Thursday, 4 August 2011

OFISAUhusiano wa Mfuko wa Pencheni (PPF) Edward Kyungu akitowa maelezo kwa mwananchi katika banda la Wizara ya Fedha, akitaka kujua muhimu wa mfuko huo katika maonesho ya wakulima ya nane nane yanayoendelea mjini Dodoma.(Picha kwa hisani ya Hazina.)    

KARAFUU ZAPANDA BEI TENA

Karafuu zapanda bei tena

Na Mwandishi Wetu
IKIWA siku chache kupita tangu serikali kutangaza bei mpya ya karafuu, bei imepandishwa tena ambapo katika bei hiyo mpya kilo moja ya daraja la kwanza itauzwa kwa bei ya shilingi 15,000 huku pishi ikiuzwa kwa shilingi 22,000.
Bei hiyo mpya, kwa kiasi kikubwa itawanufaisha wakulima na kuacha kuzisafisrisha kwa njia ya magengo kuzipeleka nchi jirani.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bishara ya Taifa Zanzibar (ZSTC), Suleiman Juma Jongo amesema bei mpya ya kilo moja ya daraja la kwanza itapanda kutoka shilingi 10,000 hadi 15, huku pishi moja ikiuzwa shilingi 22,000 badala ya shilingi 15,000 za awali.
Alisema kuwa daraja la pili la karafuu kilo moja itauzwa shilingi 14,500 badala ya 9,500, huku pishi moja ya daraja hilo ikipanda kutoka kutoka shilingi 14,250 hadi 21,500.
Aidha Jongo alisema kilo moja ya karafuu daraja la tatu itauzwa shilingi 14,000 kutoka shilingi 9,000 na pishi moja ya daraja hilo itauzwa shilingi 21,000 kutoka shilingi 13,500.
Katika tangazo hilo jipya, bei ya makonyo itauzwa kilo moja shilingi 1,500 huku kila mwenye shamba la karafuu akitakiwa kumlipa shilingi 2,000 mchumaji kwa kila pishi moja.
Mkurugenzi huyo alisema kupandishwa kwa bei hiyo mpya kunafuatia ahadi iliyowekwa na Rais wa Zanzibar kupandisha bei ya zao hilo ili liweze kuleta tija kwa wakulima.
"Katika kutekeleza ahadi ya Rais, serikali inatangaza mabadiliko ya bei ya karafuu itakayotumika hivi sasa badala ya zile zilizotangazwa hapo awali”, ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema kupandishwa huko sio mwisho wa safari kwani, serikali itapandisha bei ya zao hilo kulingana na kupanda bei katika soko la dunia.
Mkurugenzi huyo aliwaomba wananchi watoe ushirikiano kwa kuhakikisha kuwa karafuu zao zote wanaziuza kupitia shirika la ZSTC na kuacha kabisa kuzisafirisha kwa njia ya magendo ambayo yanaangusha uchumi wa Zanzibar.
Kenya inatajwa kuwa imekuwa ikipokea karafuu za Zanzibar kwa njia ya magendo na kuziuza katika soko la dunia pamoja na kwamba nchi hiyo haizalishi karafuu.
Nchi nyengine maarufu zinazozalisha karafuu ukiachilia Zanzibar ni pamoja na Indonesia, India, Madagascar, Brazil, Comoro na Sri Lanka.

SPIKA KIFICHO BACK BENCHERS NI KIBOKO

Spika Kificho: ‘Back Benchers’ ni kiboko

Asema wanawachangamshwa mawaziri
Dk. Migoro UN imefurahishwa hali ya Zanzibar
Na Himid Choko, BLW
SPIKA Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Pandu Ameir Kificho amesema wajumbe wa Baraza hilo hasa wale wasiokuwa mawaziri (Back Benchers), wamekuwa makini zaidi kufutilia utendaji wa serikali jambo ambalo ni wajibu wao wa kikatiba.
Alisema hatua hiyo imekuwa ikileta changamoto kwa mawaziri na serikali kwa ujumla na kuongeza uwajibikaji, ambapo mawaziri wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wajumbe wanaelewa zaidi kuhusiana na wizara zao kuliko wao wenyewe.
Spika Kificho alisema jana wakati akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dk. Asha Rose Migiro huko ofisini kwake Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Alisema katika mkutano wa bajeti uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita mijadala ya mkutano huo ilikuwa kivutio na kutoa msisimko mkubwa kwa wananchi kutokana na umakini wa wajumbe wa Baraza hilo kuhoji na mawaziri kujibu hoja mbali mbali.
“Ingawa hivi sasa hakuna kambi ya upinzani, lakini Baraza limekuwa likiendelea vizuri na kuwavutia wananchi wengi kwani ‘Benchers’ wamekuwa makini kuhakikisha utendaji unakwenda vizuri chini ya usimamizi wa Baraza la Wawakilishi”, Kificho alimueleza Dk. Migiro.
Naye Naibu Dk. Migiro alisema Umoja wa Mataifa umefurahishwa na hatua iliyofikiwa na Zanzibar kwa kiungia katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mafanikio makubwa yaliyofikiwa na kuwa mfano wa kuigwa duniani.
Alisema Umoja wa Mataifa unaamini kwamba mfumo huo umechangia kwa kiasi kikubwa hali ya amani na utulivu uliopo hapa nchini.
Alisema hali ya mambo Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa kwa Umoja huo katika kutoa fursa nzuri zaidi ya kusaidia nyanja mbali mbali za maendeleo hapa Zanzibar.
“Amani na utulivu ni miongoni mwa mihimili mikuu ya Umoja wa Mataifa , tutapokuwa na amani kwenye nchi ndipo na sisi Umoja wa Mataifa tunapokuwa na fursa nzuri zaidi ya kusaidia kufikia katika maendeleo”, alisisitiza Dk. Migiro ambae alikuwa akitoa salamu za Katibu Mkuu wake , Ban Kimoon.
Alisema umoja huo unafuatilia kwa karibu utendaji wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya muundo wa Umoja wa Kitaifa na umeridhishwa na utendaji wa serikali hiyo.

TENDWA SINA UBAVU KUDHIBITI UTOVU WA NIDHAMU BUNGENI.

Tendwa: Sina ubavu kudhibiti utovu wa nidhamu Bungeni

Joseph Ishengoma na Mpoki Ngoloke, Dar
MSAJILI wa vyama vya siasa nchini John Tendwa amesema ofisi yake haina upavu kisheria kukifuta chama chochote cha siasa kutokana na wabunge wake kukosa heshima bungeni.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana jinini Dar es Salaam Tendwa alisema Bunge ni mhimili wa serikali baada ya Mahakama na Utawala, na kuna kanuni lililojiwekea za kuwaongoza namna ya kufanyakazi zao.
Hivi karibuni kumekuwepo na vitendo vya vurugu bungeni, kuwasha vipaza sauti ovyo na kupiga kelele bila kuruhusiwa na Spika au Mwenyekiti wa Bunge, hali ambayo imesababisha baadhi ya wabunge kupewa adhabu ya kutolewa nje ya ukumbi kwa kukiuka kanuni.
“Wabunge wakiwa ndani ya bunge sio wangu, sina madaraka nao, lakini wakiwa nje ya kuta za bunge ni wangu. Ndani ya Bunge mikono na midomo yangu imefungwa kabisa, lakini kwa mtazamo wa wananchi wanajua kuwa mimi ninamamlaka ya kuwawajibisha kutokana na utovu wa nidhamu wanouonyesha bungeni, lakini sio,” alisema.
“Mimi nimechukia sana kuona vitendo hivi kwasababu natupiwa lawama na watu kuwa wanaofanya vurugu bungeni ni watu wanaotoka katika vyama vyangu. Ninafurahi kwakuwa vyama vyangu nilivyovisajili viko ndani ya bunge, lakini sifurahishwi na utovu wa nidhamu wanaofanya”,alisema Tendwa.
Kwa mujibu wa Msajili wa vyama vya Siasa, baadhi ya wabunge vitendo wanavyofanya ndani ya Bunge kila anayesikia au kushuhdia vitendo hivyo, lazima asikitike.
Taratibu na mamlaka ya kudhibiti utovu huo wa nidhamu uko ndani ya Bunge. Bunge ni taasisi inayojitegemea haiingiliwi na upande wowote (Mahakama na Utawala).
Baadaye mwezi huu, Msajili wa Vyama vya Siasa atakutana na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa katika baraza la vyama na kuwaelezea masikitiko yake.
“Tutakuwa katika baraza la vyama kabla ya bunge lijalo. Tutazungumzia hali hii na kutoa jibu,” amesema.

MAOFISA, WAKULIMA KUSHIRIKI MAONESHO DODOMA

Maofisa, wakulima kushiriki maonesho Dodoma

Na Shauri Makame
WAKULIMA 53 na maofisa 12 kutoka wizara ya Kilimo na Maliasili, wanatarajiwa kuondoka Zanzibar kuelekea mkoani Dodoma kwenye maonesho ya wakulima (nane nane).
Maonesha hayo ambayo yanayofanyika katika ngazi ya kitaifa mkoani humo kwa mwaka wa nne mfululizo yaliyofunguliwa rasmin juzi na rais wa Jamhuri ya Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, yanatarajiwa kumalizika Agosti 8 mwaka huu.
Msafara huo wa Zanzibar utaongozwa na ofisa Ufatiliaji na Tathmini (AM&E) wa Programu za Kuimarisha Huduma za Kilimo na Sekta ya Kuendeleza Mifugo (ASSP na ASDP-L), program ndogo ya Zanzibar, Mtingwa Ramadhan Mapuri.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kabla ya kuondoka mkuu huyo wa msafara aliwataka wakulima kuithamini ziara hiyo ya mafunzo ambayo inalengo la kubadilishana mawazo na uzowefu miongoni mwa wakulima wa Tanzania.
Alisema uzowefu wa ziara kama hizo zilizopita umeonesha kwamba wakulima na wafugaji wengi wa Zanzibar hupiga hatua kubwa ya uzalishaji kwa kuiga taaluma mbali mbali kutoka kwa wakulima wenzao wa Tanzania Bara.
Maonesho ya wakulima nane nane ambayo hufanyika kila mwaka katika mwezi wa Agosti ambapo wakulima na wafugaji hupata fursa ya kuonesha bidhaa mbali mbali wanazozalisha sambamba na kubadilishana mawazo miongoni mwao.
Ziara hiyo ambayo imefadhiliwa na progamu za ASSP na ASDP-L, progamu ndogo ya Zanzibar, imegharimu jumla ya shilingi milioni 23,220,000.
Programu za ASSP na ASDP-L ambapo lengo lake ni kumpunguzia umasikini mkulima na kumwezesha kuwa na uhakika wa chakula, zimekuwa zikiwapeleka wakulima kwenye maonesho kama hayo tangu mwaka 2008 kwa lengo la kupata mbinu mbadala za uzalishaji wenye tija zaidi.

MARUFUKU KUINGIZA BIDHAA ZA MIGAMBA KUTOKA BARA.

Marufuku kuingiza bidhaa za mgomba kutoka Bara

Na Nafisa Madai, Maelezo
WIZARA ya Kilimo Maliasili imepiga marufuku uingizaji wa bidhaa zinazotokana mgomba ikiwemo ndizi, miche ya migomba, majani ya migomba pamoja vigogo vya mgomba kutoka Tanzania bara.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari huko ofisini kwake Mwanakwerekwe wiliya ya Magharib, Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi na Utibabu wa mazao Zainab Salim Abdallah, alisema marufuku ya kuingizwa kwa bidhaa hizo inafuatia kuibuka maradhi mnyauko.
Alisema maradhi hayo yanayosababishwa na bakteria yamekuwa yakiathiri migomba pamoja na mazao yake ambapo kizuizi kilichowekwa kinalenga kuiepusha Zanzibar kukumbwa na maradhi hayo.
Mkuu huyo alisema Tanzania bara imekumbwa na maradhi hayo tangu mwaka 2007, ambapo kama Idara inalazimika kuchukua hatua ya kuzuia hasa katika kipindi hicho cha mwezi wa Ramadhani kutokana na walaji ndizi kuongezeka kuliko siku za kawaida.
Zainab alisema kuwa maradhi ya mnyauko hayamuathiri mlaji wa ndizi bali athari kubwa anaweza akaipata mkulima wa migomba endapo bidhaa hiyo kwani itamsababishia hasara kubwa mkulima huyo kwa asilimia 100.
Aliwaomba Wazanzibari kutoa mashirikiano katika kutekelezwa kwa ahizo hilo ili kuepusha kusambaa kwa maradhi hayo kwa migomba ya Zanzibar.
Zainab alisema mtu yoyote atayekamata anaingiza bidhaa hiyo kutoka bara atafikishwa katika vyombo vya sheria na sheria itashika mkono wake kwa muingizaji huyo.
Alisema kitengo chake tayari kimeshakamata ndizi amabazo zimebainika na maradhi hayo kutoka bara na mipango inaandaliwa kuziangamiza ndizi hizo ili iwe fundisho kwa wengine ambao wanampango wa kuingiza ndizi Zanzibar.
Akizungumzia nzi wa matunda alisema nzi hao hivi sasa wameshamiri sana visiwani hapa na wamekuwa wakishambulia embe kwa kiasi kubwa jambo ambalo limekua likiwavunja moyo wakulima wa zao hilo.
Aidha alisema nzi hao ambao chimbulo lake Indonesia wamekua wakileta hasara kubwa kwa wakulima kwani soko limekua dogo sana ikilinganisha na hapo awali.
Hata hivyo alisema juhudi zinafanywa za kuangamizwa nzi hao za kuwawekea mitego maalum na kwasasa tayari wameanza katika wilaya ya Kusini na wamefanikiwa kwa aslimia hamsini ambapo zoezi hilo linategemewa kufanya katika mikoa yote ya Zanzibar.
Akizungumzia mende wadogo ambao nao wameshamiri kwa wingi katika visiwa vya Unguja, alisema mende hao wanaathiri sana katika makaazi ya watu kwani hushambulia nguo na vitu vyengine majumbani.
Amesema kuwa mende hao wametokea ulaya na wamekuja kutokana na vifaa vya umeme vinavyoingizwa na ambavyo vimezagaa katika Manispaa ya mji wa Zanzibar.
Aidha alisema juhudi za makusudi zinachukuliwa za kutokomeza mende hao maarufu mende wa Ulaya, na kuwaasa wale wote wanafanya biashara hiyo ya vifaa vilivyokwisha tumika kuangalia kwa makini vifaa hiyo kwani athari yake baadae inaweza kuwa kubwa zaidi.

Tuesday, 2 August 2011

MAALIM SEIF KUKOSEKANA UMOJA KUMEREJESHA NYUMA ZANZIBAR.

Maalim Seif: Kukosekana umoja kumeirejesha nyuma Zanzibar
Na Mwanajuma Abdi
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kukosekana kwa umoja kulipelekea kujengeka uadui wa kutoaminiana, na kuheshimia miongoni mwa wananchi na kusababisha hali kuwa mbaya iliyorejesha nyuma maendeleo ya kiuchumi nchini.
Maalim Seif alieleza hayo jana wakati akifungua kongamano la siku ya Umoja wa Kitaifa, iliyotimia mwaka mmoja tokea wazanzibari kuamua mfumo huo, lililoandaliwa na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) lililofanyika ukumbi wa Beyt El Yamin, mjini hapa, ambapo kauli mbiu ni ‘Zanzibar Haitarudi tena Nyuma’.
Alisema kukosekana kwa umoja huo kulisababisha imani kudhoofika, kununiana, kutukanana, kutengana, kuhujumiana na kuuana ilimradi ubinaadamu uliondoka kabisa, jambo ambalo kwa sasa mambo hayo yameondoka.
“Wenye busara wamekuwa wakisema ‘ikiondoka imani, hakuna amani’, hakuna aliyeishi kwa amani, hata kama akilindwa nje ya maridhiano na umoja wa kitaifa”, alisisitiza maalim Seif.
Alieleza wengi wao ni mashahidi kuwa Zanzibar haijawahi kuwa na utulivu na kisiasa takriban nusu karne nzima, uanzishwaji wa mfumo wa kisiasa wa vyama vingi wakati wa ukoloni katika miaka ya 1950, ulisababisha mpasuko mkubwa wa kisiasa, ambapo kuanzia enzi hizo jamii ya kizanzibari iligawika karibu katikati katika mapande mawili na kila pande lilijitambulisha na chama kimoja au muungano wa zaidi chama kimoja.
“Kipindi cha 1957-1964 Zanzibar ilishuhudia msuguano mkali baina ya wafuasi wa Chama cha Afro Shirazi (ASP) kwa upande mmoja na muungano wa vyama vya Zanzibar Nationalist Party – Hizb al Wattan (ZNP) na Zanzibar Pemba Peoples Party (ZPPP), msuguano huo ulipelekea wazanzibari kuukaribisha uhuru wake Disemba 10, 1963 kwa mitazamo tofauti”, alisema.
Alisema masikitiko makubwa walioyashuhudia wananchi baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa ni kurejea kwa ule mpasuko wa jamii ya kizanzibari, ambapo nchi iligawika nusu ya watu wakaunga mkono chama mrithi wa ASP yaani CCM na nusu wakaunga mkono chama kipya cha CUF.
Alieleza mfumo wa utawala uliokuwepo wa mshindi kuchua kila kitu na alieshindwa kupoteza kila kitu ulichochea msuguano uliowepo.
Aidha alifahamisha kuwa, sasa ni miezi tisa tangu kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa, ambapo alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuiongoza serikali hiyo kwa hekima na busara kubwa kiasi kwamba viongozi wanashirikiana katika kazi kwa ajili ya kuwaletea maslahi wananchi wa visiwa hivi.
Aliongeza kusema kwamba, Umoja wa Kitaifa ni hazina ya wazanzibari kwa zama na zama huko nyuma, hazina hiyo ilikuwa imepotea kwa zaidi kidogo ya nusu karne sasa imepatikana kwa watu kuishi kwa kuvumiliana, kuheshimiana, kusaidiana na kutakiana kila la kheri kwa hakika na kufikia ukombozi wa kweli wa nchi na maisha kwa ujumla.
Nae Katibu wa WAHAMAZA, Mwandishi Mwandamizi, Salma Said alisema ni mwaka mmoja uliopita nchi kuripuka kwa furaha baada ya matokeo ya kura ya maoni ya kudhihirisha kuwa karibu thuluthi mbili ya wazanzibari walichagua kupiga NDIO katika kura hiyo na hivyo kufungua ukurasa mpya wa kisiasa.
Aliomba Serikali siku hiyo ifanywe iwe kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Nao watoa mada katika kongamano hilo, walishauri Serikali kuangalia changamoto mbali mbali zinazoikabili Serikali hiyo ikiwemo ufisadi na rushwa iliyotawala nchini, matumizi ya magari ya fahari ya Mawaziri na muundo mkubwa wa Baraza la Mawaziri, ambapo wengine hata Wizara hawana, jambo ambalo kwa nchi kama hii changa linaongeza umasikini.
Makamu wa Kwanza wa Rais, maalim Seif Sharif Hamad alitoa ufafanuzi juu ya maswali hayo kwa kusema si vyema wananchi wakalalamika kwani bado ni mapema kwa Serikali hiyo, ambapo aliahidi kufanyiwa kazi kasoro hizo.
Alisema suala la rushwa, mswada unatarajiwa kufikishwa katika Baraza la wawakilishi katika kikao kijacho, sambamba na kuvipongeza vyombo vya habari hasa vya Serikali kwa kupiga hatua kubwa katika utoaji wao wa taarifa.
Nao wananchi mbali mbali wakichangia katika kongamano hilo, waliomba iendelezwe na watu wasirudi kamwe walikotoka na kinachotakiwa wazanzibari wawe wamoja katika kudai mambo yanayohusu nchi yao.