Sunday 27 February 2011

Wananchi ndio wenye mamlaka kuamua kuhusu Katiba - Shivji

Wananchi ndio wenye mamlaka kuamua kuhusu Katiba - Shivji

Wazanzibari watakiwa kutodharau mchakato
Na Juma Khamis

WAKATI asasi za kiraia zilizopo Zanzibar nazo zikiungana na za Tanzania Bara katika mijadala ya katiba mpya, Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Shivji ameelezea hofu yake kwamba mchakato wa kupata katiba mpya ya wananchi huenda ukatekwa na wanasiasa.

Akitoa mada “Kwa nini Tunahitaji Katiba mpya Tanzania” katika mjadala wa wazi uliofanyika ukumbi wa Eacrotanal, Profesa Shivji alisema ipo haja kwa jumuiya za kiraia na wananchi wenyewe kushiriki moja kwa moja katika mijadala na kupata mwafaka wa katiba inayozingatia maslahi, utamaduni na silka zao.

Alisema dhana kwamba katiba ni mkataba kati ya viongozi (watawala) na watawaliwa (wananchi) imepitwa na wakati kwa sababu ni wananchi ndio wanaopaswa kuwa na mamlaka ya kuamua jinsi wanavyotaka nchi yao iendeshwe, aina ya mifumo ya uchumi wanaotaka au idadi ya serikali wanazohitaji.

“Katiba zote mbili zinatambua serikali mbili lakini ukiangalia kwa undani utagundua kwamba kuna serikali mbili na nusu,” alisema Profesa Shivji.

Profesa Shivji alisema katiba zote mbili ile ya Tanzania ya mwaka 1979 na ya Zanzibar ya mwaka 1984, zote zimetungwa bila ya kushirikishwa wananchi kwa njia yoyote hivyo hapana budi kwa katiba mpya ijayo kuandikwa kutokana na matakwa ya wananchi wenyewe kwa kushirikishwa moja kwa moja.

Profesa Shivji ambae kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alisema katiba inayowaridhisha wananchi ni ile inayotokana na wananchi wenyewe na wala sio kuamuliwa na kundi la watu wachache.

Kwa upande wake, Wakili maarufu wa Mahakama Kuu Zanzibar, Awadh Ali Said alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kutodharau kushiriki katika mijadala kuhusu katiba waitakayo kwa sababu wao pia ni sehemu ya katiba hiyo hasa kwa vile wakati mwengine wanakuwa waathirika wa katiba hiyo.

Alisema yapo mambo ya msingi yanayojadiliwa na wananchi kwa sasa kama kuwepo kwa mgombea binafsi, haki ya kupinga matokeo ya urais kama ilivyo kwa matokeo ya ubunge pamoja na madaraka makubwa ya kikatiba aliyonayo rais.

Aidha alisema mijadala hiyo ni muhimu kwa Zanzibar, kwani wananchi watapata fursa ya kujadili muundo wa muungano na mambo gani yapunguzwe au yaongezwe kwenye muungano huo.

Akichangia mjadala huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) , Mohammed Dedes pamoja na mambo mengine alisema muda umefika kwa Zanzibar kudai kupewa nafasi kushiriki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama mwanachama kamili ili iweze kulinda maslahi yake kwa kuwa mambo yaliyokubaliwa kwenye ushirikiano wa Jumuiya hiyo,hayamo katika orodha ya mambo ya muungano wa Tanzania.

Mjadala huo muhimu kwa Zanzibar, utaendelea tena Machi 5, ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) Othman Masoud Othman atawasilisha mada “Kuna Migongano kati ya Mapatano ya Muungano na Katiba ya Tanzania.

Machi 19, Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ibrahim Mzee atawasilisha mada “Katiba ya Tanzania na Zanzibar, Changamoto juu ya mianya na utata uliopo.”

Mjadala huo wa wazi umeandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Jumuiya ya Wanasheria Zanzibar (ZLS), Taasisi ya Utafiti wa Bahari ya Hindi (ZIORI) na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA).

Wakulima wa mpunga wasifia maandalizi msimu huu

Wakulima wa mpunga wasifia maandalizi msimu huu

Na Mwantanga Ame

WAKULIMA nchini wamejitayarisha vizuri kwa kilimo cha msimu ujao endapo mvua zitanyesha kwa wakati

Wakulima hao waliyasema hayo wakati Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, alipofanya ziara kuangalia hali ya jua kali na ukame uliosababisha mazao mbali mbali kufa na kilimo cha mpunga kuzorota.

Wakulima wa mabonde ya Kilombero, Muembe Mpunga, Kibokwa na Mchekeni, walieleza kuwa walijiandaa na kufanikiwa kupanda mpunga mapema lakini hali ya kiangazi imesababisha mpunga kufifia na mazao mengine ya kilimo cha juu kufa.

Mkulima Ukasha Abdi Ukasha, akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake alisema mwaka huu maandalizi ya kutayarisha mabonde ya mpunga yalikuwa mazuri ingawa kilimo chenyewe cha mpunga kimezorota kutokana na jua kali.

“Kwa hili tunaishukuru Wizara ya Kilimo, kwa kweli imetulimia kwa wakati na imetuburugia kwa wakati ila tuu mvua ndio imetukimbia lakini kama itakuja hapa tungepata mpunga mwingi usiowahi kutokea miaka yote” alisema mkulima huyo.

Mkulima huyo alisema tatizo kubwa ambalo wanakabiliana nalo hivi sasa ni kukosekana kwa mvua jambo ambalo tayari linawapa mashaka ya kuweza kufikia malengo waliyokusudia.

Waziri wa Wizara ya Kilimo na Misitu, Mansoor Yussuf Himid, alisema hekta 30,000 hadi mwezi huu zilishaburugwa na kupandwa mpunga.

Alisema kati ya hekta hizo kwa upande wa Pemba ni 16,000 na Unguja ni hekta 14, 000 ikiwa ni sawa na asilimia 75 ya malengo.

Wakulima waliahidi kutumia mbolea na pembejeo nyengine ili kwa nia ya kuongeza uzalishaji wa mazao.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Afani Othman Maalim, akizungumzia suala la uzalishaji mpunga, alisema endapo wakulima watatumia fursa ziliopo na kujishajiisha wataweza kuvuka malengo.

Upigaji dawa Kaskazini wafanikiwa

Upigaji dawa Kaskazini wafanikiwa

Na Ismail Mwinyi

MDHAMINI Mkuu wa Kitengo cha Upigaji Dawa ya Malaria Majumbani, wilaya ya Kaskazini ‘B’, Nassor Said Nassor, amesema zoezi la upigaji dawa kwa wilaya hiyo linaendelea vizuri kutokana na wananchi kutoa ushirikiano wa karibu na kitengo hicho.

Alisema kwa vile wananchi wanafahamu umuhimu ya upigaji dawa majumbani kumeweza kuwarahisishia kwa asilimia kubwa kuliendesha vizuri zoezi hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mdhamini huyo, alisema kutokana na ushirikiano walioneshwa na wananchi wa Wilaya hiyo ni kwamba zoezi hilo limekwenda vizuri ambapo shehia 26 kati ya Shehia 29 za Wilaya hiyo ziliweza kupigwa dawa.

Nassor, alieleza kuwa nyumba 10,165 zimefanikiwa kupiga dawa kati ya nyumba 10,370 zilizopo katika Wilaya hiyo.

Alisema kuwa hivi sasa ugonjwa wa Malaria hapa nchini umeweza kupungua kwa asilimia kubwa kutokana na ushirikiano wa karibu uliooneshwa kati ya wananchi na Wizara ya Afya.

Alieleza kuwa pamoja na kufanikiwa kiasi hicho lakini pia walipambana na vikwazo kadhaa ikiwemo visingizio mbali mbali ili nyumba zao zisipigwe dawa.

Alisema kuwa wananchi wengi wao walikuwa wakidang’anya kwa kudai nyumba zao zinawagonjwa hivyo hazifai kupigiwa dawa ya kuua mbu wa Malaria.

“Watu hawataki kupigiwa dawa ndio maana wanadai kuwa wanawagonjwa dani kutokana na taratibu zetu hatuwezi kupiga dawa nyumba hizo kutokana na kuwepo kwa wangonjwa,hicho ndio kisingizio chao kikubwa,”alisema.

Zoezi la upigaji dawa majumbani kupunguza Malaria katika Wilaya ya Kaskazini B, ilianza Januari 24 mwaka huu na limemalizika Februari 26.

Uchafu wasababisha mama ntilie kupigwa 'stop' Malindi

Uchafu wasababisha mama ntilie kupigwa 'stop' Malindi

Na Madina Issa

WAFANYABIASHARA ya chakula katika eneo la Malindi wametakiwa wasitishe mara moja utoaji wa huduma katika eneo hilo na kutafuta sehemu nyengine.

Mkuu wa Idara ya Afya na huduma za jamii katika Baraza la Manispaa Rajab Salum Rajab, alitoa agizo hilo aliopokuwa akizungumza na wafanyabiashara hao huko ofisini kwake.

Alisema biashara ya chakula katika eneo hilo lazima isite kutokana uchafu uliopo ambao unaweza kusababisha kuathirika afya za walaji wa chakula.

Mmoja wa wafanyabiashara hao Halima Ali Faki, aliwaomba Manispaa wawapatie sehemu za kukaa ili waendeleze biashara zao na kujikwamua kimaisha.

Pia alikiri eneo walilokuwepo haliridhishi kwa kuuza biashara zao za chakula lakini wapo hapo kwa ajili ya kujipatia riziki zao za halali na kujisaidia kusomesha watoto wao.

Sambamba na hayo wameiomba Manispaa iwastahamilie kwa kutowaondosha kwani hapo ndipo wanapopata riziki zao na kusema wataliweka eneo hilo safi zaidi.

Mamlaka yaonya waharibifu miundombinu ya maji

Mamlaka yaonya waharibifu miundombinu ya maji

Na Ahmada Ali, MCC

MAMLAKA ya Maji Zanzibar (ZAWA) imesema haitomvumilia mtu yoyote atakaebainika kuharibu miundo mbinu ya maji na kuitia hasara Mamlaka hiyo.

Hayo yalielezwa na Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo Zahor Suleiman Khatib, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika ofisi ya Mamlaka hiyo.

Alisema kumekuwa na uharibifi wa makusudi unaofanywa na baadhi ya wananchi ambao huharibu miundombinu ya maji jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo.

Khatib, alifahamisha kuwa Mamlaka hiyo, imekuwa ikijitahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la ukosefu wa maji tatizo hayo lakini bado imekuwa sugu kwa upande wao kutokana na baadhi ya wananchi kufanya uharibifu makusudi.

Hata hivyo, alisema ukosefu wa huduma ya maji katika mitaa mingi imekuwa ni tatizo linalosababishwa na mabomba ya zamani ambayo yameziba.

Afisa huyo amewataka wananchi hususan wa Makadara kushirikiana na Mamlaka hiyo kutoa taarifa kuhusu watu wanaowafikiria au kuwatambua kushiriki kwenye hujuma za miundombinu ya maji.

WANAFUNZI WATAHADHARISHWA KUEPUKA MIGOMO

Wanafunzi watahadharishwa kuepuka migomo

Na Ligwa Paulin

WANAFUNZI wanaofaulu kujiunga na vyuo vikuu nchini wametakiwa kujiepusha na migomo na maandamano yasiyo na tija na badala yake kujihusisha na kilichowapeleka vyuoni kwa manufaa yao na taifa.

Tahadhari hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki katika sekondari ya Nyuki Mwanakwerekwe na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania Kanali Kidunda Ahmed Mangiri kwenye mahafali ya pili ya kumaliza kidato cha sita skulini hapo.

Alisema baadhi ya Vyuo Vikuu, Tanzania vimekuwa vikikumbwa na migomo au maandamano ambayo kama mwanafunzi hayamsaidii na badala yake yanaweza kusababisha madhara.

Kanali Mangiri ambae pia ni Kamanda wa kikosi cha Jeshi kambi ya Mtoni Unguja, alisema hata kama baadhi ya madai au kero zao ni za msingi lakini njia wanazotumia kuwakilisha matatizo yao sio sahihi.

Alisema wanafunzi hawana budi kudai haki zao kwa kufuata taratibu za chuo husika na kuzingatia sheria za nchi.

Kanali Mangiri ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema anashangazwa na hatua za wanafunzi kama hao ambao wanakuwa na nidhamu wawapo sekondari na nyumbani kwao lakini wabadilike wanapoingia vyuoni.

"Hiyo ni dalili ya kurubuniwa na wenzao wasiolelewa kwa maadili mema majumbani kwao sambamba na sekondari wanazotoka pia wasiowatakia maendeleo mazuri wenzao," alidokeza.

Mapema mkuu wa shule hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania, Meja Khamis Lusuna akimkaribisha mgeni huyo, alisema mahafali ya mwaka huu kuna wahitimu 22 kati yao wananane wanawake, wakati mwaka jana wahitumu walikuwa 30 ambapo 20 kati yao walifaulu kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Cossovo yatinga nusu fainali

 Cossovo yatinga nusu fainali

Na Ismail Mwinyi


TIMU ya Cossovo, imefanikiwa kuingia nusu fainali ya michuano ya ‘Chombo Cup’, kwa kuichapa Love Bite magoli 2-1, katika mchezo wa robo fainali uliochezwa kwenye kiwanja cha Magomeni Jeshini.

Cossovo ilianza kulitia dosari lango la wapinzani wao kwa goli lililofungwa na Haroun Rashid katika dakika ya 20, kabla Amour Vuai kuongeza la pili mnamo dakika ya 54.

Jitihada za Love Bite kukomboa magoli hayo ziliishia kupata bao moja tu la kujifariji, lililotiwa nyavuni na Masoud Mwalim katika dakika ya 67.

Timu za Natural na Ruff Ryder zilitarajiwa kupambana jana katika mchezo mwengine wa robo fainali.

Dole wamwagiwa jezi, mipira

 Dole wamwagiwa jezi, mipira



Na Saada Mamboleo, MCC

MBUNGE na Mwakilishi wa Jimbo la Dole Syllvester Mabumba na Shawana Bukheti Hassan, wamezipa msukumo timu 22 za soka katika wadi ya Mwera, kwa kuzikabidhi jezi na mipira ili kuzipa motisha wa kufanya vyema katika mashindano mbalimbali.

Mipira 44 na seti 22 za jezi zenye thamani ya shilingi 3,438,000 zilitolewa katika hafla iliyofanyika skuli ya Regezamwendo juzi.

Makabidhiano hayo ni miongoni mwa utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Mbunge huyo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.

Akizungumza na wanamichezo wa timu hizo wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mabumba aliwashauri vijana wa jimbo la Dole, kuendeleza utamaduni wa kushiriki michezo mbalimbali na kujiepusha na vitendo viovu.

Aliwapongeza vijana hao kwa kuamua kuanzisha timu za soka, na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha afya zao na kujijengea maisha bora hapo baadae.

Mapema Mwakilishi wa jimbo hilo Shawana Bukhet Hassan, alisema ni lazima michezo isimamiwe kwa hali na mali ili kuijengea Zanzibar mustakbali mzuri kitaifa na kimataifa, na kuzitaka timu hizo kuvitumia vizuri vifaa hivyo ili hatimaye zifike ligi kuu ya Zanzibar.

Mwenyekiti wa michezo wadi ya Mwera Gharib Suleiman Omar, amewashukuru viongozi hao na kusema wamefurahishwa na msaada huo na watautumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mashabiki Gor Mahia wavunja pambano

  Mashabiki Gor Mahia wavunja pambano

NAIROBI, Kenya

VURUGU za mashabiki katika viwanja vya soka zimeendelea kushuhudiwa, kufuatia wapenzi wa klabu ya Gor Mahia kuvamia uwanja wa Nyayo wakishindwa kuvumilia kipigo mikononi mwa Rangers katika ligi kuu ya nchi hiyo mwishoni mwa wiki.

Kutokana na ghasia hizo, muamuzi wa pambano hilo alilazimika kulivunja katika dakika ya 79 ambapo Gor Mahia ilikuwa nyuma kwa magoli 3-0.

Hapo kabla, mashabiki hao walianza kurusha vitu uwanjani zikiwemo chupa na mawe katika robo saa ya mwisho baada ya kuona timu yao ikipokea kipigo kizito, kabla kuvunja uzio na kujitosa uwanjani huku baadhi yao wakiushambulia ubao wa matokeo.

Askari wa Jeshi la Polisi walilazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mashabiki hao.

Muamuzi wa mchezo huo Davis Omweno, hakuwa na njia nyengine bali kuuvunja mpambano huo ambao kabla kitendo cha wapenzi wa Gor Mahia ulikuwa mzuri huku timu zote zikicheza kiungwana.

Mtendaji Mkuu wa Ligi Kuu ya Kenya, amekilaani kitendo hicho na kuahidi kuchukua hatua kali kwa waliohusika. (Nation).



BASKELI YA HAMIS Ma - SMS YATUA KWASHAMUHUNA

 Baiskeli ya 'Hamis Ma-SMS' yatua kwa Shamuhuna

Na Juma Khamis

ZAWADI ya baiskeli katika shindano 'Hamis Ma-SMS' linalochezeshwa na kampuninya simu Zantel, imekwenda kwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati wa Zanzibar Ali Juma Shamuhuna.

Shamuhana alikabidhiwa zawadi yake iliyopokelewa kwa niaba yake, katika hafla ya kuwakabidhi zawadi washindi katika viwanja vya Malindi mjini Zanzibar.

Washindi wengine wa baiskeli ni Nassor Ali, Suleiman Salum, Salum Hamza na Mkubwa Haji, huku Hamida Ali Mwinyigogo akijinyakulia vespa.

Utoaji zawadi hizo, ulikwenda sambamba na hafla ya kuwazawadia washindi wa mbio za baiskeli zilizoandaliwa na kampuni hiyo.

Katika mashindano hayo ya kilomita 120, Juma Lukona aliibuka katika nafasi ya kwanza kwa kutumia muda wa saa 2:37:55, akifuatiwa na Ali Juma aliyeendesha kwa saa 2:39:00 na nafasi ya tatu ikachukuliwa na Khamis Juma aliyetumia saa 2:46:00.

Mashindano hayo yaliyoanzia viwanja vya Malindi kupitia Mshelishelini- Kiwengwa- Matemwe-Mkokotoni-Donge, na kumalizikia Malindi yalishirikisha washindani 20, wakiwemo wanane wa ngazi ya taifa.

VIROJA VYAAZA LIGI KUU MJINI

 Viroja vyaanza ligi Mjini

 Mashabiki, wachezaji wachapana, kanuni zakiukwa
Na Mwajuma Juma

MICHEZO miwili ya ligi daraja la pili Wilaya ya Mjini katika viwanja viwili tafauti, imeshinda kumalizika kwa sababu mbalimbali zikiwemo vurugu za mashabiki.

Pambano lililozikutanisha timu za Dynamo na University katika uwanja wa Amaan B, lilivunjika kabla ya wakati baada ya kutokea vurugu baina ya wachezaji na mashabiki.

Tafrani hiyo ilitokea katika dakika ya 79 ambapo hali ya amani ilitoweka na muamuzi Sunday Nhomba, kuamua kuuvunja mchezo huo, huku University ikiongoza kwa magoli 2-0, yaliyofungwa na Omar Mohammed na Ramadhan Rashid.

Na katika mchezo mwengine uliochezwa uwanja wa Jeshini, timu ya Maji Maji iliyokuwa imepangwa kuivaa Vijana, ilifika uwanjani bila kuwa na leseni za wachezaji, huku karatasi ya majina ya wachezaji wake ikionesha majina tafauti na ya wale waliokuwepo uwanjani.

Hata hivyo, mchezo huo ulichezwa bila Maji Maji kutimiza kanuni hiyo, lakini baada ya dakika 45 za kwanza, muamuzi Shaaban Sadik aliuvunja kutokana na timu hiyo kushindwa kuwasilisha vitu hivyo hata baada ya kupewa muda.

Hadi muamuzi anavunja mchuano huo, matokeo yalikuwa sare ya 1-1, ambapo Vijana lilifungiwa goli lake na Machano Masoud, huku Said Mbwana akipachika lile la Maji Maji.

Kuhusiana na kasoro hizo, Katibu Msaidizi wa ZFA Wilaya ya Mjini Omar Mohammed, alisema hatima za matokeo ya mechi hizo, itajulikana baada ya kupata ripoti za waamuzi na makamisaa.

Matokeo ya mechi nyengine za ligi hiyo mwishoni mwa wiki, yalikuwa FC Roma 4, Mwembenjugu 0, Zainab Bottlers 1, Star Kids 1, Super Sports 3, Magomeni 2, Jang'ombe Boys 2, Dangers 1, Spirit 2, Union Rangers 2.

Aidha Maruhubi iliifunga Kundemba 3-1, Red Stars ikang'ara mbele ya El Hilal kwa ushindi wa magoli 4-1, na Kombora ikairipua Enugu mabao 2-0.

Friday 25 February 2011

Tanzania, UAE kufufua Tume ya Pamoja

Tanzania, UAE kufufua Tume ya Pamoja

Mwandishi Maalum, Dar
Kukutana na ujumbe wa UAE na Balozi wa Brazil

UMOJA wa Falme za Kiarabu (UAE) umesisitiza umuhimu wa kuifufua Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za ukanda huo.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Nchi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu Dk. Reem Ibrahimi Al Hashimy alipokutana na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal, Ikulu jijini Dar es salaam alipokwenda kwa ajili ya kumsalimia.

Dk. Reem alisema kufufuliwa kwa Tume hiyo mapema kutasaidia kukuza na kuendeleza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo kwa vile maeneo ya ushirikiano yatafahamika na kupewa kipaumbele.

“Naamini Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ni chombo muhimu. Tunahitaji kuifufua, mara ya mwisho ilikutana mwaka 1995, ni muda mrefu. Tunahitaji kusaini makubaliano, kama vile makubaliano ya kuzuia ulipaji wa kodi mara mbili kulingana na taratibu za kodi za nchi husika, ni lazima tuwe na Tume ya Pamoja kufanikisha haya,” alisema Waziri huyo.

Akizungumzia uwekezaji Dk. Reem alisema angependa kuorodhesha fursa za uwekezaji zilizoko nchini na kuzichukua kuzipeleka UAE na wale ambao wataonesha nia ya kutaka kuwekeza waweze kuja Tanzania.

Dk. Reem ambaye alikuwa anaongoza ujumbe wa watu wapatao kumi kutoka UAE alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi ambapo alifungua jengo jipya la ubalozi wa UAE.

Katika mazungumzo hayo Dk. Bilal alimhakikishia Waziri huyo kuwa serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa Tume hiyo na kwamba mipango iko katika hatua za mwisho za kusaini makubaliano ya kuifufua Tume hiyo.

Kwa upande wa uwekezaji Makamu wa Rais alisema Tanzania inakaribisha wawekezaji kutoka UAE kuwekeza kwenye sekta mbalimbali hususan za kilimo, madini, miundombinu ya barabara, nishati pamoja na mawasiliano.

Wakati huo huo, Dk. Bilal amekutana pia na Balozi wa Brazil nchini, Carlos Soares Luz ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Brazil yakiwamo ya michezo, nishati, kilimo na ya jamii kwa ujumla.

Wanafunzi Kengeja wahaha kusaka walimu

Wanafunzi Kengeja wahaha kusaka walimu

Radhia Abdalla, Pemba

WANAFUNZI wa Chuo cha Ufundi Kengeja wamefika katika Afisi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Pemba kutaka wapatiwe ufumbuzi wa tatizo la walimu linaloikabili chuo hicho, ambalo wanadai ndio chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa.

Wakizungumza na afisa wa huduma za wanafunzi wa Sekondari, Said Massoud Othman, wanafunzi hao walisema chuo hicho kinakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu hali inayoathiri kwa kiasi kikubwa wanafunzi.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa kidato cha nne, raisi wa skuli hiyo, Ali Kombo alisema tatizo hilo linawakatisha tamaa hasa wakati huu ambapo wanakabiliwa na mitihani ya kitaifa mwishoni mwa mwaka huu

“Tunalazimika kujisomea sisi wenyewe bila ya kuwa na walimu wa uhakika kwani mwalimu mmoja hulazimika kufundisha zaidi ya madarasa matatu kwa siku na masomo matatu kwa kila siku,” alisema.

Alisema hali hiyo inawafanya walimu kutokuwa na umakini wawapo madarasani kutokana na kukosa muda wa kujitayarisha vyema na kupumzika.

Alisema licha yaskuli hiyo kuwa ndio iliyokuwa ikiongoza kwa kupasisha wanafunzi, lakini kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa nipamoja na upungufu wa walimu.

Aliyataja matatizo mengine kuwa ni uhaba wa vitabu, vifaa vya masomo kwa vitendo, uhaba wa madarasa na ufinyu wa mabweni ya kulala wanafunzi.

“Kwa mfano mabweni yaliopo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 56 lakini kwa sasa yanatumiwa na zaidi ya wanafunzi 150,” alifafanua rais huyo.

Akijibu malalamiko ya wanafunzi hao, afisa huyo kutoka wizara ya elimu Pemba, alisema serikali itafanya jitihada ili kuhakikisha kuwa walimu wanapatikana kuondoa tatizo katika kipindi kifupi kijacho.

Hata hivyo, alisema wizara ya elimu iko mbioni ili kuhakikisha chuo cha Ufundi Kengeja kinarudi katika hadhi yake ya zamani kwani ndio tegemeo kwa taifa katika masuala ya ufundi.

Mapema Januari mwaka huu, Waziri Nchi katika Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulahabib Fereji wakati akiweka jiewe la msingi jengo la madarasa manne ya skuli hiyo, aliwaahidi kuyapatia ufumbuzi matatizo mbali likiwemo la mabweni na upungufu wa walimu.

Hakuna mwananchi atakaekufa njaa-Balozi Seif

Hakuna mwananchi atakaekufa njaa-Balozi Seif

 Awataka wakulima kuwa wastahamilivu
Na Mwantanga Ame


HEKTA 50 za mpunga zimeharibika baada ya kukumbwa na kiangazi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hali hiyo imeyaathiri mabonde ya mpunga ya Kilombero, Muembempunga, Kibokwa na Machekechuni.
Mengi ya mabonde yamekauka huku mpunga uliopandwa ukishindwa kustawi huku migomba, mihogo nayo ikiwa imeungua kutokana na kiangazi kinachoendelea.

Akizungumza na wakulima, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, alisema serikali inasikitishwa na hali hiyo na kuwataka wakulima kuwa wastahamilivu wakati huu mvua ya masikika ikitarajiwa kunyesha mapema mwezi ujao.

Balozi Seif alisema serikali itahakikisha hakuna mwananchi ataekufa kwa njaa na itahakikisha wananchi wanapatiwa chakula cha dharura.

Alisema hali hiyo imesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, ambapo tayari athari za aina hiyo zimeonekana kujitokeza kwa upande wa Tanzania Bara na Pemba.

Aidha alisema serikali inajali hasara iliyowapata wakulima katika kutayarisha mashamba yao na itachukua hatua za kuwalimia mashamba yao bure mara mvua zitakapoanza kunyesha.

“Hali sio nzuri inaitia hasara serikali kwani mazao yatachelewa na itatulazimu kununua chakula kutoka nje jambo ambalo litakuwa gumu kwani duniani kumejaa hali ya machafuko, lakini tunakuombeni mstahamili na tuombe mvua inyeshe,” alisema Balozi Seif.

Tatizo la ukosefu wa mvua pia limeonekana kusababisha ukosefu wa uzalishaji wa mazao ya chakula katika wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba.

Maafisa wa Kilimo katika mabonde hayo wamesema hali huenda ikawa mbaya kuweza kupata mazao ikiwa msimu wa masikika utamalizika bila mvua kunyesha.

Hekta ambazo zimelimwa katika bonde la Mayungi ni 50 lakini tayari hekta 10 zimeungua kwa jua huku zilizobakia zikiwa zimeanza kutoa mpunga ambao hautaweza kustawi.

Walisema hali ni mbaya zaidi katika mabonde ya mpunga ya Mkoa wa Kaskazini huku upande wa Kusini ukiwa na hali inayoridhisha kwa baadhi ya mabonde likiwemo Cheju na Mtende ambapo asilimia 47 ya mpunga umeweza kuota vizuri.

Katika Bonde la Kibokwa, hali pia sio nzuri ambapo ekari 6,339 zilichimbwa huku zilizoburugwa ni 5,3505 na zilizolimwa ni ekari 3,600.75 lakini zilizoharibika ni ekari 795.5.

Zanzibar Leo imeshuhudia baadhi ya mito ikiwa imekauka katika mabonde hayo na kuathiri mashamba ya wakulima wa ushirika wa mboga mboga wa Ukweli ni Vitendo.

Mwenyekiti wa ushirika huo, Tatu Khamis alisema mto waliokuwa wakiutegemea kumwagilia kwa sasa umepungua maji.

Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo na Misitu, Afani Othman Maalim, alisema Wizara yake imeunda Kamati maalum kwa ajili ya kufuatailia suala hilo na huenda wiki ijayo ikawa na ripoti kamili juu ya kiasi gani cha athari kilichotokea.

Alisema maeneo ambayo Kamati hiyo inayaangalia ni pamoja na kutathmini maeneo ambayo yatahitaji kuburugwa tena, na athari zilizowapata wakulima ili kuona vipi serikali itaweza kuwasaidia.

13bn/ kuimarisha kilimo, mifugo Z’bar

13bn/ kuimarisha kilimo, mifugo Z’bar



Na Mwanajuma Abdi


ZAIDI ya dola za Marekani milioni tisa sawa na shilingi bilioni 13.391 zitatumika katika mradi wa kuimarisha na kuendeleza huduma za kilimo na mifugo ASSP/ASDP-L Zanzibar ili kusaidia kupambana na umasikini na kuwepo uhakika wa chakula.

Hayo yalifahamika jana, wakati Mratibu wa Mradi Zaki Khamis Juma alipokuwa akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa programu za ASSP/ASDP-L kwa mwaka 2010 katika mkutamo wa kutathmini utekelezaji wa miradi hiyo kwa wadau wa kilimo na mifugo, uliofanyika Maruhubi mjini hapa.

Alisema miradi hiyo imeanzishwa mwaka 2007, ambapo lengo lake ni kupunguza umasikini na kuwepo kwa uhakika wa chakula na kuongeza kipato kwa jamii zinazotegemea kilimo.

Mradi wa ASSP, utatumia dola za Marekani milioni 5.9777, ambao utarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka 2014, wakati mradi wa ASDP-L, utagharimu dola za Marekani milioni 3.76, na utakamilika 2015.

Alieleza miradi hiyo imekusudia kuwanyanyua wakulima wakiwemo wanawake na masikini wa vijijini kwa kuwawezesha kitaaluma ili kuzitumia teknolojia za kilimo zitazochangia kutosheleza chakula na kipato.

Aidha alitoa wito kwa watu binafsi wenye uwezo kuwekeza katika kilimo badala ya kuwekeza katika maduka na vituo vya mafuta, kwani kufanya hivyo kutasidia kukuza uchumi kupitia sekta hiyo.

Nae Katibu wa Baraza la Wakulima Mkoa wa Kusini Unguja, Mashavu Juma, alisema changamoto kubwa zinazowakabili ni wizi wa mazao na mifugo ambazo bado ni matatizo sugu katika wilaya hususan wanyama kama ng’ombe.

Alieleza changamoto nyengine ni uhaba wa maji na malisho kwa wafugaji na wakulima, wanyama waharibifu kama kima na vifo vya kuku.

Mapema akifungua mkutano huo wa siku moja Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Uendeshaji wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, Asha Ali Ameir, alisema Serikali katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara imeandaa mipango na mikakati mbali mbali yenye lengo la kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi.

Mipango hiyo inalengo la kufikia malengo ya millennia ya Umoja wa Mataifa, Dira ya Maendeleo ya 2020 na Mpango Mkuu wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) ambayo dhamira kuu ni kumoundoa mkulima kutoka katika uzalishaji duni na kuelekea katika uzalishaji wenye tija.

Kuna vikundi 360 vinavyowakilisha kaya 6,675 katika wilaya tisa Unguja na Pemba, ambavyo vimepatiwa mafunzo katika skuli za wakulima.

Wednesday 23 February 2011

Kasi ya maendeleo ya kilimo Z’bar yawaridhisha wafadhili

Kasi ya maendeleo ya kilimo Z’bar yawaridhisha wafadhili


Na Juma Mohammed, Maelezo

SHIRIKA la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa(FAO) limeridhishwa na kasi ya maendeleo ya kilimo visiwani Zanzibar na umakini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza na uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, Mwakilishi Mkazi wa FAO, Louise Setshwaelo amesema hajaona Serikali inayokwenda kwa kasi kama SMZ katika kuendeleza kilimo na wakulima.

“FAO imefurahishwa sana na Zanzibar…sijaona Serikali inayokwenda kwa kasi kama hii ya SMZ, kama nitaondoka leo basi nitajivunia mafanikio hayo, inatia moyo sana na hongereni” Alisema Louise.

Mwakilishi Mkazi huyo alisema umakini wa Wizara ya Kilimo na Maliasili katika kuendeleza sekta ya kilimo ni wa kupigiwa mfano hasa katika kuwajengea uwezo wakulima katika utafutaji wa masoko na uzalishaji bora wenye kuzingatia maelekezo ya watalaam wa kilimo.

Alisema FAO itatoa kila aina ya msukomo kuisaidia Zanzibar kufikia malengo yake ikiwa pamoja na kushawishi Washirika wa maendeleo kuendelea kuisaidia hasa katika uhakika wa chakula na lishe.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yussuf Himid alisema Serikali itawasilisha katika Baraza la Wawakilishi mswada wa sheria wa uhakika wa chakula na lishe katika kikao kijacho cha Aprili.

“SMZ imejiandaa kuhakikisha wakulima wananufaika na kukifanya kilimo kuwa kimbilio la vijana wetu… mipango madhubuti imeshawekwa ili kilimo kiwe na tija kwa wakulima wetu na ndio maana Rais wetu, Mheshimiwa Dk. Ali Mohammed Shein mara kwa mara amesisitiza suala la kilimo bora,” alisema Waziri Mansoor.

Waziri huyo alisema uhakika wa chakula na lishe bora ni jambo linalopewa umuhimu wa juu na ndio maana Serikali itawasilisha mswada wa sheria ambapo pia katika sheria hiyo imependekezwa kuwepo kwa ghala la Taifa la akiba ya chakuka Zanzibar.

Alisema kwa sasa hali ya chakula Zanzibar sio nzuri kwani umaskini wa chakula kwa wananchi ni asilimia 13. “hapa kwetu umasikini wa chakula umefikia asilimia 13, Wizara yangu imejikita kuhakikisha tutaondoka katika hali hiyo,” Aliongeza Waziri huyo.

Waziri Mansoor alisema mpango mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza kasi ya uzalishaji ili sehemu kubwa ya chakula kizalishwe hapa nchini na kupunguza uagiziaji.

Alisema mabadiliko ya tabia ya nchi yanaiathiri Zanzibar ambapo kikawaida mvua za kupandia zinanyeshe kati ya mwezi Disemba hadi Machi,lakini hadi wakati huu licha ya wakulima kuburuga mashamba yao,hakuna mvua iliyonyesha.

Alisema katika hali kama hiyo, mkakati zaidi unahitajika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uhakika wa chakula, hivyo Serikali inaendelea kubuni mbinu mbalimbali kukabiliana na hali hiyo.

Waziri Mansoor alisema Serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya kilimo inaendelea kuwa tegemeo la kuinua uchumi na kuimarisha hali za wananchi kuwa bora zaidi, kuishi katika makazi yaliyo bora na kupunguza umaskini.

Mama Mwanamwema asifu kinamama kwa kuichagua CCM

Mama Mwanamwema asifu kinamama kwa kuichagua CCM


Na Mwanajuma Abdi

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein amesema ushindi wa CCM umetokana na ridhaa ya wananchi waliyokikubali chama hicho ili kiwaletee maendeleo.

Hayo aliyasema jana Kilimahewa bondeni, wakati alipokwenda kuwapongeza wananchi na wanaCCM waliokipigia kura chama hicho na kuwawezesha Rais Shein, wabunge, wawakilishi na madiwani kushinda katika uchaguzi uliopita.

Alisema ushindi huo umetokana na ridhaa ya wananchi kukikubali chama hicho kwa kimefanya mambo makubwa ya maendeleo nchini chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzia awamu ya kwanza.

Mama Mwanamwema aliwahimiza akinamama na akinababa kwamba uchaguzi umekwisha kwa salama na amani na kilichosalia hivi sasa ni kuchapa kazi kwa bidii kwa lengo la kujiletea maendeleo katika sekta za biashara, kilimo na ufugaji.

Aidha alihimiza umoja, mshikamano, utulivu na amani iliyopo nchini iendelee kuwepo, kwa sababu ya kupatikana maendeleo ya haraka, kwani bila ya hayo nchi haiwezi kupiga hatua za haraka za kiuchumi.

Nae Mke wa Makamu wa pili wa Rais, Mama Asha Seif Ali Iddi, aliweka mkazo kwa akinamama kuendeleza kampeni za kukiletea ushindi chama hicho, kwa vile wao wanaushawishi mkubwa katika jamii.

Risala ya wananchi wa Shehia ya Kilimahewa Bondeni, ilisema kwamba walijitokeza kwa wingi katika uchaguzi uliopita, jambo ambalo limesaidia Chama hicho kushinda.

Ongezeko la baa lachangia utumiaji dawa za kulevya

Ongezeko la baa lachangia utumiaji dawa za kulevya

Na Mwanajuma Abdi

WANANCHI wa vijiji vya Paje, Bwejuu, Muyuni na Makunduchi wamesema kuzagaa kwa baa mitaani kunachangia ongezeko la watumiaji wa dawa za kulevya na kuchangia maambukizi ya mapya ya UKIMWI.

Kauli hizo walizitoa jana, katika majadiliano ya pamoja yaliyoandaliwa na Jumuiya ya ZAYEDESA chini ya ufadhili wa Shirika la ICAP na CDC kupitia watu wa Marekani, yaliyofanyika katika skuli ya Paje Mkoa wa Kusini Unguja, yaliyowashirikisha masheha, walimu na maofisa wa Wilaya na waelimishaji rika.

Walisema katika vijiji hivyo, kuna baadhi ya baa zinachangia kuharibu maadili ya vijana kutokana na kujaa ushawishi wa utumiaji dawa za kulevya, jambo ambalo linalolitilia nguvui uwezekano wa maambukizi mapya

Baadhi ya baa katika kijiji hicho zimejenga tabia ya kingza magari yakiwa na wanawake wanaodaiwa kuwa na mavazi nusu uchi

Katibu wa Sheha wa Michamvi, Abeid Juuyahaji, alishauri Serikali kutofumbia macho baa zilizoibuka kiholela, ambazo hazimo katika mahoteli makubwa ya kitalii ziondoshwe katika ukanda huo.

Alisema wananchi wamejaribu kuchukua hatua kadha kutaka kuziondosha lakini wamiliki wake huwatisha wananchi kwa jeuri zao za fedha.

Mwananchi mwengine wa kijiji hicho, Issa Juma alishauri maduka yanayokodisha kanda yawe yakikaguliwa ili kuepusha kukodishwa vijana filamu zinazokiuka maadili na mila za kizanzibari kwani kufanya hivyo kutapunguza matatizo ya UKIMWI na dawa za kulevya kwa vile kuna baaadhi ya michezo inachangia.

Naye Mwalimu Salama Jecha Zidi, aliwashauri wazazi washirikiane katika kupiga vita masuala hayo, ambapo kama katika kijiji wapo vijana watatu au sita wawekee mikatati ya kuwabadilisha tabia, wanaweza kubadilika katika kipindi kifupi.

Mapema Sihaba Saadat kutoka Tume ya UKIMWI Zanzibar alisema kundi kubwa la watumiaji wa dawa za kulevya ni vijana, ambapo waathirika wakuu ni wanaume, na kwa maradhi ya UKIMWI waathirika wakubwa ni wanawake kulingana na hali ya maumbile.

Akifungua mjadala huo, Katibu wa ZAYEDESA, Lucy Majaliwa alisema mjadala huo unalengo la kuwasaidia vijana waliojitumbukiza katika matatizo hayo kutafuta njia za kuweza kuwaokoa na janga hilo.

FAMILIA 10 MIKUNGUNI ZAKUMBWA NA MARADHI YA KUHARISHA.

Familia 10 Mikunguni zakumbwa na maradhi ya kuharisha


Na Mwandishi wetu

WATU kutoka zaidi ya familia 10 katika Shehia ya Mikunguni, wamekumbwa na maradhi ya kuharisha baada ya kutumia maji yasiyo salama yanayosadikiwa kuchanganyika na kinyesi cha binadamu.

Tatizo hilo limewakumba zaidi watoto baada ya kutumia maji hayo yaliyokuwa na ladha ya uchungu pamoja na rangi ya udongo.

Katika taarifa yake kwa Zanzibar Leo, Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), imesema hali hiyo imesababishwa na mwananchi mmoja katika eneo hilo kujenga shimo la karo na kusababisha kinyesi kuchanganyika na maji safi baada ya bomba la maji la chini ya ardhi kupasuka kwa kemikali za kinyesi.

Afisa Uhusiano wa ZAWA, Zahor Suleiman alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Mamlaka lichukua hatua ya kufunga laini ya maji katika eneo hilo na kubadilisha mfumo mzima wa usambazaji maji ili yasipite kwenye karo hilo.

Mabadiliko hayo, yamesababisha wananchi wa shehia hiyo kukosa huduma za maji na kusababisha usumbufu mkubwa, hata hivyo hatua hiyo imechukuliwa ili kunusuru maisha ya wananchi na kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wote.

Shehia ya Mikunguni kwa muda mrefu imekuwa ikikosa huduma za maji safi kutokana na uchakavu wa miundombinu, lakini wakati ZAWA ikiweka laini mpya baada ya siku tatu tu hali ya maji ilibadilika na kuwa na ladha ya uchungu.

WALIMU 3,000 MAANDALIZI KUPATIWA MAFUNZO.

Walimu 3,000 maandalizi kupatiwa mafunzo

Juma Khamis

KIASI cha walimu 3,000 wa maandalizi Unguja na Pemba watapatiwa mafunzo ya kujifunza kwa njia ya redio na video kupitia mradi wa ZTUR.

Mafunzo hayo yatawasaidia walimu wa maandalizi kuweza kubuni njia mpya za kuwafundisha wanafunzi ikiwa ni njia moya ya kuimarisha kiwango chao cha ufahamu na kupiga jeki maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya programu zilizotayarishwa na ZTUR, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ramadhan Abdulla Shaaban, alisema mradi wa ZTUR umeweka mazingira mazuri yatakayompa mwalimu mbinu tafauti za kutayarisha vipindi kwa vitendo vitakavyochangamsha ubongo wa mtoto na kuongeza ari ya kujifunza zaidi.

Aidha alisema mradi huo umekuja wakati muafaka kwa kuasaidia azma ya serikali ya kutekeleza sera ya elimu ya mwaka 2006 ambayo inawataka watoto wote walio na umri wa miaka minne kuanza skuli za maandalizi kabla ya kujiunga na skuli za msingi.

Alisema mafunzo hayo kwa walimu yatatolea kwa kusikiliza redio na kufanya mazoezi pamoja na semina katika vituo vya walimu na yanatarajiwa kuchukua muda wa hadi miaka miaka miwili na nusu, ambapo wahitimu watatunukiwa vyeti baada ya kumaliza mafunzo.

Mapema afisa kutoka Serikali ya Marekani, Robert Scott alisema mradi wa ZTUR umepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa na umekidhi malengo ya kuanzishwa kwake kwa kuzalisha wakufunzi ambao wataweza kuwasomesha walimu wengine wa skuli za maandalizi.

Mradi wa ZTUR umesaidia kutayarisha mafunzo ya walimu kwa njia ya elimu kwa redio na video na njia hii inatarajiwa kuwafikia walimu wengi zaidi katika kipindi kifupi.

Pia mradi wa ZTUR umetayarisha vipindi 20 vya redio vya Chezesha Ufundishe vinavyojumuisha Kiswahili, hesababu pamoja na sayansi, ambapo walimu wa maandalizi watasikiliza vipindi hivyo kupata mbinu za ufundishaji na wakati huo huo wakitayarisha masomo ya kufundisha watoto katika skuli zao.

Aidha ZTUR imetayarisha vitabu mbali mbali vya muongozo ambavyo vimepelekwa skuli zote za Unguja na Pemba na vituo vya walimu, ambapo kiasia cha vitabu 6,000 vimechapishwa, ambapo skuli zote zinaweza kusikiliza vipindi vya redio vya Chezesha Ufundishe na Tucheze Tujifunze kwa kutumia redio.

Mradi ya ZTUR uneandeshwa chini ya ufadhili wa Shirika ka Misaada la Marekani (USAID), Serikali pamoja na Shirika la Elimu la EDC.

CHOMBO CUP YAINGIA ROBO FAINALI

 Chombo Cup yaingia robo fainali

Na Ismail Mwinyi


KATIKA mashindano ya kuwania ‘Chombo Cup’ yanayoendelea kwenye uwanja wa Magomeni jeshini, timu ya Mbendembe imejipatia ushindi wa bure baada ya Monaco kushindwa kutia mguu uwanjani.

Kutokana na hali hiyo, Mbendembe imefuzu kuingia robo fainali na kuvaana na Msimbazi katika mchezo wa kusaka nusu fainali.

Mchezo huo ndio utakaofungua pazia la robo fainali itakayochezwa leo saa 10:30 jioni uwanjani hapo.

Timu itakayoibuka bingwa wa ngarambe hizo, itazawadiwa mbuzi na mipira mitatu, huku itakayoshika nafasi ya pili ikifarijiwa kwa zawadi ya mipira mitatu.

Michuano hiyo imeandaliwa na kufadhiliwa na Mbunge wa jimbo la Magomeni Amour Chombo.

FAINAL ZA KOMBE LA CHAN SUDAN.

WAANDAAJI wa mashindano ya soka kwa mataifa ya Afrika yanayohusisha wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) timu ya Sudan, wametupwa nje na Angola katika mchezo wa nusu fainali juzi.


Angola ilishinda kwa penelti 4-2 kwa mikwaju ya penelti baada ya miamba hiyo kumaliza dakia 120 ikitoka sare ya 1-1, katika mchezo uliokumbwa na vituko vya mashabiki wa Sudan waliokuwa wakirusha chupa uwanjani.

Sudan ilikuwa ya kwanza kuandika bao kupitia kwa mchezaji wake Saifeldin Ali Idris mwishoni mwa kipindi cha kwanza, kabla Angola kusawazisha katika dakika ya 70 kwa goli lililofungwa na Arsenio Cabungula.

Licha ya kuanza dakika 30 za nyongeza kwa kasi na mashambulizi ya mfululizo, Sudan ilijikuta ikicheza pungufu pale nahodha wake alipooneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kichwa mchezaji mmoja wa Angola na kumrushia ngumi mwengine.

Hata hivyo hakuna timu iliyoweza kuziona nyavu katika muda huo wa ziada, na kulazimisha mchezo huo uamuliwe kwa mikwaju ya penelti.

Nayo Tunisia imefauikiwa kutinga fainali baada ya kuwabwaga majirani zao Algeria kwa penelti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo mwengine wa nusu fainali.

Kwa matokeo hayo, mchezo wa fainali utazikutanisha Tunisia na Angola kesho, wakati wenyeji Sudan na Algeria watatangulia kucheza mechi ya kusaka mshindi wa tatu

PBZ YALIPIGA TAFU BONAZA LA WANAHABARI

 PBZ yalipiga ‘tafu’ Bonanza la wanahabari

Na Mwantanga Ame


UONGOZI wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, umepokea msaada wa fulana maalumu kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar kwa ajili ya kufaniksha Bonanza la kimichezo litakalojumuisha wafanyakazi wa vyombo vya habari hapa nchini.

Katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika jana kwenye Makao Makuu ya benki hiyo Darajani, Mkurugenzi wa benki hiyo Juma Amour alisema taasisi yake itaendelea kutoa misaada kwa huduma za kijamii ikiwemo michezo kwa kuthamini mchango wa wananchi katika kuimarisha huduma za benki hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema, benki hiyo ni ya wananchi wa Zanzibar na ili huduma zake ziimarike, misaada yake kwa jamii ni muhimu na pia ni sehemu ya kujitangaza kibiashara.

Aidha alifahamisha kuwa msaada wa PBZ kwa ajili ya Bonanza unalenga kuthamini mchango wa vyombo vya habari katika kuipatia taaluma jamii juu ya mambo mbali mbali.

Mkurugenzi huyo aliahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari ikiwa ni hatua itayokuza uhusiano kati yao na jamii.

Naye Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Abdallah Mohammed Juma, akitoa shukrani, alisema msaada wa benki hiyo ni faraja kwa taasisi yake, na kwamba kukubali kudhamini Bonanza hilo kutasaidia kuleta ufanisi.

Alisema Shirika lake litahakikisha ushirikiano ulioanzishwa ambao umeonesha wazi nia njema ya kujenga uhusiano, unadumishwa kwa manufaa ya taasisi yake na zile za kifedha.

Bonanza hilo linalohusisha aina mbalimbali za michezo na burudani, limepangwa kufanyika Februari 26, mwaka huu katika viwanja vya Maisara ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis.

DENI LA MUNDU LAIKAANGA ZFA

Deni la Mundu laikaanga ZFA

 Latumiwa kumkacha mjumbe wake safari ya Z’bar Ocean
Na Salum Vuai, Maelezo

KATIKA hali isiyotarajiwa, timu ya Zanzibar Ocean View iliondoka jana kwenda DR Congo kurudiana na klabu ya AS Vita bila kuambatana na mjumbe wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).

Mwandishi wetu alishuhudia kikosi cha wachezaji 16 na viongozi wanne wa timu hiyo kikiingia uwanjani kwa ajili ya kupanda ndege ya Shirika la Kenya Airways bila mjumbe wa chama hicho.

Kwa kawaida mjumbe wa ZFA anapaswa kufuatana na msafara wa klabu inayoiwakilisha nchi kwenye michuano ya klabu barani Afrika, ili iwapo kutatokezea tatizo lolote aweze kulishughulikia.

Baada ya jitihada za kumpata Msaidizi Katibu wa ZFA Masoud Attai kushindikana kwa kuwa simu zake mbili zilikuwa zimezimwa kwa muda mwingi, Mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho Mussa Soraga, alisema kuondoka bila mjumbe wa ZFA ni kosa kwa mujibu wa kanuni.

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini sababu iliyoifanya Zanzibar Ocean isichukue mjumbe wa chama hicho katika safari yake, ni kutolipwa deni la shilingi 5,000,000 inaloidai ZFA.

Imefahamika kuwa wakati klabu ya Mundu iliyokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la CAF iliposhindwa kulipia hoteli iliyofikia timu ya Red Arrows ya Zambia mwaka juzi mjini Dar es Salaam, deni hilo lililipwa na hoteli ya Zanzibar Ocean View huku ZFA ikibeba dhamana ya kurejesha fedha hizo.

Barua iliyotumwa kwa chama hicho ambayo Katibu Mkuu wa Zanzibar Ocean View aliionesha Zanzibar Leo nakala yake, ilieleza kuwa, ili mjumbe wa ZFA aweze kusafiri, chama hicho kimeruhusiwa kitoe dola 1,000 katika deni inalodaiwa, kwa ajili ya kumnunulia tiketi mjumbe wake.

Kupitia barua hiyo, uongozi wa Zanzibar Ocean ulikiambia chama hicho kwamba kutokana na hali ya fedha kuwa mbaya, wadhamini wamemudu kusafirisha idadi ya watu 20 tu ambao ni wachezaji 16 na viongozi wanne bila kuwemo mjumbe wa ZFA.

Hata hivyo, kutokana na ukata unaokikabili, chama hicho kimekosa fedha na kuamua kulinyamazia suala hilo.

Kuhusu kadhia ya kuwepo deni hilo, Soraga alisema halifahamu na kuliahidi gazeti hili kulipatia taarifa baada ya kulifanyia utafiti.

Tuesday 22 February 2011

MAJI YAHARIBI UKUTA WA BAHARI YA FORODHANI

MAJI ya bahari yakiwa yamemega sehemu ya barabara itokayo Forodhani kuelekea Bandarini Mjinmi Zanzibar ambapo hisasa shimo kubwa limejitokeza kwenya barabara hiyo, kuyafanya magari  yanayotumia barabara hiyo kupita kwa tahadhari.(Picha na Othman Maulid)

MHASIBU WA POLISI KIZIMBANI KWA TUHUMA YA WIZI WA MAMILIONI.

Mhasibu wa Polisi kizimbani tuhuma wizi wa mamilioni

Mwengine jela miaka miwili shambulio la aibu
Na Ali Chwaya Pemba

POLISI Mkoa wa Kaskazini Pemba, imemfikisha Mahakamani Mhasibu wake, Hamad Bakari Faki kwa tuhuma za kuiba fedha za askari wenzake ambazo ni mikato kwa ajili ya Benki ya watu wa Zanzibar.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Makame Khamis Ali wa Mahakama ya Mkoa Kaskazini Pemba, Muendesha Mashitaka ambaye ni Mwanasheria wa Serikali katika Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ali Haidar Mohammed alidai kuwa kati ya Julai na Disemba 2009, mtuhumiwa Hamad (44) mkaazi wa Bopwe Wete, akiwa mtumishi wa Serikali aliiba shilingi 33, 428,670 /70

Alisema kitendo hicho ni kosa chini ya sheria na kudaiwa alifanya kitendo hicho katika mikato mbali mbali ya malipo ya askari kupitia Benki ya watu wa Zanzibar PBZ.

Mtuhumiwa Hamad alikana madai hayo na yuko nje kwa dhamana hadi Machi 21, 2011 kesi yake itakapotajwa tena.

Katika masharti ya dhamana, alitakiwa kuweka dhamana ya Tshs milioni 40 za maandishi na wadhamini wawili kwa shilingi milioni 10 kila mmoja za maandishi na mmoja wao awe mtumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wakati huo huo, Rashid Hamad Faki (18)mkaazi wa Kizimbani Wete, ambaye alikuwa akikabiliwa na mashitaka matatu katika mahakama hiyo ikiwemo Shitaka la ubakaji, utoroshaji na shambulio la aibu, mahakama ya Mkoa Wete, imemfutia shitaka la ubakaji na utoroshaji baada ya upande wa mashtaka kushindwa kumuunganisha katika ushahidi uliotolewa.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Ali Haidar Mohamed kuwa Oktoba 10, 2009, usiku, huko Mtemani Wete, Mtuhumiwa huyo alimtorosha, kumbaka na kufanyia shambulio la aibu msichana huyo (16) aliekuwa chini ya uangalizi wa wazazi wake.

Hata hivyo mahakama ilimtia hatiani, Rashid Hamad Faki (18), kwa kosa moja la Shambulio la aibu na kumuamuru kwenda Chuo cha Mafunzo miaka miwili licha ya Mwendesha Mashitaka kuomba kutolewa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria.

CCM MJINI MAGHARIBI YAJIANDAA SHEREHE YA USHINDI WA DK. SHEIN

CCM Mjini Magharibi yajiandaa sherehe ushindi wa Dk.Shein

Na Mwantanga Ame

CHAMA cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharibi kimeanza shamrashamra za kuadhimisha ushindi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyekuwa Mgombea wa CCM katika nafasi ya Urais.

Shamrashamra hizo zitaanza kwa misafara ya matembezi ya pikipiki yatakayopita katika majimbo yote Mkoani humo kwa siku nne.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Katibu wa CCM Mkoa huo, Ramadhani Abdalla Ali, alisema matembezi hayo yanalenga kumpongeza, Dk. Ali Mohammed Shein kwa kupata ushindi kwenye uchaguzi huo.

Aidha, Katibu huyo, alisema sherehe hizo zitakazofikia kilele chake Februari 26, Dk. Shein, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti.

Alisema matembezi hayo yatabeba ujumbe maalum utakaofikishwa kwa wanachama ukihimiza wana CCM kujiandaa na uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho utakaofanyika mwakani.

Ujumbe mwengine utawataka wanachama kufikiria njia za kuitekeleza Ilani ya CCM kwa miaka mitano ijayo.

Kutokana na shamrashamra hizo, Katibu huyo aliwataka wana CCM katika majimbo ya Mkoa huo, kujitokeza kwa wingi kufanikisha shughuli hiyo na kuhudhuria mkutano wa hadhara.

Wakati huo huo, uongozi wa Mkoa wa Mjini umewapongeza Wawakilishi, Wabunge na Madiwani kwa kufanikisha uchaguzi mkuu.

Kikao hicho kilifanyika katika Afisi ya Chama Mkoa kikiwa chini ya Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Maharibi, Ramadhan Abdalla Ali.

Hata hivyo, Katibu huyo aliwaonya wajumbe hao kuacha kubweteka baada ya kupata ushindi wa kuongoza majimbo na badala yake washiriki katika vikao vitavyokuwa vinaandaliwa na wanachama wao katika majimbo yao.

WIZARA ELIMU KUKAMILISHA UJENZI WA MADARASA

Wizara Elimu kukamilisha ujenzi wa madarasa

Na Khamisuu Abdallah

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Abdulla Mzee Abdulla, amesema kutokana na kufaulu kwa kiwango kikubwa wanafunzi mwaka huu Serikali inafanya jitihada za kukamilisha na kujenga madarasa katika Skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake Mazizini, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kutokana na wingi wa wanafunzi waliofaulu, Serikali ya awamu ya saba imeshakamilisha ujenzi wa madarasa 150 katika Skuli mbali mbali zilizopo nchini.

Alieleza kuwa katika kukamilisha ujenzi huo, Serikali ina mpango wa kujenga madarasa 250 kwa kupitia wafadhili ambao ni kutoka nchini Sweden na Ubalozi wa Marekani ambao ni wafadhili waliojitolea kukamilisha ujenzi huo.

Abdulla, alisema hivi sasa Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kujenga Skuli mbali mbali ambazo zitakidhi mahitaji katika vijiji mbali mbali ili kuweza kutoa elimu kwa watoto wote hapa nchini.

Alisema katika kulitatua tatizo hilo, Serikali ipo katika mchakato wa kujenga Skuli mbali mbali za 21 kwa Unguja na Pemba,ikiwemo Dimani,Shamiani pamoja na Wete ambazo wanafunzi watatumia teknolojia ya kisasa ikiwemo kutumia kompyuta pamoja na intaneti ili kuweza kwenda na wakati.

"Serikali ya awamu ya saba tunataka wanafunzi wasome pazuri, wakae pazuri ili wanafunzi waweze kufaulu vizuri kwa kutumia teknolojia itakayokuwepo katika maskuli mbalimbali,"alieleza.

Aidha aliwataka wananchi kujitoa nguvu zao katika ujenzi wa maskuli ili Serikali iweze kuwaunga mkono kuweza kukamilisha ujenzi huo ili kuboresha elimu nchini.

Aidha amewapongeza Skuli ya msingi ya Mtopepo "B" pamoja na Skuli ya Mtopepo kwa kupasisha wanafunzi wengi kila mwaka, sambamba na kuwataka wazazi kuwahimiza watoto wao kujitahidi katika masomo yao.

IRAN KUJENGA CHUO CHA AMALI

Iran kujenga Chuo cha Amali



Na Haji Chapa, MUM

KATIKA kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia serikali ya Jamuhuri ya watu wa Iran, ina mpango wa kujenga chuo cha mafunzo ya amali hapa Zanzibar.

Balozi wa Iran nchini, Mohsen Movahhedi Ghomi alieleza hayo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ramadhan Abdalla Shaaban huko ofisini kwake Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Balozi huyo akiwa ameambatana na ujumbe wa watu watatu, alisema kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Iran na Zanzibar, nchi hiyo imetenga dola 500,000 za ujenzi wa Chuo hicho.

Mbali na hayo Balozi Ghomi, alisema nchi hiyo pia itaendelea kushirikiana na Zanzibr katika kukuza nyanja ya utamaduni ambapo katika hilo itaisadia Zanzibar katika kuikuza sekta ya Utalii.

Katika kuimarisha tamaduni za nchi mbili ni faraja kubwa kuwekeza katika suala la elimu kwani katika hilo vile vile wameazimia kuanzisha ofisi itakayohusika na suala la elimu na kuweka mashirikiano mazuri na taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) alieleza hayo.

Aidha Balozi huyo alisema Zanzibar sio nchi ya kubezwa kutokana na asili yake na umuhimu wake wa kitamaduni kwani unafahamika nchi nyingi duniani kwa kutaja mfano wa mwaka kogwa.

Naye Waziri Ramadhani aliishukuru Jamuhuri ya watu wa Iran kwa uamuzi wao huo wa kutaka kuwekeza katika suala la elimu kwani utaimarisha mahusiano yao ya kitamaduni na kielimu.

Aidha aliiomba Iran kuwekeza zaidi katika sekta hiyo ya elimu na utamaduni na kutumia fursa ya amani na utulivu uliopo Zanzibar kuimarisha mashirikiano.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Abdalla Mzee Abdalla, aliyaelezea mashirikiano ya Iran na Zanzibar katika sekta ya elimu ni ya muda mrefu.

Alisisitiza juu ya nchi hiyo kufanya uthibitisho wa ujenzi wa kituo hicho cha Mafunzo ya Amali ikiwa ni kupata barua rasmi.

HAKI ZA WENYE WALEMAVU ZILINDWE.

Haki za wenye ulemavu zilindwe



Na Raya Hamad, OMKR

OFISA Utetezi kutoka Idara ya Watu wenye Ulemavu, Idrissa Khamis Juma amesema jamii inayo haki ya kuelewa na kufahamu mahitaji ya msingi ya watu wenye ulemavu.

Ofisa huyo alisema kutokana na hali hiyo si busara walemavu kuendelea kunyanyaswa sambamba na kunyimwa haki zao kutokana na maumbile yao yalivyo.

Ofisa huyo alieleza hayo kijiji cha Pwanimchangani alipofanya ziara ya uhamasishaji kwa Watu wenye Ulemavu.

Akitoa ufafanuzi kuhusu haki za watu wenye Ulemavu, alisema Watu wenye Ulemavu hawana budi kufahamu na kuielewa Sera, Sheria ya Watu wenye Ulemavu na Mkataba wa Kimataifa.

Idrissa alisema kueleweka kwa haki hizo za msingi kwa Watu wenye Ulemavu kutasaidia kuondokana na mtazamo wa kuwa walemavu daima ni watu wa kusaidiwa na badala yake watafahamu kuwa wanazodai ni haki zao na sio msaada ambao wanastahiki kupewa kama walivyo wengine wowote katika nchi.

Kuhusu suala la Elimu, aliwataka Watu Walemavu kuendelea kutafuta elimu na kupatiwa elimu “Ingawa Serikali imeanzisha kitengo maalum cha elimu mwaka 1992 bado watu wenye ulemavu walio wengi wamekoseshwa haki hii kutokana na ulemavu wao kwa kufuata skuli masafa marefu na kukosa visaidizi, wazazi na walezi kuwaficha majumbani ni miongoni mwa sababu zinazopelekea kukosa rasilimali hii muhimu kwa maisha”, alisisistiza Idrissa.

Aidha Idrissa ameiasa jamii kuacha kutumia maneno yenye kudhalilisha Watu Wenye Ulemavu na kutolea mfano wa maneno hayo ikiwa ni pamoja na mtu asiyeona kumuita kipofu ,Mlemavu wa Akili kumuita Chizi au Akili taahira, Albino kumuita Zeruzeru au Dili nk.

Wakichangia mada washiriki wa mkutano huo wamesema kuwa tatizo kubwa walilonalo katika kijiji chao ni kutopewa kipaumbele hasa wakati wanapopeleka maombi ya kazi hasa mahotelini “Kazi nyengine huwa hazitaki kisomo kama kutupa taka ama kuzoa takataka za ufukweni lakini tunapokwenda kuomba huwa hatupewi kwa sababu ya Ulemavu tulionao”alisema Madai Haji.

Madai Haji Silima ni Mlemavu wa macho na mtoto wake pia ni kiziwi na mwenye matatizo ya macho ambae ameacha kusoma darasa la 7 mwaka 2010 kutokana na matatizo aliyonayo na hivyo amebakia nyumbani akiwa hana la kufanya.

Nae Hamad Khamis aliiomba Serikali kuwasaidia Watu wenye Ulemavu kama wanavyosaidiwa Wazee wasiojiweza pamoja na Idara ya Watu Wenye Ulemavu kuendelea kutoa Elimu juu ya uelewa wa haki za Watu wenye Ulemavu.

Idara ya Watu wenye Ulemavu imeandaa utaratibu maalum wa kuwahamasisha Watu wenye Ulemavu na wasio na Ulemavu kuanzia Mjijni hadi Vijijini kwa Unguja na Pemba.

Tuesday 1 February 2011

DK. BILAL AHIMIZA WAFANYABIASHARA UTURUKI KUWEKEZA NCHINI.

Dk. Bilal ahimiza wafanyabiashara Uturuki kuwekeza nchini


Mwandishi Maalum, Dar es Salaam


MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal amehimiza wafanyabiashara wa Uturuki kuwekeza nchini Tanzania ili waweze kunufaika na soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Dk. Bilal alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na Balozi wa Uturuki nchini, Dk. Sander Gurbuz ambaye alimtembelea ofisini kwake Ikulu, Jijini Dar es salaam.

Alisema amefurahi kusikia Uturuki imetambua kuna fursa za biashara nchini na kusema kwa vile Tanzania ina uhusiano mzuri na majirani zake wafanyabiashara wa nchi hiyo watapata fursa pia ya kutumia soko hilo kubwa na la aina yake.

“Nimefurahi kusikia serikali ya Uturuki imetambua kuna fursa za biashara nchini. Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye watu zaidi ya milioni 120 na Tanzania ni nchi pekee ambayo inaaminika kuwa na amani,” alisema Dk. Bilal na kuongeza

“Nje ya EAC, tuna uhusiano mzuri pia na nchi za SADC. Hivyo kwa kuwekeza na kufanya biashara Tanzania, wafanyabiashara kutoka Uturuki watanufaika na soko hilo kubwa la EAC na SADC.”

Katika mazungumzo hayo, Dk. Sander Gurbuz alimweleza Makamu wa Rais kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu toka Ubalozi wa Uturuki uanzishwe nchini, akiwa kama Balozi wa kwanza ameweza kufanikisha mambo mbalimbali yanayolenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki.

Alisema katika kipindi hicho ameweza kufanikisha safari za viongozi wa kitaifa wa nchi hizo mbili, shirika la ndege la Uturuki limeanza safari zake nchini na mikataba mitano ya ushirikiano imetiwa saini iliyowawezesha wafanyabiashara wa Uturuki wameanza kuja Tanzania kuwekeza katika maeneo mbalimbali kama ya madini, utalii na kilimo.

Hivi sasa ujumbe wa watu wapatao 7 wamewekeza katika maeneo ya migodi iliyoko wilayani Mpanda mkoa mpya wa Katavi na wengine wako Zanzibar ambako wanashughulikia Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.

Aidha, alisema katika jitihada za kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili hizi Spika wa Bunge la Uturuki anatarajia kuitembelea Tanzania hivi karibuni na hali kadhalika mwezi ujao Waziri wa Biashara wa Uturuki ataongoza ujumbe wa wafanyabiashara wapatao 100 kutembelea Tanzania kwa madhumuni ya kujadiliana namna ya kushirikiana kiuchumi.

MZAHA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA UTAANGAMIZA TAIFA ; MAALUM SEIF.

Mzaha dhidi ya dawa za kulevya utaangamiza Taifa: Maalim Seif



Na Abdi Shamnah, Pemba

MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amezitaka taasisi za Serikali, vyombo vya Ulinzi na Usalama, kushikamana katika harakati za kupiga vita uingizaji wa dawa za kulevya.

Amesema uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya ni vita na suala la mapambano ya Taifa, na kuonya kuwa pale litakapofanyika mzaha, ni wazi kuwa linaweza kuangamiza nguvu kazi ya Taifa.

Maalim Seif, ameyasema hayo leo, Machomane Pemba, alipozungumza na wafanyakazi wa Idara zilizo chini ya Ofisi yake, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake kutembelea Ofisi hizo na kupata taarifa za utendaji pamoja na changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Alisema katika mapambano hayo mkazo zaidi unahitajika kuelekezwa katika kukinga, kwa kujenga ushirikiano na Wananchi ili kuwafichua waingizaji na wasambazaji wa dawa hizo.

Aidha alielekeza umuhimu wa wananchi kuelimishwa juu ya madhara ya dawa za kulevya, sambamba na kuwa tayari kushiriki katika Ulinzi shirikishi.

Maalim Seif aliagiza kitengo cha Utoaji na Elimu kaika Idara hiyo kufanya kazi ya ziada ya kuwafikia wananchi popote pale walipo, iwe mjini au vijijini.

Alisisitiza umuhimu wa kuwepo uaminifu huruma kwa waathirika na uzalendo katika utekelezaji wa kazi hiyo, kwa kigezo kuwa maadui wakubwa katika vita hivyo ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha.

Alisema Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha masuala ya nyenzo, taaluma pamoja na usafiri, yanapatiwa ufumbuzi kadri hali itakavyoruhusu.

Akizungumzia suala la watu wenye ulemavu, Maalim Seif alisema, Serikali inajali jamii hiyo kwa kuwa na haki sawa kama ilivyo jamii nyengine na kutaka kuwepo takwimu sahihi ili Taifa liweze kupanga mipango yake ya kuisaidia jamii hiyo pamoja na kuelewa mahitaji yao kwa kila kundi.

Alionya ulemavu kutotumika kama kigezo cha kuikosesha jamii hiyo haki, ikiwemo fursa za ajira na kuagiza majengo yote ya utoaji wa huduma lazima yawe na visaidizi.

Aidha alisema ni lazima kuwepo na mipango na mikakati madhubuti katika mapambano dhidi ya ukimwi na kutaka mkazo zaidi kuelekezwa katika kuzuia maambukizo mapya ya ugonjwa huo.

Alisema suala la elimu kwa jamii ni muhimu, ili kuhakikisha ujumbe umefika kwa walengwa na kutaka uwepo umuhimu katika kurudisha maadili mema ya wazanzibari.

Maalim Seif alisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na kusema mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, kumetokana na uchafuzi wa mazingira kufuatia vitendo vinavyofanywa na binaadamu.

Alikemea wimbi la uingizaji wa bidhaa kutoka nje, hususan zile za Electronic na kumainisha kuwa ni kiwango kidogo tu ndio zenye kufaa kwa matumizi.

Alikipongeza kikosi cha KMKM katika kukabiliana na uharibifu huo wa kimazingira, kufuatia tukio la kukamata Tani 40 ya mifuko ya Plastik.

Aidha amerudia kauli yake na kukemea matumizi ya misumeno ya moto, na kusema Kisiwa cha Pemba kimo hatarini kupoteza mandhari yake iwapo hatua thabiti zitasita kuchukuliwa kwa haraka na kwa nguvu zote.

Mapema Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Juma Kassim Tindwa aliwatka watendaji wa Idara hizo kujenga mashirikiano na viongozi wa Serikali katika ngazi zote, wakielewa wana kazi kubwa katika kusimamia utendaji wa Idara zao. Nao baadhi ya wafanyakazi wa Idara hizo walimueleza Makamo wa Kwanza wa Rais juu ya changamoto zinazowakabili ikiwemo ufinyu wa Ofisi, vitendea kazi pamoja na mahitaji ya Taaluma kwa watendaji.

BALOZI SEIF ; SMZ YAJIDHATITI KUONDOSHA UHABA WA MADAWATI.

Balozi Seif: SMZ yajidhatiti kuondosha uhaba wa madawati

Na Mwantanga Ame

MBUNGE wa Jimbo la Kitope, Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi madawati 100 kwa wanafunzi wa Skuli ya Kitope, Kilombero na Fujoni ikiwa ni hatua ya kutimiza ahadi yake kwa wananchi Jimbo hilo.

Balozi Iddi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alikabidhi madawati hayo jana katika ziara aliyoifanya katika skuli hizo kwa nyakati tofauti ambapo pia alikabidhi shilingi milioni moja kwa Skuli ya Kitope kwa ajili ya kuwezesha kumaliziwa kwa darasa linalotarajiwa kutumika kwa shughuli za maabara.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo, Mbunge huyo alisema kuwa viongozi wa Jimbo hilo wamedhamiria kuona suala la watoto kuandika wakiwa wamepakata mabuku yao katika mapaja linaondolewa kwa vile hawawezi kuona tatizo hilo linashindwa kupatiwa ufumbuzi.

Alisema serikali hivi sasa imo katika mkakati mkubwa wa kupambana na tatizo la ukosefu wa madawati katika skuli zake za Unguja na Pemba, ambapo inahitaji kupata vikalio 30,000.

Alifahamisha kuwa katika kuitekeleza azma hiyo serikali inajiandaa kutoa tamko litalowashurutisha Wabunge wa Jamhuri ya Muungano kuchangia kuondoa matatizo ya aina hiyo katika majimbo yao kupitia fedha za mfuko wa majimbo.

Alisema hatua iliyofikiwa katika Jimbo hilo hivi sasa ni ya kuridhisha kwa baadhi ya skuli jambo ambalo linatarajiwa wanafunzi wa skuli hizo kufanya vizuri katika masomo yao.

Akizungumzia matatizo ya baadhi ya walimu wanaojitolea kuweza kusaidiwa kupata posho la kuwakimu, alisema ataendelea kuliangalia suala hilo kwa kufuata utaratibu uliowahi kutumika hapo awali kwa kuwalipa walimu hao.

Aidha Mbunge huyo aliwataka walimu ambao waliomba kupatiwa vyombo vya moto kwa njia ya mkopo alisema suala hilo tayari Wizara ya Elimu imekubali kuwapatia mikopo hiyo kupitia SACCOS.

Aidha madai ya ukosefu wa maji kutoka kwa wanachi wa eneo la Kirombero na Upenja, alisema tayari hatua za awali imeshazichukua za kutafuta vifaa ambavyo walitakiwa na mamlaka ya maji kuwa navyo na kinachosubiriwa sasa ni shughuli za kitaalamu kufanyika ili kupata huduma hiyo.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Shaaban, akitoa shukrani zake kwa Mbunge huyo alisema serikali imefarajika kuona Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo hilo Makame Mshimba wameweza kuanza kutoa misaada hiyo kwa vile ni moja ya mpango mkubwa unaokusudiwa kutekelezwa.

Alisema tatizo la madawati katika maskuli ya Unguja na Pemba hivi sasa ni kubwa na hivi sasa serikali inajiandaa kutekeleza mradi mkubwa kupitia wafadhili, kuchongesha madawati yatayotosheleza kwa skuli zilizopo pamoja na kumaliza mabanda ya skuli.

Waziri huyo alisema kutokana na mchango ulioanza kutolewa na Mbunge huyo Wizara hiyo itahakikisha inalipatia Jimbo hilo madawati 135 ikiwa ni hatua ya kwanza na kuwataka wanafunzi wa skuli hizo kuanza kujiandaa na matumizi ya kutumia mitandao.

Waziri huyo alisema mpango wa serikali wa kuanza matumizi ya mitandaao kwa wanafunzi wa darasa la kwanza unatarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi huu, ambapo kila mwanafunzi atakuwa na kompyuta yake kauli ambayo ilishangiriwa na wanafunzi hao.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Abdalla Mzee alisema serikali imekuwa ikitumia shilingi milioni 200 kwa mwaka kwa ajili ya kununulia madawati ambapo huweza kupata madawati 1,200 ambapo skuli zinazohitaji madawati hayo ni 450.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Vuai Ali Vuia, alisema uhaba wa vikalio katika skuli za Mkoa huo ni mkubwa lakini inafurahisha kuona uongozi wa Jimbo la Kitope umekuwa ukipambana nalo na kuwataka viongozi wa majimbo mengine kuiga mfano huo.

MAUAJI YA VICHANGA YALAANIWA.

Mauaji ya vichanga yalaaniwa



Na Mwanajuma Abdi

MKURUGENZI wa Haki za Binadamu, Francis Nzuki, amesema kuzikwa kwa vichanga 10 katika kaburi moja huko Mwananyamala kwa Kopa, ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Mkurugenzi huyo alisema hayo jana alipokuwa akifanya mahojiano na gazeti hili, hoteli ya Zanzibar Beach Resort, baada ya kumalizika mafunzo ya wiki moja ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Tume hiyo.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha wadau kutoka Jeshi la Polisi, Mafunzo, KMKM Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kuzikwa vichanga hivyo katika kaburi moja (kwenye shimo la taka lililokuwa linatumiwa na wananchi, wakiwa wamezongwa shuka lenye lebo ya Bohari Kuu ya Madawa (MSD) ya hospitali ya Mwananyamala, ni kitendo kisichopaswa kunyamaziwa kwani kimekiuka haki za binadamu.

Alieleza tayari wameshaituma timu yao kufuatilia tukio hilo la kinyama, kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina ili wahusika waliofanya mambo hayo waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aidha aliwakemea baadhi ya madaktari wanaojihusisha na utoaji wa mimba, ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa kuua viumbe vinavyotarajia kuja duniani.

Alifahamisha kuwa, tukio hilo linaonesha utata mkubwa kwa vile maiti hizo zimefunikwa shuka la hospitali, hivyo alionesha wasiwasi wake kwamba baadhi ya wauguzi wanahusika na mauaji wa watoto hao waliokuwa hawana hatia.

Mkurugenzi huyo, alisema mtoto ana haki tokea anapokuwa tumboni kwa mama tangu wa siku moja hadi anapozaliwa.

Hata hivyo alieleza masuala ya haki za binadamu ni endelevu duniani kote, hivyo ametoa wito kwa jamii kuheshimu uhuru wa mwenzake na kujua haki yake na wajibu wake katika kuhakikisha hakiuki matakwa ya msingi iliyowekwa katika Umoja wa Mataifa juu ya utekelezaji huo.

Nao washiriki mbali mbali walisikitishwa na habari hizo, ambazo walisema kutokana na mafunzo waliyoyapata kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

MAFUNZO USHIRIKIANO NI NGUZO UPATIKANAJI HAKI ZA BINAADAMU.

Mafunzo, ushirikiano ni nguzo upatikanaji haki za binadamu

Na Salum Vuai


IMEELEZWA kuwa suala la upatikanaji wa haki za binadamu linahitaj utendaji wa pamoja kati ya taasisi zinazohusika na utoaji haki na jamii ili kuhakikisha kila raia anahudumiwa kwa njia stahiki.

Aidha, mafunzo juu ya mbinu za kufanya upelelezi unaolenga kujua kama haki inatendeka, yameelezewa kuwa muhimu hasa kwa kipindi hichi ambacho dunia inakabiliwa na mabadilko ya sayansi na teknolojia.

Akifunga semina ya siku tisa jana juu ya ufahamu wa uchunguzi na utendaji haki iliyofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania Mary Massay, alisema kujifunza ni jambo linalohitaji kuendelezwa.

Alifahamisha kuwa kutokana na umuhimu huo, Tume hiyo itahakikisha inaendelea kuwapatia watendaji wake mafunzo ya mara kwa mara ili kuwapa njia sahihi na zinazokwenda na wakati katika ufanyaji kazi zao.

Alisema kuwa watendaji wa taasisi muhimu zinazotumainiwa kutoa haki kwa umma, ni lazima wajue mbinu mbalimbali za uchunguzi, kuwahoji mashahidi, waathirika wa matendo ya jinai, watuhumiwa, mateso au vifo ndani ya mahabusu na udhalilishaji wa kijinsia sambamba na kuandika ripoti.

Alieleza matumaini yake kuwa washiriki wa semina hiyo wamepata uelewa wa kutosha na kwamba watayatumia mafunzo hayo katika kuwasaidia wanajamii kupata haki, pamoja na kuwa mabalozi kwa wengine ndani ya taasisi zao na katika jamii inayowazunguka.

Aidha alisema kukusanyika kwao hapo, kumesaidia kujenga uhusiano na urafiki ambao kwa njia moja au nyengine utatoa mchango katika dhamira ya kufanikisha kazi za utoaji haki kwa walengwa.

Massay alizishukuru taasisi zote zilizowezesha kufanyika kwa semina hiyo, akizitaja kuwa ni APCOF ya Afrika Kusini, ICD ya Pretoria Afrika Kusini pia, Kituo kinachoshughulikia migogoro na usuluhishi (CSVR) pamoja na taasisi ya GIZ (zamani GTZ).

Mapema akitoa ufafanuzi juu ya lengo la kufanyika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria katika Tume ya Haki za Binadamu Tanzania, Nabor Balthazar Assey, alisema ni kuwapatia mafunzo yanayokwenda na wakati watumishi wake kulingana na mahitaji ya wakati uliopo.

Alieleza kuwa Tume hiyo katika utendaji wake, imegundua mapungufu kadhaa ambayo ni lazima yafanyiwe kazi ili kujenga imani kwa wananchi wanaohitaji haki.

Alizitaja taasisi kubwa ambazo zinategemewa kutoa haki kuwa ni pamoja na Polisi, Magereza, Vyuo vya Mafunzo na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo ambazo zote zilitoa washiriki katika semina hiyo.

Mafunzo hayo yalifanyika kwa makundi mawili, moja likianza Januari 24 hadi 28, na jengine Januari 29 hadi jana Februari 1, ambapo washiriki walitoka katika Jeshi la Polisi Tanzania na Zanzibar, Magereza, Vyuo vya Mafunzo na KMKM.

TANZANIA YAJUMUISHWA KUSAKA AMANI IVORY COAST.

Tanzania yajumuishwa kusaka amani Ivory Coast



Rais Kikwete azindua muongo vita dhidi ya malaria
Na Mwandishi Maalum, Addis-Ababa

TANZANIA imeteuliwa kuwa moja ya nchi tano zitakazounda kamati ya Umoja wa Afrika katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Ivory Coast, kati ya Rais anayemaliza muda wake Laurent Gbagbo na Alassane Outtara.

Nchi nyengine katika kamati hiyo ni Chad, Mauritania, Nigeria na Afrika Kusini, ambazo zitaungana na Burkina Faso ambayo tayari inashughulikia mgogoro huo.

Kamati hiyo imefanya mkutano wake wa kwanza juzi mjini Addis Ababa ambapo imekubaliwa kuwa kila nchi itachagua mwakilishi wake katika kamati ndogo ya wataalamu hapo kesho, ambao watakwenda nchini Ivory Coast kuangalia na kutathmini hali ilivyo.

Kamati ya wataalamu watatakiwa kutoa taarifa na ushauri kwa viongozi ambao hatimaye watakwenda Ivory Coast na kukutana na viongozi hao wawili wanaogombea madaraka.

Wakati huo huo, Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amesema mwaka 2011 ni mwanzo wa muongo wa vita dhidi ya malaria barani Afrika.

Rais Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Mshikamano wa Viongozi wa Afrika Dhidi ya Malaria (African Leaders Malaria Alliance-ALMA), alisema hayo wakati akifungua kikao cha viongozi wa nchi 35 za Afrika zinazounda mshikamano wa kupambana na malaria barani Afrika.

“Mwaka wa 2011 ni mwanzo wa muongo mpya katika Afrika dhidi ya malaria, pia unaashiria mstari wa mwisho katika kukaribia mwisho wa juhudi hizi katika kufuta vifo vinavyotokana na malaria kuelekea mwaka 2015”, Rais Kikwete aliueleza mkutano huo.

Amesema hatua muhimu iliyopigwa na nchi za Afrika katika kufikia malengo ya milenia ambayo yamewekwa na nchi hizi kama wanachama wa familia ya Umoja wa Mataifa na kubainisha kuwa kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2010, vifo vinavyotokana na malaria vimepungua barani Afrika.

Katika kikao hicho nchi nne zimefuzu na kupokea tunzo ya kwanza ya ubora na umakini katika juhudi za kupambana na malaria zikiwemo Tanzania, Guinea, Kenya na Uganda.

Juhudi zilizofanywa na nchi hizi ni pamoja na kukuza uhusiano na kuharakisha upatikanaji wa fedha, kudhibiti na kukuza matumizi ya kinga ya malaria, mfano ikiwemo matumizi ya vyandarua, kufuta na kusitisha utengenezaji, usambazaji na matumizi ya dawa aina ya Artemisinin, kuondosha kodi na kuunga mkono utengenezaji na uzalishaji wa dawa za malaria barani Afrika.

Rais Kikwete alipokea tunzo hiyo katika kikao hicho na kushuhudiwa na nchi wanachama akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, mwenyeji wa Mkutano wa Viongozi wa Afrika wanaohudhuria kikao jijini Addis Ababa Waziri Mkuu Meles Zenawi viongozi wa mashirika ya kimataifa na nchi rafiki.

Kikao hicho kimemchagua Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf kuwa Makamu Mwenyekiti wa ALMA.

SERIKALI KUIELIMISHA JAMII ATHARI ZA TABIANCHI

Serikali kuielimisha jamii athari za tabianchi

Na Evelyn Mkokoi, Mtwara
SERIKALI imedhamiria kuelimisha jamii ya kitanzania juu ya athari na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kupitia wa kwa wadau wa sekta mbali mbali.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi, alieleza hayo jana katika warsha ya wadau wa kanda ya kusini iliyofanyika mkoani Mtwara.

Muyungi alisema nchi zinaoendelea ikiwemo Tanzania zinakabiliwa na changamoto mbali mbali zitokanazo na mabadiliko ya Tabia nchi ikiwa ni pamoja na mafuriko akitolea mfano mafuriko ya Kilosa.

Aidha alisema kuwa athari nyengine ni ongezeko la magonjwa kama vile malaria zaidi katika maeneo ambayo awali malaria haikuwa tishio kama vile Lushoto, kituro Rungwe na Njombe.

Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa kuna kila sababu ya jamii kuelewa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi umuhimu wake na changamoto zake ikiwa ni pamoja na umaskini.

Akifungua warsha hiyo mwakilishi wa Ofisa tawala wa Mkoa wa Mtwara, Smythies Pangisa alisema athari zaidi ya mabadiliko ya tabia nchi katika vizazi vijavyo ni ukosefu wa maji safi, kuongezeka kwa hali ya jangwa katika baadhi ya maeneo na viumbe kutoweka.

Warsha hiyo ya siku mbili iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, imehusisha mada ya mabadiliko ya Tabia nchi na Sera ya Taifa ya Mazingira, sheria ya usimamizi wa mazingira na utekeleazaji wake, imehudhuriwa na wadau mbali mbali wakiwemo maofisa maliasili na mazingira, mahakimu, wadau kutoka katika asasi za kiraia, NGO’s na wanahabari.