makontena zilivyoimarika na kuahidi kuleta meli zaidi kwenye bandari yetu",alisema Shilton.

Alisema upakuaji wa haraka wa makontena uliopo katika Bandari ya Malindi , unatokana na shirika hilo kuwa na vifaa vya kisasa hali inayochangia kuziondoshea meli adha ya kupiga foleni ya kusubiri kufunga gati.

Spika Kificho awaapisha Ferouz, Asha Bakari

Na Halima Abdalla
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho jana aliwaapisha wajumbe wawili wapya wa Baraza la Wawakilishi Asha Bakari Makame na Saleh Ramadhan Ferouz, walioteuliwa juzi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Amani Abeid Karume kuwa wajumbe wa Baraza hilo.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, aliwaapisha wajumbe hao katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, katika hafla iliofanyika barazani hapo mbele ya wajumbe wa baraza hilo.

Aidha Kificho aliwakabidhi wajumbe hao Katiba, kanuni pamoja na sheria No.3 ambayo inahusu haki na kinga ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe hao wameapa kuwa watakuwa waaminifu kwa Zanzibar katika kazi zao za Uwakilishi pamoja na kuitumikia kwa moyo mmoja ,kuhifadhi na kuilinda na kuzitetea kwa dhati katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uteuzi wa wajumbe hao umezingatia Katiba ya Zanzibar kifungu cha 66,ambacho kinampa Mamlaka Rais wa Zanzibar kuteua wajumbe 10 wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar

Miezi michache iliopita, Rais wa Zanzibar aliwateua wajumbe wengine Nassor Ahmed Mazrui na Juma Duni Haji.



Mwenyekiti wa kamati


MWENYEKITI wa kamati ya watu sita ya kusimamia utekelezaji wa azimio la la Baraza la Wawakilishi kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar,Ali Mzee Ali (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa kamati hiyo katika ukumbi wa Baraza hilo jana, kushoto mjumbe wa kamati hiyo Ali Abdalla Ali na Katibu wa Baraza Ibrahim Mzee.(Picha na Abdallah Masangu).

Wizara ya fedha kukusanya 171b/- 2010/2011

Na Halima Abdalla
WIZARA ya Fedha na Uchumi Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2010/2011 inategemea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani yanayokadiriwa kufikia shilingi billioni 171.687.

Misaada ya kibajeti itafikia shilingi bilioni 55.236 na shilingi 211.714 kama misaada ya mikopo kutoka nje kwa ajili ya programu na miradi ya maendeleo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, DK. Mwinyi Haji Makame alipokuwa akiwasilisha bajeti wa Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2010/2011.

Alisema kwa upande wa matumiz, Wizara inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi Billioni 93.616 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.

Aidha, alimesema Wizara ya Fedha na Uchumi itaendelea na majukumu yake ya kusimamia mwenendo wa hali ya Uchumi pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vya ndani na nje ya Nchi ili kudhibiti matumizi ya Serikali.

DK. Mwinyi Haji alisema pia katika kuratibu utekelezaji wa MKUZA na Mkakati wa Ukuzaji Uchumi pia itaimarisha hali ya watenda kazi kiutendaji na kitalamu na kuendelea kusimamia mali za Serikali pamoja na kulipa mafao ya uzeeni kwa wastaafu.

Alisema kwa mwaka 2010/2011 Wizara ya Fedha na Uchumi itasimamia ujenzi unaoendelea wa majengo ya Wizara na Taasisi zake,ikiwemo jengo la Afisi huko Pemba ,Afisi mpya ya ZRB hapo Mazizini,Afisi mpya ya BIMA, Maisara, jengo la Dakhalia, Chuo cha Uongozi wa Chwaka na uwekezaji unaotarajiwa kufanywa na PBZ, ZSSF na Mfuko wa Barabara katika maeneo mbali mbali Zanzibar na Tanzania Bara.

Aidha alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mwaka wa fedha 2010/2011 imepangiwa kukusanya jumla ya shilingi 69.241billioni ambapo Idara ya Forodha imekadiriwa kukusanya 39.5 billioni na Idara ya kodi za ndani inakadiriwa kukusanya 29.7 billioni.

Alisema Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) inakadiriwa kukusanya mapato ya jumla ya shilingi 60.091 billioni sawa na asilimia 95.0ya makadirio ya mwaka.

Alifahamisha kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita 2009/2010 kwa upande wa matumizi Wizara ilipangiwa kutumia jumla shilingi billioni 56.4 zikiwemo shilingi 19.82 billioni kwa kazi za kawaida na shilingi 36.60 billioni kwa kazi za maendeleo .

Aidha alisema Serikali ilichangia jumla ya shilingi 12.89 billioni ambapo ruzuku na misaada kutoka nje iligharimu shilingi bilioni 23.71

Dk. Karume amtumia rambirambi Museveni

Na Rajab Mkasaba Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume amemtumia salam za rambirambi Rais Yoweri Kaguta Museven kufuatia vifo vya zaidi ya watu 70 na wengine 70 kujeruhiwa vilivyotokea nchini Uganda kutokana na shambulio la bomu.

Katika salamu hizo za rambirambi kufuatia vifo hivyo vilivyotokea nchini Uganda. Rais Karume alieleza kuwa kwa niaba yake pamoja na wananchi wa Zanzibar wanaungana pamoja na ndugu zao wa Uganda katika kuomboleza msiba huo mkubwa.

Salamu hizo zilieleza kuwa Rais Karume amepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa hiyo ya vifo na kuwaombea malazi mema wale wote waliopoteza maisha yao na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu kupata nafuu ya haraka kwa wote waliopata majeraha.