Monday, 29 March 2010

Jela miaka saba kwa kubaka mototo wa miaka mitatu

Na Omar Hassan, Pemba
MAHAKAMA ya Mkoa wa Chake Chake, Pemba imemuhukumu kutumikia chuo cha mafunzo Muhammed Maganga Sebastian (25) mkaazi wa Vikunguni Chake Pemba kwa muda wa miaka saba baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumsababishia maumivu mtoto wa miaka mitatu.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Haji Omar wa mahakama hiyo, alisema kuwa ametoa hukumu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani, pia iwe fundisho kwa mshtakiwa na watu wengine wenye tabia ya kuwaingilia watoto.

Mapema akisomewa shitaka lake na mwendesha mashtaka wa Serikali Ali Bilali, alidai kuwa Aprili 14 mwaka 2009 saa 1:30 asubuhi huko Magome Vikunguni, Wilaya ya Chake chake, Mkoa wa Kusini Pemba, mshtakiwa Mohammed Maganga alimuingilia kwa nguvu mtoto wa miaka mitatu, jina linahifadhiwa.

Mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu 125 (1) (2) (e) na 126 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Kesi hiyo imeanza kutajwa katika Mahakama ya Chake chake April 23 mwaka jana na kutolewa hukumu hiyo juzi.

Karibu sana visiwani kwetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,DK Amani Abeid Karume,akibadilishana mawazo na Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Heimo Laakkomen, aliyekuja kumuaga huko Ikulu Mjini Zanzibar, baada ya kumaliza muda wake wakazi nchini. (Picha na Ramadhan Othman).

Wazanzibari wachoshwa na mifarakano- Wawakilishi

Mwanajuma Abdi

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wamesema wamechoshwa na mifarakano na migogoro ya kisiasa iliyodumu kwa takrima miaka 15 tokea kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Hayo waliyasema jana, wakati wakichangia mswada wa sheria ya kuweka masharti ya kufanyika kura ya maoni kwa mara ya kwanza uliowasilishwa katika Baraza hilo na Waziri wa Nchi, Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma.

Walieleza kuwa Wazanzibari wamechoshwa kushuhudia migogoro na mifarakano inayoendelea siku hadi siku na iliyosababisha kuyumbisha maendeleo, sambamba na kujengeana chuki na uhasama miongoni mwa wananchi.

Akichangia Mswada huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza hilo, Haji Omar Kheri, ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu alisema anaunga mkono mswada huo ili uwe chachu ya maendeleo na kufuta mifarakano iliyodumu tokea mwaka 1995 katika kisiwa hicho.

“Naunga mkono mswada huu mia kwa mia kwa niaba ya wananchi wa jimbo ninaloliongoza la Tumbatu ili kutumia nafasi ya demokrasia ili kuondosha mifarakano nchini”, alifahamisha Mwakilishi huyo.

Nae Said Ali Mbarouk (Gando), alionesha wasiwasi kwamba muda unaweza kutosha kwa vile Tume ya Uchaguzi imepewa dhamana ya kuendesha kura ya maoni wakati huku pia ikikabiliwa na matayarisho ya uchaguzi mkuu, sambamba inaendelea na zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu awamu ya pili.

Hata hivyo, alimpongeza Rais Mkapa kwa kusaini muafaka wa mwaka 2001 pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume kukutana na Katibu Kuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad mnamo Novemba 5, mwaka jana kwa mustakabali wa maslahi ya wananchi wa visiwa hivi.

UNICEF kuendeleza program kuchapuza huduma Z'bar

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo watoto (UNICEF) limeeleza azma yake ya kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wakiwemo akinamama na watoto.

Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF anayemaliza muda wake Heimo Laakkonen, aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar alipozungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume jana.

Laakkonea alimueleza Rais Karume kuwa UNICEF inajivunia hatua za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar hasa katika uimarishaji wa huduma za jamii zikiwemo za afya.

Alieleza kuwa kutokana na hatua hiyo UNICEF itaendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa kuendeleza programu mbali mbali ambazo zitaongeza kasi za huduma ya afya kwa watoto hapa nchini.

Aidha Laakkonea alieleza kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya UNICEF na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni mkubwa ambao umemsaidia katika utendaji wake wa kazi katika kipindi chote alichofanya kazi nchini Tanzania.

Rais Karume kwa upande wake alitoa shukurani kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar kutokana na ushirikiano na misaada mbali mbali inayotolewa na UNICEF.

Alisema UNICEF imekuwa mstari wa mbele kusaidia uimarishaji wa huduma za kijamii zikiwemo huduma za afya kwa watoto na akina mama.

Wenye ulemavu wapewa mafunzo kujikinga na VVU

Na Jafar Abdalla, Pemba
MIKUSANYIKO isiyokuwa ya lazima na isiyo salama kwa jamii inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maambukizi mapya virusi vinavyosababisha UKIMWI.

Hayo yameelezwa katika mafunzo ya siku tatu kwa watoto wenye ulemavu wa usikivu na mabubu kutoka Wilaya zote za Pemba yaliyofanyika ukumbi wa Afisi ya Waziri Kiongozi kisiwani humo.

Mwezeshaji Muhammed Said alisema, mafunzo hayo yanalenga kuwakinga watoto wenye walemavu na kupata maambukizi mapya ya VVU.

Mohammed alisema kuna uwezekano wa kuwaepusha watoto na makali ya UKIMWI kwa kuwajenga tabia ya kupima afya mara kwa mara pamoja na kuwapatia huduma waazostahiki watoto wanaobainika kuwa wameambukizwa.

Nao washiriki wa mafunzo hayo ambao ni walemavu wa usikivu na mabubu wameziomba taasisi zinazojishughulisha na utoaji elimu kuhusu UKIMWI kuendelea kuwapatia elimu kuhusiana na tatizo hilo ili waongeze kasi ya kujikinga na kuwakinga wengine.

Friday, 26 March 2010

NAIBU Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna akiwasilisha muswaada wa marekebisho ya sheria ya baraza la Michezo la Zanzibar (BTMZ), katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea mjini hapa.(Picha na Abdulla Masangu). 

Biashara ya vinyago kupigwa marufuku Mjimkongwe

Na Mwantanga Ame
BIASHARA ya vinyago katika maeneo ya Mji Mkongwe ipo hatarini kufutwa kuendelea kufanyika katika Mji huo baada ya kuonekana itaharibu soko la utalii wa Zanzibar.

Hilo limebainishwa juzi jioni baada ya Mwakilishi wa Chama cha CUF Zakia Omar, kuliambia baraza hilo kuwa biashara hiyo inafaa kuondolewa katika Mji huo ili kulinda Soko la Utalii la Zanzibar.

Hoja ya Mwakilishi huyo ilikuja wakati akichangia mswada wa kufuta sheria ya Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe, pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mwakilishi huyo akichangia alisema wakati serikali ikiwa tayari imeamua kubadili sheria hiyo ni lazima iliangalie suala la biashara ya uuzaji wa vinyago kwani inaweza ikasababisha soko la watalii wanaokuja Zanzibar ikapungua.

Akifafanua kauli yake hiyo alisema watalii wengi wanaokuja Zanzibar, huwa tayari wanatokea katika vivutio vya utalii vilivyopo Arusha ambapo kwa kiasi kikubwa soko la vinyago huwa vimejaa kwa wingi.

Watendaji watakaochelewasha malipo kwa wadai kukionaNa Mwantanga Ame
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kwamba Watendaji wa Serikali wataochelewesha malipo kwa wadai wa serikali sasa watakiona baada ya sheria mpya iliyopitiwa na Baraza la Wawakilishi kutiwa saini na Rais.

Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais anaeshughulikia Fedha na Uchumi Dk. Mwinyihaji Makame, aliyasema hayo jana wakati akitoa ufafanunuzi wa hoja mbali mbali za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wakijadili mswada huo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Alisema mswada wa sheria ya kuweka Haki na Wajibu wa Serikali katika kesi za madai na utaratibu wa mwenendo wa madai dhidi ya serikali na mambo mengineyo hauna lengo la kumkomoa mtu yeyote ila upo kwa ajili ya kuleta uwajibikaji wa utawala bora.

Waziri huyo alisema serikali imeamua kuandaa sheria hiyo kuhakikisha utawala bora unazingatiwa katika pande zote na haina nia ya kuwakomoa wananchi kwani serikali imekuwa ikipata hasara inayotokana na uzembe wa watendaji kulipa madeni .

Alisema ndani ya mswada huo kuna vipengele kadhaa vitakavyowawajibisha watendaji wa serikali ambao kwa makusudi huchelewesha kufanya malipo ya wadai jambo ambalo sasa litakuwa na kikomo kwa vile sheria hiyo imeelezea kuwawajibisha wazembe hao.

“Kuna maafisa wa serikali wamekuwa wakihangaisha watu katika kulipa madeni yao licha ya kuwa serikali inawaingizia fedha hizo, lakini hawalipi na huendekeza matakwa binafsi jambo linaloibebesha serikali mzigo mkubwa wa madeni”, alisema Waziri huyo.

China yasaidia kuimarisha sekta ya Afya Zanzibar

Na Ali Mohamed, Maelezo
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesifu mashirikiano yaliyopo baina na Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China katika sekta ya Afya na kueleza kuwa mashirikiano hayo yatazidi kuimarika.


WAZIRI wa Afya na Usatawi wa Jamii Sultan Mohamed Mugheir aliyasema hayo Vuga mjini Zanzibar alipofungua rasmi nyumba ya timu ya wataalamu wa Afya kutoka China iliyofanyiwa matengenezo makubwa hivi karibuni.


Aliyaelezea mashirikiano hayo kuwa yamesadia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa huduma za Afya nchini kupitia kwa wataalamu hao wa China.

Alisema kufunguliwa kwa nyumba hiyo na nyumba nyengine iliyopo Kisiwani Pemba ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika kutawawezesha wataalamu hao wa China kufanya kazi vyema za kutoa huduma za Afya nchini.

Nae Mshauri Mkuu wa timu hiyo ya wataalamu wa China hapa Zanzibar Li Yiping alisema China ilianza mashirikino na Zanzibar tangu mwaka 1964 na aliyaelezea mashirikiano hayo kuwa ni yamafanikio makubwa.

Mtambwe wahamasika kujiandikisha

Na Bakari Mussa , Pemba
Wananchi wapatao 5357 wa Jimbo la Mtambwe , wamejiandikisha katika Daftari la kudumu la Wapiga kura linaloendelea Kisiwani Pemba.

Kazi hiyo inakwenda kwa kasi kubwa sambamba na kutawaliwa na amani na utulivu licha ya Wananchi wengi kuhamasika na zoezi hilo la marejeo baada ya awamu ya kwanza kutojitokeza katika vituo hivyo.

Habari zilizopatikana kutoka Afisi ya Tume ya Uchaguzi zinaeleza kuwa katika Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wananchi wamekuwa na hamasa kubwa katika zoezi hilo tafauti na awamu ya kwanza ambapo waliojitokeza walikuwa wachache .

Kwa mujibu wa Afisa Uandkishaji Wilaya ya wete, Bakar Suleiman Ali ni kuwa kati ya wananchi waliojiandikisha katika Jimbo hilo Wanawake walikuwa 2935 na wanaume 2422.( Kwa habari zaidi soma Zanzibar Leo)

Thursday, 25 March 2010

Mama Shadya Karume

Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Shadya Karume (kushoto), akiwa na mwenyeji wake huko ziarani nchini China.(Picha na Othman Maulid). 

Wabunge, Wawakilishi wapashwa Pemba

Na Bakari Mussa, Pemba
WANANCHI kisiwani Pemba, wameonesha kuchoshwa na vitendo wanavyofanyiwa na viongozi wao wa majimbo wakiwemo wa Wabunge na Wawakilishi kwa kudai kuwa viongozi hao hawawajali.

Wananchi hao walieleza kuwa matunda ya dharau wanazofanyiwa na viongozi hao watayona na kufaidika nayo katika uchaguzi ujao kwa kuvuna walichokipanda.

Wapiga kura hao walieleza kuwa ahadi nyingi zilizokuwa zikitolewa katika kampeni na kuamua kuwapa kura zao na kukinyima Chama cha Mapinduzi jambo ambalo limechangia kuwapa unyonge mkubwa kwani viongozi waliowanyima kamwe hawajawaonesha kiburi cha aina yoyote.(Kwa habari zaidi soma Zanzibar Leo).

Vifaa vya MACEMP vyahujumiwa

Na Husna Mohammed
BAADHI ya wanavikundi waliopewa vifaa vya Uvuvi Kupitia Mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Ukanda wa Pwani (MACEMP), wamedaiwa kuvihujumu kwa kuviuza kwa bei chee kwa maslahi binafsi.
 
Hayo aliyasema jana Meneja wa MACEMP Unguja, Sheha Idrissa Hamdani, huko katika Hoteli ya Bwawani Mjini Unguja, katika kikao cha Wenyeviti wa Kamati za Uvuvi Unguja.

Wananchi katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba wamegaiwa vifaa kadhaa vya Uvuvi kupitika Kamati za Uvuvi kwenye Shehia zao ikiwa ni jitihada ya Serikali kupitia mradi huo kuwaondoshea wananchi umasikini wa kipato.
 
Hata hivyo, baadhi ya Kamati hizo wanadaiwa wameviuza na kasha kutafuna fedha hizo na kuvunja matarajio ya mradi huo ya kupambana na umasikini. (Kwa habari zaidi soma Zanzibar Leo)

'Hakuna mwenye hatimiliki ya Jimbo'

Na Mwantanga ame
WAKATI hofu ya kuporwa majimbo ikizidi kutanda kwa Wawakilishi na Wabunge wanaoyashikilia Majimbo hivi sasa, kigogo wa juu wa Chama Cha Mapinduzi amewataka wakongwe wenye majimbo hayo wasiwawekee nongwa kwa vile ni haki yao kuwania nafasi hizo.

Hatua ya kiongozi huyo imekuja baada ya kuanza kubainika kuwapo kwa makundi makubwa ya wanachama wa CCM wanaonyesha nia ya kutaka kunyakua majimbo ya Wajumbe waliopo sasa.

Kuanza kwa kashkash hizo tayari imebainika baadhi ya Wawakilishi na Wabunge wapo katika hali ngumu kiasi ambacho watahitaji kufanya kazi ya ziada ili kuweza kurudi katika majimbo yao.

Akizungumza na Wananchi katika Jimbo la Kitope wakati akimkaribisha Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba na Utawala Bora, Ramadhan Abdalla Shaaban, katika sherehe ya kuzawadia wanafunzi wa Jimbo hilo Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini 'B' ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Ueneezi Vuai Ali Vuai alisema kuwa hakuna haja ya kununa kwa viongozi hao. (Kwa habari zaidi soma Zanzibar Leo).

Friday, 5 March 2010

UMEME KUREJEA ZANZIBAR MACHI 9

Umeme kurudi machi tisa

SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO), limesema matengenezo ya urejeshaji wa huduma ya umeme katika kisiwa cha Unguja yanatarajiwa kukamilika Machi 7, 2010 na wananchi wataipata huduma hiyo kuanzia Machi 9, 2010.
Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar, Hassan Ali Mbarouk, aliyaeleza hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha kupokelea umeme Fumba Wilaya ya Magharibi Unguja.
Kabla ya maelezo ya Kaimu huyo Zanzibar Leo ilishuhudia mafundi wa Kampuni ya Elmeridge Cable Services, EHT Cables ya Afrika Kusini, ambao ni washauri, Kampuni ya Nexans ya Norway ambayo ni wasimamizi wa kazi hizo wakisaidiana na wataalamu wazalendo wakiendelea na kazi katika kituo hicho.
Akitoa maelezo Kaimu huyo alisema kwa asilimia kubwa kazi za urejeshaji wa huduma ya umeme zipo katika hatua ya mwisho baada ya wataalamu hao kuanza kuunga vipande vya waya unaotoka baharini na kuingia katika kituo cha kupokelea umeme cha Fumba.
Alisema kazi hiyo imeanza jana baada ya kujitokeza tatizo katika zoezi la awali la kuunganisha waya huo kulikosababishwa na mafuta kuchafuka.
Alisema kuchafuka kwa mafuta hayo ndiko kulikosababisha kuongezeka kwa muda wa kurejesha huduma hiyo ndani ya Mwezi Februari, ambapo hapo awali ulikadiriwa kungekuwa na uwezekano katika kipindi hicho.
“Tulisema Februari 20 lakini likajitokeza tatizo la kuchelewa kufika kwa vifaa na wakati vifaa viliwasili pia muda wa pili wa ndani ya mwezi Februari haikuwezekana tena kutokana na kuchafuka kwa mafuta wakati tukiendelea na kazi” alisema Kaimu Meneja huyo.
Alisema walilazimika kujipa muda zaidi kutokana na wataalamu hao kutaka kufanya vipimo vipya kwa vile isingewezekana kutumika kwa mafuta hayo na yangeliweza kuleta athari katika kazi hiyo.
“Tumelazimika kulifanya hilo kwa vile waya huu hauhitaji kupata unyevunyevyu hata kidogo kwani ungeweza kuleta athari nyengine”, alisema Kaimu huyo.
Kutokana na hali hiyo Kaimu Meneja huyo alisema tayari hivi sasa sehemu kubwa ya matengenezo hayo yameanza kukamilika ambapo uwekaji waya unaotoka baharini katika viungo hivyo itachukua muda wa siku tatu.
Alisema baada ya kukamilisha kazi hiyo Wataalamu hao Machi 4, 2010, wanatarajiwa kwenda katika kituo cha kupokelea umeme kutoka Ubungo Dar es Salaam, cha Ras -Kiromoni kumalizia hatua za mwisho za kuunga pampu za mafuta.
Meneja huyo alisema kazi hiyo itafanywa kwa muda wa siku moja na Machi 5, 2010, wataalamu hao wataendeleza kazi katika kituo cha Fumba Wilaya ya Magaharibi Unguja kwa kukamilisha kazi ndogo ndogo.
Alisema kazi kamili za matengenezo hayo zinatarajiwa kukamilika Machi 7, 2010, na Machi 8, 2010 wataalamu hao watafanya vipimo vya mafuta yatayoambatana na kazi za majaribio katika kituo cha Ras Kiromoni, Fumba na Mtoni.
Kutokana na ratiba hiyo Kaimu Meneja huyo alisema huduma hiyo kwa upande wa wananchi inatarajiwa kurejea kuanzia asubuhi ya Machi 9, 2010 ambapo wananchi watapaswa kuanza kuchukua tahadhari ili kuepuka kutokea athari wakati huduma hiyo ikirejea.
Hata hivyo Kaimu Meneja huyo aliendelea kuwaomba radhi wananchi kutokana na kuongezeka kwa muda wa kurejeshewa huduma hiyo kulikosababishwa na matatizo ya kitaalamu.
“Tunaendelea tena kuwaomba radhi wananchi, tunajua usumbufu unaowapata lakini isingewezekana kufanya haraka kisha tukaharibikiwa zaidi ya vile jambo ambalo lingesababisha kuchukua muda zaidi tunawaomba radhi tena” alisema Kaimu Meneja huyo.
Viunganishi vilivyowekwa katika waya huo ‘Joint’ vina uzito wa tani 1.7 ikiwa ni pamoja na kubadilishiwa mfumo wa upokeaji umeme katika kituo cha Ras Kiromoni Dar es Salaam pamoja na Fumba Wilaya ya Magharibi Unguja.
Mabadiliko hayo yanakuja baada ya kuharibika kwa kifaa kilichokuwa kikitumika kupokelea umeme katika kituo cha Fumba aina ya ‘Spliter’ kuungua na kusababisha huduma ya umeme kukosekana kuanzia Disemba 10, 2009.