Monday, 30 August 2010

WAHIMIZWA KUTUMIA VYEMA FEDHA ZA MIRADI

Wahimizwa kutumia vyema fedha za miradiRaya Hamad, Maelezo

WANANCHI na wavuvi wanaoishi katika maeneo ya ukanda wa pwani wameshauriwa kuzitumia fedha za mradi wa usimamizi wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani MACEMP kwa kuziwekeza katika ufugaji wa samaki katika maeneo ya Bahari.

Mkurugenzi wa Idara ya uvuvi na mazao ya baharini, Mussa Aboud Jumbe, ameyasema hayo kwenye mkutano wa mwaka uliowakutanisha wenyeviti na makatibu wa kamati tendaji za wavuvi na wakulima wa mwani wenye lengo la kutathmini mafanikio na matatizo mbali mbali.

Mussa amewataka wavuvi kuukubali mpango huo endelevu wenye tija ya uhakika wenye gharama nafuu za uwekezaji na wenye mavuno makubwa yenye faida ambao hutumia utaalamu wa kisasa kwa kupata ushauri wa wataalamu kutoka Idara ya uvuvi ili kuepuka uharibifu na uchafuzi wa mazingira .

Aidha, Mussa amesisitiza kuwa ufugaji wa viumbe wa baharini utawawezesha wavuvi kuwa na tija ya uhakika kwa vile ufugaji wake ni wa kawaida wenye gharama ndogo za uwekezaji na faida ya mavuno ni kubwa “Sisi tuna eneo kubwa la bahari na maeneo mengi ya bahari yameingia ndani hii ni faraja kubwa kwani ufugaji wa mazao ya baharini unakuwa rahisi zaidi hasa kisiwa cha Pemba”, alisema Mussa

Mussa amesema uchumi wa nchi unakua kutokana na rasilimali zilizomo nchini na ndio maana Serikali kupitia mradi wa MACEMP umekuwa ukiwawezesha wavuvi na wakulima wa mwani kwa kuwapa taaluma,kuwaweka pamoja ,na kuwapatia vifaa vya kisasa, pamoja na kuwa na uwezo wa kubuni miradi mbadala ili wakuze kipato chao na kusaidia kukuwa kwa uchumi wanchi .

Mkurugenzi huyo amesisitiza miradi ya ufugaji wa samaki itakapo imarika zaidi itatowa fursa ya pekee kwa wawekezaji wa ndani na wanje kuweza kuja kuwekeza hapa nchini na hivyo kuwa na ongezeko la ajira .

Akitowa mada kuhusu ufugaji wa viumbe vya baharini, Hashim Moumin amesema wakati umefika kwa wavuvi kubadilisha mfumo uliopo wa wavuvi wote kutegemea bahari pekee bali wajikite zaidi na ufugaji wa viumbe wa baharini kwa lengo la kuinuwa kipato cha mvuvi na kuondokana na umasilikni

Hashim amesema ufugaji wa viumbe wa baharini sio jambo geni hapa visiwani lakini bado mwamko ni mdogo hivyo amewataka wavuvi kujitahidi kujikita katika ufugaji wa viumbe wa baharini zaidi ili kuepusha msongamano wa wavuvi na wakulima wa mwani wanaokwenda baharini.

Miongoni mwa nchi zinazojishughulisha na ufugaji wa samaki ni pamoja na China, Norway, Japan, Indonesia Philipine, Korea ambazo zimepata mafanikio makubwa kwa kukuza kipato cha wavuvi ,na kukuza uchumi nchi zao.

Mkutano huo ulifunguliwa na Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Mazingira na kuhudhuriwa na Wakuu wote wa Wilaya za Pemba,Maafisa Tawala, Wataalamu kutoka Idara ya Uvuvi, Meneja wa Mradi wa Mradi wa MACEMP na watendaji wake .

WAGOMBEA WARUDISHA FOMU KWA MBWEMBWE.

Wagombea warudisha fomu kwa mbwembwe Wengine wathibitisha kukubali matokeo

Na Mwantanga Ame, ZJMMC

WAKATI zoezi la urejeshaji fomu za kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar, Uwakilishi na Udiwani, likikamilika baadhi ya wagombea wamefanikiwa kurejesha fomu zao huku wengine wakiwa wamekwama baada ya kuzuka mivutano ndani ya vyama vyao.

Zanzibar Leo, jana asubuhi imeshuhudia baadhi ya wagombea wa vyama vilivyochukua fomu kuwania nafasi hizo wakizirejesha Tume ya Uchaguzi Zanzibar pamoja na Afisi ya Tume Wilaya ya Mjini.

Mgombea wa kwanza ambaye alijitokeza katika Tume hiyo majira ya saa 4.20, ni wa Chama cha TADEA, kilichowakilishwa na Katibu wa Chama hicho upande wa Zanzibar Juma Ali Khatib, na kufuatiwa wa Chama cha Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wenyeviwanda na Wakulima, Said Soud na baadae ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi Zanzibar Haji Ambar Khamis.

Wagombea hao walifika Tume hiyo wakiwa katika mbwembwe za kusindikizwa na wapambe wao kwa misururu ya magari yaliyokuwa yakipiga honi barabarani huku wakiongozwa na kasida za dufu pamoja na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kauli mbiu za vyama vyao.

Wagombea hao walikabidhi fomu hizo kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Khatib Mwinchande na kuiarifu Tume hiyo kuwa wamekamilisha kupata wadhamini kwa idadi waliyotakiwa ya wadhamini 200 kwa kila Mkoa wa Zanzibar.

Akizungumza baada ya kupokea fomu hizo Mwenyekiti wa Tume hiyo, alivitaka vyama vyote kuhakikisha vinajiandaa vyema kuingia katika uchaguzi wakidumisha hali ya amani na utulivu kwa kufanya kampeni za kistaarabu.

Alisema haitategemewa baada ya wagombea hao kupitishwa na Tume hiyo kuwa wagombea halali wa uchaguzi ujao, na vyama hivyo kuendesha kampeni kwa kutoa matusi hadharani .

Mwenyekiti huyo alisema Zanzibar hivi sasa haihitaji kampeni chafu na ndio maana Tume yake imeamua kutoa uhuru wa kutosha wa kuvipa fomu kwa kila chama ikiwa na lengo la kukuza demokrasia hapa nchini.

Alifahamisha kuwa demokrasia inayohitajika kufuatwa ni ya kuwaelezea watu juu ya maendeleo gani vyama vyao vinakusudia kuwapatia wananchi na sio demokrasia ya kupigana.

"Tushindane lakini tusipigane", alisema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo aliwataka wagombea hao kuwasilisha ratiba zao za kampeni ili Tume hiyo iweze kuandaa ratiba ya kampeni ya Kitaifa.

Wakitoa shukrani zao vyama kwa nyakati tafauti wagombea hao walieleza kuwa watahakikisha wanatimiza masharti ya Tume hiyo kwa kufanya kampeni za kistaarabu na kuipongeza Tume hiyo kwa kuwapa haki sawa vyama vyote.

Mgombea wa Chama cha TADEA Juma Ali Khatib, alisema Chama chake baada ya kupata ridhaa ya wananchi kipaumbele chao ni kuhakikisha nafasi za viti vya wanawake inafikia asilimia 50 wakiwa na lengo la kuwawezesha kushika uongozi katika mambo mbali mbali.

Aidha, Mgombea huyo alisema suala jengine ambalo atalishughulikia ni kuimarisha elimu kwa wanafunzi wa Zanzibar, ili wasome vizuri kwa lengo la kuwawezesha kukabiliana na ajira katika soko la Afrika Mashariki.

Nae Mgombea wa Chama cha Wakulima na Wenyeviwanda (AFP), Said Soud, alisema chama chao kitakuwa na vipaumbele vinne kikiwemo cha kukuza kilimo na biashara kwa kila Mkulima kupandiwa na mazao ya asili bure kazi ambayo itasimamiwa na serikali.

Alisema Wananchi katika kuitekeleza sera hiyo kila mtu ataweza kupandiwa miti ya minazi bure katika shamba lake na maeneo ya wazi huku akipata ofa ya kulimiwa katika shamba lake mara moja kwa mwaka kazi ambayo itafanywa kwa kutumia matrekta ya serikali.

Eneo jengine ambalo alilitaja ni linalohusu elimu ya juu kufanywa kuwa ni la Zanzibar, badala ya kuwa chini ya usimamizi wa Tanzania bara huku, na pia kujenga Chuo Kikuu Pemba badala ya Unguja pekee na kukuza sekta ya afya kwa kupata wataalamu zaidi.

Nae Mgombe wa Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis, alisema Chama chake kitakubali matokeo yoyote yatayojitokea katika uchaguzi ujao kwa vile wanaamini kuwa Tume hiyo itawatendea haki vyama vyote.

Makamu huyo alisema Chama chao kitahakikisha kinadumisha amani na utulivu kwa wakati wote wa kampeni zao kwani kimepata msukumo mzuri wa kuwania nafasi hiyo kwa vile mazingira yaliyopo hivi sasa ni tofauti na uchaguzi wa mwaka 2005.

Wagombea hao wote waliikabidhi Tume ya Uchaguzi shilingi milioni 2 ikiwa ni ada ya uchukuaji wa fomu hizo kwa kila Mgombea anaewania nafasi hiyo

Afisa Msimamizi wa Wilaya ya Mjini Mwanapili alifahamisha kuwa katika majimbo 10 ya Wilaya hiyo wagombea 20 wa CCM na CUF, wameresha fomu hizo huku wagombea 10 kutoka chama cha NCCR Mageuzi, Tadea, Jahazi, NRA baadhi yao yao wameshindwa kurejesha fomu hizo.

Alisema wagombea wa Udiwani 57 waliochukua fomu walirejesha fomu zao na pingamizi kwa wagombea hao zinatarajiwa kuanza kuwekwa Septemba 2 hadi 3 mwaka huu.

2,000,000/ ZASABABISHA MMOJA ANG' OKE MBIO ZA URAIS ZANZIBAR.

2,000,000/ zasababisha mmoja ang'oke mbio za Urais Z'bar


 Akimbilia Mkwajuni kujaza fomu za Uwakilishi


 Wagombea wanne wafanikiwa kuzirejesha jana

Na Mwanajuma Abdi

HAJI Mussa Kitole ambaye alichukua fomu Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuwania Urais wa Zanzibar kupitia chama cha Sauti ya Umma (SAU) ameshindwa kurejesha fomu hadi ulipofika muda wa mwisho wa kurejesha fomu hizo saa 10 jioni jana.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Kitole alisema hakuweza kurejesha fomu hizo kwasababu chama chake cha Sauti ya Umma hakijampatia fedha za kulipa dhamana ya fomu hiyo shilingi 2,000,000.

Hata hivyo, alisema kutokana na kushindwa kuingia katika kinyang'anyiro cha Urais ameamua kujaza fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia chama hicho katika jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salum Kassim Ali alilithibitishia gazeti la Zanzibar Leo jana jioni, kwamba mgombea huyo hakurejesha fomu yake.

Hata hivyo, alieleza kuwa Kitole hajaitaarifu Tume ya Uchaguzi Zanzibar kitu chochote juu ya kushindwa kwake kurejesha fomu hiyo.

Chama cha Sauti ya Umma (SAU), kilianza mtafaruki mapema wakati wa uchukuaji fomu hiyo, baada ya wagombea wake wawili kujitokeza kwa wakati mmoja Tume ya Uchaguzi kutaka kuchukua fomu kuwania urais, jambo ambalo lilisababisha Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuwanyima fomu hizo.

Wanachama hao Kitole na mwenzake Haji Ramadhan walishindwa kukabidhiwa foimu hizo na kushauiriwa na tume hiyo wakakae ili waweze kutoa mgombea mmoja, na baadaye Kitole kwenda kukabidhiwa fomu hiyo.

Wakati huo huo, mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia kwa Chama cha Jahazi Asilia, Kassim Ali Bakari jana alirejesha fomu hiyo majira ya saa 7:30 mchana, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinyichande alizipokea fomu hizo, baada ya kukamilisha taratibu za ujazaji wa fomu.

Mgombea huyo alisema pindi akipewa ridhaa ya kuongoza ataweka mbele kukuza uchumi wa nchi katika kukabiliana na soko la Afrika Mashariki pamoja na kuimarisha kilimo.

Mgombea mengine aliyerejesha fomu ya Urais wa Zanzibar kutoka Chama cha Mwamko wa Umma (NRA), Haji Khamis Haji ambae alifika majira ya saa 8:00 mchana katika Makao Makuu ya Tume hiyo kwa ajili ya kurejesha fomu hizo.

Mwenyekiti wa ZEC, Khatib Mwinyichande alipokea fomu hizo, ambapo alimpongeza kwa kuweza kurejesha fomu hizo kabla ya muda wa mwisho kumalizika.

Nae, Mgombea Haji Khamis aliipongeza ZEC kwa kufanya kazi vizuri na kuwahimiza viongozi wa tume hiyo kuendelea kusimamia sdemokrasia vizuri.

Kutokana na kung'oka kwa mgombea wa SAU, sasa wagombea Urais wa Zanzibar wamebakia saba ambao ni Dk. Ali Mohammed Shein (CCM), Maalim Seif Sharif Hamad (CUF), Haji Ambar Khamis ( NCCR Mageuzi), Juma Ali Khatib (TADEA), Said Soud (AFP), Haji Khamis Haji (NRA) na Kassim Ali Bakari wa Jahazi Asilia.

KIFICHO KUFUNGUA ITIFAKI YA KIMATAIFA

Kificho kufungua itikafu ya kimataifaNa Mwajuma Juma

SPIKA wa Baraza la Wawakilishi aliyemaliza muda Pandu Ameir Kificho leo anatarajiwa kuifungua Itikafu ya Kimataifa itakayofanyika huko katika Msikiti wa Said Washoto Welezo Wilaya ya Magharibi Unguja.

wenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Itikafu Khatib Twahir, alilieleza hayo alipokuwa akizungumza na muandishi wa hizi huko Welezo wilayani ya Magharibi.

Alisema Itikafu hiyo itakuwa ya siku tisa au kumi itaaza majira ya saa 10:45 za jioni ambapo itajumuisha waumini wa dini ya kiislamu zaidi ya 500, kutoka nchini mbali mbali za ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti huyo alisema tayari baadhi ya wawakilishi kutoka nchi zitakazoshiriki Itikafu hiyo wameshawasili ambapo wengine waltarajiwa kuingia mchana wa jana.

Twahir alizitaja baadhi ya waumini waliokwisha wasili ni kutoka nchi za Burundi, Uganda, Zambia na Pemba, ambapo nchi zilizotarajiwa kuwasili jana ni Kenya, Malawi na Tanzania Bara.

Alifahamisha kwamba katika Itikafu hiyo zilitarajiwa kuwasili nchi 10 lakini kwa sasa hivi zitashiriki nchi nane baada ya Oman na Emirates kushindwa kuwasilishwa washiriki wao.

Itikafu ya Kimataifa hufanyika kila mwaka ifikapo mwezi 20 wa Ramadhan, ambapo katika kikao hicho waumini kupata fursa ya kusoma hadithi, qurani na kutoa mawaidha.

Aidha pia kufanyika mashindano ya kuhifadhi qurani na hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W) kwa vijana waliochini ya umri wa miaka 16.

Mwenyekiti huyo alisema Itikafu ya mwaka huu kiasi cha shilingi milioni 20 zinatarajiwa kutumika.

MUFTI KUZIKWA LEO.

Mufti kuzikwa leo

Na Mwandishi wetu

MUFTI Mkuu wa Zanzibar, marehemu Sheikh Harith bin Khelef, anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Muyuni, Mkoa wa Kusini Unguja.

Taarifa zilizotolewa na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, zimeeleza kwamba, kabla ya mazishi Mufti atasaliwa saa tatu asubuhi Masjid Mushawwar, Muembeshauri Mjini Zanzibar na kuondoka hapo kuelekea Muyuni kwa mazishi yatayofanyika saa nne asubuhi.

Maiti ya Mufti huyo iliwasili Zanzibar jana jioni, ikitokea India, ambako marehemu alifariki akiwa matibabuni.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere Mjini Dar es Salaam, mapokezi ya maiti ya Mufti, yaliongozwa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Katiba na Utawala Bora, Abdulghani Himid Msoma, pamoja na wanafamilia na watendaji wa Ofisi ya Mufti wakiongozwa na Katibu wa Mufti, Sheikh Fadhil Soraga.

Marehemu Sheikh Harith alifariki dunia Alkhamis, huko Chenay, akiwa amelazwa hospitali kwa ajili ya matibabu kwa karibu wiki tatu.

Friday, 27 August 2010

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Amani Abeid Karume,(kushoto) akikagua gwaride la Jeshi la wananchi wa Kenya katika Uwanja wa Ndege wa Nchi hiyo jana,alipohudhuria Uzinduzi wa katiba mpya ya Nchi hiyo, akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Mrisho Kikwete,(kulia) mwenyeji wake waziri wa Usafirishaji wa Kenya Chirau Ali Mwakwere.(Picha na Ramadhani Othman.)

Rais Karume Ashuhudia Kenya Ikizaliwa Upya.

Rais Karume ashuhudia Kenya ikizaliwa upya

 Kibaki aeleza matumaini ya mshikamano, maendeleo zaidi
 Wakenya wafurika Uhuru Park kukaribisha Katiba mpya


Na Mwandishi Maalum
WANANCHI wa Kenya jana waliingia katika ukurasa mpya wa historia ya nchi hiyo, baada ya Katiba mpya ya Taifa hilo kuzinduliwa na Rais Mwai Kibaki, katika sherehe kubwa iliyofanyika viwanja vya Uhuru Mjini Nairobi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, aliongoza Ujumbe wa Tanzania kushuhudia sherehe hizo kubwa za kuzaliwa upya kwa Jamhuri ya watu wa Kenya.

Dk. Karume aliongozana na viongozi mbali mbali akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa, waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, anaeshughulikia fedha na Uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame na Naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Iddi.

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Ali Mzee Ali, ambae pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Watu Sita ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia kura ya maoni, pamoja na Makamo Mwenyekiti wake na Mkuu wa Kambi ya upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakary.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Kenya waliohudhuria sherehe hizo, baada ya kutia saini Mswada huo kuwa Sheria, Rais Mwai Kibaki wa Kenya, alisema Katiba mpya inafufua matarajio ya wananchi wa Nchi hiyo kuhusu mustakbali wa maendeleo yao.

Kibaki aliieleza hadhara hiyo kwamba Katiba hiyo mpya, mbali ya kufungua ukurasa mpya wa historia ya Kenya, pia italibadilisha Taifa hilo kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Akizungumzia changamoto zitazotokana na Katiba hiyo mpya, Rais Kibaki aliwataka wananchi wa Kenya, kujenga matumaini zaidi kwa kuwepo muundo mpya wa uendeshaji nchi hiyo.

Aidha Kibaki aliwataka Wakenya kuitumia Katiba mpya kwa kubadilisha mitazamo na uendeshaji wa masuala ya kisiasa nchini humo.

"Kwa Katiba hii mpya tutabadilisha mitazamo ya kuendesha siasa nchini mwetu, jambo ambalo linategemea kuungwa mkono na Wakenya wote, ili kona zote za nchi yetu ziendelee." alisema Kibaki.

Katika hafla hiyo Rais Kibaki, alikula kiapo cha kuiongoza nchi hiyo kwa kutumia Katiba mpya, ambapo baadae Majaji na Wabunge pia waliapishwa kwa kutumia Katiba mpya.

Akimkaribisha Rais Kibaki kutoka hotuba yake, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alisema kuzinduliwa kwa Katiba hiyo ya Kenya, ambako kumeashiria kuzaliwa kwa mara ya pili Jamhuri hiyo ni kukamilika kwa safari moja na mwanzo wa safari nyengine kwa nchi hiyo.

"Kenya imeamka...hatutaki kurudi nyuma. Utawala mpya umeanza. Uongozi wa Kiimla na dhuluma tumeweka katika kaburi la sahau..." alisisitiza Raila.

Hotuba za sherehe hiyo zilianza kwa Makamo wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka kuwapongeza Wakenya kwa uzinduzi wa Katiba mpya.

Msanii maarufu wa Kenya, Eric Wainaina, alitumbuiza hadhara hiyo kwa wimbo maarufu wa 'Daima Kenya', wimbo ambao unapendwa kama wimbo wa taifa na wananchi wa nchi hiyo, kutokana na kutoa wito kwa Wakenya kuwa Wazalendo zaidi.

Pamoja na Rais Karume aliyeiwakilisha Tanzania, wageni wengine maarufu waliohudhuria sherehe hizo ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, Mke wa Rais Kibaki, Mama Lucy Kibaki, na Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel Arap Moi.

Wengine ni Rais wa Sudan, Omar Hassan Al-Bashir, Rais Abdalla Sambi 'Ayatollah' wa Visiwa vya Comoro, Rais Museveni wa Uganda na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Pia Rais Mstaafu wa Ghana, John Kuffour, Rais Mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo na Mke wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mama Grace Machel na Mwenyekiti wa Kamisheni Umoja wa Afrika (AU), Jean Ping.

Wananchi wa Kenya waliipitisha Katiba mpya kufuatia kupiga kura za maoni Agosti nne mwaka huu, ili kuunda Kenya mpya baada ya nchi hiyo kukumbwa na ghasia za kisiasa.

Huzuni Zatawala Kifo Cha Mufti Mkuu wa Zanzibar.

Huzuni zatawala kifo cha Mufti Mkuu Zanzibar


Alikuwa matibabuni India
Anatarajia kuzikwa kesho

Na Mwanajuma Abdi

MUFTI Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Harith bin Khelef Khamis amefariki dunia alfajiri ya kuamkia jana katika hospitali ya Meyot, Mjini Chenay, India.

Katika mahojiano na gazeti hili jana, mmoja wa watu wa familia yake, Abdallah Seif Khelef Khamis, akizungumza kutoka nyumbani kwa marehemu Migombani mjini hapa, alisema Marehemu alifariki dunia kati ya saa 10:00 na 10:24 alfajiri katika hospitali Meyot Chenay nchini India alikokuwa amelazwa.

Alisema Marehemu Sheikh Khelef alipelekwa matibabuni India wiki tatu zilizopita na kufikwa na mauti alfajiri ya jana.

Aidha, aliongeza kwa kusema kabla ya mauti yake, alifanyiwa upasuaji mdogo wa kibofu cha mkojo ambapo baadae alfajiri wanafamilia hao walijulishwa juu ya habari za msiba huo kwa njia ya simu.

Nae Katibu wa Mufti Mkuu Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga akitoa taarifa ya kifo hicho kwa vyombo vya habari, alifahamisha kuwa, nchi imepatwa na msiba mkubwa kwa kuondokewa na kiongozi wa dini visiwani, ambae alikuwa matibabuni India.

"Taarifa juu ya kifo cha Mheshimiwa Mufti Mkuu wa Zanzibar zimepokelewa alfajiri ya jana na mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu inaendelea kwa mashirikiano makubwa na ubalozi wetu nchini India," Alisema Sheikh Soraga.

Aidha, Soraga alisema maandalizi ya kuupokea mwili wa marehemu kwa heshima zote za kitaifa unaendelea na wananchi watajuulishwa kuwasili kwa maiti na siku ya maziko muda utakapofika", alifafanua Sheikh Soraga.

Hata hivyo, taarifa zilizotolewa na kiongozi mmoja

wa msikiti wa Mushawar, Mwembeshauri zilieleza kuwa mwili wa marehemu ulitarajiwa kuondoka India jana kupitia Qatar na baadae kuwasili Dar -es salaam.

Alisema maziko ya marehemu yanatarajiwa kufanyika kesho Jumapili.

Sheikh Soraga aliwataka waumini na wananchi wote kwa ujumla kuwa watulivu na kuungana pamoja katika kuukabili msiba huo mkubwa wa kitaifa, ambapo alisisitiza kubwa zaidi ni kumuombea Marehemu maghfira kwa Mwenyezi Mungu ili amlaze mahali pema peponi aamin.

Alisema Serikali iko pamoja na wafiwa wote katika msiba huo mkubwa na anawaomba wawe na subira katika kupokea qadar ya Mwenyezi Mungu.

Mufti Mkuu wa Zanzibar ameacha kizuka mmoja.

DK. Karume Kuzinduwa Nyumba ya Mpya ya Mayatima Zanzibar.

Dk. Karume kuzindua nyumba mpya ya Mayatima ZanzibarNa Mwanajuma Abdi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume leo, anatarajiwa kufungua nyumba ya kulelea watoto yatima ya kisasa Mazizini nje kidogo wa mji wa Zanzibar.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya ZAYEDESA, ambae pia ni Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Shadya Karume alisema Rais Karume ataifungua nyumba hiyo asubuhi kutokana kukamilika kwa ujenzi wake, ambapo sherehe hiyo itahudhuriwa na watoto wenyewe wa Forodhani na wageni mbali mbali.

Mama Shadya Karume alieleza nyumba ya watoto wa Yatima ya Mazizini imejengwa na Jumuiya ya ZAYEDESA, ambayo itatoa nafasi kwa watoto yatima wanaoishi nyumba ya kulelea watoto Forodhani waliokuwa chini ya udhamini ya Serikali kuhamia katika nyumba hiyo mpya.

Alifahamisha kuwa, kujengwa kwa nyumba hiyo kunatokana na nyumba ya Forodhani kuwa finyu ukilinganishwa na idadi ya watoto wanaolelewa kuongozeka.

Aidha alisema sababu nyengine ya kujengwa kwa nyumba hiyo ni Mji Mkongwe wa Zanzibar umekua zaidi katika shughuli biashara, utalii na kuongezeka kwa idadi ya watu, jambo ambalo Jumuiya ya ZAYEDESA imeona ipo haja ya kujenga nyumba nyengine itayowaweka watoto katika mazingira mazuri ya kujisomea, malaazi na kushiriki katika michezo kwa ajili ya kujenga afya kutokana nyumba ya Mazizini kuwa na eneo kubwa la kufanya shughuli hizo.

Alieleza nyumba mpya ya Mazizini itakuwa na darasa maalum la kusomea, chumba cha kompyuta na chumba cha kujifundisha ushoni kwa kutumia vyarahani kwa watoto wanaishi humo.

Mama Shadya Karume alisema kwamba, sehemu ya iliyokuwa ikitumiwa na watoto yatima Forodhani iliyochini ya Ustawi wa Jamii inatarajiwa kuwa ni Makumbusho ya Uhusiano wa Usafiri wa Bahari ya Hindi na Historia ya Zanzibar katika pwani ya Afrika Mashariki.

Thursday, 26 August 2010

Wanajeshi wa JWTZ wakifanya Usafi katika majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ikiwa ni kuadhimisha miaka 46 ya jeshi hilo, tangu kuanzishwa kwake.(Picha na Othman Msaulid)  

OPERESHENI YAGUNDUWA KUWEPO DAWA KADHAA FEKI ZANZIBAR.

Opresheni yagundua kuwepo dawa kadhaa feki ZanzibarNa Fatma Kassim, Maelezo

BODI ya Chakula Dawa na Vipodozi imegundua kuwepo dawa hatari endapo zitatumiwa na bindaamu.

Mrajis wa Bodi hiyo, Dk. Burhan Othman Simai alieleza hayo alipokuwa akitoa ripoti ya operesheni maalum iliyopewa jina la 'Operesheni Mamba III', ambayo iliendeshwa kwa kushirikiana jeshi la Polisi Tanzania na Shirika la Polisila Kimataifa Interpol.

Dk. Simai alisema katika operesheni hiyo, ilibainika kuwepo dawa zenye viwango duni na feki visiwani hapa ambazo nyingi zao hutengenezwa chini ya viwango kwa lengo la kujipatia kujipatia fedha za haraka.

Alisema Operesheni Mamba III, imegundua kuwepo aina ya dawa ya uzazi wa mpango iliyotengenezwa kwa miti shamba ambazo ina madhara makubwa endapo zitatumiwa na mwanamke.

Alisema iwapo mwanamke atatumia dawa hizo uzazi wa mpango ataongezeka uzito usio wa kawaida kutokwa na damu nyingi sambamba na mtoto atakayezaliwa na mama aliyetumia dawa hizo kupata ukubwa kabla ya kufikia muda.

"Dawa hii ya Kichina ya miti shamba ni hatari sana kwa mama na mtoto atakayezaliwa, akizaa wa mtoto wa kike atakua kabla ya siku zake na akiwa wa kiume takuwa na sauti nene kabla ya kufikia umri wa kubaleghe, pamoja na kuota nywele kwenye sehemu zao za siri kabla ya wakati ",alisema Dk. Simai.

Aidha katika ripoti hiyo, Mrajis huyo alianisha dawa nyengine feki zilizopatikana ni pamoja na dawa za kuongeza nguvu za kiume (urijali), chanjo feki ya pepo punda, dawa ya kutibia maleria na vipodozi vilivyopigwa marufuku.

"Madhara ya kutumia dawa bandia ni pamoja na kufeli kwa matibabu, usugu wa dawa na baadae hata kusababisha kifo", alisema Mrajis huyo.

Dk. Burhan alisema baada ya kuzikamata dawa hizo walizipima kwenye maabara yao pamoja na maabara ya Health science Authority ya nchini Singapore ambapo ilibainika kuwa hazifai.

Alisema tatizo la dawa duni na bandia ni ugaidi wa kibaologia na inaambatana na fedha chafu, uhalifu wa kifamasia, uhalifu wa hataza, uhalifu zidi ya ubinadamu na mauaji ya pole pole kwa ambae atatumia dawa zilizokuwa hazina viwango na zilizopita muda wa matumizi.

Alifahamisha kuwa takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni WHO kuhusiana na dawa feki na dawa bandia zinaonesha kuwa asilimia 10 ya dawa zilizo sokoni ulimwenguni ni bandia na feki na asilimia 25 dawa zipo katika soko la nchi masikini, na inakisiwa kuna watengenezaji wa dawa duni na bandia wanapata jumla ya dola bilioni 32.

Aliwataka wafanyabiashara kujali maisha ya watu na sio kufanya biashara tu kwa kujipatia fedha za haraka kwani athari kubwa itapatikana kufuatia dawa zilizopita muda, feki pamoja na vipodozi vyenye viambato vya sumu.

Operesheni hiyo ni ya kwanza na ya aina yake kufanyika Visiwani hapa ambapo ilifanyika sambamba kwenye nchi zote za Afrika Mashariki na ilifanyika Zanzibar nzima.

Marufuku kuchimba mchanga kwenye fukwe - Mazingira

Mwanajuma Abdi na Maryam Ally (MSJ)
IDARA ya Mazingira Zanzibar imesimamisha uchimbaji wa mchanga wa pwani katika Hoteli ya kitalii ‘Uroa Bay Beach Resort’ iliyopo Uroa Wilaya ya kati Unguja.

Hatua hiyo inafuatia Mkurugenzi wa Mazingira, Ali Juma na watendaji wa Idara walipofanya ziara ya ghafla katika hoteli hiyo na kujionea chungu za mchanga pembezoni mwa fukwe hiyo.

Alimuagiza Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo, Mussa Durio Savio kuwa haruhusiwi kuchimba mchanga katika fukwe kwani kufanya hivyo anaharibu mazingira kukiuka sheria za nchi.

Alisema sheria za nchi haziruhusu kuchimbwa mchanga wa pwani kwa ajili ya kufanya ujenzi katika sehemu nyengine.

Alimueleza kwamba, kuanza jana hawaruhusiwi kuendelea na uchimbaji huo ambapo wakikaidi amri hiyo atawafikisha mahakamani.

Aidha alionya juu ya tabia ya baadhi ya wamiliki wa hoteli kuchimba mchanga kwa ajili ya ujenzi na kuwataka kuacha mara moja.

Alisema fukwe nyingi katika ukanda wa utalii zimekumbwa na mmong’onyoko wa ardhi unaosababishwa na uchimbaji mchanga katika fukwe, ukataji ovyo wa mikoko na kuongezeka kina cha maji ya bahari.

Meneja Mkuu wa hoteli hiyo, Mussa alikiri kuchimba mchanga huo kwa ajili ya kujaza katika maeneo mbali mbali ya Hoteli yake kutokana kujitokeza kwa mashimo yanayosababishwa na mawimbi ya maji ya bahari yanayopiga kwa kasi kubwa.

Alisema wamelazimika kujenga ukuta ili kusaidia hali hiyo, ambayo inayojitokeza kutokana na mawimbi ya maji ya bahari yanapojaa.

Aidha alifafanua kuwa, hoteli hiyo haijaanza kazi rasmi, ambapo wanategemea kuifungua Julai mwaka huu katika msimu wa utalii.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Mkurugenzi wa Mazingira Ali Juma, alikwenda katika kijiji cha Kiwengwa, ambapo ametoa wiki mbili kuondosha vigogo vya miti vilivyowekwa pembenzoni mwa fukwe kwa ajili ya kuzuia mawimbi ya maji ya bahari, sambamba na uchimbaji wa mchanga wa pwani.

BAADHI YA WAGOMBEA URAIS ZANZIBAR NGOMA NZITO.

Baadhi ya wagombea Urais Z'bar ngoma nzito Wahaha kutafuta wadhamini dakika za mwisho


 Wengine wasingizia Ramadhan inawakwamisha


 Dk. Shein avunja rekodi kwa watu wengi kujitokeza

Na Mwandishi wetu

WAKATI muda wa mwisho wa kurejesha fomu za kuwania Urais wa Zanzibar ukikaribia hapo Agosti 30, baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo wamekumbwa na wakati mgumu katika kutafuta wadhamini 200 kutoka kila mkoa Zanzibar, hali inayozua hofu huenda baadhi yao watashindwa kufanikisha kazi hiyo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini licha ya baadhi ya wagombea hao kuchukua fomu za urais mapema, hadi sasa wamekuwa katika harakati kubwa za kutafuta wadhamini hao katika mikoa ya Unguja na Pemba huku mafanikio yakiwa ni madogo.

Ukiachia mbali mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein na yule wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambao walifanikisha kazi hiyo kwa urahisi, wagombea wengine wote bado hawajakamilisha kazi hiyo, licha ya baadhi yao kusema kwamba wameshafikia hatua nzuri.

Dk. Shein ambaye anarejesha fomu yake Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) leo saa nane mchana, kwa kishindo alivunja rekodi ya kupata wadhamini wengi waliojitokeza kutaka kumdhamini kote Unguja na Pemba na baadhi ya wanachama kulazimika kukosa fursa hiyo.

Alipokuwa kisiwani Pemba juzi, Dk. Shein alipata makundi ya wanachama wa chama hicho na wananchi waliotaka kupata fursa ya kumdhamini, hatua iliyopelekea baadhi yao kukosa nafasi hiyo na kushauri idadi ya watu wanaotakiwa kuwadhamini wagombea iongozwe ili wengi zaidi waweze kupata fursa hiyo.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia TADEA, Juma Ali Khatib alipozungumza na gazeti hili alisema kwamba alikuwa anaendelea na kazi hiyo ya kutafuta wadhamini katika mkoa wa Kaskazini Pemba na kwamba anatarajia kukamilisha kazi hiyo kabla ya muda wa mwisho.

Baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo walisema wamekuwa wakipata wakati mgumu kupata wadhamini hao kwa vile wananchi wengi hivi sasa hawapatikani kutokana na kuwepo katika harakati nyingi za mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

"Unajua wanachama wangu wengi ni wanawake ambao sasa wanakabiliwa na majukumu magumu majumbani kutokana na mwezi mtukufu wa Ramdhan", alisema mgombea mmoja wa Urais.

Mgombea wa Sauti ya Umma, Mussa Haji Kitole alisema kwamba alikuwa akiendelea vizuri na zoezi hilo katika mikoa ya Unguja kabla ya kuelekea Pemba kukamilisha wadhamini hao, ambapo amebakisha Mikoa ya Kusini Unguja na Kaskazini Pemba.

Wanachama wa chama hicho, wameeleza kuwa hali hiyo inasababishwa na kuendelea kuwepo mgogoro ndani ya chama hicho, ulioanzia kipindi cha uchukuaji fomu ambapo chama hicho kiliwasilisha majina mawili ZEC, badala ya moja kama sheria inavyotaka.

Mjumbe wa Baraza Kuu la SAU, Peter Magwira, amesema suala la kupata wadhamini hawalielewi maendeleo yake, kwa vile Mgombea analisimamia mwenyewe na kueleza kuwa mgogoro wao watauwasilisha kwa Msajili wa Vyama Kisheria kwa hatua, baada ya kumalizika uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake mgombea wa nafasi hiyo kupitia NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis alisema kwamba tayari amepata wadhamini wanaohitajika na hivi sasa fomu zake zinahakikiwa tume ya uchaguzi Zanzibar.

Alisema tayari ameshakula kiapo mahakamani kutimiza masharti yaliyowekwa na ZEC, kwa wagombea wa nafasi ya Urais.

Naye Juma Ali Khatib ameeleza kuwa atarejesha fomu Jumatatu ijayo asubuhi, baada ya kukamilisha wadhamini kwa mujibu wa sheria, ambapo ataiarifu ZEC leo kuhusu mpango wake huo.

Jumla ya wagombea wanane wamechukua fomu za kuwania nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Wagombea hao ni Dk. Ali Mohammed Shein kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF, Juma Ali Khatib wa chama cha TADEA, Haji Ambar Khamis wa NCCR Mageuzi na Said Soud wa AFP.

Wagombea wengine ni Kassim Ali Bakar wa chama cha Jahazi Asilia na Haji Mussa Kitole wa Sauti ya Umma na Haji Khamis Haji wa chama cha NRA.

TUKIO LA UVUNJWAJI MEZA MWANAKWEREKWE


Waliovunja ni wahuni - Halmashauri


L Manispaa kuburuzwa mahakamani


Husna Hamid na Hamisuu Abdalla, MCC
KADHIA ya uvunjwaji wa meza za wafanyabiashara katika soko la Mwanakwerekwe imeingia katika sura mpya, baada ya Halamshauri ya Wilaya ya Magharibi kueleza uvunjwaji huo umefanywa na wahuni.

Afisa mmoja katika Halmshauri hiyo, alilieleza gazeti hili kuwa hawaamini kama Baraza hilo linaweza kuchukua uamuzi wa kuzivunja meza za wafanyabishara hao, ikizingatiwa kuwahi kufanyika mazungumzo baina ya Halmashauri hiyo, Baraza la Manispaa pamoja na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha.

Afisa huyo ambaye alikataa katakata kutajwa jina lake gazetini, alisema kutokana na mazungumzo yaliyozishirikisha pande hizo, Manispaa haiwezi kuzivunja meza za wafanyabiashara hao ambao walitengewa eneo hilo kwa ajili ya kuondosha msongamano ndani ya soko kuu la Mwanakwerekwe.

"Manispaa haiwezi kuzivunja meza hizo kwani wanafahamu vilivyo uwepo wa wafanyabiashara nyuma ya soko hilo kufuatia mazungumzo ya pamoja tuliyowahi kuyafanya, nadhani waliovunja meza za wafanyabishara ni wahuni",alisema Afisa huyo.

Afisa huyo alithibitisha kuwa Halmashauri iliwapa wafanyabiashara eneo hilo kwani liko chini ya milki yao kwa mujibu wa sheria nambari 4 ya mwaka 1995.

"Hata hili soko liko kwenye eneo letu kwa mujibu wa mamlaka ya kiutawala lakini serikali imeamua kuwapa Manispaa", alisema.

Wakati huo, Afisa Habari wa Baraza la Manispaa alishindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa waandishi wa habari ambapo waliwataka waende kwa Mkuu wa Mkoa kutafuta habari hizi.

Naye Mohammed Gharib wa ZJMMC, anaripoti kuwa wafanyabiashara waliovunjiwa meza wanakusudia kuliburuza mahakamani Baraza la Manispaa la Zanzibar ambalo wanalituhumu kuhusika na uvunjaji wa meza hizo.

Katibu wa kamati ya wafanyabiashara hao Mkubwa Khamis Hamad alisema wameshafungua kesi katika kituo cha Polisi Mwanakwerekwe na wanachosubiri taratibu za sheria zitakazochukuliwa na jeshi hilo.

Mkubwa alisema katika jalada walilofungua kituoni hapo, malalamiko yao ya msingi ni kuvunjiwa meza zao mpya 13 ambapo kila moja meza ina gharama ya shilingi 130,000.

Alisema mbali ya meza hizo pia baraza hilo limevunja meza ndogo ndogo zipatazo 70 ambapo wamechukua hatua hiyo kinyume na utaratibu.

Katibu huyo alifahamisha kuwa pia eneo hilo ambalo meza zao zimevunjwa waliliwekea kifusi gari nane huku kila gari moja ikigharimu shilingi 130,00.

"Waliingia na kuvunja kupitia lango kubwa la soko na baada ya kufika hapa walimuamuru mlinzi wetu aondoke na kuzivunja meza zetu", alisema Katibu hiyo.


Nao Salma Lusangi (ZJMMC), Kassim Kassim (TUDARCO), wanaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi na Baraza la Manispaa kuzungumza kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.

Alisema alimuomba Mkurugenzi wa Manispaa awaachilie wafanyabiashara hao kuendelea na biashara zao katika eneo hilo kwa kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani huku likitafutiwa ufumbuzi wa kudumu suali hilo juu ya nani mmiliki halali wa eneo hilo.

Aidha Katibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi alithibitisha juu ya kuwaruhusu wafanyabiashara hao kuwepo katika eneo hilo huku wakijua ni sehemu ya Halmashauri kutokana na sheria nambari 4 ya mwaka 1995.

Alisema siku nyingi eneo hilo lilikuwa na mgogoro baina yao na Baraza la Manispaa wakidai ni eneo lao lakini Wizara husika itaendelea kushughulikia suali hilo.

Aidha alisikitika kwa kitendo walichofanyiwa wafanyabiashara hao bila kuarifiwa juu ya uamuzi wa kuondolewa eneo hilo wakati serikali inahimiza vijana kujiajiri wenyewe katika kujitafutia riziki zao za halali.

MICHEWENI BADO WALIA NA AJIRA ZA WATOTO

Micheweni bado walia na ajira za watoto

Zaidi ya 100 hukosa kuhudhuria masomo kwa mwezi

Na Bakari Mussa, Pemba

ZAIDI ya watoto 100 katika Skuli ya Msingi Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wanakosa fursa ya kuhudhuria skuli kila mwezi.

Mwalimu Mkuu skuli ya msingi, Micheweni Kai Pandu Kai amesema idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 1,720 wa Skuli, ambao wamebainika kujihusisha na ajira za watoto.

Alisema umasikini wa kipato umesababisha ongezeko ajira zisizokuwa salama kwa watoto, hali ambayo imeathiri zaidi vijiji vya Micheweni na Vitongoji vyake.

"Watoto wanne hadi watano wanakosa masomo kila siku kwa kila darasa na kubakia wastani wanafunzi 58 kila darasa.

Aliendelea kusema kuwa Skuli imekuwa ikishirikiana na kamati mbali mbali za Vijiji na Shehia wakiwemo Wazazi lakini imeonekana baadhi ya Wazazi kuwa na mawazo finyu juu ya suala hilo kwa kisingizio cha Umaskini wa kipato.

Unapomwambia mzazi juu ya kumpeleka mtoto wake skuli anakwambia yeye hana uwezo labda umsaidie….. wakati na wewe una wako anataka elimu,” alisema mwalimu huyo.

Aliongeza kuwa tatizo la ajira za watoto lipo katika Skuli ya Micheweni na lina athari kubwa kwa vile wanafunzi walio wengi huwa hawaendi skuli kikawaida.

Hata hivyo, alisema skuli yake imeanza kupata unafuu kutokana na misaada inayopata kupitia kamati mbali mbali za taasisi zisizokuwa za kiserikali kama PIRO, yenye Makao makuu Chake Chake, Pemba.

Kwa jumla Mwalimu huyo alisema baada ya wazazi kupatiwa taaluma ya kutosha sasa wameamua kuwarejesha watoto wao skuli badala ya utaratibu wa zamani ambapo walikuwa wakiwapeleka malezini na kuingia kwenye ajira mbaya.

Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo, Omar Mwinyi Suwed, alisema skuli hiyo imepoteza wanafunzi watatu waliofariki mwaka 2008/2009 kwa kujihusisha na ajira za uchimbaji mawe baada ya muda wa skuli na wengine wawili walipoteza maisha kwenye uchimbaji mawe.

Aidha, Msaidizi Mwalimu huyo alisema pamoja na hali ya umasikini lakini ushirikiano mdogo kati ya walimu na uongozi wa majimbo huchangia kuwepo ajira hizo.

Ajira zinazowavutia vijana hao ni pamoja na uvunjaji wa mawe, kupara Samaki, uchungaji wa mifugo, uvuvi na ukataji wa matufali na wanaojihusisha zaidi ni wanafunzi wa msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la Saba.

Katika hali kama hiyo, Mwalimu Muu wa Sekondari Micheweni, Mutrib Hamad Mbarouk , alisema wanafunzi 80 hadi 100 wa Sekondari Micheweni Pemba, hawahudhurii skuli kila siku, wengi wao wakiwa katika ajira hizo.

Mwalimu mkuu huyo wa Sekondari ya Micheweni Pemba aliwahimiza wazee kufahamu faida ya elimu na kusema rasilimali pekee inayomfaa mtoto ni elimu na sio ajira ya Muda.

Alisema bila elimu maisha ya binadamu yanakosa baadhi ya mambo hivyo akahimiza watoto wsapatiwe elimu ili hatimae wajiendeshee maisha yao kwa uhakika zaidi.

Pamoja kuzungumzia wanafunzi wa madarasa ya chini lakini mwalimu huyo alisema hata wanafunzi wa elimu ya juu nao wanavutika na ajira hizo na kuathiri mwenendo wao wa masomo.

“Tunashirikiana na Kamati ya Skuli na Walimu wa Ushauri Nasaha, Masheha na Watu maarufu wa Vijiji kupita kwa Wazazi kuwaeleza tatizo la watotowao na ajira hizo ingawaje mafanikio sio makubwa” alisema.

Hata hivyo, afisa elimu Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Sheha, amesema kwa upande wa Afisi yake hajapokea kesi ya aina yoyote juu ya sula hilo hata mara moja na yeye anasikia hivo hivo.

"Zamani sana alipokuwepo Kamanda wa Polisi Mbirikira, katika Mkoa wa Kaskazini, yeye alikuwa ananieleza pindipo akipata kesi za aina hiyo,” alimaliza afisa huyo.

Micheweni ni eneo ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imwekeza nguvu nyingi na kukifanya ‘Kijiji cha Milenia’, ili kuhakikisha inawakomboa wananchi wa eneo hilo na umasikini.

Aidha huduma mbali mbali muhimu za kijamii kama vile barabara, afya na elimu, zimeimarishwa kimiundombinu, ikiwa ni kijiji cha mfano wa kupambana na umasikini Zanzibar, lakini bado muamko na kubadilika wananchi wake ni kudogo.

Wednesday, 25 August 2010

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume, akizungumza na Mabalozi wa Heshima wa Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wakati ujumbe huo wa mabalozi ulipofika Ikulu Mjini Zanzibar.(Picha na Othman Maulid)     

JWTZ KUSAFISHA HOSPITAL MJI WA ZANZIBAR

JWTZ kusafisha hospitali, mji wa Zanzibar


Na Mwantanga Ame (ZJMMC)

JESHI la Waananchi Tanzania, (JWTZ), litazifanyia usafi Hospitali za Zanzibar pamoja na maeneo mbali mbali ya kijamii katika Mji wa Zanzibar.

Jeshi hilo la wananchi litachukua hatua hiyo ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 46 tangu kuanzishwa kwake.

Jeshi la Wananchi wa Tanzania lilianzishwa rasmi Septemba 1, 1964, baada ya vijana 1,000 kutoka Jeshi la Ukombozi Zanzibar (JLU) na Kings African Rifles (KAR) kutoka Tanzania bara kumaliza mafunzo yao ya pamoja.

Taarifa ya Jeshi hilo iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari hapa imeeleza kuwa kazi hizo zinatarajiwa kuanza leo katika maeneo mbali mbali ya Mji wa Zanzibar na Kisiwani Pemba.

Baadhi ya maeneo ambayo yatafanyiwa usafi kwa mujibu wa tarifa hiyo ni pamoja na Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Bustani ya Jamhuri, Maruhubi Miembe mingi na Kinazini.

Eneo jengine ambalo wanajeshi watafanya kazi ya usafi ni pamoja na la Uwanja wa Ndege, Bustani ya migombani, Hospitali ya Wazee Welezo Beit Ras Chuo cha Ualimu na sehemu nyengine.

Aidha zoezi hilo pia litaihusisha hospitali ya Kivunge pamoja na Hospitali za SMZ iliopo Chake Chake na Vitongoji, kazi kama hizo pia zinatarajiw akufanyika katika maeneo kadhaa ya Tanzania bara.

WAZANZIBARI KUMTUNZA DK. KARUME

Wazanzibari kumtunza Dk. KarumeIssa Mohammed

MKUU wa Mkoa mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis amesema kuwa wananchi wa Zanzibar watamtunuku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Aman Abeid Karume nishani ya Uongozi Mahiri.

Akizungumza na waandishi wa habari afisini kwake Vuga mjini hapa, Mkuu huyo alisema hatua hiyo inatokana na kiongozi huyo kuiongoza vyema Zanzibar katika kipindi cha miaka 10.

Alisema nishani hiyo atakatotunzwa Dk.Karume itakuwa ya dhahabu ambapo itakabidhiwa kabla ya kumalizika kipindi cha uongozi wake.

Alifahamisha kuwa wazo la kutunukiwa nishati kiongozi huyo limetokana na yeye na kwamba limeungwa mkono na wananchi kadhaa wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa.

Alisema baadhi ya wananchi wamechangia kiasi cha fedha za kununua dhahabu ya kutayarishia nishati hiyo ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni tano zimekusanywa kwa ajili hiyo.

Mkuu wa mkoa aliwataja baadhi ya waliochangia fedha hizo kuwa ni Chama cha Mapinduzi kilichotoa shilingi milioni mbili na chama cha wananchi CUF kilichotoa shilingi milioni mbili.

Aidha alisema maskani ya Dk. Mohammed Gharib Bilal imechangia shilingi milioni moja na kwamba wananchi kadhaa wameahidi kuchangia fedha kwa ajili yakifanikisha utayarishaji wa Nishati hiyo.

Mkuu wa mkoa amewataka wananchi wengine kuchangia mpango huo kwa kupitia afisi za wakuu wa wilaya za Unguja na Pemba.

DK. KARUME AWAELEZA MABALOZI WA MESHIMA MAFANIKIO YA MKUZA .

Dk. Karume awaeleza Mabalozi mafaniko ya MKUZA


 Asema sekta nyingi za kijamii, kiuchumi zimeimarika

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amesema kuwa juhudi za makusudi za kupambana na umasikini na kukuza uchumi zimechukuliwa hapa Zanzibar kupitia MKUZA na kuweza kupata mafanikio makubwa.

Rais Karume aliyasema hayo jana wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Mabalozi wa Heshima wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya nchi, yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umasikini, MKUZA umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika suala zima la kupambana na umasikini na kukuza uchumi hapa Zanzibar.

Rais Karume alieleza kuwa juhudi za makusudi zimeweza kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha maendeleo endelevu yanaimarika nchini kwa kuweza kuimarisha Mkakati huo.

Rais Karume alisema kuwa Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo hatua ambayo imeweza kustawisha ustawi wa jamii na ukuzaji uchumi.

Aidha, Rais Karume aliueleza ujumbe huo kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana Zanzibar katika sekta zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Akieleza kwa upande wa sekta ya utalii, Rais Karume alisema kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta hiyo ambayo hivi sasa imekuwa ni muhimili mkuu wa uchumi.

Alieleza kuwa wawekezaji mbali mbali wameweza kuekeza Zanzibar katika sekta ya utalii ambayo imeonekana kuimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Rais Karume pia, aliupongeza ujumbe huo wa Mabalozi wa Heshima kwa ujio wao hapa Zanzibar sanjari na mafunzo waliyoyayapata ya wiki moja yaliyofanyika hapa nchini.

Pamoja na hayo, Rais Karume aliueleza ujumbe huo kuwa ujio wao umekuja wakati muwafaka ambapo Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wake kwa lengo la kujipatia maendeleo endelevu kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Nae kiongozi wa ujumbe huo wa Mabalozi wa Heshima, Balozi Dallas Browne alimueleza Rais Karume jinsi ujumbe huo ulivyofarajika kufika Zanzibar na kujionea hatua mbali mbali za maendeleo zilizofikiwa.

Dk. Dallas alieleza kuwa hatua za maendeleo yaliyofikiwa Zanzibar ni ya kujivunia na kuyatangaza ndani na nje ya nchi.

Aidha, ujumbe huo ulipongeza mafanikio yote ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yaliyopatikana Zanzibar.

Pamoja na hayo, ujumbe huo ulimpongeza Rais Karume kwa hatua na juhudi kubwa za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar, chini ya uongozi wake.

DK, SHEIN WANACCM PEMBA PUUZENI GHILBA ZINAZOENEZWA.

Dk.Sheni: Wana CCM Pemba puuzeni ghilba zinazoenezwa

 Ni madai ukipigia kura upinzani sawa na umempigia yeye


 Nahodha ataka kambi zivunjwe auungwe mkono Dk. sheni


Abdulla A. Abdulla, Pemba

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohammed Shein amewasihi wanachama, wapenzi na wananchi kisiwani Pemba kutoghilibika na kauli za wapinzani zinazodai kuwa kuwapigia kura wapinzani ni sawa na kumpigia kura Dk. Sheni.

Dk. Shein alisema hayo huko Mkoani, Kusini pemba katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu Kisiwani Pemba ya kuzungumza na viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali katika chama hicho.

Alisema tayari wapinzani wake wameshaanza kupiga kampeni za nyumba kwa nyumba na kuwaeleza wananchi kuwa kutokana na maridhiano yaliyopo hivi sasa wakimpa kura mpinzani ni sawa na kumpa Dk. Sheni, jambo ambalo halina ukweli.

Aidha, mgombea huyo alisema chama CCM mwaka huu kinakusudia kufanya kampeni za kiistaarabu zenye lengo la kudumisha amani na kuepusha bughudha mitaani.

Wakati huo huo, Waziri Kiongozi wa Zanzibar na Mlezi wa Chama cha CCM katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, Shamsi Vuai Nahodha alitaka kundi lililokuwa likimuunga mkono alipokuwa akiwania urais livunjike na limuunge mkono Dk. Sheni.

Nahodha aliyasema hayo alipokuwa akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya viongozi wa Mkoa huo katika mkutano wa Mgombea Urais huyo na viongozi wa Chama wa ngazi mbali mbali uliofanyika Micheweni.

Nahodha alisema, Dk. Ali Mohammed Shein ni kiongozi makini, mwenye uwezo mkubwa na uzoefu wa muda mrefu wa kuongoza, hivyo chama hakikufanya makosa kumteuwa kupeperusha bendera ya Zanzibar.

“Ushindi wa CCM ni ushindi wetu sote wala hatutopoteza, iwapo Dk. Shein atashinda na kuwa Rais wa Zanzibar kwani yeye ni Mwana CCM”, alisema Nahodha.

Waziri Kiongozi alisisitiza kuwa CCM ina viongozi wazuri wengi wanaofaa kwa sasa na baadaye, hivyo kumuunga mkono Dk. Shein ni kuendelea kuwekeza ili kurahisisha urithi wa madaraka baada ya kumaliza muda wake wa uongozi.

WALIMU WALIOSIMAMISHWA CHUO CHA KIISLAM UTETEZI WAO KUZINGATIWA LEO.

Walimu waliosimamishwa Chuo cha Kiislamu utetezi wao kuzingatiwa leo


Na Mwantanga Ame (ZJMMC)

BAADA ya Uamuzi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuusimamisha Uongozi wa walimu wa Chuo cha Kiislamu Zanzibar, leo Wizara hiyo inakusudia kukaa na kulizungumzia suala hilo.

Uongozi huo ulisimamishwa wiki mbili zilizopita akiwemo Mkuuwa chuo, baada ya Wizara hiyo kubaini kuwapo kwa baadhi ya walimu kuhusishwa na mchezo mchafu wa kupokea rushwa kutoka kwa wanafunzi .

Uamuzi wa kusimamishwa walimu hao ulitokana na madai ya kuwepo wanafunzi ambao waliingia katika Chuo hicho kwa njia ambazo hazikustahili kwa vile walikosa sifa za kujiunga na chuo hicho kwa ngazi ya Stashahada.

Kubainika hilo Wizara hiyo iliamua kuwasimamisha baadhi ya wanafunzi waliobainika kufanya udanganyifu huo ambao walikuwa wakiendelea kuchuku mafunzo kwa ngazi ya Stashahada.

Mbali ya kusimamishwa kwa wanafunzi hao Wizara hiyo pia iliwataka walimu wa hao kuwarejeshea fedha walizozitoa wanafunzi hao kwa ajili ya kujiunga na Chuo hicho.Akizungumza na Zanzibar Leo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abdllah Suleiman alisema uongozi wa Wizara hiyo unakusudia kulifanyia kazi suala hilo leo ambapo kutakuwa na kikao cha kutathmini tukio hilo.Alisema hatua hiyo Wizara inaichukua baada ya kuwapa muda walimu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo kutoa maelezo yao juu ya kujitetea.Alisema katika kikao hicho Wizara hiyo itapitia utetezi huo na baadae kuona ni hatua zipi itaweza kuzichukua kwa vile walimu hao hivi sasa wamesimamishwa ili kuweza kupisha uchunguzi kufanyika juu ya tukio hilo.Naibu huyo alieleza kuwa kikao kitachokaa leo kitakuwa ni cha ndani ambapo kitauhusisha uongozi wa juu pekee wa Wizara hiyo baada ya wadaiwa hao kumaliza kutoa utetezi wao.Hata hivyo, hakueleza wazi kama kikao hicho baada ya kumaliza kama kitakuwa ndio hatma ya tukio hilo kwani kitazingatia na upande mwengine kama utahitaji kufanyiwa kazi zaidi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonsos Lenhardt alipofika Ikulu Mjini  Zanzibar kuonana na Rais jana, ambapo aliwasilisha salamu rasmi za Rais Obama wa Marekani.(Picha na Ramadhani Othman )    

Tuesday, 24 August 2010

CUF YAPATA PIGO

CUF yapata pigo Wagombea wake wawili wafariki dunia

Na Mwantanga Ame, ZJMMC

WAGOMBEA wawili wa nafasi za ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Oktoba mwaka huu, kupitia chama cha CUF, wamefariki dunia.

Wagombea hao ni aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kojani, Omar Ali Jadi, aliefariki katika hospitali ya Chake Chake baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa ini kwa muda mrefu, na aliyekuwa mgombea Udiwani wa Wadi ya Kilimani, jimbo la Kikwajuni, Shani Ahamada Shani aliyefariki kwa ajali ya barabarani juzi.

Jadi alikuwa Mwakilishi wa Jimbo Kojani tangu mwaka 1995 na katika kipindi cha miaka 20 aliyoteuliwa kuwa Mwakilishi na miaka mitano kati ya hiyo alikuwa ni miongoni mwa Wawakilishi waliofukuzwa baada yakushindwa kuingia katika vikao vitatu mfululizo kutokana na msimamo wa chama hicho kususia matokeo ya uchaguzi huo.

Mbali ya kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kojani, Jadi pia alikuwa ni Mjumbe wa Mkutano mkuu Taifa wa CUF na pia alikuwa ni Mjumbe wa Mkutano mkuu wa Wilaya ya Wete Pemba.

Katika baraza la Wawakilishi lililovunjwa hivi karibuni Jadi alikuwa mjumbe wa kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Mawasiliano na Ujenzi.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani alisema Mwakilishi huyo alifariki juzi usiku alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo ya Chake Chake.

Alisema CUF imepokea taarifa ya vifo hivyo kwa masikitiko makubwa kutokana na kutegemea mchango wa Mwakilishi pamoja na mgombea Udiwani kuendeleza Changamoto katika chama hicho katika kukipatia ushindi katika uchaguzi Mkuu ujao.

"Kifo ni mapenzi ya Mungu, lakini tumepata pigo kubwa sana kwani alikuwa Wagombea wetu walikuwa ni changamoto muhimu kwa uchaguzi Mkuu ujao" alisema Msemaji huyo.

Bimani alisema Jadi, alikuwa tayari ameshapitishwa na wananchi wa Jimbo la Kojani na Baraza Kuu la CUF, kukiwakilisha chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao jambo ambalo litawatia huzuni kwa wananchi wa Jimbo hilo.

Hapo awali msemaji huyo alifahamisha kutokana na ugonjwa huo kumsumbua kwa muda Mwakilisi huyo aliweza kupatiwa matibabu na Afisi ya Baraza la Wawakilishi kaika Hospitali za Tanzania Bara katika pindi cha mienzi minne iliopita.

Alisema kutokana na kifo cha Mgombea huyo chama hicho kitamsimamisha Hamad Omar Hamad, aliyechukua nafasi ya pili kwenye kura ya maoni.

Alisema hadi anafariki Mwakilishi huyo alikuwa tayari ameshachukua fomu Afisi za Tume ya Uchaguzi Wilaya Kisiwani Pemba kwa ajili ya kuomba kuwania Jimbo hilo na alikuwa bado hajairejesha.

Mazishi ya Jadi ylifanyika jana huko Kojani ambapo Spika wa Baraza hilo aliyemaliza muda wake, Pandu Ameir Kificho, katibu wa Baraza Ibrahim Mzee na maofisa wa baraza hilo walihudhuria mazishi hayo, huku Chama cha CUF kiliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Machano Khamis Ali.

Katika hatua nyengine Bimani alifahamisha kuwa aliyekuwa mgombea wa Udiwani Jimbo la Kikwajuni, Shani Ahmada Shani,(63), Mkaazi wa Miembeni Mjini Unguja, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akielekea ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar kurejesha fomu yake baada ya kuijaza.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib, Aziz Juma ambapo alisema kuwa Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Wakati huo huo mtu mmoja Mkaazi wa meli nane Jecha Haji Khamis, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari lenye namba Z 497 AL aina ya Escudo katika eneo la Bububu Wilaya ya Mjini Unguja.

Kamanda Aziz, alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo ambapo alieleza kuwa mtu huyo aligongwa na gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Matendo Andrew Mgeni saa 3:30 za asubuhi juzi.

Kamanda huyo alisema kuwa watuhumiwa wote wapo mikononi mwa Polisi wakiendela kufanyiwa uchunguzi ili kujua chanzo cha ajali hiyo.

NRA NAYO YASIMAMISHA MGOMBEA URAIS ZANZIBAR

NRA nayo yasimamisha mgombea Urais Z'bar


Mwanajuma Abdi na Kassim Kassim, TUDARCO

MGOMBEA wa Chama cha Muamko wa Umma (NRA), Haji Khamis Haji, jana alijitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar katika Makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Maisara mjini hapa.

Mgombea huo amefanya idadi ya wagombea waliochukua fomu za kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar katika Tume hiyo kufikia wanane hadi sasa, ambapo Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali alimkabidhi fomu mgombea huyo majira ya saa nne asubuhi.

Mkurugenzi huyo wa Tume ya Uchaguzi akimsomea maelezo ya fomu hizo, alimueleza mgombea anatakiwa kuzijaza fomu hizo kwa usahihi, ambapo siku ya mwisho ya kurejesha fomu Agosti 30, majira ya saa 10:00 jioni.

Aidha alimpongeza mgombea huyo kwa uamuzi wake wa kufika afisini hapo kuchukua fomu za kuwania kiti cha Urais Zanzibar.

"Kwa mujibu wa barua ya chama cha NRA ya Agosti 23 kimemteua Haji Khamis Haji kuwa mgombea wake wa kiti cha Urais Zanzibar," alisema Salum.

Nae Mgombea wa Urais kwa tiketi ya NRA, Haji Khamis Haji alisema ameamua kuchukua fomu ili chama chake kiwe mbadala katika kuelekea Serikali ya Umoja wa Kitaifa badala ya kuviacha vyama viwili vyenye ushindani vya muda mrefu vya CCM na CUF.

Alisema chama hicho kimeamua kuingia katika mchakato huo ili kuweza kuleta mageuzi ya kisiasa na kiuchumi nchini.

Wakati huo huo, wagombea wa Udiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Yussuf Idrissa anayewania udiwani Wadi ya Magomeni na Takidir Hamad Suleiman anayewania Wadi ya Meya wamerejesha fomu za uteuzi wa nafasi hizo katika Afisi ya Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Mjini Unguja jana.

Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Mjini, Mwanapili Khamis Mohammed alizipokea fomu hizo baada ya kuzifanyia uhakiki na kuwataka wagombea hao kufika katika Afisi hiyo Agosti pili, majira ya saa 10:00 jioni, kuja kuangalia pingamizi ama wao kama wanataka kuwawekea pingamizi wagombea wenzao.

Wagombea hao wamefika majira saa tano asubuhi katika Afisi hiyo wakiwa wameongozana na mapikipiki na gari mbali mbali.

RAIS OBAMA AMPONGEZA DK. KARUME

Rais Obama ampongeza Dk. Karume


 Avutiwa na ukuaji demokrasia Zanzibar


 Asema mafanikio ya kisiasa Zanzibar ni chachu ya maendeleo


 Rais Karume asema Wazanzibari wanajivunia amani, utulivu uliopo

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Marekani Barack Obama ametoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, kutokana na mafanikio ya kisiasa yaliofikiwa Zanzibar.

Pongezi hizo zilitolewa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Leinhardt kwa niaba ya Rais Obama, Ikulu mjini Zanzibar na kueleza kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kupatikana ridhaa ya Wazanzibari katika uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.

Katika maelezo yake, Balozi Leinhardt alimueleza Rais Karume kuwa hatua hiyo imeonesha wazi kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa kidemokrasia na ndio sababu kubwa iliyomvutia Rais Obama.

Leinhardt alisema kuwa Marekani ina matumaini makubwa kuwa Zanzibar itazidi kupata maendeleo endelevu kutokana na mafanikio hayo yaliofikiwa sambamba na uongozi imara wa Serikali ya Mpinduzi Zanzibar.

Balozi huyo wa Marekani alimuhakikishia Rais Karume kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi mbali mbali ya maendeleo.

Akieleza juu ya mradi wa teknolojia ya kompyuta kwa wanafunzi wa skuli za Zanzibar, Balozi Leinhardt alimueleza Rais Karume kuwa nchi yake itasaidia kuendeleza mradi huo ambao utakuwa kwa Tanzania nzima lakini Zanzibar imechaguliwa kuwa ni sehemu ya kuanzia.

Katika mradi huo lengo ni kumfanya kila mwanafunzi kuwa na kompyuta yake kwa ajili ya kujisomea pamoja na kupata elimu zaidi kupitia kifaa hicho.

Aidha, Balozi Leinhardt alieleza kuwa mbali ya nchi yake kutoa misaada mikubwa katika kuimarisha miradi ya maendeleo hapa Zanzibar kupitia MCC, ikiwemo ujenzi wa baadhi ya barabara kisiwani Pemba pamoja uwekaji wa umeme mpya kutoka Dar-es-Salaam hadi Zanzibar, nchi yake itaendelea kuisaidia zaidi Zanzibar.

Balozi Leinhardt alisisitiza kuwa katika nchi nyingi duniani ambazo zimepata maendeleo juhudi kubwa zimefanywa katika kuimarisha sekta ya nishati na elimu ambazo kwa Zanzibar ni miongoni mwa sekta ambazo zimepata mafanikio makubwa na zimeimarika kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na hatua hiyo, Balozi huyo alisema kuwa Marekani inathamini juhudi hizo za Zanzibar na kusisitiza kuwa itaendelea kuwasaidia wananchi wa Zanzibar katika maendeleo yao.

Sambamba na hayo, Balozi Leinhardt alitoa pongezi kwa Rais Karume kwa uongozi wake imara uliopelelea Wizara zote zilizo chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata mafanikio mazuri chini ya Mawaziri wake pamoja na watendaji wake wengineo.

Nae Rais Karume alimueleza Balozi Leinhardt kuwa mafanikio hayo ya kisiasa yaliopatikana Zanzibar si ya viongozi peke yao bali ni ya Wazanzibari wote.

Rais Karume alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanajivunia amani na utulivu iliopo nchini mwao na ndio maana waliamua kuuendeleza utamaduni huo kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wao.

Alieleza kuwa Wazanzibari wenyewe waliona jinsi nchi yao inavyokuwa wakati wakikaribia kuingia kwenye uchaguzi mkuu, ambapo utulivu na mshikamano hupotea kiasi ambacho husababisha kukosekana kwa amani na ndio maana wakaamua kutafuta njia ya kuimarisha umoja na mshikamano wao.

Rais Karume alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano, ushirikiano na misaada mbali mbali ya kimaendeleo inayotolewa na Marekani na kuahidi kuwa Zanzibar itaendeleza ushirikiano huo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume Karume alisema kuwa Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kupiga vita Malaria ambapo juhudi za Serikali ya Watu wa Marekani zilisaidia katika kuunga mkono na hatimae kupata mafanikio makubwa.

Akieleza katika mafanikio yaliopatikana kwenye sekta ya elimu, Rais Karume alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni kuimarisha elimu ya Sekondari ambapo tayari mikakati maalum imeshawekwa katika kufanikisha changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kujenga skuli mpya za kisasa Unguja na Pemba.

Rais Karume alisema kuwa katika kuhakikisha kila mwanafunzi anapata kitabu chake cha kujisomea tayari hatua hiyo imefikiwa na kuishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada wake wa vitabu. Aidha, Rais Karume alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar tayari imeshapiga hatua kubwa katika kutekeleza malengo ya Milenia kwa kuweza kuimarisha sekta zake za maendeleo.

ZATI KUJADILI CHANGAMOTO ZA UTALII

ZATI kujadili changamoto za utaliiNa Salum Vuai, Maelezo

JUMUIA ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), asubuhi hii inatarajia kufanya mkutano maalumu utakaojadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Mkutano huo umepangwa kufanyika katika hoteli ya Serena Inn kuanzia saa 3 za asubuhi ambapo wajumbe wa bodi ya jumuia hiyo watakutana na watendaji wakuu wa taasisi nyengine za serikali kutafuta njia za kutatua matatizo yanayojitokeza katika biashara ya utalii hapa nchini.

Mwenyekiti wa jumuia hiyo Simai Mohammed Said alilieleza gazeti hili kuwa, kumekuwa na changamoto nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi katika mikakati ya kuimarisha utalii wa Zanzibar, ambazo nyengine zimekuwa zikielezwa na wadau wa sekta hiyo kupitia vyanzo tafauti zikiwemo warsha zinazohusu biashara ya utalii.

Alizitaja kuwa ni pamoja na suala zima la usalama wa wageni katika maeneo mbalimbali zikiwemo fukwe sambamba na kero ya mapapasi ambao kwa njia moja au nyengine wanachangia kuleta taswira mbaya kwa watalii wanaotembelea nchini.

Aidha alisema jambo jengine ni kufanya upembuzi wa malalamiko ya kuwepo utaratibu usioridhisha wa mikataba kati ya waajiri na wafanyakazi wa mahoteli, mikahawa ya kitalii na mengineyo yanayohusiana na sekta hiyo.

Said alisema mkutano huo utahudhuriwa na watendaji wa sekta mbalimbali ikiwa pamoja na Mkurugenzi wa Masoko katika Kamisheni ya Utalii, Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Rais wa Jumuia ya Wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima Zanzibar na wengineo.

Alisema mwisho wa kikao hicho kinachokadiriwa kuchukua muda wa saa nne, kutatolewa mapendekezo ya njia za kuimarisha utalii kwa kuzifanyia kazi kero mbalimbali zitakazoibuliwa.

ZATI imekuwa na utaratibu huo kila mwaka, ambapo imekuwa ikikutana na wadau wa taasisi za umma zinazohusika kwa njia moja au nyengine katika kuimarisha sekta ya utalii nchini.

PEMBA ICHAGUENI CCM - MAMA SHEIN

Pemba kichagueni CCM - Mama Shein


Zuhra Msabah, Pemba


MKE wa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanamwema Shein amewataka wananchi wa mkoa wa Kaskazini Pemba kukichagua chama cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi mkuu ujao utakapowadia.

Mama Shein alisema hayo katika ukumbi wa Benjamini Mkapa Wete Pemba alipokuwa akizungumza na wajumbe UWT na akina mama wa mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema chama hicho kina kila sababu ya kuchaguliwa na kushinda kwenye uchaguzi mkuu ujao, kwani kina ilani ambayo ndiyo dira ya maendeeleo kwa wananchi.

Sambamba na hilo mama Shein, alisema ilani ya chama hicho imekuwa ikitekelezwa kivitendo ambapo kila mwananchi amekuwa akishuhudia maendeleo yaliyofikiwa hapa nchini.

Mama Shein alisema wanawake wakishikana kwa umoja wao wanaweza kukiwezesha chama hicho kushinda kwa ushindi wa kishindo.

"Akina mama tunaweza lakini muhimu tushikamane na tuwe wamoja ili tuweze kupata ushindi wa kishindo",alisema mama Shein.

Alisema chama cha Mapinduzi kimekuwa kikisitiza umuhimu wa kuwapatia maendeleo wananchi wake sambamba na kuendeleza amani na utulivu ambao unawezesha wananchi hao kufanya shughuli zao bila ya bughdha.

Naye Katibu wa UWT mkoa wa Kaskazini, Mafunda Khamis Ali alisema akinamama wapatao 70 katika mkoa huo walitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbali mbali.

Alisema kati ya hao 26 wamefanikiwa kupitishwa kuwania nafasi hizo huku wakisubiri kuingia kwenye uchaguzi mkuu.

Mafunda alisema katika mkoa huo, hali ya kisiasa imekuwa tulivu tofauti na miaka iliyopita.

Katika ziara hiyo Mama Shein alifuatana na Mke wa Waziri Kiongozi Asha Shamsi, Waziri wa Kazi, Vijana na Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Asha Abdulla Juma na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii ya Jamhuri ya Muungano Dk. Aisha Kigoda.

Monday, 23 August 2010

MWENYEKITI wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ali Mzee Ali akitowa maelezo kwa Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Alfonso Lenhardt alipotembelea Baraza la Wawakilishi na kupata maelezo ya mafanikio ya kura ya maoni iliofanyika hivi karibuni. lZanzibar 

MAREKANI YAPONGEZA ZANZIBAR KWA KUPEVUKA KIDEMOKRASIA

Marekani yaipongeza Zanzibar kwa kupevuka kidemokrasia

 Ali Mzee avipongeza vyombo vya habari kufanikisha kura ya maoni


Na Mwandishi wetu


SERIKALI ya Marekani imeipongeza Zanzibar kwa kuonesha kukomaa kidemokrasia, na kuamua kujenga Zanzibar mpya kufuatia kupiga kura ya maoni ya muundo mpya wa kisiasa kwa amani na utulivu Julai 31 mwaka huu.

Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt, alipozungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya watu sita ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Ali Mzee Ali, Afisi za Baraza hilo Mbweni Zanzibar jana.

"Nilipofika Zanzibar kwa mara ya kwanza, nilieleza hamu na matumaini yangu kwamba wananchi wa visiwa hivi vizuri wataungana na kujenga Zanzibar mpya iliyojaa amani.......nashukuru ndoto yangu hiyo imetimia muda mfupi sana" alisema Balozi huyo.

Balozi Lenhardt alieleza hatua hiyo ya viongozi na wananchi wa Zanzibar, imejenga historia ulimwenguni kote na kuichora Zanzibar katika ramani ya nchi zinazofuata demokrasia ya kweli.

Akizungumzia jengo jipya la Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Balozi Lenhardt alisema ni kiashirio kikubwa kwamba Wazanzibari wameamua kubadilika na kujenga Zanzibar mpya yenye mambo mapya ya kimaendeleo.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, Balozi huyo alisema una kila ishara ya kuwa wa mafanikio, huru na uliojaa amani, kama ilivyokwishaonekana kupevuka kwa wananchi wa Zanzibar, walipopiga kura ya maoni mwezi uliopita.

Alisema ni jambo la kufurahisha kuona Wazanzibari ndiyo wenye kufanya maamuzi kuhusiana na mustakbala wa nchi yao, pamoja na kushirikiana kuendesha nchi kwa pamoja baada ya uchaguzi mkuu na kuzifanya sauti za wananchi wote kusikilizwa, jambo ambalo Marekani na dunia nzima inalipongeza.

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya watu sita ya Baraza la Wawakilishi iliyoundwa kusimamia kura ya maoni, Ali Mzee Ali, aliishukuru Serikali ya Marekani kwa kuunga mkono harakati za maendeleo na kujenga amani na utulivu Zanzibar, ikiwemo kuendeshwa kura ya maoni Julai 31 mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alimuomba Balozi huyo kuwasilisha salamu za shukurani kutoka kwa wananchi wa Zanzibar kwa Rais Barack Obama wa Marekani, kutokana na hatua za nchi hiyo kuiunga mkono Zanzibar katika kujenga taifa lenye amani na utulivu wa kudumu.

Mzee ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, aliwapongeza waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali nchini, kwa kutoa mchango mkubwa kwa Kamati hiyo, ambao ulisaidia kutoa taaluma kwa wananchi wa Unguja na Pemba kuhusiana na kura ya maoni.

Alisema bila ushiriki kikamilifu wa wanahabari, basi kazi ya kamati yake kuelimisha wananchi kuhusiana na kura ya maoni ingekuwa ngumu, ikizingatiwa muda uliokuwepo ulikuwa mfupi.

Aliwataka waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi zao kwa uzalendo na kuelimisha wananchi kuhusiana na mambo yatayojenga mustakbala mzuri kwa nchi yao.

Akizungumzia umuhimu wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru, Balozi Lenhardt, alisema vina mchango mkubwa ndiyo maana vikafanikisha kura ya maoni kuhusiana na muundo mpya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuvitaka mara zote kuwa tayari kuonesha changamoto zinazoikabili jamii ili ziweze kurekebishwa.

MAALIM SEIF AHIMIZA UCHAGUZI WA UWAZI

Maalim Seif ahimiza uchaguzi wa uwazi

 Asema hatakuwa na sababu ya kukataa matoe

Na Mwanajuma Abdi


MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia chama cha CUF, Seif Sharif Hamad amekuwa wa kwanza kurejesha fomu ya kuwania nafasi hiyo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) hapo jana na kuihimiza tume hiyo kusimamia uchaguzi mkuu ujao mwizi Oktoba kwa uwazi.

Fomu hizo alizikabidhi jana kwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Salum Kassim Ali, majira ya saa 9 alasiri baada ya kukamilisha taratibu mbali mbali ikiwemo la kupata wadhamini katika mikoa mitano ya Zanzibar.

Mkurugenzi huyo alizikagua fomu hizo na baadae kumkabidhi risiti ya malipo ya shilingi 2,000,000 ikiwa ni dhamana ya mgombea anayewania nafasi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabishi fomu hizo, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema katika kinyang'anyiro cha uchaguzi lazima kuna mshindi na aliyeshindwa hivyo akishindwa atakubali matokeo kama ZEC itaendesha uchaguzi wa uhuru na haki.

Alishauri ZEC iendelee kuwa wazi kama ilivyofanya zoezi la kura ya maoni pamoja na kuwashirikisha wagombea watakaoshiriki katika nafasi mbali mbali ili kuondosha matatizo yasitokee.

Aliishauri Tume hiyo kutangaza matokeo mapema, hasa ya Urais mara baada ya uchaguzi na yasikae kwa siku mbili hadi tatu bila ya kutangazwa.

Alisema kufanya hivyo ni kuwapunguzia imani wananchi na wagombea kwa kuwatoa wasiwasi na shaka ya matokeo yanayotolewa.

Wagombea wengine waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo ni Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM, Juma Ali Khatib TADEA, Haji Ambar Khamis NCCR Mageuzi, Haji Mussa Kitole Sauti ya Umma na Jahazi Asilia

DK. SHEIN AHUTUBIA WAGOMBEA PEMBA NA KUSEMA .KUNA KILA SABABU YA CCM ITASHINDA.

DK. SHENI AHUTUBIA WAGOMBEA PEMBA NA KUSEMA


Kuna kila sababu CCM itashinda

Na Bakar Mussa, Pemba

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohammed Sheni amesema chama hicho kimejipanga vizuri na kuna kila sababu ya kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Dk. Sheni amesema CCM kina wanachama wengi pamoja na wagombea makini wenye uwezo mkubwa wa kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho na kukipatia ushindi mkubwa.

Dk, Shein, alieleza hayo huko katika ukumbi wa hoteli ya Mbuyu Mkavu Vitongoji nje, Mkoa wa Kusini Unguja wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM wa Mikoa miwili ya Pemba, ambao walijitokeza kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi katika Majimbo yao.

“CCM, tumejipanga kwa hilo kwani Wanachma tunao na wagombea tunao wazuri wa kuinadi Ilani yetu ya Uchaguzi ‘ alisema Dk, Shein.

Dk. Sheni hata hivyo, amewataka wanachama wa CCM kuelewa kuwa kazi kubwa inayowakabili kwa sasa ni kujenga mazingira bora yatakayopelekea azma hiyo ya ushindi inafikiwa.

Alisema kuwa ushindi kwa CCM, upo wazi kwani ni chama chenye Sera sahihi na Ilani madhubuti jambo ambalo wananchi waliowengi ,wanaimani nacho hivyo wagombea wazidishe hamu ya kushirikiana na WanaCCM wengine kwa kuendeleza Ushindi utakao kifanya kiendelee kuongoza nchi.

Aliwataka wanachama hao ambao walijitokeza katika kinyang’anyiro hicho kushirikiana na na kusaidiana pamoja kwa nia moja tu ya Ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi, kwani waliomba watu wengi lakini kwa utaratibu wa kidemokrasia ndani ya CCM anaetakiwa kusimama ni mmoja.

“CCM, inajivunia kwa kufanya mambo yake kwa mpango bila ya kuiga kutoka kwa Chama chengine kwa vile ndie mwalimu wa Siasa wa mageuzi ya vyama vingi Tanzania", alieleza.

Alisema kutokana na ubora huo CCM, itafanya kampeni zake kwa ustaarabu kwani wanayo kila sababu ya kufanya hivyo, kwani watakayo yaeleza ni yale ambayo yalinadiwa na na CCM, katika Uchaguzi mkuu uliopita ambayo yametekelezwa kwa asilimia kubwa.

“Tuliyo yaahidi kwa wananchi wakati tukiinadi ilani yetu ya Uchaguzi wa mwaka 2005-2010, tumeyatekeleza , sasa kwanini wananchi wasiendelee kutupa ridhaa wakatuchagua tena kuongoza nchi.”alisema Mgombea huyo.

Alifahamisha kuwa ni wakati wakufanya kamapeni za kistaarabu uliomkubwa ,kwani mazingira ya kufanya hivyo yapo na yameletwa na wanccm wenyewe kwa kuleta umoja , amani na mshikamano kwa wananchi.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar kuhakikisha wanailinda Katiba ya nchi na ile ya CCM, kwani ndio inayohubiri amani, umoja na mshikamano jambo ambalo Zanzibar inajivunia kwa kuwa na maendeleo makubwa katika sekta mbali mbali.

Dk. Shein amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Aman Abeid Karume, na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Sief Sharif Hamad, kwa kuamua kuwaunganisha pamoja wazanzibar kua kitu kimoja, na kuleta mazingira mazuri ya kisiasa kwa Zanzibar.

Alisema anaimani kwa ubora wa Ilani na Sera madhubuti za CCM wananchi waliowengi watamchagua kua rais wa Zanzibar na ataangonza kwa mjibu wa katiba ya nchi na kamwe hatomdhulumu mtu wa aina yoyote.

Aliwataka wagombea watakapokua katika kampeni zao kuyanadi na kuyaeleza yale aliomo katika Ilani ya ya Uchaguzi kwanza na ndio waeleze memgine waliojipangaia ya kuwaletea wananchi maendeleo katika Mjimbo yao na kutosahau kuwaombea kura wenzao.

Mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya CCM ,aliongeza kwa kusema kua katika uongozi wake pindi akipewa ridhaa atahakikisha mambo manne anayasimamia kwa nguvu zake zote ikiwa ni pamoja na kuwataka wananchi kuyalinda na kuyadumisha Mapindzui ya Zanzibar ya mwaka 1964,kwani ndio dira ya wanzanibari yalioleta uswa na kuwepo kwa Serikali hii.

Alilitaja jambo la pili kua kuulinda na kuuendeleza na kuuheshimu muungango wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maslahi ya nchi mbili hizo.

Aliendelea kusema kuwa atahakikisha umoja , amani na utulivu wa watanzania kwa kuishi vizuri bila ya matatizo kwa kuelewa kua wote ni wamoja.

Dk Shein alifafanua kua jambo la nne ni kusimamia na kuelta maendeleo kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.

Hivyo malengo ya CCM kikatiba ni kuendelea kushika hatamu kwa ngazi zote kwa Tanzania nzima pia na hilo litapatikana iwapo wagombea wataitaangaza vyema Ilani ya uchaguzi ya CCM na huivyo Tanzania yenye neeema itapatikana.

MANISPA KUBURUZWA MAHAKAMANI

Manispaa kuburuzwa mahakamani

Mohamed Gharib, ZJMMC

WAFANYABIASHARA ndogo ndogo wa soko la Mwanakwerekwe wamekusudia kuliburuza mahakamani Baraza la Manispaa la Zanzibar kutokana na hatua ya kuzivunja meza zao za biashara.

Katibu wa kamati ya wafanyabiashara hao Mkubwa Khamis Hamad alisema washamefungua kesi katika kituo cha Polisi Mwanakwerekwe, na wanachosubiri kuelezwa hatua nyengine za jeshi hilo.

Mkubwa alisema malalamiko waliyoyawasilisha kwenye jalada hilo walilolifungua polisi ni kuvunjiwa meza mpya 13 ambapo kila moja meza hiyo ina gharama ya shilingi 130,000.

Alisema mbali ya meza hizo pia baraza hilo limevunja meza ndogo ndogo zipatazo 70 ambapo wamechukua hatua hiyo kinyume na utaratibu.

Katibu huyo alifahamisha kuwa pia eneo hilo ambalo meza zao zimevunjwa waliliwekea kifusi gari nane huku kila gari moja ikigharimu shilingi 130,00.

"Waliingia kuja kuvunja kupitia lango kubwa la soko na baada ya kufika hapa walimuamuru mlinzi wetu aondoke na kuzivunja meza zetu",alisema katibu hiyo.

Mkubwa alisema kuvunjiwa meza zao hizo ni kinyume na misingi ya sheria kwani kwenye eneo hilo wao wamepewa na kihalali na Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi.
Maelfu wajitokeza kumdhamini Dk.Shein


 Ambar akamilisha mikoa minne


 Juma Khatib mambo safi

Na Mwantanga Ame, ZJMMC


WANACHAMA wa CCM wamejitokeza kwa wingi kumdhamini mgombea wa Chama Cha Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, ili aweze kuwania kiti cha Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Katibu wa Idara ya Uenezi, Itikadi na siasa wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliyaeleza hayo jana wakati akizungumza na Zanzibar Leo Mjini Zanzibar kuhusu zoezi hilo linavyokwenda kwa pande wa mgombea huyo wa Urais.

Vuai alisema zoezi hilo linakwenda kwa kasi na kumejitokeza wanachama wengi wa kumdhamini Dk.Shein.

Dk. Shein alichukua fomu hiyo wiki iliyopita, huko Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo, ambapo baadhi ya wanachama wa CCM wa Mkoa wa Mjini walijitokeza kutaka kumdhamini.

Licha ya Mkoa huo, pia wanachama wengine ambao walijitokeza kutaka kumdhamini ni kutoka Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo zoezi hilo limepata mafanikio makubwa na linaendelea kisiwani Pemba.

Vuai alisema zoezi hilo lilitarajiwa kukamilka jana jioni katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo hadi mchana wa jana wanachama wa chama hicho kisiwani Pemba walijitokeza kwa wingi kumdhamini mgombea huyo.

Hata hivyo, Vuai hakutaja idadi halisi ya wanachama waliojitokeza kutaka kumdhamini mgombea huyo ingawa alisema idadi yao ilipindukia kiwango kilichowekwa kisheria na Tume ya Uchaguzi cha watu watu 200 kwa kila Mkoa ambapo kila Mkoa waliowasajili walipindukia idadi hiyo.

"Watu wapo wengi sana wamejitokeza kumdhamini Dk. Shein, kwani kila Mkoa amepata watu kupindukia idadi ya Tume hatuna wasi wasi wa kupata wadhamini tumepata wa kutosha" alisema.

Akizungumzia juu ya tarehe ya kuanza kufanya kampeni zake kupitia chama cha Mapinduzi Zanzibar, alisema wanakusudia baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani visiwani Zanzibar.

Katibu huyo alisema kuwa licha ya Tume ya Uchaguzi kutangaza Agosti 10,2010 Chama cha Mapinduzi kinakusudia kuanza kufanya kampeni hizo mara tu baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

Alisema wameamua kufanya hivyo kwa lengo la kupisha mfungo huo umalizike ili kuwapa waumini wa dini ya kiislamu kuweza kukamilisha funga zao vizuri zaidi lakini hakusema tarehe kamili ya kuanza zoezi hilo.

Nae Mgombea Urais kwa Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis, alisema amekamilisha Mikoa minne kupata wadhamini wake na hivi sasa yupo katika hatua za mwisho kukamilisha kazi hiyo katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema hadi sasa wadhamini waliojitokeza kumdhamini ni katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na Kusini Pemba ambapo kazi ya mkoa uliobaki inatarajiwa kukamilika kuanzia kesho na kusema anatarajia kurejesha fomu Agosti 29, mwaka huu saa 8.00 za mchana.

Katibu wa Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib, alisema amekamilisha kupata wadhamini katika mikoa yote a Unguja na hivi sasa yumo katika hatua za mwisho kudhaminiwa na wananchi wa kisiwa cha Pemba ambapo Mkoa mmoja tayari kazi hiyo imekamilika.

Kesho ameitaja kuwa siku atakayoweza utoa jibu la lini atarejesha fomu zake.

.

WAWAKILISHI MADIWANI WASUASUA KUREJESHA FOMU ZA UTEUZI

Wawakilishi, madiwani wasuasua kurejesha fomu za uteuziNa Mwanajuma Abdi

JUMLA ya wagombea 53 wa nafasi za Uwakilishi na wagombea 90 wa Udiwani wamejitokeza katika majimbo ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kuchukua fomu za kuwania nafasi hizo kupitia vyama mbali mbali vya siasa.

Idadi hiyo imepatikana hadi jana ambapo gazeti hili lilitembeleza Afisi zaTume ya Uchaguzi ya Wilaya ya Mjini iliyopo Maisara na ya Wilaya ya Magharibi huko Mwanakwerekwe.

Kati ya wagombea hao wa Uwakilishi waliochukua fomu ni 11 ndio waliorejesha fomu huku kati ya maombi 90 ya madiwani kukiwa na idadi ya fomu 19 zilizorejeshwa.

Msimamizi Msaidizi wa Tume ya Uchaguzi Wilaya Mjini, Mohammed Ali Abdallah aliwataja waliorejesha fomu hizo ambao wote ni wagombea kupitia tiketi ya CCM, Nassor Salum Ali (Jazeera) wa jimbo la Rahaleo, Suleiman Othman Nyanga (Jang'ombe), Mahmoud Mohammed Mussa (Kikwajuni), Ali Salum Haji (Kwahani), Salmin Awadh Salmin (Magomeni) na Fatma Said Mbarouk (Amani).

Aidha alisema kwa upande wa Udiwani wagombea waliochukuwa ni 50 kati ya hao wagombea 12 wamerejesha fomu hizo ni Ameir Makungu Makame (CCM), anayegombea Wadi ya Rahaleo, Bikwao Hamad Khamis (CHADEMA) Wadi ya Jang'ombe, Abdallah Ali Chum (CCM) Wadi ya Amani na Saleh Fasih Mzee (CCM) Wadi ya Jang'ombe.

Alieleza wagombea wengine wa Udiwani ni Khamis Mabrouk Khamis (CCM), Wadi ya Mlandege, Khatib Abdurhman Khatib (CCM) Wadi ya Miembeni, Mahabubu Juma Issa (CCM) Wadi ya Kikwajuni, Zubeir Juma Salum (CCM) Wadi ya Meya, Asha Ali Abeid (CCM) Wadi ya Nyerere, Juma Ngwali Juma (CCM) Chumbuni, Machano Mwadini Omar (CCM) Kwahani na Awena Abdallah Mkubwa (CCM) Wadi ya Mikunguni.

Nae Msaidizi Afisa wa Uchaguzi wa Wilaya ya Magharibi, Khamis Mussa Khamis alisema wagombea waliochukuwa fomu za kuwania nafasi za Uwakilishi walikuwa ni 28 kati ya hao watano ndio waliorejesha fomu hadi jana mchana.

Aliwataja wagombe hao ni Thuwaybah Kissasi (CCM) jimbo la Fuoni, Ali Abdalla Ali (CCM) Mfenesini, Asha Mohammed Hilal (CCM) Magogoni, Khamis Jabir Makame (CCM) Mtoni na Mansoor Yussuf Himid wa Kiembesamaki.

Maalim Khamis aliwataja waliochukuwa fomu za Udiwani ni 40 kati ya hao wagombea saba wamesharejesha fomu zao katika Afisi hiyo.

Aliwataja walioresha fomu hizo ni pamoja na Mahammed Haji Kitete (CCM) Wadi ya Mwanakwerekwe, Nyange Haji Haji (CCM) Wadi ya Mbuzini, Amina Ali Mohammed wa CCM (Bububu), Msim Seif Abdulla Wadi ya Mfenesini (CCM), Bernard Lutoba Kanungu wa CCM Wadi ya Tomondo, Hamza Khamis Juma (CCM) Wadi ya Mwanyanya na Mwatima Talib Said (CCM) Wadi ya Magogoni.

Wakati huo huo, wagombea wa Udiwani kupitia CCM, Msimu Seif Abdallah (Wadi ya Mfenesini), Bernard Lutoba (Tomondo) na Nyange Haji (Mbuzini) walirejesha fomu jana, katika Wilaya ya Magharibi, ambapo Maalim Khamis alizipokea na kuwaambia waende katika Afisi hiyo, Septemba pili mwaka huu saa 10:00 jioni ili kuangalia kama hawajawekewa pingamizi au kama wanataka kuweka pingamizi kwa wagombea wengine.

Katika Wilaya ya Kati Unguja, Afisa wa Uchaguzi, Maalim Mussa Ali Juma alifahamisha kuwa, katika Wilaya hiyo wagombea tisa wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania Uwakilishi kutoka vyama mbali mbali vikiwemo cha CCM, CUF, Jahazi Asilia, TLP, CHADEMA, ambapo hadi mchana wa jana hakuna aliyerejesha fomu.

Aidha kwa upande wa nafasi za Udiwani waliochukuwa fomu za kuwania wadi mbali mbali walikuwa 25, ambapo pia hakuna aliyerejesha fomu hadi jana mchana.

Saturday, 21 August 2010

NEC YAZIBWAGA PINGAMIZI

NEC yazibwaga pingamizi


Na Mwajuma Juma

TUME ya Uchaguzi ya Taifa ya Tanzania (NEC), Wilaya ya Mjini imezitupilia mbali pingamizi dhidi ya wagombea wa tatu wa nafasi za Ubunge.

Tume hiyo ilipokea pingamizi dhidi ya wagombea wa Ubunge wa majimbo Kikwajuni na Mpendae baada ya wagombe hao kwenda kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na tume hiyo.

Akizungumza na gazeti hili Msimamizi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Masha Said, alisema Yussuf Masauni anayewania Ubunge jimbo la Kikwajuni aliekewa pingamizi na mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CUF Dk. Idarous Habib Mohammed.

Katika madai yake mgombe huyo wa CUF liwasilisha tuhuma za Masauni kughushi umri kwenye fomu yake ambapo alidai amezaliwa Oktoba 3, mwaka 1979 wakati fomu ya kuwania Ubunge alijaza kazaliwa Oktoba 3, mwaka 1973.

Kwa upande wa mgombea wa jimbo la Mpendae mgombea Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM Salim Hassan Turkey aliwekewa pingamizi na wagombea wawili.

Turkey aliwekewa pingamizi Hussein Hassan Sultani ‘Malayka’ mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Jahazi Asilia na Mohammed Hemed wa CHADEMA.

Katika dai lake dai lake la msingi Hussein Hassan Sultani ‘Malayka’ alisema Turkey ametoa rushwa huku mgombea wa CHADEMA Mohammed Hemed akidai Tukery amekiuka sheria ya gharama za uchaguzi.

“Malayka katika pingamizi yake hiyo alidai kuwa Turkey alitoa rushwa ya shilingi 200 kwa kila aliyekuwepo katika Tawi la CCM la Mpendae pamoja na mchele”, alisema msimamizi huyo.

Hata hivyo Msimamizi huyo wa NEC, alisema kwamba katika pingamizi hizo zote tatu hakuna hata mlalanmikaji alietoa kielelezo cha kuthibitika makosa na badala yake Tume imeamuwa kuwathitisha wagombea wote wawili na kwamba ni halali.

“Hakuna vielelezo vyovyote vya kuthibitisha hilo, ambapo kwa upande wa mlalamikaji Malayka alileta mashahidi watatu ambao wote hawajathibitisha kutolewa kwa rushwa bali kila mmoja alisema kwamba Turkey alitoa sadaka”, alisisitiza Masha na kuongeza kwamba kwa msingi huo nimewateua rasmi kuwa wagombea halali kupitia chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika hatua nyengine mgombea wa CUF Dk. Idarous yeye ameamua kukata rufaa Tume ya Uchaguzi ya Taifa baada ya kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa na tume ya Wilaya ya mjini.

Katika rufaa yake hiyo ambayo aliiwasilisha majira ya saa 7:00 mchana mlalamikaji huyo alidai kuwa katika usikilizwaji wa pingamizi yake hakutendewa haki ikiwemo kutoitwa yeye wala mlalamikiwa katika usikilizwaji huo, dai ambalo msimamizi wa Tume hiyo alilipinga.

Msimamizi huyo alieleza kuwa mlalamikaji huyo wa CUF katika rufaa yake alitoa taarifa za uongo kutokana na kuwa wakati wa kusikiliza pingamizi hizo waliwaita kwa pamoja na kila mmoja alitoa maelezo yake.

“Nashangaa baada ya kupata rufaa hii kuona mlalamikaji anasema hakutendewa haki, wakati niliwaita wote wawili na kila mmoja alitoa maelezo yake”, alisema.

Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya wilaya ya Mjini imetoa fomu kwa wagombe 65 wanaowania kuteuliwa nafasi ya Ubunge wa ambapo wagombea 55 ndio waliorejesha fomu hizo.

TUVUNJE MAKUNDI NA KUBAKIA NA KUNDI MOJA TU LA CCM - DK. SHEIN

Tuvunje makundi na kubakia na kundi moja tu la CCM - Dk. SheinMwandishi Maalum

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, amewataka wanaCCM kutambua kuwa kazi kubwa iliyo mbele yao hivi sasa ni kuhakikisha kuwa chama hicho kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.

Dk. Shein ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa mbalimbali wa CCM katika wilaya za Kusini na Kati katika mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema sababu za kushinda zinatokana na uamuzi wa chama kwa mujibu wa Katiba yake na jinsi CCM ilivyojipanga.

Dk. Shein alisema kauli ya chama hicho ya ushindi ni lazima inayotokana na agizo la chama katika Ibara ya 5 kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya chama, ambacho kinasema inapofika wakati wa uchaguzi jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha kinashinda uchaguzi na kushika dola ni dalili nzuri za ushindi wa chama hicho.

Akifafanua zaidi alisema ushindi huo unatokana na chama hicho kujivunia mtaji mkubwa wa watu wanaokiunga mkono chama hicho, sera nzuri na utekelezaji mzuri wa Ilani yake.

Aliwapongeza wanaCCM kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuchagua wagombea ndani ya chama hicho ambao ni makini katika kuleta maendeleo.

Alibainisha idadi kubwa ya wanaCCM waliojitokeza mwaka huu katika kuwania kuteuliwa nafasi mbali mbali za ubunge, uwakilishi na udiwani inadhihirisha kupanuka kwa demokrasia ndani ya chama.

Aliwataka wanaCCM kwa mara nyingine kuvunja makundi na kujenga kundi moja kwa lengo la kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi.

“Wakati wa kuunga mkono mtu mmoja umekwisha, tuna kundi moja la CCM…hapa lengo ni kupata ushindi na ndio jambo la msingi. Tumepewa dhamana na chama chetu, hatuwezi kwenda kinyume na taratibu za chama,” alisema Dk. Shein.
MGOMBEA Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao kupitia tiketi ya CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizugumza na wanachama wa Chama hicho baada ya kurejesha fomu ya kugombea Urais Tume ya Uchaguzi (NEC) katika mkutano uliofanyika Afisi Kuu ya CCM Lumumba Mjini Dar-es-Salaam.

WAKULIMA WA KARAFUU WAIOMBA ZSTC KUWAPATIA MAJAVI.

Wakulima karafuu waiomba ZSTC kuwapatia majamviNa Madina Mohamed, ZJMMC, Pemba

WAKULIMA wa zao la karafuu kisiwani Pemba, wameliomba Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), kuangalia uwezekano wa kurejesha mikopo ya majanvi ya kuanikia karafuu, ili kuepusha kuharibika kwa zao hilo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tafauti, wakulima hao walisema wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa halisi vya kuanikia karafuu, hali inayowalazimisha kuzianika maeneo yasiyo salama hali inayoshusha kiwango na kusababisha hasara.

Walisema uvunaji wa zao hilo unaendelea vizuri na tayari wanazo za kutosha lakini tatizo hilo ndio kikwazo kwao.

Mkulima Suleiman Abdallah Khalfan mkaazi wa Chumbageni Mkoani, alieleza kuwa zamani katika msimu wa karafuu ZSTC ilikuwa ikiingiza vifaa kama majamvi, magunia na taa kwa kuwauzia au kuwakopesha wamiliki wa mashamba ya karafuu ili kuliokoa zao hilo.

Alifahamisha kuwa tangu kuachwa kwa utaratibu huo, baadhi ya wakulima wanapata usumbufu hasa wakati wa kuanika karafuu zao.

Naye Mohammed Shadhil mkaazi wa Chumbageni Wilaya ya Mkoani, alisema kutokana na kukosa vifaa hivyo, hulazimika kuanika karafuu zao juu ya mapaa ya nyumba zilizoezekwa mabati, mabusati au pembezoni mwa barabara.

"Zamani ZSTC ilikuwa ikitupatia majamvi na magunia ya kuhifadhia japo kwa mkopo lakini sasa hakuna, hivyo tunapata shida sana kuanika", alisema Shadhil.

Asha Kombo Khamis aliyeko katika kambi ya uchumaji wa karafuu kijijini Tumbi alisema, siku hizi wanatumia mikeka na mabusati ambayo hata hivyo hayatoshi kutokana na mrundikano mkubwa wa karafuu ambazo hazina pahala pa kuanikiwa.

"Ukitaka majamvi ununue kwa mtu binafsi na bei ni ghali kwani jamvi moja huuzwa kati ya shilingi 5,000 na 6,000 na hakuna mengi", alifafanua Asha.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba Wizara ya Utalii, Biashara na Uwekezaji kupitia shirika lake ZSTC, kurudisha tena uagiziaji wa vifaa hivyo ili kulinusuru zao hilo ambalo ni muhimu kwao na kwa uchumi wa taifa.

Juhudi za kumapata Naibu Meneja Mkuu wa ZSTC Pemba ili azungumzie suala hilo, hazikufanikiwa na zinaendelea, ingawa taarifa za karibuni zilieleza kuwa, ZSTC iliondoa utaratibu huo kuepuka hasara kama ilivyotokea miaka ya nyuma ambapo wamiliki walikopeshwa na kushindwa kulipa.

MASHINDANO KUHIFADHISHA KURAN KUFIKIA KILELE LEO.

Mashindano kuhifadhi Kuran kufikia kilele leoNa Aboud Mahmoud

KAIMU Kadhi Mkuu wa Zanzibar,Sheikh Khamis Haji anatarajiwa kuwa mgeni rasmin katika mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi kuran yanayotarajiwa kufanyika katika Msikiti wa Afraa Bint Issa Kidongo Chekundu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Amir wa maswala ya uenezi, Maalim Mustafa Basha,zinasema kuwa Kaimu Kadhi huyo anatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo ambayo yatakuwa ni ya siku ya mwisho na kushindaniwa juzuu 30 tu.

Maalim Mustafa alisema kuwa mashindano hayo
Kwa wanaume na kwa upande wa wanafunzi wa kike, wanatarajia kufunga mashindano hayo leo katika ukumbi wa Salama Bwawani.

Aidha, alizitaja nchi zitakazoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na wenyeji Zanzibar,Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Msumbiji na Visiwa vya Comoro.

Alieleza kuwa mashindano hayo yataendeshwa kwa njia ya kuhifadhi usomaji wa kuran pamoja na njia ya Tashjii Tahkik.

Mashindano ya kuhifadhi Kuran yaliendelea juzi katika msikiti Sahaba Mtoni, Kidato na wanawake yalifanyika katika ukumbi wa Haile Selassie ambapo mashindano hayo yalikwenda kwa njia ya Tashjii tahkik.

Katika mashindano wanafunzi kutoka visiwani Zanzibar walikuwa wakiendelea kuwa mbele katika mashindano hayo .

Kwa upande wa wanaume mashindano hayo yalikua ni kuanzia juzuu 5,10,15,20na 25 ambapo mshindi wa juzuu 30 alikuwa ni Ali Khamis aliepata alama 100 mshindi wa pili Ali Salum aliepata alama 99.95 na Ali Ahmad alipata alama 69.65.

Mshindi wa kwanza juzuu 25 alikuwa ni Nabil Masoud aliepata alama 93.00 wakati mshindi wa pili alikuwa Abdulawal Khamis aliepata alama 70.65 .

Kwa upande wa juzuu 20 mshindi alikuwa ni Abdulaziz Abdullah alipata alama 100, Jaffar Hajji alipata alama 86.00 na Muhidin Suleiman alipata alama 77.99.

Kwa upande wa wanawake mwanafunzi Husna alipata alama 100 na kuwa mshindi wa juzuu 30 huku mwanafunzi Mariama Mohammed alikuwa mshindi wa juzuu 25 kwa kupata alama 100,Juzuu 15 alikuwa Sabah Abdullah na Zulfa Abdullah alikuwa mshindi wa juzuu tano.

Wananfunzi hao walioshinda walizawadiwa fedha taslim pamoja na vitu mbali mbali ikiwemo tv.