Monday, 25 July 2011

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akiweka ngao katika Mnara ya Kumbukumbu ya Mashujaa Mkoani Mtwara, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Mashujaa Tanzania.(Picha na Ramadhani Othman ) 

JK AONGOZA WATANZANIA KUKUMBUKA MASHAJAA

JK aongoza Watanzania kukumbuka mashujaa

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amewaongoza maelfu ya wananchi na viongozi mbali mbali wa kitaifa, akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya Mashujaa.
Maadhimisho hayo yamefanyika jana katika viwanja vya Naliendele Mjini Mtwara eneo ambalo pana makaburi ya mashujaa waliopigana vita vya Msumbiji.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Waziri wa Ulinzi na Majeshi ya Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, Philipe Nyasi.
Wengine ni Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar, Ramadhan Haji, baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Wakuu wa vikosi vya Ulinzi wa Tanzania na Msumbiji, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania, Majenerali wastaafu waliopigana vita vya Msumbiji pamoja na vita vya dunia na viongozi wengineo.
Katika maadhimisho hayo kama ilivyo kawaida baadhi ya viongozi akiwemo Rais Kikwete waliweka silaha za asili ambapo kwa uande wake aliweka Mkuki na Ngao, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange aliweka sime, Kiongozi wa Mabalozi, Balozi wa DRC, Balozi Juma Khalfan aliweka shada la maua ambapo Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mstahiki Suleiman Mtalika aliweka upinde na mshale.
Baada ya tukio hilo dua na sala kutoka kwa viongozi wa Dini zilizomwa ambapo Sheikh Jamaldin alisoma dua kwa upande wa Waislamu, Mchungaji Lucas Mendule aliwakilisha Kanisa la CCT na Kanisa Katoliki liliwakilishwa na Padri Gabriel Mule.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na baadhi ya viongozi wengine wakuu walitembelea makaburi ya mashujaa hao na baadae kuwasalimia wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, ambapo katika salamu zake Rais Kikwete alieleza kuwa kila mwaka Taifa limekuwa na utaratibu wa kuhifadhi kumbukumbu za mashujaa na kutoa pongezi kwa wananchi wengi kujitokeza katika maadhimisho hayo.
Rais Kikwete alisema kuwa kabla ya sherehe hizo kufanywa tarehe hiyo ya jana hapo mwanzo zilikuwa zikifanyika Septemba mosi kutokana na kumbukumbu za kuwapokea Majeshi kwa ushindi walioupata huko nchini Uganda.
Alisema kuwa hivi sasa kila ifikipo tarehe 25 husherehekea maisha ya wakombozi hao kutokana na juhudi kubwa walizozifanya katika kuikomboa nchi ya Msumbiji na sio kusherehekea kufa kwao.
Akieleza historia ya mashujaa hao kwa ufupi, Rais Kikwete alisema kuwa wanajeshi wa Tanzania waliokufa nchini Masumbiji katika jitihada za kuikomboa nchi hiyo kutoka kwa Wakoloni wa Kireno.
Alieleza kuwa Tanzania ilitoa msaada mkubwa katika vita hivyo kutokana na kiongozi wa FRELIMO wakati huo hayati Samora Mashel kumuomba hayati Mwalimu Nyerere kusaidiwa mafunzo na hatimae Majeshi ambapo pia, baada ya ukombozi huo kulitokea watu wachache waliokuwa hawakufurahishwa na ukombozi huo na ndipo walipowatumia waasi wa RENAMO na kuanzisha vita vingine.
Alieleza kuwa katika mapambano ambapo hatimae walisambaratishwa na Majeshi ya Msumbiji kwa mashirikiano na Majeshi ya Tanzania na ndipo baadhi ya wanajeshi wa Tanzania walipoteza maisha katika vita hivyo.
Aidha, alieleza kuwa Mashujaa hao awali walizikwa nchini Msumbiji na baadae ndipo ikaamuliwa kuzikwa katika eneo hilo ambapo pia, alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa Jeshi la Tanzania kwa kuwawekea mazingira mazuri mashujaa hao.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapainduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa wananchi wa Mtwara kwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kuwapa salamu za wananchi wa Zanzibar.
Nae Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji alieleza kuwa uhuru wa Msumbiji ulitokana na damu za Mashujaa hao na kupelekea nchini yao hivi sasa kuendelea kuwa na amani na utulivu mkubwa.
Baada ya hapo viongozi hao wakuu kwa pamoja pamoja na viongozi wengine wakiongozwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete walitembelea nyumba ya Makumbusho ya Naliendele iliyopo katika eneo hilo ambapo mna vifaa mbali mbali vilivyotumiwa na mashujaa hao katika ukumbozi wa Msumbiji. Katika maadhimisho hayo mizinga ilipigwa pamoja na wimbo wa Taifa sambamba na kutolewa salamu za Rais.

WANAHABARI WATAKIWA KUWAUNGANISHA WA ZANZIBARI.

Wanahabari watakiwa kuwaunganisha Wazanzibari

Na Mwandishi Wetu
VYOMBO vya habari vina wajibu wa kuwaunganisha wananchi Zanzibar, umuhimu wa kuwa na serikali ya Umoja wa Kitaifa, hasa baada ya wananchi hao kupita katika kipindi kigumu na cha muda mrefu cha hitilafu za maelewano zilizotokana na hali ya siasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alieleza hayo jana alipokuwa akitoa mada kwenye warsha ya siku mbili inayoelezea nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha serikali ya Umoja wa kitaifa.
Mhadhiri huyo alisema kihistoria Zanzibar imepitia katika mkondo mrefu wa wa kuhitilafiana kisiasa, hali ambayo imezikwa na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa baina ya vyama vya CUF na CCM.
Alifahamisha kuwa baada ya kupatikana kwa serikali ya Mapindui ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, ambayo imekuwa msingi imara wa utengamano baina ya Wazanzibari hivi sasa umefika wakati wa kuzienzi na kuzitunza tunu za taifa.
Alizitaja tunu hizo ambazo hazijawekwa katika utaratibu mzuri na baadhi yao zinahitaji kufanyiwa mapitio ni pamoja na amani, umoja,, uzalendo, mshikamano, usawa, haki, muungano, uvumilivu katika dini, rangi na siasa.
Muwezeshaji huyo alisema jamii ipaswa kuelimishwa kwa undani umuhimu wa tunu hizo ambazo zina umuhimu mkubwa katika kujiletea maendeleo, na kueleza kuwa kazi hiyo inaweza kufanywa kwa usahihi na vyombo vya habari.
Kwa upande wake Rashid Omar Kombo ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Habari Zanzibar, akiwasilisha mada katika warsha hiyo alisema vyombo vya habari vinawajibu wa kuitathmini hali ya utawala bora kwa kutumia viashiria vilivyopo hasa wakati huu ambapo Zanzibar ina serikali ya umoja wa Kitaifa.
Alisema utawala bora una mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya nchi yoyote sambamba na upatikanaji wa haki za msingi ambazo kila mwanadamu anatarajiwa kuzipata bila ya kuwepo mizengwe yeyote.
Wakichangia washiriki wa warsha hiyo walipendekeza uwepo uwajibikaji wa vyombo vya habari katika kutoa taarifa sahihi kwa wasikilizaji, wasomaji na watazamaji wa vyombo vyao na kutaka uweledi utumike ili kuepusha kuandika habari zinazoweza kusababisha mifarakano katika jamii.
Awali akifungua warsha hiyo waziri wa Biashara na Viwanda, Nassor Ahmed Mazrui, kwa niaba ya waziri wa Habari, Utamaduni Utalii na Michezo, Abdilahi Jihad Hassan, alivitaka vyombo vya habari viandike habari zao kwa misingi ya uweledi ili kuepuka kuwa msingi wa mitafaruku katika jamii.
Waziri huyo alisema umefika wakati wananchi kuelimishwa na kuzielewa tunu za taifa ikiwemo Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, ambayo ndiyo yaliyomkomboa kila Mzanzibari.
Waziri Jihad Hassan alivitaka vyombo hivyo viandike habari zao kwa misingi ya uweledi ili kuepuka kuwa msingi wa mitafaruku katika jamii na kueleza kuwa Zanzibar tuitakayo inaweza kujengwa na wazanzibari wenyewe.
Warsha hiyo ya siku mbili inawashirikisha waandishi wa habari, watendaji wa vyama vya siasa pamoja na taasisi za kiraia, na imeandaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET).
WANAFUNZI wa kidatu cha Nne wsakifanya mitihani yao ya taifa ya majaribio wakiungana na Wanafunzi wato Tanzania, wakiwa katika chumba cha mitihani wakifanya mitihani jana.(Picha na Othman Maulid)

ATEKWA NYARA KWA KUTAKA KUUZA MCHELE BEI NAFUU.

Atekwa nyara kwa kutaka kuuza mchele bei nafuu

• SMZ yawakoromea wafanyabiashara wanyanyasaji
• Yahamasisha wote wenye uwezo kuagiza bidhaa
Na Abdi Shamnah, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wafanyabiashara wenye uwezo wa kuleta bidhaa mbali mbali nchini, kufanya hivyo na kusema Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano.
Maalim Seif, ambae pia ni Katibu Mkuu wa CUF, amesema hayo jana kwa nyakati tofauti alipozungumza na wananchi wa majimbo ya Matemwe na Chaani, kufuatia ziara zake za kuyatembelea Majimbo yote Unguja na Pemba kuonana na wajumbe wa CUF pamoja na kuzungumza na wananchi.
Amesema wakati huu wananchi wakilalamika kupanda kwa gharama za maisha kutokana na ongezeko la bei za bidhaa, kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaopinga hatua ya wafanyabiashara wengine kuleta bidhaa ikiwemo mchele kwa hofu ya bidhaa hizo kuteremka bei.
Alisema katika tukio la hivi karibuni kuna mfanyabiashara (hakumtaja jina) aliedhamiria kuleta mchele na kuuza kwa bei ya chini, lakini wamejitokeza baadhi ya wafanyabiashara wanaomtishia maisha kupitia meseji za simu, ili aondokane na dhamira hizo.
Bila kufafanua kwa undani, Maalim Seif alisema taarifa zilizopo ni kuwa mfanyabaishara huyo ametekwa nyara.
Alisema wafanyabiashara hao wanafanya hivyo kwa kuamini kuwa pale mfanyabiashara huyo atakapoleta bidhaa hizo na kuuza kwa bei nafuu, watalazimika kupunguza bei za bidhaa zao au zitawaozea madukani.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashirikiana na wafanyabiashara wote wenye dhamira ya kuwaondolea wananchi dhiki ya maisha inayotokana na kupanda kwa gharama za bidhaa pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo visivyokubalika na jamii.
Maalim Seif aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imedhamiria kunyanyua kipato chao kupitia mazao ya biashara, ikiwemo mwani ambao hivi sasa umekuwa ukiuzwa kwa bei ya chini mno.
Alisema Serikali imeipa Wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko jukumu la kuhakikisha bei ya zao hilo inapanda kama ilivyo kwa karafuu, na kubainisha changamoto iliyopo, kufuatia zao kutokuwa mikononi mwa Serikali.
Alisema hali ya bei ya zao hilo hivi sasa hairidhishi, kwani wakulima hulipwa wastani wa shilingi 400/- tu kwa kilo, wakati bei katika soko la dunia ni zaidi ya shilingi 2,500/-.
Aliwatupia lawama wafanyabiashara (matajiri) wanaojishughulisha na ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima, kwa kuwakandamiza kwa makusudi wakulima na kutoa visingizio vya uongo vya kupanda kwa gharama za uendeshaji.
Alisema tayari kuna taarifa zinazoonesha nia ya kuja kwa makampuni yenye lengo la kupandisha bei ya zao hilo na hivyo kutoa ushindani katika soko la ndani ya zao hilo.
Aliweka wazi kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha bei ya zao hilo inapanda kutoka shilingi 400/- hadi kufikia shilingi 1,000/- kwa kilo, hatua aliyosema itamuwezesha mkulima kunufaika kutokana na jasho lake.
Katika hatua nyengine Maalim Seif aliwahakikishia wananchi wa Majimbo hayo kuwa Serikali imekusudia kulivalia njuga na kulizamaliza kabisa tatizo la ukosefu wa maji safi na salama, ndani ya kipindi cha miaka mitatu, kupitia bajeti yake ya kila mwaka.
Vile vile Maalim Seif alitumia fursa ya kukutana na wananchi hao kuwaeleza azma za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Bungeni mswada wa kuundwa kwa katiba mpya, hivyo aliwataka kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao bila woga, pale Tume itakapopita kukusanya maoni.
Aliwataka wananchi hao kutoa mawazo yao juu ya aina gani ya Muungano wanaoutaka na mambo mbali mbali yaliyomo ndani ya Muungano huo, ili hatimae Tanzania iweze kuwa na Katiba nzuri yenye maslahi kwa pande zote mbili za Muungano huo.

NEC - CCM ZANZIBAR YATANGAZA SAFU MPYA.

NEC-CCM Zanzibar yatangaza safu mpya

Na Mwanajuma Abdi
KAMATI Maluum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar, imewateuwa wajumbe wapya wa sekretarieti ya Kamati hiyo pamoja na kupitia majina 21 ya UVCCM wanaowania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, oOisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Itikadi na Uenezi Zanzibar, Issa Haji Ussi, amesema wajumbe hao wameteuliwa baada ya kufanyika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Jumapili Ofisi hiyo mjini hapa, chini ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume.
Alisema walioteuliwa kushika nyadhifa za wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar ambao wataongoza katika Idara mbali mbali ni Machano Othman Said ameteuliwa kuwa katibu Kamati Maalum ya NEC- Organaizesheni, ambapo awali alikuwa ni Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) nafasi ambayo kwa sasa itashikiliwa na Haroun Ali Suleiman.
Alieleza wajumbe wengine walioteuliwa ni Issa Haji Ussi atakuwa ni Katibu wa Kamati Maalum ya NEC- Itikadi na Uenezi, ambapo nafasi hiyo awali ilikuwa ikishikiliwa na Vuai Ali Vuai ambae ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar na Mansoor Yussuf Himid ataendelea kuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Uchumi na Fedha kwa chama hicho.
Aidha aliongeza, kikao hicho kilijadili majina 21 ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) waliojitokeza kuomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja huo, ambapo mapendekezo ya kamati hiyo yametolewa.
"Jumla ya wanachama 21 wa UVCCM wamejitokeza kuomba kugombea nafasi hiyo kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Hamad Masauni Yussuf mnamo Mei 18, mwaka jana", alisema Issa.
Alifafanua kuwa, kati ya majina hayo 19 ni vijana kutoka Zanzibar na wawili kutoka Tanzania Bara, ambapo alisisitiza kwa mujibu wa utaratibu na kanuni za UVCCM kwamba Makamu Mwenyekiti akitokea Tanzania, lazima Mwenyekiti awe Mzanzibari hivyo majina hayo mawili yatakuwa hayawezi kufuzu katika mchujo hapo baadae.
Alisema tayari kanuni zishawekwa haziwezi kuvunjwa, ambapo wagombea hao wawili wa Tanzania Bara wametumia haki yao ya kidemokrasia lakini wamekiuka kanuni.
Hata hivyo, Issa alikanusha kuchukuwa fomu ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM, ambapo alisisitiza kwa waandishi waamini kauli yake na sio kusikia maneno pembeni.
Alieleza kwamba, CCM ni chama kikubwa chenye wanachama wengi, kimbilio la wanyonge, kinaheshimika na kinafuata misingi ya kidemokrasia, ambapo alihahakisha ushindi mkubwa wa kishindo utapatikana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Alisema Kamati Maalum ilimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010-2015, pamoja na ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi kuanza kuzitekeleza kwa vitendo.
Aliendelea kusema, hatua zinazochukuliwa na Dk. Shein zina lengo la kuinua hali za wananchi wa Unguja na Pemba za kuwapunguzia mzigo wa maisha ili kufanikisha lengo la kupunguza umasikini, ambapo miongoni mwa hatua hizo ni kuongeza mishahara ya watumishi wa Serikali kwa asilimia 25, kupandisha bei ya karafuu kutoka shilingi 5,000 hadi shilingi 10,000 kwa kilo moja ya daraja la kwanza na shilingi 9,500 kwa daraja la pili.
Issa alifahamisha kuwa, Serikali imeelekeza nguvu katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutumia kauli mbiu ya 'Mapinduzi ya kilimo' kwa kupunguza bei ya pembejeo za kilimo na gharama za matrekta, ambapo kwa polo moja la mbolea ya TSP itauzwa kwa shilingi 16,000 badala ya shilingi 32,000 na mbolea ya UREA ni shilingi 10,000 badala ya 20,000, punguzo hili ni la asilimia 50 pamoja na mbegu ya mpunga itauzwa kwa shilingi 10,000 kwa kilo badala ya shilingi 25,000.
Hata hivyo, alieleza Serikali imepunguza kwa asilimia 75 bei ya kuchimbua na kuburuga mashamba kwa kutumia trekta kutoka shilingi 32,000 kwa eka hapo mwanzo na sasa ni shilingi 16,000 kwa eka, sambamba na kupunguzwa kwa bei ya dawa ya kuua magugu kutoka shilingi 12,500 kwa lita hadi shilingi 6,000 ikiwa ni punguzo la asilimia 52.
Alisema kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Zanzibar imeridhiswa na hatua zilizofikiwa na Serikali, ikiwemo utekelezaji wa vitendo wa ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Dira ya maendeleo ya 2020 na mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar wa mwaka 2010-2015 (MKUZA II).

WANAOTELEKEZA WATOTO WADHIIBITIWE.

Wanaotelekeza watoto wadhibitiwe

Na Halima Abdalla
BAADHI ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesikitishwa na kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa watoto na wanawake kutelekezwa vinavyofanywa na baadhi ya akinababa.
Waliishauri Serikali kuweka sheria kali na nzito kwa yeyote atakaepatikana na hatia hiyo kupewa adhabu nzito na itangazwe katika vyombo vya habari ili kuweza kutoa somo kwa wabakaji wengine.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, wanawake na Watoto, Asha Bakari Makame, aliishauri Serikali kuweka sheria kali kwa wanaume wanaofanya kazi Serikalini ambao wanatelekeza wanawake na watoto kuwakata kima cha mshahara wao kila mwezi ili aweze kupewa mwanamke kiweze kumsaidia yeye na mtoto wake.
Alisema wanawake sasa hivi wamekazana kwa kujishughulisha shughuli mbali mbali za kujipatia kipato, lakini wamekuwa wakirudi nyuma kutokana na kutelekezwa na akinababa kwa kuwaachia familia bila ya kuwashughulikia.
Sambamba na hayo aliwashauri kinababa kuwaonea huruma kinamama kutokana na kazi ngumu wanazozifanya pamoja na kuangalia familia na kazi nzito zinazowakabili.
Nae Mtumwa Kheir Mbarouk (Nafasi za wanawake ) aliwataka kinababa kuwa na imani kuacha kuwaharibu watoto wadogo walemavu na mataahira kwani vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Sambamba na hayo aliwashauri wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa vitendo hivyo kutokubali kuyamaliza mitaani, ila wayafikishe katika vyombo husika pamoja na mahakama zisichelewe kesi hizo pamoja na kutoa hukumu.
Aisha alimshauri Wizara ya Ustawi wa jamii kuelimisha wananchi kuwa wanapofanyiwa vitendo hivyo vya ubakaji wasifiche kwani wanaofanyiwa vitendo hivyo ni masikini na wenye uelewa mdogo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Micheweni, Subeit Khamis Faki aliishauri Wizara hiyo kubuni miradi mbali mbali ya kuweza kusaidia kuajiri vijana ili kuondokana na watoto wa mitaani kwani ajira za utotoni hazifanywi kwa maksudi ila hali hiyo inatokana na hali za wazee wao kuwa ngumu na yeye ili apate kuishi.
''Hawa watoto hawafanyi kwa hiari yao wanafanya kwa lazima ili waweze kupata chakula cha kuwasaidia ili waweze kuendelea kuishi,''alisema Subeit.
Aidha alishauri Serikali kuwasaidia vijana waliopo katika wilaya ya Micheweni kwa sababu inaongoza kwa ajira za utotoni pamoja na umasikini kwa kuweza kuwatembelea na kuwapatia elimu sambamba na kuwasaidia ili kuondokana na umasikini.
Nae panya Ali Abdalla (Nafasi ya wanawake) alizishauri mahkama kuacha kuwasumbua wanawake wanapofuatilia kesi za ubakaji mahkamani kutokana na nenda rudi za kila siku ambazo zinasababisha wanawake kukata tamaa na kupelekea kesi hizo kushindwa kuendelea.
Kwa upande wake Viwe Khamis Abdalla (Nafasi ya wanawake) aliishauri akinamama wanaojifungua kuacha kutelekeza watoto kwa kuwatupa aliishauri Serikali kuchukuliwa hatua kali wanawake hao kwani wanachofanya ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Saturday, 23 July 2011

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumina Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee akitiliana saini na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen Qinman, msaada wa kuwawezesha Watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata mafunzo nchini China, utiaji saini huo umefanyika ukumbi wa Wizara ya Fedha Vuga Mjini Zanzibar (Picha na Othman Maulid)   

MAOFISA SMZ KUPIGWA MSASA CHINA.

Maofisa SMZ kupigwa msasa China

Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetilia saini na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China mkataba wa msaada wa kuwajengea uwezo watendaji wa SMZ utaogharimu zaidi ya dola za Marekani 507,000.
Utiaji saini huo umefanyika jana, katika ukumbi wa wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, ambapo Waziri wa Wizara hiyo, Omar Yusssuf Mzee aliiwakilisha SMZ na Serikali ya China imewakilishwa na Balozi Mdogo wa China aliyopo Zanzibar, Chen Qinman.
Waziri Omar alisema msaada huo ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kimafunzo watendaji wa Serikali, ambapo watakwenda nchini China kwa awamu tofauti kuanzia mwezi Augosti, Novemba na kundi la mwisho Februari mwakani.
Alieleza mafunzo hayo yatayochukuwa karibu siku tisa hadi 10 nchini China yatawajumuisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa SMZ, Wenyeviti wa Kamati wa Baraza la Wawakilishi, baadhi ya wakuu wa wilaya, baadhi ya watendaji wa Halmashauri na maofisa Wadhamini.
Alifahamisha kuwa, programu za mafunzo hayo yatajumuisha mapinduzi ya uvuvi, ambao utajumuisha mafunzo katika ufugaji wa samaki baharini, ufugaji wa chanza, kamba, kilimo cha umwagiliaji maji, elimu na miundombinu na mawasiliano.
Nae Balozi Mdogo wa China, aliyekuwepo Zanzibar alisema wamekuwa na uhusaino wa muda mrefu katika nyanja mbali mbali katika kasi ya kukuza uchumi wa nchi.
Alieleza mwaka jana, China iliwapeleka katika mafunzo Wazanzibari 50, ambapo mwaka huu watawapeleka zaidi ya 200 ili kujifunza masuala mbali mbali hususani katika kilimo, uvuvi, elimu na mawasiliano.
Katika hatua nyengine Balozi Chen alimueleza Waziri Omar kwamba China inakusudia kuijenga upya ICU ya hospitali kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na kuwapatia madaktari mafunzo kwa ajili ya kuiendesha, sambamba na kuleta vifaa ili iweze kufafanana na za kimataifa.
Nae Waziri Omar alishukuru kwa hatua hiyo Serikali ya China kutaka kuleta wataalamu wake ili waje kufanya tathmini katika ICU na baadae kujengwa upya, ambapo aliwataka wananchi kuwa wastahamilivu maendeleo makubwa yatafanyika nchini katika huduma za kiafya na kukuza uchumi na kupunguza umasikini.

TANI 140 ZA NERICA KUSAMBAZWA.

Tani 140 za NERICA kusambazwa

Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI imesema inakusudia kusambaza wastani tani 140 za mbegu mpya ya mpunga wa juu ya NERICA kwa wakulima wa Unguja na Pemba na kudhibiti uingizwaji na matumizi wa msumeno wa moto nchini.
Katibu mkuu wa wizara Kilimo na Maliasili, Affan Othman Maalim alieleza hayo jana huko ofisini kwake Darajani mjini hapa kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Mansour Yussuf Himid alipokuwa akitia mwelekeo wa bajeti ya wizara mbele ya waandishi wa habari.
Alisema tani hizo za mbegu hiyo mpya ya NERICA zitasambwa kwa wakulima mbegu ambayo inaweza kuzalishwa katika eneo lisilo na maji mengi, huku pia kanuni zikiwa zimeshaandaliwa kuhakikisha misumeno ya moto inapigwa marufuku nchini ikiwa ni hatua ya kudhibiti ukataji ovyo wa miti.
Alisema kilimo cha mpunga cha mabondeni kwa mbegu BKN, super India, TXD 88 na TXD 306 zitaongezwa upatikanaji wake kutoka tani 124 kwa mwaka uliopita na kufikia tani 215 kwa mwaka 2011/2012.
Alieleza usambazaji wa mbegu huo utakuwa unakwenda sambamba na kuongezeka kwa zana za kisasa za kilimo kama matrekta, majembe ya kulimia na kuburugia, power tillers, seed drillers, mini combine harvestors, rice reappers na threshers, ambapo malengo hayo ni kwa ajili ya kufikia kauli mbiu ya Mapinduzi ya Kilimo.
Alisema dunia hivi sasa imekabiliwa na hali ya upungufu mkubwa wa chakula na tishio la njaa, hali hiyo inasababisha upungufu wa uzalishaji wa nafaka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa na kupanda kwa gharama za bei za mafuta, hivyo kunakuwepo ushindaji mkubwa wa chakula katika masoko ya kimataifa.
Alifahamisha kuwa wizara imeazimia kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji maji na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua kwa kushirikiana na wahisani kutoka KOICA, USAID, TASAF na JICA katika kufanikisha hilo, pamoja na nguvu zitaendelea katika utafutaji wa mitego ya nzi wanaoharibu matunda.
Aidha alifahamisha kuwa, wizara hiyo imepania kuimarisha mkakati maalum wa uendelezaji wa kilimo cha matunda na viungo kwa kuongeza uzalishaji wa kibiashara ni pamoja na karafuu, pilipili kichaa, manjano, mdalasini, vanilla, pilipili manga na mchaichai, ambapo mvuje, mrehani, hina, zingifuri, tangawizi, hiliki na kungumanga zitaimarishwa kwa ajili ya utafiti, mafunzo na matumizi ya ndani, ikiwemo maonyesho ya watalii.
Alisema katika kikabiliana na hali hiyo Wizara imepanga kuzalisha miche milioni moja ya viuongo, matunda, misitu ya mapambo, ikiwemo ya zao la karafuu ili kuliongezea nguvu kwa vile linasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza pato la uchumi wa taifa.
Katibu Mkuu Affan aliongeza kwamba, kilimo cha mazao ya juu nacho kimepewa kipao mbele katika uzalishaji huo pamoja na kuendeleza kufanya utafiti katika mazao mbali mbali hasa ya chakula kama muhogo, viazi, migomba, mpunga na mboga mboga.
Aidha alieleza wataendeleza matumizi ya mbegu bora na utaalamu kwa wakulima wengi kwa mazao mbali mbali kupitia skuli za wakulima ili kuongeza uzalishaji pamoja na kusambaza mbegu mpya za muhogo zenye kustahamili maradhi na wadudu, ambazo zimezalishwa Kizimbani, Machui, Mahonda na Kama kwa ajili ya kuwapatia wakulima.
Alisisitiza kwamba kilimo cha maweni kitaendelezwa uzalishaji wa mbaazi, mtama, uwele, fiwi, viazi vikuu na pilipili hoho, ambazo ni mazao makuu ya ukanda wa maweni, ambapo itawahamasisha wakulima matumizi endelevu ya rasilimali za ardhi na maji katika kuendeleza kilimo hicho bila ya kuathiri mazingira na maliasili zilizopo.
Alisema bajeti hiyo inakusudia kujenga masoko wilayani yatayotoa huduma za uhifadhi wa bidhaa zinazoharibika, ujenzi wa viwanda viwili vya kuzalisha barafu, kuanzisha mfumo wa utoaji wa huduma za kifedha vijijini na kuimarisha vikundi vya wajasiriamali katika usindikaji na usarifu wa bidhaa za kilimo.
Alieleza sekta ya kilimo inachangia asilimia 24 ya pato la taifa na inakadiriwa kuwa asilimia 75 ya wananchi wanategemea sekta hiyo katika chanzo cha ajira na mapato yao.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Maalim, Seif Sharif Hamad akiangalia uharibifu wa mazingira unaotokana na uchimbaji wa matofali ya mawe huko Sanani Muwambe, mkoa wa Kusini Pemba. (Picha na OMKR).

MAALIM SEIF VIWANGO VYA KODI KUANGALIWA UPYA.

Maalim Seif: viwango vya kodi kungaliwa upya

Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema serikali itaangalia viwango vya kodi vinavyotozwa kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini.
Alisema anaamini viwango vikubwa vya kodi havisaidii, bali ni njia ya kuwaumiza watu na kuwafanya wafanyabiashara wakimbie, sambamba na kuwanufaisha baadhi ya watu wachache kutoka taasisi zinazosimamia makusanyo hayo.
Maalim Seif amesema hayo jana ofisini kwake Migombani, alipokuwa na mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, wenye viwanda na Wakulima Zanzibar, waliofika kujitambulisha na kubadilishana mawazo.
Alisema kuna umuhimu wa viwango vya kodi vinavyotozwa kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa nchini kuangaliwa upya, ili Zanzibar irejeshe hadhi yake ya kuwa kituo muhimu cha kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema iwapo viwango vya kodi vitapungua, ni wazi kuwa bidhaa nyingi zaidi na zilizo bora zitaingia nchini na kuuzwa kwa bei nafuu, hivyo kufungua milango kwa wafanyabiashara wa ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika kuja Zanzibar, badala ya kwenda ughaibuni.
“Iwapo Zanzibar itafanikiwa kuleta kwa wingi bidhaa zilizo bora na kuziuza kwa bei nafuu, hakutakuwa na sababu kwa wafanyabiashara kutoka Malawi,Kenya, Msumbuji na kwengineko kwenda Dubai au Thailand”, alisema.
Akizungumzia hoja ya kubinafsishwa kwa zao la karafuu kwa lengo la kumnufaisha zaidi mkulima, Maalim Seif alisema serikali inaifanyiakazi hoja hiyo, ikitilia maanani uepukaji wa matatizo mbali mbali yanayoweza kujitokeza.
Alisema moja mifano inayoangaliwa kwa karibu na serikali ni ule wa bidhaa ya mwani, ambapo umeonekana kuwanufaisha zaidi mawakala na wafanyabiashara wakubwa huku ukiwaacha wakulima wakiendelea kusumbuka kutokana na kiwango kidogo cha bei ya bidhaa hiyo, ikilinganishwa na linavyouzwa katioka soko la Dunia.
Alisema utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa matajiri wamekuwa wakiwakandamiza wakulima kutokana na bei ndogo wanayowalipa ikilinganishwa na faida waipatayo.
Maalim Seif alisema serikali iko tayari kushirikiana na wafanyabiashara wazalendo wenye uwezo wa kuwekeza katika miradi mbali mbali ya maendeleo, hivyo aliwataka wanachama wa jumuiya hiyo kueleza azma zao.
Alitumia fursa hiyo kuwathibitishia wanachama hao uwezekano wa wajumbe wake kushirikishwa katika Bodi mbali mbali zinazoundwa na serikali, hususan katika sekta zinazohusika na biashara au uchumi.
Aidha aliwahakikishia viongozi hao uwezekano wa kuhusishwa katika mijadala mbali mbali ya kisheria katika hatua za maandalizi ya awali (draft) kwa lengo la kupatikana mawazo yao.
Alibainisha kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, kwa mujibu wa sheria zilizopo ndie mwenye jukumu la kuzingatia iwapo upo uwezekano wa wanajumuiya hiyo kuhusishwa katika mijadala ngazi za kamati.
Mapema Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, wenye viwanda na Wakulima Zanzibar, Mbarouk Omar Mohamed, alisema hali ya amani na utulivu iliopo hivi sasa nchini, imeifanya Zanzibar kuwa mahala pazuri zaidi pa kuishi na kuwa kichocheo katika kukuza biashara.
Alisema Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi, wana fursa nzuri ya kuwekeza katika miradi mbali mbali na kuendeleza biashara, kwa maslahi na maendeleo ya nchi.
Alishauri Serikali kupunguza viwango vyake vya kodi, hususan katika bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, hatua aliyosema itaifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha kibiashara na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka mataifa mbali mbali jirani kuja kununua bidhaa hizo badala ya kukimbilia nchi za mbali.
Alitoa mfano wa nchi kama Dubai na kusema imefikia maendeleo makubwa ya kibiashara kutokana na mfumo wa ulipaji kodi nafuu, unaowawezesha wafanyabiashara kutoka sehemu mbali mbali Duniani, ikiwemo Zanzibar kukimbilia huko.

MAPATO BAHARI KUU YAZUA MJADALA BARAZANI.

Mapato bahari kuu yazua mjadala Barazani

Mwakilishi asema ni kero nyengine ya Muungano
Na Mwantanga Ame
MWAKILISHI wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu ameibua tuhuma nzito juu ya Zanzibar kukoseshwa haki yake katika Muuungano ya mapato yatokanayo na leseni uvuvi wa bahari kuu.
Mwakilishi huyo aliibua hoja hiyo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka wa fedha 2011/2012 iliyowasilisha na waziri wa wizara hiyo Said Ali Mbarouk.
Jussa alimtaka waziri huyo kuliangalia vyema suala la fedha za leseni katika bahari kuu kwani Zanzibar inakoseshwa mapato yake na hawaoni kama serikali ya Muungano ina nia ya kushirikiana na SMZ juu ya mapato ya mgawano wa fedha zinAzokusanywa katika uvuvi wa bahari kuu.
Alisema sheria ya makubaliano juu ya mgawano wa mapato ya uvuvi wa bahari kuu yanataka Zanzibar kupewa asilimia 40 na bara asilimia 60 lakini hali iliyopo ni kwamba hiyo asilimia 40 Zanzibar haipewi.
Akifafanua kauli yake alisema katika kikao cha mwezi Juni 15, 2011, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo wa Tanzania, Benedict Ole Nangoro, akijibu Mbunge wa viti maalum Thuwaiba Idrisa Muhammed ambaye alitaka kujua kiasi gani na Zanzibar imeweza kufaidika na fedha za magao wa lesini za bahari kuu ambapo Naibu huyo alijibu fedha walizokusanywa na sio mgao wa Zanzibar
Alisema Naibu huyo aliliambia Bunge hilo kuwa kwa mwaka 2010/ 2011, meli ambazo zilivua baada ya kupatiwa leseni zilikuwa ni 71 na mapato yaliopatikana yalikuwa dola za kimarekani 2,074,000.
Alisema inasikitisha kuona mapato ya Zanzibar katika suala hilo imekuwa haipatiwi huku serikali ikiwa inatoa mchango wake wa kujenga jengo la Makao Makuu ya uvuvi wa bahari kuu huko Fumba.
Mwakilishi huyo anayechachafya Barazani alisema ipo haja ya wizara hiyo kuanza kufanya uchunguzi kwa kutafuta ni kwanini mgao uliotakiwa kupatikana kwa uvuvi wa bahari kuu mapato hayakufikishwa Zanzibar.
Alisema ni lazima serikali iliangalie hilo kwa vile Waziri wa wizara hiyo amekuwa akilalamikia ukosefu wa fedha kwa ajili ya utoaji wa huduma za baadhi ya ofisi kuwa na mchango mdogo huku kukiwa na fedha ambazo zingeweza kusaidia kukabiliana na changamoto za wizara hiyo.
Alisema tatizo hilo ni muendelezo wa vitendo vya serikali ya Muungano katika mambo ya mgawano wa mapato jambo ambalo hapo awali lilielezwa kuwa limeshapata ufumbuzi katika vikao vya kero za Muungano.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Matemwe, Abdi Mosi Kombo, alisema ipo haja kwa wizara hiyo kuwaandalia mazingira mazuri ya kuwapatia vifaa vya kisasa wavuvi wa eneo ili kazi yao hiyo iweze kuwafaidisha kimapato.
Nae Mwakilishi wa Kojani Hassan Hamad Omar, alisema ipo haja ya serikali kuliangalia suala la baadhi ya wavuvi wanaoenda kuvua Tanzania bara kutozeshwa kodi ya leseni ya shilingi 20,000 wakati wanaotoka bara kuja Zanzibar hawatozwi fedha hizo.
Mwakilishi wa Mkoani Abdalla Mohammed Ali, akitoa mchango wake alisema ipo haja kwa serikali ikaona inaimarisha sekta ya mifugo kwa kuwapatia wafugaji ng’ombe wa kisasa kwa mkopo kwani baadhi ya wafugaji hawana uwezo wa kununua mifugo hiyo.
Mwakilishi wa Jimbo la Amaan, Fatma Mbarouk Said, alisema ipo haja kwa serikali ikawaangalia vijana ambao hivi sasa wanajishughulisha na ajira za Punda na ng’ombe kwa kuwapatia kazi ikiwa ni hatua itayowawezesha kuacha kuwatumia wanyama hao vibaya.
Nae Mwakilishi wa Mkwajuni Mbarouk Wadi Mussa Mtando, ameitishia kuzuiya bajeti hiyo ikiwa Wizara hiyo itashindwa kump maelezo juu ya gari lililonunuliwa kwa ajili ya mradi MACEMPU iliyokuwa ikitumiwa na Mkurugenzi wa Uvuvi ambayo hivi sasa haijulikani ilipo.
Wawakilishi wengine waliipongeza Wizara hiyo juu ya utekelezaji wa dhamira yake ya kuinua sekta ya uvuvi wa bahari kwa kufikiria kutoa boti kwa kila Wilaya zitazowawezesha wavuvi wapatao 20 kuvua bahari kuu.

Monday, 18 July 2011

BALOZI SEIF VIJANA ACHENI KUKAA VIJIWENI KUTEGEMEA MJOMBA,

Balozi Seif: Vijana acheni kukaa vijiweni kutegemea 'mjomba'

Awahamasisha kufanya kazi za kujitolea
Na Aboud Mahmoud
VIJANA nchini wametakiwa kuwa tayari kufanya kazi za kujitolea zenye manufaa kwao na Taifa.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi,wakati wa uzinduzi wa Kampeni endelevu ya usafi wa Mazingira iliyoandaliwa na Jumuiya isiyo ya Kiserikali ya ZASOSE katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema vijana wanapaswa kufahamu kwamba Wazanzibari na Watanzania lazima wafanye kazi wenyewe na kuacha tabia ya kudhania kuna mtu atakuja kuwafanyia kazi,
"Nataka niwape wasia aliotuachia Mzee Abeid Amani Karume unaosema lazima mfahamu kwamba sisi Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla hatuna mjomba wa kuja kutufanyia kila kitu,"alifafanua.
Balozi Seif alitoa historia ya kufanya kazi za kujitolea iliyofanyika miaka mingi na kuweza kujipatia umaarufu ni pamoja na ujenzi wa nyumba za maendeleo, Unguja na Pemba, Ujenzi wa uwanja wa Amaan ,ujenzi wa barabara mbali mbali, skuli na mambo mbali ambayo yameweza kuleta maendeleo makubwa ya nchi.
Alieleza kuwa kwa upande wa kilimo, vijana walianzisha makambi ya kilimo sehemu mbali mbali ikiwemo Bambi na sehemu nyenginezo na Unguja na Pemba, ambapo kwa sasa vijana wengi walioshiriki wamekuwa wakulima wa kupigiwa mfano.
Alifahamisha kuwa hakuna shughuli za maendeleo zilizofanyika visiwani Zanzibar bila ya nguvu za vijana ambapo kwa pamoja waliamua kujitolea.
Balozi Seif alichukuwa nafasi hiyo kuwapongeza vijana na hasa Jumuiya ya ZASOSE kwa kufanya uamuzi wa kuanzisha kampeni ya usafi unaotokana na kuguswa na tamko la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein lililosema kuwa hali ya Mji wa Zanzibar hairidhishi.
"Napenda kuwapongeza vijana mbali mbali mlioshiriki katika kampeni hii pamoja na Jumuiya ya ZASOSE kutokana na kufanya uamuzi wa kuanzisha kampeni hii inatokana na kuguswa na tamko la Rais,"alifahamisha.
Akisoma risala ya Jumuiya ya ZASOSE, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Shaka Hamdu Shaka, alisema kuwa lengo kuu la kuanzisha Jumuiya hiyo ni kusimamia, kuhakikisha na kutoa muamko kwa vijana na jamii juu ya suala la usafi na uhifadhi wa mazingira.
Katika uzinduzi huo, Jumla ya shilingi milioni 2,600,000 zilikusanywa kwa ajili ya kuchangia Jumuiya hiyo huku wengine waliahidi kutoa jumla ya shilingi milioni 5,555,000.
Miongoni mwa waliochangia ni Balozi Seif Ali Iddi (Milioni moja) na bado milioni moja na nusu, Mohammed Raza (Milioni moja) na Mwakilishi Mgeni Hassan Juma (500,000).
Wengine ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Sira Ubwa Mamboya (Milioni moja) na Mwakilishi wa Kikwajuni, Mahmoud Mohammed Mussa (300,000).

MILIONI 48 KUFANYIWA MATENGENEZO BWAWA LA MICHEZANI.

Milioni 48 kufanyiwa matengenezo bwawa Michenzani

Na Essau Msabila, DSJ
BARAZA la Manispaa la Zanzibar linatarajiwa kutumia shilingi milioni 48 kulifanyia matengenezo makubwa bwawa la Michenzani ili kulirejesha katika haiba yake.
Mkurugenzi wa Baraza hilo, Rashid Ali Juma amesema ukaguzi wa awali kuhusu ujenzi huo umekamilika kwa kiasi cha asilimia 30 ikiwa ni pamoja na kuunganisha paipu zote zinazorusha maji.
Mkurugenzi huyo alisema mambo mengine yaliyokwishafanyiwa marekebisho ya awali ni pamoja na kusafisha eneo la bwawa, kuziba paipu zilizooza na zile zinazovuja na kazi ya upakaji rangi vinavyotarajiwa kurekebishwa hivi karibuni.
Rashid alisema mazungumzo yameshafanyika kati ya Baraza na wawekezaji wa kiwanja cha kufurahishia watoto cha bustani ya Jamhuri na wale wa bustani ya Forodhani, ili kuwapatia mashine tatu maalum za kurushia maji zenye thamani ya shilingi milioni 33.
Hata hivyo, alisema pamoja na uchache wa vifaa vya kufanyia kazi, pia wanakabiliwa na tatizo la uwezo mdogo wa kielimu, lakini alisema itahakikishwa kwamba bwawa hilo linafanya kazi wakati wa sikukuu ya Idd.
Akizungumzia suala la kubandika matangazo, Rashid alisema baraza liliwaalika wafanyabiashara wa aina mbali mbali zikiwemo kampuni za simu, Zanzibar Cool pamoja na "Drop" ili watengeneze kwa kuweka matangazo yao, lakini hakuna aliyejitokeza kukubali kufanya hivyo.
Aidha, alisema kampuni pakee iliyojitokeza ni ile ya Kampuni ya simu Zanzibar, ZANTEL lakini baadae kampuni hiyo haikuendelea na majadiliano na baraza ndipo likaamua kuifanya kazi hiyo yenyewe.

WANAFUNZI WAONYWA KUEPUKA HADAA ZA WENYE MAGARI.

Wanafunzi waonywa kuepuka hadaa za wenye mgari

Na Mwanajuma Abdi
WANAFUNZI katika ngazi mbali wameonywa kuwapuuza watu wenye fedha wanaojaribu kuwahadaa na baadae kuwaambukiza magonjwa ya zinaa ikiwemo ukimwi na homa ya ini.
Ofisa kutoka Idara ya kupambana na dawa za Kulevya na kurekebisha Tabia, katika Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Fatma Mussa alisema hayo jana, wakati akitoa mada ya Uhusiano wa dawa za kulevya na UKIMWI.
Semina hiyo ya siku moja iliyofanyika katika Skuli ya Sekondari ya Ben Bella, iliyoandaliwa na Jumuiya ya ZAYEDESA, chini ya Ufadhili wa Aga Khan kupitia Hoteli ya Serena Inn katika mradi wa Mji Mkongwe.
Semina hiyo ilizishirikisha skuli 11 za sekondari na msingi zilizokuwepo katika Mji Mkongwe, ambazo zimewajumuisha wanafunzi 60 na walimu 10, ambapo mafunzo hayo maalum katika upigaji vita matumizi ya dawa za kulevya na kupambana na UKIMWI katika Mji huo wenye urithi wa kimataifa.
Alisema baadhi ya wanafunzi hususani wa kike wanarubuniwa na waendesha magari, zikiwemo daladala na TAXI, hali ambayo inachangia kujiingiza katika matendo maovu, sambamba na kupata maambukizi ya maradhi ya UKIMWI.
Akitoa ushuhuda wake kwa wanafunzi hao kwamba aliwahi kupanda daladala lakini mlango wa mbele ulifungwa na baada ya kuchungulia ndani alimkuta mwanafunzi amekaa na dereva pekee yake, hali ambayo ni hatari kwa vijana kujiingiza katika masuala hayo wakati bado wakiwa na umri mdogo.
Aidha alieleza wimbi la watumiaji wa dawa za kulevya linaongezeka kila uchao, ambapo katika mitaa mingi hivi sasa ni hatari kupita nyakati za jioni ukiwa unazungumza na simu ikiwemo Muembemakumbi, ambapo wazee wanawaogopa watoto wao hata wakifanya makosa wanawaona hawawambii kitu.
Alifahamisha kuwa, madawa ya kulevya yanauhusiano mkubwa kwa maradhi ya UKIMWI, hususani wanaojidunga sindano, ambapo wengi wao hawana muamko wa kutumia bomba moja mtu mmoja, hivyo hutumia kwa kupokezana.
Afisa huyo, alisema mbali ya kujidunga sindano, pia baaadhi ya vijana waliojiingiza katika matumizi hayo wanapokosa hulazimika kufanya ngono zisizo salama ili waweze kupata dawa hizo kwa vile anajiona katika mwili wake amepungukiwa.
Nae Mwanafunzi wa skuli ya Hamamni aliiomba Jumuiya ya ZAYEDESA kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupita maskuli kwa ajili ya kuhimiza uundwaji wa kamati maskuli kwa lengo la kupiga vita matumizi ya dawa za kalevya na UKIMWI, kwani vijana wengi wanapatikana huko, ambao wanakabiliwa na vishawishi vingi mitaani.
Nao walimu walitoa wito kwa wanafunzi hao kujifunza kwa mashuhuda waliotoa mada ambao walikuwa wakitumia dawa za kulevya kwa muda mrefu tokea skuli, hali ambayo imewasababishia kupoteza muelekeo wa masomo na hatimae kukimbia na kubakia mitaani.
Walisema mashuhuda hao walieleza kwa hamasa na uchungu mkubwa, hivyo wanafunzi wana kila sababu ya kijifunza kutoka kwao na kuachana matumizi ya dawa hizo pamoja na kujikinga na maradhi yasiyokuwa na tiba hadi sasa ya UKIMWI.
Walifahamisha kuwa dawa za kulevya zinaingizwa kupitia Viwanja vya Ndege, Bandari kuu na zisizo rasmi na kushauri serikali iongeze jitihada katika kuzuia matumizi na uingzaji dawa hizo nchini.
Semina hiyo, imefungwa na Katibu Mkuu Jumuiya ya ZAYEDESA, Lucy Majaliwa, aliewahimiza wanafunzi kusambaza taalum awalioipata kwa wenzao.

SENSA YA MAJIMBO AGOSTI

Sensa ya majaribio Agosti

Na Mwantanga Ame
WAZANZIBARI kote nchini wanatarajiwa kuanza kuhesabiwa ifikapo mwezi Agosti mwaka huu katika zoezi la majaribio ili kuweza kujulikana idadi yao kamili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Waziri huyo alisema serikali itaendesha zoezi hilo la sensa kwa ajili ya kuwahesabu Wazanzibari kote nchini ikiwa ni hatua ya kuweza kutambulika idadi yao.
Alisema sensa ya idadi ya watu itaweza kusaidia serikali kuipa fursa nzuri kuweza kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake.
Alisema wanalazimika kufanya sensa hiyo hivi sasa kutokana na kutimiza miaka 10 tangu kuendeshwa kwa zoezi na kuhesabu watu na makaazi mwaka 2002 jambo ambalo tayari kuna mabadiliko makubwa yanayohitaji kuangaliwa.
Alisema maandalizi ya sensa hiyo hivi sasa yapo katika hali nzuri chini ya usimamizi wa Mtakwimu Mkuu wa serikali Zanzibar na Tanzania Bara.
Kutokana na kuanza kukamilika matayarisho hayo Waziri aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa kukubali kuhesabiwa kwa kuwapa ushirikiano wataokuwa wanaifanya kazi hiyo ili lengo la serikali liweze kufanikiwa.
Alisema suala la ongezeko la idadi ya watu ni moja ya changamoto kubwa yenye uzito ambayo inahitaji kuangaliwa na pande zote za jamii ikiwa ni hatua itayoweza kupunguza tatizo hilo.
Waziri huyo alisema ili kupatikana mafanikio ni vyema wadau wote kuona umuhimu wa kutumia takwimu katika shughuli zao, ziwawezeshe kupanga mipango itayokuwa na usambazaji sawia wa raslimali huduma na miundombinu baina ya Mijini na Vijijini.
Alisema hali hiyo haitaweza kupunguza kasi ya vijana kukimbilia mijini bali itasaidia kupunguza dhana ya kwamba watu wa vijijini kulala mapema.
Kutokana na tafiti mbali mbali Waziri huyo alisema changamoto nyingi zinazohusu vizazi, vifo, uchafuzi wa mazingira na ujenzi holela ni mambo yenye uhusiano mkubwa na viwango vya elimu na hali ya utajiri au umasikini wa wananchi.
Hata hivyo Waziri alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, alisema bado serikali itahakikisha juhudi za makusudi zinafanyika kupitia utekelezaji wa mpango wa MKUKUTA na MKUZA.

WAJASIRIAMALI WA ZANZIBAR WAJIFUNZA MATUMIZI YA NGOZI MWANZA.

Wajasiriamali wa Zanzibar wajifunza matumizi ya ngozi Mwanza

Na Ali Mohamed, Maelezo
WIZARA ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika imesema itaendelea kuwajengea uwezo wa elimu wanaushirika na wajasiriamali wengine kama mbinu ya kuwapa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa bora na kukuza fursa za ajira.
Akitoa maelekezo kwa wajasriamali waliokuwa wakijiandaa kwenda Mwanza kwa mafunzo ya ujasiamali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Asha Ali Abdulla alisema serikali itafikia lengo hilo kwa watu wengi zaidi,
Alisema katika kipindi ambacho ni cha ushindani wa kibishara na huduma wajasiriamali Zanzibar lazima wabadilike na kutegeneza bidhaa zitakazomudu ushindani katikamasoko ya kibiashara nchini,
“Nia ya seriki ni kuwatoa wajasiriamali katika hali waliopo na kuwapeleka mbele kwa kuwaendeleza na kuwawezesha kutengeneza bidhaa zenye ubora kwa kutumia soko la ndani, alisema Asha.
Wajasiriamali wanaohudhuria mafunzo ya matumizi ya ngozi kutengeneza viatu aina ya kubadhi kutoka Pemba na Unguja kuwa makini katika mafunzo hayo na kuchukua elimu ili watakaporudi nyumbani wawe walimu kwa wenzao.
Ziara hiyo imegharamiwa na serikali kupitia Wizara Kazi na Uwezeshaji kwa kushirikiana na Wawakilishi wa Majimbo ya Kikwajuni na Wawi Pemba.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ali Juma alisema inashangaza kuona bidhaa nyingi zinazotokana na sanaa za mikono katika Mji wa Zanzibar hazitoki Zanzibar.
Alisema bidhaa nyingi na sanaa zinatoka nje ya Zanzibar hivyo hazioneshi utamaduni halisi wa Zanzibar na aliwataka wajasiriamali kuwa wabunifu zaidi ili kuleta ushindani kibiashara.

WAJASIRIAMALI WA ZANZIBAR WAJIFUNZA MATUMIZI YA NGOZI MWANZA.

Wajasiriamali wa Zanzibar wajifunza matumizi ya ngozi Mwanza

Na Ali Mohamed, Maelezo
WIZARA ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika imesema itaendelea kuwajengea uwezo wa elimu wanaushirika na wajasiriamali wengine kama mbinu ya kuwapa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa bora na kukuza fursa za ajira.
Akitoa maelekezo kwa wajasriamali waliokuwa wakijiandaa kwenda Mwanza kwa mafunzo ya ujasiamali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Asha Ali Abdulla alisema serikali itafikia lengo hilo kwa watu wengi zaidi,
Alisema katika kipindi ambacho ni cha ushindani wa kibishara na huduma wajasiriamali Zanzibar lazima wabadilike na kutegeneza bidhaa zitakazomudu ushindani katikamasoko ya kibiashara nchini,
“Nia ya seriki ni kuwatoa wajasiriamali katika hali waliopo na kuwapeleka mbele kwa kuwaendeleza na kuwawezesha kutengeneza bidhaa zenye ubora kwa kutumia soko la ndani, alisema Asha.
Wajasiriamali wanaohudhuria mafunzo ya matumizi ya ngozi kutengeneza viatu aina ya kubadhi kutoka Pemba na Unguja kuwa makini katika mafunzo hayo na kuchukua elimu ili watakaporudi nyumbani wawe walimu kwa wenzao.
Ziara hiyo imegharamiwa na serikali kupitia Wizara Kazi na Uwezeshaji kwa kushirikiana na Wawakilishi wa Majimbo ya Kikwajuni na Wawi Pemba.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ali Juma alisema inashangaza kuona bidhaa nyingi zinazotokana na sanaa za mikono katika Mji wa Zanzibar hazitoki Zanzibar.
Alisema bidhaa nyingi na sanaa zinatoka nje ya Zanzibar hivyo hazioneshi utamaduni halisi wa Zanzibar na aliwataka wajasiriamali kuwa wabunifu zaidi ili kuleta ushindani kibiashara.

VITA YA UKIMWI KUELEKEZWA ZAIDI KWA MAKUNDI HATARISHI.

Vita ya UKIMWI kuelekezwa zaidi kwa makundi hatarishi

Na Mwandishi wetu
MKAKATI wa pili wa kukabiliana na ukimwi (MPIKU II) utatoa kipaumbele zaidi kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja (MSM),watu wanaofaya biashara ya ngono (CSW) na watumiaji wa dawa za kulevya, hasa wanaotumia sindano (IDU).
Kwa mujibu wa sheria za Zanzibar ni marufuku mtu kushiriki mapenzi ya jinsia moja na kufanya biashara ya kuuza mwili wake.
Makundi mengine yanayolengwa ni wanafunzi wa vyuo vya mafunzo na jamii kwa ujumla.
Halima Ali Mohamed kutoka Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) alisema makundi hayo matatu yanaonekana kuathirika zaidi na ukimwi, ambapo tafiti zinaonesha maambukizi yamefikia asilimia 30.
Aidha alisema kuna maambukizi yanayofikia asilimia 2.8 kwa wanafunzi wa vyuo vya mafunzo.
Tayari tafiti zinafanywaa kupata idadi kamili ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja (mashoga) pamoja na maeneo walipo ili iwe rahisi kuwafikia wakati wa utekelezaji wa mkakati huo.
Mkakati wa kwanza ulikuwa hauyakaribishi baaadhi ya makundi yakiwemo hayo kupata huduma kutokana na silka na utamaduni wa Zanzibar.
Alisema mkakati unalenga kupunguza kiwango cha taifa cha maambukizi kwa asilimia 33 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 0.6 hadi asilimia 0.4 ifikapo mwaka 2016.
“Lengo kuu ni kuzuia usambaaji VVU kwa Wazanzibari yakiwemo makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa ,kuwapatia huduma bora na kamili wanaoishi na VVU pamoja na kukabiliana na athari mbaya za kijamii zinazotokana na ukimwi,” alisema katika semina iliyowahusisha wadau mbali mbali wa masuala ya ukimwi.
Mapema Said Juma kutoka ZAC alisema mkakati wa kwanza uliomalizika mwaka 2009 kwa kiasi kikubwa ulifanikiwa kutoa uelewa kuhusu masuala ya ukimwi lakini uelewa huo hauwiani na mabadiliko ya tabia kwa wananchi.
Katika upande wa huduma , MPIKU II unalenga kupunguza madhara ya kiafya na watu wanaoshi na VVU kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2016.
Aidha asilimia 80 ya wanaoishi na VVU watapata huduma za matibabuya magonjwa nyemelezi.
Wakichangia rasimu ya mkakati huo, washiriki wa semina hiyo walisema, vita dhidi ya ukimwi vinapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee hasa katika taasisi za elimu ya juu, ambapo baadhi ya washiriki walisema kuna udhalilishaji mkubwa dhidi ya wanafunzi wa kike unaofanywa na wahadhiri, ambao unaweza kuwa sababu ya kuongezeka maambukizi mapya ya VVU.
Aidha walisema tabia ya wanaume kuwa wanawake wengi (MCP) inahatarisha kuongezeka kwa maambukizi ya VVU na hivyo wakaishauri ZAC pamoja na taasisi nyengine zenye wajibu wa kutekeleza mkakati huo kutojikita zaidi katika makundi matatu na kusahau makundi mengine ambayo bado yako salama au maambukizi sio makubwa.
MPIKU II ambao utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2011/2016 utahakikisha kila taasisi za umma na asasi za kiraia pamoja na jamii wanashiriki katika mapambano dhidi ya Ukimwi ipasavyo.

Sunday, 17 July 2011

MIMBA, NDOA ZAENDELEA KUWAKOSESHA ELIMU WATOTO WA KIKE,

Mimba, ndoa zaendelea kuwakosesha elimu watoto wa kike

Na Mwanajuma Abdi
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imesema kesi 28 za wanafunzi kupata ujauzito na kesi 22 za ndoa zimeripotiwa katika mwaka 2010/2011.
Waziri wa Wizara hiyo, Ramadhan Abdalla Shaaban aliyasema hayo, ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya makadirio na mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Alisema kesi 28 za ujauzito zimeripotiwa, kati ya hizo kesi tatu ziliwahusisha wanafunzi kwa wanafunzi, ambapo kesi 10 ziliweza kujadiliwa katika Ofisi ya Mrasjis wa elimu na wanafunzi wanane walikubali kuendelea na masomo, wawili walikataa, ambapo 18 hawakuhudhuria katika kikao cha majadiliano.
Aidha alieleza katika kipindi hiki kesi 22 za ndoa za wanafunzi ziliripotiwa na kati ya hizo kesi mbili ziliwahusisha wanafunzi kwa wanafunzi.
Waziri Shaaban alifafanua kuwa, wanafunzi 24 wamefukuzwa skuli wakihusisha wanawake 22 na wanaume wawili kwa makosa mbali mbali, ambapo kwa mwaka 2011/2012 Kitengo cha Urajis kitaendelea kushughulikia kesi za ujauzito na ndoa za wanafunzi.
Alisema juhudi zitachukuliwa katika kupambana na mimba za utotoni, ndoa za mapema na madawa ya kulevya pamoja na kuelimisha stadi za maisha kwa walimu, wazee na wanafunzi katika skuli zote za Unguja na Pemba.
Aliongeza kusema kwamba, katika juhudi za kusimamia utaoji wa elimu katika skuli za sekondari katika mwaka wa feddha imekusudia kufungua skuli mpya 16 pamoja na kuongeza walimu wenye sifa hasa wa masomo ya sayansi, kuongeza idadi ya vitabu vya kusomea na vifaa vya maabara.
kizungumzia elimu ya msingi alieleza Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto duniani (UNICEF) na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika linakusudia kutoa mafunzo juu ya mbinu za kukomesha utumikishwaji wa watoto kama mpango wa kitaifa unavyoelekeza.
Alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wataendelea na mpango wa kutokomeza maradhi ya kichocho kwa watoto waliopo maskulini.
Hata hivyo, alifafanua mradi wa uhamasishaji wa walimu juu ya matumizi ya adhabu mbadala maskulini unaofadhiliwa na Shirika la Save the Children unaendelea vizuri na utekelezaji wake katika skuli 10 za majaribio zikiwemo sita za Unguja na nne za Pemba.
Alifahamisha kuwa, lengo kubwa la mradi huo ni kuwahamasisha walimu wa skuli, walimu wa vyuo vya kuran, walezi na wazazi kutumia adhabu mbadala badala ya kutoa adhabu zenye madhara kwa wanafunzi na watoto majumbani.
Alisema hiyo itasaidia kujenga uhusiano mzuri baina ya walimu na wanafunzi, wazee na watoto wao na jamii kwa ujumla, ambapo hadi sasa umewahamasisha walimu, kamati za skuli, masheha, Serikali za wanafunzi, wakaguzi, Maofisa wa Wilaya na Mikoa na walimu wa madrasa na vyuo vya kuran.
Alizitaja skuli zilizokuwepo katika majaribio ni pamoja na Regezamwendo, Kinyasini, Fujoni, Kisiwandui, Kitogani na Marumbi kwa Unguja na Pemba ni Pondeani, Ng'ombeni, Wingwi na Minungwini.
Alieleza mikakati yao ni kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa haki ya elimu iliyo bora kwa kuwajengea mazingira rafiki yanayomjali mtoto bila ya ubaguzi au vikwanzo.
Waziri Shaaban alisema katika mwaka wa fedha 2011/2012 aliomba Baraza liidhinishe matumizi ya Wizara hiyo shilingi 102,618,054,000, ambapo kati ya hizo shilingi 45,308,000,000 kwa ajili ya kazi za kawaida na shilingi 57,310,054,000 kwa kazi za maendeleo.

UN KUIPATIA ZANZIBAR BILIONI 17.7

UN kuipatia Zanzibar bilioni 17.7

Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetiliana saini na Umoja wa Mataifa nchini Tanzania mpango wa msaada wa maendeleo wa shilingi bilioni 17.7 (dola milioni 11.6) unaanza mwezi huu hadi Juni mwaka 2015.
Hafla ya utiaji saini huo imefanyika jana, ukumbi wa Jumba la Makumbusho ya Kasri, Forodhani mjini hapa, ambapo kwa upande wa SMZ imewakilishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Khamis Mussa Omar na UN imewakilishwa na Mwakilishi Mkaazi wake Tanzania, Alberic Kacou.
Akizungumza mara ya utiaji saini hiyo, Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa,Tanzania, Alberic Kacou alisema mpango wa msaada huo umejumuisha mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Tanzania kwa ajili ya kutoa kipaumbele katika kukuza uchumi, huduma za afya ikiwemo ugonjwa wa UKIMWI, lishe bora, elimu, mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, maji, utawala bora na msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi.
Alisema Mpango huo utatoa nafasi katika masuala ya uwajibikaji wa UN katika mchango wake kupunguza umasikini ikiwemo mikakati ya kitaifa ya MKUKUTA kwa Tanzania Bara na MKUZA II kwa Zanzibar ambao utanufaisha kwa ujumla, ambapo mwezi uliopita Juni 24 mwaka huu walitilia saini na Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania jijini Dar es Salaam katika kutelekeza miradi mbali mbali, ambapo programu hiyo ya miaka minne itatumia Dola za Marekani milioni 777 kwa nchi mzima.
Alieleza mpango huo utasaidia Zanzibar katika kuimarisha uchumi kupitia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II), kujengea uwezo taasisi na kuongeza uzalishaji katika kilimo pamoja na huduma za kijamii hususani katika upatikanaji wa haki za binadamu katika viwango vya kimataifa.
Aidha alipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi, ambapo msaada huo utaongeza kasi za ukuaji wa uchumi.
Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Khamis Mussa alisema Zanzibar ina mashirikiano na muda mrefu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa katika kusaidia miradi mbali mbali ya kimaendeleo na kukuza uchumi, ikiwemo afya, elimu na kusaidia mpango mkuu wa miaka mitano Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA).
Alieleza UN imeipatia Zanzibar shilingi bilioni 17.7 katika mpango huo wa msaada, ambapo kipaumbele ni sekta ya afya, elimu, mazingira katika kasi ya kukuza uchumi wa nchi.

WAHADHIRI WAIKIMBIA SUZA KWENDA KUSOMESHA DODOMA.

Wahadhiri waikimbia SUZA kwenda kusomesha Dodoma

Na Halima Abdalla
WIZARA ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imetakiwa kuchukua hatua ili kuwafanya wahadhiri kutokimbia kufanya kazi katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Akichangia akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya mwaka 2011/2012, Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jusa Ladhu, alisema inasikitisha kuona wahadhiri waliobobea katika fani muhimu walio katika kiwango cha Udaktari wa falsafa (PHD) kukikimbia chuo hicho na kwenda kusomesha Chu Kikuu cha Dododoma.
Jusa alisema hali hiyo inatia shaka kwa wahadhiri wanaosomea PHD hivi sasa nao hawatorudi kutokana na kutokuwepo maslahi mazuri chuoni hapo.
Aidha Wizara hiyo imeshauriwa kuweka muda wa masomo ya ziada nyakati za jioni katika maskuli ili kuepusha wanafunzi kwenda kusoma masomo hayo vichochoroni au skuli za binafsi.
Ushauri huo umetolewa na Omar Ali Sheikh (Chake Chake) katika kikao cha Baraza la Wawakilishi alipokuwa Alisema masomo hayo ya ziada yakipelekwa maskulini itasaidia katika maskuli kujipatia pesa ikiwemo walimu kujipatia posho za kuweza kusaidia kujikimu na maisha.
Aidha alisema tatizo la walimu kukimbia katika vyuo vikuuu lina sababishwa na mishahara midogo wanayolipwa aliishauri Serikali kuwaongezea wataalamu mishahara ili kuzuia kuondoka.
Akichangia Bajeti hiyo Ashura Sharif Ali (Nafasi za wanawake) aliishauri Wizara ya Elimu kufanya juhudi japo kwa kutafuta wafadhili kuwapatia posho japo la sabuni walimu wa vyuo vya madrasa ili kuwapa nguvu ya kufundisha walimu hao.
Alisema elimu ya madrasa ndio ya mwanzo anapoanzia mtoto kupatia elimu ya akhera hivyo inahitaji kusukumwa.
Nae Subeit Khamis Faki (Micheweni) aliishauri Wizara elimu kuwapunguzia michango walimu kwani mishahara yao walimu haiwatoshi hivyo alimtaka Waziri wa Elimu kukaa pamoja na kuzingatia jinsi gani ya kuwapunguzia walimu mzigo huo.
Aidha waliishauri Wizara ya Elimu kuacha kuwa changisha wanafunzi karatasi za mitihani kipindi cha mitihani ikifika kwani kunarejesha nyuma maendeleo ya wanafunzi maskulini.
Sambamba na hayo aliishauri Serikali kuwalipa walimu fedha zao za kusimamia mitihani kwa wakati muafaka wanapomaliza kusimamia mitihani hiyo kwani Serikali imekuwa ikiwacheleweshea walimu fedha zao wanapomaliza kusimamia mitihani .
Kwa upande wake Abdalla Muhammed Ali (Mkoani) aliishauri Serikali ifanye jitihada ya kuongeza walimu kwani waliopo hawatoshi kwani Zanzibar kuna skuli 700 na kwa sasa Serikali ina mpango kuajiri walimu 800 aliishauri Serikali kuongeza idadi hiyo kwani hitoshi na kwa sasa Zanzibar inakabiliwa na uhaba wa walimu.
Alisema kuna walimu wengi hawajaajiriwa mpaka sasa ambao wanafika mikumbo minne ambayo imemaliza vyuoni hivyo aliishauri Serikali kuongeza idadi ya walimu ki wa kuwaajiri ili kupunguza tatizo la walimu maskulini.

SENSA YA MAJARIBIO AGOSTI.

Sensa ya majaribio Agosti

Na Mwantanga Ame
WAZANZIBARI kote nchini wanatarajiwa kuanza kuhesabiwa ifikapo mwezi Agosti mwaka huu katika zoezi la majaribio ili kuweza kujulikana idadi yao kamili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Waziri huyo alisema serikali itaendesha zoezi hilo la sensa kwa ajili ya kuwahesabu Wazanzibari kote nchini ikiwa ni hatua ya kuweza kutambulika idadi yao.
Alisema sensa ya idadi ya watu itaweza kusaidia serikali kuipa fursa nzuri kuweza kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake.
Alisema wanalazimika kufanya sensa hiyo hivi sasa kutokana na kutimiza miaka 10 tangu kuendeshwa kwa zoezi na kuhesabu watu na makaazi mwaka 2002 jambo ambalo tayari kuna mabadiliko makubwa yanayohitaji kuangaliwa.
Alisema maandalizi ya sensa hiyo hivi sasa yapo katika hali nzuri chini ya usimamizi wa Mtakwimu Mkuu wa serikali Zanzibar na Tanzania Bara.
Kutokana na kuanza kukamilika matayarisho hayo Waziri aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa kukubali kuhesabiwa kwa kuwapa ushirikiano wataokuwa wanaifanya kazi hiyo ili lengo la serikali liweze kufanikiwa.
Alisema suala la ongezeko la idadi ya watu ni moja ya changamoto kubwa yenye uzito ambayo inahitaji kuangaliwa na pande zote za jamii ikiwa ni hatua itayoweza kupunguza tatizo hilo.
Waziri huyo alisema ili kupatikana mafanikio ni vyema wadau wote kuona umuhimu wa kutumia takwimu katika shughuli zao, ziwawezeshe kupanga mipango itayokuwa na usambazaji sawia wa raslimali huduma na miundombinu baina ya Mijini na Vijijini.
Alisema hali hiyo haitaweza kupunguza kasi ya vijana kukimbilia mijini bali itasaidia kupunguza dhana ya kwamba watu wa vijijini kulala mapema.
Kutokana na tafiti mbali mbali Waziri huyo alisema changamoto nyingi zinazohusu vizazi, vifo, uchafuzi wa mazingira na ujenzi holela ni mambo yenye uhusiano mkubwa na viwango vya elimu na hali ya utajiri au umasikini wa wananchi.
Hata hivyo Waziri alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, alisema bado serikali itahakikisha juhudi za makusudi zinafanyika kupitia utekelezaji wa mpango wa MKUKUTA na MKUZA.

ATOLEWA DONGE LA DAMU KILO 5.5 TUMBONI.

Atolewa donge la damu kilo 5.5 tumboni

Na Lulua Salum, Pemba
WANANCHI wametakiwa kubadilika na kuachana na imani potofu za kishirikina zaidi katika kutafuta tiba na badala yake wajenge tabia ya kwenda hospitali wanapojibaini na matatizo ya kiafya.
Kauli hiyo imetolewa na Ramon Contrera, daktari bingwa wa Upasuaji kutoka Cuba, ambae anafanyakazi katika hospitali ya Chake Chake Pemba, baada ya kukamilisha upasuaji mgonjwa alielazwa hospitalini hapo akisumbuliwa na tatizo la mayoma kwa muda mrefu.
Mgonjwa huyo alibainika kuwa na pande la nyama ndani ya tumbo lake lenye uzito wa kilogramu 5.5 ambalo amedumu nalo kwa muda mrefu na hiyo inadaiwa imechangiwa na hofu ya kwenda hospitali kutokana na umuhimu wa kukimbilia hospitali mapema badala ya kuelemea kwenye tiba za asili.
Daktari Ramon, alisema kujengeka kwa imani za kishirikina ndani ya nyoyo za watu wengi ni sababu ya ongezeko kubwa la maradhi na kupoteza maisha.
Alisema imefika wakati jamii kubadilika na kujenga tabia ya kuchunguza afya zao hata mwaka mara moja ili kujimbua endapo muhusika atakuwa amekumbwa na maradhi yoyote,
Daktari huyo bingwa ameishauri serikali iiangalie hospitali ya Chake chake na kuomba Serikali kuiangalia hospitali ya Chake Chake kwa kusema kuwa hospitali hiyo inafanya kazi nzito zisizolingana na ukubwa wa hospitali yenyewe,
Mgonjwa aliefanyiwa upasuaji huo ambae hakutaka kutaja jina lake gazetini alisema alisumbuka na tatizo hilo kwa muda mrefu na kuamini kwamba linaweza kuondoka kwa kufanya tiba za asili lakini aliona tatizo linazidi siku hadi siku na ndipo alipoamua kwenda hospitali kupatiwa tiba.
“Kiukweli nilishakata tamaa kabisa ya kupona tatizo hili lakini namshukuru Mungu kwani nimeshindwa kuamini kile kilichotoka tumboni mwangu ambapo awali niliamini nasumbuliwa na matatizo ya kiswahili,” alisema.

ABIRIA MV SERENGETI WANUSURUKA KUFA

Abiria MV Serengeti wanusurika kufa

Yawasili Mkoani kwa injini moja baada ya nyengine kufeli
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ABIRIA waliokuwa wakisafiri kwa meli ya MV Serengeti usiku wa kuamkia jana wakitokea Zanzibar kwenda Pemba, wamenusurika kufa baada ya injini moja ya meli hiyo kushindwa kufanya kazi ikiwa safarini.
Taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), zimefahamisha kuwa, meli hiyo iliyosajiliwa Zanzibar iliondoka bandarini huko mnamo saa 3:00 usiku wa juzi ikiwa na abiria wapatao 810 pamoja na mizigo.
Imefahamika kuwa, ikiwa njiani, injini moja ya meli hiyo ilipata hitilafu na kushindwa kuendelea kufanya kazi.
Kutokana na hali hiyo, vikosi vya ulinzi na uokozi viliandaliwa ili kukabiliana na dharura yoyote ambayo ingeweza kutokea kufuatia hitilafu hiyo.
Hata hivyo, taarifa ya SUMATRA ilisema, kwa mwendo mdogo, meli hiyo iliweza kuendelea na safari kwa kutumia injini moja na kuwasili katika bandari ya Mkoani kisiwani Pemba mnamo saa 4:35 asubuhi, badala ya saa 12 jana Julai 15, 2011, ikiwa imechelewa kwa takriban saa tano.
Abiria wote waliokuwemo katika meli hiyo pamoja na mabaharia, walishuka bandarini hapo salama usalimini.
Katika siku za hivi karibuni, kumeripotiwa malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wasafiri wa meli zinazokwenda kati ya Pemba na Unguja, kwamba zimekuwa mbovu na kutaka mamlaka husika zizidhibiti.
Katika tukio la hivi karibuni, meli uya Burak ambayo pia ilikuwa ikitokeac Zabziabr kwenda Pembva, ilijikuta ikitia nagnga katika bandari ya Tanga kutokana na upepo mkali wa Kusi unaoendelea kuvuma nchini.

Friday, 15 July 2011

MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Maji Zanzibar ZAWA,Mustafa Ali Garu akibadilishana hati ya makubaliano ya kuujengea uwezo Mradi mkubwa wa Maji unaoendeshwa na Mamlaka hiyo baada ya kutiliana saini na Mwakilishi wa Kampuni ya NIRAS Michael Juel kutoka Denmark, katikati Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,Makaazi, maji na Nishati Mwalim Ali Mwalim,(Picha na Abdallah Masangu)

WAWAKILISHI WAIBANA BAJETI MIUNDOMBINU.

Wawakilishi waibana bajeti miundombinu

• Yapita baada ya utetezi mzito wa Mawaziri
Na Mwanajuma Abdi
MAKADIRIO ya Mapato na Matumzi ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano yalipitishwa jana huku kukijitokeza mvutano kuhusu baadhi ya vipengele ambavyo baadhi ya wawakilishi hawakuridhika na maelezo yake.
Waziri wa Wizara huyo, Hamad Masoud akalazimika kufanya kazi ya ziada kuikwamua bajeti yake ya mwaka wa fedha 2011/2012 na kupitishwa baada ya saa kadhaa kutumika kutolewa maelezo ya ufafanuzi.
Mvutano huo ulitokea ilipofika wakati wa upitishaji wa vifungu, hali iliyowafanya Mawaziri wa Serikali kutoa ufafanuzi mara kwa mara na hatimae kupita bila ya mabadiliko.
Mwakilishi Hamza Hassan Juma (Kwamtipura), alishauri iundwe Tume teule kuchunguza kasoro mbali mbali zilizojitokeza katika Idara ya Anga ikiwemo uajiri uliofanyika kinyume cha sheria kwa kuajiriwa baadhi ya vijana ambao bado wapo masomoni lakini huku tayari wameshapewa ajira hiyo.
Alisema kutokana na kasoro mbali mbali katika Idara hiyo ikiwa pamoja na uonevu uliofanywa wa kubadilishwa kada mfanyakazi na kupelekwa eneo jengine ambalo sio la taaluma yake kutokana na kitendo chake cha kuomba tenda akishirikiana na mume kuanzisha kampuni ya ubebaji wa mizigo katika uwanja wa ndege, ambapo licha ya taratibu zote kuzifuata mwisho wa siku hakupewa na matokeo yake ndio hayo yaliyomfika.
Alieleza Idara hiyo inakabiliwa na kasoro nyingi hivyo, alitaka iundwe Tume Teule ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kuchunguza mambo hayo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, alilazimika kusimama kwa kumueleza Mwakilishi huyo kwamba kazi hiyo itafanywa na kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ambayo inawajumuisha wajumbe wa Baraza hilo, jambo ambalo lilikuwa na mvutano na hatimae alikubaliana nalo.
Mwakilishi wa Mkwajuni, Mbarouk Wadi Mussa (Mtando), alihoji kwamba ujenzi wa Makao Makuu ya Wizara hiyo awali ulikuwa ufanyike Mtoni lakini ulihaulishwa na kupewa mtu mwengine kwa shilingi milioni 200, ambapo alionesha wasiwasi kama taratibu na sheria zimefuatwa katika uhaulishwaji huo na sasa jengo hilo litajengwa Mazizini na kutaka kujua fedha hizo ziko wapi.
Waziri Hamad Masoud alieleza kwamba baada ya kuonekana kasoro mbali mbali katika eneo la Mtoni, Idara ya Ardhi iliamua kupima kiwanja Mazizini, ambako kutajengwa Makao Makuu na litakuwa na Wizara mbili, lakini hadi sasa ujenzi haujaanza kutokana kutotayarishwa michoro.
Kutokana na majibu hayo, Mtando hakuridhika hadi Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Issa Haji Ussi (Gavu), alipofafanua kuwa, uhaulishwaji huo umefanyika kisheria kwa vile Rais wa Zanzibar katika awamu iliyopita alikubali ombi hilo.
Nae Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alisema kuna baadhi ya gari za abiria zinazokatisha ruti kwa kukataa kuwafikisha abiria katika eneo wanalokwenda licha ya kupewa kibali cha kwenda huko, jambo ambalo linasababisha ajali.
Waziri Masoud alisema Idara ya Leseni inawaelekeza madereva na makondata hususani wa daladala, ambao wanakiuka taratibu hizo wakibainika wataadhibiwa ikiwa ni pamoja na kunyang'anywa leseni, kwani wanasababisha ajali.
Mapema akifanya majumuisho alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha inaimarisha ujenzi wa barabara zote za Unguja na Pemba ili kuwaondoshea usumbufu wananchi, ambapo katika bajeti ya mwaka huu alimuahidi Mwakilishi wa Kiwani Hija Hassan kujengwa barabara ya Jimbo hilo kwa kutengewa shilingi milioni 300.
Aidha alisema ujenzi wa jengo la abiria la Bandari yanafanyika mazungumzo na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), ili ijenge jengo hilo kuwawekea mazingira mazuri abiria.
Baraza hilo linajadili makadirio na mapato ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali iliyowasilishwa jana na Waziri wa Wizara hiyo, Ramadhan Abdalla Shaaban.

BILIONI 67 KUIJENGEA UWEZO ZAWA.

Bilioni 67 kuijengea uwezo ZAWA

Na Halima Abdalla
WIZARA ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, jana imetiliana saini na Kampuni ya Niras kutoka Denmark mradi wa kuijengea uwezo Mamlaka ya Maji (ZAWA) ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Hafla hiyo ilifanyika ukumbi wa jengo la Wizara hiyo Shangani mjini Zanzibar, ambapo kwa upande wa Zanzibar ilitiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA, Dk.Mustapha Ali Garu na Kampuni ya Niras ilisainiwa na mwakilishi wao Michael Juel.
Mradi huo utatumia zaidi ya shilingi bilioni 67 hadi kukamilika kwake na unatarajia kufaidisha zaidi ya watu 489,400 kwa kupatiwa huduma ya maji na usafi wa maskulini.
Akizungumza na watendaji kutoka Wizara ya Ardhi pamoja na wataalamu kutoka Kampuni ya Niras, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Mwalimu Ali Mwalimu, alisema mradi huo wa miezi 24 utaanza mwezi ujao.
Alisema mradi katika kipindi hicho utaweza kuisaidia Mamlaka ya Maji kwa kuwapa elimu ya kuweza kuwajengea uwezo kuweza kufanya kazi kwa ufanisi, kusambaza maji na kupeleka katika vijiji tisa vya Unguja na Pemba.
Aidha alisema mradi huo pia utaweza kusaidia uimarishaji wa rasilimali maji nchini na sehemu ya vianzio vya maji.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Niras, Michael Juel, alisema kampuni yake ina uwezo wa kutosha kuhakikisha yaliomo katika mkataba yanatekelezwa.
Aidha aliahidi kufanya kazi kama inavyotakiwa ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Dk. Garu kwa upande wake alisema ZAWA imefuata njia zote katika kuichagua kampuni ya Niras hivyo wana imani kampuni hiyo itatekeleza mradi huo kwa kiwango kinachokubaliwa.
Mradi huo ni seheu ya Mradi mkubwa wa maji unaoendeshwa Zanzibar kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ADB na UN-HABITAT.

ZANZIBAR KUTUMIA TAMASHA LA OMAN KUJITANGAZA KIUTALII

Zanzibar kutumia tamasha la Oman kujitangaza kiutalii

Na Salum Vuai, Maelezo
NAIBU Waziri wa Urithi na Utamaduni wa Oman, Hamed Bin Hilal El Maamary, ameishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuiandikia barua rasmi Serikali ya nchi yake iweze kulifanyia kazi ombi la kuanzisha kitivo cha lugha ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Ushauri huo aliutoa jana kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilahi Jihad Hassan, alipomtembelea na ujumbe wake, Waziri huyo kumsalimia na kuishukuru Serikali kwa mapokezi mazuri pamoja na kufanikisha tamasha la utamaduni la nchi yake.
Naibu Waziri huyo aliongoza tamasha hilo lililozinduliwa juzi huko Beit El Ajaib, alisema fikra ya kuitaka Oman ifungue kitivo hicho ni njema na inastahili kufanyiwa kazi haraka kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar na Oman.
Kutokana na umuhimu huo, alisisitiza haja ya kuwasilisha ombi rasmi na kuwahakikishia Serikali yake italipa uzito mkubwa kwa lengo la kukuza na kuendeleza uhusiano na mawasiliano kati ya wananchi wa nchi mbili hizo.
“Nimefurahishwa na fikra ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua tamasha letu, kuitaka nchi yangu ianzishe kitivo cha lugha ya Kiarabu (SUZA), hili linawezekana, naahidi kulifanyia kazi baada ya kupokea barua rasmi kutoka kwenu”, alifafanua.
Aidha, aliwasilisha salamu za Waziri wa Urithi na Utamaduni wa Oman, Haitham Bin Tariq Al Said kwa Waziri huyo na Serikali ya Zanzibar na wananchi wake na kusema kufanyika kwa tamasha la utamaduni la nchi yake hapa ni ishara njema na muhimu katika kuimarisha udugu wa damu wa wananchi wa nchi zao.
Akimkariri Waziri wake kupitia salamu hizo, El Maamary alisema tamasha hilo ni sehemu ya utekelezaji makubaliano yaliyofikiwa na nchi hizo katika mkataba uliotiwa saini baina yao Agosti 17, mwaka jana na kusisitiza haja ya kutanua wigo wa ushirikiano utakaoleta manufaa kwa wananchi wao.
Kwa upande wake, Waziri Jihad alisema ni matumaini yake kuwa wananchi wa Zanzibar watajifunza mengi kutokana na maonesho ya utamaduni yanayoendelea, na kwamba mavazi yanayooneshwa ambayo ni ya staha sawa na yanayovaliwa hapa, yatawapa changamoto ya ubunifu wa mitindo mipya.
Aidha, alisema mbali na uhusiano wa kiutamaduni, ziara ya ujumbe wa Oman itafungua milango ya kuimaraisha sekta ya utalii, kwani ujio wao unaitangaza nchi yao sambamba na wao kuinadi zaidi Zanzibar wakiwa nchini kwao na kwengineko wanakoendesha matamasha kama hayo.
Jihad aliuhakikishia ujumbe huo kulifanyia kazi pendekezo la Makamu wa Pili, na kwamba Wizara yake haitachelewa kuandika ombi rasmi la kuanzishwa kitivo cha lugha ya Kiarabu katika chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Alisema anaamini kuwa Wazanzibari wataweza kujifunza lugha hiyo kwa wepesi kutokana na lugha yao ya kiswahili kujengeka mno kwa misamiati ya kiarabu, pamoja na dini ya Kiislamu ambayo inasimama kwa msingi wa lugha hiyo.
Jihad alitumia fursa hiyo kuwakaribisha katika ufunguzi wa tamasha la utamaduni wa Mzanzibari lililopangwa kufanyika Julai 18, mwaka huu huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alimshukuru Naibu Waziri huyo, ujumbe aliokuja nao, na Serikali ya Oman kwa kuendeleza udugu wao na Zanzibar, na kuwatakia ziara ya furaha na marejeo mema watakaporudi kwao.
El Maamary pia alimzawadia Jihad zawadi ya kazi ya mkono iliyosanifiwa katika sahani ya fedha, inayoonesha ngome zinazotumiwa na Waomani katika mambo mbalimbali, pamoja na kumpa mualiko wa kufanya ziara Oman ili kuangalia maeneo na namna ya kufanya tamasha la utamaduni wa Zanzibar nchini humo.
Katika mazungumzo hayo, alikuwepo pia Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Majid Abdallah Al Abadi, watendaji wengine wa ofisi yake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Dk. Ali Mwinyikai, na maofisa wa ngazi za juu wa wizara hiyo.

MVUVI AHOFIWA KUPOTEA BAHARINI PEMBA

Mvuvi ahofiwa kupotea baharini Pemba

Na Zuhra Msabah, Pemba
MTU mmoja mwanamme, hajulikani aliko akisadikiwa kupotea baharini alikowenda kuvua katika kijiji cha Tumbe wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Rashid Bugi, alimtaja mtu huyo kuwa Mbarouk Faki Hamad (49) mkaazi wa Tumbe Shangani, ambaye aliondoka Julai 12 mwaka huu kwenda kuvua uvuvi wa madema kwa kutumia dau.
Kamanda Bugi alifahamisha kuwa Hamad aliondoka bandarini Tumbe saa 1:00 asubuhi ya siku hiyo lakini hadi ilipofika jioni hakuwa amerejea.
Kufuatia hali hiyo, Bugi alisema ndipo wananchi walipoamua kwenda kumtafuta, lakini kwa mshangao, walikikuta chombo chake kikielea bila yeye mwenyewe kuonekana.
Hadi wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana mvuvi huyo alikuwa hajaonekana wala kupata fununu zinazomuhusu na kueleza jitihada za kumtafuta zinaendelea.
Kamanda huyo alisisitiza kwa wavuvi kuacha tabia ya kwenda baharini mtu mmoja peke yake, ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa endapo kutatokea jambo lolote lisilotarajiwa.

WAZIRI wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Abdillah Jihad Hassan kushoto,akizungumza na Naibu Waziri wa Urithi na Utamaduni wa OmanHamed Bin Hillal Al Maamary ofisini kwake jana,kulia Balozi mdogo wa Oman Majid Abdallah Al Abadi,(Picha na Abdallah Masangu).

KAMPUNI MPYA YAJITOKEZA KUNUNUA MWANI KUSINI.

Kampuni mpya yajitokeza kununua mwani Kusini

Na Ameir Khalid
MKUU wa Wilaya ya Kusini Haji Makungu Mgongo amezishauri Kampuni zinazonunua mswani kujali maslahi wakulima wa zao hilo, kutokana na kazi nzito wanayoifanya.
Alisema zipo kampuni zinazojitokez kwa wakulima kununua zao hilo na kuangaza bei ya chini ya ununuzi wakiwa na lengo la kujinufaisha zaidi wakisahau ugumu wa kazi hiyo unaowakabili wakulima.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na uongozi wa kampuni ya Shopping Center, pamoja na wakulima wa zao hilo wakati wa kuitambulisha kampuni hiyo kwa wakulima.
''Huu ni wakati mzuri kwa wakulima kunufaika na jasho lao kwani endapo zitakuwepo kampuni nyingi za kununua mwani kila mkulima atakwenda anakotaka ambako anaona kuna maslahi na yeye''alisema.
Aliongeza kusema kuwa wilaya yake ipo tayari kukaribisha kampuni yoyote ambayo itakuwa miongoni mwa kampuni zitakazonunua zao hilo, baada ya kupata vibali na taratibu za biashara hiyo.
Mkurugenzi wa kampuni ya mwani shopping center Omar Haji, alisema kampuni yake imeamua kununua mwani kwa wilaya nzima ya Kusini kwa lengo la kuongeza kipato kwa wakulima wa zao hilo.
Alisema kampuni yake itajikurubisha zaidi kwa wakulima ili iweze kujua matatizo yanayowakabili, pamoja na kushirikiana nao ili mafanikio ya pande zote mbili yaweze kupatikana.
Aidha ameahidi kutoa vifaa mbali mbali ambavyo zinatumika katika kilimo cha zao hilo, bila ya malipo kwa lengo la kuwafanya wakulima hao wazidishe kulima kwa wingi.
Katika mkutano huo wakulima hao walielezea matatizo mbali mbali yanayowakabili katika kilimo cha mwani, ambapo waliomba zipatiwe ufumbuzi wake kwa lengo la kuongeza tija zaidi kwa zao hilo.
Miongoni mwa matatizo hayo ni ukosefu wa vifaa vya kulimia ikiwemo kamba, jambo linalochangia kurudisha nyuma utendaji wao.

VIJANA EPUKENI MAKUNDI YASIOPENDA KUJIELIMISHA - MWAKILISHI.

Vijana epukeni makundi yasiopenda kujielimisha-Mwakilishi

Na Khamisuu Abdalla
VIJANA wameshauriwa kujiepusha na makundi yenye mitizamo ya kubeza elimu na kujiingiza katika makundi yasiokuwa na maana ambayo wakati wote yanafikiria kutumia njia za mkato katika kuendesha maisha yao.
Akizungumza na wajumbe wa kituo cha (Suza American Conner) katika kuadhimisha miaka mitano ya kituo hicho, Mwakilishi wa Amani, Fatma Mbarouk Said, alisema huu ni muda muafaka kwa vijana kujihusisha na masomo badala ya kuzurura mitaani.
Alisema vitendo viovu ambavyo sehemu kubwa ya vijana wameviweka mbele haitawasaidia kuwaondoshea matatizo badala yake vinawaingiza kwenye vitendo viovu kila kukicha.
Aidha, mwakilishi huyo alisema pamoja na huduma ya Intaneti inayotolewa na kituo hicho lakini itakuwa haiwasaidii vijana hao kwa kuitumia kinyume na dhamira iliyokusudiwa.
Hata hivyo, Mwakilishi Fatma alisema kuwa amefurahishwa na uendeshaji wa kituo hicho kwa kuhusisha somo la kujifunza kingereza (American Corner English Club) na kuwataka kuitumia fursa hiyo hasa vijana wa kike ambao ni wachache kwenye klabu hiyo ikilinganishwa na vijana wa kiume.
Kiongozi wa klabu hiyo, Mbarouk Kheir Othman alisema kituo hicho kimeweza kuendesha programu tofauti za kuendesha maendeleo ya jamii kwa kushirikiana na taasisi zisizokuwa za kiserikali kama vile Ukimwi, dawa ya kulevya, Mtoto wa Afrika, Siku ya wanawake, Siku ya Wafanyakazi na pia kushirikiana na serikali na taasisi mbali mbali kuendesha programu hizo.
Alisema umefika wakati Baraza la Wawakilishi kutumia kituo hicho katika kuelimisha juu ya masuala ya uendeshaji wa shughuli za Baraza ili kituo hicho kichukue elimu hiyo na kusambaza kwa wananchi wa kawaida.
American Corner ni kituo kilichofadhiliwa na Wamarekani chini ya chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kilichofunguliwa Julai 13, 2006 na aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Michael Retzer.
Ujumbe wa mwaka huu kutoka kituo hicho "American Conrner ni Sehemu sahihi kwa kupata habari kuhusu Marekani".

Thursday, 14 July 2011

MAMIA WAMZIKA MZEE WA ASP.


Mamia wamzika mzee wa ASP
Na Mwandishi wetu
MAMIA ya wananchi wa Zanzibar na vitongoji vyake, jana walihudhuria maziko ya Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, mzee Masoud Sururu, aliyezikwa kijijini kwao Kiombamvua, Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mkoa wa Kaskazini, Unguja.
Maziko hayo yaliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia ni Rais (Mstaafu) wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume.
Aidha, viongozi wengine wa chama na serikali walihudhuria ikiwa ni  pamoja na Makamu wa Pili  Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Nchi (OMPR),  Mohamed Aboud Mohamed, baadhi ya Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM   na viongozi mbali mbali wa CCM  wa Mikoa mitatu ya Unguja.
Marehemu Sururu (89), alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) - Lugalo, mjini Dar es Salaam, baada ya kuugua maradhi ya kiharusi  kwa muda mfupi.
Wakati wa harakati za siasa, marehemu Sururu, alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa ASP katika miaka 1957, ambapo alibahatika kushika nyadhifa kadhaa ndani ya chama na serikali ikiwemo Mwenyekiti wa Tawi la ASP Mangapwani na Jimbo la Bumbwini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ASP na CCM, Ubunge pamoja na Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, wadhifa alioushikilia hadi kufariki kwake.
Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa mshituko, huzuni na masikitiko makubwa  taarifa ya kifo cha mzee Sururu, kwani kimekuja wakati huu chama hicho kikiwa  kimo katika harakati za kuleta mageuzi ya kiuongozi na Kiutendaji, ambapo hekima, busara na mchango wake, ulikuwa bado unahitajika katika kukijenga na kukiimarisha.
Hivyo, CCM imesema daima itamkumbuka marehemu Sururu, kutokana na ujasiri, uadilifu, ukaribu wake na watu wa rika na jinsia zote na kubwa zaidi alikuwa ni miongoni mwa wana CCM walioadiriki kutoa ushauri, nasaha, maelekezo katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi sio tu kwa maslahi ya chama, bali pia kwa taifa na wananchi wake.
Chama Cha Mapinduzi kimesema kinaungana na wanafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu wa mzee Sururu hasa katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na kwamba kinawaomba wawe na moyo wa subra kwa kuondokewa na mpendwa wa huyo.
Marehemu mzee Masoud Sururu Jumanne, ameacha vizuka wawili , watoto 14 na wajukuu kadhaa.
 Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema Peponi, Amiin.


MAMIA WAMZIKA MZEE WA ASP.


Mamia wamzika mzee wa ASP
Na Mwandishi wetu
MAMIA ya wananchi wa Zanzibar na vitongoji vyake, jana walihudhuria maziko ya Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, mzee Masoud Sururu, aliyezikwa kijijini kwao Kiombamvua, Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mkoa wa Kaskazini, Unguja.
Maziko hayo yaliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia ni Rais (Mstaafu) wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume.
Aidha, viongozi wengine wa chama na serikali walihudhuria ikiwa ni  pamoja na Makamu wa Pili  Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Nchi (OMPR),  Mohamed Aboud Mohamed, baadhi ya Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM   na viongozi mbali mbali wa CCM  wa Mikoa mitatu ya Unguja.
Marehemu Sururu (89), alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) - Lugalo, mjini Dar es Salaam, baada ya kuugua maradhi ya kiharusi  kwa muda mfupi.
Wakati wa harakati za siasa, marehemu Sururu, alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa ASP katika miaka 1957, ambapo alibahatika kushika nyadhifa kadhaa ndani ya chama na serikali ikiwemo Mwenyekiti wa Tawi la ASP Mangapwani na Jimbo la Bumbwini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ASP na CCM, Ubunge pamoja na Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, wadhifa alioushikilia hadi kufariki kwake.
Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa mshituko, huzuni na masikitiko makubwa  taarifa ya kifo cha mzee Sururu, kwani kimekuja wakati huu chama hicho kikiwa  kimo katika harakati za kuleta mageuzi ya kiuongozi na Kiutendaji, ambapo hekima, busara na mchango wake, ulikuwa bado unahitajika katika kukijenga na kukiimarisha.
Hivyo, CCM imesema daima itamkumbuka marehemu Sururu, kutokana na ujasiri, uadilifu, ukaribu wake na watu wa rika na jinsia zote na kubwa zaidi alikuwa ni miongoni mwa wana CCM walioadiriki kutoa ushauri, nasaha, maelekezo katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi sio tu kwa maslahi ya chama, bali pia kwa taifa na wananchi wake.
Chama Cha Mapinduzi kimesema kinaungana na wanafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu wa mzee Sururu hasa katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na kwamba kinawaomba wawe na moyo wa subra kwa kuondokewa na mpendwa wa huyo.
Marehemu mzee Masoud Sururu Jumanne, ameacha vizuka wawili , watoto 14 na wajukuu kadhaa.
 Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema Peponi, Amiin.