Tuesday 30 November 2010

OLE WAO WANAOCHEZEA UMOJA WETU - MAALIM SEIF

Ole wao wanaochezea umoja wetu – Maalim Seif


Na Abdi Shamnah, Pemba

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amewaonya watu wanaochezea na kutia chokochoko umoja na mshikamano uliopo nchini.

Alisema umoja, amani na utulivu uliopo Zanzibar hivi sasa ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo amewataka Wazanzibari kutokuwa tayari kuruhusu mtu yeyote kuvunja au kutia doa umoja huo.

Katibu Mkuu huyo, alisema hayo katika kiwanja cha Tibirinzi Chake Chake Pemba, alipokuwa akizungumza na wananchi na wanachama wa CUF, ambapo pamoja na mambo mengine aliwashukuru kwa kushiriki kwenye zoezi zima la uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni.

Maalim Seif aliwataka wananchi kutokubali kurejeshwa walikotoka na kutowapa nafasi watia chokochoko kwani umoja na mshikamano uliopo hivi sasa miongoni mwa wananchi ndio silaha pekee ya kufikia maendeleo ya haraka kiuchumi na kijamii.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Umoja wa Kitaifa chini ya Rais Ali Mohamed Shein na Makamu wawili wa Rais, itaendeleza mshikamano huo na kumuomba Mwenyezi Mungu aubariki milele.

Alieleza kuwa azma ya wananchi ya kuwa na Serikali ya umoja wa Kitaifa kama walivyothibitisha katika kura ya maoni imetimia baada ya vyama vikuu vya CCM na CUF kupata viti vinavyowiana katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31,2010.

Alifafanua kuwa matokeo ya kura za urais na mgao wa viti katika majimbo ni ushahidi tosha jinsi ya umuhimu wa kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Maalim Seif aliwashukuru wananchi wa kisiwa cha Pemba kwa kushiriki katika kampeni za amani na utulivu, kiasi ambacho mchakato huo umemalizika bila kuwepo ugomvi au matusi katika majukwaa.

Mapema katika risala ya Mikoa miwili ya Pemba, wanachama wa CUF walipaza sauti kuiomba Serikali kusambaza Mabwanashamba katika wilaya zote ili kukabiliana na tatizo kubwa linalojitokeza la uharibifu wa mazao mbali mbali katika mashamba ya wakulima.

Nae mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa alisisitiza haja ya wananchi kufanya kazi kwa bidii na kuonya kuwa kamwe hakutokuwa na neema bila ya kila mmoja kujituma kwa kufanya kazi.

Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wananchi na viongozi wa ngazi mbali mbali wa chama hicho pia ulihudhuriwa na Mjumbe wa kamati Kuu ya CCM Haji Omar Kheir, ambae alifuatana na ujumbe wa Makamu huyo kutoka Unguja.

Katika salamu zake kwa wanachama na wapenzi wa CUF waliohudhuria mkutano huo, mjumbe huyo ambae ni Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, aliwaahidi kuwatumikia wananchi wote wa Zanzibar kwa mashirikiano na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

DK. SHEIN ATEUA MAJAJI, MWENYEKITI MAHAKAMA YA ARDHI

Dk. Shein ateua Majaji, Mwenyekiti mahakama ya ardhi

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amefanya uteuzi wa majaji wanne wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, imewataja majaji walioteuliwa ni Jaji Fatma Hamid Mahmoud, Jaji Rabia Hussein Mohammed, Jaji Mkusa Isaac Sepetu na Jaji Abdul-hakim Ameir Issa.

Kwa mujibu wa barua hiyo uteuzi huo umefanywa na Rais wa Zanzibar chini ya kifungu 94(2) cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Aidha katika barua hiyo Katibu Mkuu Kiongozi alieleza kuwa umeanza rasmi Novemba 26 mwaka huu.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amemteua Haroub Sheikh Pandu kuwa Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi imeeleza kuwa uteuzi wa Mwenyekiti huyo ambao umeanza rasmi Novemba 26, umefanywa na Dk. Shein chini ya kifungu 4(1) cha Sheria ya Mahakama ya Ardhi namba 7 ya mwaka 1994.

POLISI ZANZIBAR WAAGIZWA KUJIANDAA KUKABILI UHALIFU WA MITANDAO

Polisi Z'bar waagizwa kujiandaa kukabili uhalifu wa mitandao


Na Mwantanga Ame

JESHI la Polisi Zanzibar limetakiwa kuanza kujiandaa kwa namna litakavyoweza kupambana na uhalifu wa kimataifa kwa kutumia mitandao ya kompyuta na silaha nzito, ulioanza kushamiri duniani.

Waziri asiekuwa na Wizara Maalum, Machano Othman Said, alitoa ushauri huo jana wakati akifungua semina ya siku moja kwa maafisa wa Jeshi la Polisi wanaosimamia mradi wa ulinzi wa Polisi Jamii, iliyofanyika ukumbi wa Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.

Waziri huyo alisema uhalifu wa kutumia kompyuta na mitandao ya intaneti na silaha nzito ni mpya katika Afrika na sasa umeanza kujitokeza katika sehemu mbali mbali ikiwemo mataifa yanayoendelea.

Alisema suala kama hilo linahitaji kufanyiwa kazi kwa vile uchumi wa Zanzibar unategemea sana soko la utalii na katika hatua yoyote linaweza kuingia dosari endapo wahalifu watafanikiwa kulipenya.

Hata hivyo, alisema kitendo cha kupungua kwa matukio ya matumizi ya nguvu na silaha kumejenga taswira nzuri kwa wageni na kushauri jambo hilo lisimamiwe zaidi ili hata dosari ndogo ndogo ziweze kudhibitiwa.

Kutokana na mafanikio hayo, Waziri huyo alisema serikali itahakikisha inatoa mchango wake ili kulifanya Jeshi hilo liwe na uwezo mkubwa zaidi wa kuimarisha amani ya nchi kuwawezesha wananchi kushughulikia maendeleo bila ya kubughudhiwa.

Waziri Machano aliwataka watendaji hao kuendeleza ushirikiano na wananchi kwa kuieneza zaidi elimu ya Polisi jamii kwa kutumia vyombo vya habari.

Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alieleza Polisi kwa kiasi kikubwa inawapongeza wananchi kutokana na mchango wao mkubwa uliofanikisha

dhana ya Polisi jamii kukubalika kwa wananchi.

Semina hizo zinatarajiwa kufanyika katika maeneo mbali mbali kwa muda wa siku tano ndani ya vitengo vya jeshi hilo ambapo lengo lake ni kuhakikisha kunakuwepo fursa zaidi za mawasiliano kati ya wananchi na Polisi.

MADRASAT TAQWA YATAKIWA KUZIKABILI CHANGAMOTO

Madrasat Taqwa yatakiwa kuzikabili changamoto


Na Masanja Mabula, Pemba


MWAKILISHI wa Shirika la Agakhan Foundation Zanzibar, Khamis Said ameuagiza uongozi wa Madrasat Taqwa ya Bubujiko wilaya ya Wete kisiwani Pemba, kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili madrasa hiyo ikiwemo kukamilisha banda la kusomea pamoja na kuwahimiza wazazi kulipa ada kwa wakati.

Akizungumza na Uongozi, wazazi na wanafunzi wa madrasa hiyo katika sherehe za siku ya Afya ya madrasa, alisema ni vyema uongozi huo ukashirikiana na wazazi ili kusaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa baadhi ya changamoto katika madrasa hiyo na kuacha tabia ya kusubiri wafadhili kuja kuwatatulia matatizo yao.

Alisema viongozi wa madrasa hiyo wanapaswa kutambua umuhimu wa afya, lishe na elimu kwa watoto wao, hivyo ni wajibu wao kutoa ushirikiano utakaoweza kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na walimu wa madrasa hiyo kuwapatia elimu bora ya maandalizi watoto kabla ya kuingia elimu ya msingi.

Aidha alifahamisha kuwa Shirika la Agakhan Foundation kanda ya Zanzibar, litaendelea kuzisaidia madrasa kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu ya kielimu pamoja na kuimarisha hali ya afya na lishe kwa wazazi na watoto.

Mapema Mratibu wa Zanzibar Madrasa Resource Centre Ofisi ya Pemba, Hassan Ali Bakar, alisema siku ya afya ya madrasa ni miongoni mwa mikakati ya Jumuiya ya ZMRC katika kutoa elimu ya afya na lishe kwa wazazi na wanajamii wa jamii mbali mbali za Zanzibar, sherehe ambazo hufanyika kila baada ya miezi mitatu katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa katika kusherekea siku hiyo , Jumuiya hualika wataalamu wa afya na lishe na kutoa mafunzo kwa wazazi na wanajamii kulingana na mahitaji ya jamii husika ambapo madaktari hupata fursa ya kuchunguza afya za watoto.

Katika sherehe hizo ambazo mgeni rasmi alikuwa ni Sheikh Khazal, alichagia mifuko kumi ya saruji ili kusaidia ujenzi wa madrasa hiyo na kuwataka wazazi kutilia umuhimu suala la afya na lishe katika makuzi ya watoto.

Kwa mwaka huu wa 2010, hapa Kisiwani Pemba, sherehe hizo zimefanyika kwa mara ya nne ambapo zaidi wa watoto 50 waliobahatika kuchunguza afya zao huku mtoto mmoja aliyepatikana kuwa na maradhi ya utapiamlo.

SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI -- HAROUN

Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji - Haroun


Raya Hamad, Maelezo


WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman, amesema serikali ina nia thabiti na itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga uchumi imara wa visiwa hivi kwa maslahi ya wananchi.

Haroun alisema hayo jana huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja kwenye ufunguzi wa utanuzi wa hoteli ya La Gemma dell'Est, ambapo waziri huyo alimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein.

Alisema, suala la kuishirikisha sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Zanzibar, limewekwa bayana na kupewa kipaumbele katika programu ya Mpango Mkuu wa Kukuza Uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar (MKUZA).

Kwenye mpango huo, amesema serikali imeweka mipango ya kuweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji pamoja na sekta binafsi kushirikishwa moja kwa moja katika uchangiaji wa uchumi wa Taifa.

"Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kibiashara na uwekezaji ili sekta hiyo nayo iweze kuchangia uchumi wa Taifa kwa lengo la kuinua maisha ya Wazanzibari", alisema Waziri huyo.

Waziri huyo aliupongeza uongozi wa hoteli ya La Gemma, kwa upanuzi huo ambao una lengo la kuvutia watalii zaidi nchini ambao ni muhimu katika kuongeza pato la Taifa.

Alisema upanuzi huo ambao umegharimu dola milioni sita, ni mfano wa kuigwa kwa hoteli nyengine hapa nchini na kuitaka hoteli hiyo kuzidi kujitangaza na kutumia vivutio vya Zanzibar kwa lengo la kuongeza watalii.

Naye Murugenzi wa Kampuni ya RENCO, Paolo Chiaro alisema ataendelea kuitangaza Zanzibar kimataifa kuwa kituo muhimu cha utalii duniani.

Mkurugenzi huyo alisema kampuni hiyo pia ina mipango thabiti ya kuongeza ajira kwa wazalendo ili kupunguza tatizo la ajira.

ZEC YATANGAZA MADIWANI VITI MAALUM

ZEC yatangaza Madiwani viti maalum


Na Mwandishi Wetu


TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeteua Madiwani 42 wa viti maalum Wanawake kuingia katika Baraza la Manispaa la Zanzibar na Halmashauri ya Wilaya na Miji ya Chake Chake, Mkoani na Wete.

Kulingana na uteuzi huo Chama cha Mapinduzi (CCM), kimepata viti 23 vya wanawake wa viti maalum, baada ya kushinda Wadi 75 kati ya wadi 141.

Chama cha CUF, kimepata viti 19 maalum vya wanawake baada ya kuibuka na ushindi kwenye Wadi 66 kati ya wadi 141.

Kwa mujibu wa barua ya ZEC iliyosainiwa na Idrisa Haji Jecha kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, imeeleza kuwa uteuzi wa madiwani umefanywa kwa mujibu wa sheria namba 3 ya mwaka 1995 ya Baraza la Manispaa la Zanzibar na sheria namba 4 ya mwaka 1995 ya Halmashauri za Wilaya na Mabaraza ya Miji.

Waliopenya kwenye uteuzi huo kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Micheweni ni pamoja na Khadija Ali Khamis, Hadia Amir Hamad na Naima Nassor Khamis ambao wote wanatoka chama cha CUF.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkoani ambao wote kutoka chama cha CUF ni pamoja na Fatma Chum Omar, Zuleikha Ali Othman na Amina Ali Mohammed.

Walioteuliwa kuingia katika baraza la Mji la Mkoani ni pamoja na Amina Abdulla Mohammed kutoka CUF na Naima Nahodha Faki kutoka CCM.

Walioteuliwa kuingia katika Halmashauri ya Wilaya ya Wete kutoka CUF ni Salma Ali Omar, Bimkubwa Ali Mgeni na Hadia Sudi Mzee, huku Rabia Omar Salihi na Fadhila Nassor Hamad kutoka CUF wakiteuliwa kuingia katika baraza la mji wa Wete.

Kutoka Wilaya ya Chake Chake, walioteuliwa kuingia katika Halmashauri ya Wilaya ya hiyo ni Mariam Hamad Bakari, Hinaya Said Mohammed na Fatma Mohammed Saleh wote kutoka chama cha CUF.

ZEC pia imewateua Mariam Ali Suleiman na Biabu Nassor Suleiman kutoka CUF kuingia katika baraza la mji wa Chake Chake.

Kwa upande wa Wilaya ya Mjini walioteuliwa kuingia katika Baraza la Manispaa Saada Ramadhan Mwenda, Salma Abdi Ibada, Zaitun Khatib Maulid, Salma Mselem Sleyoum na Shara Ame Ahmed ambao wote wanatoka chama cha CCM.

Aidha Tume hiyo imemteua Arafa Mohammed Said kutoka CUF, kuingia katika Baraza la Manispaa la Zaznibar.

Kwa upande wa wilaya ya Magharibi, walioteuliwa kuingia kwenye Halmashauri kutoka CCM, Halima Salum Abdulla, Aziza Abdulla Amour, Asha Khamis Juma, Fatma Ramadhan Masorwa huku Hidaya Ali Hamad akiteuliwa kuingia kwenye halmashauri hiyo akitokea chama cha CUF.

Waliochaguliwa kuingia Halmashauri ya Wilaya ya Kati ambao wote ni kutoka CCM ni Zakia Mussa Chum, Maua Mohammed Ali na Maryam Khamis Hamad.

Walioteliwa kuingia katika halmashauri ya wilaya ya Kusini ambao wote kutoka CCM, Salama Ali Hamad, Nali Makame Haji na Riziki Abdulla Abdulla.

Katika Wilaya ya Kaskazini A, waliochaguliwa kuingia katika halmashauri hiyo ambao wote ni kutoka CCM ni Kiembe Vuai Jecha, Hidaya Ali Ali, Nali Makame Ngwali na Mwamvua Juma Hussein.

Katika Wilaya ya Kaskazini B, walioteuliwa kuingia katika halmashauri ya wilaya hiyo ambao wote ni kutoka CCM ni pamoja na Mtumwa Abdulla Saleh, Habiba Juma Said na Zakia Makungu Marished.

BIMA ZANZIBAR KUKUSANYA BILIONI 10

Bima Zanzibar kukusanya bilioni 10


Na Mwandishi wetu

Jumla ya shilingi bilioni kumi zinatarajiwa kukusanywa na Shirika la Bima la Zanzibar kwa mwaka huu ukilinganisha na shilingi bilioni 5 kwa miaka mitatu iliyopita.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar, Iddi Khamis Haji, katika hafla ya kuwaaga Wajumbe wa Bodi ya Shirika hilo ambao wamemaliza muda wao.

Mkurugenzi Iddi amesema kiwango hicho kimefanikiwa kutokana na kutekeleza kwa vitendo mikakati waliojipangia ya kuongeza mapato ya shirika hilo chini ya usimamizi wa Bodi iliyomaliza muda wake.

"Hali ya shirika linaendelea vizuri hadi sasa kutokana na kuongeza mapato ya shirika hilo zaidi" amesema.

Akizungumzia mikakati ya baadae ya shirika hilo Mkurugenzi Mkuu huyo amesema jengo la makao makuu ya bima Zanzibar linaloendelea kujengwa katika maeneo ya Maisara linatarajiwa kuwa tayari mapema mwakani na hadi sasa matengezo ya jengo hilo yamefikia asilimia 60.

Amesema jengo hilo likimalizika linatarajiwa kutumika kama ofisi pamoja na kulifanyia biashara kwa kukodisha kwa lengo la kuongeza mapato zaidi ya shirika hilo kwa siku zijazo.

Mbali na jengo hilo Khamis amesema shirika la bima la Zanzibar lipo mbioni kuanzisha bima inayoendana na misingi ya dini ya kiislamu ambapo huduma hiyo wanatarajiwa kuwa ni wa kwanza kuanzisha Tanzania kati ya makampuni 28 ya bima yaliyopo Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo aliyemaliza muda wake, Mohammed Fakih Mohammed, amesema Shirika la bima linatakiwa kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazojitokeza ikiwemo ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo makampuni mbalimbali ya bima yatafungua matawi yake nchini.

Mbali na hilo pia amewataka kutilia mkazo zaidi kuimarisha huduma kanda ya Pwani Tanzania Bara kutokana na kuwa asilimia 70 hadi 80 ya mapato yote ya bima ya Zanzibar yanapatikana kutoka huko.

Bodi ya bima iliyomaliza muda wake ilichaguliwa mwaka 2007 ambapo kwa mujibu wa sheria inatakiwa kuka madarakani kwa muda wa miaka mitatu.

Monday 29 November 2010

ASKARI wa Usalama Barabarani wakitumia chomba cha kugunduwa mwendo wa kasi kiwa magari ili kuepusha ajali wakiwa katika barabara ya Michezani.(Picha na Abdalla Masangu)

DK. SHEIN AHUDHURIA MKUTANO WA EU LIBYA.

Dk.Shein ahudhuria mkutano wa EU Libya


Na Mwandishi wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameondoka nchini jana kuelekea Libya kushiriki mkutano wa tatu wa EU kwa Afrika.

Taarifa zilizopatikana zinaeleza kwamba katika mkutano huo, Dk. Shein anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Katika mkutano huo wa siku mbili, Dk.Shein amefuatana na ujumbe wa viongozi mbali mbali kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar, Dk.Shein aliagwa na viongozi mbali mbali.

Dk. Shein na ujumbe wake wanawatarajiwa kurejea nchini Novemba mosi.

WACHACHE WAJITOKEZA UCHAGUZI MADIWANI.

Wachache wajitokeza uchaguzi Madiwani

CUF yanyakua Wadi zote 3 Pemba


IDADI ya watu waliojitokeza kupiga kura za udiwani katika wadi mbali mbali ambazo hazikuishiriki uchaguzi uliopita imepungua ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.

Washiriki wa uchaguzi huo walikuwa wachache wakilinganishwa na waliojitokeza kwenye upigaji kura wa Oktoba 31, ambapo ulimchagua rais wa Zanzibar, Rais wa Muungano, wabunge na Wawakilishi.

Akizungumza na Mwandishi wetu aliyefika katika Kituo cha kupigia kura Sebleni wadi ya Sogea, Zahrani Juma, alisema idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura imezorota sana hata watu wanaokuja kupiga kura wamekuwa wakijitokeza kidogo kidogo .

‘’Idadi iko chini sana mpaka sasa mchana watu hata 100 hawafiki waliojitokeza kupiga kura,’’Alisisitiza Mkuu huyo.

Aidha alisema zoezi limekwenda vizuri na hakuna kasoro zozote zilizojitokeza zinazoashiria uvunjaji wa amani.

Nae Mkuu wa Kituo cha Mwembe Shauri, wadi ya Kwahani, Suhuba Daudi alisema zoezi la upigaji kura limeenda vizuri isipokuwa idadi ya wapigaji kura waliojitokeza ni ndogo.

Alisema mpaka muda huo wa mchana hakuna muangalizi yeyote aliyefika kuangalia mwenendo wa uchaguzi isipokuwa wagombea na makatibu wa vyama.

Nae Mkuu wa Kituo cha Miembeni Haji Makame Ussi,alisema zoezi limeenda vizuri na hakuna kasoro zozote zilizojitokeza za uvunjaji wa amani katika zoezi hilo .

Aidha alisema mwamko si mkubwa kwa watu waliojitokeza kupiga kura ikilinganishwa na Uchaguzi Mkuu.

Alisema wasimamizi waliofika katika kituo chake ni waangalizi wa ndani TEMCO.

Majimbo mengine yaliopiga kura za udiwani ni jimbo la Magomeni, Wadi ya Nyerere, jimbo la Mji Mkongwe, Wadi ya Mchangani, Jimbo la Makunduchi wadi ya Kajengwa,Jimbo la Bumbwini Wadi ya Mangapwani,kwa Upande wa Pemba Jimbo la Ziwani wadi ya Wara, Jimbo la Wawi Wadi ya Nga’mbwa, na Jimbo la Chake Chake Wadi ya Msingini.

WAKATI huo huo BAKARI MUSSA, Pemba anaripoti ZOEZI la upigaji kura za Udiwani katika Wadi tatu za Pemba, umefanyika vizuri ingawaje wapiga kura hawakuwa wengi katika vituo vya kupigia kura.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Chake Chake Pemba, Afisa Uchaguzi wilaya ya Chake Chake, Rashid Suleiman Omar, alisema vituo vimefunguliwa mapema na upigaji wa kura umeanza tokea saa 1.00 asubuhi na hakuna matatizo ambayo yalijitokeza katika zoezi hilo.

Alisema wapiga kura wengi wamekwenda Vituoni kwa ajili ya kupiga kura na kurejea majumbani mwao ingawaje wapiga kura hao wamekwenda mmoja mmoja kinyume na ilivyotarajiwa.

Aliendelea kusema kuwa kwa upande wa ZEC, vifaa vyote vya Uchaguzi walivipeleka mapema ili zoezi hilo liende kwa wakati, jambo ambalo limefanya uchaguzi huo kuanza kama ilivyopangwa na Tume.

Omar, alieleza kuwa baadhi ya Wapiga kura walikwenda mapema vituoni kupiga kura na mapema ili kuwahi shughuli zao walizojipangia na ndio baadhi ya vituo kukawa na watu kidogo.

Wadi ambazo zimefanya uchaguzi huo wa Madiwani baada ya hapo mwanzo kuwepo na matatizo ya kiutendaji ni, Wadi ya Wara, Ng’ambwa, Msingini na Uwandani, ambazo ni majimbo ya Wawi , Ziwani na Chake Chake Pemba.

CHUMBUNI WAMPONGEZA PERERA.

Chumbuni wampongeza Pereira



Na Simai Tano, MUM

WANANCHI wa jimbo la Chumbuni Zanzibar jana walijitokeza kwenye Uwanja wa ndege wa Abeid Aamani Karume mjini hapa kumpokea mbunge wa jimbo lao akitokea mjini Dodoma.

Wananchi hao wakiwa wamevalia sare za Chama cha Mapinduzi walimpokea Mbunge huyo aliekuwa akitokea Dar es salaam, ambapo wiki iliopita aliapishwa na Rais Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi katika serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Pereira ambae ni mbunge wa jimbo la Chumbuni katika Mkoa Mjini Magharibi, aliteuliwa kuwa miongoni mwa mawaziri wa baraza la mawaziri la Rais Kikwete aliloliteua wiki iliopita.

Wananchi wa jimbo hilo wakiwa na furaha walimvisha shada la maua mbunge huyo katika hafla iliyofanyika Uwanja wa ndege na kuongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa jimbo hilo, Juma Haji Juma.

Akizungumza na wapiga kura wake na wananchi wengine, Pereira

aliwataka wananchi hao kuachana na malumbano yasiokuwa na maana na kuvunja kambi zao ili kushughulikia maendeleo ya jimbo lao na serikali kwa jumla .

vile vile alisema watu wa jimbo lake wasiwe na wasi wasi juu ya kuteuliwa kwake kuwa naibu waziri wa fedha msimamo wake utakua pale pale kuleta maendeleo katika jimbo lake amewataka vijana wa jimbo lake kukaa pamoja na kutafakari ni kitu gani cha kuanza mwanzo katika ahadi alizozitoa za kuleta maendeleo ya jimboni kwao.

Aliwataka kuendelea kukiunga mkono chama cha Mapinduzi na pia kufanyakazi kwa juhudi popote walipo kama njia ya kuharakisha maendeleo ya ncjhi yao.

Aliwashukuru wananchi hao na kusema kwamba yeye yuko pamoja na wananchi na kusisitiza kwamba atatekeleza ahadi zake kwa wananchi wote kama alivyozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Mbunge Pereira Ame Silima hii ni mara yake ya kwanza kuwa mbunge, ingawa ameitumikia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda mrefu na katika nafasi kadha ikiwemo Maliasili Misitu, na Naibu Katibu mkuu Wizara ya Biashara.

TINDWA AELEZA IMUHIMU WA BARAZA LA USAFIRISHAJI.

Tindwa aeleza umuhimu wa baraza la usafirishaji

Na Maryam Talib, Pemba

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, amewataka wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo kisiwani Pemba kuunga mkono uundwaji wa Baraza la usafirishaji, ambalo litawasaidia katika harakati zao za kibiashara.

Tindwa alisema hayo hoteli ya Clove Inn, Chake Chake alipokuwa akilizindua baraza la usafirishaji mizigo Zanzibar kwa upande wa kisiwa cha Pemba.

Alisema kuanzishwa kwa baraza hilo kutasaidia kuirejesha Zanzibar kuwa kituo muhimu cha kibiashara Afrika Mashariki na Kati.

Aidha alisema kuanziswa kwa baraza hilo, kutakuwa ni chachu ya kushuka bei kwa bidhaa mbali mbali zinazoingizwa nchini ambazo hivi sasa kwa kiasi wananchi wamekuwa wakizinunua kwa bei ya juu.

Alisema baraza hilo lina lengo la kuwaunganisha wafanyabiashara sambamba na wasafirishaji mizigo yao, na kuwataka wafanyabiashara kulithamini baraza hilo.

Nae Mwenyekiti wa baraza hilo Salim Taufiq, alisema lengo la kuanzishwa baraza hilo ni kuwapa nafasi wasafirishaji kuwa na sauti moja katika kulinda maslahi yao.

“Hii itasaidia katika kusimamia kushuka gharama za usafirishaji kiasi ambacho hali hiyo ikiwa itatekelezwa kikamilifu na wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo itasababisha kila mmoja kuweza kumiliki anachotaka”, alisema Mwenyekiti huyo.

WAVAZIRI MSITAEALKIWE NA UPONDELEO, ITIKADI -- SAID SOUD

Mawaziri msitawaliwe upendeleo, itikadi - Said Soud


Na Lulua Salum, TSJ

MWENYEKETI wa Chama AFP, Said Soud Said amewashauri Mawaziri waliochaguliwa kuunda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, kuondosha upendeleo na itikadi za kisiasa katika kuijenga Zanzibar mpya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Soud alisema ili kuijenga Zanzibar mpya mawaziri hao wawe tayari kuwajibika katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mwenyekiti huyo aliyewania Urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu uliopita, alisema mawaziri hao wakiwajibika vyema na watendaji wao watakuwa kioo na hivyo wananchi wataweza kufikia ndoto ya matarajio kwa Serikali hiyo.

Alisema ni vyema wakaondosha mivutano kati yao na watendaji wa chini ambao watateuliwa na Rais, kwani kipindi kilichopita Wizara nyingi zilikuwa na matatizo ya watendaji na ndio sababu kubwa ya kuibuka kwa migogoro.

Aidha alimuomba Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, kufanya mabadiliko ya watendaji wake kwani wananchi wengi wameonekana kukosa imani nao.

Alisema watendaji wengi wa wizara hiyo wamekuwa hawajali maslahi ya wananchi na badala yake kuweka maslahi yao mbele.

Alisema licha ya serikali kuunda Mahakama ya Ardhi, lakini imeshindwa kutatua suluhisho la kuondoa matatizo yaliyopo na imeonekana kuzidisha matatizo na migogoro kwa wananchi hasa kisiwani Pemba.

Mwenyekiti huyo alimtaka waziri husika kuliangalia kwa kina tatizo hilo na kulitafutia njia mbadala ya kuliondosha ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya watendaji wake ili kuleta sura halisi ya Zanzibar mpya inayotakiwa na wananchi.

WASAFIRI PEMBA WALAKAMIKIA UTARATIBU WA KUBADILISHA BOTI

Wasafiri Pemba walalamikia utaratibu wa kubadilisha boti


Na Lulua Salum, TSJ

ABIRIA wanaosafiri kwa kutumia vyombo vya baharini wameulalamikia Uongozi wa Kampuni ya Azam Marine, juu ya mpangilio wao wa kuwabadilisha boti inayotoka Dar -es- Salaam kwenda Pemba.

Wasafiri hao walisema mpango huo wa kubadilishiwa boti, umekuwa ukiwapa usumbufu kwani wanaposafiri huwa na mizigo mingi pamoja na watoto.

Walisema licha ya kampuni hiyo kuandaa watu wa ya kushusha mizigo wakati wa kubadiliswa boti, bado tatizo la kubadilishwa na mingine kuharibika hujitokeza.

Mmoja kati wasafiri hao aliyezungumza na gazeti hili, Asha Kombo alisema kuwa mara nyingi boti wanayobadilishwa tayari imeshajaa hivyo kuwawia vigumu kwenye safari yao.

Naye Mwanajuma Rashid aliiomba kampuni hiyo kuchukua tahadhari wakati ili kuepuka matatizo hayo yanayojitokeza.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Azam Marine, Hussein Said, alikiri kuwepo utaratibu wa kubadilishwa boti na kueleza kuwa hajapokea malalamiko yoyote.

Alisema boti hizo zina uwezo wa kuchukua abiria zaidi ya 450 na baadhi ya siku hurejea Dar-es-Salaam, zikiwa na abiria wachache na kushangazwa suala la abiria kusema wanakosa nafasi za kukaa wanapoingia katika boti hizo.

PEMBA WAPIGA KURA KWA MURUA.

Pemba wapiga kura kwa murua

Na Bakari Mussa, Pemba

ZOEZI la upigaji kura za Udiwani katika Wadi tatu za Pemba, umefanyika vizuri ingawaje wapiga kura hawakuwa wengi katika vituo vya kupigia kura.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Chake Chake Pemba, Afisa Uchaguzi wilaya ya Chake Chake, Rashid Suleiman Omar, alisema vituo vimefunguliwa mapema na upigaji wa kura umeanza tokea saa 1.00 asubuhi na hakuna matatizo ambayo yalijitokeza katika zoezi hilo.

Alisema wapiga kura wengi wamekwenda Vituoni kwa ajili ya kupiga kura na kurejea majumbani mwao ingawaje wapiga kura hao wamekwenda mmoja mmoja kinyume na ilivyotarajiwa.

Aliendelea kusema kuwa kwa upande wa ZEC, vifaa vyote vya Uchaguzi walivipeleka mapema ili zoezi hilo liende kwa wakati, jambo ambalo limefanya uchaguzi huo kuanza kama ilivyopangwa na Tume.

Omar, alieleza kuwa baadhi ya Wapiga kura walikwenda mapema vituoni kupiga kura na mapema ili kuwahi shughuli zao walizojipangia na ndio baadhi ya vituo kukawa na watu kidogo.

Wadi ambazo zimefanya uchaguzi huo wa Madiwani baada ya hapo mwanzo kuwepo na matatizo ya kiutendaji ni, Wadi ya Wara, Ng’ambwa, Msingini na Uwandani, ambazo ni majimbo ya Wawi , Ziwani na Chake Chake Pemba.

Thursday 11 November 2010

MGAO WA MAJINA YA WABUNGE NEC HUU HAPA

Mgao majina ya wabunge NEC huu hapa


Na Mwandishi Wetu

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza mgao wa majina ya wabunge wa viti maalum kwa vyama vitatu vya siasa vilivyopata kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Lewisi Makame alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipata nafasi 65 ya viti maalum, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) viti 23 na Chama cha CUF kimepata viti 10 huku vyama vyengine 15 vilivyoshiriki uchaguzi mkuu vimekosa viti hivyo.

Kwa mujibu wa ibara ya 66 (1) (b) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano, sura ya pili kutakuwa inasema kutakuwa na wabunge wanawake idadi isiyopungua asilimia 30 ya wabunge wote.

Hata hivyo, mwaka 2009, Serikali kupitia Baraza la Mawaziri iliamua uchaguzi wa mwaka huu, idadi ya viti maalum iongezeke hadi asilimia 40, badala ya asilimia 30 iliyotumika mwaka 2005.

Jaji Lewisi aliwataja majina hayo kwa CCM ni Sophia Simba, Amina Makilagi, Gaudensia Kabaka, Ummi Ally Mwalimu, Agness Hokororo, Martha Umbulla, Lucy Mayenga, Faida Mohammed Bakari, Felister Bura, Kidawa Hamid Saleh, Injinia Stella Manyanya, Maria Hewa, Cynthia Hilda Ngoye, Josephine Genzabuke, Ester Midimu, Maida Hamad Abdallah, Asha Mshimba Jecha, Zaria Madabida na Namelok Sokoine.

Wengine wa CCM ni Munde Abdallah, Benardetha Mushashu, Vicky Kamata, Pindi Chana, Fatuna Mikidadi, Mchungaji Dk. Getrude Rwakatare, Betty Machangu, Diana Chilolo, Fakharia Shomar Khamis, Zynabu Vullu, Abia Nyabakari, Pudenciana Kikwembe, Lediana Mng'ong'o, Sara Ally na Catherine Magige.

Wajumbe wengine wa viti vya wanawake CCM ni Ester Bulaya, Neema Hamid, Tauhida Cassian, Asha Mohamed Omari, Rita Mlaki, Anna Abdallah, Dk. Fenella Mukangara, Dk. Terezya Huvisa, Al- Shaymaa Kwegyir, Margareth Mkanga, Angella Kairuki, Zainab Kawawa, Mwanakhamis Kassim Said na Riziki Lulida.

Aidha wengine ni Devotha Likokola, Dk. Christine, Ishengoma, Mariam Mfaki, Margaret Sitta, Subira Mgalu, Ritta Kabati, Martha Mlata, Dk. Maua Daftari, Elizabeth Batenga, Azza Hamad, Mary Mwanjelwa, Josephine Changulla, Bahati Abeid, Kumbwa Makame Mbaraka, Rosweeter Kasikila, Anastazia Wambura na Mary Chatande.

Hata hivyo wajumbe wa viti maalum wa CHADEMA ni pamoja na Lucy Owenya, Esther Matiko, Muhonga Ruhwanya, Anna Mallac, Paulina Gekul, Conchesta Rwamlaza, Suzan Kiwanga na Grace Kiwelu.

Wengine ni Suzan Lyimo, Regia Mtema, Christowaja Mtinda, Anna Komu, Mwanamrisho Abama, Joyce Mukya, Leticia Nyerere, Naomi Kaihula, Chiku Abwao, Rose Kamili, Christina Lissu Mughiwa, Raya Ibharim, Filipa Mturano, Mariam Msabaha na Rachael Mashishanga.

BALOZI AMINA SALUM ALI AMESEMA USHIRIKIANO ULIJENGWA NA VYAMA VYA CCM NA CUF UENDELEZWE.

Na Mwanajuma Abdi

MWAKILISHI wa kudumu wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa, Balozi Amina Salum Ali, amesema ushirikino mkubwa uliojengeka baina ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa vyama vya siasa vya CCM na CUF uendelezwe baada ya kukosekana kwa muda mrefu.

Hayo aliyasema jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani nje kidogo wa mji wa Zanzibar.

Alisema hli ya ushirikiano inahitaji kudumishwa na kuendelezwa ili nchi iweze kupiga hatua za kimaendeleo, ambapo kwa muda miaka 13 Zanzibar ilikumbwa na misukosuko ya kisiasa.

Alieleza nchi ya Tanzania ikiwemo Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka huu umefanyika kwa amani na utulivu, ambapo mataifa mbali mbali duniani yamekuwa yakipongeza hatua hiyo pamoja na nchi za Afrika Mashariki.

Hata hivyo, aliwataka Wawakilishi wanawake wawe wabunifu katika kuhakikisha taifa linapata kasi ya maendeleo pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kutetea sheria za wanawake na watoto katika kupiga vita unyanyasaji na ukandamizaji.

Balozi Amina alisema Baraza la mwaka huu wanawake kutoka chama cha CCM na CUF kuwa na mwamko katika elimu, hivyo anatarajiwa kuwepo kwa mabadiliko makubwa katika maendeleo ya nchi.

Mapema Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho aliwashukuru wajumbe hao kwa kumrejesha tena kuwatumikia katika shughuli hizo, aliwakumbusha kwamba Julai 31 mwaka huu wananchi walipiga kura ya maoni iliyoandaliwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na waliowengi wameunga mkono.

Alisema ZEC iliandaa kura hiyo baada ya wawakilishi kupitisha mswaada wa kuundwa kwa Serikali hiyo baada ya uchaguzi mkuu, hivyo aliwashauri wailinde Serikali hiyo itayoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mahammed Shein kwa kuwateuwa mawaziri na manaibu.

Alieleza tukio lililofanyika jana linaumuhimu mkubwa kwa vile ndilo litalomuwezesha Dk. Shein kuchagua viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya Saba.

BUNGE LA EAC LAMPONGEZA DK. JK.

Bunge EAC lampongeza JK




BUNGE la Jumuia ya Nchi za Afrika Mashariki limempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika salamu zake kwa Rais Kikwete, Spika wa Bunge hilo, Abdirahim Haithar Abdi alisema kwa niaba ya wabunge wa bunge hilo na kwa niaba yake binafsi linampongeza Rais Kikwete kwa kupata ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 uliofanyika nchini.

Spika Abdirahim, amesema ushindi wa Rais Kikwete unatokana na imani ya watanzania kwake ni kubwa na alistahiki kupata ushindi huo kutokana na mafanikio makubwa katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi.

Alisema Jumuia hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbali mbali yakiwemo yale yanayohusu eneo zima la bara la Afrika hasa katika kuhakikisha bara hilo linatilia mkazo sualsa la amani na kuwepo hali ya utulivu ya kudumu.

Abdirahim alisema hali ya utulivu ilioijengeka Tanzania inatokana na udhibiti wa hali ya amani ya kudumu katika Tanzania, ambapo Jumuia hiyo inaipongeza hali hiyo.

Aidha amempongeza Rais Kikwete kwa kuonesha umahiri na kwamba serikali, uchaguzi mkuu Tanzania kwa kusema serikali yake, vyama vya upinzani na wananchi wenyewe wa Tanzania wameonesha ukomavu wa kisiasa na kuithibitishia dunia kwamba uchaguzi huru na wa haki unaweza kufanyika barani Afrika.

Spika huyo alisisitiza kwamba bnunge hilo linamuunga mkono Rais Kikwete na kumuombea afya njema na kwamba katika miaka ijayo, Tanzania itaendelea kuonesha njia na mwelekeo wa kudumu kwa amani na utulivu wa nchi na Afrika ya Mashariki iliyoungana.

WAJITOKEZA 103 WAPIMA VVU CHINI YA ABCZ.

103 wapima VVU chini ya ABCZ


Na Khamis Mohammed


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.Mohammed Saleh Jidawi, amesema, Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za taasisi na mashirika mbalimbali katika vita dhidi ya maambukizi mapya ya vurusi vya ukimwi nchini.

Hayo aliyaeleza wakati akizindua upimaji wa virusi vinavyosababisha ukimwi hoeli ya Bwawani mjini hapa jana ikiwa ni siku maalum kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sehemu za kazi.

Alisema kwa kuthamini michango inayotolewa na taasisi hizo, Serikali itakuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo na kutoa ushirikiano katika vita hivyo vinavyoyakabili mataifa mbalimbali duniani.

Hivyo, Katibu huyo aliwataka wananchi kujitokeza mara kwa mara wakati zinapotekea fursa hizo kwa lengo la kutambua afya zao na kuweza kujikinga iwapo watakuwa hawajapata maambukizo hayo.

Aidha aliwataka wakuu wa taasisi kutilia mkazo juu ya upimaji afya kwa wafanyakazi wao sambamba na kuwapatia huduma za lazima iwapo watakuwa wamepata maambukizi.

"Ukimwi ni maradhi kama yalivyo mengine, tujitokeze kupima afya zetu ili tuweze kuishi tukijielewa tupo katika hali gani", alieleza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar, Asha Abdalla, alisema, pamoja na kuwa hali ya maambukizi ya ukimwi hapa Zanzibar si ya kiwango cha juu, lakini ni vyema kwa wanajamii kuchukua kila tahadhari kuhakikisha haitumbukii katika janga hilo.

Jumla ya watu 133 walijitokeza kupima katika uhamasishaji huo wa upimaji wa virusi vya ukimwi kwa wafanyakazi wa taasisi za binafsi na makampuni hapa Zanzibar ambapo watu wawili waligundulika kupata maambukizi.

Hivi sasa Zanzibar inakisiwa kuwa na watu waliopata maambukizo ya virusi vya ukimwi zaidi ya 6,000.

Zoezi hilo la uhamasishaji wa upimaji wa virusi vya ukimwi liliendeshwa na Umoja wa Unaojihusisha na masuala ya ukimwi kwa sekta binafsi Zanzibar (ABCZ), ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Baraza la Biashara la Afrika Mashariki katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kila ifikapo Novemba 11.