Tuesday, 28 June 2011

MAALIM SEIF WANAFUNZI WAHAMASISHWE MASOMO YA SAYANSI

Maalim Seif: Wanafunzi wahamasishwe masomo ya sayansi

Na Abdi Shamnah, Morogoro
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wahitimu wanaomaliza masomo yao katika Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, kuwahamasisha wanafunzi kuyapenda masomo ya sayansi ili kukidhi mahitaji ya serikali ya kuwa na wataalamu wa kutosha.
Maalim Seif alitoa changamoto hiyo katika ukumbi wa hoteli ya Bene mjini Morogoro, kwenye hafla iliyoandaliwa na Jumuiya ya ZAMUMSA (Zanzibar University of Muslim Sudents Association), inayowashirikisha wanafunzi kutoka Zanzibar walio katika chuo hicho.
Alisema hatua hiyo inatokana na tatizo la msingi linaloikabili Zanzibar ambapo wahitimu wake wengi ni wale waliojikita katika masomo ya sanaa (art), hali inayoongeza idadi ya wasomi wanaobaki bila ya kuajiriwa, hususan katika sekta ya elimu, baada ya wizara hiyo kusheheni wahitimu wa kada hiyo.
Aliwataka wahitimu hao kulipa uzito unaostahili suala hilo kwa kuzingatia ushindani uliopo mbele yao katika soko la ajira, hususan pale Jumuiya ya Afrika Mashariki itakapoanza kufanyakazi rasmi.
Akizungumzia kushuka kwa kiwango cha elimu Zanzibar, Maalim Seif alisema tatizo hilo linatokana na sababu kadhaa, ikiwemo ya ukosefu wa walimu wenye uwezo wa kutoa elimu bora itakayomuwezesha kijana wa Kizanzibari akimaliza masomo yake kumudu kufanya kazi mahala popote pale Afrika Mashariki.
Alisema serikali ina mipango ya kuzipatia skuli vifaa vyote ikiwemo vitabu na maabara ili kuwawezesha wanafunzi kuendana na wakati uliopo wa Sayansi na Teknolojia.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona skuli za Zanzibar zinashika mkia katika mitihani ya kitaifa kidato cha nne na sita kila mwaka, huku skuli ya SOS pekee ikifanya vizuri kwa kile kinachoonekana kuwepo katika mazingira mazuri.
Katika hatua nyingine Maalim Seif aliwataka wahitimu hao watarajiwa kuwa wazalendo na kurudi nyumbani kulitumikia Taifa badala ya kuendekeza fedha mbele na kwenda nje ya visiwa hivyo kufanyakazi.
Nae Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Kusini Pemba Mohammed Habibu Mnyaa, aliwataka wahitimu hao kuondokana na dhana potofu kuwa ajira ni ile itokanayo na serikali pekee na badala yake kuangalia umuhimu wa elimu na kuibua njia za kujiajiri.
Mbunge huyo aliitupia lawama Bodi ya Mikopo Tanzania kwa kujenga mazingira yanayowafanya wasichana kujiingiza katika vitendo vya uasharati kutokana na udhaifu wa bodi hiyo, huku serikali ikipaza sauti kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.
Katika risala yao wahitimu watarajiwa, walimweleza Makamu wa kwanza wa Rais, juu ya hali ya elimu Zanzibar na mustakbali wake na kuainisha matokeo mabaya kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita.
Wakitolea mfano walisema katika mwaka wa 2011, ni wanafunzi watatu tu ndio waliofanikiwa kupata kiwango cha daraja la kwanza kisiwani Pemba, huku kutoka Unguja kukiwa na wanafunzi sita pekee kutokana maelfu ya watahiniwa wa kidato cha sita.
Jumla ya wahitimu 93 wanatarajiwa kumaliza masomo yao, ikiwa ni muhula wa nne wa chuo hicho, ambapo kati ya wanafunzi hao asilimia 40 ni kutoka Zanzibar, huku wahitimu 50 tayari wakiwa wameshajaza fomu za kuomba ajira katika sekta tofauti Tanzania Bara.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na watu mbali mbali, wakiwemo wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya MUM, Mzumbe, UDSM, UDOM pamoja Wabunge mbali mbali wakiwemo wale wanaotoka Zanzibar.

BALOZI SEIF ATAKA VIONGOZI WASHIRIKI KUTEKELEZA ILANI YA CCM

Balozi Seif ataka viongozi washiriki kutekeleza ilani ya CCM

Na Mwantanga Ame
AHADI ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwatunza wazee, imeanza kutekelezwa kwa vitendo na baadhi ya Wawakilishi, kwa kujitolea kuwapatia misaada wastaafu waliokuwa wakitumikia serikali wa Jamhuri ya Muungano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alipokea misaada hiyo jana baada ya Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo, Nassor Salum Ali ‘Al-Jazira’, Mbunge wa Jimbo hilo Abdalla Juma Mabodi na mfanyabiashara Amani Makungu kuwasaidia shilingi 700,000 kwa ajili ya wazee hao.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana kati ya Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi na Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo, Nassor Salum, katika Chumba cha Maalum cha Wageni mashuhuri ndani ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mwakilishi huyo alisema wameamua kutoa fedha hizo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kuitekeleza ilani ya CCM ambayo imeahidi kuwatunza Wazee pamoja na makundi mengine.
Alisema wazee wastaafu ni moja ya hazina muhimu kwa taifa na suala la kuwapa matunzo ni moja ya jambo linalohitajika kuzingatiwa na jamii yote.
Kutokana na umuhimu huo, alisema ndio maana Chama cha Mapinduzi katika ilani yake kimeamua kwa makusdi kuhakikisha inawapa kipaumbele wazee kwa kuwapatia matunzo bora.
Alisema hatua hiyo ya serikali ni sehemu ya kuendeleza malengo ya chama cha A.S.P ambacho kimeahidi kuwapa makaazi mema wazee pamoja na kuwatunza.
Nae Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, alisema serikali inafarajika kuona viongozi wake wamekuwa wakishiriki kuitekeleza vyema ilani ya CCM katika suala zima la kuwatunza wazee kwani ni moja ya mambo ya msingi iliyoahidi katika kampeni zake.
Alisema serikali itahakikisha utekelezaji wa ilani unaenda sambamba kwa kuwashirikisha wazee katika shughuli mbali mbali zikiwemo za maendeleo ikiwa ni moja ya hatua muhimu ya kuwafanya kujisikia kuitumikia nchi yao.
Alisema mchango wa Wazee ni muhimu katika maendeleo ya Zanzibar kutokana na ndio uliosababisha kulifanya taifa hili kuwa huru hivi sasa na haiwezekani wazee kuachwa nyuma.
Alisema ingawa kuna changamoto nyingi za maisha zinazowakabili wazee lakini serikali itahakikisha inapambana nazo na kuitaka jamii kuona nayo inashiriki kuwapatia misaada wazee ili wawe katika maisha mazuri.
Balozi Seif, aliahidi kutimiza ahadi yake ya kuwapatia wazee hao shilingi milioni 1,000,000 ikiwa ni mchango wake kwa Wazee wastaafu wa Muungano.
Mapema mwezi uliopita wazee hao walikabidhiwa boti moja na mashine kwa ajili ya kufanya shughuli zao za maendeleo pamoja na charahani na Mfanyabiashara Mohammed Raza, sherehe ambayo ilifanyika katika viwanja vya bahari ya Kizingo na kuendeshwa harambee iliyochangisha shilingi milioni nne za ahadi na fedha halisi shilingi 400,000.
WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad, akipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana juu ya tuhuma za rushwa dhidi ya Serikali, zilizoandikwa na gazeti moja la kila wiki (sio Zanzibar Leo) kuhusiana na kiwanja cha Ndege Kisiwani Pemba. (Picha na Abdallah Masangu). 

KUNA MATUMAINI MAKUBWA ZANZIBAR KUENDELEA - WB

Kuna matumaini makubwa Zanzibar kuendelea – WB

• Dk.Shein: Viongozi SMZ wamejidhatiti kufikia malengo
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
BENKI ya Dunia imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo na kueleza matumaini yake kutokana na juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha uchumi na huduma za kijamii.
Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, John Mclntire, aliyasema hayo jana alipofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kuaga na kuzungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
McIntire alimueleza Dk. Shein kuwa Benki ya Dunia inathamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuziimarisha sekta zake za maendeleo hatua ambayo Benki hiyo imeingia moyo kuisaidia Zanzibar.
Alisema Benki ya Dunia itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katikia kuimarisha sekta zake za maendeleo kwa kutambua malengo yaliyowekwa katika kuimarisha uchumi na maendeleo hapa nchini.
McIntire ametoa shukurani kwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar na uongozi wake kwa kutoa mashirikiano makubwa ambayo yameweza kufanya kazi zake kwa ufanisi katika kipindi chote cha miaka minne aliyofanya kazi Tanzania.
Aidha, katika maelezo yake Mkurugenzi huyo Mkaazi alimueleza Dk. Shein matumaini yake makubwa kwa Zanzibar katika kujiletea maendeleo.
Nae Dk. Shein alitoa pongezi kwa Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana vyema na Zanzibar hatua ambayo imepelekea kupata maendeleo na mafanikio makubwa katika miradi ya maendeleo.
Alisema juhudi za Mkurugenzi huyo zimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa uimarishaji wa miradi ya maendeleo hapa Zanzibar na kutoa pongezi zake za dhati kutokana na jitihada zake hizo.
Dk. Shein alisema kuwa McIntire amefanya kazi kubwa katika uongozi wake kwenye Benki hiyo hapa Tanzania na kueleza kuwa juhudi zake zitaendelea kuthaminiwa na kukumbukwa licha ya yeye kutokuwepo nchini.
Aidha, Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi huyo kuwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa pamoja wamedhamiria kufanya kazi kwa mashirikiano na juhudi kwa lengo la kuiletea maendeleo Zanzibar kwa kuelewa kuwa mabadiliko ni suala la lazima.
Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa mabadiliko hayo ni pamoja na kuhakikisha miradi yote ya maendeleo wanaisimamia vilivyo na kwa umahiri mkubwa kutokana na kutambua umuhimu wake katika maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Benki ya Dunia imeweza kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira ya Bahari na Viumbe wa Baharini (MACEMP), TASAF, Mradi wa BEST na miradi mingineyo.
Pia, Benki ya Dunia imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Zanzibar kwenye kuendeleza mradi wa ujenzi wa skuli mpya za kisasa za Sekondari Unguja na Pemba ambazo zimefikia hatua nzuri ya ujenzi.
Sambamba na hayo Benki ya Dunia ilitoa ushirikiano wake mkubwa katika ujenzi wa njia ya kurukia na kutulia ndege katika kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume Zanzibar.
Aidha, Benki ya Dunia imeweza kuunga mkono ujenzi wa miundombinu ya barabara zikiwemo barabara za ndani ya mji wa Zanzibar na zile za nje ya mji ikiwemo barabara ya Mahonda-Kinyasini na Mkwajuni-Mkokotoni.

WAWAKILISHI WAPINGA UCHIMBAJI MATOFALI PEMBA.

Wawakilishi wapinga uchimbaji matofali Pemba

Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI imeshauriwa kuzuia ukataji wa matofali katika kisiwa cha Pemba hadi hapo patakapotolewa muongozo wa kutayarishwa kanuni za udhibiti na utunzaji wa mazingira kutokana kujitokeza uharibifu mkubwa.
Ushauri huo umetolewa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa juu ya utekelezaji wa bajeti ya Ofisi wa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Mwanajuma Faki Mdachi wakati akichangia katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja.
Alisema ni vyema Serikali ikazuia ukataji huo ili kudhibiti uharibifu wa mazingira usiendelee Pemba kunakosababishwa na ukataji wa matofali, ambapo aliwashutumu viongozi na wanasiasa wanachangia katika kadhia hiyo.
“Sisi viongozi wanasiasa tunachangia eti vijana watafanya kazi gani hapa duniani kuna kazi nyingi za kufanya ambapo mtu atapata riziki bila ya kuhifadhi mazingira ambayo huko mbele wakeshaacha mashimo makubwa na ardhi ikiwa haifai tena, vizazi vijavyo wataishi vipi na kama wazee wao walikata miamba kukawa na mashimo kama wanavyoyaacha hivi sasa wao wangeliridhika”, alihoji Mwanajuma Mdachi.
Aidha alitaka Wizara ya Miundombinu waache tabia ya kuchimba vifusi kwa miradi ya ujenzi wa barabara hasa inayofanywa na wafadhili bila ya kushauriana na kupata miongozo kutoka Idara ya mazingira ambapo wajenzi wakeshaondoka huacha mashimo makubwa, jambo ambalo huifanya ardhi isiweze kutumika tena.
Alieleza licha ya uchimbaji huo unaelekeza kulipwa kodi kwa asilimia 10 katika Idara ya Mazingira lakini fedha hizo hazilipwi, ambapo uharibifu unapotokea kunakuwa hakuna nyezo za kuweza kurejesha hali hiyo.
Makamu Mwenyekiti huyo, alishauri Idara kuainisha maeneo ya vianzio vya maji ili kuvihifadhi visikatwe miti na kutoa muongozo wa upandaji wa miti inayosaidia kuongeza maji ardhini ili kuzifanya chemchem ziendelee kutoa maji kwa wingi na kwa muda mrefu bila ya kukauka.
Alifahamisha kuwa, jamii ikatae matumizi ya mifuko ya plastiki lakini pia jitihada za makusudi zinahitajika kuzuia uingizwaji wa mifuko hiyo nchini, ambapo jitihada kubwa zielekezwe katika kuifanyia marekebisho sheria ya utunzaji wa mazingira ambayo inaonekana kutoa mwanya kwa waingizaji na watumiaji wa mifuko hiyo.
Aliongeza kwamba, baada ya marekebisho hayo utekelezaji wa sheria iweke bayana kwa yule atakayekwenda kinyume achukuliwe adhabu kali ili kukomesha vitendo hivyo.
Akichangia katika Idara ya Watu Wenye Ulemavu alisisitiza kutekelezwa kwa sheria ya ujenzi wa majengo rafiki kwa walemavu, kwani inaonekana dhahiri wajenzi wengi hususani majengo ya Serikali yanajengwa bila ya kuzingatia mahitaji ya walemavu hivyo atakwenda kinyume achukuliwe hatua kali za kisheria.
Nae Mwakilishi wa Magomeni, Salmin Awadh akichangia katika bajeti hiyo, alisema uchafu wa mazingira uangaliwe upya kwa vile mji ni mchafu, ukianzia Mji Mkongwe na maeneo mbali mbali ya mji wa Zanzibar hali ambayo inaweza kuathiri mapato yanayotokana na utalii kutokana na hali hiyo.
Hata hivyo, alipendekeza kupandishwa kwa miti kwa wingi katika kuleta haiba nzuri na uhifadhi wa mazingira Zanzibar katika kulinda rasilimali iliyopo.
Mwakilishi wa Mji Mkongwe Ismail Jussa alihoji fungu kubwa la fedha kwa Tume ya UKIMWI Zanzibar zilizotengewa ukiacha Idara nyengine ikiwemo ya dawa za kulevya.
Ali Waziri Fatma Fereji akijakufanya majumuisho amueleze fedha hizo zilizotengwa zitawanufaisha vitu watu wenye virusi vya UKIMWI, au zitatumika kwa semina ya mafunzo kwa watendaji na wengine wakijigawia mapesa, ambapo akitolea mfano wa Jumuiya ya ZAPHA+ katika bajeti hiyo haikuanisha kwamba wanawasaidia vipi watu wanaoishi na VVU kwani wanaishia omba omba.
Mwakilishi Rashid Seif wa Ziwani, alisema nyumba za kurekebisha tabia ziongezwe kwani zinawasaidia vijana wanaoacha dawa za kulevya, sambamba na kuomba Serikali iwasaidia fedha nyumba hizo kwa vile zinajiendesha wenyewe, ambapo alihoji misaada mbali mbali ya wahisani wanaoitoa hadi shilingi milioni 10 lakini aliuliza ni kweli zinawafikia walengwa isijekuwa watu wanagawana na zilizobaki kama 200,000 ndio zinapelekwa kwa walengwa.

Thursday, 23 June 2011

DK. SHEIN VIONGOZI CCM MSIDANYANYIKE

Dk.Shein: Viongozi CCM msidanganyike
Na Rajab Mkasaba, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, amewaeleza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuwa wasidanganyike na kauli kuwa hali ya maisha na kupanda kwa bei ya bidhaa imesababishwa na CCM, serikali iliyoko madarakani ama viongozi wake.
Dk. Shein aliyasema hayo kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya kuzungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya ya Mkoani na wilaya ya Chake Chake Pemba akimalizia mfululizo wa ziara zake za kuzungumza na viongozi wa CCM wa ngazi zote kuanzia ngazi za Shina, Tawi, Wadi, Jimbo, Wilaya hadi Mkoa Unguja na Pemba.
Dk. Shein aliwataka viongozi hao wajue na watoe maelezo kwa wale wasiofahamu kuwa hali ya kupanda kwa maisha inatokana na kupanda kwa bei ya bidhaa za vyakula katika soko la dunia.
Alisema kuwa viongozi wanapaswa waelewe kuwa uongozi ulioko madarakani, serikali na Chama kinachoshika hatamu hakiusiani na suala la mfumko wa bei kwani hilo ni tatizo la wote na kikubwa kinachofanywa na seikali yake hivi sasa ni kukabiliana na tatizo hilo kwa kukiimarisha kilimo.
Dk. Shein alisema kuwa serikali imo katika mikakati maalum ya kuimarisha sekta hiyo kwa kuhakikisha Mapinduzi ya Kilimo yanafikiwa kwa kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza pembejeo na utaalamu wa kilimo kwa kuzalisha chakula kwa wingi na chengine kuweka akiba.
Alisema serikali anayoiongoza imeandaa mipango imara ya kuhakikisha sekta ya kilimo inapiga hatua ikiwa ni pamoja na kukiimarisha kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji, kilimo cha mazao kama muhogo na viazi kwa kutoa mbegu bora pamoja na kuimarisha kilimo cha matunda na mbogamboga.
Aidha Dk. Shein aliwataka viongozi waliopata nafasi za uongozi kutowakimbia wanachama na viongozi wa ngazi za chini wakiwemo viongozi wa Matawi na kusisitiza kushirikiana pamoja katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Dk. Shein alisema kuwa wakati wakitafuta nafasi za uongozi walikuwa karibu na wanachama kwa hali zote usiku na mchana, lakini analoshangazwa kuwaona viongozi hao kuwakimbia viongozi wenzao na wanachama ambao wametoa mchango mkubwa kupata uongozi wao.
Dk. Shein pia, amewataka viongozi hao kushirikiana na viongozi wa ngazi za chini kwa lengo la kuwaeleza mafanikio yaliopatikana nchini ikiwa ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika kutekeleza Ilani ya CCM kwa muda mfupi.
Katika maelezo yake alisema kuwa tayari hatua za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM zimeanza kuchukuliwa kwa kasi ikiwa ni pamoja na kufanya semina ya viongozi wa Serikali nzima kwa kueleza namna ya kufanya kazi ili kuwatumikia wananchi.
Dk.Shein pia, alisisitiza kuwa ajira zitaongezwa na pale patakapokuwa na ajira za serikali vijana wataajiriwa na patakapotokea fursa ya kusaidiwa ili wajiajiri wenyewe watasaidiwa kwani suala la ajira limezungumzwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Dk. Shein amemaliza ziara yake kwa kuzungumza na viongozi wa Wilaya 10 za Unguja na Pemba ambapo pia, katika mazungumzo hayo aliwaahidi kuwa wakati mwengine atakapofanya ziara zake kama hizo itakuwa ni zamu yao kuzungumza, kuuliza, kuchangia, kuhoji ana kwa ana na yeye atawasilikiza na hatimae kutoa majumuisho.
Kwa upande wa maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya Umma, Dk. Shein alisema kuwa tayari taratibu zimepangwa katika kuhakikisha wafanyakazi za serikali wanafanyiwa makerekebisho katika mishahara yao sambamba na kuangaliwa suala zima la pencheni.
Nao viongozi wa CCM Wilaya hizo walimpongeza Dk. Shein kwa kazi kubwa anayoifanya katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi. Pia, walitoa shukurani kwa Mama Mwanamwema Shein kwa kushiriki kikamilifu katika kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, alieleza kuwa ziara za Rais zimetoa miongozo mikubwa katika kukiimarisha chama hicho na kumuhakikishia kuwa kwa kushirikiana na viongozi wenzake wote kuanzia Shina hadi Mkoa wa Unguja na Pemba watazifanyia kazi.

DAWA MCHANGANYIKO ZA MALARIA BURE.

Dawa mchanganyiko za malaria bure

Na Mwanajuma Abdi
WAZIRI wa Afya, Juma Duni Haji ameeleza sababu zilizochelewesha Zanzibar kuanza kwa mradi wa upatikanaji wa dawa za mchanganyiko 'artemisinin' za kutibu malaria kwa bei nafuu ulioanza mwaka jana na kumalizika mwaka 2012, ni kutokana upatikanaji wa fedha za uagiziaji dawa hizo na kuziingiza nchini.
Hayo aliyasema jana, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa mradi huo, ambapo kitaifa utazinduliwa leo katika viwanja vya Tumbaku, Miembeni mjini hapa.
Mradi huo kwa Zanzibar utatumia shilingi milioni 700 hadi utakapokamilika kwa awamu ya kwanza, ambapo tathmini yake itafanyika Novemba mwaka huu kwa nchi zote nane kwa lengo la kuangalia mafanikio ili nchi nyengine ziweze kuingizwa katika mpango huo awamu nyengine.
Alisema mradi wa upatikanaji wa dawa bora na sahihi za kutibu malaria kwa gharama nafuu ulianza mwaka 2010 na kumaliza mwaka 2012, ambapo nchi nane kutoka katika Bara la Afrika na Asia zimebahatika kuwa miongoni mwa nchi hizo lakini Zanzibar ilishindwa kuanza kwa wakati kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo upatikanaji wa fedha za kuagiza dawa hizo na kuziingiza nchini.
Alizitaja nchi hizo, ni Cambodia, Ghana, Kenya, Madagascar, Niger, Nigeria, Tanzania Bara na Uganda, ambapo na Zanzibar imeingia kama nchi katika mradi huo, unaofadhiliwa na wahisani mbali mbali duniani ambao waliamua kuunganisha nguvu zao kwa pamoja na kuanzisha Mfuko wa Fedha wa Dunia (Global Fund) wa kupambana na UKIMWI, TB, na malaria, ambao mfuko huo unasaidia zaidi ya nchi 100.
"Dawa hizi kimsingi bado zina gharama kubwa kuzinunua, lakini kutokana na makubaliano ya nchi husika zitafaidika na punguzo la takribani asilimia 95 zitalipwa kupitia mfuko wa 'Global Fund' na kufanya dawa ziuzwe kwa gharama nafuu kabisa kwa walengwa na asilimia tano zitalipwa na nchi husika", alisema Duni.
Alieleza dawa za mchanganyiko wa 'artemisinin' zilikuwa zinauzwa kwa bei ya juu baina ya shilingi 6,000 hadi 12,000, jambo ambalo lilisababisha wagonjwa wengi kushindwa kumudu gharama hizo, ambapo kwa sasa katika vituo vya afya vya Serikali zitatolewa bure na katika maduka ya dawa na hospitali binafsi zitauzwa kwa dozi ya mtu mzima isiyozidi shilingi 1,000 na mtoto isiyozidi shilingi mia nane.
Waziri Duni alifafanua kuwa, dawa hizo zina chapa ya alama ya jani lenye maandishi yanayosomeka 'ACTm', ambapo jani hilo linatokana na mti wenyewe asili uliotengenezewa, hivyo jamii ina jukumu na kuhakikisha kuzitambua dawa hizo, sambamba na kuuziwa kwa bei iliyopendekezwa na Serikali na si vyenginevyo.
Alitoa onyo kwa wauza dawa kuwa sio ruhusa kuuza dawa hizo kwa mtu asiyekuwa hana cheti cha daktari, ambapo aliwataka madaktari kufuata maadili yao ili kuepusha uibaji wa dawa hizo katika hospitali za Serikali na kuziuza vituo binafsi kwani atayepatikana na kadhia hiyo atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Aidha alitanabahisha kwamba, dawa nyengine mchanganyiko ambazo hazina alama hiyo, zinakubalika kutibu malaria ila hazihusiki katika punguzo la bei hiyo, hivyo bei zake zitategemea na soko huria la dawa.
Duni alitahadharisha kwamba baadhi ya malengo yaliyokuwemo katika mradi huo ni pamoja na kuhakikisha kuwa kila duka la dawa, hospitali na vituo vya afya vya sekta binafsi zinatunza na kuuza dawa hizo kwa bei iliyopangwa, kutunza kumbukumbu zote za manunuzi ya dawa na mauzo kwa ajili ya ukaguzi.
Aliongeza kusema kwamba, mazingatio mengine ni kuruhusiwa kwa wafadhili kukagua na kupewa taarifa ya mwenendo wa mradi huo kwa sekta binafsi na serikalini na kuhakikisha kuwa dawa hizi hazivuki mipaka ya Zanzibar na kuuzwa katika nchi ambazo hazishiriki katika mradi huo kwani kufanya hivyo itakuwa kwenda kinyume na mkataba.
Hata hivyo, alisema ripoti za Shirika la Afya Duniani zinakadiria takribani wagonjwa 225 milioni waliugua malaria mwaka 2009 na idadi ya vifo kutokana na malaria ilikuwa 781,000 kwa dunia mzima.
Alisema kwa Zanzibar tafiti zinaonyesha mwezi Mei hadi Julai mwaka jana takwimu zinasema kiwango cha maambukizi ya malaria kimeshuka hadi kufikia asilimia 0.07 tofauti na takwimu za mwaka 2007 zilionesha asilimia 0.8.
Alifahamisha kuwa, kutokana na ripoti hizo bado malaria ni janga la kimataifa linalozikabili nchi nyingi hasa zinazoendelea kusini mwa jangwa la Sahara, ambao unaendelea kuua maelfu ya watu duniania na hasa watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka mitano na kinamama wajawazito.
Wakati huo huo, Mratibu wa Mradi huo, Shija Joseph alitoa wito wakati akiwafunda wenye maduka ya vituo vya watu binafsi kuhakikisha wanauza dawa hizo kutokana na vigezo vilivyowekwa ili kuwafikishia huduma hiyo wananchi walio wengi na sio kama awali wachache ndio waliweza kumudu gharama za dawa hizo.
Alisema mradi huo unalenga kuwasaidia wananchi na kuokoa maisha ya watu kutokana na ugonjwa hatari wa malaria, ambapo aliushukuru Mfuko wa Fedha wa Dunia kwa kusaidia sehemu kubwa ya gharama za dawa hizo.

MAGENDO YA KARAFUU YAIKOSESHA ZANZIBAR DOLA MILIONI 16

Magendo ya karafuu yaikosesha Zanzibar dola milioni 16

• SMZ yapanga mkakati kudhibiti bei
• Yasisitiza mafuta kutolewa kwenye muungano
Na Ramadhan Makame
SERIKALI katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, imepoteza kiasi cha dola za Marekani milioni 16, kutokana na vitendo vya usafirishaji nje kwa magendo zao la karafuu.
Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui alilieleza Baraza la Wawakilishi lililopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipokuwa akichangia bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012.
Waziri huyo alisema vitendo vya usafirishaji magendo karafuu nje ya Zanzibar vimekuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Zanzibar kutoka na kuikosesha mapato serikali.
Mazrui alisema usafirishaji magendo wa zao la karafuu limeifaya nchi ya Kenya kuwa muuzaji mashuhuri wa zao la karafuu kwa zaidi ya tani 2,000 katika soko la dunia huku ikizingatiwa kuwa katika nchi hiyo hakuna mikarafuu inayolimwa.
“Nawasihi sana, tuache kuuza karafuu kwa magendo, zao la karafuu litumike kuwanufaishana wananchi wa Zanzibar. Serikali itapandisha bei nzuri sana na ni lengo letu kukifufua kilimo cha karafuu”, alisema waziri huyo.
Akizungumzia suala la Zanzibar kuwa bandari huru, alisema kuna kampuni imeajiriwa kulifanyia utafiti la kuifanya Zanzibar kuwa ni miongoni mwa eneo tengefu kiuchumi.
Alisema baada ya ripoti kukamilika itawasilishwa katika baraza la wawakilishi kupata michango ya viongozi hao na kuifanya Zanzibar kuwa nchi itakayokuwa uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa.
Akizungumzia juu ya tatizo la upandaji ovyo wa bei za vyakula alisema upo mpango ambao utahakikisha uwekaji wa bei za bidhaa muhimu za vyakula unashirikisha baina ya serikali na wafanyabishara.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Makazi Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna alisema serikali ya awamu ya saba imesimama pale pale kwa kusema kuwa mafuta na gesi asili lazima yatolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.
Waziri huyo alisema shindikizo la kutaka kuiondoa rasilimali hiyo katika mamlaka ya Muungano lazima lifikishwe Bungeni kwa ajili ya kuondolewa kwani suala la uchumi si katika mambo ya Muungano.
Alisema katika visiwa vyote vya Unguja na Pemba kUna akiba kubwa ya gesi asilia na wala hakuna ubishi wa kufanywa utafiti wa mafuta kwani yapo ya kutosha.
Naye Fatma Abdulhabib Ferej alisema kutokana na serikali kutopandisha kodi, ni vyema msisitizo na mkazo ukawekwa katika kudhibiti mvujo wa mapato, wigo wa kuongezwa ukusanyaji mapato, kuondosha misamaha ya kodi pamoja na kupunguza matumizi ya serikali.
Aidha waziri huyo alionesha kuridhishwa kutokana na bajeti hiyo kutoa vipaumbele zaidi katika sekta za jamii ikiwemo afya, elimu na maji huku akisema kuwa hizo ndizo kero zinazowakabili Wazanzibari.
Bajeti hiyo ilitarajiwa kupitishwa jana jioni baada ya kuchangiwa na wajumbe kadhaa za Baraza hilo na waziri wa Nchi Ofisi Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo kufanya majumuisho.

JAMII YAHIMIZWA KUWATUNZA YATIMA, WZEE.

Jamii yahimizwa kuwatunza yatima, wazee

Na Mwantanga Ame
JAMII imeshauriwa kujenga utamaduni wa kuwapenda kwa kuwatunza watoto yatima na wazee ikiwa ni hatua ya msingi itayoweza kufuata misingi ya maadili ya marehemu Mzee Karume.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Seif Iddi, aliyasema hayo jana baada ya kuwakabidhi televisheni tatu Wizara ya Ustawi wa Jamii na maendeleo ya Wanawake na Watoto kwa ajili ya Watoto yatima wa Mazizini, Wazee wa Sebleni na Welezo ambapo kwa kila moja ina thamani ya shilingi milioni 1.5.
Sherehe ya makabishiano hayo ilifanyika Makao Makuu ya Wizara hiyo huko Vuga Mjini Zanzibar ambapo Mama Asha aliwataka viongozi wa Wizara hiyo kuona wanaendeleza maadili ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume kuwapenda watoto na wazee.
Alisema Rais Karume aliyapenda makundi hayo kwa kuona nao wanakuwa katika hali nzuri ya kimaisha na ndio maana baada ya Zanzibar kuwa huru aliamua kuanzisha nyumba za wazee pamoja na nyumba za watoto yatima.
Alisema kutokana na kuthamini utamaduni huo ndio maana serikali zote zimeamua kuona makundi hayo yanaendelea kupatiwa matunzo bora ya maisha na haitakuwa busara kuacha kuendeleza maadili hayo.
Alifahamisha kuwa serikali ya awamu ya saba itahakikisha inaendeleza maadili hayo ya Mzee Karume kwa kuwajali Wazee pamoja na watoto yatima kila pale inapoona haja ya kuwa nao pamoja.
Hata hivyo Mama Asha, aliwataka viongozi wa Wizara hiyo kuona wanawapa umuhimu wazee pale inapojitokeza kutaka kupatiwa msaada wa fedha kutokana na baadhi yao hujitokeza maofisini kuhitaji msaada baada ya kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
“Kuna watu wanaweza kuwajia kuwaomba hata 500 ya nauli baada ya kwenda hospitali sasa msije mkawadharau kuwapa msaada wasaidieni kwani ukitoa moja Mungu atakupa nyengine tuwaenzini wazee” alisema Mama Asha.
Aidha, Mama Asha, aliwataka viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo, kumpa ushirikiano mzuri Katibu Mkuu mpya kwa kuona kuwa wote ni wamoja kwa vile Wizara hiyo inatarajiwa kuwa kiungo kizuri cha kuwaunganisha wanawake kote nchini.
Nae Waziri wa Wizara hiyo, Zainab Omar Mohammed, akitoa shukrani zake, alisema msaada huo utawawezesha walengwa kujenga upeo wao bora kwa kupata habari matukio na taarifa za maeneo mbali mbali duniani na ndani ya nchi.
Waziri huyo aliahidi kuwa msaada huo unawafikia walengwa ili waweze kuwaelimisha walengwa waliokusudiwa yakiwemo makundi hayo.
Waziri huyo alitoa wito kwa jamii kuiga mfano huo wa kutoa misaada yao kwa hali na mali kwani bado kutoa sio kama wanacho bali kuyasaidia makundi hayo ili nayo yawe katika hali nzuri za kimaisha.
Wakati huo huo, Mama Asha alikabidhi msaada kama huo ikiwemo na mashine ya DVD, kwa kituo cha Polisi cha Mfenesini na kuwataka askari hao kukitumia chombo hicho kuweza kufuatilia mambo mbali mbali duniani ikiwa ni hatua itayowasaidia kupata mbinu mpya za kukabiliana na wahalifu.
Alisema amelazimika kuwapatia msaada huo kwa vile muda mwingi hutakiwa kuwa macho kutimiza wajibu wao na kuwapo kwa vitu hivyo vitawasaidia kutekeleza vyema wajibu wao.
Msaada umetolewa na kwa pamoja na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein, ambapo kesho Mama Asha anatarajiwa kuwakabidhi wazee wa kisiwani Pemba.

JK VYUO VIKUU MALAYSIA NJOONI TANZANIA.

JK: Vyuo Vikuu Malaysia njooni Tanzania

Na Mwandishi Maalum, Malaysia
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, ameiomba Serikali ya Malaysia kuvishawishi Vyuo Vikuu vya nchi hiyo kuanzisha ama kuhamishia shughuli zao, hata ikiwezekana kujenga majengo ya vyuo hivyo, katika Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete ameiomba Serikali ya nchi hiyo kuwashawishi wawekezaji wa nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania ili kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano uliotangazwa majuzi na Rais Kikwete na hatimaye kuridhiwa na Bunge.
Maombi hayo ya Tanzania yamewasilishwa kwa Malaysia na Rais Kikwete mwenyewe wakati wa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Malaysia, Dato’ Sri Mohammed Najib Tun Abdul Razak.
Viongozi hao wawili walikutana juzi kwenye Cyberview Lodge, iliyoko Cyberjaya, mjini Kuala Lumpur baada ya kushiriki mkutano wa Wakuu wa Nchi, Serikali na viongozi wa ujumbe mbali mbali waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa mwaka huu wa taasisi ya maendeleo ya Langkawi International Dialogue (LID) 2011, uliomalizika juzi.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete amemwomba Waziri Mkuu Razak kuwashawishi Wakuu wa vyuo vikuu na makampuni ya Malaysia kukubali kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Rais Kikwete amemwelezea Razak kuhusu Mpango huo wa maendeleo ambao ni sehemu ya Visheni ya Maendeleo ya 2025 inayolenga kuitoa Tanzania katika umasikini na kuifanya nchi yenye uchumi wa kati.
Rais Kikwete pia amemweleza Razak kuwa Mpango wa Maendeleo mpya wa Tanzania ni mpango mzuri na kwamba changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa mpango huo unatekelezwa na hivyo kuleta matunda na matokeo mazuri kwa Watanzania.

SERIKALI KUZITAFUTIA UFUMBUZI KERO ZA WALIMU

Serikali kuzitafutia ufumbuzi kero za walimu

Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema ni jukumu la serikali kuhakikisha kila mkoa hapa nchini unakuwa na walimu wa kutosha na wenye sifa ili kuimarisha kiwango cha elimu.
Maalim Seif alisema hayo jana ofisini kwake Migombani mjini hapa alipokuwa akizungumza na ujumbe ya Chama cha Walimu Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine ulizungumzia changamoto mbali mbali zinazoikabili kada ya ualimu na sekta ya elimu kwa jumla.
Kauli hiyo Maalim Seif inafuatia malalamiko yaliotolewa na viongozi wa Chama hicho ya walimu wa kike walioko Pemba, kutengwa na familia zao (waume) zilioko Unguja, hata baada ya kuomba uhamisho kwa muda mrefu.
Alisema suala la walimu wa kike kisiwani humo kuishi mbali na familia zao linatokana na tabia iliojengeka miongoni mwa wafanyakazi kutopenda kufanyakazi kazi kisiwani humo.
Alisema imekuwa ni jambo la kawaida kwa wasichana kuomba ajira ya kufanyakazi kisiwani huko, lakini baada ya kuajiriwa hutumia ujanja wa kudai uhamisho kwa kile wanachodai ‘kwenda Unguja kuishi na waume zao’.
“Ni kweli kuwa kuishi mbali na familia ni tatizo, serikali haitaki watu watengane, lakini tukianza kukaribisha jambo hili kila mtu aje Unguja, Pemba itabaki bila ya walimu”, alisema.
Alisema kuna umuhimu wa kuliangalia suala hilo katika upande wa pili wa shilingi, kuzingatia ulazima wa walimu kubaki huko na kuondokana na tatizo la upungufu wa walimu maskulini.
Aliuhakikishia ujumbe huo kuwa serikali inalenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi wakiwemo walimu, ambapo mishahara itategemea sifa na muda wa utumishi kwa mfanyakazi, kutoa nyongeza za mishahara kila mwaka, kulipa malimbikizo ya posho mbali mbali, ikiwemo za likizo pamoja na kuwepo uwiano wamaposho kwa wizara zote ili kuondoa manung’uniko.
Alieleza kuwa tatizo la kuchelewa mishahara kwa walimu kisiwani Pemba, kutokulipwa ‘area’ pamoja na kukosekana kwa fedha za likizo nayo ni miongoni mwa masuala yatakayopatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Alifafanua kuwa mazingira mabaya yaliokuwepo hapo nyuma ndiyo yanayopelekea vijana wengi kuikimbia nchi baada ya kusomeshwa na serikali, hivyo aliwahakikishia wajumbe hao kuwa serikali itafanya kila iwezalo kuona wataalamu wake wanabaki nchini.
Akizungumzia hoja ya Wizara ya Elimu kuwachangisha walimu na wafunzi, Maalim Seif alisema kuna ulazima wa kuwepo utaratibu ulio wazi na utakaofahamika na walimu, jinsi ya fedha hizo zinavyotunzwa na zinavyotumika.
Akigusia juu ya tatizo la fedha zilizotengwa katika Bajeti na kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi lakini hatimae kutotolewa zote, alisema ni tatizo la Wizara zote ambapo kiini chake ni uchache wa fedha zilizopo hizo na kutokidhi mahitaji yaliolengwa, huku miradi ya maendeleo akisema ndiyo inayoathirika zaidi.
Alisema fedha zinazopatikana hulengwa kutumika katika miradi iliopewa kipaumbele, na kutoa indhari katika matumizi ya fedha kwa ajili ya safari (kama kipaumbele), akisema sio kila safari yafaa kupewa kipaumbele.
Maalim Seif alitumia fursa hiyo kuwataka walimu nchini kote kuelewa jukumu lao kubwa kwa taifa la kuwapatia elimu yenye kiwango vijana, na kuainisha kuwa hakuna ‘haki bila ya wajibu’.
Mapema Katibu mkuu wa Chama hicho Mussa Omar Tafurwa alimweleza Makamu wa Kwanza wa Rais, changamoto mbali mbali zinazowakabili walimu, ikiwemo michango kadhaa kutoka mishahara yao inayokatwa na serikali kwa ajili ya masuala mbali mbali.
Michango hiyo ni pamoja na ule wa Tamasha la Elimu bila malipo, Juma la Elimu ya watu wazima, Siku ya Walimu Duniani na ule wa kuendeleza TC.
Mbali na kusema michango hiyo haiwanuafaishi walimu hao zaidi ya ule wa kuendeleza TC, viongozi hao walionyesha mashaka makubwa juu ya udhibiti wa fedha hizo na matumizi yake, sambamba na michango ya kila mwaka inayotolewa an wanafunzi

SERIKALI KUFANIKISHA MAPINDUZI YA KILIMO-- MANSOOR

Serikali kufanikisha mapinduzi ya kilimo – Mansoor

Na Khamis Ali
WAZIRI wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yussuf Himid amewataka wakulima kutarajia mabadilko katika sekta ya kilimo kwani bajeti ijayo itaruhusu kutokea kwa mapinduzi ya kilimo.
Waziri Mansoor aliyasema hayo wakati akizungumza na wakulima wa zao la muhogo baada ya kufanya ziara katika kijiji cha Machui wilaya ya Unguja.
Alisema serikali hivi sasa imo katika matayarisho makubwa ya kukabiliana na matatizo yanayoikabili sekta ya kilimo na inakusudia kuyafanyia kazi katika mwaka mpya wa bajeti ili wakulima waweze kupata nafuu hasa katika upatikanaji wa zana za kilimo.
Alisema serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein, imedhamiria kuleta mapinduzi ya kilimo kupitia ilani yake na Wizara yake itahakikisha inatimiza nia hiyo.
Alisema serikali inachokusudia kukifanya hivi sasa ni kuendesha utafiti wa zaidi kwa kuviangalia vyakula vyote vya mizizi ambapo hatua itayoweza kukuza kilimo pamoja na wakulima.
Waziri huyo aliwataka wakulima hao kuona wanaongeza juhudi na kutokata tamaa kutokana na gharama zinazowapata katika ununuzi wa pembejeo ambapo serikali tayari imeshazingatia mahitaji yao.
Waziri huyo alisema mazingatio hayo yamo katika bajeti ijayo ya Wizara hiyo ambapo itaweza kuongeza upatikanaji wa matrekta, mbolea ili kuwafanya kulima kwa wakati na vifaa muhimu vya kilimo ikiwemo miundombinu.
Nao wakulima wa kijiji hicho wameeleza hatua yao ya kufurahishwa na ziara ya Waziri huyo kwa kuweza kuyatambua mahitaji yao kabla bajeti ya wizara hiyo kuanza kusomwa.
Mkulima Suleiman John, alimweleza Waziri huyo kuwa hapo awali walikuwa wakikabilwa na tatizo kubwa na mbegu asili baada ya kupata ugonjwa wa kansa ya muhogo lakini hivi sasa tayari tatizo hilo wameweza kukabiliana nalo baada ya kuanzisha mbegu mpya nne ambazo zilifanyiwa utafiti na kuonekana kufaa kwa eneo lao.
Akizitaja mbegu hizo alisema ni pamoja na ya Mahonda, Machui, Kama na Kizimbani ambazo zimeweza kutoa kiasi kikubwa cha zao la muhogo lakini hivi sasa wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la masoko.
Alisema katika mbegu hizo, mbegu ya Machui imeonekana kufanya vizuri zaidi kutokana na kukubaliana na ardhi ya sehemu hiyo ambapo hivi sasa wanaitumia wakulima wengi.
Ziara hiyo pia ilimshirikisha Mkurugenzi wa Idara ya Kilimo Mberik Rashid na Mkurugenzi wa Utafiti Haji Hamid na maofisa wengine wa wizara hiyo.

WAKE VIONGOZI WA AFRIKA WAPEWA CHANGAMOTO

Wake viongozi wa Afrika wapewa changamoto

Na Anna Nkinda – Putrajaya, Malaysia
WAKE wa viongozi wa Afrika wameshauriwa kutunza uhusiano uliopo baina yao ili waweze kutatua matatizo yanayowakabili wanawake na watoto katika nchi zao, kwani kundi hili limesahaulika katika jamii.
Mke wa waziri Mkuu wa Malaysia Datin Paduka Seri Rosmah Mansor alieleza hayo alipokuwa akizungumza na wake wa viongozi kutoka nchi za Tanzania, Lesotho, Kenya na Zambia wakati walipotembelea nyumbani kwake Putrajaya.
Alisema kuwa moja ya malengo ya kazi zao ni kuhakikisha kuwa kina mama na watoto wanaishi katika mazingira salama hivyo basi kama wanataka kufanikiwa zaidi jambo la muhimu ni kufanya kazi kwa pamoja na kubadilishana mawazo waliyonayo kwani Afrika ni moja na changamoto zinazowakabili wanawake na watoto zinafanana.
“Kazi mnazozifanya zinafanana na kuna malengo ambayo mmejiwekea ili muweze kufanikisha kazi zenu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kina mama na watoto wanaishi katika mazingira salama hivyo basi ni lazima muungane na kuwa kitu kimoja hakika kwa kufanya hivi mtaweza kumkomboa mwanamke na mtoto wa kiafrika”, alisema Mama Mansor.
Mke huyo alisema kutokana na uhalisia ni rahisi kwa wanaume kujiangalia wao wenyewe na kutatua matatizo yao lakini kwa wanawake na watoto wanatakiwa kupewa uangalizi wa ziada na msaada wa lazima hasa kwa wale wanatoka katika familia maskini.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alisema kuwa wao kama wake wa viongozi wanakazi kubwa ya kuhakikisha kuwa kinamama na watoto wanapata huduma muhimu katika jamii ikiwa ni pamoja na elimu na afya.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kwa upande wa Tanzania amekuwa akijitahidi kuhakikisha kuwa watoto wa kike ambao ni yatima wanapata elimu na vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua.
“Taasisi yangu ya WAMA imesaidia katika jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa vifo vya kinamama wajawazito na watoto vinapungua kwa kuchangia vifaa vya afya katika Hospitali, vituo vya Afya na Zahanati na kutoa elimu kwa jamii kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji”, alisema Mama Kikwete.

TANZANIA KUANDAA MKUTANO WA SMART PARTNERSHIP.

Tanzania kuandaa mkutano wa Smart Partnership

Mwandishi Maalum, Malaysia
TANZANIA imekubali kuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa taasisi ya kujadili maendeleo miongoni mwa nchi zinazoendelea ya Langkawi International Dialogue na Smart Partnership Movement utakaofanyika mwaka 2013 mjini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alipokea heshima ya kuandaa mkutano huo kwa niaba ya Tanzania wakati wa sherehe ya kufunga mkutano wa mwaka huu wa taasisi hiyo uliofanyika mjini Kuala Lumpur, Malaysia chini ya jina la Langkawi International Dialogue 2011.
Tokea mwishoni mwa wiki wakati ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Rais Kikwete ulipowasili mjini Kuala Lumpur kwa ajili ya mkutano wa taasisi hiyo wa mwaka huu uliomalizika uliomalizika jana kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Putrajaya (PICC), Makao Mapya ya Serikali ya Malaysia, waandalizi wa mkutano huo walikuwa wkaiishawishi Tanzania ikubali kuandaa mkutano ujao.
Awali, Rais Kikwete alionyesha kusita kukubali kuwa Tanzania iwe mwenyeji wa mkutano huo hasa kwa sababu waandalizi wa mkutano huo walikuwa wanashikilia kuwa Tanzania iandae mkutano huo mwakani, 2012.
Lakini Rais Kikwete aliwambia kuwa kwa sasa ni vigumu kwa Tanzania kukubali jukumu hiyo kwa sababu Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2011/2012 imekwishakuwasilishwa Bungeni ili ipitishwe, msimamo ambao Rais Kikwete aliukubali hadharani.
Kutokana na msimamo huo wa Tanzania, waandalizi hatimaye waliomba kuwa kwa sababu Tanzania haiwezi kuandaa mkutano huo mwaka ujao kwa sababu nzuri za kibajeti, basi ukibali kuwa mwenyewe mwaka 2013, ombi ambalo Rais Kikwete amelikubali.
Rais Kikwete aliwaambia wajumbe 540 waliohudhuria mkutano wa mwaka huu wakiongozwa na wakuu wa Nchi, Serikali na mawaziri kutoka nchi 17 kuwa ni heshima kubwa kwa Tanzania kuombwa iwe mwenyeji wa mkutano huo ambao umaarufu wake umekuwa unaongezeka tokea kufanyika kwa mara ya kwanza miaka 15 iliyopita.
Kwa kawaida mikutano ya taasisi hiyo hufanyika kwa kupokezana baina ya Malaysia na nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika na nchi za Caribbean. Mkutano huo unapofanyika katika Malaysia huandaliwa chini ya jina la Langkawi International Dialogue na unapoandaliwa katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika hujulikana kama Southern Africa International Dialogue (SAID).
Mkutano wa mwaka huu umehudhuriwa na wakuu wa nchi na Serikali kutoka Tanzania, Zimbabwe, Lesotho na Swaziland, Makamu wa Rais kutoka Kenya na Uganda, Naibu Waziri Mkuu kutoka Namibia na wawakilishi wa viongozi wa Botswana, Cameroun, Gambia, Mozambique, Syechelles, Zambia na wenyeji Malaysia.
Mkutano huo ulikutanisha washiriki 540 kutoka katika Serikali, sekta binafsi, wasomi, taasisi zisizokuwa za kiserikali, pamoja na wawakilishi wa CPTM.

JIHAD AITAKA SOS KUANZISHA KITUO CHA MICHEZO

Jihad aitaka SOS kuanzisha kituo cha michezo

Na Ali Amour, WHUUM
SHIRIKA la vijiji vya kulelea watoto yatima SOS, limeshauriwa kuanzisha kituo cha michezo ili kuibua na kukuza vipaji vya wanamichezo wachanga ambao ni rasilimali kubwa kwa taifa.
Changamoto hiyo imetolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, katika hafla ya siku ya michezo ya kijiji hicho ikiwa miongoni mwa shamrashamra za kutimia miaka 20 ya kuanzishwa kwake hapa Zanzibar.
Jihad amesema kuwa, hatua iliyofikiwa na SOS katika nyanja za taaluma na michezo ni kubwa, ambapo vipaji vya michezo mbali mbali vimeibuliwa na kuijengea Zanzibar matumaini ya kufanya vizuri katika medani za michezo.
Alifahamisha kuwa, ili taifa liendelee kimichezo, vituo vya kulea vipaji ni la vya lazima, kwani mafanikio ya jambo lolote hutegemea msingi ulio imara.
Waziri huyo ameeleza matumaini aliyonayo juu ya jambo hilo, kwa vile kijiji hicho kina viongozi na wataalamu mahiri katika fani ya michezo.
Aidha amelipongeza shirika la SOS kwa uamuzi wa busara kuanzisha kijiji cha aina hiyo hapa nchini, na kulitaka liongeze ushirikiano na mawasiliano ya karibu na wadau wengine wa michezo vikiwemo vyama ili kupata ushauri, maelekezo na hata walimu wa michezo mbali mbali watakayoamua kuianzisha.
Nae Mkurugenzi wa SOS Zanzibar Suleiman Mahmoud Jabir, alimshukuru Waziri Jihad kwa mchango wake mkubwa katika kukiendeleza kijiji hicho, na kusema kwa upande wao wako tayari kupokea na kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri wa kuendeleza michezo nchini.
Katika tamasha hilo, kulifanyika michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na pambano na fainali ya mpira wa miguu baina ya Evarest na Kilimanjaro, ambapo Evarest iliibamiza Kilimanjaro kwa magoli 3 - 1 na kutwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.
Maadhimisho ya kutimia miaka 20 tangu kuanzishwa kijiji cha SOS Zanzibar, yanafikia kilele leo Juni 23, 2011.

SI KAZI YA TFF, ZFA KUCHAGUA WACHEZAJI TAIFA STARS.

Si kazi ya TFF, ZFA kuchagua wachezaji Taifa Stars

Na Madina Issa
SHIRIKISHO la Soka Tanzania 'TFF' na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), havina jukumu la kuchagua wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.
Akijibu suala la Mwakilishi wa nafasi maalumu wanawake, Viwe Khamis Abdallah katika kikao cha Baraza la Wawakilishi jana, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii, na Michezo Bihindi Hamad Khamis, alisema jukumu hilo ni la kocha mkuu aliyepewa dhamana ya kuinoa timu hiyo.
Katika suala lake la nyongeza, Mwakilishi huyo alitaka kujua ni wachezaji wangapi waliochaguliwa kutoka Zanzibar kuchezea timu hiyo.
Akijibu, Naibu Waziri huyo alisema wachezaji wa Zanzibar waliomo kwenye kikosi cha timu hiyo sasa ni wanne.
"Ukweli ni kwamba vyombo hivi TFF na ZFA huwa havikai pamoja katika kutayarisha timu ya tafa ya Tanzania, kwa vile jukumu hilo ni la kocha aliyepewa dhamana ya kufundisha timu hiyo" alisema Bihindi.
Naye Waziri wa Wizara hiyo Abdilahi Jihad Hassan, alitoa ufafanuzi kuhusu msaidizi wa kocha mkuu kwa kusema, kocha huyo pia ndiye anayeamua na kuagiza ni nnai awe masidizi wake bia kuangalia upande anaotoka.
Jihad alitoa ufafanuzi huo kufuata suala la Mwakilishi wa jimbo la Rahale Nassor Salum Ali 'Jazeera', aliyehoji kwa nini utaratibu wa kugawana nafasi za ukocha kati ya pande mbili za muungano haufuatwi sasa.
Mapema, Mwakilishi huyo alisema siku za nyuma, Taifa Stars iliundwa na makocha kutoka nchi mbili huku upande mmoja ukitoa kocha mkuu na mwengine msaidizi wake

SUWEDI AKABIDHIWA TUNZO YAKE YA MSANII BORA.

Suwedi akabidhiwa tunzo ya msanii bora

Na Mohammed Mzee,
MSANII maarufu wa taarab asilia hapa Zanzibar Iddi Suleiman Suwedi, jana alikabidhiwa tunzo yake ya mwanamuziki bora wa fani hiyo, ambayo ilitolewa katika Tamasha la Zanzibar Music Award 2011, lililofanyika Juni 10, mwaka huu katika ukumbi wa Salama, hoteli ya Bwawani.
Hafla ya makabidhiano ya tunzo hiyo ilifanyika katika klabu ya Culture kwa vile mutribu huyo hakuwepo kwenye tamasha hilo kwa kuwa alikuwa safarini nchini Ujerumani.
Katibu Mkuu wa Culture Taimour Rukuny Twaha, aliyemuwakilisha katika hafla ya Bwawani, alimkabidhi msanii huyo tunzo yake pamoja na fedha taslim shilingi 150,000.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Iddi Suwedi aliwashukuru kwa dhati waandaaji wa tamasha hilo, Zanzibar Media Corporation, inayomiliki kituo cha redio cha Zenj FM na gazeti la Nipe Habari, sambamba na wapenzi wote waliompigia kura, na kumuwezesha kuwa miongoni mwa wasanii bora mwaka huu.
Aidha aliishukuru klabu yake ya Culture kwa mchango wake mkubwa kwa kumlea hadi akafikia kuwa maarufu na kupendwa na wengi.
"Naishukuru klabu yangu ya Culture kwa kunifikisha hapa nilipo kiusanii. Kama sio klabu hii nisingefikia nafasi ya kuonekana na hatimaye kuchaguliwa kuwa mmoja wa wasanii bora," alisema mkongwe huyo wa taarab asilia, aliyepachikwa jina la ‘mpendwa na wengi’.
Hii ni mara ya pili kwa msanii huyo kuibuka na tunzo hiyo, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2006 kupitia tamasha hilo, ambalo mwaka huu lilidhaminiwa na Kampuni ya Simu, Vodacom.

POLISI NETIBOLI YAENDELEZA MKONG'OTO

Polisi netiboli yaendeleza mkong'oto

Na Mwajuma Juma
TIMU ya netiboli ya Jeshi la Polisi wanaume, imeendelea kutamba kwenye ligi kanda ya Unguja, kwa kuifunga Jitegemee mabao 63-25 kwenye uwanja wa Gymkhana.
Ikiwatumia wafungaji wake Amiri Muhidin na Ali Hamad, Polisi ilitawala mchezo na kuwaweka roho juu wachezaji wa Jitegemee, ambapo hadi mapumziko walikuwa mbele kwa mabao 30-15.
Katika mchezo wake wa kwanza wa ligi hiyo, maafande hao waliibwaga Msambweni kwa mabao 45-26.
Ligi hiyo inayoshirikisha timu 15 zikiwemo nane za wanawake na saba za wanaume, inatarajiwa kuendelea tena leo uwanjani hapo kwa michezo miwili kati ya Msambweni na Pangawe, na baadae Ikulu na Zimamoto.

FAINI YAIPONZA AMANI FRESH.

Faini yaiponza Amani Fresh

Na Mwajuma Juma
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mjini, kimeipa ushindi wa bure timu ya Enugu kufuatia hatua ya kuzuiwa wapinzani wao Amani Fresh kwa kushindwa kulipa faini iliyopigwa na chama hicho.
Amani Fresh inayoshiriki ligi daraja la pili hatua ya 12 bora, ilitakiwa kulipa faini ya shilingi 50,000, baada ya kubainika kufanya vurugu siku ilipocheza na timu ya Jang’ombe Boys mara baada ya kumalizika kwa mchezo.
Kwa mujibu wa Katibu Msaidizi wa chama hicho Omar Mohammed, timu hiyo ilifanya vurugu Juni 18, mwaka huu katika uwanja wa Mao Dzedong kwa kuwashambulia waamuzi pamoja na kamisaa wa mchezo, ambapo ilifungwa bao 1-0.
Enugu na Amani Fresh zilipangwa kucheza juzi saa 8:00 mchana katika uwanja wa KMKM Maisara, kabla kuzuiliwa na ushindi kupewa wapinzani wao.
Mbali na mchezo huo, wakati wa saa 10:00 timu za Kilimani na Mwembeshauri zilichuana na Kilimani ikakala kwa bao 1-0, huku katika dimba la Mao Dzedong wakati wa saa 8:00 mchana, Jang’ombe Boys ikaifunga Red Stars bao 1-0.

MORO YAANDAA BONANZA KUIBUA VIPAJI VYA USANII.

Moro yaandaa bonanza kuibua vipaji vya usanii

Na Nalengo Daniel, Morogoro
KITUO cha Utamaduni wa Maendeleo ya Vijana Tanzania (KIUMAVITA), kinaandaa bonanza la kwa ajili ya kuinua vipaji vya usanii katika wilaya sita za mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa kituo hicho Mohamed Ngwenje, alivitaja vipaji vitakavyovumbuliwa kuwa ni pamoja na uimbaji wa nyimbo za asili, muziki wa kizazi kipya na muziki wa Injili.
Ngwenje ambaye pia ni mratibu wa bonanza hilo, alisema kuwa uibuaji huo wa vipaji utahusisha watu wa rika zote, kwa lengo la kupata wasanii ambao watasaidiwa kurikodi katika studio inayofahamika kwa jina la 'Moro Town Records' ya mjini Morogoro.
Alisema bonanza hilo litaanzia katika wilaya ya Kilosa Juni 26 kwa kutumbuizwa na wasanii watano ambao ni Yussuf Ngwenje ambaye anatamba na kibao cha ‘moyo wangu,’ Khalifa Ramadhan, Emmanuel Ruchamuzi kutoka Uganda na wengine aliowataja kwa jina moja moja, Asia na Linda.
Alifahamisha kuwa, baadaye bonanza hilo litaendelea katika wilaya ya Ulanga, kabla kuhamia Kilombero na katika wilaya nyengine zilizobaki.
Ngwenje aliwataka vijana wanaohisi wana vipaji mbalimbali kujitokeza katika bonanza hilo ambalo litakuwa la kwanza katika mkoa wa Morogoro.
Wavu, mikono Zenj zawika Umiseta
Na Donisya Thomas
TIMU za mpira wa mikono na wavu kutoka Zanzibar kwa wanaume na wanawake zimefanikiwa kutinga nusu fainali ya michuano ya Umiseta inayoendelea kutimua vumbi Wilayani Kibaha.
Kwa upande wa mpira wa mikono vijana wa Zanzibar wametinga nusu fainali baada ya kuichakaza Kaskazini Mashariki kwa mabao 39-14.
Aidha katika mpira wa wavu, Zanzibar imezidi kutamba baada ya kuirarua bila ya huruma timu ya Ziwa kwa seti 3-1.
Mkuu wa msafara wa timu hizo za Zanzibar Mussa Abdurabi, ameliambia Zanzibar Leo kwamba kwa upande wa riadha Zanzibar haishikiki na tayari imejiongezea medali nyengine moja ya dhahabu na hivyo kufikisha medali tano, fedha mbili na shaba tano.

Tuesday, 21 June 2011

MANDHARI  ya  harakati za kila siku katika  eneo la darajani  kama linavyoonekana picha wakati wa  kazi asubuhu ndivyo hali inavyokuwa kama hivi eneo hilo lnalokabiliwa na uhaba wa maegesho ya magari na (Picha na Othman Maulid)

DK. SHEIN AWASHANGAA WABUNGE,WAWAKILISHI WANAOWAKIMBIA WANANCHI

Dk.Shein awashangaa Wabunge, Wawakilishi wanaowakimbia wananchi

• Ahimiza mshikamano viongozi CCM, Serikali
Na Bakari Mussa, Pemba
MJUMBE wa Kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka viongozi wa Chama hicho kushirikiana na Serikali yao kutatuwa kero za wananchi kwa kufuata Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho iliyoinadi wakati wa kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2010.
Alisema CCM, itajitahidi kutekeleza ahadi ilizozitowa kupitia Ilani yake hiyo kwa vile ilizitowa kwa kujiamini na imeanza kutekeleza kwa vitendo baadhi ya ahadi hizo.
Dk. Shein, alieleza hayo ukumbi wa mikutano wa Benjamin Mkapa Wete, alipozungumza na viongozi wa CCM wa wilaya hiyo, kuanzia ngazi ya Shina hadi wilaya.
Alisema kwa kasi inayochukuliwa naCCM ya Utekelezaji wa Ilani hiyo, inategemea kumaliza utekelezaji wake kwa mujibu ilivyopangwa na Chama hicho ili kuwaondoshea kero wananchi.
Aliendelea kusema kuwa sio wakati tena wa viongozi kukaa maofisini, bali wateremke na wawe na mabadiliko waende matawini kuimarisha Chama chao na waweeleze wafuasi wao na wananchi kwa ujumla namna Serikali inavyofanya kazi na Chama cha Mapinduzi kinavyosimamia maendeleo ya wananchi bila ya kubaguwa.
Dk.Shein, alikemea mtindo wa baadhi ya Viongozi kukimbia wapiga kura wao Majimboni baada ya kuchaguliwa kwani wao ndio wanaotakiwa wawe karibu na wananchi wao ili kuelewa matatizo yao na kuyapatia ufumbuzi.
Mjumbe huyo wa Kamati kuu ya CCM Taifa, aliwataka wanaCCM, kuwa na mshikamano, umoja na maelewano miongoni mwao kwani ndio nguzo pekee itakayokiwezesha Chama kusonga mbele na daima kukiwezesha kutawala nchi hii.
“ Sio wakati wa Viongozi kukaa kimya, lazima wawe wazi na waeleze ukweli uliopo” alisema Dk. Shein.
Akizungumzia ugumu wa maisha inayoikabili Zanzibar, alisema hilo lipo lakini ukali wa maisha unaosababisha kupanda kwa gharama za maisha si la Zanzibar pekee bali ni la kidunia.
Alifahamisha kuwa Serikali haifanyi biashara imetowa uhuru kwa Wafanyabiashara wenyewe kuagiza bidhaa lakini si vyema kuwabana wananchi kibei, waangalie na bei waliyonunuwa.
Aliendelea kusema kuwa Serikali inaelewa hali hiyo, na sasa imeandaa mipango mikubwa ili Wananchi waweze kukabiliana na suala hilo na mataifa mbali mbali yanaonesha nia ya kuunga mkono juhudi hizo.
Dk, Shein, alieleza dawa ya kuwafanya wananchi waondokane na ukali wa maisha ni kukifanyia mageuzi kilimo, ili wananchi walime zaidi na kupata mazao mengi sambamba na kuwapatia pembejeo mbali mbali ikiwemo mbolea, mbegu za mazao mbali mbali.
Alisema Serikali katika msimu ujao imejipanga vyema ili iweze kukabiliana na upungufu wa chakula na kuwafanya wakulima wakipende kilimo kwa vile watakuwa wanazalisha zaidi.
“Hakuna njia ya mkato kuhusu chakula ila kwa kuboresha kilimo ili kiwe bora zaidi” alifahamisha.
Dk. Shein, aliwahakikishia viongozi na wananchi kwa ujumla kuwa ahadi zilizotolewa na CCM, katika Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2005-2010, zipo pale pale na katu haitazisahau.
“Ahadi za CCM, sio za utani kwani inatowa ahadi zinazotekelezeka “ alisema.
Alisema Serikali anayoiongoza haitambaguwa mtu wa aina yoyote kwani Serikali ni ya watu wote na kila mtu anaestahiki kupatiwa haki yake atafanyiwa hivyo, kwani yeye alikula kiapo kuwa ataongoza kwa mujibu wa Sheria.
Aliwataka wanaCCM, viongozi naWananchi kwa ujumla kuzidisha Amani, Umoja na mshikamano, iliwaishi vizuri nawaendelee kuipa heshima nchi yao .

MPAKA VINYESI SKULI MBARONI

Mpaka vinyesi skuli mbaroni
• Asema wako kundi lililopangwa ‘shifti’
• Yahusishwa na ushirikina
Na Ameir Khalid
HATIMAE wananachi wa kijiji cha Muungoni Wilaya ya Kusini Unguja wamefanikiwa kimtia mikononi mtu anaedaiwa kupaka kinyesi skuli ya msingi Muungoni kwa muda mrefu katika mazingira ya kutatanisha.
Kazi hiyo ya kukamata mtu huyo haikuwa rahisi baada ya kuhangaika kwa kipindi kirefu ambali limekuwa likihusihwa na masuala ya uchawi na iliwalazimu kutumia kila mbinu ili kufanikisha lengo hilo na hapo jana limetimia.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika eneo la tukio mmoja ya wanakijiji hao ambaye ndiye hasa aliyemkamata mtu huyo, Mohamed Busra alieleza mkasa mzima jinsi ilivyokuwa katika siku hiyo.
Alisema kuwa baada ya kukaa na wananchi wenzake na kutafakari jambo hilo kwa muda mrefu huku visomo mbali mbali vikipitishwa, bila ya kufanikiwa kumpata mtu huyo, ndipo alipopata mawazo kutoka kwa mzungu raia wa Ujerumani aliyemtaja kwa jina Mr. Chadi.
Alifafanua kuwa mzungu huyo alitoa wazo hilo na ndipo wananchi hao walipoamua kuanzisha ulinzi, muda wote lakini kwa kipindi hicho chote hawakuweza kumkamata, huku vitendo hivyo vikizidi kushamiri huku wakitumia pesa nyingi kwa kufanya dawa.
''Kila siku tumekuwa tukikesha hapa skuli lakini mara tu tunapoondoka basi vitendo hivyo vinafanywa, tena wakati mwengine mchana utakuta kinyesi kinarushwa''alisema.
Akieleza kuwa usiku wa kuamkia Jumanne wakati wakijitayarisha kutoka majira ya saa 11: 45 alfajiri, walimkuta kijana huyo akiwa anatembea nyuma ya majengo ya skuli, akiwa na mfuko wa plastic mkononi.
Alieleza kuwa baada ya kumhoji kwa muda mrefu ndipo kijana hayo alijulikana kwa jina la Kassim Ali Ame, mwenye umri wa miaka 13 mkaazi wa Muungoni mwanafunzi wa darasa la tano skuli ya Muungoni alieleza jinsi alivyokuwa akishiriki vitendo hivyo.
Alisema kuwa yeye alikuwa akitumwa na bibi mmoja aliyemataja kwa jina la Fatuma Kitanzi Mtaji (65), mkaazi wa Muungoni uwandani ili afanye kazi hiyo, akiwa na wenzake 7 wakifanya kazi hiyo huku wakipishana zamu.
Kijana huyo alieleza kuwa walikuwa wanafanya kazi hiyo kwa nyakati tofauti, ambapo wakati mwengine walikuwa wanaenda usiku wa manane kupaka kinyesi hicho, huku wakiwa wamefuatana na mtu mmoja ambaye yeye mwenyewe alidai kuwa hamfahamu,lakini alikuwa ni mrefu sana na mwenye upara.
Alisema kuwa wakati alipokuwa akifanya kazi hiyo yeye na wenzake walikuwa wakipewa pesa ambazo alizitaja kati ya kiasi cha shilingi 5000 mpaka 3000, ambazo alikuwa akitumia wakati anapokwenda skuli.
Alieleza kuwa wakati kupaka kinyesi hicho hutumia mikono kupaka na mengine hurusha kupitia madirisha ya skuli, bila ya kuonekana na mtu yoyote kwa kipndi hicho.
Mapema mwalimu mkuu wa skuli hiyo Mrisho Pandu Ali alisema kuwa kukamatwa kwa mtu huyo kutaleta afueni, kwani walikuwa wanaathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na jambo hilo.
Alisema kuwa walilazimika kuwafungia skuli wanafunzi wa madarasa ya chini kutokana na kadhia hiyo, iliyokuwa imeshamiri skuli hapo na kulazimika kufupisha silibasi yao.
Kwa upande wake bibi huyo ambaye anashutumiwa kuwatumia vijana hao wadogo kufaya vitendo hivyo vya kishirikina,imebainika kuwa anafanya hivyo kutokana na skuli hiyo kujengwa katika eneo lake.
Wananchi wa Muungoni walisoma halbadiri kadhaa na visomo vya kila kumuoamb Mwenyezi Mungu awaondoshee balaa hilo lakini kila kisomo kikipigwa ndipo kinyesi hicho kinapozidi.

SEREKALI YATAHADHARISHWA MASLAHI YA WANAJESHI

Serikali yatahadharishwa maslahi ya wanajeshi

Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la Mkanyageni Kisiwani Pemba Mohammed Habib Mnyaa, ameitahadharisha serikali ya Muungano kuepuka kutengeneza maandamano ya Wanajeshi kutokana na serikali kushindwa kuwalipa stahili zao askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Tahadhari hiyo aliitoa jana wakati akichangia bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano huko Mjini Dodoma ambapo matangazo hayo yamekuwa yakirushwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa TBC1.
Mbunge huyo alisema inashangaza hivi sasa kuwepo kwa tatizo kubwa la taasisi hizo kutoingiziwa fedha kwa ajili ya huduma mbali mbali na kuwafanya askari kushindwa kupata stahili zao hata pale wanapoewa uhamisho
Alisema hivi sasa kuna tatizo kubwa katika kufanya malipo ya utoaji wa huduma kwa askari wa vikosi vya ulinzi huku ikifikia taasisi zao kukatiwa umeme kutokana na kuwa na madeni mengi.
Akitoa mfano mbunge huyo alisema kuna askari wa Zanzibar wamehamishiwa katika mikoa mbali mbali ya Tanzania tangu mwaka 2008, lakini jambo la kushangza hadi leo hakuna alielipwa fedha za uhamisho.
Hali hiyo alisema inaweza kusababisha hatari ya kuwaandalia askari mazingira ya kuingia barabarani na kuanzisha maandamano ya kudai haki zaobaada ya kukosa stahili zao kwa muda mrefu kunakosababishwa na serikali yao.
Alisema haitapendeza Tanzania kuona vurugu za maandamano zinaondoka kwa raia na kuhamia katika vikosi vya ulinzi jambo ambalo serikali inapaswa kuiona inachukua tahadhari za awali kuinusuru nchi na jambo hilo kwani inaweza kuleta hatari kubwa.
Wanashangaa kuona taasisi hiyo hivi sasa imekuwa inadaiwa na Shirika la Umeme TANESCO kwa Tanzania Bara na ZECO kwa Zanzibar ambapo zimeshawahi kukatiwa umeme mara kwa mara jambo ambalo ni la kushangaza kuona fedha kwa ajili ya kutumia mambo mengine zimekuwa zikiingizwa lakini tofauti katika utoaji wa huduma hazionekani na kuhoji kuna nini katika taasisi hizo.
Alisema jambo la kusikitisha kuona madeni hayo hayapo kwa wanaopewa uhamisho tuu bali pia yapo kwa askari waliostaafu ambapo hivi sasa kuna watu hawajalipwa mafao yao kwa muda mrefu.
Aidha, alisema jambo la kusikitisha kuona wanapojaribu kutoa madai yao hutakiwa kuyafuata Makao Makuu Dar- es -Salaam jambo ambalo limekuwa likiwapa usumbufu kwani inawezekana wanapojaribu kufuatiatilia kukuta kukiwa hakuna fedha za kuwalipa kwa wakati huo.
Mbunge huyo alisema anashangazwa askari hao wa Zanzibar wanapojaribu kudai kuambiwa waende Makao Makuu wakati wale walioko katika Mkoa ya Arusha na mingine hupelekewa fedha zao walipo bila ya kuitwa kufuata Makao Makuu.
Alisema haoni sababu ya askari wa Zanzibar kutakiwa kwenda Makao Makuu wakati Zanzibar, ikiwa na tawi la Benki Kuu ya Tanzania, ambapo ingelitosha taasisi hiyo kuitumia kuwapatia fedha zao.
Kutokana na adhabu hizo Mbunge huyo, aliiomba serikali kujiangalia katika taasisi hizo na kama imekuwa inaingiziwa fedha kidogo basi ibadili utaratibu wake ili kuiepusha nchi kuingia katika hatari maandamano ya askari kwani bado askari wa Tanzania ni watii kwa serikali yao.
MKE wa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar  Mama Asha Balozi akimkabidhi seti ya TV Mwenyekiti wa Bodi ya Kijiji cha Watoto cha SOS  Mohammed Baloo kwa ajili ya watoto  wa Kijiji, katika sherehe za kuwazawadia Wafanyakazi wastaafu wa SOS zilizofanyika katika viwanja hivyo.(Picha na Othman Maulid)

POLISI YABAMBA MAGUNIA YA BANGI

Polisi yabamba magunia ya bangi

Na Ramadhan Himid, POLISI
KITENGO cha kupambana na dawa ya kulevya kilicho chini ya Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, kimefanikiwa kuwakamata watu wawili wakiwa na viwango tofauti vya majani makavu yanayodhaniwa kuwa ni bangi.
Akithibitisha kukamatwa kwa watu hao Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi Muhudi Juma Mshihiri, alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na ushirikiano wa wananchi kufuatia operesheni mbali mbali zinazoendeshwa na Jeshi hilo ili kukomesha biashara ya bangi pamoja na dawa kulevya nchini.
Aliwataja watu hao kuwa ni Othman Issa Mdabe (22) wa Kilindoni Mafia aliyekamatwa na mafurushi 277 ya bhangi akitokea Tanzania Bara ambapo mafurushi hayo aliyahifadhi ndani ya mito ya sponji 11, mtuhumiwa huyo alikamatwa kutokana na ushirikiano wa wafanyakazi wa Bandarini kutoa taarifa za kumtilia shaka kijana huyo.
Mwengine ni Shaaban Salum Othman (40) wa Miembeni aliyekamatwa na mifuko 10 ya plastiki ikiwa na majani ya bhangi huko Miembeni Mjini Unguja.
Wakati huo huo Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi imefanikiwa kuwakamata watu watatu wakiwa na bhangi, akithibitisha kukamatwa kwa watu hao Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Azizi Juma Mohammed amewataja watu hao kuwa ni Nyange Makame Ali (61) wa Shauri Moyo aliyekamatwa na robo kipolo cha bhangi huko Shauri Moyo Mjini Unguja.
Kamanda Azizi pia aliwataja Hamad Said Omar (38) wa Kilwa na Izshaka Yumbeshi (30) wa Saateni Unguja ambao wote walikamatwa na nusu kipolo kikiwa na bhangi, mkoba wa rasketi na nyongo 38 za bhangi.
Kamanda Azizi amewataka wananchi kuyendelea kutoa taarifa mbali mbali za wahalifu ili kukomesha utumiaji wa bangi pamoja na madawa ya kulevya.
Watuhumiwa wote hao watafikishwa Mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.

SUZA YAPATA BARAZA JIPYA

SUZA yapata Baraza jipya

Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ramadhan Abdulla Shaaban
amewateuwa wajumbe 1 wapya wa Baraza la Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali, Mwanaidi Saleh Abdulla, Waziri Shaaban
amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa sheria namba 8 ya mwaka 1999 ya Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kifungu cha 12(d).
Walioteuliwa kuwa wajumbe wa Baraza hilo ni Said Mohammed Said
Mwakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi, Dk. Narman Saleh Jiddawi
kutoka Taasisi ya Sayansi ya Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Simai Mohammed Said ambae ni mfanyabiashara, Amina Khamis Shaaban Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar,
Khamis Mussa Omar Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na
Mipango ya Maendeleo na Mwanaidi Saleh Abdulla Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali.
Wengine ni Dk. Zakia Mohamed Abubakar, kutoka SUZA, Mmanga Mjengo Mjawiri kutoka SUZA, Maulid Omar Haji kutoka SUZA, Profesa Mustafa Roshash
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar na Mtumwa Ali Ameir
Mwenyekiti wa Serikali ya Wanafunzi SUZA.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, Hassan Nassor Moyo ataendelea kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Uteuzi huo umeanza tarehe 15 Juni mwaka huu.
WATOTO wa Kijiji cha SOS  wakionesha umahiri wao wa mchezo wa sarakasi katika sherehe za kuwatunukia Vyeti Wafanyakazi  wastaafu  wa SOS  waliotumikia kijiji hicho kwa m,uda mrefu  wakiwa katika viwabja hivyo ( Picha na Othman Maulid)

ZANZIBAR OCEAN, SIMBA KUNDI MOJA KAGAME.

Zanzibar Ocean, Simba kundi moja Kagame
Itafungua dimba na Wasomali Ettcel
Na Kunze Mswanyama, Dar es Salaam
WAWAKILISHI wa Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Kagame timu ya Zanzibar Ocean View, wamepangwa katika kundi A pamoja na wekundu wa Msimbazi Simba ya Tanzania Bara.
Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania 'TFF' Angetile Osiah, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa timu zote zinazoshiriki mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Juni 26, mwaka huu, zimepangwa katika makundi matatu.
Osieh alisema mbali na timu hizo za Zanzibar na Tanzania Bara, kundi A pia litakuwa na timu ya Ettcel ya Somalia na Vital’O kutoka Burundi, ambapo kundi B linaundwa na timu za Yanga, El Mirrekh ya Sudan, Bunamuaya kutoka Uganda na Elmaan ya Somalia.
Kundi C linajumuisha timu za APR ya Rwanda, Ports FC ya Djibout, Saint George ya Ethiopia na mabingwa wa Kenya Ulinzi.
Kwa mujibu wa Osieh, siku ya ufunguzi wa mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya bia ya TBL, Zanzibar Ocean View itashuka uwanja wa taifa kumenyana na Ettcel ya Somalia wakati wa saa 8:00 mchana, huku Simba ikiivaa Vitalo mnamo saa 10:00 jioni uwanjani hapo.
Katibu huyo wa TFF alieleza kuwa mbali na uwanja wa taifa wa Dar es Salaam, ngarambe hizo pia zitakuwa zikirindima katika dimba la Jamhuri mkoani Morogoro.
Timu ya Yanga imeweza kushirikishwa katika mashindano hayo baada ya kulilipa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) deni la dola 35,000 za Kimarekani ilizokuwa ikidaiwa baada ya kugomea mchezo wa kutafuta ushindi wa tatu dhidi ya Simba katika mashindano kama hayo mjini Dar es Salaam.
Michuano hiyo inafanyika kufuatia wasiwasi wa kukosa mdhamini, baada ya kuokolewa na kampuni ya TBL iliyokubali kuibeba na kuikabidhi TFF shilingi milioni 300 juzi.
Bingwa wa mashindano hayo atanyakua dola 30,000 huku washindi wa pili na wa tatu wakizoa dola 20,000 na 10,000 mtawalia, ambazo hutolewa na Rais wa Rwanda Paul Kagame.
Awali mashindano hayo yalikuwa yafanyike Zanzibar, na baadae kuhamishiwa Sudan kwa sababu tafauti, lakini yakahamishiwa Dar es Salaam kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo.

MSHINDO AWATAKA WANAFUNZI KUJIKITA MICHEZONI

Mshindo awataka wanafunzi kujikita michezoni

Na Aboud Mahmoud
WANAFUNZI nchini wameshauriwa kujenga tabia ya kujishirikisha katika michezo kwani hiyo ni sehemu muhimu katika maisha.
Ushauri huo umetolewa na Kamishna wa Michezo na Utamaduni Hamad Bakari Mshindo, kwenye sherehe ya siku ya michezo ikiwa ni shamra shamra za kutimiza miaka 20 ya kuanzishwa kijiji cha SOS.
Alisema kuwa baadhi ya wazee wamejenga dhana ya kuwa michezo ndio chanzo kikuu kinachowafanya wanafunzi wasishughulikie masomo yao jambo alilosema kuwa sio kweli.
Alieleza kuwa michezo na elimu ni miongoni mwa mambo yanayoweza kumfanya mwanafunzi ajenge ufahamu na kufaulu katika masomo yake.
"Mimi napinga dhana ambayo baadhi ya wazee wanasema kwamba michezo inawafanya wanafunzi wasisome," alisema.
Mshindo alifahamisha kuwa ili akili iweze kupumzika baada ya masomo lazima vijana wajishirikishe katika michezo.
Aidha Kamishna Mshindo aliupongeza uongozi wa kijiji cha SOS kwa kuandaa siku maalum kwa ajili ya michezo akisema hiyo ni dalili tosha ya kuwapa mafunzo wazazi kuhusu umuhimu wa michezo.
Nae Mkurugenzi wa kijiji cha SOS Suleiman Mahmoud Jabir, amesema kuwa lengo la kuandaa siku ya michezo kwa wazazi ni kuwaunganisha wazazi na wafanyakazi wa kijiji hicho kwa lengo la kukuza ushirikiano.
Katika sherehe hizo, michezo mbali mbali ilichezwa kwa kushindana baina ya wazazi na wafanyakazi wa kijiji hicho, ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, kutembea, mbio za vijiti, kunywa soda, kupiga penalti pamoja na mpira wa pete.

NEW GENERATION QUEENS ZIARANI MOSHI.

New Generation Queens ziarani Moshi

Na Khamis Amani
TIMU ya soka la wanawake New Generation Queens, iko mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kwa ajili ya kushiriki mashindano ya CHRISS yanayoshirikisha timu za Afrika ya Mashariki na Kati.
Wanasoka hao 16 na viongozi wao, wanashiriki michuano hiyo iliyoanza jana Moshi, chini ya udhamini wa Jumuiya ya Kikristo duniani.
Kwa mujibu wa Meneja wa timu hiyo Salum Jenga Simba, timu yake imeondoka na kikosi kamili kitakachoweza kutoa ushindani mkubwa kwa wapinzani wao watakaopangiwa, kwa lengo la kujihakikishia ushindi wa ngarambe hizo.
"Ni faraja kubwa kwetu, kwani haya ni mashindano yetu ya kwanza tokea kuanzishwa kwa timu yetu, naamini ni fursa pekee ya kuitangaza kisoka timu yetu katika ramani ya Afrika Mashariki na Kati pamoja na duniani kwa ujumla", alisema Salum Jenga.
Hivyo amewahakikishia wapenzi wake kutokuwa wasiwasi juu ya vijana wao hao, ambao wameondoka wakiwa kamili kamili kukabiliana na upinzani wowote utakaowakabili kwa lengo kujinyakulia ushindi.

WAWAKILISHI WAJINOA KWENDA ARUSHA

Wawakilishi wajinoa kwenda Arusha

Na Hamad Hija, Maelezo
TIMU ya soka ya Baraza la Wawakilishi, inatarajia kuanza mazoezi wiki hii kwa ajili ya kujiandaa na ziara ya kimichezo mkoani Arusha mwezi wa Agosti.
Kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na kocha Juma Sumbu, kitakuwa kikifanya mazoezi hayo kwenye uwanja wa Mao Dzedong nyakati za asubuhi.
Afisa Michezo wa Baraza la Wawakilishi Dau Hamad Maulid, amesema ziara hiyo ni ya kawaida ambapo kila mwaka kikao cha bajeti kinapomalizika, huwa inakwenda Kilimanjaro ikiwa wageni wa rafiki zao Wazee Sports ya huko.
“Huo ni utamaduni tuliojiwekewa kila tunapomaliza kikao cha bajeti huwatembelea ndugu zetu wa Wazee Sports, kwa lengo la kuimarisha umoja wetu”, alisema.
Dau amesema kabla ya safari hiyo, wanatarajia kucheza mechi kadhaa za kirafiki ili kujipima nguvu na baadhi ya timu za hapa nchini.
Alizitaja timu walizopanga kupambana nazo kuwa ni Unguja Ukuu, Kiwengwa na Makunduchi.
Miongoni mwa wanandinga wanaotegemewa na waheshimiwa hao wa baraza la kutunga sheria ni Hamza Hassan Juma, Ali Abdulla na Issa Gavu pamoja na mlinda mlango Hashim Jaku.
Mbali na timu hiyo ya soka, timu hiyo pia kutakuwa na timu ya netiboli, kuvuta kamba na mbio za magunia, ambapo msafara wake unatarajiwa kuongozwa na Spika wa baraza hilo Pandu Ameir Kificho.

Monday, 20 June 2011

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete akibadilishana mawazo na Waziri Mkuu wa Zamzni wa Malaysia  Mahahir Mohammed, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Taasisi ya Smart Partneship Dialogue unmaojulikana kama Langkawi International Dialogue uliofanyika mjini Kuala Lumpur Malaysia,(Picha na John Lukuvi)   
H

WAPINGA KUWEPO JAA MAGOFU YA MARUHUBI

Wapinga kuwepo jaa magofu ya Maruhubi

Na Asya Hassan
WANANCHI wameilalamikia Serikali juu ya utupaji taka uliokithiri na kufanyika kwa jaa kubwa katika magofu yaliopo Maruhubi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mkaazi wa eneo hilo, Nassor Muhammed alisema kuwa eneo hilo la magofu ambalo lilikuwa ni kivutio kikubwa cha watalii hivi sasa kumekuwa hakuna haiba ya kuvutia kutokana na kukithiri kwa utupaji taka.
Aidha alisema kuwa kuwepo kwa jaa hilo kunaweza kuhatarisha afya za wakaazi wa eneo hilo kutokana na moshi mkubwa unaotoka wakati wa kuchomwa moto taka hizo na kusambaa majumbani.
Pamoja na hayo alisema kuwepo kwa jaa hilo Serikali inaweza ikapunguza pato lake la uchumi ambalo linatokana na utalii, kwani watalii hawatavutiwa na eneo hilo ambalo halina mandhari nzuri ya kuvutia na kuiomba serikali kupitia idara husika kusitisha zoezi hili utupaji taka ili eneo hilo lirudi katika hali yake ya mwanzo.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha mambo ya kale Zanzibar, Abdalla Khamis Ali, alithibitisha kuwepo kwa jaa hilo na kusema kwamba eneo hilo limeruhusiwa kutupwa taka kwa muda maalum na sio eneo la kudumu kama inavyodhaniwa ili kufukia mashimo yaliyotokana na uchimbaji ovyo wa mchanga.
Alifahamisha kwamba kwa kuwa eneo hilo lina matatizo hayo kitengo chake kwa kushirikiana Idara ya mazingira walikaa kikao cha pamoja na kujadili namna gani wataweza kuyafukia mashimo hayo ndipo walipoamua kuruhusu Baraza la Manispaa kumwaga taka zake hapo ili kuzuia hali hiyo.
Mkuu huyo alifafanua kuwa kwa vile serikali ina malengo mazuri juu ya kurekebisha eneo hilo hivyo haitaishia kutupa taka tu bali ina lengo la kumwaga fusi katika eneo baada ya kukaa sawa kwa mashimo hayo.

MRADI KUMOSHA BAKORA WAFANIKIWA.

‘Komesha bakora’ wafanikiwa

Na Hamad Hija, Maelezo Zanzibar
MRADI wa majaribio wa mwaka mmoja kuhamasisha kutumia adhabu mbadala maskulini na kuacha kutumia bakora ulioanza Julai 2010 utamalizika Juni 2011 ukiwa umefanikiwa kwa kiasi kubwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake Mazizini mjini Zanzibar mratibu wa mradi huo Safia Ali Rijaali, alisema mradi huo unaoendeshwa kwa pamoja kati ya Wizara ya elimu na na shirika linaloshughulikia watoto SAVE THE CHILDREN kupata maendeleo makubwa karibu asilimia 70 za malengo yake yamefikiwa.
Amesema Mradi huo uliolenga kupunguza matumizi ya bakora na walimu kutumia njia nyengine kwa kiasi umezaa matunda kwa vile matumizi ya akora yameanza kupunguwa.
Kwa awamu ya kwanza ya majaribio ya mradi huo umezishirikisha skuli 10 za msingi za unguja na Pemba, ambapo kwa upande wa Unguja zilihusishwa skuli za Kisiwandui kwa Wilaya ya mjini na Wilaya ya Magharibi skuli ya Regezamwendo.
Kaskazini ‘A’ ni skuli ya Kinyasini na Kaskazini ‘B’ skuli ya Fujoni na Wilaya ya Kati ni Marumbi, ambapo Kusini ni Kitogani, Pemba ni Chake Chake skuli ya Pondeani, Wete ni Minungwini, Micheweni skuli ya Wingwi na Mkoani ni skuli ya Ng’ombeni, ambazo zimefaidika na mradi huo.
Aidha Mratibu huyo alisema mradi kama huo haukufikia malengo kwa kuwa muda ni mdogo sana, ambao ulihitaji angalau miaka miwili ama mitatu.
Mradi huo ambao umetumia 71 milioni, awamu hii ya kwanza ukiwa unalenga zaidi kupunguza adhabu ya bakora na kutumika adhabu nyengine ambazo hamuathiri mwanafunzi ili kujenga mahusiano mazuri kwa walimu na wanafunzi pamoja na wazee wenye watoto.
Mratibu alisema mradi kwa kiasi ni mgumu kwani kumtowa mtu katika mazoea ya kutenda jambo na kumuondoa kwa muda mdogo inakuwa vigumu kwa kiasi fulani, lakini pamoja na hayo kwa kiasi kikubwa umefanikiwa.
Akifafanua njia wanazotumia kutowa elimu ya kuhamasisha kutumia adhabu mbadala kwa wanafunzi maskulini, mratibu huyo alisema njia zinazotumika katika kufikisha ujumbe huo ni pamoja na kutumia vyombo vya habari kama vile Redio, magazeti na vipindi vya televisheni.

BAJETI YA ZANZIBAR YAPOKEWA KWA MAONI TAFAUTI.

Bajeti ya Zanzibar yapokewa kwa maoni tafauti

Na Waandishi wetu
WADAU, wananchi na wanasiasa wametoa maoni yao kufuatia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee hapo juzi kuwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/2012.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha (AFP) Said Soud, alisema pamoja na serikali katika bajeti hiyo kuonesha nia ya kukuza kilimo lakini pia ilipaswa kutoa msukumo zaidi katika biashara.
Alisema kukuzwa kwa sekta hiyo kutaweza kuwepo kwa mzunguuko wa fedha na hivyo serikali kujipatia mapato makubwa sambamba na kuhakikisha inaondoa kodi kwa bidhaa za vyakula ili kuleta ahuweni ya maisha kwa wananchi.
Naye Katibu Mkuu wa TADEA, Juma Ali Khatib, alisema itakuwa jambo la busara endapo serikali itarahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo pamoja na kutoa mikopo kwa wakulima wa Zanzibar.
Alisema katika watu wenye maisha ya dhiki ni wakulima hivyo kama serikali inataka kukuza uchumi sambamba na kuondosha tatizo la ajira ni vyema kilimo kikarahisishwa kwa kutolewa mikopo huku pia akielezea wakulima hao kupatiwa masoko ya uhakika.
Naye Rais wa Jumuia ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar (Chamber of Commerce), Mbarouk Omar Mohammed, alisema bajeti ya serikali kwa kiasi kikubwa imeisahau sekta ya biashara.
“Pengine ni bajeti nzuri kwa sekta nyengine lakini ni bajeti ambayo mimi naiona haikuzingatia sana namna ya ukuzaji wa biashara hasa ikizingatiwa mazingira ya visiwa vyetu”,alisema.
Aidha alisema pamoja na kushirikishwa kwenye mchakato wa utengenezaji wa bajeti hiyo, lakini kwa kiasi kikubwa mapendekezo yao muhimu hayakuwasilisha kikamilifu.
“Tulidhani kwa kiasi waziri angetueleza namna ya kuumaliza ugonjwa wa kensa wa wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, lakini hatukuelezwa na hili limekuwa tatizo ambalo halina dawa”,alisema.
Alisema urari wa utoaji wa uingizaji bidhaa visiwani (balance of trade), utaonekana mkubwa endapo vikwazo vya kufanya biashara nje ya visiwani havitapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Khamis Mwinyi, alisema mfumo wa utayarishaji wa bajeti ya Zanzibar una matatizo kwa sababu makundi mengi hayashirikishwi Katika uandaaji wa bajeti hiyo na wamekuwa wakilalamikia utaratibu huo mwaka hadi mwaka.
Katibu huyo alisema kwa mujibu wa sheria kifungu namba 10 ya mwaka 1986 imeweka kamati za uongozi katika kila idara pamoja na kamati za uongozi katika kila wizara za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini tatizo kubwa wizara haziwashirikishi katika uandaaji wa bajeti.
“Shirikisho letu halikushirikishwa katika uandaaji wa bajeti hii hasa katika suala la maslahi kwa wafanyakazi na kama tunavyojua wafanyakazi wetu kwa muda mrefu kilio chao kikubwa ni mishahara kutaka kuongezewa…
….bajeti imetaja kuongezwa kwa kiwango cha mishahara lakini kwa nini kuwepo na usiri mimi nadhani suala hilo liwekwe bayana ni kiwango gani cha ziada kitakachoongezwa ili wafanyakazi wenyewe wajue na hiyo ni haki yao ya msingi wao kujua” alisema Katibu huyo.
Naye mwananchi kutoka wilaya ya Kati Mwanajuma Salmin, alisema ingawa serikali inakusudia kukibadili kilimo, lakini inapaswa kuhakikisha inaangaliwa vyema hila za wafanyabiashara kupandisha bei za vyakula.
Mwanajuma alisema bidhaa kama vile mchele, unga ngano, sembe na sukari, hazigusiki madukani na kila siku zimekuwa zikibadilika bei wa kupanda juu huku vikiwepo visingizio mbali mbali ambavyo serikali ina uwezo wa kuvidhibiti.

BALOZI SEIF AFUMANIA UZEMBE HOSPITALI YA MNAZIMMOJA

Balozi Seif ‘afumania’ uzembe hospitali Mnazimmoja

• Ashitukiza usiku ashangazwa alichoshuhudia
• Akuta umeme umezimwa, mwashaji jenereta hayupo
• Alia maisha ya wagonjwa kuwekwa rehani
Na Abdulla Ali, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amekemea vikali tabia isiyoridhisha ya baadhi ya wahudumu wa afya katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja ya kuhatarisha maisha ya wananchi wenzao kwa kutowajibika ipasavyo.
Balozi Seif Iddi alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya ghafla usiku hospitalini hapo juzi, kufuatia shutuma na malalamiko ya wananchi juu ya vitendo visivyoridhisha hospitalini hapo na utoaji mbaya wa huduma uanofanywa na baadhi ya watendaji.
Alisikitishwa, kushangazwa na kukasirishwa na kitendo cha fundi wa jenereta kutowepo kazini wakati umeme ulipokatika na kusitisha huduma zote za hospitali hadi alipofuatwa nyumbani kwa gari la kuchukulia wagonjwa baada ya muda wa zaidi ya nusu saa.
Makamu huyo wa Pili wa Rais alisema kitendo hicho kimeonesha dharau kazini na kingeweza kusababisha vifo kwa waliokuwa wakihudumiwa kwa wakati huo.
Hata hivyo alieleza kuridhishwa kwake na baadhi ya Madaktari na wahudumu wengine kwa namna wanavyochapa kazi sambamba na jitihada za Serikali za kudumisha huduma hiyo na kuwataka waongeze bidii wakati Serikali inajitahidi kuimarisha mazingira yao.
Alisisitiza haja ya uvaaji wa sare kazini ili waonekane nadhifu na kuwatafautisha na watu wa kawaida wanaoingia bila ya mpango na kusababisha vurugu kwa wagonjwa Mawodini.
Kuhusu uimarishaji wa huduma hizo, Daktari wa zamu katika wodi mbili za Surgical, Dk. Abdulrahman Yussuf aliyekuja kwa mazoezi ya vitendo kutoka Tanzania Bara, alisema ametiwa moyo na jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) za kuimarisha huduma pamoja na za kwao na kusema yuko tayari kufanya kazi Zanzibar baada ya kuhitimu Chuo.

WAWAKILISHI KUJADILI BAJETI LEO

Wawakilishi kujadili bajeti leo

• Spika awataka kuwawakilisha vyema wananchi
Na Mwanajuma Abdi
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, leo wataanza kujadili Bajeti ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Majadiliano hayo yatafanyika ukumbi wa Baraza hilo huko Chukwani, ambapo wajumbe watapata nafasi ya kujadili, kuchangia, kuchambua na kutoa ushauri kwa Serikali juu ya Bajeti hiyo.
Mbali ya bajeti hiyo wakati wa asubuhi wajumbe wa Baraza hilo wataendelea katika uulizaji maswali na kupatiwa majibu na Mawaziri wa wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kujadiliwa kwa bajeti hiyo inatokana na kuwasilishwa Jumatano iliyopita katika Baraza hilo, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee aliwasilisha ikiwa ni mara ya kwanza tokea Serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kuingia madarakani mwaka jana.
Waziri Omar alipowasilisha hotuba ya bajeti hiyo alisema
Serikali inatarajia kutumia shilingi bilioni 613.08 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na y a maendeleo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Bajeti hiyo, imeweka wazi kwamba Serikali haikusudii kupandisha kodi yoyote, ambapo imekusudia kuimarisha zaidi usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vianzio vilivyopo na kuziba mianya inayotumika katika kuepuka, kupunguza au kukwepa kulipa kodi pamoja na kuendelea kufuatilia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini.
Miongoni mwa maeneo yaliyoainishwa kuwa ni kipaumbele katika bajeti hiyo ni pamoja na kutekeleza mkakati wa muda wa kati, unaolenga ukuaji wa haraka ambao utahakikisha maendeleo ya wananchi na ukuaji wa uchumi endelevu na huduma bora kwa ustawi wa jamii.
Kulingana na malengo ya mkakati huo ni kuimarisha huduma za afya, misisitizo zaidi ukilenga katika ununuzi wa vifaa vya hospitali, dawa muhimu pamoja na kuimarisha huduma zinazotolewa na vituo vya afya vya wilaya/mikoa.
Aidha mengine ni kuimarisha elimu kwa kupunguza tatizo la uhaba wa madawati, vifaa vya maabara, vifaa vya kufundishia na kumaliza ujenzi wa madarasa yaliyoanzishwa na wananchi pamoja na kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama.
Waziri Yussuf alieleza vipaumbele vyengine ni kuimarisha sekta ya kilimo cha umwagiliaji, mbegu bora, mbolea na matumizi ya matrekta pamoja na miuondombinu ya kiuchumi kiwani ni kuendeleza miradi ya barabara, umeme katika maeneo ya kilimo na kufanyika tafiti mbali mbali za uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo.
Wakati huo huo, Himid Choko kutoka Baraza la Wawakilishi anaripoti kuwa, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, amewahimiza Wajumbe wa Baraza hilo kuwawakilisha vyema wananchi wao kwa kuwatetea katika vipaumbele vitakavyowasaidia kuimarisha hali zao za maisha kwa upatikanaji wa huduma muhimu wakati wa kujadili Bajeti ya Serikali.
Amesema Wajumbe wa Baraza hilo ndio dhamana wa kuidhinisha matumizi ya fedha za serikali hivyo hawana budi kuhakikisha kwamba fedha hizo zinaelekezwa katika miradi inayolenga kupunguza matatizo ya wananchi wenyewe.
Kificho aisema hayo jana wakati akifunga semina ya kuwajengea uwezo waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu mchakato na uchambuzi wa Bajeti katika ukumbi wa Zanzibar Ocean View Kilimani.
Hivyo Kificho amewataka wajumbe hao kuipitia kwa kina Bajeti ya Serikali na hatimae kuichambua na kuijadili katika maeneo yote hasa yale yanayogusa utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Nae mkufunzi kutoka chuo cha Utawala wa fedha Chwaka Said Mohammed Khamis akitoa mada kuhusiana na Uchambuzi wa Bajeti ya Serikali, amesema ni muhimu kwa wajumbe hao kutambua viashiria vya uchumi kama vile Pato la Taifa, Mabadiliko ya Bei za Bidhaa na Huduma, Hali ya Ajira Nchini, urari wa mapato na matumizi ya Nchi na hali ya Biashara nchini ili waweze kuijadili vyema Bajeti hiyo.
Aidha Said amesema mbinu nyengine ya uchambuzi wa bajeti ni kuzingatia sera za kifedha na kodi ambazo huwa zinatumika kudhibiti mzunguko wa fedha ambao unaathiri katika uchumi pamoja na kutathmini mwenendo mzima wa ukusanyaji wa mapato .
Akiwasilisha mada juu ya mchakato na changamoto za bajeti Mtaalamu kutoka Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo amesema Zanzibar kama nchi nyengine zinazoendelea inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo Vyanzo vidogo vya kodi, kasi ya ukuaji wa utalii usiolingana na na kasi ya ukuaji wa mapato yanayotokana na utalii huo pamoja na mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali kama ilivyoelekezwa katika Mpango mkuu wa wa kupunguza umasikini hapa nchini.
Ameongeza kwamba changamoto nyengine inayoikabili Bajeti ya Zanzibar ni kiwango kikubwa cha utegemezi wa wahisani pamoja na shinikizo la kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani na kiwango kidogo cha fedha za ndani kwa matumizi ya miradi ya maendeleo.
Nae Katibu wa Baraza la Wawakilishi Ibrahim Mzee Ibrahim, amewahimiza wajumbe hao kuzingatia kanuni za majadiliano ya Kibunge huku wakitilia mkazo hoja inayohusika pamoja na kuwatetea wananchi wao.
Semina hiyo ya siku moja imeandaliwa kwa pamoja na Ofisi ya Baraza la Wawakilishi kwa kushirikiana na Ofisi ya Raisi, Fedha, Uchumi na Mipango ya maendeleo ikiwa ni miongoni mwa juhudu za kuwajengea Uwezo wawakilishi ambao mara nyingi wao sio wataalamu wenye elimu na ujuzi wa masuala ya fedha na uchumi ingawa kwa mujibu wa Katiba ndio wenye kazi ya kujadili na kupitisha bajeti ya serikali.
Bajeti ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 20011/2012 iliwasilishwa Jumatano iliyopita na leo inaaza kujadiliwa katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea leo.

MAALIM SEIF ; MSIONGOZE KWA CHUKI, UONEVU WALA UPENDELEO.

Maalim Seif: Msiongoze kwa chuki, uonevu wala upendeleo

Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka viongozi na watendaji wa Ofisi yake, kuwa waadilifu na kufanyakazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuleta ufanisi mahala pa kazi.
Maalim Seif ametoa changamoto hiyo jana, Ofisini kwake Migombani alipokutana na Kamati ya uongozi ya Ofisi hiyo, iliyojadili mapendekezo ya marekebisho ya sheria Nam. 9 ya 2009 ya udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar.
Amewataka viongozi na watendaji hao kuwa makini katika usimamizi wa majukumu yao, kuwa waadilifu kwa wanaowasimamia, pamoja na kutilia mkazo suala la nidhamu.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi hao kujiheshimu binafsi kabla ya wao kuheshimiwa na wanaowaongoza na kuwataka kusimamia vyema majukumu yao bila ya upendeleo, chuki au kumuonea mfanyakazi kwa kuamini kuwa wafanyakazi ni binaadamu kama watu wengine.
Alisema kuna ukweli kuwa nidhamu imeshuka katika maeneo ya kazi, hali inayotokana na usimamizi usioridhisha kutoka miongoni mwa viongozi na watendaji.
Maalim Seif alisema Serikali inalenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuzingatia sifa, muda wa utumishi na utendaji wao wa kazi za kila siku.
Alisema lengo la utaratibu huo ni kuweka tofauti kati ya watumishi waliolitumikia Taifa kwa kipindi kirefu na wale wanaoanza kazi, sambamba na kuwapandisha vyeo wafanyakazi kutokana na utendaji wao uliotukuka.
Aidha aliwataka watendaji hao kujenga ushirikiano wa karibu kati ya taasisi moja na nyingine kwa kuzingatia kuwa mashirikiano ndio njia pekee katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Mapema Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Dk. Omar Shajak, aliwasilisha madhumuni ya waraka huo na kuainisha mapendekezo ya marekebisho katika baadhi ya vifungu vya sheria Nam 9 ya 2009 ya uratibu wa dawa za kulevya Zanzibar.
Mapendekezo yaliyojadiliwa na wajumbe hao yalikuwa ni juu ya matatizo yatokanayo na mapungufu ya sheria husika pamoja na matatizo yatokanayo ni usimamizi wa sheria (ya kiutawala).
Hicho ni kikao cha kwanza cha Kamati ya Uongozi ya Ofisi hiyo, kinachopaswa kukaa kila baada ya miezi mitatu.