Wednesday 9 June 2010

Jinamizi lagubika uhakiki wanachama CCJ

Na Mwanajuma Abdi
CHAMA cha Jamii (CCJ), kimezidi kukumbwa na jinamizi kwenye zoezi la uhakiki wa wanachama wake hapa Zanzibar, baada ya wanachama na wafuasi wa chama hicho Mkoa Kusini Uinguja kuingia mitini.

Chama hicho kiko kwenye hatua za kuhakikiwa wanachama wake na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, ili kiweze kupata usajili wa kudumu.

Katika harakati za usajili huo, uliofanyika jana atika Mkoa wa Kusini Unguja, mwanachama mmoja tu ambae ni Naibu Katibu wa CCJ, Zanzibar, Ali Khatib ndie pekee alijitokeza kuhakikiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Rajab Mbaraka.
 
Naibu Msajili huyo aliikagua nambari ya kadi ya mwanachama huyo ambayo ilikuwa ni Na. 3910, na kubaini kuwa ni halali, baada ya kuangalia fomu zake.
 
Naibu katibu huyo wa CCJ alipotakiwa na Naibu Msajili kuwapeleka wanachama wake wakasajiliwe alikataa kata kata.

Naibu katibu huyo wa CCJ, alsiema Chama chake kimeshampelekea barua kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, kusitisha zoezi la uhakiki huo kwa sasa hadi hapo baadae.
 
“Makao makuu ya Chama changu yaliyopo Dar es Salaam yameshaniagiza kuwa zoezi la uhakiki limesitishwa, hivyo hakuna haja ya kuendelea kufanyiwa uhakiki na ratiba zinazopangwa na Msajili ni zake mwenyewe”, alisisitiza Ali Khatib.
 
Alisema katika Mkoa wa Kusini anawanachama 231 lakini kutokana chama chake cha CCJ, kuamua kusitisha zoezi la uhakiki hajaweza kuwapa taarifa wanachama wake wala kutoa taarifa kwa Sheha na Polisi kwa vile hakuna uhakiki kwa sasa.
 
Mapema Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Rajab Mbaraka, alionana na Mkuu wa Wilaya ya Kusini Haji Makungu Mgongo, ambapo alimwambia hana taarifa ya kufanyika kwa uhakiki wa chama CCJ jana.
 
Zoezi la uhakiki wa chama hicho ulipangwa kwa Mikoa minne kwa awamu ya kwanza lakini katika mikoa yote hiyo, wanachama wameshindwa kujitokeza, huku wale waliojitokeza wamekumbwa na utata wa uanachama wao.
 
Hata hivyo, Rajab alisema baada ya kukamilisha zoezi hilo jana wanategemea kufanya tathmini ili kuangalia kama wataendelea na zoezi hilo katika mikoa sita iliyobakia au ndio basi.

No comments:

Post a Comment