Friday, 6 May 2011

MWANAHIJA KUCHEZESHAA PAMBANO LA ANGOLA , ZIMBABWE

 Mwanahija kuchezesha pambano la Angola, Zimbabwe

Na Donisya Thomas
SHIRIKISHO la Soka Afrika (Caf), limemteua muamuzi pekee wa kike kutoka Zanzibar, Mwanahija Fumu, kupuliza firimbi katika pambano la michuano ya All African Games kwa vijana chini uya umri wa miaka 23.
Mwanahija, atakuwa muamuzi wa kati katika mchezo huo utakaowakutanisha vijana kutoka Angola na Zimbabwe ambao umepangwa kufanyika Aprili 10 mwaka huu jijini Harare, Zimbabwe.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,Katibu Msaidizi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Masoud Attai, alisema, chama chake kimeupokea uteuzi huo kwa heshima kubwa.
Attai, alisema, ZFA imefarijika kutokana na mwamuzi huo kuonekana na Caf na kwamba uteuzi huo mbali ya kuwa ni sifa kwa chama hicho, lakini pia ni kwa wadau wa soka nchini.
Alisema, tayari chama chake kimeshaandika barua ya kumuombea ruhusa mwamuzi huyo ambae ni mwajiriwa wa Jeshi la kujenga Uchumi ( JKU) na kumruhusu bila kinyongo.
“ Tumefurahi kwa mwamuzi wetu kuchaguliwa na Caf katika mchezo huo wa vijana huko Zimbabwe", alisema, Attai.
"Ni sifa kubwa kwetu ukizingatia huyu ni mwamuzi mwanamke na Caf imemuamini jukumu hilo zito kwa kuthamini uwezo wake”, alisema, Attai.

Tuesday, 3 May 2011

DK. SHEIN AWATAKA WAWEKEZAJI WA UTURUKI KUWEKEZA ZANZIBAR.

Dk.Shein awataka wawekezaji wa Uturuki kuwekeza Zanzibar

• Awambia mazingira, miundombinu inavutia
• ZIPA yafafanua mipango iliyowekwa
Na Rajab Mkasaba, Uturuki
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa wito kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini Uturuki kuweka vitega uchumi vyao Zanzibar ikiwa ni njia mojawapo kuinua uchumi na kuimarisha mahusiano baina ya pande mbili hizo.
Akizungumza katika mkutano maalum na wawekezaji na wafanyabiashara katika mji wa Istambul nchini Uturuki jana, Dk. Shein amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeimarisha Sera za uwekezaji Zanzibar ili kupunguza usumbufu na kuwavutia zaidi wawekezaji kutoka maeneo mbali mbali duniani.
Dk. Shein ambaye amemaliza ziara yake inayotokana na mwaliko wa Rais wa Uturuki, Abdallah Gul, amesema Benki ya Dunia imeipa nafasi ya pili Zanzibar kati ya nchi 37 zenye uchumi unaofanana katika kurahisisha taratibu za uwekezaji ambapo nchi ya kwanza ni Singapore.
Amesema hatua hiyo inathibitisha utayari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutoa huduma kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Zanzibar.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha taratibu za kuwekeza zinafanywa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi, serikali imeunda Mamlaka ya Vitega Uchumi (ZIPA) ambayo inashughulikia masuala ya uwekezaji Zanzibar.
Aidha, Dk.Shein amesema Zanzibar inayo maeneo mengi ya kuwekeza hasa kwenye sekta ya utalii kutokana na utamaduni wa nchi hiyo unaofanana na Uturuki.
Alisema idadi ya watalii wanaoitembelea Zanzibar kutoka bara la Ulaya imekuwa ikiongezeka kila mwaka na mahitaji ya hoteli na huduma nyengine yamekuwa yakiongezeka sambamba na mahitaji zaidi ya watalii hao.
Alisisitiza kuwa hadi sasa Zanzibar kuna hoteli 225 tu pamoja na nyumba za kulala wageni ambazo zinafanya jumla ya vyumba 5301. Amesema mashirika mbali mbali ya ndege yanatoa huduma kwa watalii wanaotembelea Zanzibar lakini alieleza haja ya wawekezaji wa Uturuki kuangalia uwezekano wa kuongeza safari za ndege kati ya Zanzibar na Jimbo la Utalii la Antalya ambalo linachukua idadi kubwa ya watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Akizungumzia maeneo mengine ya uwekezaji, Dk. Shein alisema kuwa zaidi ya utalii, wawekezaji wanayo nafasi kubwa ya kuwekeza katika maeneo ya uvuvi pamoja na viwanda vidogo vidogo vinavyotokana na rasilimali zilizopo Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein amesema Zanzibar inayo fursa ya kushirikiana kiuchumi na kibiashara kwa kutumia bandari yake iliyopo na kuwa na uwezo wa kupitisha bidhaa kutoka Mashariki ya Kati na Ulaya.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wawekezaji hao kuwa pia, wanaweza kuwekeza katika sekta ya elimu na huduma za afya hasa katika elimu ya juu.
Akitoa maelezo juu ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wafanyabiashara na wawekezaji hao Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum Khamis Nassor alisema kuwa Sera ya uwekezaji Zanzibar imeanzishwa ili kutoa maelekezo kwa taasisi za serikali kwa lengo la kukaribisha wawekezaji kutoka sekta binafsi ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi Zanzibar.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa (ZIPA) imepewa jukumu la kusimamia uwezeshaji wa utekelezaji wa miradi ya kiuchumi bila ya urasimu.
Alisema hadi kufikia Disemba 2010 ZIPA imeidhinisha utekelezaji wa miradi 444 katika sekta mbali mbali, ambapo kati ya hiyo 282 inajishughulisha na biashara ya utalii katika nyanja mbali mbali.
Aliendelea kueleza kuwa wawekezaji wanaendelea kukaribishwa Zanzibar ikiwemo seka ya uvuvi wa bahari kuu, ili rasilimali za bahari ziweze kunufaisha uchumi wa Zanzibar.
Aidha, alisema katika sekta ya kilimo wawekezaji wanakaribishwa kujikita katika kilimo cha mbogamboga kwa kutumia taaluma ya kisasa (Green House) hasa kwa kuzingatia uhaba wa ardhi ya Zanzibar.
Hata hivyo, alieleza kuwa msisitizo pia, umewekwa kwamba ardhi ya uwanda inaweza kutumika kwa kilimo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Mkurugenzi huyo pia, alitaja maeneo mengine katika sekta ya utalii ambayo ni uwekezaji wa mahoteli makubwa ya kuanzia nyota tano. Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa ujenzi wa nyumba za biashara katika maeneo huru ya kiuchumi ambao utaenda sambamba na uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo na vya kati vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hasa matunda na mazao mengine ya kilimo.
Nao wawekezaji na wafanyabiashara wa kupitia Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Uturuki (TUSKON) wameeleza nia yao ya kuwekeza Zanzibar na kupongeza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uwekezaji na biashara ikiwemo Sera yake madhubuti.
Aidha, walieleza pia, kuvutiwa zaidi katika miradi ya miundombinu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ‘Puplic Private Partnership’(PPP).
Pamoja na hayo, wafanyabiasahara na wawekezaji hao wamesifu na kueleza kuwa kuwepo kwa amani na utulivu Zanzibar kutawavutia zaidi kuja kuwekeza katika sekta mbali mbali za maendeleo haraka iwezekanavyo.
Dk. Shein na ujumbe wake wamerejea nchini jana baada ya kumaliza ziara yake hiyo.

MISRI YAAHIDI KUWAWEZESHA WANANCHI KIUCHUMI

Misri yaahidi kuwawezesha wananchi kiuchumi

Na Ali Mohamed, Maelezo
ZANZIBAR na Misri zimeazimia kuongeza mashirikiano zaidi katika kuwawezesha wananchi wa nchi mbili hizo kiuchumi kupitia kilimo, biashara na utalii.
Akizungumza na Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika katika Makao Makuu ya Wizara hiyo Mwanakwerekwe Balozi mkaazi wa Misri Zanzibar, Walid Ismail alisema maeneo hayo ni muhimu kwa mashirikiano ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Pamoja na nchi hiyo kuwa katika kipindi cha mpito cha kuelekea kupatikana kwa serikali yenye ridhaa ya wananchi Balozi huyo alisema Misri italeta wataalamu wa kilimo Zanzibar kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa.
Alisema katika sekta hiyo ya kilimo tayari nchi yake inashirikiana na Zanzibar katika mradi wa kilimo cha umwagiliaji unaendeshwa na Jeshi la Kujenga Uchumu Zanzibar (JKU).
Alisema kutokana na uhaba wa ardhi wakulima wanapaswa kulima kilimo cha kisasa kinachotumia ardhi ndogo na kuzalisha mazao mengi hivyo nchi yake itatuma timu ya wataalamu zaidi kuja kutoa mafunzo kwa wakulima wa Zanzibar.
Katika sekta ya utalii Balozi huyo mkaazi wa Zanzibar alisema Zanzibar ni kama pepo kutokana na kuwa na vivutio vingi vya utalii ambapo wananchi wengi wa Misri wanapenda kuja Zanzibar.
Alisema kikwanzo kilichopo kwa watalii wa Misri kushindwa kuja kwa wingi Zanzibar ni kukosekana kwa usafiri wa uhakika wa ndege kuja moja kwa moja katika visiwa vya Zanzibar.
Kwa upande wake Waziri wa Kazi na Uwezeshaji, Haroun Ali Suleiman alisema Zanzibar inafatilia kwa karibu matokea ya Misri na inaungana na wananchi wa nchi hiyo kuiombea kurudi katika hali yake ya kawaida.
“Kama nchi marafiki Zanzibar tunafatilia kwa karibu sana matokeo ya Misri na tunaungana na wananchi wa Misri kuwatakia mafanikio na kurudi katika hali ya kawaida”. Alifahamisha Waziri Haroun.
Alisema kihistoria nchi hizo zinafanana hivyo mashirikiano baina ya nchi mbili hizo ni kuendeleza hitoria na kuwawezesha wananchi kiuchumi na kupunguza makali ya maisha kwa wananchi.
Aidha Waziri Haroun alisema kuna umuhimu kwa watendaji wa wizara ya uwezeshaji Zanzibra kufanya ziara nchini Misri kwa lengo la kuona na kujifunza namna ya kuwawezesha wananchi kutokana na nchi hiyo kupiga hatu katika maeneo hayo hasa katika sekta ya kilimo.
Alisema kupatikana kwa ufumbuzi wa safari za ndege kutoka Misri kuja moja kwa moja Zanzibar kutaimarisha sekta ya utalii na biashara na kuimasha uchumi wa nchi mbili hizo.

SINA UTAJIRI WA KUTISHA - RIDHIWANI KIKWETE

Sina utajiri wa kutisha – Ridhiwani Kikwete

Asema wanasiasa wapuuzwe, wanadanganya umma
Na Kunze Mswanyama
WAKILI wa kujitegemea nchini, Ridhiwani Kikwete,amekanusaha tuhuma alizobebeshwa na wanasiasa wawili maarufu kuwa ana utajiri mkubwa kiasi cha kutisha, ilhali ameanza kazi hivi karibuni mara baada ya kumaliza masomo yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwanasheria huyo aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa atatoa ushirikiano kwa mtu yeyote atakaye taka kuthibitisha utajiri wake huo, ambapo ilitajwa pia anamiliki vyombo mbalimbali vya usafiri yaliwemo malori, mabasi, majengo makubwa ya kupangisha na kutembelea gari lenye thamani ya shilingi milioni 400.
Alisema wanasiasa hao wanaomtuhumu wanaudanganya na kuuhadaa umma wa Watanzania dhidi ya madai yao hao iliwaamini kuwa ana mali nyingi
Rikadhaniwa zinatokana na nafasi aliyo nayo mzazi wake yaani Jakaya Kikwete ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa.
"Mimi ni raia wa kawaida, mtanzania na wakili sina kinga za aina yoyote, na ninatambua utawala bora unapoheshimu haki za binadamu. Hivyo natoa rai kwa wazee hawa ambao mimi pia nawaheshimu kuwa watumie vyombo vya habari walivyovitumia ili kutengeneza habari njema na siyo kutafuta sifa za kisiasa au kuonekana wao wanajua sana kuongea,wasiwe makanjanja wa habari",alisema Ridhiwani.
Wakili huyo alisema, "kuwa habari hizi hazikuwa za kweli ni za kizushi, zilizojaa uongo na ambao madhumuni yake nayaona yanalenga kunichafua mimi na wazazi wangu katika umma wa watanzania na kujenga chuki kati yetu na jamii hii”.
Aidha alisema kuwa umma wa watanzania uelewe kuwa hamiliki mali hizo zilizotajwa na kama kuna mtu ana ushahidi autoe ambapo yuko tayari kuwajibika mbele ya umma.
Ridhiwani alisema si mara ya kwanza kwa baadhi ya wanasiasa kutoa taarifa za uongo ambapo mmoja wa wanasiasa hao, aliwahi kusema yeye na vijana wengine 50 walijifungia katika hoteli ya La Cairo iliyopo Mwanza kuharibu uchaguzi wa mwaka jana.
“Pia amewahi kuwaongopea watanzania kuwa kuna makontena ya kura yamekamatwa huko Tunduma Mkoani Mbeya,bila ya aibu Mzee huyu anaudanganya umma huu, hivi tunaweza kweli kuwa na rais muongo na tukaendelea kiuchumi, si atatudanganya hata mambo mengine muhimu?"
Ridhiwani alisemaalitoa rai kwa watanzania kwa kuwataka kutowasikiliza kwani vyanzo vya habari vya wanasiasa hao vinatoa taarifa potofu.

MANISPAA, ILO KUSHIRIKIANA KUZOA TAKA

Manispaa, ILO kushirikiana kuzoa taka

Na Halima Abdalla
BARAZA la Manispaa Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeandaa mradi wa kuzoa taka na kusafisha michirizi ya maji machafu ambao utawashirikisha vikundi binafsi vya usafi vilivyopo kwenye shehia.
Akizungumza na mwandishi wetu huko ofisini kwake Mkuu wa Huduma za jamii kutoka Baraza hilo Rajab Salum Rajab alisema tayari mtaalamu wa shirika hilo ameshafanya ziara ya kuangalia vikundi hivyo na kuangalia hali ya mazingira ya Zanzibar.
Rajab alisema lengo la mpango huo ni kuweza kuwapatia ajira ya kazi ndogo ndogo za usafi kwa kila shehia kwa vijana na akina mama ili kuwasaidia kupata ajira na kuondokana na masikini.
Alisema kuwa vikundi hivyo vitakuwa vinashughulika kwa kutoa huduma za ukusanyaji taka katika maeneo ya majumbani, kusafisha michirizi ya maji machafu ili kupunguza malalamiko ya kutopata huduma za uzoaji wa taka na usafishaji katika maeneo ya Manispaa ya Zanzibar.
Alifahamisha kuwa mpango huo utakapoanza itabidi wananchi wachangie gharama ili kusaidia upatikanaji wa fedha za kuwasaidia watu hao.
''Mpango huo wa usafishaji katika shehia utasimamiwa na Diwani na Sheha pamoja na wakuu wa vikundi hivyo,''alisema Rajab.
Alieleza kuwa tayari wameshafanya mafunzo kwa wanavikundi hivyo kuhusiana na mradi huo na pia watatoa vifaa vya vitendea kazi pamoja na kufanya ziara ya kujifunza kuona wenzetu wanafanya nini kuhusiana na hilo.
Mradi huo wa uzoaji wa taka kwa shehia mbali mbali za Manispaa ya Zanzibar umefadhiliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

CAG AVIJIA JUU VYOMBO VYA HABARI

CAG avijia juu vyombo vya habari

Na Kunze Mswanyama
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Uttoh, amekanusha tuhuma zilizoelekezwa kwake na kwa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) juu ya matumizi mabaya ya fedha za umma hasa malipo ya shilingi bilioni moja kwa kampuni ya Dowans zilitolewa na baadhi ya vyombo vya habari mapema wiki iliyopita.
CAG Uttoh alisema kuwa katika ripoti yake aliyoipeleka kwa Rais Dk. Jakaya Kikwete mapema mwishoni mwa Machi haina kipengele chochote kinachosema kuwa "Tanesco kuna ufisadi mpya na pia vyama vya siasa pia kuna ufisadi,hakuna kifungu hata kimoja nilichokiandika katika ripoti yangu kinachosema hivyo",alisema.
"Katika uwasilishaji wa ripoti zangu kumetokea mapungufu katika ufafanuzi na uchambuzi wa ripoti hizi. Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti baadhi ya taarifa potofu za shirika la umeme nchini na vyama mbalimbali vya siasa, nawaomba waandishi muwe mnaitafuta ofisi yangu ili kujua baadhi ya ripoti zinazohitaji ufafanuzi".
"Ninapenda ieleweke wazi kuwa katika taarifa zangu za ukaguzi hakuna sehemu yeyote niliyotumia neno kashfa mpya au ufisadi kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.Habari zilizoandikwa si tu kwamba si sahihi lakini pia hazipo kabisa katika taarifa za mwaka ulioishia Juni 30,2010",alisema CAG.
Alisema baadhi ya taarifa zisizokuwa sahihi kuwa ni pamoja na ile ya Tanesco kuilipa Dowans dola 1.2 milioni badala ya 120,000 za kusafirishia mitambo hiyo kuja nchini.Pia matumizi hayo yanakadiriwa kufikia shilingi bilioni 1.4 kwamba ziliingizwa katika akaunti ya Dowans kimakosa.
Pia,hadi sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali amesema Tanesco imeshindwa kumpelekea ripoti ya matumizi ya fedha hizo alizoziita kuwa za ufisadi pia kwamba waliokatiwa umeme na shirika hilo bado wanatumia ilhali wanadaiwa bili ya dola 65,000 habari hizo zote si za kweli.
Kwa upande wa vyama vya siasa alisema kuwa yeye kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu hajakagua hesabu za vyama hivyo ila anavisihi kupeleka taarifa zao za mapato na matumizi kwa Msajili ili nae azipeleke kwake ili kuwepo na uwazi kwa matumizi ya fedha za umma hasa kwa vyama vile ambavyo vilipata ruzuku ya serikali ili kuendeshea uchaguzi uliopita wa mwaka 2010.
Taarifa hiyo ilisema kuwa ,"vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi vimetumia vibaya fedha hiyo hilo sio sahihi kwa kuwa bado sijakagua hesabu zao",alisema Uttoh.
Baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini (siyo hili), kwa muda wa wiki moja iliyopita vimekuwa vikiripoti habari za ufisadi hasa kutokana na ripoti ya CAG jambo lililofanya taasisi hiyo kubwa na nyeti nchini katika dhana nzima ya utawala bora, kuwaita waandishi wa habari na kukana kutoa taarifa hizo.

ASHIKILIWA NA NYARA ZA SERIKALI

Ashikiliwa na nyara za serikali

Na Nalengo Daniel, Morogoro
JESHI la polisi mkoni hapa linamshikilia Sudy Pazi (26) mkazi wa jijini Dar es salaam kwa tuhuma za kuingia ndani ya hifadhi ya Mikumi na kukutwa na nyara za serikali zenye thamani ya shilingi milioni 9.6.
Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa polisi mkoni hapa Adolphina Chialo alizitaja nyara hizo kuwa ni vipande 8 vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilo 10.3 , vyenye thamani ya shilingi milioni 9.5, mikia miwili ya tembo na ngozi paka mwitu vyenye thamani ya shilingi 168,000.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 30 mwaka huu saa 4:30 asubuhi na kwamba mtu huyo alikamatwa na askari wa hifadhi ya wanyamapori Aloyce Munka (63) aliyekuwa doria ndani ya hifadhi hiyo.
Alisema kuwa askari huyo alimkamata mtuhumiwa ndani ya hifadhi hiyo katika eneo la Magogoni tarafa ya Mvuha wilaya ya Morogoro vijijini na kwamba uchunguzi unaendelea na kwamba atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika tukio jingine watu wawili wanashikiliwa na polisi mkoni hapa kwa tuhuma za kumiliki shamba la bangi lenye ukubwa wa hekari moja.
Kamanda Chialo aliwataja watu hao kuwa ni Hamisi Charasa(45 na Juma Charasa (20) wote wakazi wa kijiji cha Ihombwe kata na Tarafa ya Mikumi Wilayani Kilosa.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 30 mwaka huu saa 1:30 asubuhi katika kitongoji cha Minazini Kijiji cha Ihombwe tarafa na kata ya Mikumi.
Alisema kuwa askari mwenye cheo cha Inspekta Munuo akiwa na askari wenzake waliteketeza shamba la watuhumiwa hao kwa moto lilokuwa na miche ya bangi iliyokuwa tayari kwa kuvunwa.
Hata hivyo kamanda huyo alisema kuwa watuhumiwa wote wanashikiliwa na polisi na kwamba watafikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya uchunguzi kukamilika.