Monday 31 May 2010

Hakuna maendeleo bila mageuzi ya kifedha kimataifa- Dk. Karume



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume ametoa wito wa kuwepo mabadiliko katika taasisi za kifedha za Kimataifa ili kutoa nafasi sawa katika mataifa yote makubwa na madogo ulimwenguni.
Wito huo ametoa wito huo katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi Duniani (WEF) uliomalizika jana mjini Doha, Qatar.

Katika mkutano huo Rais Karume alisisitiza kuwa maendeleo ya uhakika hayawezi kupatikana bila ya kuwepo mageuzi ya kifedha ya kimataifa hasa kwa kuzingatia kuwa taasisi hizo ziliundwa wakati ambao kulikuwa na nchi chache zenye uwezo wa kiuchumi na kiutawala duniani.


Alieleza kuwa wakati huo taasisi hizo ziliundwa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya nchi hizo chache.

“Taasisi hizo ziliundwa ili kukidhi mahitaji hayo lakini sasa wadau ambao ni sisi sote tuko wengi na ni lazima kupatikana usawa wa fursa ili kuweza kushiriki kikamilifu”, alisema Dk. Karume.


Aidha, Rais Karume alizungumzia umuhimu wa elimu katika kuleta maendeleo ya binaadamu na kusisitiza haja ya kuiimarisha sekta hiyo.

“Elimu ndio ufunguo wa maisha katika maendeleo ya binaadamu”, alieleza Rais Karume.

Rais Karume alisisitiza umuhimu wa kuwepo ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya elimu.

Katika mkutano huo, Rais Karume alikuwa ni miongoni mwa wazungumzaji wakuu katika ufunguzi wa mkutano huo.

Wazungumzaji wengine katika mkutano huo uliofunguliwa na Amir wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani, aliyekuwa mrithi wa Mfalme wa Norway Prince Haakon, Mke wa Mfalme wa Jordan Malkia  Rania, Waziri wa Maendeleo wa Singapore na wengineo.


Katika mazungumzo hayo walisisitiza haja ya kuimarisha sekta ya elimu kwani ndio mkombozi katika kuimarisha sekta zote za maendeleo na ukuzaji wa uchumi.


Akifungua mkutano huo mkubwa wa kiuchumi duniani, Amir wa Qatar alisisitiza ushirikiano wa kimataifa na kubuni mikakati itakayosaidia katika kupambana kwa pamoja na matatizo ya kiuchumi duniani.

Nae mke wa Mfalme wa Jordan, Malkia Rania alizungumzia umuhimu wa maendeleo ya vijana hasa katika elimu.


Malkia Rania alieleza kuwa kukosekana kwa elmu kunasababisha ukandamizaji wa vijana na watoto sambamba na kukosa fursa za kujiimarisha kimaendeleo.

Ufunguzi wa mkutano huo uliendeshwa na Profesa Claus Schwab ambaye ndie Mwenyekiti Mtendaji wa WEF.

Mkutano huo ulitanguliwa na mikutao midogo midogo ya majadiliano juu ya mada mbali mbali zikiwemo elimu, afya, maendeleo ya ushirikiano wa kimataifa, uimarishaji wa uchumi na fedha, mazingira, usalama na nyenginezo ambayo iliwashirikisha viongozi mbali mbali kutoka sekta tafauti za serikali na zile za kibinafsi wakiwemo mawaziri,wataalamu na wakuu wa taasisi mbali mbali ambapo Tanzania pia imewakilishwa na baadhi ya Mawaziri waliomo katika nyanja hizo.

Wanawake 21 wajitokeza kuwania uongozi Zanzibar

Na Ananiel Nkya -Tamwa
WANAWAKE 21 wa Zanzibar wametangaza nia ya kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama mbali mbali vya siasa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Oktoba mwaka huu.

Wanawake hao ni wale ambao wamenufaika na mradi wa kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi, Zanzibar (WEZA) unaoendeshwa katika Mkoa wa Kusini Unguja na Kaskazini Pemba tokea 2008.

Wanawake 13 kati ya hao wanatoka Mkoa wa Kaskazini Pemba na wanane ni kutoka Mkoa wa Kusini Unguja.

Waratibu wa Shehia za mikoa hizo wamesema wamefurahishwa na uamuzi wa wanawake hao kutaka kugombea uongozi na kwamba hayo ni maendeleo makubwa ikizingatiwa kuwa katika chaguzi zilizopita wanawake walikuwa hawajitokezi kwa wingi kugombea.

Mratibu wa Shehia ya Tumbe Magharibi, Salma Tumu, ambaye Shehia yake imetoa wanawake watano wanaogombea, amesema jitihada za kuwawezesha wanawake wa Zanzibar kujiamini kijamii na kiuchumi zikiendelezwa lengo la kupata asilimia 50 ya wanawake katika uongozi wa kuchaguliwa litafikiwa kirahisi.

Raya Majid Salim ambaye ametangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Tumbe huko Pemba amesema ameamua kugombea kwa sababu anajiamini kuwa anao uwezo wa kusimamia maendeleo ya wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo ya kijamii yanayowakabili wanawake.

“Wanawake sasa tunafahamu haki zetu katika uongozi na kilichobaki ni kuzipigania ili kuzipata na kuzitumia kwa ajili ya kuharakisha maendeleleo ya jamii nzima-wanawake, wanaume na watoto”, alisema Raya Majid Salim.

Aliyataja matatizo yanayokwamisha maendeleo ya familia na taifa huko Zanzibar ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na viongozi kuwa ni pamoja na watoto wa kike kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo na wanaume na wanawake wasio na kipato kukosa mitaji kwa ajili ya kuendesha miraji ya kiuchumi.

Khadija Omar Kibano ambaye anagombe udiwani wadi ya Mtambwe kaskazini amewataka wanawake nchini kote kugombea nafasi mbali mbali katika uchaguzi wa mwaka huu kama wanavyojitokeza wanaume

Mradi wa WEZA unaendeshwa kwa mashirikiano kati ya Care Tanzania, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Umoja wa Ulaya (EU), Serikali ya Austria na Care Austria.

Mbunge Sanya, Jussa watamba Mji Mkongwe


  • Fatma Ferej, Najma, Nabahan waangukia kisogo

  • Msanii Abdulla Isaa atafuta mchawi
Na Aboud Mahmoud


MWAKILISI wa jimbo wa la Mji Mkongwe kwa tiketi ya Chama cha Wananchi CUF, Fatma Abdulhabib Ferej ameangushwa katika kinyang’anyiro cha kura ya maoni ya CUF.

Fatma ambae amepata kura 183 ameangushwa na Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Ismail Jussa Ladhu aliyepata 334 ambapo nafasi ya tatu ikishikiliwa na Abdullah Uhuru aliepata kura 93 na Othman Hamad, kura 2.

Katika uchaguzi huo, uliofanyika katika ukumbi wa Wakf wa Wangazija Kiponda mjini Unguja, umempitisha tena Mbunge wa jimbo hilo, Ibrahim Mohammed Sanya kwa kupata kura 327.

Sanya amemuangusha msanii maarufu wa muziki wa taarab, Zanzibar, Abdullah Issa Khamis aliyepata kura 115 huku Amina Abdullah, amepata kura 119 na Ali Majid, akaangukia kura 54.

Katika hatua nyengine, uchaguzi huo wa kura za maoni kwa tiket ya CUF katika jimbo la Mji Mkongwe uliwachagua wagombea udiwani ambapo katika wadi ya Mkunazini, Diwani anaeshikilia nafasi hiyo Nassor Amin amepata kura 174 na kumuangusha Ramadhan Adnan aliepata kura 152.

Katika wadi ya Mchangani mgombea nafasi hiyo hakua na mpinzani naye ni Amir Said Bashut ambae amepata kura 317.

Uchaguzi huo ambao wengi walikuwa wakiutizamia kuwa na vishindo uliendeshwa kwa amani na utulivu huku kila mgombea akikubaliana na matokeo.

Aidha uchaguzi huo ulikuwa kivutio kikubwa kwa kuvuta hisiaa za wananchi wengi wa jimbo hilo kutokana na kila mmoja kujinadi kuzikamata nafasi hizo.

Baadhi ya Wawakilishi kupitia chama hichowalioangushwa katika nafasi hiyo ni pamoja na Naibu Spika na Kiongozi wa juu wa jumuiya ya Wanawake ya CUF, Aziza Nabahan Suleiman.

Mwengine alieangushwa ni pamoja na mwandishi wa habari wa na mtangazaji wa zamani, Najma Khalfan Juma ambao wote walipata alama ya nne katika uchaguzi huo, huku Zakia Omar, akishikilia nafasi ya pili.

Binti afariki baada kuangukiwa na jiwe

Zuhura Msabaha, Pemba
MTOTO wa kike mwenye miaka 13, Tauhida Haji Abdul-rahman, amefariki dunia hapo hapo na mwenziwe Time Burhani Haji (12) amejeruhiwa baada ya kuangukiwa na jiwe wakati wakichimba mawe huko Mkwaju Mgoro, Micheweni.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Mkoa kaskazini Pemba, Yahya Rashid Bugi, alisema Tauhida alifariki alipokuwa anachimba mawe na wenziwe kwa ajili ya kuvunja kokoto.

Alisema, katika harakati hiyo ya kuchimba mawe, jiwekubwa lilichomoka jiwe kubwa lililomuangukia na kupoteza uhai wake ambalo pia lilimjeruhi Time.

Kamanda Bugi alisema tukio hilo lilitokea Mkwaju Mgoro, Micheweni mnamo majira ya saa 7:00 mchana.

Kamanda alisema hali ya Time ambaye amejeruhiwa amelaza katika hospitali ya Micheweni anaendelea kupata matibabu huku hali yake ikielezwa kuwa siyo mbaya sana

Alisema mabinti hao walikuliwa wakichimba mawe kwa ajili ya kuvunjwa kokoto ili kuziuza

Kamanda alitoa wito kwa wachimbaji mawe kuwa na tahadhari katika kazi h yao hiyo hasa katika kipindi cha mvua kutokana na ardhi kushibwa maji hali ambayo inasababisha ardhi hiyo kuwa laini.

Daktari dhamana wa hospitali wa Wilaya ya Micheweni, Hamad Ali Hamad, alisemabinti aliyefariki aliumia kifua na mbavu huku aliyejeruhiwa aliumia mguu na mbavu.

Tuesday 25 May 2010

Bandari yafungua tenda ujezi wa mnara mwana wa mwana

Na Ramadhan Makame
MKURUGENZI wa Ufundi Shirika la Bandari, Abdi Omar Maalim amesema Shirika hilo litachagua kampuni yenye uwezo zaidi katika ujenzi wa mnara wa Mwana wa Mwana.

Mkurugenzi huyo alisema hayo jana katika hafla fupi ya ufunguzi wa zamani za ujenzi wa mnara huo zilizotumwa na makampuni ya ujenzi.

Alisema shirika hilo lingependa kuona mnara huo unafanyiwa matengenezo na kuwa kwenye hali bora zaidi ya ulivyo hivi sasa.

Aliyakahikishia makapuni yaliyoomba zabuni ya ujenzi huyo kuwa uadilifu wa hali ya juu utakuwepo kwenye mchakato wa kuipata kampuni hiyo.
 
“Tunaomba mtuamini kuwa kazi hii itafanywa kwa imani na kampuni zitakazoshindwa zisichoke kuomba kazi nyengine ikitokea kwenyeshirika letu”,alisema Mkurugenzi huyo.
 
Alifahamisha kuwa ili mnara huo ujengwe vizuri ni lazima kampuni bora kati ya zilizojitokeza ichaguliwe katika ujenzi wake.

Mkurugenzi Maalim, alisema mnara wa Mwana wa Mwana ni miongoni mwa minara muhimu sasa katika kuviongoza vyombo vya usafiri wa baharini.
 
“Huu ni mnara muhimu sana katika kuviongoza vyombo vya baharini, ujenzi wake lazima upate kampuni iliyo imara”,alisema.
 
Alisema baada ya ufunguzi wa zabuni hizo, zitapelekwa kwenye kamati ya uongozi wa shirika na kujadiliwa kabla ya kuelezwa kampuni ipo iliyoshinda zabuni.

Kampuni sita yalitokeza kuomba zambani ya ujenzi wa manara wa kuongozea vyombo vya baharini uliopo Tumbatu,kati ya kampuni hizo kampuni nne ndizo zilizorejesha zabuni hiyo kwa wakati.

Kampuni zilizojesha ombi la ujenzi wa huo ni Jamaa Constructions Compay ambayo imeomba zaidi ya shilingi milioni 75.5 za ujenzi wa mnara huo kwa wiki 14.
 
Kwa upande wa kampuni ya Salem Constructions Limited, imeeleza kuwa itaifanya kazi hiyo kwa wiki 10 kwa shilingi milioni 119.

Aidha kampuni ya Azim Constructions imetaka milioni 138 na ujenzi utachukua muda wa wiki 16.

Huku kampuni ya mwisho ya Zeccon Limited ikihitaji milioni 108.9 za ujenzi utakaochukua wiki 22.



Wataalamu bado wanahitajika uchimbaji mafuta Z’bar-Nahodha

Na Mwanajuma Abdi
WAZIRI Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha amesema watalaamu wanahitajika katika suala la uchimbaji wa mafuta na kusimamia athari za kimazingira katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini nchini.

Nahodha aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, baada ya Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid kufunga semina ya sikuiliyozungumzia mafuta na gesi asilimia.

Alisema changamoto kubwa inayoikabili Zanzibar ni kuhakikisha inakuwa na wataalamu watakaosaidia kuepusha uchafuuzi wa mazingira ya baharini na nchi kavu wakati zoezi la uchimbaji mafuta litakapoanza.

Alisema watalaamu wa Norway katika semina hiyo wameonesha njia kwa kutoa rai jinsi ya kuwapata wataalamu wa ndani na nje katika kusimamia suala hilo, kwa vile litakapoanza athari za kimazingira zinaweza kujitokeza katika maeneo mbali mbali yakiwemo ya bahari na ardhini.

Alisema katika kukabiliana na athari hizo, lazima ziandaliwe mbinu za kukabiliana nazo kwa vile waathirika wakubwa ni wananchi.

Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume amekuwa akichukua jitihada mbali mbali kuboresha uchumi wa Zanzibar na katika kufanya hivyo ameimarisha miundo mbinu, ikiwemo umeme, barabara,maji, elimu na kilimo cha umwagiliaji maji.

Nahodha alisema Serikali imekuwa ikipitisha sera mbali mbali katika kukuza uchumi ikiwemo ya Utalii, ambapo suala la mafuta linahitaji kuwepo sheria madhubuti zitakazosaidia kuleta kasi ya maendeleo nchini.

Nae Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Abdallah Juma, alisema semina hiyo imewasaidia kwa kiasi kikubwa kuelewa kwa undani juu ya uchimbaji wa mafuta.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Ujenzi Nishati na Ardhi Mwalim Ali Mwalim alisema utawala bora katika uchimbaji wa mafuta unahitajika kuweza kufaidika nayo.

Alifafanua kuwa, mafuta kuwepo au kutokuwepo kunahitaji kufanyika kwa uchunguzi wa muda mrefu, ambapo baadhi ya nchi kama Zanzibar zimeanza kuona dalili za viashirio katika bahari na ardhini, ambapo Zanzibar nako kunaonesha dalili hizo.

Akifunga semina hiyo, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid, amesema serikali itawasomesha vijana 10 nje ya nchi kuhusu njia za uchimbaji mafuta likiwemo la uangalizi wa athari za kimazingira.

Alisema Serikali itahakikisha kuwa, sheria ya mafuta na gesi asilia inakwenda sambamba na kuangalia sekta nyengine zikiwemo usalama wa fedha katika kukabiliana na rushwa.

Semina hiyo iliwashirisha Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wanasheria na Watendaji kutoka Taasisi mbali mbali za SMZ na wataalamu wa Norway ambao ni wakufunzi wa mafunzo hayo ya siku mbili.

Bodi rufaa ya kodi kusimamia malalamiko ya wafanyabiashara

Na Mwanajuma Abdi
BODI ya Rufaa ya Kodi Zanzibar, imesema itasimamia ipasavyo shauri la kodi litalofikishwa na walalamikaji wakiwemo watu wa kawaida, wafanyabiashara na Serikali katika upandishwaji na ulipaji kodi katika kipindi cha wiki moja ili haki itendeke.

Hayo aliyasema jana, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Khamis Ramadhan wakati akizungumza na waandishi wa habari huko, Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar.
 
Bodi hiyo itakuwa ikifanya kazi ya kupokea malalamiko hayo kwa muda katika Afisi ya Kitengo cha utawala na Huduma katika Wizara ya Fedha, hadi Afisi yao itakapokamilika katika jengo la zamani la Maktaba Kuu ya Zanzibar, Vuga mjini hapa.

Alisema Bodi hiyo itakuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa baina Bodi ya Mapato (ZRB) na Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato Tanzania (TRA), ambapo ndio wakusanyaji wa kodi mbali mbali kuanzia mshahara wa mfanyakazi, wafanyabiashara hadi wawekezaji waliopo nchini.
 
Alisema Bodi hiyo itakuwa ikisikiliza malalamiko ya wateja mbali mbali, watakaonesha vielelezo wanayoyalalamikia ili haki itendeke.
 
“Malalamiko hay pia yapo kwa Serikali kutokana na baadhi ya wawekezaji na wafanyabiashara kukwepo kulipa kodi kwa wakati, ambapo kuwepo kwa Bodi hiyo kutasaidia upatikanaji wa kodi ya SMZ katika kukuza maendeleo ya uchumi wa nchi,” Alifafanua
 
Mwenyekiti huyo, alifahamisha kuwa, Bodi hiyo inafanya kazi chini ya sheria namba moja ya mwaka 2006 na kanuni ya Aprili 21 ya mwaka huu, ilitangazwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar kupitia gazeti la Serikali ili kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila ya kuingiliwa na chombo chochote.
 
Alisema uamuzi wa kuwepo Bodi ya Rufaa ya Kodi Zanzibar umekluja kufuatia malalamiko mengi ya wafanyabiashara kutozwa kodi kubwa na ZRB na TRA, pamoja na Serikali kutolipwa mapato yake kwa wakati, huku serikali ikiwadai fedha nyingi wawekezaji na wafanyabiashara wanaochelewesha malipo ya kodi.

Thursday 20 May 2010

Uwanja safi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Amani Abeid Karume akingalia uwanja mpya wa Amani baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Unauona uwanja wetu

Huu ndio uwanja wa Amani uliofanyiwa ukarabati na Wachina na kukabidhiwa rasmi kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.(Picha na Othman Maulid).

Tuesday 18 May 2010

Kituo cha Umeme Mtoni

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume,akiulizaa masula kwa watalamu,wakati alipotembelea sehemu itakayowekwa majenerta ya Akiba pindi Umeme utakapokuwa na Hitilafu huko Mtoni Kituo Kikuu cha Umeme. (Picha na Ramadhan Othman).

Wanasiasa waaswa kutopenyeza sumu vikundi vya ushirika

Na Hashim Mlenge
BAADHI ya wanasiasa nchini wameshauriwa kusimamia maedneleo nchini badala ya kutumia muda mwingi kulumbana kisiasa.

Wameelezwa kuwa suala la maendeleo lazima lipewe umuhimu wa kwanza katika mijadala ya kisiasa na viongozi hao wahakikishe kuwa wanawaunga mkono wananchi kufikia maendeeo yao.
 
Wito huo umetolewa na Katibu wa Umoja wa Vijana wa (CCM) Wilaya ya Magharibi, Abubakar Ali Hamdani, wakati akizungumza na gazeti hili hivi karibuni huko Fuoni Wilaya ya Maghabi Unguja.
 
Alisema wamechipuka baadhi ya wanasiasa wanaoingilia kati vikundi vya maendeleo kwa kuwatwisha mzigo wa propaganda za kisiasa, hali inayowafanya wasisimamievizuri maendeleo yao ya kila siku.
 
ikuwa kumekuwapo na baadhi ya wanasiasa kuingiliana kati vikundi vya maendeleo vinavyoanzishwa na wananchi halia mabyo huwafanya kuingiza siasa zao ambazo zinaeza kupelekea kuivunjika kwa umoja uo.
 
Alifahamisha kuwa hali hiyo ikizidi kutawala katika nyoyo za watu ni wazi kuwa inaweza kuvunja umoja baina ya wanavikundi vya ushirika na kutawanyika.

Katibu huyo alisisitiza kuwa si haki wala si ruhusa viongozi wa kisiasa kutumia muda wao kuingilia kati jitihada za wananchi za kutafuta maendeleo ambazo zimelekezwa zaidi kwenye njia ya ujitegemea.
 
“Sioni busara yoyote kwa wanasiasa kuzinadi siasa zao katika vkundi vya ushirka, hali ambayo huweza kuleta migongano baina ya wananchi kwa sababu vikundi hivyo havikuanzishwa kisiasa bai wa nia ya kiuchumi.
 
“Nndani ya Vikundi hakuna wanasiasa wa vyama tofauti, hivyo, tusijaribu kuzitangaza siasa zetu katika vikundi hivyo kwani tunaweza kusababisha matukio mabaya vikundini humo”.
 
Hivyo, alisema kuwa ni wajibu wa viongozi hao kuwa pamoja na wanavikundi ili kuunga mkono jitihada za kuwaletea maendeleo na kuondokana na umasikini.
 
Hatua ya Katibu huyo inaokana imetokana na kuzuka kwa baadhi ya wanasiasa wanaojaribu kuingilia kati jitihada zilizofanywana wananchi wa jimbo la Fuoni ya kuanzisha kwa kamati ya Wanafunzi ya kuwaendeleza kielimu.

Kumi waburuzwa mahakamani kwa tuhuma za unyangaji wa kutumia nguvu

VIJANA kumi wakaazi wa maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Magharibi Unguja, wakiwemo wanne wenye umri kati ya miaka 15 na 16, wamefikishwa Mahakamani Vuga, wakikabiliwa na tuhuma za unyang’anyi wa kutumia nguvu.
 
Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu, Nassor Ali Salim wa Mahakama ya Mkoa Vuga, na kusomewa mashitaka na Mwanasheria wa serikali, Sabra Mselem kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
 
Habari zilizopatikana kutoka mahakama hiyo jana, zinasema bada kukana tuhuma hizo, pamoja na upande wa mashitaka kutopinga dhamana juu yao, Hakimu Nassor Ali Salim aliwanyima dhamana watuhumiwa hao na kuwapeleka rumande kwa muda wa siku tisa.

Watuhumiwa hao ni Said Khamis Juma (15), Mkaazi wa Magogoni, Dadi Khamis Talib (15), wa Makondeko, Khamis Hamadi Bakari (19), anayeishi Magogoni, Makame Jumanne wa Magogoni na Othman Khamis Othman (21) Mkaazi wa Mwanakwerekwe.
 
Watuhumiwa wengine katika kundi hilo ni Rashid Mohammed Simba (10) wa Magomeni, wilaya ya Magharibi, Said Salum Hamadi (15), Khamis Mngwali Juma (18), Mohammed Said Salum (17) na Kassim Hamadi Abdallah (16) ambao wote ni wakaazi wa Magogoni.

Mapema, wakiwa mbele ya kizimba cha mahakama hiyo, Mwendesha Mashitaka, Sabra Mselem aliwasomea watuhumiwa hao shitaka la unyang’anyi wa kutumia nguvu kinyume na kifungu cha 285 na 286 (1) cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
 
Katika maelezo yake, Sabra Mselem aliiambia mahakama kwa kudai kuwa, vijana hao kwa pamoja bila ya halali na kwa makusudi, waliyang’anya mali inayokisiwa kuwa na thamani ya shilingi 255,000.
 
Sabra aliiambia mahakama iliojaa waskilizaji kuwa mali inayodaiwa kuibiwa ni mabegi matatu ya nguo, radio Kaseti moja pamoja na fedha taslimu shilingi 200,000 mali ya Yussuf Ali Hamadi.
 
Kabla ya unyang’anyi huo, mahakama hiyo ya Mkoa ilifahamishwa kuwa waLIMshambulia Yussuf Ali Hamadi na Omar Juma Omar kwa kuwapiga mawe miguuni na kifuani na hatimae kufanikiwa kuwa nyang’anya mali hiyo, shitaka ambalo walilikana.
 
Pamoja na kukana huko, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, na kuiomba mahakama hiyo kulipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa pamoja na kutolewa kwa hati za wito kwa mashahidi.
 
Hakimu Nassor Ali Salim, alikubaliana na hoja hizo na kuliahirisha shauri hilo hadi Mei 26 mwaka huu kwa kusikilizwa, na kuutaka upande huo wa mashitaka kuita mashahidi siku hiyo.
Na Khamis Amani

SACCOS ya elimu yajiandaa kutoa mikopo, kufanyakazi kama Benki

USHIRIKA Wa Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (Elimu Saccos) unakusudiwa kuimarishwa kwa kufanyiwa mabadiliko ili uweze kutoa mikopo kama zifanyazo benki mbali mbali hapa nchini.
 
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa ushirika huo Salma Simai Rajab mbele ya waandishi wa habari mwanzoni mwa wiki, imeeleza kuwa mikakati ya kufikia hatua hiyo inatarajiwa kukamilika karibuni na kwamba lengo hilo likifikiwa, benki hiyo itakuwa na fursa nyingi za utoaji mikopo kwa wanachama na watu wengine.
 
Alisema kuwa hatua hiyo inafuatia ushirika huo ulioanzishwa mwaka 1997 kwa lengo la kuwakomboa kiuchumi wafanyakazi wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kuimarika kifedha.
 
''Ushirika wetu umeimarika sana tulianza kutoa mikopo ya vifaa mbali mbali vikiwemo vya ujenzi na sasa tunakusudia kuufanya benki ili kutoa mikopo ya fedha, '' alisema Salma.

Alisema maandalizi ya kuubadili ushirika huo kuwa kuwa benki yameshaanza ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo yanayohusisna na masuala ya fedha baadhi ya wanachama wake ambayo yametolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB na Benki ya Maendeleo Vijijini CRDB.
 
Salma alifahamisha kuwa Benki zimekubali kuwa wafadhili wa ushirika huo kwa kutoa mikopo ya fedha ambazo hutumika kuwakopesha wanachama wa ushirika huo ambapo hivi karibuni benki ya CRDB iliupatia mkopo wa shilingi milioni 530 ushirika huo.
 
Alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika yenye Makao yake Makuu mjini Tunis Tunisia na ya CRDB ya mjini Dar es salaam zimeahidi kutoa mtaji wa fedha baada ya mipango ya kuanzisha BenkI hiyo kufanikiwa.

''Matumaini yetu ni kwamba tutafanikiwa kuugeuza ushirika wetu kuwa Benki hasa ukizingatia mshikamano tulionao kati ya Benki hizo zenye umaarufu na uwezo mkubwa,'' alisema Salma.
Na Issa Mohammed

Saturday 8 May 2010

Darasa la kompyuta

WanaCCM chagueni wanaochagulika – Membe

Na Mwantanga Ame
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amewataka wanachama wa CCM Jimbo la Kitope kuchagua viongozi wataoweza kuchagulika katika ngazi zote.

Hayo aliyasema jana katika sherehe fupi ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Jimbo hilo.
 
Katika ujenzi huo, alichangia kwa kutoa shilingi milioni 15 ambazo alimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ali Idd.
 
Waziri Membe alikabidhi fedha hizo kwa kutoa shilingi milioni 8 taslim na kuahidi kumalizia shilingi milioni 7 baada ya wiki moja.
 
Fedha hizo zilizotolewa ni kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi huo ambao unatarajia kumalizika mwezi Disemba mwaka huu na utagharimu shilingi milioni 35 hadi kukamilika kwake.
 
Waziri Membe, alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) kiko katika harakati za kukabiliana na uchaguzi Mkuu hivyo ni vyema wakati wa kupiga kura ya maoni ya kutafuta wagombea wanachama wahakikishe wanachagua viongozi wataoweza kuchagulika katika nafasi yoyote.
 
Alisema CCM katika uchaguzi mkuu ujao kimeamua kutanua demokrasia katika kupata wagombea, lakini ikiwa hawatazingatia kuitumia vyema kuchagua viongozi bora watakuwa wanafanya makosa.
 
Alisema jambo la msingi ambalo wanapaswa kulizingatia wakati wakifanya uteuzi wa viongozi wao ni kuhakikisha wanachagua viongozi ambao watakuwa wanateulika katika ngazi zote.
 
Alisema hatua hiyo ni muhimu kuzingatiwa na wanachama wa Chama cha Mapinduzi kwani viongozi bora wataowachagua ndio wataompa nafasi nzuri ya kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu Rais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
 
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu alisema Chama cha Mapinduzi kinafahamu umuhimu wa maendeleo na kuwepo kwa ukumbi huo wa mikutano utaweza kuchangia kuinua shughuli za chama.
 
Membe alisema wazo la viongozi wa Jimbo hilo kuamua kuanzisha ukumbi huo ni moja ya jambo zuri linalostahiki kupongezwa.
 
Mjumbe huyo katika sherehe hiyo pia aliwakabidhi kadi wanachama wapya 210 wa Jimbo hilo pamoja na kukubaliana kushirikiana kati ya Jimbo la Kitope na Jimbo lake cha Mtama liliopo Kusini mwa Tanzania.
 
Naye mfanyabiashara Mohammed Raza alichangia ujenzi wa jengo hilo kwa kutoa mabati 50 pamoja na vifaa vya michezo ikiwemo kikombe, mipira na jezi kwa timu 21 za Jimbo hilo.
 
Aidha Raza alitoa mchango kama huo wa vifaa vya michezo kwa timu za Jimbo analoliongoza Waziri Membe la Mtama.
 
Baada ya kukabidhi msaada huo Raza aliwaeleza wanachama hao kuwa hatua yake ya kutoa msaada huo ni muhimu na kukuza ushirikiano kati ya wafanyabiashara na wananchi.
 
Alisema bila ya wananchi kuchangia kutumia huduma zao wafanyabiashara wasingeweza kunufaika na ndio maana ameamua kutoa misaada kwa wananchi kwa vile wanathamini mchango wao.
 
Hata hivyo Raza alionya wafanyabiashara waliojijengea tabia ya kuwakandamiza wananchi kwa kuwauzia bidhaa zao kwa bei ya juu kiasi cha kuwafanya maisha kuyaona magumu.
 
Naye Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Idd, alimpongeza Waziri Membe kwa moyo wake aliouonesha wa kulichangia Jimbo hilo jambo ambalo litaongeza ushirikiano wa pande mbili za Muungano.
 
Alisema mchango alioutoa ni mwanzo mwema wa kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo ambalo litawasaidia wananchi wa Jimbo hilo kwa vile hivi sasa wamekuwa wakifuata huduma za ukumbi wa mikutano maeneo ya mbali.

Mvua zateketeza mashamba ya mpunga Zanzibar

• Wakulima roho juu wahofia kukosa mavuno
Na Haji Nassor, ZJMMC
WAKULIMA wa kilimo cha mpunga wanaolima kwenye maeneo yanayopitiwa na maji katika maeneo mbali mbali wilaya ya Magharibi Unguja, wamebainisha kuwa huenda msimu huu wasipate mavuno mazuri kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kusomba mipunga yao.

Walisema kuwa hali hiyo kwa sasa imekua ikiwaweka roho juu kwa vile baadhi ya shamba zao mipunga inakaribia kuchanua huku iking’olewa kutokana na nguvu za maji ya mvua.

Wakizungumza na mwandishi wa habari katika bonde la Melinane, shehia ya Kihinani,Chuini, Mbuzini na Bububu, wamesema kuwa mashamba mengi ya mpuga umeng’olea na maji.
 
Walieleza kuwa pamoja na kutumia nguvu nyingi kwa ajili ya kutayarisha kilimo hicho na kuwa na matarajio mema kwenye mavuno, wameshavunjika moyo na wanachoangalia kwa sasa ni rehema za Mwenyezi Mungu.
 
Mmoja kati ya wakulima hao Hassan Ali Mjaka (55) wa Chuwini, alieleza kuwa hapo awali,walikua wakilia kutokana na kilimo chao kukosa maji (mvua), lakini kutokana na kuchezwa na miongo wameshakumbwa na wasiwasi mkubwa juu ya kupata mavuno bora.

“Mwanzoni mwa matayarisho ya kilimo chetu hichi cha mpunga tulikua tukililia kwamba mara hii mpunga wetu hauna maji, na ndio maana baadhi yetu hata tulichelewa kusia (kumwaga mpunga), lakini sasa maji mengi na athari tumepata.
 
Nae Juma Mcha Juma ambae ni mkulima njia mbili (Mbuzini), alisema katika eneo lao pana mfano wa ziwa, na maji hutuwa kwa kipindi kirefu, ndio hasa wamepatwa na wasiwasi ya kutokua na mavuno ya uhakika.
 
Aliongeza kwa kusema kuwa, ufumbuzi pekee juu ya hilo kwa msimu jao ni kuhakikisha wanawezeshwa ili kupigia misingi shamba zao ili maji yanapokuja waweze kuyatumia kwa mujibu ya mahitaji yao.

Kwa pande wake Mwanajuma Mzombe Issa (50) wa Shehia ya Kikangoni, alisisitiza suala pekee la kuyakinga maji ya mvua ambayo hawayahitaji kwa matumizi ya papo hapo, ni kuwepo kwa misingi ya kudumu pembezoni mwa shamba zao ili kudhibiti hali hiyo.
 
Taarifa ambazo Gazeti hili imezipata zinaeleza kuwa zaidi ekari 40 za mpunga hususani zilizopo karibu na maeneo ya njia kuu za maji ya mvua katika maeneo mbali ya Kisiwani cha Unguja zimeharibika, hali ambayo inaashiria kutokuwepo kwa mavuno ya uhakika kwa baadhi ya maeneo.

Zoezi la kuandikishwa waliokosa vitambulisho ladorora

Na Mwanajuma Abdi
ZEOZI la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, linaloendeshwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kwa watu maalum walioorodheshwa baada ya kukosa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi katika zoezi lililopita, limeanza kwa kusuasua, huku idadi ndogo ya watu waliojitokeza.

Waandishi wa habari waliotembelea katika vituo vya Mkoa wa Mjini Magharibi, wamejionea idadi ndogo ya watu waliojitokeza kujiandikisha.

Zoezi hilo la siku mbili, ambalo limeanza jana, na leo litamaliza kwa wilaya zote 10 za Unguja na Pemba kwa watu maalum walioorodheshwa na Tume hiyo, Februari 22 hadi 28 mwaka huu, waliokosa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, wakati wa uandikishaji ulipofanyika wa awamu ya kwanza na wa pili Zanzibar mzima.
 
Gazeti hili lilipata nafasi ya kuzungumza na Afisa wa wilaya ya Magharibi Unguja, Suluhu Ali Rashid katika kituo kilichopo Skuli ya Mwanakwerekwe ‘C’, alisema idadi ya watu waliojitokeza ni ndogo katika zoezi hilo maalum.
 
Alisema hadi kufikia majira ya saa 6.40 mchana watu waliojitokeza kujiandikisha ni 12 katika kituo hicho kati ya watu 337 walioorodheshwa katika daftari hilo.
 
Alieleza changamato nyengine zinawakabili katika hicho ni pamoja na kwenda watu wengi, ambao hawamo katika orodha ya majina waliyonayo kituoni hapo, wengi wanaojitokeza wakidai hawakuwepo nchini.
 
Aidha alifahamisha kuwa, watu hao waliwarejesha kwa vile zoezi hilo halihusiani na kesi zao, kwani zoezi la uandikishaji huo halihusishi masheha wala mawakala wa vyama hivyo sio rahisi kuwakubali watu waliokuwa hawamo katika orodha yao waliyoitayarisha.
 
Nae Afisa wa Uandikishaji wa wa wilaya ya Mjini, Khadija Ali, alisema zoezi linakwenda vizuri, ambapo hadi majira ya mchana watu 32 wameshaandikishwa kati ya watu 100.

Hivi juzi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ilitangaza kwamba zoezi hilo litaendeshwa jana (Mei 8 hadi 9 mwaka huu) kwa nchi nzima.
 
Aidha taarifa hiyo imefafanua kuwa watakaohusika ni wananchi walioorodheshwa majina yao katika zoezi lililofanyika Februari 22 hadi 28 mwaka huu, ambao tayari wameshapatiwa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, ndio wataohusika na zoezi hilo la siku mbili Unguja na Pemba.

Taswira ya mvua

VIJANA wakiweka mkingo barabarani kuziongoza gari kutokana na mvua kubwa inayoendelea kupiga kwenye maeno kadhaa hapa Zanzibar. (Picha na Othman Maulid).

Kijana ajitokeza kumrithi Mbunge Laizer Arusha

MBUNGE wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Lekule Laizer ameendelea kupata wapinzani, baada ya Mkurugenzi wa shirika la wafugaji la Elimu na Afya (LOPEHCO), Kashuma Ole Sayalel kutangaza kugombea kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Jimbo hilo.
 
Sayalel amekuwa mwanachama wa CCM wa pili kutangaza kuwania kiti hicho, ambapo awali mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Arusha, Francis Ole Ikayo pia alitangaza kugombea kiti hicho ambacho, Laizer atakuwa akikitetea.
 
Akizungumza, Sayalel alisema ameamua kugombea ubunge ili kusaidia kuokoa maisha ya jamii ya wafugaji ambao wanaendelea kuwa masikini kutokana na kukosa utetezi wa haki zao na kupewa mbinu sahihi za kubadilisisha maisha yao.
 
"Hali ya wafugaji wa jamii ya kimasai Longido ni mbaya sana licha ya kuwa na rasilimali nyingi kama wanyamapori na madini, naimani ninaweza kushirikiana na wadau wengine kuboresha maisha ya wananchi wa Longido"alisema Sayalel.
 
Alisema hivi sasa vijana wengi wa kimasai wa Longido wamekimbilia mijini kufanyakazi za ulinzi kutokana na maisha duni ambayo yamechangiwa na ukame ambao mwaka jana uliua mifugo yao kwa kukosa malisho na kushindwa kupewa njia mbadala ya kuendesha maisha yao.
 
"Leo hii vijana wa Longido wamejaa mjini wanalinda, wasichana wanafanyabiashara za kuuza kuni na vitu vingine ambavyo havina tija kwao hivyo naamini nina uwezo wa kukaa na makundi haya ya vijana wenzangu na kupeana mbinu mpya za kubadilisha maisha yetu"alisema Sayalel.
 
Alisema wilaya ya Longido ni moja ya wilaya ambazo zina matatizo makubwa ya miundombinu, upatikanaji wa maji na mahitaji mengine muhimu hali ambayo imemsukuma kugombea ili ashirikiane na wadau wengine kupunguza kama sio kumaliza matatizo ya wilaya hiyo.

Wilaya ya Longido ambayo awali ilikuwa ni sehemu ya wilaya ya Monduli, imekuwa ikiongozwa na Mbunge wake, Lekule Laizer kwa zaidi vipindi viwili sasa.
Na Ramadhani Juma, Arusha

Wednesday 5 May 2010

Dk.Karume akizungumza



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume akizungumza na Atzaal Malk wa kampuni ya Coca Cola, kwenye mkutano wa kimataifa wa Uchumi unaofanyika katika hoteli ya  ya Moevenpick Royal Palm mjini Dar-es-Salaam.  

Rais Karume aridhishwa na mchango wa IFAD kwenye kilimo

Na Rajab Mkasaba, Dar es Salaam
MFUKO wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), umeeleza kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kusaidia mikakati ya kutafuta ufumbuzi wa kuua wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo Zanzibar hasa nzi wa matunda.

Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Kanayo Nwanze, aliyasema hayo jana alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume, katika Hoteli ya Moevenpick Royal Palm mjini Dar-es-Salaam.
 
Dk. Karume na na kiongozi huyo wa IFAD, walikutana baada ya kikao cha asubuhi cha mkutano mkuu wa kiuchumi duniani kuhusu bara la Afria (WEF), uliozungumzia juu ya suala la kilimo.
 
Nwanze alimueleza Rais Karume kuwa mfuko huo umefarajika na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wake katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Alisema kuwa kutokana na hatua hiyo IFAD, itaendelea kuunga mkono juhudi hizo na kusisitiza kuwa miongoni mwa mipango iliyoweka katika kuimarisha sekta ya kilimo ni pamoja na kuendeleza mradi mkubwa wa kifedha utakaovinufaisha vikundi vya wanawake.
 
Nwanze leo atafanya ziara ya siku moja Zanzibar ikiwa ni pamoja na kutembelea vikundi vya kilimo, vikundi vya akinamama pamoja na kuangalia mradi wa kuua wadudu waharibifu wa kilimo huko Mwakaje.
 
Alieleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa kazi hiyo nzuri iliyooneshwa na vikundi vya kilimo, Mfuko wake utasaidia kuongeza nguvu ili kuona kazi hiyo inapata mafanikio baada ya majaribio ili iweze kutumika kwa wakulima wa mazao ambayo yamekuwa yakisumbuliwa na wadudu kwa muda mrefu.
 
Rais huyo wa IFAD alieleza kuwa zaidi ya dola za Marekani milioni 150 zimetengwa na IFAD kwa kushirikiana na taasisi nyengine za kimataifa kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini Tanzania ambapo pia Zazibar itafaidika na fedha hizo.

Alisema kuwa tayari nchi mbali mbali zikiwemo za Asia, Amerika ya Kusini na Afrika zimo katika mchakato wa mradi huo mkubwa wa kuimarisha sekta ya kilimo uliochini ya IFAD.

Nae Rais Karume kwa upande wake alimueleza Kiongozi huyo kuwa amefarajika kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi za Mfuko huo za kuimarisha kilimo Zanzibar.

Rais Karume alimueleza Nwanze kuwa hatua hiyo ya kuunga mkono vikundi vya akinamama vya kuimarisha kilimo Zanzibar ni jambo la busara kwa maendeleo ya wanawake na taifa kwa jumla.
 
Alieleza kuwa kumsaidia mwanamke ni hatua nzuri na jambo kubwa katika jamii na kusisitiza kuwa unapomuelimisha mwanamke mmoja na kumjengea uwezo ni sawa na kuielimisha jamii.
 
Alisema kuwa kutokana na Zanzibar kutegemea kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii ni jambo la busara iwapo sekta ya kilimo itapewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika sekta ya utalii.

Rais Karume alieleza haja ya kuwajengea uwezo wakulima kwa kuwapa elimu itakayowasaidia katika kuimarisha sekta ya kilimo na kusisitiza kuwa sekta hiyo pia imekuwa ni mkombozi katika suala zima la ajira.

Rais Karume alimueleza kiongozi huyo hasara kubwa inayofanywa na wadudu hao na kumtaka kusaidia katika kupambana nao.
 
Aidha, Rais Karume alieleza kufarajika kwake na azma ya IFAD ya kuunga mkono na kuongeza nguvu kwa kikundi cha kijamii katika suala zima la utafiti juu ya kuua wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo.
 
Katika mazungumzo yake Rais Karume alieleza kuwa umefika wakati wa kuweka mikakati madhubuti juu ya kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kutafuta njia juu ya maendeleo ya sekta hiyo.

Sambamba na hayo, Rais Karume alisema kuwa ipo haja katika kukuza sekta hiyo ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wakulima wadogo kwa kuwajengea uwezo wa kifedha pamoja na masoko na hivyo kutoa wito kwa mabenki kuekeza katika sekta hiyo.
 
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa IFAD Tanzania, Dk. Mwatima Juma alieleza kuwa mradi huo mkubwa pia utasaidia miundombinu ya kilimo, ukuzaji wa uwezo wa kifedha kwa vikundi vya kilimo pamoja na kuunga mkono mikakati megine ya kilimo Zanzibar.

Dk. Mwatima alieleza hatua za IFAD za kushirikiana na wananchi katika utafiti wa kutumia viungo kwa ajili ya kutengenezea dawa ya wadudu waharibifu wa mazao ya kilimo wakiwemo inzi.

Uandikishaji wapiga kura

AFISA wa Uandikishaji katika daftari la kudumu akimuongoza kijana aliyefika kujiandikisha katika kituo cha kupigia kura huko Makunduchi. (Picha na Othman Maulid).

‘Mafanikio dhidi ya Malaria yasiifanye jamii kubweteka’

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk, Mohammed Saleh Jiddawi amesema Zanzibar imepiga hatua nzuri katika mapambano dhidi ya Malaria na juhudi zaidi zinaendelea kuhakikisha mkakati wa kumaliza maradhi hayo unafanikiwa.

Kauli hiyo aliitoa jana kwenye ukumbi wa Hoteli ya Chavda Shangani mjini hapa, wakati akifungua mkutano wa sita wa majadiliano ya hali ya Malaria pamoja na mkakati wa kumaliza Malaria Zanzibar.

 
Alisema jitihada za pamoja kati ya serikali, wananchi na washirika wa maendeleo zimewezesha kwa kiasi kikubwa Malaria kupungua.

Dk. Jidawi amewataka wananchi kutobweteka na mafanikio hayo, badala yake waendelee kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa pamoja na kukubali kupigiwa dawa kwenye nyumba zao kufika kwenye vituo vya afya kupatiwa tiba sahihi ya Malaria mara watakapoona dalili za ugonjwa huo.
 
Nae Mratibu wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria PMI, Tim Ziemer, alisema Serikali ya Marekani kupitia mfuko wa Rais utaendeleza jitihada zake za kuipatia fedha Zanzibar katika mapambano dhidi ya Malaria ili kufikia lengo la kumaliza ugonjwa huo.
 
Alisema kwa sasa Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa ya mapambano dhidi ya Malaria na kinachohitajika ni kuongeza nguvu za kitaalamu na utoaji wa elimu kwa wananchi ili maradhi hayo yaondoke kabisa nchini.

Aidha amevitaka vyombo vya habari kusaidia katika utoaji wa elimu juu ya mapombano hayo.

Katika mkutano huo, mada mbali mbali zilijadiliwa ikiwemo sualala kuwabakisha watu tabia yaani BCC, ushughulikiaji wa mwenendo wa Maradhi, masuala ya upigaji dawa pamoja na matumizi ya vyandarua.
Alisema suala la maradhi hayo kwa sasa limedhibitiwa kwa kiasi kikubwa haPA Zanzibar, ambapo wananchi wameweza kuelewa athari zinazopatikana kutokana na ugonjwa huo.
Na Fatma Kassim, Maelezo
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete akifungua mkutano wa kimataifa unaozungumzia uchumi katika hoteli ya Moevenpick Royal Palm. (Picha na Ramadhan Othman). 

Kampuni ya C-Weed yawapa sare watoto 95 Kidoti

Na Halima Abdalla
ZAIDI ya watoto 95 waliocha masomo katika skuli ya Kidoti, wamepatoa misada ya sare na vifaa mbali mbali kutoka kampuni ya C-Weed Corporation.

Wanafunzi hao waliacha skuli kutokana na kutokuwa na huduma muhimu kwa ajili ya masomo yao pamoja na kuishi kwenye mazingira magumu.

Kampuni hiyo imetoa msaada wa sare kwa wanafunzi 95 zenye thamani ya shilingi 712,000 kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao wanaoishi mazingira magumu na waweze kurejea skuli.

Akizungumza katika ghafla ya makibidhiano yaliyofanyika Shehia ya Kidoti, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, mshauri wa Kampuni ya Mwani C-Weed Corporation, Makame Nassor Salum, alisema msaada huo ni utekelezaji wa sera ya kampuni yake.

Alisema fedha hizo zimetokana na kutoa shilingi tano kwa kila kilo moja ya mwani wanaoununua kutoka kwa wakulima ili kusaidia jamii.

“Sera ya kampuni yetu ni kutumia kutoa shilingi tano ya kila kilo ya mwani tunaoununua kutoka kwa wakulima na fedha hiyo hutumika kuisaidia jamii”,alisema Salum.

Alisema fedha hizo ni muhimu katika kusaidia na kuharakisha harakati za maendeleo vijijini, huku akibainisha kuwa utekelezaji wa sera hiyo ni kwa vijiji vyote wanavyonunua mwani Unguja na Pemba.

Sambamba na hayo, alisema kwa mwaka huu kampuni hiyo imepandisha bei ya mwani mara tatu na ikilinganisha na kampuni nyengine zinazouza bei ya shilingi 180.
 
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’,Riziki Juma Simai ,alishukuruku Kapuni ya C-Weed Corporation kwa kuweka shilingi tano kwa kusaidia jamii na kuziomba Kampuni nyengine kuiga mfano huo.

Alisema Kampuni nyengine hazina utamaduni huo hivyo kampuni hii inahitaji kupewa pongezi na kujali maendeleo ya vijiji.

Aidha aliwashauri wakulima hao wa mwani kujitahidi kuzalisha mwani ili soko liweze kukua na kuimarika.

Mkutano wa Uchumi

WAZIRI wa Nchi anayeshughulikiwa Fedha na Uchumi Dk. Mwanyihaji Makame (kushoto), akiwa kwenye mkutano wa unazungumzia masuala ya uchumi katika hoteli ya Moevenpick Royal Palm mjini Dar-es-Salaam, kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo na  Mazingira, Khalid Mohammed.

Tuesday 4 May 2010

ZSSF yasisitiza kulipa michango ni lazima

IMESISITIZWA kuwa, suala la kujisajili kwa waajiri na waajiriwa katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) si la hiyari bali ni lazima kwa lengo la kustawisha hali za wafanyakazi nchini.
 
Hayo yamesemwa na Mwanasheria wa Mfuko huo Ramadhan Juma Suleiman alipokuwa akitoa mada katika mkutano kati ya uogozi wa ZSSF na waajiri kutoka taasisi mbalimbali nchini uliofanyika kwenye ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani juzi.
 
Mwanasheria huyo alisema kila mwajiri anapaswa kujisajili ndani ya siku 14 kutoka siku aliyoanza kuendesha mradi wake, pamoja na kuwasajili waajiriwa kwa kipindi kama hicho kuanzia siku ya uajiri wao.
 
Suleiman alieleza kuwa kushindwa kufanya hivyo, ni kosa la jinai ambalo adhabu yake ni faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha mwaka mmoja jela au zote mbili kwa pamoja.
 
Kuhusu uwasilishaji michango katika ofisi za ZSSF, mwanasheria huyo alisema kwa mujibu wa sheria, mwajiri anawajibika kupeleka asilimia tano ya mshahara wa mwajiriwa na kuunganisha na mchango wake wa asilimia 10 ndani ya siku 14 pia.
 
Alifahamisha kuwa iwapo mwajiri atakwepa kutimiza wajibu wake, atahesabika amefanya kosa na hivyo atalazimika kulipa kiasi kama hicho pamoja na adhabu.

Makosa mengine ambayo alisema yanaweza kufanywa na mwajiri ni kukata asilimia tano ya mfanyakazi lakini akashindwa kuiwasilisha katika mfuko, pamoja na kukata au kuchukua chini ya kiwango kinachostahili kisheia.

Alisema kila mwajiriwa ambaye ni mwanachama wa ZSSF anayo haki ya kufuatilia katika ofisi za mfuko zilizoko Kilimani mjini Zanzibar ili kuhakikisha kama mwajiri wake anatimiza wajibu wa kuwasilisha michango hiyo.
 
“Kwa kuwa serikali imeridhia kuanzishwa kwa mfuko huu kwa nia njema kama zilivyo nchi nyengine, ni wajibu wa waajiri kufuata sheria ili kusaidia jitihada za kuwajengea wafanyakazi wetu mazingira mazuri ya kuishi pale muda wao wa kustaafu unapofika”, alifahamisha mwanasheria huyo.
 
Alisema pamoja na kufahamu ulazima wa kuchangia mfuko huo, baadhi ya waajiri wamekuwa wagumu kutekeleza wajibu wao, jambo linalolazimisha kuwepo na misuguano katika kuwafanya wafuate sheria ikiwa pamoja na kufikishana mahakamani.

Mapema akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Abdulwakil Haji Hafidh alisema, hifadhi ya jamii inalenga kuendeleza kipato cha mtu pale ajira yake inapokoma kwa sababu mbalimbali ikiwemo kustaafu, ugonjwa, ajali, uzee pamoja na kifo.

Alisema ni haki ya msingi kwa kila mwananchi kuwa na hifadhi itakayomuhakikishia maisha mazuri anapokuwa nje ya ajira au kuwafaa warithi wake wakati maisha yake yatakapofikia hatima.
 
Hata hivyo alieleza kuwa imeonekana iko haja kuifanyia marekebisho sheria namba mbili iliyoanzisha mfuko huo ya mwaka 1998 ambayo ilifanyiwa mapitio makubwa na kuundwa upya mwaka 2005.
 
Alisema kwa mujibu wa ripoti ya mapitio ya matumizi ya hifadhi ya jamii na bajeti iliyotokana na mradi wa ILO-DFID, imeazimiwa kuleta mageuzi ya dhati kwa sekta ya hifadhi kwa kupanua wigo wake.

Hafidh alifahamisha kuwa miongoni mwa mapendekezo ya ripoti hiyo ni pamoja na kuufanya mfumo wa hifadhi ya jamii uwe wa wote ikizingatiwa kuwa wigo wa sekta hiyo ni mdogo ambapo hapa Zanzibar ni asilimia 6.6 tu ya watu wake ndio wenye hifadhi ya jamii.

Kutokana na tafiti kuonesha changamoto nyingi zinazoukabili mfumo wa hifadhi, alisema Bodi ya Wadhamini imeona iko haja ya kupata maoni na ushauri wa wanachama na wadau wengine ili kuufanyia marekebisho yatakayokidhi haja kulingana na mahitaji ya wakati uliopo.
 
Wanachama waliohudhuria mkutano huo walitoa mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuleta ufanisi kwa mfuko huo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa jumla.
 
Walitaka baadhi ya mambo ambayo yameonekana kuwa yanaleta urasimu yafutwe au kufanyiwa muundo mpya utakaowanufaisha waajiri na waajirwa kwa pamoja.
Na Salum Vuai, Maelezo

Kilelel cha siku ya Uhuru wa Habari duniani

MKUU wa Mkoa Kusini Pemba Juma Kassim Tindwa (kulia), akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani kwenye kilele cha sherehe za siku ya Uhuru wa Habari Duniani.

Wapiga kura 67,789 waandikishwa awamu ya pili Pemba

ZOEZI la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili limemalizika katika wilaya zote nne kisiwani Pemba baada ya kufanyika kwa muda wa siku 63 kwa majimbo yote 21.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Msaidizi Afisa wa Uandikishaji Pemba, Ali Mohammed Dadi, alisema katika zoezi hilo jumla ya wapigakura wapatao 67,789 wameandikishwa .

Dadi alisema katika zoezi hilo wanawake wapatao37,002 na wanaume wapatao 30,787 walijitokeza katika shehia zao kwa kujiandikisha katika daftari hilo, jambo ambalo litawawezesha kutumia demokrasia yao wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
 
Akizitaja takwimu hizo kiwilaya afisa huyo alisema wilaya ya Wete jumla ya wapiga kura 27,080 wakiwemo wanawake 14,650 na wanaume 12,430 wakati katika wilaya ya Chake Chake, jumla ya wapiga kura 18,227, wakiwemo wanaume 8,177 na wanawake 10,050 walijiandikisha kwa awamu hiyo.
 
Wilaya ya Mkoani jumla ya wapiga kura 17,813 walijitokeza kujiandikisha katika zoezi hilo wakiwemo wanawake 9,768 na wanaume 8,045 na wilya ya Micheweni jumla ya wapiga kura wapatao 4,669 wakiwemo wanawake 2,534 na wanaume 2,135 walijiandikisha katika zoezi hilo la awamu ya pili.
 
Alieleza katika zoezi hilo lililoanza Machi 1 na kumalizika Me 2, akinamama wameonekana kujiandikisha kwa wingi kuliko wanaume na kufikia asilimia 54.6.
 
Dadi alisema pamoja na malalamiko ya hapa na pale lakini hakupata barua yoyote katika ofisi yake inayo lalamikia zoezi hilo la awamu ya pili.
 
Hivyo amewataka wale wote waliondikishwa katika daftari hilo, kutunza risiti zao jambo ambalo litawapa urahisi wakati wa kuchukua vitambulisho vyao.
Na Bakar Mussa, Pemba

Masheha Kusini toweni ushirikiano kukabili uhalifu-Polisi

Na Fauzia Muhammed
MASHEHA wa katika Mkoa wa Kusini Unguja wametakiwa kutoa ushirikiano wa kuwabaini wageni wanaoingia katika shehia zao ili kuhakkisha masuala ya uhalifu yanapigwa vita.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa upelelezi ya makosa ya jinai Mkoa wa kusini Unguja Makarani Khamis alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Mwera.

Makarani alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza matukio ya uhalifu yanayongezeka kila kukicha kwenye shehia na mitaa mbali mbali.

Aidha, Makarani alifahamisha kuwa pamoja na ulinzi wa doria ulioanza kwenye vijiji mbali mbali, pia ipo haja kwa masheha kuwa waangalifu kuhusu wageni wanaoingia kwenye shehia zao ili kudhibiti uhalifu.
 
Makarani alizitaja sehemu hizo ambazo zimeshaanza kupata huduma ya ulinzi wa doria kuwa ni Hawaii na Mwera Mtofani.
 
Vile vile alieleza kuwa polisi wamejianda kufanya msako wa mara kwa mara, ndani ya mwezi mmoja ili kuhakikisha uhalifu unapungua ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
 
Hivyo, Makarani amewataka wananchi wema kuendelea kutoa taarifa na ushirikiano katika sehem zinazo husika ili kuhakikisha uhalifu unapungua zaidi katika Mkoa huo.