Saturday 30 April 2011

ZIARA DK. SHEIN YAZIDISHA USHIRIKIANO UTURUKI, ZANZIBAR.

Ziara Dk. Shein yazidisha ushirikiano Uturuki, Z’bar

Yaahidi kutuma timu ya watalaamu
‘Turkish Airline’ kutua visiwani
Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Uturuki, Abdullah Gul amesema ziara ya rais wa Zanzibar na Mwewnyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein nchini Uturuki, ni muhimu na itazidisha ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizo.
Rais Gul, alieleza hayo alipokuwa na mazungumzo na rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein katika makazi yake huko mjini Ankra.
Alisema ziara ya Dk. Shein nchini humo ni muhimu sana na itaendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo hasa kwenye nyanja ya maendeleo.
Rais Gul alisema ushirikiano kwenye nyanja za maendeleo baina ya mataifa unahitajika hivi sasa kuliko wakati mwengine wowote kutokana na ushindani wa kiuchumi uliopo.
Alisema Uturuki ina uzoefu mkubwa katika biasahara ya Utalii, hivyo Zanzabar kwa kiasi kikubwa ambayo uchuimi wake umekuwa ukitegemea utalii, itafaidika kwa kubadilishana uzoefu kwenye sekta hiyo.
Rais Gul alifahamisha kuwa upo uwezekano wa shirika la ndege la nchi hiyo, ‘Turkish Airline’, kuleta ndege zake moja kwa moja visiwani, ikiwa ni hatua moja ya kuimarisha sekta ya utalii.
Aidha nchi hiyo imeahidi kukisaidia kwa kukiongezea uwezo Chuo Cha Maendeleo ya Utalii kilichopo Maruhubi pamoja na ujenzi wa hoteli za kisasa na kushirikiana katika masuala mazima ya utamaduni.
Aidha rais Gul, aliahidi kuwa serikali yake itatuma timu ya wataalamu visiwani hapa kwa lengo la kuja kufanya tathmini ya mahitaji ya ndani ya sekta za kimaendeleo na kiuchumi ambazo inaweza kuisaidia Zanzibar.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Rais huyo alisema kuwa Serikali ya Uturuki itashirikana na Serikali ya Mapinduzi Zanzbar katika kuimarisha sekta ya elimu hasa elimu ya juu kwa kuongeza nafasi za masomo zinazotolewa na Serikali ya Uturuki na pia, kubadilishana wataalamu baina ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na vyuo vyengie vya elimu ya juu nchini Uturuki.
Pamoja na hayo, Rais alisema kuwa Uturuki imo katika mipango ya kujenga Chuo Kikuu nchini Tanzania ambacho kitajengwa Tanzania Bara ambapo alisema kuwa Zanzibar nayo itanufaika moja kwa moja na chuo hicho.
Kwa upande wake Dk. Shein alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wana matumaini makubwa na serikali yao na hatua za serikali ya Uturuki kuendeleza ushirikiano na Zanzibar nako kutachangia juhudi za kuendeleza na kufikia matarajio ya wananchi hao.
Aidha, Dk. Shei alisema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafanya juhudi za kuimarisha sekta ya utalii na kutokana na Uturuki kupiga hatua katika seta hiyo itakuwa endapo nchi zitashirikiana pamoja.
Dk. Shein alisema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanya juhudi kubwa katika kuimarisha sekta ya elimu hasa elimu ya msingi lakini jitihada za ziada zinahitajika katika kuimarisha elimu ya juu.
Mapema Dk. Shein alifika eneo la kumbukumbu ya kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo marehemu Kemal Atyaturk mjini Ankara na kuweka shada la maua akiwa amefuatana na mkewe Mama Mwanawmema Shein.
Baada ya hapo alikutana na Spika wa nchi hiyo katika ofisi za Bunge la nchi hiyo na kufanya mazungumzo ambayo yalilenga kuendeleza ushirikiano baina ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Bunge la Uturuki.

MZEE MOYO AIBUKA TENA

Mzee Moyo aibuka tena

Ashangaa kusikia Muungano hauna hati
Asema alimuona nazo mzee Karuma
Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Kwanza wa elimu katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, amekuja juu na kueleza kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una hati.
Mzee huyo mwenye kuheshimika, alieleza hayo kwenye mahijiano maalum na kituo cha redio cha sauti ya Ujerumani.
Alisema madai yanaibuka hivi kuwa hati ya Muungano haipo hayana ukweli na wanaosema haipo hawafahamu ukweli juu ya suala hilo, na kubainisha kuwa anaamini hati hiyo ipo.
Mzee Moyo alisema anashangazwa sana na hoja zinazoletolewa hivi sasa kudaiwa hati ya muungano haipo wakati yeye alikuwa shahidi aliyemshuhudia Mzee Karume akiweka saini kwenye hati hiyo.
Ushuhuda mwengine aliyoutoa mzee Moyo kuelezea uwepo wa hati hiyo ni hatua ya mzee Karume kuwafikishia hati hiyo mbele ya Baraza la Mapinduzi baada ya kuweka saini huko Tanganyika.
“Mkataba wa Muungano niliuona ukiwa umetiwa saini, kwani hati hizo baada ya kutiwa saini ilikabidhiwa serikali ya Zanzibar” alisema Mzee Moyo.
Aidha alipinga vikali kwa kusema wakati baraza hilo likipokea hati hizo za Muungano, hakuwepo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Wolfgang Dorado siku ya kikao hicho.
Akizungumzia hoja zilizojitokeza wakati wa mjadala wa rasimu ya Katiba mpya, alisema rasimu hiyo ilipaswa kuondolewa kutokana na kujitokeza kasoro nyingi ambazo hazikuwa zinatoa haki kwa maslahi ya Zanzibar.
Hata hivyo alisisitiza suala la msingi ni kuwepo mjadala wa katiba mpya ya Muungano ambapo ndio moja ya suluhu ya mambo yote ambapo wananchi watatumia haki hiyo kuweza kuchagua yepi wanayoona yanafaa kwenye Muungano uliopo.
Alisema katika mambo ya Muungano hivi sasa kuna mambo mengi yanahitaji kuangaliwa kwani makubaliano ya awali yaliletwa yakiwa na mambo 11 ambayo kupitishwa kwake yalifanyika zaidi kwa makubaliano ya viongozi waliopo wakati huo.
Alisema hivi sasa tayari kuna vijana wenye mawazo ya kustawisha Zanzibar katika muundo wa Muungano na ni lazima wapewe nafasi kuelezea matakwa yao ili baadae serikali iyazingatie kwa maslahi ya taifa kwa yale ambayo yataonekana kuwa na manufaa.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe katika mjadala huo alisema pande zote za Muungano zimekuwa na lawama kwani wamebaini kuwapo kwa baadhi ya mambo yanalalamikiwa.
Alisema kilichotokea ni kuzuiliwa kwa hoja ya Muungano, akisema wananchiliwe waalizungumze na pia wasema aina ya Muungano unaowafaa.
Zitto alisema Zanzibar inataka mafuta na gesi kutolewa katika mambo ya Mungano jambo lenye kuwezekana kwani haiwezekani uchimbaji wa madini ya dhahabu mafuta na gesi kuwa ni mambo ya Muungano wakati hakuna faida inayokwenda Zanzibar.
Mjadala wa Muungano umekuwa ukikuwa siku hadi siku katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi ambapo mwanzoni mwa wiki hii Muungano ya Tanganyika na Zanzibar ulitimiza miaka 47 sherehe ambazo zilifanyika Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na umati wa wananchi.

HAROUN ATAKA MAONESHO YASHIRIKISHE TAASISI ZA NJE

Haroun ataka maonesho yashirikishe taasisi za nje

Na Ali Mohamed, Maelezo
WAZIRI wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Haroun Ali Suleiman amesema shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), kuzishirikisha taasisi za nchi za Tanzania Bara na Afrika Mashariki kwenye maonesho ya ‘May Day’.
Akizungumza na vyama vya ushirika, taasisi za umma na za binafsi na wananchi walioshiriki katika maonyesho ya biashara na huduma katika viwanaja vya Amani nje, alisema kufanya hivyo kutakuza soko la nje na kuingeza pato la taifa.
Alisema lengo la maonyesho hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya kwanza Zanzibar ni kutangaza bidhaa na huduma zinazopatikana Zanzibar, hivyo taasisi za umma na binafsi pamoja na vyama vya ushirika ni vyema wakatumia fursa hiyo kujutangaza kibishara.
Alisema mapungufu yaliyojitokeza yawe changamoto kwa waandaji na kuyafanikisha maonyesho yajayo ikiwemo kuzishirikisha taasisi na vyama vya ushirika vingi zaidi vya ndani na nje ambapo kuahidi serikali kuunga mkono.
"Tuonyeshe wananchi shughuli, huduma na majukumu yetu ya kazi tunayoyatekeleza katika sehemu mbali mbali za kazi ikiwa ofisini, viwandani na kwengineko na maonyesho haya yawe sehemu ya kuona na kukunua bidhaa na huduma na kupata kipato cha kuendeleza maisha yetu",alifahamisha waziri Haroun.
Alisema serikali inafahamu kutokuwepo eneo maaluma la maonyesho ya biashara na huduma ambayo hiyo ni changamoto na aliahidi kuwa itafanya kila liwezekanalo kutafuta sehemu maalumu ya maonyesho hayo ambayo yatakuwa yanafanyika kila mwaka ikiwa ni miongoni mwa ratiba za maazimisha ya siku ya wafanyakazi May Day.
Aidha Waziri Haroun alisema kuwa Zanzibar kama nchi nyengine lipo tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana ambapo serikali imedhamiria kupunguza tatizo hilo kwa kujenga vituo vya kutoa taaluma kwa vijana, (skills Development Cetre) kuunda kamati za ajira katika wilaya zote kwa lengo la kuzalisha ajira kwa vijana.
Alisema maonyesho hayo pia yalenge kuwashajihisha vijana kubuni njia za biashara na miradi amabayo itawasaidia kujiaajiri, kuwaajiri wenzao na kutengeza nafasi za ajira.
Waziri Haroun alitoa ushauri kwa wafanyakazi kujiunga na vayama vya wafanyakazi na shirikisho la wafanyakzi ili kuongeza umoja mshikamano na kutetea maslahi yao katika mazingira ya kazi.
Kwa niaba ya wafanyakazi katibu wa shirikisho hilo la Wafanyakazi Zanzibar ZATUC, Khamis Mwinyi Mohammed alisema wafanyakazi wanahaki ya kushirikishwa katika mambo yanayowahusu amabayo ni kauli mbuyu ya maazimisho ya siku ya wafanyakazi mwaka huu.

MAKAMPUNI YA UTURUKI KUKARABATI VIWANJA VYA NDEGE

Makampuni ya Uturuki kukarabati viwanja vya ndege

Na Rajab Mkasaba,
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetiliana saini makubaliano ya maelewano na makampuni matatu makubwa ya Uturuki ambayo yatashughulikia ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba.
Makubaliano hayo yalisaini jana katika Hoteli ya Sheraton mjini Ankara Uturuki, ambapo kwa upande wa Zazibar iliwakilishwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee.
Akizungumza kabla ya kutiwa saini makubaliano hayo, Mzee alsema kuwa mradi huo ambao umekisiwa kuharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 40, utahusisha matengenezo makubwa katika uwanja wa ndege wakimaifa wa Zanzibar unaotumika hivi sasa kwa ujenzi wa jengo la abiria.
Aidha, alisema kuwa kwa upande wa uwanja wa ndege wa Pemba, kampuni hizo zitaujenga uwanja huo pamoja na kutiwa taa ili kuwezesha ndege kuweza kutua usiku na mchana.
Mzee alisema kuwa serikali inaendelea na hatua kukamilisha mkataba kwa ajili ya mradi huo ili ikiwezekana utekelezaji wake uanze katika mwaka ujao wa fedha.
Nae mwakilishi wa Makampuni hayo ya YDA-ORIZZONTE-SARAYLI (YDA –ORSA) Huseyin Arslawa alisema kuwa hatua hiyo ni mwanzo katika utekelezaji wa miradi mengine inayokusudiwa kuekezwa na makampuni hayo kwa hapa Zanzibar.
Alisemasambamba na utekelezaji wa mradi huo kampuni hiyo itajenga hoteli ya kisasa kisiwani Pemba ambayo inatarajiwa kuanza kazi rasmi mara tu baada yakukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo wa ndege.
Pamoja na hayo alisema kuwa Uturuki imeamua kwa dhati kuelekeza nguvu zake za uwekezaji katika nchi za Afrika hasa katika maeneo ambayo amani na utulivu vimetawala ikiwemo Zanzibar.

CHADEMA YAISHITAKI BAJETI KWA WANANCHI.

CHADEMA yaishitaki bajeti kwa wananchi

Na Jumbe Ismailly,Singida
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Singida kimeanza ziara ya kuwaelezea wananchi wa jimbo la Singida Magharibi namna madiwani, walivyopitisha mapendekezo ya bajeti ya mapato na matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 29,na kushindwa kuhoji zaidi ya shilingi milioni mia sita zilivyotumika.
Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA) Christowaja Mtinda alitoa kauli hiyo alipokuwa akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Puma,wilayani Singida.
Mbunge huyo alisema madiwani wa CCM kwa kutumia uwingi wao waliungana na bila kujali matatizo ya wananchi kwa kupitisha zaidi ya shilingi bilioni 29 kwa mwaka 2011/2012.
Kutokana na hatua hiyo Chadema wanatarajia kumfikisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa wananchi ili akawaeleze alipozipeleka asilimia ishirini ya fedha za fidia ambazo ni zaidi ya shilingi milioni mia sita zilizotolewa na serikali kuu kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mtinda ambaye ni Waziri kivuli wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi alifafanua kuwa Mei mosi mwaka 2002 serikali ilifuta ushuru wa mazao, licha ya kwamba bado kuna vizuizi vingi kwenye vijiji vya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo ushuru huo wa mazao uliofutwa ulikuwa chanzo kikubwa cha mapato katika vijiji na kuongeza kwamba serikali kwa kulitambua hilo ikalazimika kurejesha asilimia ishirini ya mapato hayo kama fidia kwa kila mwaka.
Aliweka wazi mbunge huyo kwamba katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 ilipokea kutoka serikali kuu zaidi ya shilingi milioni 247 zilizotakiwa kwenda vijijini kama fidia kwa ajili ya kufanikisha shughuli za maendeleo.
Hata hivyo Mtinda hakusita kuwafahamisha wananchi wa kijiji cha Puma kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2010/2011 wilaya hiyo ilipokea zaidi ya shilingi milioni 283 kama fidia za vyanzo mbalimbali vya mapato vilivyofutwa hazikupelekwa katika vijiji kama zilivyokusudiwa.
Alisema kwa mwaka huu Halmashauri hiyo imeomba zaidi ya shilingi milioni 163 kama fidia za vyanzo mbalimbali vya mapato kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.

KITOPE KUANZISHA ULINZI SHIRIKISHI

Kitope kuanzisha ulinzi shirikishi

Na Zainab Ali, MCC
WANANCHI wa shehia ya Kitope wapo mbioni kushirikiana kuanzisha Ulinzi shirikishi kutokana na kukithiri vitendo vya uhalifu katika shehia yao.
Sheha wa shehia ya Kitope, Bakari Khamis Simai alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwaandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Kitope wilaya ya Kaskazini ‘B’.
Sheha huyo alifahamisha kuwa ulinzi huo utasaidia kupiga vita vitendo viovu vikiwemo wizi wa mifugo, na mazao katika mashamba wakilima wa kijiji hicho.
Sambamba na hayo jeshi la polisi likishirikiana na wananchi wamesema mtu atakayekamatwa akijihusishwa na uhalifu ikiwemo wizi atachukuliwa hatua za kisheria.
Vile vile Bakari Khamis alisema wananchi wake wajitokeze kwa wingi ili kulisawazisha suala hili kwapamoja kuondokana na udhalilishaji wa kijamii.
Hata hivyo aliwaomba wananchi hao wawe wastahamilivu sana na usumbufu utakaotokezea kwani wapo mbioni kulifanyia matayarisho ili kudumisha usalama na amani katika shehia yao.

TUMBATU UVUVINI WATAKA BWANASHAMBA

Tumbatu Uvuvini wataka mbwanashamba

Na Biubwa Hafidh MCC
WANANCHI wa shehia ya Tumbatu Uvivini wameiomba serekali kipitia wizara ya Kilimo na Maliasili, kuwapatia mabwanashamba ili waweze kujiendeleza katika shughuli zao za kilimo.
Ushauri huo umetolewa na wananchiwa shehia hiyo walipokuwa wakizungumza na wandishi wa habari hizi huko wilaya ndogo Tumbatu.
Walisema kuwa kutokana na ukosefu wa wataalam wanaotoa elimu upandaji wa mimea, ndio chanzo kinachorejesha nyuma shughuli za kilimo katika kisiwa hicho.
Hali hiyo inatokana na hali halisi ya kisiwa hicho kuzunguukwa na mawe jambo ambalo husababisha kutoimarika kwa mazao wanayozalisha kwa ajili ya chakula ili kukabiliana na tatizo la njaa ambalo huwaathiri wakaazi wa kisiwa hiucho katika kipindi cha ukame.
Miongoni mwa mazao wanayozalishwa na wakazi wakisiwa hicho ni pamoja na mihogo,mahindi choroko,mtama na viaazi vitamu.
Aidha walisema kuwa pindipo serekali itakapowapatia wataalam utawawezesha wananchi hao kujiimarisha kiuchumi na kiondokana na utegemezi.
Nae sheha wa sheha wa shehia hiyo Nyange Vuai Nyange alisema kuwa mbegu ni kikwazo kikubwa kinacho wakabili wananchiwa eneo hilo hawana uwezo kununua mbegu wanazozikitaji katika misimu ya kilimo.
Hivyo aliiomba serekali kuwapatia mbegu za mazao mbalimbali ili waweze kuzalisha kama wanavyozalisha wananchi wa maeneo mbali mbali hapa nchini .

WANAFUNZI WASUFA ZIARANI KILIMANJARO , MANYARA.

Wanafunzi wa Sufa ziarani Kilimanjaro, Manyara

Na Ameir Khalid
JUMLA wanafunzi na walimu 55 wa skuli ya sekondari ya Sufa iliopo Tomondo wilaya ya Magharibi wako kwenye ziara ya kimasomo katika Mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha kwa lengo la kujifunza.
Walisema kuwa katika ziara hiyo ya wiki moja ambayo walitembelea sehemu tofauti imewajengea uelewa mzuri, kwa kufahamu Geografia ya Mikoa hiyo ambao utaweza kuwasaidia kwenye kujibu mtihani wao mwishoni mwa mwaka.
Katika ziara hiyo wanafunzi hao ni wenyeji wa skuli ya Ufundi ya Moshi iliyopo wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, wakiwa katika Mkoa wa Kilimanjaro watapata fursa ya kupanda mlima mkubwa kuliko yote barani Afrika, Kilimanjoro.
Pamoja na kutembelea maporomoko ya maji katika kijiji cha Materumi yanayotirikia katika ziwa la nyumba ya Mungu ambalo linasaidia kutoa kiwango cha umeme wa megawati 8 kwenye gridi ya taifa.
Katika Mkoa wa Manyara walitembea katika msitu wa hifadhi wa Tarangere ambapo walipata kuona aina mbali mbali za wanyama, sambamba na kujuwa historia kamili ya hifadhi hiyo na aina ya wanyama waliomo katika hifadhi.
Wanafunzi hao walimalizia ziara yao kwa kutembea katika Mkoa wa Arusha na kupata kuona hifadhi ya nyoka, sambamba na kupata kufahamishwa historia ya kabila la wamasai ambalo bado linaonekana kuwa na nguvu pamoja na kuvishwa mavazi ya kabila hilo.
Akizungumzia na mwandishi wa habari hizi mwalimu mkuu wa skuli ya Sufa, Abubakar Suleiman alisema kuwa ziara hiyo ni moja ya mipango ya skuli yake, ambayo kila baada ya muda huwatembeza wanafunzi sehemu tofauti kwa lengo la kujifunza zaidi.
Alisema kuwa ziara kama hizo ni mzuri katika kuzidisha ufahamu wa wanafunzi hivyo skuli itaziendelezai kwa manufaa ya wanafunzi wake katika kufahamu mambo tofauti juu ya masomo yao ya darasani.

Friday 29 April 2011

BALOZI SEIF KUMUWAKILISHA DK. 'SHEIN MAY DAY'

Balozi Seif kumuwakilisha Dk. Shein ‘May Day’

Asya Hassan na Kauthar Abdalla
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kumuwakilisha rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kilele cha siku ya wafanyakazi duniani ‘May Day’.
Katibu Mkuu wa shirikisho la Wafanyakazi Zanzibar, Khamis Mwinyi Mohammed alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Kikwajuni mjini hapa.
Kilele cha siku ya Wafanyakazi duniani hapo awali kilikuwa kifanyike katika kiwanja cha Amaan mjini hapa lakini habari zilizokuwepo ni kwamba sherehe hizo zitafanyika katika viwanja vya hoteli ya Bwawani, huku maandamano yakitarajiwa kuanzia viwanja vya Malindi.
Katibu huyo alisema kutokana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mainduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kuwa ziarani nchini Uturuki, Balozi Seif atamuwakilisha Rais kwenye hafla hiyo inayofanyika kila mwaka duniani kote.
Alisema siku moja kabla ya Rais kuondoka nchini, maofisa wa shirikisho hilo walipata fursa ya kuzungumza naye ambapo katika mazungumzo hayo Dk. Shein aliwaomba radhi kutokana na kutokuwepo kwake kwenye sherehe hizo.
“Rais alituomba radhi nasi tumemuelewa kwani ziara yake ni muhimu kwa nchi yetu, na akatueleza kama ingewezekana zinge sogezwa mbele sherehe hizo, jambo ambalo haliwezekani”, alisema katibu huyo.
Katika hatua nyengine katibu huyo alisema ipo tamaa kubwa ya serikali kuwapandishia mishahara watumishi wake.
Alisema Rais ameahidi kuipandisha mishahara ya watumishi kauli ambapo pia imetolewa na baadhi ya mawaziri wanaohusika na masuala ya fedha na utumishi.
Hata hivyo katibu huyo alisema hajajua mshahara huo utapandishwa kwa kima gani kutoka kima cha chini cha shilingi 100,000 kwa mwezi hivi sasa.
Katibu huyo alisikitishwa na hali inavyoendelea ya wafanyakazi kuendelea kupokea mshahara usio na nyongeza kwa hata miaka 20.
“Mfanyakazi Zanzibar anaweza kupokeza kima cha chini kwa miaka 20 kama haijatokea fursa ya kupandisha mishahara”, alisema.

KADA YA UDAKTARI IREJESHEWE HESHIMA

Kada ya Udaktari irejeshewe heshima

Wanaojiita madaktari bila sifa wapondwa
Na Mwanajuma Abdi
WAZIRI wa Afya Juma Duni Haji ameitaka Bodi ya Baraza la Madaktari kufanya kazi zao kwa kufuata maadili na sheria ili waweze kurejesha heshima ya kada hiyo.
Kauli hiyo aliitoa jana, wakati akizindua Bodi hiyo katika ukumbi wa Wizara ya Afya, Mnazi Mmoja mjini Zanzibar.
Bodi ya Baraza hilo ni Mwenyekiti wake Dk. Malik Abdullah Juma na wajumbe ni Dk. Shaaban Issa Mohamed, Dk. Semeni Shaaban Mohammed, Dk. Hakim Gharib Bilal, Dk. Yunus Pandu Buyu, Dk. Omar Saleh Omar, Omar Juma Khatib, Dk. Faiza Kassim Suleiman na Fatma Saleh Amour.
Waziri Duni alisema Bodi hiyo ina kazi kubwa ya kusimamia maadili ili kuipa heshima taaluma hiyo, ambapo huko nyuma imepoteza muelekeo kutokana kuvujisha siri za wagonjwa na baadhi ya watu kujiita madaktari wakati hawana sifa hizo.
Alisema taaluma yeyote isiyokuwa na maadili haiwezi kufika mbali, ambapo alitoa mfano fani ya ualimu nayo imepoteza muelekeo kutokana na baadhi ya walimu kufanya mapenzi na wanafunzi hadi kuwapa ujauzito.
Waziri Duni alisema si vyema kila mtu akajiita daktari wakati hana sifa hiyo kwa vile mwili wa binadamu si sawa na kuchinja mbuzi na ng’ombe.
Aliongeza kusema kumekuwa na wimbi kubwa la watu kijiita madaktari wakati hawana sifa hizo, lakini Bodi hiyo itafuta kasoro hizo zilizokuwa zinajitokeza huko nyuma.
Aidha alisema kuwa Bodi hiyo ina jukumu kubwa la kuhakikisha siri za wagonjwa hazitolewi kwani ni moja ya jambo lenye kukiuka maadili ya kazi zao.
Alifahamisha kuwa, Baraza lililojiuzulu lilikuwa na madai mbali mbali ikiwemo kuingiliwa uhuru katika utendaji ambapo aliahidi kuwa hilo halitotokea kama ilivyokuwa Bodi ililopita labda wawe na mambo yao mengine.
Hata hivyo aliwataka wafanye kazi vizuri bila ya woga na kamwe uongozi hautoingiliwa na watafuata sheria na kanuni zilizopo.
Aidha alifahamisha kuwa, utendaji wa kazi uanze mara moja na wasisubiri hadi mabadiliko ya sheria, ambapo muda utakapofika wa marekebisho hayo yatafanywa huku utekelezaji ukiendelea.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari, Dk. Malik Abdullah alisema uteuzi wa Baraza hilo unafanyika kila muda wa miaka mitatu.
Alieleza mambo ya kuzingatiwa ni pamoja na kufanyiwa marekebisho ya baadhi ya vipengele vilivyokuwemo katika sheria pamoja na kuomba wasiingiliwe katika utendaji wao wa kazi.
ENEO la Soko la Marikiti  likiwa na  nafasi baada ya kuwaondowa wafanyabiashara ya kupanga bidhaa zao chini mbele ya soko hilo na kuleta   msongamano wa wananchi wanaofika kupata huduma ya bidhaa mbalimbali wakati wa asubuhi.(Picha na Othman Maulid)

MASHIRIKA YAWAANDAMA WALIMU 'VITANGI'

Mashirika yawaandama walimu ‘vitangi’

Na Mwandishi Wetu, Dar
VIONGOZI wa mashiriki sita yanayotetea haki za binadamu na maendeleo wamependekeza hatua zichukuliwe kurejesha maadili ya kitaifa na kuwaadhibu vikali walimu wanaowapa mimba wanafunzi.
Wamesema bila kuchukua hatua madhubuti kurejesha maadili ya taifa, sekta ya elimu itaendelea kushuhudia ongezeko la mimba maskulini na hivyo kukwamisha jitihada za taifa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.
Wamesisitiza kuwa walimu wanaobainika kufanya mapenzi na kuwapa mimba wanafunzi wafukuzwe kazi, washitakiwe kwa kosa la kubaka na walazimishwe kulipa fidia za matunzo ya mtoto anayezaliwa.
Wamewahimiza wanafunzi hasa wasichana kuwafichua bila kuona woga au unyanyapaa walimu wote wanaofanya mapenzi na wanafunzi ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, katika kipindi cha miaka mitano, 2004-2008, jumla ya wanafunzi 28, 590 wakiwepo 11,599 wa sekondari na 16,991 wa skuli za msingi, walikatisha masomo kwa kupata mimba.
Viongozi hao waliozungumza na TAMWA kwa nyakati tofauti wiki hii ni Mkurugenzi Mtendaji wa ForDIA, Bubelwa Kaiza, wa Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Ussu Mallya na wa Chama cha Wanawake Wanasheria (TAWLA) Ann Marie Mavenjina.
Wengine ni wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) Scholastica Jullu, wa shirika la Kutetea Haki za wanawake Kivulini lenye makao yake Mwanza, Maimuna Kanyamala na Mkurugenzi wa Utetezi na uboreshaji wa sera na shirika, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Utafiti wa habari zinazochapishwa unaonesha kuwa katika kipindi cha miezi minne kuanzia Desemba 2010 hadi mwisho wa mwezi Machi mwaka huu matukio 11 ya wanafunzi kupata ujauzito walimu ndio waliohusika.
Viongozi hao wanaharakati wamesema wanafunzi kukatishwa masomo kwa mimba kunasababisha madhara mengi kwa taifa ikiwa ni pamoja na ongezeko la ujinga na umaskini miongoni mwa wanawake, vifo vinavyotokana na ujauzito na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU).
Utatifi wa kitaifa (Demographic Health Survey) uliofanyika mwaka 2010 unaonyesha vifo vya uzazi bado ni tatizo kubwa la kitaifa ambapo zaidi ya wanawake 8,000 wanakufa kila mwaka hapa nchini kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika.
Kwa upande wa maambukizi ya VVU utafiti wa kitaifa uliofanyika 2007/2008 unaonyesha kuwa idadi ya asilimia 5.7 ya Watanzania wote wameambukizwa lakini wanawake na wasichana ndio wameambukizwa zaidi ambapo asilimia 6.6 ya idadi yao nchini wameambukizwa ikilinganishwa na asilimia 4.6 ya wanaume.

WANAOWATUHUMU UFISADI ROSTAM,LOWASA WAKATHIBITISHE MAHAKAMANI.

Wanaowatuhumu ufisadi Rostam, Lowasa wakathibitishe mahakamani

Na Nalengo Daniel, Morogoro
KADA wa Chama cha Mapinduzi (CCM), David Msuya amewataka wanaodai kuwa mbunge wa jimbo la Igunga Rostam Azizi, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Monduli Edward Lowasa kuwa ni mafisadi wakathibitishe mahakamani badala ya kuendeleza fitina.
Kada huyo alisema hayo mjini hapa wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ,na kwamba serikali haijawahi kutoa tamko juu ya watuhumiwa hao, na shutuma ya ufisadi inayozungumzwa na baadhi ya watu na kwamba hayo ni majungu yanayotengezezwa na watu wachache.
Alisema kuwa wanaodai kuwa Rostam Azizi na Lowasa ni wafisadi anatakiwa kwenda mahakamni wakiwa na ushahidi wa kutosha na kueleza hizo fedha ziliibiwa wapi na kwa ushahidi upi ili wananchi wawelewe badala ya kuongea bila uthibitisho.
“Hili suali linashangaza kwa nini chama kiseme serikali ikae kimya? na kama ni kweli ni mafisadi, kwa nini serikali isitoe tamko”, alihoji kada huyo.
Msuya alisema kuwa ni nani wa kumwamini ndani ya Chama na kwamba watu wanaosema kuwa watu hao ni mafisadi wanatakiwa kutambua kuwa hao ni watumishi wa serikali kupitia vyama vyao.
Aliwataka watu wanaowanyoshea vidole, kuacha tabia hiyo kwa kuwa kufanya hivyo ni kumdhalilisha mtu bila ushahidi na kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Aidha kada huyo alisema kuwa Mwananchama wa CCM ikiwa amekosea huitwa kwenye kamati ya maadili na kuonywa na masuala hayo hutakiwa kuishia ndani ya chama.
Alisema anashangazwa na tabia ya baadhi ya viongozi ‘CCM’ ambao wamekuwa wakitoa taarifa za siri zinazotakiwa kubaki ndani ya chama na kuhoji kuwa huo ndiyo utaratibu wa chama?
Hata hivyo kada huyo amesema kuwa pamoja na kutishwa na badhi ya viongozi kutokana na msimamo wake, hataacha kuendelea kuwatetea wasio na makosa, na kwamba kwenye ukweli ataongea.

MIFUKO YA PLASTIKI IMEJAA MJINI

Mifuko ya plastiki imejaa Mjini

Na Halima Abdalla
ZAIDI ya kilo 1,500 za mifuko ya plastiki imekamatwa katika maeneo mbali mbali ya masoko Mkoa wa Mjini Magharibi.
Hayo yameelezwa na Afisa elimu ya Mazingira, Hamza Rijaal, kutoka Idara ya Mazingira alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu huko ofisini kwake Maruhubi.
Hamza alisema mifuko hiyo imekamatwa katika masoko mbali mbali ikiwemo soko la Mwanakwerekwe, Malindi, Darajani, Mombasa, Mikunguni na kwa Haji tumbo.
Alieleza kuwa lengo la kuikamata mifuko hiyo ni kuufanya Mji kuwa katika haiba ya kupendeza na muonekano na haiba ya kupendeza.
Alisema kuwa baada ya kukamatwa kwa mifuko hiyo Idara ya mazingira iliamua kwenda kuichoma moto katika eneo la Maruhubi ili moshi wake usiweze kuleta madhara wa wananchi waliokatika maeneo ya karibu.
Alifahamisha kuwa kabla ya kuipeleka Maruhubi walikuwa na wazo la kutaka kuipeleka Dar esSaalam kwenda kuichoma moto katika tanuri kubwa lililopo huko.
Aidha alisema mtu yeyote atakaekamatwa na mfuko wa plastiki japo mmoja atatakiwa kulipa faini kuanzia 500,000 mpaka milioni 1500,000 au kwenda jela miezi 6 au kutumikia adhabu zote mbili.
Alisema kuwa Idara yao sasa imejipangia kwa kila siku asubuhi kufanya opresheni kwa kupita katika maeneo mbali mbali ya masoko kukamata mifuko ya plastiki ili kuepusha kueneo mifuko hiyo katika maeneo ya Mji hasa katika kipindui hiki cha masika ili kuepusha maradhi ambayo yanatokana na uchafu.
Sambamba na hayo Afisa huyo alitoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kuacha kutumia na kuuza mifuko ya plastiki ili kuepusha matatizo yasiokuwa na lazima.

MWERA, KIANGA UHALIFU JUU.

Mwera, Kianga uhalifu juu

Na Ramadhan Himid, POLISI.
KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amewataka wananchi wa Mwera Meli sita, Mtofaani na Kianga kuanzisha kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii ili kupunguza uhalifu kwani takwimu zinaonyesha kuwa uhalifu umepanda kwa kasi katika maeneo yao wanayoishi.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii katika shehia za Mwera Meli sita, Mtofaani na Kianga katika mfululizo wa ziara zake za kutembelea shehia mbali mbali ili kuweka mikakati imara ya kukabiliana na uhalifu nchini.
Alisema takwimu zinaonesha kwamba mwaka 2009/2010 matokeo makubwa ya uhalifu yamepungua lakini kuna maeneo bado uhalifu wa uvunjaji, dawa za kulevya, wizi wa mazao, mifugo na uhalifu mwengine umekuwa ukipanda mno siku hadi siku.
Alisema kwa upande wa makosa ya uvunjaji kipindi cha mwaka huu 2011 mwezi Januari pekee makosa yaliyoripotiwa maeneo ya Mjini ni matatu(3) wakati Mwera na Kianga ni makosa 14 na mwezi Februari makosa ya uvunjaji Mjini ni kosa moja tu wakati Mwera na Kianga ni 16.
“Nimekuwa nikijiuliza masuali mengi kichwani mwangu kwa nini Mjini ambako kuna idadi kubwa ya watu uhalifu unapungua lakini maeneo ya Mwera na Kianga uhalifu umekuwa ukipanda kwa kiwango kikubwa, nadhani inatokana na nyinyi wenyewe kuwa hamjajipanga kwani huko Mjini Kamati za ulinzi na usalama zinafanya kazi na ndio maana wahalifu hao wanakimbilia maeneo yenu”, alisema Kamishna.
Alisema Kamati za Ulinzi na Ustawi wa jamii ni muhimili muhimu wa kutatua kero za uhalifu kwani zipo Shehia ambazo zilikuwa na matatizo sugu ya kihalifu lakini baada ya kuanzishwa kwa Kamati hizo Uhalifu umepungua.
Alibainisha kwamba iwapo Kamati hizo zitafanya vikao mara kwa mara, kupeana taarifa na kuzipatia ufumbuzi taarifa hizo, vitendo vya kihalifu vinaweza kutoweka lakini kama wataendelea kuoneana muhali miongoni mwao watajikuta wakiishi katika hali ya wasi wasi.
Aidha aliwataka wananchi hao kuunga mkono falsafa ya Polisi Jamii kwani Majeshi yote duniani yenye sura ya upolisi yamefanikiwa kupunguza uhalifu kwa kuwashirikisha wananchi, na kumtaka kila mwananchi ashiriki kikamilifu kwa nafasi yake aliyo nayo katika kukabiliana na uhalifu ambao umekuwa ukirejesha nyuma harakati za kiuchumi.
Alisema Polisi Jamii ni sera kama zilivyo sera za vyama na taasisi nyengine hivyo sera hiyo ni sera ya majeshi yote duniani inayotilia mkazo ushirikishwaji wa jamii katika kutatua kero za uhalifu, kwani bila ya kuwepo mashirikiano ya dhati kati ya pande hizo mbili suala la usalama litabakia kuwa ndoto.
Alisema Polisi Jamii/Ulinzi Shirikishi ni ushirikishwaji wa wananchi katika suala zima la kukabiliana na kero mbali mbali zilizomo ndani ya jamii yao inayowazunguka ili wananchi hao waweze kufanya shughuli zao za maendeleo kwa hali ya amani na usalama.
Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya Mwera, Shani Omar Mbena alikiri kuwa uhalifu katika maeneo ya Mwera umekuwa mkubwa na hivyo wananchi hawanabudi kuyaunga mkono yale yote yaliyotolewa na Kamishna kwa faida ya kujilinda wao wenyewe na mali zao.
Diwani huyo alimpongeza Kamishna Mussa na kusema kwamba amekuwa ni mfano kwani tokea kuzaliwa kwake hajawahi kumuona Kamishna wa Polisi akipita kwa wananchi kusikiliza kero zao.

UZINDUZI MASHINDANO YA KLABU BINGWA AFRIKA MASHARIKI NA KATI ZANZIBAR.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akirusha mpira kuashiria kuyazinduwa Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati  yanayofanyika katika Uwanja wa Gymkhana. ikizikutanisha timu za NIC ya Uganda na Mafunzo ya Zanzibar.(Picha na Othman Maulid)

BALOZI SEIF KUKATA UTEPE NETIBOLI A/MASHARIKI LEO

Balozi Seif kukata utepe netiboli A/Mashariki leo

Mafunzo, NIC Uganda wanawake kufungua dimba
Na Salum Vuai, Maelezo
PAZIA la mashindano ya mchezo wa netiboli kwa klabu za Afrika Mashariki, linatarajiwa kufunguliwa leo kwenye uwanja wa Gymkhana Maisara mjini hapa.
Ufunguzi huo utafanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambaye amepangwa kuwa mgeni rasmi katika siku ya kwanza ya michuano hiyo, ambapo kutashuhudiwa pambano kati ya timu ya NIC kutoka Uganda na Mafunzo ya Zanzibar kwa upande wa wanawake.
Kwa mujibu wa ratiba ya sherehe za ufunguzi iliyotolewa na Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA), timu zote zinazoshiriki mashindano ya mwaka huu zinatakiwa kuwa zimefika uwanjani ifikapo saa 8:00 mchana.
Mara baada ya mgeni rasmi kuwasili mnamo saa 10:00, wachezaji wa timu zote watapita mbele yake na wageni waalikwa kwa ajili ya maamkizi, wakiongozwa na bendi ya Jeshi la Polisi Zanzibar, na baadae wanamuziki wa bendi hiyo watapiga nyimbo za mataifa yote shiriki.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa waamuzi wa mashindano hayo watakula kiapo cha utii na baadae kusomwa taarifa fupi ya michuano, kabla Rais wa Shirikisho la Netiboli Afrika Mashariki kutoa shukurani, kitendo kitakachofuatiwa na nasaha za mgeni rasmi.
Aidha Balozi Seif Ali Iddi atakagua timu na baadae kurusha mpira ikiwa ishara ya kuyafungua mashindano hao yanayoshirikisha timu za mchezo huo za wanawake na wanaume kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
Mbali ya mgeni rasmi, waalikwa wengine watakaoshuhudia ufunguzi huo ni watendaji wa ngazi mbalimbali kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, wadau na wapenzi wa michezo.
Timu kadhaa miongoni mwa zile zinazoshiriki mashindano hayo, ziliwasili Zanzibar jana alasiri, huku nyengine zikitarajiwa kufika leo.
Kaimu Katibu wa CHANEZA Rahima Bakari Abdi, amesema ratiba kamili ya mashindano hayo itapangwa leo baada ya timu zote kuwasili nchini

KITAMBI NOMA WAPELEKA MAZOEZI PEMBA.

Kitambi noma wapeleka mazoezi Pemba

Na Abdi Suleiman, Pemba
JAMII kisiwani Pemba, imeshauriwa kuwa na mwamko wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kujiepusha na maradhi mbalimbali.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Mipango wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Pemba, Khatib Juma Mjaja, alipokuwa akizungumza na wanamichezo wa kikundi cha 'Kitambi noma' katika uwanja wa michezo Gombani.
Mjaja ambaye alikuwa akimuwakilisha Afisa Mdhamini wa wizara hiyo, alisema kuwa mazoezi ni chanzo kizuri cha kujenga afya bora kwa mwanadamu, pamoja na kuwa mazoezi ni urafiki na pia husaidia kuuweka mwili vyema na uwezo wa kujihami na matukio mbalimbali ya ghafla.
Alisema wizara yake itakuwa bega kwa bega na vikundi vinavyojihusisha na mazoezi ya viungo ili viwe endelevu, ikiamini kuwa taifa litajengwa na watu wenye afya nzuri, na kwamba mazoezi ni njia muhimu ya kutokomeza maradhi kama sukari, shindikizo la damu, kupunguza mafuta mwilini na kujijenga kisaikolojia.
Naye Katibu wa kikundi hicho Amina Talib, alisema kuwa bado mwamko wa kujiunga na vikundi vya mazoezi kisiwani Pemba ni mdogo, kwa vile watu wengi hawajui wapi pa kuanzia katika kujiunga na vikundi hivyo.
“Mtu mmoja hawezi kufanya mazoezi akiwa peke yake, bali watu wakijiunga pamoja wataweza kujiimarisha na kufanya vizuri", alisema Amina.
Alieleza kuwa lengo la ziara yao kisiwani Pemba, ni kuishajiisha jamii ili ihamasike kufanya mazoezi kwa manufaa yao na taifa kwa jumla.
Katika ziara hiyo, wanachama 50 kati ya 100 wa kikundi cha 'Kitambi noma', walitembelea wilaya tafauti za Pemba kwa muda wa siku tatu kushajiisha uundwaji wa vikundi kama hivyo.

HABARI YATINGA FAINALI IKIIZIMA ZECO.

Habari yatinga fainali ikiizima ZECO

Na Mwajuma Juma
TIMU ya soka ya Wizara ya Habari, imefanikiwa kuingia fainali ya mashindano ya 'May Day', baada ya kuilaza Shirika la Umeme (ZECO) mabao 5-2 katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza uliochezwa juzi kwenye uwanja wa Amaan nje.
Katika mchezo huo uliochezwa juzi, wakata umeme walionekana kuzidiwa mno na kushindwa kutumia koleo na pakari zao kuwakatia umeme vijana hao wa Habari Sports ambao hivi juzi tu wametoka katika mashindano ya NSSF walikoishia robo fainali.
Vijana wa Habari ambao walionesha mchezo mzuri na soka la kufundishwa, walifungiwa magoi yao na Amour Nassor (mawili)i, Ramadhan Khamis, Abdulghani Mussa na Yussuf Saleh.
Magoli yote ya ZECO katika patashika hiyo, yalipachikwa kimiani na mchezaji Mussa Hassan.
Hata hivyo, hatima ya Habari Sports kama itacheza fainali au la, itajulikana baada ya kusikilizwa rufaa iliyokatwa na wapinzani wao waliodai kuwa timu hiyo ilichezesha majeshi ya kukodi (mamluki).
Michuano hiyo inayoshirikisha timu za mashirika na wizara za serikali, imeandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), ikiwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani 'May Day', ambapo fainali yake itachezwa keshokutwa siku ya kilele cha sherehe hizo.

MJASIRIAMALI AZOA KITITA CHA COCA COLA

Mjasiriamali azoa kitita cha Coca Cola

Na Mwanajuma Abdi
KAMPUNI ya vinywaji baridi 'Zanzibar Bottlers Ltd', imekabidhi zawadi ya fedha kwa washindi wa promosheni ya kamata kitita na Coca Cola.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika jana katika kiwanda cha Coca Cola huko Muembemakumbi, ambapo Meneja Uzalishaji wa kampuni hiyo Ally Kassim alimkabidhi Jabir Amour Dadi shilingi 1,000,000 baada ya kushinda kutokana na kunywa soda za kampuni hiyo.
Aidha Meneja Ufundi wa kampuni hiyo Amour Ally, aliwakabidhi washindi wawili wa shilingi laki tano kila mmoja, ambao ni Makame Juma Makame na Rajab Ibrahim Khamis.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Meneja Mauzo Haji Khatib, alisema promosheni ya kamata kitita na Coca Cola inaendelea hadi kesho Aprili 30, ambapo zawadi zitaendelea kutolewa hadi Mei 15.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kunywa soda za Coca Cola, Sprite na Fanta, ili waweze kujishindia fedha, akisema zawadi zipo nyingi zikiwemo shilingi 100,000, 50,000, 10,000, na 1,000 pamoja na soda za bure.
Akielezea furaha yake, Jabir Amour mkaazi wa Darajabovu aliyeshinda shilingi milioni moja, alisema fedha hizo zitamsaidia kuongeza mtaji wa biashara zake ndogondogo alizojiajiri.
Nae mshindi wa shilingi laki tano Makame Juma Makame, alisema baada ya kunywa soda kumi na kufanikiwa kushinda zawadi hiyo, atajiimarisa zaidi katika biashara yake ya samaki hapo Malindi.
Promosheni ya kamata kitita na Coca Cola ilianza katikati ya mwezi wa Machi mwaka huu..

Thursday 28 April 2011

RAIS WA ZANZIBAR SAFARINI UTURUKI.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akizungumza  na Makamu wa Kwanza wa Rais  Zanzibar Maalim Seif Shariff, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume  kabla ya kuondoka Nchini kwenda Nchini Uturuki.(Picha na Othman Maulid) 

MESHEHA, MADIWANI PEMBA WATAKIWA KUSHIRIKIANA.

Masheha, Madiwani Pemba watakiwa kushirikiana

Na Bakari Mussa, Pemba
MASHEHA na Madiwani kisiwani Pemba, wametakiwa kufanya kazi pamoja na kujenga ushirikiano ili kupeleka mbele maendeleo ya wananchi chini ya Serikali ya Awamu ya Saba ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Akizungumza na viongozi hao wa wilaya ya Mkoani, katika ufunguzi wa mafunzo ya uongozi juu ya Mfumo wa Serikali hiyo kwa Viongozi, katika ukumbi wa Umoja ni Nguvu Mkoani, Afisa Mdhamini Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba, Jokha Khamis Makame, alisema Wazanzibari hawana budi kuufuata mfumo huo kwa vile wameukubali wao wenyewe kwa kuelewa kuwa utakuwa na maslahi kwao.
Alisema viongozi hao hawana budi kuwaelimisha dhana nzima ya utawala bora pamoja na utawala wa sheria, kwani huo ni chachu ya maendeleo jambo ambalo Zanzibar imepiga hatua kubwa na sasa amani na utulivu imeendelea kudumishwa.
Afisa huyo, alieleza pamoja na changamoto zinazowakabili viongozi hao lakini Serikali imo mbioni kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria zake kama vile Sheria No. 1/1998 na Sheria N. 3 na 4 ya mwaka 1995, ili ziandane na wakati wa sasa ziweze kufanya kazi ipasavyo kutokana na mfumo huo.
Nae Afisa Tawala wa Wilaya hiyo , Abdalla Salim Abdalla, aliishukuru Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kutoa mafunzo hayo kwa viongozi hao ambao wako karibu sana na wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa maendeleo kwa nafasi walizonazo.
Alisema maelezo yaliotolewa na Afisa Mdhamini huyo, ameahidi kuyafanyia kazi katika wilaya yake kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya hiyo, hatua kwa hatua kwa kujenga mashirikiano ya pamoja kwa lengo la kuijenga nchi yao.
Alifahamisha kuwa changamoto zilijitokeza hapo nyuma tayari zimeanza kufanyiwa kazi na sasa hivi pande zote zinashirikiana katika masuala ya kijamii na ya kiserikali bila ya kujali itikadi zao.
Aidha Mkurugenzi wa TAMISEMI Zanzibar, Naimu Ramadhani Pandu, aliwataka viongozi hao kuona haja ya ule muda walioupoteza wa malumbano ya kisiasa ambao ulidumaza kwa kiasi fulani harakati za maendeleo sasa wanaufanyia kazi kwa kujenga umoja wa Wazanzibari lengo likiwa kuleta maendeleo kwa pamoja.
Alieleza kuwa mfumo huu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umekuwa na mabadiliko makubwa juu ya suala zima la amani ya nchi na sasa hivi hakuna anaeweza kubisha juu ya suala hilo hasa pale baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.
Hivyo aliwasisitiza kujenga mashirikiano ya pamoja na upendo bila ya kuangalia tafauti zao za itikadi za kisiasa kwa kuelewa wote ni kitu kimoja ni Wazanzibari ambao wanapaswa kuijenga nchi yao.

BIHINDI AITAKA UNICEF KUISAIDIA ZANZIBAR.

Bihindi aitaka UNICEF kuisaidia Zanzibar

Na Zuwena Amour, WHUUM
NAIBU waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis ameliomba shirika la Umoja wa Mataifa lenye kushughulikia watoto (UNICEF), kuendelea kuisaidia Zanzibar.
Bihindi alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na ujumbe wa maofisa wa Shirika hilo waliofika ofisini kwake Kikwajuni mjini hapa.
Alisema UNICEF ni Shirika lenye miradi mbalimbali ya kijamii ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kuwanufaisha wananchi wa Zanzibar.
Aidha Naibu huyo alilipongeza shirika hilo kwa ushirikiano wake na Zanzibar sambamba na miradi ya kijamii inayoisaidia Zanzibar ambayo imekuwa na faida kubwa kwa wananchi.
“Naomba ushirikiano kati yetu uzidi kuimarika kwa faida ya wananchi”, alisema Naibu huyo.
Bihindi pia alitumia nafasi hiyo kuliomba shirika hilo kutoa vifaa mbali mbali pamoja na mafunzo kwa taasisi za habari za Zanzibar.
Nao kwa upande wao maofisa hao wa UNICEF, Ruth Leano na Bisa Cameron walimhakikishia waziri huyo kuwa shirika hilo litaendelea kuisaidia Zanzibar.
Walisema shirika hilo linakusudia kuanzisha programu katika vyombo vya habari ambayo itaelezea athari za mimba za utotoni, elimu ya UKIMWI, matatizo ya wanawake pamoja na udhalilishaji.
Katika ziara hiyo pia maofisa hao waliangalia miradi ambayo wameisaidia wizara hiyo likiwemo gari la sinema ambalo limekuwa likitumika kutolea elimu kwa wananchi.

OMARYUSSUF ; CCM HAIYUMBISHWI NA HILA ZA MAFISADI

Omar Yusuf: CCM haiyumbishwi na hila za mafisadi

Na Ismail Mwinyi
MJUMBE wa Kamati Kuu CCM, Omar Yussuf Mzee amesema chama hicho kikongwe nchini, hakitayumbishwa na wala kubabaishwa na hila za mafisadi.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati wa sherehe za uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama katika Jimbo la Kikwajuni, sherehe zilizokwenda sambamba na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo Hamad Yussuf Masauni.
Alisema mafisadi hawana nguvu za kukitambia chama hicho na wasidhani kuwa wanaweza kukidhoofisha kwani CCM iko imara, haitishiki na wala kushughulishwa na mafisadi.
Mzee aliwaeleza wanachama wa Jimbo hilo kuwa Chama cha Mapinduzi, si Chama cha wababaishaji bali ni chama kuendeleza misingi yake ya kuwajali wakulima, wafanyakazi na wanyonge.
Alisema uamuzi wa chama hicho kujivua gamba kwa kujiuzulu sekritarieti ni uamuzi mzuri na wa busara ambao unalenga kuleta maendeleo na mabadiliko ndani ya chama hicho.
Aidha waziri huyo alitoa wito kwa viongozi mafisadi kwenye ngazi za matawi, wadi na majimbo nao kujivua gamba kwa kujiondosha kwenye nyazifa kabla ya kutimuliwa.
Alisema endapo watajiondosha wenyewe watakisaidia chama hicho na wanachama kurejesha imani na kukitumikia chama chao.
Sambamba na hilo aliwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kutokubali kuongozwa na viongozi mafisadi wasio na uchungu na chama ili kuepusha kutokea kwa mgawanyiko wa wanachama wake.
Mzee aliwataka wanachama wa CCM wa jimbo hilo kuongeza mashirikiano na viongozi wao na kuachana na maneno ya mafisadi wasiopenda maendeleo ya jimbo hilo.
Aidha waziri huyo aliwapongeza viongozi na wanachama wa Jimbo hilo kwa kuanzisha mradi wa maji safi na salama ambapo alisema hatua hiyo ni hatua mojawapo ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Waziri Mzee alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza kuimarisha mradi huo ili kuweza kutoa huduma hiyo kwa wananchi wote wa mjini na vijijini.
Nae Mbunge wa Jimbo hilo Hamad Yussuf Masauni, alimueleza waziri huyo kuwa licha ya kuweza kutatua tatizo hilo la maji jimboni hapo mradi huo utaendelea na shughuli zake za kuchimba visima vya ziada pamoja na kuvisaidia vikundi vya ujasiriamali vilivyopo jimboni hapo kwa lengo la kujikomboa na hali ngumu ya umasikini.

MKE WA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS MAMA AWENA ATOA VIFAA KIVUNGE.

MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama  Awena Seif Shariff (kushoto)akimkabidhi Naibu Waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya msaada wa Vifaa vya Hospitali kwa ajili ya Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja, Vifaa hivyo vimetolewa na Umoja wa Kinamama wa CUF.(Picha na  AMKR) 

UDHAIFU, UBINAFSI SUMU YA MUUNGANO -RAZA

Udhaifu, ubinafsi sumu ya Muungano - Raza

Na Ramadhan Makame
MFANYABIASHARA maarufu visiwani Zanzibar Mohammed Raza, amesema matatizo yanayojitokeza kwenye mchakato wa katiba mpya na masuala ya Muungano yanatokana na udhaifu wa watendaji wanaojali maslahi yao binafsi na kuliyumbisha taifa.
Raza alieleza hayo jana katika hoteli Grand Palace, iliyopo Malindi mjini hapa alipokuwa akitoa tathmini aliyoombwa kuitoa juu ya mchakato wa katiba na masuala ya Muungano.
Alisema watendaji wa ngazi za kati ndio wababaishaji wa mambo, ambapo wamekuwa na unafiki, tamaa, uchu na uroho wa madaraka hali inayosababisha kujitokeza kwa matatizo.
“Wakati mwengine tumekuwa tukiwalaumu Watazania bara mengine yanasababishwa na watendaji wetu kwa kuwa wanafiki na wasiojali maslahi ya wananchi”, alisema Raza.
Alisema viongozi wakuu wa nchi wana nia njema ya kuliongoza taifa hili kwa amani na utulivu, lakini uchu wa madaraka na unafiki wa watendaji umekuwa ukiliyumbisha taifa kwa kujali maslahi yao zaidi ya wananchi.
“Wananchi wa Zanzibar ni watulivu, wapenda amani wanaopenda kushirikiana na wasiopenda ugomvi, lakini matatizo yapo kwa hawa wasaidizi wa viongozi wa juu”,alisema Raza.
Raza alisema suala lililo mbele ya wananchi wa Zanzibar ni kusimama pamoja na kujenga hoja wakiongozwa na hadidu rejea ‘terms of reference’ kuwa Zanzibar nchi iliyokuwa huru kabla ya kuungana.
“Hili lazima tuliweke wazi na nimelisema kwa zaidi ya miaka 20, na wabunge wetu walielewe, Zanzibar ilikuwa nchi kamili kabla ya kuungana na wala tusikubali kuburuzwa”, alisema.
Alisema wakati wa wananchi kuwekewa ‘menu’ na kikundi cha watu 20 na kuambiwa haya ndio maamuzi umekwisha, bali washirikishwe kikamilifu katika kila lenye maslahi ya kujenga nchi.
Alisema ufike wakati Watanganyika na Wazanzibari wavumiliane na kila mmoja asione mzigo kwa mwenziwe na kusisitiza kuwa aandamwe mwenye kutaka kuvunja Muungano.
Alisema hata hivyo wakati utakapofika wa kijadili katiba wananchi waruhusiwe aina ya Muungano wanaoutaka na serikali wanazozitaka.
Raza amelezimika kuitisha mkutano huo akidai kuwa ameombwa kufanya hivyo na wananchi wa Zanzibar na hiyo imekuwa kawaida yake kila yanapotokezea masuala yanayolihusu taifa.

MAGUFULI AINGIA HOMA UFISADI KIGAMBONI.

Magufuli aingia homa ufisadi Kigamboni

Na Kunze Mswanyama, Dar
WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli, amevunja ukimya na kuwanyooshea kidole wakala wa serikali wa ufundi na umeme nchini (TEMESA), kukithiri ufisadi na hasa kwenye kivuko cha Magogoni kinachosimamia vivuko vya kwenda na kurudi Kigamboni.
Waziri Magufuli, alieleza hayo alipokuwa akizindua bodi mbili zilizo chini ya wizara yake za wakala wa Majengo na Wakala wa Ufundi na Umeme jijini Dar es salaam, jana kufuatia kuziteua bodi hizo hivi karibuni.
"Boti kubwa yenye uwezo wa kupakia watu zaidi ya 2,000 na magari 60 na ina injini nne nilipokwenda niligundua kuwa zinazofanya kazi ni injini mbili, lakini mafuta yanayoagizwa ni injini zote nne, huu ni ufisadi mkubwa, inaniuma kweli",alisema Dk. Magufuli.
Waziri huyo alisema hayo aliyashuhudia alipofanya ziara ya kushtukiza katika kivuko cha Magogoni na hatimaye kubaini ufisadi ambapo alivaa kanzu na kofia kubwa "pama" hali iliyofanywa watumishi kutomgundua.
“Haiwezekani kivuko hicho kuingiza mapato ya shilingi milioni 7.5 kwa siku ilhali ukaguzi uliofanywa ulionyesha kuwa kuna kila sababu ya kuingiza zaidi ya milioni 10, siku moja nitafanya ziara mimi na Mwakyembe tuone kama hatutapata kiasi hicho",alisema.
Alisema ameamua kuingiza wanajeshi katika bodi hiyo ili kurudisha nidhamu ndani ya chombo hicho kilichoanza kupoteza mwelekeo siku za hivi karibuni.
Wakala huyo ambaye pia aliwahi kulalamikiwa sana na Naibu waziri wa Ujenzi Dk.Harison Mwakyembe kwa ufisadi,umekabidhiwa wanajeshi wawili wenye vyeo vya Ujenerali ili kuongeza uwajibikaji zaidi na hivyo kuiingizia serikali mabilioni ambayo kwa sasa kwa kiasi kikubwa yanaishia kwenye mifuko ya mafisadi.
Aidha, Magufuli aliwataka wajumbe hao ambao watakuwa madarakani kwa muda wa miaka mitano na wakiongozwa na Pro.Idris Mshoro ambaye ni Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Ardhi kufanya kazi kwa bidi ili kuiwezesha wakala huyo kuwa na uwezo wa kujihudumia na hivyo kuboresha mishahara ya watumishi wao.
Pia Magufuli alisema anaamini kuwa kwa kutumia bodi hiyo mpya ya ushauri sasa watahakiksha kuwa magari, mitambo na mashine mbalimbali ya serikali na hata ya watu binafsi inapelekwa kutengenezwa na kufanyiwa marekebisho hapo na hiyo itarudisha heshima yao ilyoanza kushuka tofauti na ilivyokuwa ni Idara ya Ujenzi.
Aidha, alihoji kwa nini magari na mitambo ya serikali ipelekwe kutengenezwa kwenye gereji za "chini ya mwembe" wakati TEMESA wapo nchi nzima na ambapo alitaka kujua kama mafundi wao (TEMESA) hawana ujuzi au wanaiba vifaa kiasi cha kuwakatisha tamaa wateja.
Kwa upande mwingine Magufuli aliisifu Wakala wa Majengo kwa kuwa kupitia kwao serikali imewezesha kujengwa kwa nyumba zaidi ya 1025 ambazo zinaweza kuuzwa kwa watumishi au kuwa za kuishi watumishi waliopo kazini.

RC AWAOMBEA MISAADA WAATHIRIKA MAFURIKO MOROGORO.

RC awaombea misaada waathirika mafuriko Morogoro

Na Nalengo Daniel, Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Luteni Kanali Msataafu Issa Machibya, amewaomba wafanyabiashara, tatasisi zisizo za serikali, mashirika ya dini na watu binafsi kuwasaidia wananchi 6,643 walioathirika na mafuriko yaliyotokea wilayani Kilombero mkoni hapa.
Mkuu huyo alitoa ombi hilo jana mkoani hapa kwenye kikao cha pamoja kati ya uongozi wa mkoa wa Morogoro na wafanyabiashara wa mkoni humo kuangalia namna ambavyo wanaweza kuwasaidia wahanaga hao.
Aliwaomba wananchi kwa ujumla nchini, kuona maafa hayo si ya wilaya ya Kilombero,na mkoa wa Morogoro pekee na kwamba, yanamgusa kila mwananchi bila kujali ni mkazi wa eneo gani.
Akisoma mahitaji muhimu kutokana na mafuriko hayo kwa wafanyabiashara hao kaimu katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro, Stephen Bushir aliyataja kuwa ni tani za mahindi 239.14, maharage tani 59.7, mafuta ya kula lita 38,861, chumvi kilo 1438, na sukari kilo 23,000 na kwamba mahitaji hayo ni kwa siku 90.
Alisema mahitaji mengine ni mbegu za mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na kutaja kuwa ni mahindi ya muda mfupi tani 6 pamoja na vipando vya mbegu ya muhogo mizigo 14,950.
Kaimu huyo alisema kuwa mafuriko hayo yameathiri miundo mbinu ya barabara yakiwemo madaraja 6, na kwamba kila daraja moja linahitaji kiasi cha shilingi milioni 35, ili liweza kukamilika wakati yote yanahitaji kiasi cha shilingi milioni 210 ili yakamilike.
Alisema kwa upande wa barabara shilingi milioni 340 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa barabara zenye urefu wa kilomota 34, wakati fedha ya matengezo ya barabara ya Ifakara Taweta ambayo haipitiki kwa sasa kutokana na kuharibiwa vibaya na mafuriko hayo inahitaji kiasi cha shilingi milioni 949.4.
Jumla ya kata nne za Mofu, Mbingu, Mngeta na Ideta wilayani Kilombero zimehabiwa vibaya na mvua zilizonyesha kuanzia Aprili 20 mwaka huu na kusababisha watu 6,643 kukosa makazi.
Katika mafuriko hayo nyumba 673 zilibomoka na 777 kuzingirwa na maji na hekta 596 zikiwa zimeathiriwa na mafuriko pamoja na upotevu wa mali na vyakula vya wakazi wa kata hizo.

Tuesday 26 April 2011

FIKRA ZA KUVUNJA MUUNGANO ZAPINGWA.

….Fikra za kuvunja Muungano zapingwa

• Lipumba: Ni dhambi kubwa
• Himid Ameir: Ni utashi wa wachache
• Fatma Karume: Wasioutaka wana lao jambo
Na Mwantanga Ame
WAKATI watanzania jana wakiadhimisha miaka 47 ya Muungano, Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipimba, amesema wenye kutoa mawazo ya kutaka kuvunjwa kwa Muungano wasifikirie hata siku moja kuleta dhana hiyo kwani imejaa dhambi na haina faida kwa watanzania.
Profesa Lipumba aliyasema hayo jana wakati akitoa mawazo yake katika maadhimisho ya sherehe hizo zilizofanyika katika kiwanja cha Amaan Mjini Unguja ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tudumishe Muungano matunda ya miaka 47 ya Mapinduzi na miaka 50 ya Uhuru’.
Lipumba alisema, Muungano uliopo ni mzuri, lakini haipaswi kutumia changamoto zilizojitokeza kwa kujenga hoja ya kuuvunja kwani hiyo ni dhana iliyojaa dhambi na haina faida kwa watanzania pindipo wakishikilia wazo hilo.
Alisema wazo la kutaka kuvunjika kwa Muungano ni baya kwani linaweza likaleta athari kubwa kwa baadhi ya watanzania kutokana na kuwa tayari wamezaliwa wakiwa ndani ya muungano bila ya kuzingatia maeneo waishio nchini Tanzania.
Akitoa mfano alisema hivi sasa kuna Wazanzibari 400,000 hawana haki ya kupiga kura Zanzibar, ambao wamezaliwa Tanzania bara na watu wa Zanzibar ambao hawapigi kura Bara kutokana na sheria zilizopo jambo ambalo ikiwa muungano utavunjika hawatakuwa na sehemu ya kushika.
“Kuna athari kubwa ya kibinadamu itayotokea kama tukianza kujenga hoja za kutaka kuvunja muungano na nnawaomba wananchi wasifikirie jambo hili hata siku moja kwani bado kuna jambo la kheri katika Muungano” alisema Lipumba.
Akiendelea alisema ingawa ni ukweli rasimu iliyotayarishwa kwa ajili ya kukusanya maoni ya mchakato wa kupatikana katiba mpya ilikuwa na kasoro zake lakini bado watanzania wanahitaji kutumia nafasi zao kutoa maoni ambayo yatakidhi mahitaji na sio jazba za kutaka kuvunjwa kwa muungano.
Alisema jambo linalotakiwa kufanywa ni kuangalia namna ya vipi wataweza kukabiliana na changamoto zilizopo na kufanyiwa mabadiliko ambayo yataweza kuufanya Muungano kuwa katika hali nzuri miaka 50 ijayo. .
“Jambo la kheri kuwa na muungano ni kweli kuna matatizo lakini yanaweza kutatuliwa na kurekebishwa na kukawepo utaratibu mzuri kupata katiba nzuri sio kuvunja Muungano, kama tunaweza kuliangalia kwa mfumo mwengine basi hayo ndio mambo ya kuyatazama sio usiwepo… hapana” alisema Lipumba.
Nae Mzee wa CCM Hamid Ameir Ali, akizungumzia juu ya mtazamo wake katika sherehe hizo alisema hoja za kutaka kuvunjwa kwa muungano ni utashi wa kilimwengu na haupaswi kufuatwa kwa wanaotoa ushawishi wa aina hiyo.
Alisema hilo linapaswa kuzingatiwa kutokana na Muungano uliopo ni wa kupigiwa mfano kwani ulitokana na nguvu ya kushindwa kwa wakoloni kuzitawala nchi mbili hizi na kuzifanya kuwa huru.
Alisema Changamoto zinazojitokeza za kujengewa dhana hizo ni ukuwaji wa maendeleo jambo ambalo watantazia watapaswa kuona kuwa yanayojitokeza ni maendeleo ya kuudumisha muungano ili waweze kupata manufaa zaidi na sio kuwaza kuuvunja.
Nae mjane wa Muasisi wa Muungano Zanzibar, Mama Fatma Karume, alisema Muungano wa Tanzania ni wa kupigiwa mfano kwani baadhi ya mataifa ndio kwanza wanafahamu umuhimu wa kuunganisha nchi zao.
Alisema kama baadhi ya mataifa yameweza kuunganisha nchi zao na kuwa na aina ya fedha zao kwanini Muungano wa Tanzania nao usionekane kuwa na faida na hoja za kutaka kuuvunja ni sawa na kurejesha nyuma maendeleo hayo.
Mama Fatma alisema hoja ambazo sasa zimekuwa zikitolewa kutaka kuvunjwa kwa muungano hazina msingi na wanaoleta mawazo hao ni kwamba inaonekana kuwa wana jambo lao.
Nae Waziri wa mambo ya Nje Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, alisema Muungano wa Tanzania ni urithi ulio bora kwa wananchi wa Tanzania hasa kwa kizazi cha sasa na haitapendeza kuona urithi huo unapotezwa.
Alisema changamoto ni kweli zipo na hazihitaji kupuuzwa kutokana na kukua kwa maendeleo na jambo ambalo linahitajika kufanywa kwa hivi sasa ni kupatiwa ufumbuzi ili uweze kwenda sambamba na matakwa ya wananchi.
Wananchi mbali mbali walishiriki katika sherehe hizo zilizoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambapo aliweza kukagua gwaride lililotayarishwa na vikosi vya Ulinzi na Usalama ambapo liliweza kuonesha umahiri kwa kutembea mwendo wa pole na haraka kiwanjani hapo na kufanya kushangiriwa kwa vikosi ambavyo vilionekana kufanya vizuri.
Vikosi hivyo ni vya JWTZ, Magereza, Polisi, Askari wa Majini, JKT, KMKM, Mafunzo, JKU na KVZ vilivyokuwa na gadi za askari wanaume na wanawake viliongozwa na kikosi cha bendera na bendi za vikosi hivyo.
Kwenye kiwanja hicho kilionekana kujaa wananchi waliokuwa wakishereheka kwa wakati huku wakipeperusha mabofu yaliokuwa na rangi ya Muungano na kuinua juu vitambara maalum vya bendera ya Muungano na kundi kubwa la wanafunzi wa skuli mbali mbali za Zanzibar waliovalia fulana maalum za muungano ambapo kwa muda wote walionekana kushajiisha sherehe hizo kwa kupiga makofi kwa mtindo maalum.
Viongozi wengine walioshiriki katiks sherehe hiyo ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowasa, nae pia alishiriki katika sherehe hizo na Rais wa Tanzania Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma na Waziri Kiongozi Wastaafu Ramadhan Haji Faki na Shamsi Vuai Nahodha na wake wa viongozi hao Mwaziri wa SMZ na SMT na Makatibu Wakuu na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania na Zanzibar.

WAVUVI WAPEWE ELIMU KUEPUKA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Wavuvi wapewe elimu kuepuka uharibifu wa mazingira

Na Halima Abdalla
JUMUIA ya maendeleo ya jamii na uhifadhi wa Mazingira Zanzibar (CODECOZ), imetakiwa kuelimisha wavuvi kuhusiana na zana bora za kuvulia ambazo haziharibu mazingira ya baharini ikiwemo matumbawe.
Mjumbe wa bodi ya udhamini wa CODECOZ, Dk.Nerrman Jidawi alieleza hayo alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa jumuia hiyo unaohusiana na mapato na matumizi yaliyotumika kwa mwaka uliopita na yatakayotumika kwa mwaka huu uliofanyika katika ukumbi wa Takwimu Mwanakwerekwe mjini hapa.
Aliwataka kuendelea kuelimisha jamii umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira sambamba na kuelimisha wavuvi kuhusu umuhimu wa matumbawe ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii na ni sehemu ya mazalio ya samaki, hivyo yanahitaji kutunzwa ili yaweze kuongeza pato la Taifa.
Aidha aliwataka wanachama wa CODECOZ, kushirikiana na serikali katika kudhibiti suala zima la uingiaji wa mifuko ya plastiki ambayo inaendelea kuzagaa nchini.
Dk. Jidawi alisema suala la kuzagaa kwa mifuko ya plastiki limeenea kila sehemu kwa Zanzibar hasa mifuko inayotokana na mauzo ya bidhaa mbalimbali ambayo imetapakaa mjini pamoja na mifuko inayotumiwa kwa ajili ya kununulia bidhaa.
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Hamza Rijaal, alisema jumuia yao inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa ofisi ya kudumu, ukosefu wa fedha za kuweza kuajiri watendaji wa kudumu pamoja idadi ndogo wa wanachama.
Katika mkutano huo wa mwaka wa jumuia ya CODECOZ kuhusiana na mapato na matumizi yaliotumika kwa mwaka uliopita ambao umeishia na Disemba 2010, umeweza kutumia shilingi milioni 32,264,500 mapato ambayo yanatoka kwa wafadhili pamoja ada za wanachama na michango ya wanachama.
Aidha kwa mwaka huu kuanzia mwezi Januari 2011 hadi Disemba 2011 Jumuia hiyo inategemea kutumia milioni 46,569,000 katika kufanikisha shughuli zao ambazo zitatokana na vyanzo vyao vya mapato.
Jumuia ya CODECOZ imeanzishwa mwaka 1996 na ina wanachama 49.

WALIMU WAPEWE STADI KUWAEPUSHA MIMBA WANAFUNZI

Walimu wapewe stadi kuwaepushia mimba wanafunzi

Na Mwandishi Wetu, Dar
CHAMA cha Walimu Wanawake (TAWOTEA), kimependekeza serikali ilipe kipaumbele suala la elimu ya maadili na stadi za maisha katika vyuo vya ualimu ili kuepusha walimu kuwapa mimba wanafunzi.
Mkurugenzi mtendaji wa TAWOTEA, Neema Kabale alisema utovu wa maadili kwa walimu unasababishwa na udhaifu uliopo katika vyuo vya ualimu ambapo suala la kuwajengea waalimu misingi ya maadili ya kazi yao halipewi uzito unaostahili.
Alisema walimu wana kazi nyeti ya kujenga maadili mema kwa wanafunzi, serikali inapaswa kuhakikisha vyuo vya ualimu vinakuwa na wawezeshaji makini wa kuwajengea walimu maadili mema yanayotakiwa katika kazi yao ili wawe mfano kwa jamii.
Alifahamisha kuwa mwalimu anayekuwa chuoni miaka miwili au zaidi, kama chuo chake kimejiandaa vyema kumjenga kimaadili atakuwa amewiva na atakapokuwa kazini, kama ufuatiliaji wa maadili unafanyika kikamilifu, hatothubutu kujihusisha na mambo yaliyo kinyume na maadili ya kazi yake.
Akizungumza katika mahojiano maalum na TAMWA kuhusu chanzo cha walimu kuwapa mimba wanafunzi, Mkurugenzi huyo wa TAWOTEA alisema walimu wengi siku hizi wamepotoka kimaadili kwa sababu vyuo vingi vinavyofundisha kazi ya ualimu vinafanya kazi hiyo kwa mtindo wa “bora liende”.
Alitaja jambo jengine linalofanya walimu kukosa maadili na hivyo baadhi kujiingiza katika mapenzi na wanafunzi kuwa ni walimu kutopatiwa mafunzo mara kwa mara kuhusu stadi za maisha ili kuweza kujiepusha na vishawishi vinavyotokana na mazingira yanayobadilika.
Kabale alisema mwalimu anaweza kufanya kazi hata kwa kipindi cha miaka 20 bila kupatiwa mafunzo au stadi zozote zenye kumsaidia kujikumbusha masuala ya maadili ya kazi yake.
Mkurugenzi alisema kuwajengea uwezo waalimu walioko kazini kuhusu stadi za maisha zinazoweza kuwasaidia kuepuka vishawishi vya kufanya mapenzi na wanafunzi kunaweza kufanywa na taasisi, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyama vya walimu na vyombo vya habari.
Alifahamisha kuwa suala la kupambana na tatizo la mimba maskulini linahitaji serikali kuweka rasilimali zaidi kuboresha vyuo vya ualimu na wadau wengine nje ya vyuo kuwa wabunifu na kujitolea kufanya shughuli zitakazoelimisha na kuhamasisha wale wote wanaofanya mapenzi na wanafunzi kuacha tabia hiyo.
Utafiti wa habari zinazochapishwa na magazeti kuhusu masuala ya mimba mashuleni unaonesha kuwa katika kipindi cha miezi minne kuanzia Disemba 2010 hadi mwisho wa mwezi Machi mwaka huu matukio 11 ya wanafunzi kupata ujauzito yalihusisha walimu.
Aidha tatizo la wasichana kukatisha masomo kutokana na mimba ni kubwa hapa nchini, ambapo kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, katika kipindi cha miaka mitano, 2004-2008, jumla ya wanafunzi 28,590 wakiwepo 11,599 wa sekondari na 16,991 wa skuli za msingi, walikatisha masomo kwa kupata mimba.

WENYE MAHITAJI MAALUM WANA HAKI KUPEWA ELIMU - MKURUGENZI

Wenye mahitaji maalum wana haki ya kupewa elimu - Mkurugenzi

Na Luluwa Salum, Pemba
WALIMU wanaofundisha skuli zenye vituo vya elimu mjumuisho wametakiwa kutowabagua watoto wenye mahitaji maalumu na kuhakikisha wanawapatia elimu sawa na watoto wengine.
Akizindua vituo vya Elimu mjumuisho katika skuli za Kangani na Michenzani Pemba, Mkurugengezi Idara ya Elimu Msingi Zanzibar, Uledi Juma Wadi, alisema Elimu ni haki ya kila mtu, hivyo kuna ulazima wa kupatiwa bila ya ubaguzi wowote.
Mkurugenzi huyo alisema watu wenye mahitaji maalumu ni sawa na binaadamu wengine wa kawaida hivyo suala la kupewa alimu ni haki yao ya msingi miongoni mwa haki za binaadamu.
Alisema serikali imeona umuhimu wa kuwepo vituo hivyo katika skuli mbali mbali za Zanzibar, ikiwa lengo ni kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata elimu.
Aliwataka wazazi na walezi kutowafungia ndani watoto wao wenye ulemavu na kuwafichua wale wote wenye watoto walio na mahitaji maalum ambao wanapinga agizo la serikali la kuwapeleka skuli.
Alifahamisha kuwa mashirikiano kati ya wazazi na walimu ndio chachu ya mafanikio na kuwataka walimu wanaofundisha katika skuli zilizo na vituo vya elimu mjumuisho kuwa na hekma na busara wakati wanapofundisha na kuepukana na kutoa adhabu nzito.
Aidha aliwata Walimu kujiendeleza kimasomo na kutoridhika na elimu waliyonayo na endaopo zitatokea nafasi za kusoma masomo ya elimu mjumuisho basi wasizikatae nafasi hizo kwa dhana ya kuwa ni mzigo kubwa kufundisha walemavu.
Kwa upande wao walimu wanaofundisha katika skuli hizo wameahidi kutoa elimu sawa kwa watoto wote bila ya kujali tofauti zao na kuiomba serikali kuwapatia nyenzo za kufundishia sambamba na kuhakikisha nafasi za masomo zinazotolewa zinawafikia walegwa.

WATOTO WADHIBITIWE WASICHEZEE MAJI MACHAFU

Watoto wadhibitiwe wasichezee maji machafu

Na Rahma Suleiman
WANANCHI wametakiwa kuwadhibiti watoto wao hasa waliochini ya umri wa miaka mitano, kutochezea maji machafu ili kuweza kuepuka maradhi ya mripuko hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika.
Mwenyekiti wa kamati ya Mazingira na Diwani wa Viti Maalum wa Halmashauri wa wilaya ya Magharib, Halima Salum Abdallah alipokua akizungumza na muandishi wa habari hizi huko ofisini kwake.
Alisema kwa kiasi kikubwa Halmshauri imejiandaa kuiepusha jamii na maradhi ya miripuko ikiwemo kuyasafisha majaa mbali mbali kama vile Kwamchina, Kwamzungu, Mwanakwerekwe na Melinne Taveta.
Mwenyekiti huyo alitoa onyo kwa Mama lishe kuweka usafi katika maeneo yao ya biashara ili kuweza kujikinga na maradhi ya mripuko na waweze kuchemsha maji ya kunywa na wavae mavazi yenye kutambulikana.
Alifahamisha kuwa tayari wameshaandaa utaratibu wa kuvaa sare kwa mama lishe hao kinachotakiwa ni kufika katika Halmashauri ya wilaya na kufika kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira na Ustawi wa Jamii ili kuweza kupewa maelekezo ya sare hiyo.
Hata hivyo aliwataka wananchi wawe tayari kwa kulipa ada za usafi hususan katika maeneo ambayo yenye utaratibu wa kulipia ada ya utupaji wa taka na tayari wanataka kuanzisha kamati ya mazingira katika shehiya nyengine.
Pia mwenyekiti huyo aliwaomba watu wenye uwezo kuweza kujitokeza kuwajengea maslahi ya kuweza kuhifadhia taka ili kuweka mazingira safi.

MBUNGE AJITOLEA KUWALIPA FAINI WAFUNGWA MAHABUSU

Mbunge ajitolea kuwalipia faini wafungwa, mahabusu

Na Nalengo, Morogoro
MSICHANA aliyefungwa kwa kushindwa kulipa faini kwenye gereza kuu la Morogoro mjini, Nasra Ramadhani anayekadiriwa kuwa na umri kati ya (13-15) mkazi wa Chamwino Manispaa ya Morogoro amemtia Simanzi Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Abdulaazizi Abood, na kulazimika kutoa shilingi milioni 7 kuwalipia faini aliyoshindwa kulipa.
Mbunge huyo alisema atatoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuwalipia faini wafungwa 50 waliofungwa, baada ya kushindwa kulipa faini, ili kupunguza msongamano wa wafungwa kwenye gereza hilo.
Wafungwa watakaolipiwa ni wale waliotakiwa kulipa faini na kushindwa, kuanzia kiasi cha shilingi 10,000 hadi 120,000, na kwamba msamaha huo ni pamoja na msichana huyo.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa wakati alipofanya ziara ya kutembelea gereza hilo kwa ajili ya kusikiliza kero za wafungwa na mahabusu, soko kuu pamoja na kuongea na askari polisi, ambapo alibaini kuwepo kwa idadi kubwa ya wafungwa na mahabusu kwenye gereza hilo na kusababisha kuwa na msongamano.
“Baadhi ya wafungwa wamefungwa kwa kushindwa kulipa faini ya shilingi 10,000, 70,000, na wameniahidi kuwa hawatarudia tena kufanya makosa, wanasema wamejifunza, nimeona ni bora niwalipie faini ili watoke wapunguze msongamano”, alisema Mbunge huyo.
Abood alisema gereza hilo ambalo linauwezo wa kuwa na idadi ya mahabusu 144 kwa sasa lina mahabusu 565, kiwango ambacho ni kikubwa na kuweza kuhatarisha wa afya zao.
Aidha Mbunge huyo alisema kuwa mahabusu hao wamekuwa wakilalamikia ucheleweshwaji wa kesi zao na kwamba zinakaa sana mahakamani, ambapo baadhi yao wamemwambia kuwa kesi zao zina miaka sita hazijasikilizwa.
Alisema baadhi ya mahabusu hao wamelalamikia kukosa dhamana kutokana na kukosa wadhamini ambao ni watumishi serikalini, na hivyo kuomba kesi ambazo ni nyepesi wapewe dhamana ili kupunguza msongamano wa mahabusu kwenye gereza hilo.
Kwa upande wake mkuu wa Gereza hilo, Mwaluka Dugange alimwambia Mbunge huyo kuwa gereza hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali na kuzitaja baadhi kuwa ni ukosefu wa vifaa vya kupikia na kwamba masufuria yaliyopo yamepasuka.
Alisema kutokana na msongamano uliopo masufuria hayo yanashindwa kuhimili kupika chakula cha watu 565, pamoja na uhaba wa maji na kwamba hayatoshelezi kutokana na msongamano huo.

MAALIM SULE AOMBA USHIRIKIANO KUHIFADHISHA KUR-ANI WATOTO

Maalim Sule aomba ushirikiano kuhifadhisha kur-ani watoto

Na Aboud Mahmoud
WAZAZI wa watoto wa kiislamu wameshauriwa kushirikiana na Jumuiya ya kuhifadhisha kur-ani Zanzibar ili vijana hao waweze kukitumia kwa ufasaha kitabu hicho.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya kuhifadhisha kur-aan, Suleiman Omar Ahmed ‘Maalim Sule’ katika mashindano maalum ya kuhifadhi kur-ani katika ukumbi wa salama uliopo hoteli ya Bwawani.
Maalim Sule alisema kuwa jumuiya pekeyake haiwezi kufanya kazi bila ya kushirikiana na wazazi wa wanafunzi hao ili waweze kukihifadhi uzuri kitabu hicho.
Alieleza kwamba ni vyema kwa wazazi kutoa mashirikiano ya dhati kwa kuweza kuwapa vijana muongozi mzuri wa kukitunza na kuhifadhi kur-an.
“Napenda kutoa ushauri kwa wazazi wenzangu kuwa bega kwa bega na jumuiya yetu ili tuweze kuwapa muongozo mzuri wa kitabu cha Quraan,”alisema Maalim Sule.
Akisoma risala ya ufunguzi wa mashindano hayo Maalim Faki alisema kuwa Jumuiya hiyo tangu kuanzishwa kwake imeweza kupata mafanikio mbali mbali ikiwemo kuweza kuhifadhisha wanafunzi msahafu mzima wapatao 100,kupatikana kwa nafasi za ushiriki wa mashindano ya kimataifa.
Nyengine ni kuitangaza nchi kimataifa na kupatikana vijana wenye vipaji vya kuhifadhisha kur-an.
Risala hiyo ilieleza kuwa jumuiya hiyo inakabiliwa na changmoto kadhaa ikiwemo mashirikiano madogo baina ya wazee na walimu.
Katika mashindano hayo Jumla ya wanafunzi kutoka katika kanda mbali mbali za Unguja walishiriki katika mashindano hayo ya kuhifadhi kur-ani.
Juzuu zilizoshindaniwa ni Juzuu 30,20,10 na 5 ambapo pia wanafunzi hao waliweza kushiriki kwa njia ya tashjii tahkik.

Monday 25 April 2011

LEO NI SIKU YA MUUNGANO

LEO NI SIKUKUU YA MUUNGANO

Muungano watimiza miaka 47 leo
• Maadhimisho kufanyika Amaan Zanzibar
• Rais Kikwete Mgeni rasmi
Na Mwandishi wetu
WANANCHI wa Tanzania, leo wanaadhimisha kutimia miaka 47 tokea kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26 mwaka 1964, uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sherehe za maadhimisho hayo yatafanyika uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar, ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Baada ya kupewa salamu ya heshima kwa kupigiwa mizinga 21, Rais Kikwete anatarajiwa kukaguwa vikosi vya ulinzi na usalama na baadae vikosi hivyo vitacheza gwaride la mwendo wa pole na mwendo wa haraka.
Vikosi hivyo ni pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Wanamaji, Magereza na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKT).
Miongoni mwa viongozi wa Kitaifa wataohudhuria maadhimisho hayo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal na viongozi wengine.
Mabalozi wanaowakilisha Nchi zao hapa Tanzania nao watashiriki kwenye maadhimisho hayo, ambayo wananchi kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar watahudhuria sherehe hizo kubwa nchini.
Katika maadhimisho hayo, pia vikundi mbali mbali vya utamaduni kutoka Bara na Zanzibar vitatumbuiza, zikiwemo ngoma za asili.
Aidha wanafunzi kutoka skuli za Zanzibar na Tanzania Bara wataimba kwaya huku wakifanya onesho maalum la halaiki, maalum kwa sherehe hizo.

KINAMAMA WASHAJIISHWA KUWANIA UONGOZI.

Kinamama washajiishwa kuwania uongozi

Na Aboud Mahmoud
AKINA mama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama hivho wakati wa uchaguzi utakapowadia hapo mwakani.
Mbunge wa Viti maalum wanawake CCM, Faharia Shomari aliwakati alipokuwa akizungumza na akina mama wa Umoja wa Wanawake wa Wilaya ya Mjini 'UWAWIMI SACCOS' huko Miembeni.
Faharia alisema umefika wakati wa akina mama kujitosa kuwania nafasi za uongozi wa chama hicho ili waweze kutoa mchango wao katika kukiimarisha na kuwatumikia wananchi kwa ujumla.
Aidha alisema mbali na kuwania nafasi za uongozi wa chama, lakini pia aliwataka akina mama kufanya maandalizi ya kujitokeza kuwania nfasi za juu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
"Napenda kukushaurini akina mama wenzangu kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi katika chama chetu na pia kujitokeza kuwania nafasi za juu katika uchaguzi mkuu",alisema.
Katika mkutano huo aliokutana na akina mama wa UWAWIM, Mbunge huyo alichangia shilingi milioni moja kwa ajili ya kuongezea mfuko wa Saccos ya akina mama hao.
Mbunge huyo alimkabidhi fedha hizo Katibu wa Saccos hiyo,Salma Mohammed Seif na kusema kuwa hiyo ni ahadi yake aliyoitoa kwa akina mama wa UWAWIM.
Akitoa shukurani kwa Mbunge huyo,Mjumbe wa Saccos ya UWAWIM, Mtumwa Mussa Kibendera alimpongeza kwa msaada wake alioutoa na pia kuwataka akina mama wenzake kufuata maneno ya Mbunge huyo.
Aidha mjumbe huyo aliwataka akina mama hao kudumisha umoja wao na mapenzi ambayo yatasaidia kukiinua zaidi chama na kujiletea maendeleo binafisi.

WAATHIRIKA MAFURIKO MOROGORO WAOMBA KUSAIDIWA.

Waathirika mafuriko Morogoro waomba kusaidiwa

Na Nalengo Daniel, Morogoro
SERIKALI imeombwa na wananchi waliokumbwa na mafuriko wilayani Kilosa mkoni hapa, kufanya ukarabati wa eneo lilokumbwa na mafuriko wilayani humo ili waweze kurudi katika maeneo yao na kuishi maisha ya kawaida.
Hayo yalibainishwa na wananchi hao kwenye mkutano wa kuunda kamati ya nguvu mji, ikiwa ni lengo la kuwasilisha malalamiko yao kwa viongozi husika.
Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa kamati hiyo Nchimbi Nackam, alisema wameamua kuiomba serikali baada ya kuona viongozi husika kulisahau eneo hilo katika kulirudisha katika hadhi yake kama ilivyo kuwa zamani.
Nchimbi alisema kwa sasa serikali haina budi kupanga mipango ya kuboresha mji huo hasa, baada ya kujengwa kwa kingo za uzio wa kuzuia mto mkondoa, ili usipoteze tena mwelekeo ambao ndio chanzo kikubwa katika kuleta mafuriko eneo hilo.
Alisema wameridhishwa na serikali katika kudhibiti yasitokee tena mafuriko katika eneo hilo, pamoja na JWTZ kuendelea kujenga tuta katika mto huo, lakini pia wameridhishwa na ujenzi wa bwala la kidete ambalo linapunguza kasi ya maji yanapotiririka.
Mwenyekiti huyo alisema mbali na baadhi ya nyumba za watu kubomoka katika mafuriko hayo pia huduma za kijamii zimeathirika, ikiwa ni pamoja na Machinjio,Shule ya msingi mkondoa, ofisi ya CCM, Misikiti,soko,Miundombinu ya barabara na mifereji nayo iliharibika.
Alisema kuwa pamoja na Mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo kutoa msaada wa ujenzi wa msikiti katika eneo hilo, lakini selikali inatakiwa kufanya haraka kurudisha mji katika hali yake kwa kujenga huduma hizo za kijamii.
Kwa upande wao wakazi wa mji huo wakiongea kwa nyakati tofauti katika mkutano huo Masoud Bombolage,Haji Nasoro,Kasamila Kibwana, Rebeka Salum,Amina Khasim,na Ally Waziri wameiomba selikali kutimiza ahadi zake kwa wahathirika wa mafuriko hayo, ikiwa ni pamoja na kupewa viwanja waliohaidiwa sambamba na kuboreshwa kwa mji huo, ili baadhi yao wanaokaa katika makambi waweze kurudi katika maisha yao ya kila siku.
Wananchi hao walisema maeneo ambayo yaliathirika na mafuriko hayo ambayo yanatakiwa kuangaliwa na kurudishwa katika hadhi yake ni pamoja na Mbumi B, Kasiki,Mbumi A, Behewa,kibaoni,Kondoa,Mbwamaji,Masenze na kichangani
Mwishoni mwa mwaka 2009 Wilaya ya Kilosa ilikumbwa na mafuriko ambapo watu watu wawili walipoteza maisha na nyumba kadhaa kubomoka huku wananachi 4610 wakikosa makazi.

MAEGESHO YAWA SHIDA DARAJANI

UKOSEFU wa maegesho ya magari katika maeneo ya Mji Mkongwe kunasababisha kuegeshwa magari sehemu amboyo hairuhusiwi kuweka gari kama inavyoonekana eneo hili la darajani likiwa na bango hil linavyosomeka hairuhusiwi kuweka gari na faini yake ukiegesha.(Picha na Othman Maulid)

CHUMBAGENI WAHITAJI MSAADA UJENZI MADRASA.

Chumbageni wahitaji msaada ujenzi madrasa

Na Haji Nassor ZJMMC
ZAIDI ya shilingi milion tano zinahitajika kumalizia ujenzi wa Madrasatul Anuwar ilioko Chumbageni wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini huko Mwalimu Mkuu wa Madrasa hiyo Omar Juma Ussi, alisema fedha hizo wanatarajia kuziomba kwa wafadhili mbali mbali ikiwa ni pamoja na wazaliwa wa Chumbageni, wahisani, wafanyabiashara kutoka kwa wananchi.
Alisema kwa sasa ujenzi wa madrasa hiyo ambao uko katika hatua ya msingi tayari wameshatumia shilingi 950,000, ambapo ni michango kutoka kwa wazazi, waalimu, wanafunzi, pamoja na wahisani mbali mbali.
Mwalimu Omar alieleza waliamua kuanzisha ujenzi huo wa kudumu kutokana na eneo husika kuwa na ukosefu madrasa kwa ajili kuwasomeshea wanafunzi, ambapo kwa sasa wanatumia baraza ya nyumba ya mwalimu huyo.
“Kwa kweli kwa sasa tunalazimika kusomo tu kwa siku hizi za jua kazi na zile siku za mvua hulazimika kukatisha masomo jambo ambalo huwapotezea muda’’, alifafanua.
Alifafanua kua mara tu madrasa hiyo itakapomalizika ambayo imeanza miaka miwili iliopita, itakapomalizika itakua na uwezo wa kusomewa na wanafunzi zaidi ya 200 kwa wakati mmoja.
Akizungumzia juu ya ushirikiano uliopo baina yake na wazazi wa wenye watoto katika madras hiyo , alieleza sio mzuri sana kwa vile baadhi ya wazazi ,wamekua wagumu kufika wakati wanapoitwa kwa ajili ya mikutano .
Katika hatua nyengine Mwalimu Mkuu huyo wa Madrsatul Anuwar ya Chumbageni Mkoani, Omar Juma Ussi alieleza kua wakati umefika sasa kwa wazazi na walezi kufuatilia kwa karibu neyenendo za watoto wao.

UKOSEFU WA ELIMU WAKWAMISHA UCHANGIAJI WA DAMU.

Ukosefu wa elimu wakwamisha uchangiaji damu

Na Juma Haji, MCC
BENKI ya damu ya Zanzibar imesema ukosefu wa elimu kwa makundi hatarishi yamekuwa ni kikwanzo kinachochelewesha kufikia malengo ya kimaendeleo kwa benki hiyo.
Hayo yameelezwa na katibu Mkuu wa benki hiyo Bakari Hamadi Magarawa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Amani mjini hapa.
Alisema maendeleo katika benki hiyo yamekuwa ni madogo kutokana na vijana wengi kujiingiza katika makundi hatarishi.
Alisema kuwa kukosekana kwa mchango wa vijana hao kwenda kutoa damu kwa hiari imekuwa ni sababu ya kuzorotesha kwa maendeleo ya huduma za benki hiyo.
Magarawa aliyataja makundi ya vijana kuwa ni wanaotumia dawa za kulevya na wanaojidunga sindano amabao pia wana mchango mkubwa kwa jamii kupitia benki hiyo.
Hata hivyo aliwataka wanawake wasiogope kuchangia damu kwa kisingizio cha kujulikana afya zao na wanajamii.
"Wanawake wengi wamekuwa wakiogopa kwenda kupima afya zao kwa kisingizio cha kujulikana na jamii utaona kwenye wanawake 50 wanakwenda 5 wamezidi 10", alisema mkuu huyo.
Nae mshiriki wa uchangiaji wa utoaji damu katika benki hiyo Abrahamani Salum, alipongeza huduma hizo zinazotolewa na kitengo hicho kwa kuwa bado zinalenga maisha ya binaadam.
Hata hivyo alisema kwa marayakwanza walikuwa na usiri kushiki katika zoezi hilol lakini sasa wameshajihishika juu ya umuhimu wahuduma hiyo.

SINGIDA WAMTAKA CAG KUKAGUA HESABU HALMASHAURI.

Singida wamtaka CAG kukagua hesabu halmashauri

Na Jumbe Ismailly, Singida
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Singida kimesema kinakusudia kumwandikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kuomba uchunguzi maalumu (Special Ordit) wa fedha za Halmashauri ya wilaya ya Singida.
Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu kwenye mkutano maalumu wa baraza la madiwani ulioandaliwa kwa ajili ya kupitisha mapendekezo ya bajeti ya mapato na matumizi ya Halmashauri hiyo kwa
mwaka 2011/2012.
Lissu alisema kwamba chama hicho kinakusudia pia kumwandikia waziri wa Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI), kumwomba afanye uchunguzi wa namna ya uendeshaji wa vikao vya Halmashauri ya wilaya ya Singida.
Kwa mujibu wa mbunge huyo kupitia tiketi ya Chadema haiwezekani na haiingii akilini kabisa bajeti ya mabilioni ya shilingi ikapitishwa ndani ya muda wa dakika 30 kama hakuna mambo ya kuficha na kama hakuna uchafau wa kuficha.
“Sasa tunataka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu ya serikali aje afanye uchunguzi maalumu ili ajiridhishe na aturidhishe na sisi kwamba hakuna uchafu unaofichwa”,alisema Mbunge huyo kijana wa Chadema.
Lissu ambaye ni waziri Kivuli wa wizara ya Sheria na Katiba alizitaja hatua zingine watakazochukua ni pamoja na kwenda kila kijiji cha jimbo la Singida mashariki kuwaeleza wananchi juu ya maamuzi yanayo pitishwa na madiwani wao.
“Jambo la pili walipoanza kupitisha pitisha hivi tuliwasiliana na Naibu waziri wa TAMISEMI, Aggry Mwanry na akasema atampigia simu katibu tawala wa Mkoa wa Singida haraka iwezekanavyo ili aje kuzuhakiki”, alisema mbunge huyo.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu (CHADEMA) Christo Mtinda, alisema kikao hicho hakikufuata taratibu za vikao na kwamba ni kikao ambacho kilikuwa kimepangwa kivurugwe kwa makusudi.
Kwa mujibu wa Mtinda ambaye pia ofisa Mwandamizi kwenye Kurugenzi ya mafunzo ya Chama hicho alisema yeye binafsi
ameshindwa kuelewa vitu gani ambavyo vipo kwa muda ule ambao alipewa lile kabrasha lenye kuonyesha mapendekezo hayo ya bajeti ya Halmashauri.
Mbunge huyo alisema jambo lililomshangaza ni kuona Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, alionekana kuwa yeye ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri.
Akijibu hoja za wabunge hao Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Joseph Sabore licha ya kukiri kwamba kikao hicho kilitakiwa kuijadili taarifa ya mapato na matumizi ya mwaka2010/2011, lakini alishindwa kutoa ushahidi wa namna kanuni hiyo ilivyotekelezwa kwenye kikao hicho.

WAUMINI WA KIKIRISTO WAASWA KUENDELEZA IBADA.

Waumini wa kikiristo waaswa kuendeleza ibada

Na John Mpiga Picha
WAUMINI wa dini ya Kikristo hapa wametakiwa kuendeleza ibada za kumkumbuka Mungu, sambamba na kujiepusha na makatazo kwenye mafundisho ya dini hiyo.
Paroko wa Parokia ya Kitope, Faida Shio alieleza hayo kwenye mahubiri ya ibada ya Pasaka iliyofanyika kwenye kanisa hilo, lilioko Kitope Wilaya ya Kaskazini ‘B’.
Alisema dunia imekubwa na matatizo mengi na kwamba njia ya kuepukana na matatizo hayo ni kwa waumini wadini kuongeza kufanya ibada na matendo mema kwa nia ya kumuomba Mungu muumba.
Shio alisema Mungu hapendelei viumbe wake kupata matatizo yakiwemo maradhi pamoja na majanga mbalimbali yanayotokea ulimwenguni na akhera na kuwa mwepesi zaidi kuwaepusha na matatizo hayo waja wake wanapomuomba katika ibada.
Sambamba na hilo kiongozi huyo wa kanisa aliwahimiza waumini hao kuwa na ushikamano kati yao na waumini wa dini nyengine katika kuala zima la kuleta maendeleo ya nchi.
"Ubaguzi wa dini tuondosheni katika nchi na kuwa sote kitu kimoja katika kuendeleza kuijenga nchi yetu ambayo inahitaji kuwa na mabadiliko yatokanayo kwa nguvu yetu moja,"alisisitiza kiongozi huyo.
Alisema suala la maendeleo ya nchi linamuhusu kila mwananchi bila ya kujali dini wala kabila lake ambapo aliwataka kushirikiana kikamilifu katika masuala ya ujenzi wa taifa ikiwa pamoja na kujenga shule pamoja na vituo vya afya.
Katika kusherehekea sikukuu hiyo ya Pasaka waumini kadhaa wa Kikristo, jana walijazana katika makanisa mbali mbali kwa kuifanya ibada za Pasaka.
Waumini wa dini hiyo wanaadhimisha kukumbuka mateso na kufufuka kwa kiongozi wao Yesu Kristo.

TUMAINI MICHEZO KUDUMISHA UDUG, MUUNGANO

'Tumieni michezo kudumisha udugu, muungano'

Na Mwajuma Juma

WANAMICHEZO wa afisi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, wameshauriwa kuitumia michezo kama njia ya kujenga ushirikiano, upendo, udugu pampoja na kudumisha muungano wa Tanganyika na Zanzbar.
Ushauri huo umetolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar Fatma Mohammed Said, katika hafla ya uzinduzi wa tamasha la michezo kwa afisi hizo, lililofanyika viwanja vya Chuo cha Afya Mbweni.
Amesema kimsingi michezo ni miongoni mwa njia za kuleta maelewano na sio ugomvi, na kuwataka waichukulie kwa malengo hayo na si kwa ajili ya kupata kikombe au zawadi kutokana na michezo hiyo.
Nae Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Selina Lymo, amewataka wanamichezo hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za michezo ili waendelee kujenga ushirikiano uliopo miongoni mwao.
Mapema Katibu Msaidizi wa timu ya Soka ya ukaguzi alisema kuwa umoja na mshikamano walionao baina ya taasisi mbili hizo utazidi kuendelezwa ili kuwa mfano mzuri kwa wafanyakazi watakaofuatia baada yao.
Katika uzinduzi huo uliotanguliwa na maandamano ya wanamichezo, timu ya Soka ya Ukaguzi ya Zanzibar ilishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya wageni wao Ukaguzi kutoka Tanzania Bara, mabao yaliyofungwa na Haji Mohammed na Hakim Khamis.

UJAMAA YAFANYA MAUAJI.

Ujamaa yafanya mauaji

Na Suleiman Bangaya

KATIKA ligi ya soka daraja la pili Wilaya ya Mjini inayopendelea kupamba moto kwenye viwanaj mbalimbali, timu ya Ujamaa juzi ilifundisha soka G. S. United kwa kuichapa magoli 6-0.
Katika mchezo mwengine wa michuano hiyo, Bondeni ikawa uchochoro mbele ya Kilimani ilipokubali kichapo cha mabao 2-0.
Na katika matokeo ya mashindano ya Kombe la 'May Day', maveterani wa KMKM wakala sahani moja kwa kufungana bao 1-1 na Ardhi.
Bao la KMKM lilipachikwa nyavuni na Ibrahim Said katika dakika ya nne, huku lile la Ardhi likifungwa na Abdulrahim mnamo dakika ya 18.

ZANZIBAR DCMA KUWASHA MOTO UFARANSA

 Zanzibar DCMA kuwasha moto Ufaransa

Na Aboud Mahmoud


WALIMU watano wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi Zanzibar (DCMA), wanatarajiwa kuondoka leo kwenda Ufaransa kwa ajili ya kushiriki tamasha la muziki lijulikanalo kwa jina la 'Festival Bombard'.
Adel Dabo na Mohammed Issa Matona ambao ni miongoni mwa walimu hao wanaounda kikundi cha 'Saffar', wameliambia gazeti hili kuwa, wakiwa huko watafanya maonesho katika miji tafauti.
Waliwataja walimu wengine wataokuwa pamoja nao katika ziara hiyo, Rajab Suleiman, Godfrey Chinga na Juma Begu.
Walisema wakiwa nchini humo, watapika kambi kwenye mji wa Cleguerek na kufanya maonesho katika miji ya Pontivy na Rennes Kirgis ambapo wakijumuika pamoja na wasanii wa nchi nyengine .
"Maonesho tutakayofanya Ufaransa, yatakuwa kwa ushirikiano na wenzetu wa kutoka nchi mbalimbali ambao pia wanatumia ala ya zumari kama sisi", alisema Dabo.
Baada ya kumalizika kwa maonesho hayo ya pamoja, Dabo alisema pia wamepata mualiko maalumu wa kuonesha utamaduni wa Zanzibar, katika onesho watakalofanya peke yao.
Matona alifahamisha kuwa, heshima hiyo ya pekee waliyopewa inatokana na hamu ya watu wa nchi nyengine kutaka kujua ngoma za utamaduni wa Zanzibar, hivyo wameipokea kwa mikono miwili na kuongeza kwamba hiyo ni fahari kwa visiwa hivi.
"Kila nchi imepewa nafasi ya kufanya onesho moja katika kila mji, lakini sisi tumepewa nafasi maalumu ikikumbukwa kuwa tulipokuwa huko mwaka 2009, tuliwavutia wengi kwa jinsi tulivyofanya vyema, na Wafaransa wengi wameomba twende tena mwaka huu", alifafanua.
Ziara ya kikundi hicho cha Saffar kinachoundwa na wakufunzi wa muziki na ala za asili, inatarajiwa kuchukua muda wa wiki mbili.