Thursday 3 June 2010

Umeme ufungue milango uwekezaji Pemba

Na Mwandishi Wetu, Pemba
KUPATIKANA kwa umeme wa uhakika kisiwani Pemba, kufungue milango ya uwekezaji kisiwani humo katika sekta mbali mbali ikiwemo viwanda vidogo vidogo na viwanda vya kati, pamoja na kuwataka wazalendo kujitokeza kuwekeza badala ya kuwaachia wageni peke yao.

Hayo yalielezwa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, alipohutubia wananchi katika uzinduzi wa Mradi wa umeme wa uhakika Zanzibar, uwanja wa Gombani kisiwani Pemba jana.

Alieleza kukamilika Mradi huo ni kukamilisha malengo ya Mapinduzi ya Januari 1964 ya Zanzibar na ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2000-2010, zinazoeleza wazi umuhimu wa kuwajengea mazingira mazuri ya maendeleo wananchi wake, ili waweze kufaidika na rasilimali za nchini kwao.
 
Alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika, ambapo imefikia asilimia 82 ya wananchi wake mijini na vijijini wanapata umeme wa uhakika na inatarajia kufikia asilimia 90 mwaka 2012.

Alisema umeme huo utasaidia kurahisisha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto, kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa miundombinu ya sekta hiyo kuimarika.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar kujiamini na kutumia uwezo wao wa hali na mali, kwani wakijiamini watafikia maendeleo makubwa zaidi.
 
Dk. Karume aliishukuru Serikali ya Norway kwa kutoa msaada mkubwa uliofanikisha kukamilika Mradi huo.
 
Norway imetoa dola milioni 71 kufadhili Mradi huo, ambao umebadilisha historia ya kisiwa hicho na Zanzibar kwa jumla kwa upande wa nishati ya umeme, ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilichangia dola milioni 10 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT), ilichangia dola milioni 5.
 
Aidha alizishukuru kampuni za NEXAN za Norway ambayo ndiyo iliyojenga mradi huo, kampuni ya ADC ya Sweden kwa kusaidia vifaa vya mradi huu, pamoja na kutengeneza hitilafu za kukatika umeme kisiwani Unguja, pamoja Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Mkuu wa wilaya ya Tanga.

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, Rais Karume aliwataka wananchi kuungana na kwenda katika uchaguzi kwa kuimarisha umoja, amani na utulivu, ili kujenga Zanzibar yenye amani na maendeleo.

Aliwapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa mchango wao wa dola milioni 10 kufanikisha Mradi huo, pamoja na ndugu zao wa Tanzania Bara kwa kuchangia dola milioni tano na kuutaja Mkoa wa Tanga kutokana na kutoa ushirikiano mkubwa kwa vile umeme huo umeunganisha kutokea huko.

Akitoa salamu za nchi yake, Balozi wa Norway nchini Tanzania, John Lomoy, alisema kuzinduliwa kwa Mradi huo ni kielelezo cha uhusiano mwema na ushirikiano baina ya nchi yake na Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Akizungumza kwa kiswahili alisema maamuzi ya wananchi wa Norway kusaidia Mradi huo ni kuelewa umuhimu wake kwa wananchi wa Zanzibar,
 
Mbali ya hotuba sherehe hizo ambazo wananchi walifurika katika uwanja wa Gombani, zilipambwa kwa utenzi na ngoma za utamaduni.

Akitoa taarifa za kitaalamu kuhusiana na Mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Ujenzi Nishati na Ardhi, Mwalimu Ali Mwalimu, alisema kabla ya umeme huo wa uhakika Pemba ilikuwa ikipata umeme kwa kutumia majenereta.

Alisema Mradi huo utaokoa mamilioni ya fedha za dizeli na matengenezo ya zilizokuwa zikitumika kwa majenereta ya kuzalisha umeme Pemba.

Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansoor Yusuf Himid, alisema kuwezekana kwa Mradi huo kumetokana na juhudi na ujasiri mkubwa wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, aliyelifungia kibwebwe suala la umeme wa Pemba.

"Nataka niwahakikishie wananchi wenzangu kwamba bila ya uongozi imara wa Rais Karume, Mradi huo usingefikia mafanikio yaliyopo sasa" alisisitiza Mansoor.

Aidha alimtaja Meneja Mradi wa umeme Vijijini Zanzibar kutoka Norway, Rodrigue, ambae kwa kushirikiana na Rais ndiyo waliobuni na kusimamia Mradi huo kwa nguvu zao zote hadi kukamilika kwake.

Aidha alisema Mradi huo ni wa kipekee kwani waya wake umetandikwa katika kina kirefu zaidi cha maji cha Kilomita moja ya kina cha maji cha bahari na umbali wa Kilomita 78 kutoka Tanga hadi Pemba na pia Norway haijawahi kufadhili Mradi kama huo barabi Afrika na kuwa wa kipekee kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi kwa Afrika na duniani ni wa kipekee.

Mbali ya umeme pia waya huo uliotandikwa chini ya bahari unatoa huduma ya mawasiliano kupitia 'fibre' maalum, hivyo kuifanya Pemba kupiga hatua kimawasiliano kama dunia za mwanzo' First world'.

Sherehe hizo pia zimehudhuriwa na Mke wa Rais Mama Shadya Karume, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna, Mawaziri viongozi wastaafu, Ujumbe kutoka Norway, Mawaziri na viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.

No comments:

Post a Comment