Tuesday 25 January 2011

DK. BILAL AFUNGUWA SEMINA ELEKEZI.

MAKAMO wa Rais wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal akifunguwa Semina elekezi ya Wabunge wa Wabenge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iliofanyika katika Ukumbi wa Ubungio Plaza.(Picha na Amour Nassor)

DK.SHEIN ATEUA WAKURUGENZI, MAKAMISHNA WAPYA.

Dk. Shein ateua Wakurugenzi, Makamishna wapya

Na Mwandishi Wetu
Jumatano 26, Januari 2011

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein jana amefanya uteuzi wa wakuu wa taasisi mbali mbali serikalini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, iliezea kuwa uteuzi wa watendaji hao umeanza rasmi jana.

Walioteuliwa katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mkurugenzi Idara Mipango, Sera na Utafiti, Fauzia Mwita Haji, Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi Is-hak Ali Bakari, huku Sheha Mjaja Juma akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Mazingira.

Wengine ni Mkurugenzi Idara ya Watu Wenye Ulemavu, Abeida Rashid Abdulla, ambapo Dk. Omar Makame Shauri anakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya UKIMWI na Fatma Mohammed Omar anakuwa Ofisa Mdhamini wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Pemba.

Katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Sera na Utafiti ni Khatib Said Khatib, huku Hassan Khatib Hassan akiteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi.

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ni Ahmada Kassim Haji, huku Issa Ibrahim Mahmoud akiteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa.

Wengine ni Ali Juma Hamad anakuwa Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, ambapo Iddi Suleiman Suweid anakuwa Mkurugenzi wa Idara ya Upigaji Chapa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali.

Ofisa Mdhamini wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba ni Amran Massoud Amran.

Katika Ofisi ya Rais (Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo), aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ni Idrissa Abeid Shamte, ambapo Ramadhan Senga Salmin ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi.

Omar Hassan Omar ameteuliwa kuwa Mhasibu Mkuu wa Serikali, ambapo Msaidizi Mhasibu Mkuu wa Serikali ni Mwanahija Almasi Ali.

Rais pia amemteua Khatib Mwadini Khatib kuwa Kamishna wa Bajeti, ambapo Said Mohammed Hussein ameteuliwa kuwa Kamishna wa Uhakiki Mali na Mitaji ya Umma.

Aidha Saada Mkuya Salum ameteuliwa kuwa Kamishna wa Fedha za Nje ambapo Mkurugenzi wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dar es Salaam ni Shumbana Ramadhan Taufiq, ambapo Ofisa Mdhamini Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Pemba ni Bakari Haji Bakari.

Rais pia amefanya Uteuzi katika Tume ya Mipango ambapo Ahmed Makame Haji ameteuliwa kuwa Kamishna wa Mipango ya Kitaifa, Maendeleo ya Kisekta na Kupunguza Umasikini.

Kamishna wa Ukuzaji Uchumi, aliyeteuliwa ni Mwita Mgeni Mwita ambapo Seif Shaaban Mwinyi ameteuliwa kuwa Kamishna wa Mipango na Maendeleo ya Watenda Kazi.

MAALI SEIF ATAKA KUMALIZWA UTEGEMEZI WA CHAKULA.

Maalim Seif ataka kumalizwa utegemezi wa chakula

Na Abdi Shamnah
Jumatano 26, Januari 2011
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ameitaka Wizara ya Kilimo na Maliasili kuhakikisha inapunguza kasi ya utegemezi wa chakula kutoka nje.

Maalim Seif alitoa changamoto hiyo jana huko Maruhubi alipokuwa akizungumza na watendaji na wataalamu wa Wizara hiyo ambapo pia alielezwa majukumu na changamoto mbali mbali zinazoikabili wizara hiyo.

Alisema wakati umefika kwa wataalamu wa wizara hiyo kuhakikisha wanamaliza tatizo la utegemezi wa chakula kwa kukuza uzalishaji nchini pamoja na kuiepusha nchi na balaa la njaa.

Alifahamisha kuwa jukumu la Wizara hiyo kuhakikisha kuwa wananchi wa Unguja na Pemba hawafi kwa njaa na kutaka kuwepo mipango itayohakikishia kunakuwepo chakula kutosha na ikiwezekana akiba.

Aidha Maalim Seif, alitaka kuwepo umakini katika matumizi ya ardhi, kwa kigezo kuwa Zanzibar ina eneo dogo la ardhi, linalokaliwa na watu wengi huku kukiwa na mahitaji mengi yakiwemo kilimo, ujenzi, uwekezaji na viwanda.

Aliitaka Wizara hiyo kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha maeneo ya ardhi yanatumika kama ilivyoanishwa, vinginevyo katika kipindi kifupi kijacho kutakuwa hakuna tena eneo la kilimo.

Katika hatua nyingine Maalim Seif aliitaka wizara hiyo kufanya utafiti wa kutosha kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao yanaozalishwa nchini, ikiwemo yale ya matunda na biashara.

Akitoa mfano wa zao la karafuu, Maalim Seif alisema kuna nchi nyingi duniani kama vile Brazil, Indonesia na Comorro zinazozalisha zao hilo kwa wingi, ikilinganishwa na Zanzibar inayozalisha wastani wa tani 6,000 kwa mwaka, hivyo alitaka utafiti huo uimarishe thamani ya karafuu za Zanzibar ili iweze kushindana katika soko la dunia.

Akizungumzia madai ya vijana kuikimbia sekta ya kilimo, alisema mazingira yaliopo katika sekta hiyo hayavutii na kuamini kuwa upo uwezekano wa kupata kiwango kikubwa cha mapato.

Alisema wakati umefika kwa kilimo kuondokana na matumizi ya zana za kizamani na kuelekea katika zana za kisasa sambamba na matumizi ya mbegu bora.

Mapema Waziri wa wizara hiyo, Mansour Yussuf Himid alimueleza Makamu huyo kuwa moja ya tatizo linaloikabili Wizara hiyo ni uhaba mkubwa wa mabwana shamba, ambapo wastani wa mtaalamu mmoja huwatumikia wakulima 1,500 badala ya 450 kama inavyokubalika.

Alisema lililo baya zaidi ni kuwa wataalamu wengi katika fani hiyo wana umri mkubwa, ambao siku zao za kutaafu kazi zinahesabika.

Naye Naibu Katibu mkuu Maliasili Bakar Aseid alisema moja ya changamoto inayoikabili sekta hiyo ni hulka ya binadamu ya kuwinda wanyama na ndege wa asili kiasi cha kutoweka kabisa.

Katika ziara hiyo Maalim Seif alitembelea maeneo mbali mbali ya kilimo ikiwemo mradi wa minazi Kijichi, kitengo cha Utafiti wa kilimo Kizimbani, Chuo cha kilimo, pamoja na mashamba ya viungo.

WIZARA YAANDAA MUONGOZO MATUMIZI YA DAWA.

Wizara yaandaa muongozo matumizi ya dawa



Na Fatma Kassim, Maelezo
Jumatano 26, Januari 2011
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Mohammed Saleh Jidawwi, amesema kuwa kuwepo kwa muongozo wa dawa muhimu katika hospitali, kutasaidia kufanikisha matumizi mazuri ya dawa na kutoa matibabu bora na ya uhakika.

Akizindua kitabu cha nne cha muongozo wa orodha ya dawa muhimu huko Wizara ya Afya, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa kitabu hicho ni muhimu katika suala zima la upatikanaji wa dawa muhimu ambazo zinahitajika hapa nchini.

Alifahamisha kuwa lengo kuu la kuwepo kwa kitabu hicho ni kuweza kujua aina ya dawa ambazo zinatumika hapa nchini na kuziwezesha kufanya marekebisho kwa dawa ambazo hazitumiki na kuingiza zile ambazo kwa wakati huu zinazoonekana zinafaa.

Aidha alisema shabaha ya serikali ni kuwapatia wananchi wake matibabu yaliyobora na ya uhakika, ambapo lengo halitofikiwa iwapo hakutakuwa na utaratibu unaokubalika katika kutekeleza kwa vitendo sera ya afya pamoja na sera ya dawa.

Alisema katika kuzifahamu dawa ambazo zinatumika hapa nchini ni vyema washirika wa maendeleo kutoa misaada yao kwa dawa ambazo zimo katika orodha ya dawa muhimu kwa lengo la kuepuka dawa ambazo hazitohitajika katika mahospitali.

Nae Mfamasia Mkuu wa Wizara ya Afya, Habib Ali Sharif alisema katika kufanikisha huduma za utoaji dawa katika visiwa vya Unguja na Pemba, wana mpango wa kuwa na bohari kuu zaidi ya dawa kwa lengo kutoa huduma zenye ufanisi zaidi.

Alisema kuzinduliwa kwa kitabu hicho cha nne cha muongozo wa dawa ni kujua mahitaji ya dawa katika hospitali na vituo vya afya.

Kitabu hicho hadi kukamilika kwake kimedhaminiwa chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA).

VIKUNDI VYA WEZA VYAPIGWA JEKI MILIONI 33

Vikundi vya WEZA vyapigwa jeki milioni 33

Na Mwandishi Wetu
Jumatano 26.Januari 2011


WANAVIKUNDI 189 wa mradi wa WEZA kisiwani Pemba, wamechangisha jumla ya shilingi 33,145, 000 kupitia washirika wa maendeleo kwa ajili ya kukuza miradi yao midogo midogo.

Afisa Muwezeshaji wa WEZA, Pemba, Zuwena Khamis Omar, aliwataja wafadhili hao kuwa ni Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mradi wa Ushirikishaji na Uwezeshaji (PADEP) na Mpango wa Msaada wa Huduma za Kilimo (ASSP).

Alisema PADEP waliweza kuchangia shillingi 23,045,000, TASAF ilitoa shilingi 9,000,000 na ASSP ilichangia shilingi 1100000.

Alisema fedha hizo zimewafaidisha wanavikundi kutoka Shehia za Mtemani Wingwi wanachama 76, Njuguni 18, Tumbe mashariki 10, Tumbe magharibi wanachama 10, Ukunjwi wanachama 60 na Ole wanachama15.

Kwa upande wake Bimkubwa Omar Othman, Mratibu Shehia ya Mtemani, alisema kikundi cha “WEZA ROHOYO”, kimepata mbuzi 34 na jumla ya shilingi milioni nne taslim kutoka kwa PADEP, mbuzi hao wapo katika hali nzuri na wengine wameanza kuzaa.

Alisema utaalamu wa kuchangisha fedha umewasaidia katika kutafuta wafadhili kwenye miradi yao inayowasaidia kujikwamua kwenye dimbwi la umasikini.

Naye msaidizi mratibu wa Shehia ya Njuguni, Fatma Juma alisema wanavikundi wamebadilika na kwamba wanafanyakazi kutafuta wafadhili kuimarisha miradi yao.

Hata hivyo alisema kuna umuhimu wa kuongezewa ujuzi wa kuchangisha fedha ili wanawake waimarike zaidi kiuchumi.
MAKAMO wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamadi akipata maele
kezo kutoka kwa mtaalamu wa Kilimo cha matndunda katika kituo cha kilimo kizimbani wakati alipofanya ziara kushoto Waziri wa Kilimo Mansoor Yussuf Himid.(Picha na Afisi wa Rais )

WAZIRI FEREJI AITAKA JAMII KUSAIDIA VITA DAWA ZA KULEVYA.

Waziri Ferej aitaka jamii kusaidia vita dawa za kulevya

Na Aboud Mahmoud
Jumatano 26,Januari 2011

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, imesema itaendelea na juhudi na kutoa kila aina ya msukumo kuongeza kasi katika kukabiliana na usafirishaji, uingizaji na utumiaji wa dawa ya kulevya nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej, ameeleza hayo kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Jumuia ya Vijana waliooacha matumizi ya dawa ya kulevya pamoja na wazee katika ukumbi wa Baitul Yamin uliopo Malindi mjini hapa.

Waziri Fatma, alisema serikali na taasisi zake itaendelea kuchukuwa hatua katika kukabiliana na suala la dawa za kulevya na hivyo kuomba mashirikiano ya pamoja katika kukabiliana na vita hivyo.

Aidha Waziri huyo alisema matumizi ya dawa za kulevya yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, kutokuwepo mani, magonjwa ya akili , UKIMWI na hata vifo ambapo jamii imekuwa ikishuhudia.

Alifahamisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya yanachangia kudumaza maendeleo na mustakabali wa vijana ambao ndio watumiaji wakubwa wa dawa hizo.

“Vijana na wazazi tuliopo hapa sote ni mashuhuda wa haya na ndio maana tupo hapa hivyo nina imani maazimio na majadiliano yetu yatakuza ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na vijana”,alisema Waziri huyo.

Aliiomba jamii kutowatenga wale walioamua kuachana na matumizi ya dawa hizo na kuwa nao karibu kwa vile wanahitaji msaada wa kifamilia na kupata huduma zinazotahili.

Katika mkutano huo Waziri Fatma alimkabidhi Nishani maalum kijana Abdurahman ambaye ametimiza mwaka mmoja bila ya kutumia dawa za kulevya, ambaye anaishi katika nyumba za kurekebisha tabia na kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ‘Sober House’ iliyopo Tomondo.

Mkutano huo umedhaminiwa na Taasisi ya American International Health Alliance (AIHA) ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Dk. Omar Dadi Shajak, Mkurugenzi wa Idara ya Kupambana na Dawa za kulevya, Wawakilishi wa Taasisi mbali mbali za kupambana na Dawa za kulevya kutoka Tanzania Bara pamoja na wazazi wa walioacha madawa ya kulevya.

DIWANI FUONI AWAONYA WANAOCHAFUA MAZINGIRA.

Diwani Fuoni awaonya wanaochafua mazingira

Na Haji Nassor ZJMMC.
Jumatano 26, Januari 2011.

DIWANI wa wadi ya Fuoni, Wilaya ya Magharibi Unguja, Shaka Hamdu Shaka, amelaani tabia inayofanywa na baadhi ya wananchi hapa Zanzibar ya uchafuzi na uharibifu mazingira ikiwa ni pamoja na ukataji miti, uchimbaji mchanga, mawe na ujenzi holela.

Alisema ni vigumu kwa sasa kurejesha haiba ya visiwani kutokana na jamii kuendelea kufanya uharibifu wa mazingira siku hadi siku.

Akizungumza katika hafla ya kugawa vifaa vya usafi wa mazingira kwa wananachi wa Shehia ya Maungani, Wilaya ya Magharibi jana, Diwani huyo alisema wakati umefika jamii kujikosoa kwa kuchukia aina yoyote ya uharibifu wa mazingira kwa vile ni hatari kwa mendeleo.

Hivyo, aliwashauri wananchi kuhakikisha wanayatunza na kuyadumisha mazingira yanayowazunguuka, ili kizazi kijacho kirithi haiba nzuri yenye vivutio kama ambavyo ilikuwa katika miaka iliyopita.

Alisema uhifadhi wa mazingira hauhusishi taasisi maalum lakini ni jukukumu la watu wote kwa sababu hali ikiwa mbaya itamuathiri kila mtu.

Katika hatua nyengine, Diwani huyo aliwashauri wananchi wa wadi yake kuhakikisha hawawapi nafasi wananchi wakorofi wanaotupa taka ovyo pamoja na kutohifadhi umwagaji maji mitaani.

Alibainisha kwa kusema hilo likiachiwa kuchukua nafasi basi hali itakuwa mbaya wakati wowote mvua zitakaponyesha na kuiathiri jamii kwa kuzuka maradhi ya miripuko.

Aidha aliwasifu wananchi wa wadi ya Maungani kutokana na uamuzi wao wakufanyakazi pamoja kwa kupambana na uchafuzi wa mazingira.

Alifafanua kua kikundi hicho bila ya nguvu za wanashehia wenzao hakitoweza kufikia malengo yao ambapo Diwani huyo katika kuhakikisha Maungani inadhibiti suala la usafi wa mazaingira pia alikabidhi mifuko mitano ya saruji ili kuendeleza ''dampo'' kuhifadhia taka.

Pia alikabidhi vifaa mbali mbali vya usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na mabero, slesha, majembe, mapanga, reki ambapo vifaa hivyo pamoja na saruji vinathamani zaidi ya shilingi 700,000 na kuahidi kuchangia kifedha hali itakaporuhusu.

VIINGILIO KMKM, MOTEMA PEMBE VYATAJWA.

 Viingilio KMKM, Motema Pembe vyatajwa



Na Mwajuma Juma
Jumatano 26, Januari 2011

UONGOZI wa timu ya KMKM, umetangaza bei za tiketi kwa ajili ya kushuhudia mpambano wa kuwania Kombe la Shirikisho la Soka Afrika kati ya timu hiyo na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mchezo kati ya miamba hiyo umepangwa kurindima Januari 29, saa kumi na nusu alasiri kwenye uwanja wa Amaan, na ule wa marudiano utafanyika wiki mbili baadae mjini Kinshasa DRC.

Akivitaja viingilio hivyo kwa mwandishi wa habari hizi, Katibu wa Michezo wa kikosi hicho Sheha Mohammed, amesema kwa wale watakaopenda kukaa katika jukwaa kuu, watalazimika kujikamua shilingi 5,000, na pembezoni mwake shilingi 2000, ambapo jukwaa la Urusi na nyuma ya magoli bei itakuwa shilingi 1000.

Alieleza kuwa uongozi wake umeamua kuweka viingilio nafuu ili mashabiki wa soka wa Zanzibar wamiminike kwa wingi na kupata fursa ya kuwaona wawakilishi wao wakipeperusha bendera ya nchi yao katika soka la kimataifa.

Hivyo, aliwataka wapenzi na wadau wa soka nchini kujitokeza kuwashangiria wanamaji hao watakaokuwa wakijaribu kukata tiketi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Imefahamika kuwa katika mchezo huo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,

KENNEDY CENTER KUWAFUNDA WASANII ZANZIBAR

 Kennedy Center kuwafunda wasanii Zanzibar

Na Aboud Mahmoud
Jumatano Januari 26, 2011
TAASISI ya kimataifa ya sanaa ‘Kennedy Center’ ya Marekani, imeandaa mafunzo maalumu kwa wadau wa sanaa wa Zanzibar, yaliyopangwa kufanyika Februari 12, katika ukumbi wa Makumbusho ya Kasri Forodhani.

Mratibu wa semina hiyo ambae pia ni mwanafunzi wa kituo hicho Kheri Abdullah Yussuf, amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuendeshwa na Rais wa taasisi hiyo Michael M. Kaiser.

Alifahamisha kuwa, mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu juu ya nyanja mbalimbali za kisanaa, ikiwemo kustawisha taasisi za sanaa zinazojitegemea, mikakati ya sanaa ya muda mrefu, utafutaji wa rasilimali ya kuendeshea kazi hizo, pamoja na utendaji bora kwenye bodi za sanaa.

Kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo, Kheri alifahamisha kuwa, semina hiyo itawashirikisha wadau mbalimbali miongoni mwa viongozi wa sanaa nchini kutoka katika taasisi za kiserikali na binafsi.

Kheri alieleza kuwa kufanyika kwa semina hiyo ya mafunzo hapa Zanzibar, kutaleta faraja kubwa katika tasnia ya sanaa ambayo ni miongoni mwa mambo yanayoitangaza nchi kimataifa.

Mbali na Zanzibar, Kheri alisema mtaalamu huyo wa sanaa, ataendesha kozi kama hizo katika nchi nyengine nne za Afrika ambazo ni Nigeria, Uganda, Kenya na Zimbabwe ambazo zote zina wanafunzi wa kituo hicho.

Kheri ni mwanafunzi pekee Mtanzania katika kituo hicho kilichoko Marekani, tangu ajiunge nacho mwaka 2009.

ABBAS KUIBEBA ZANZIBAR OCEAN VIEW AFRIKA

Abbas kuibeba Zanzibar Ocean View Afrika

Na Salum Vuai
Jumatano  Januari 26, 2011.
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimemruhusu kocha wa timu za vijana Abdelfatah Abbas, kuungana na benchi la ufundi la wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Zanzibar Ocean View, kuisaidia katika resi za kusaka ubingwa.

Msaidizi Katibu wa ZFA Masoud Attai, amesema chama chake kimeridhia ombi la mabingwa hao wa soka Zanzibar kwa vile kinatambua ushiriki wake kwenye mashindano hayo, ambapo itakuwa ikipeperusha bendera ya Zanzibar.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo Hashim Salum, amesema baada ya kutafakari ugumu wa michuano hiyo, uongozi wa klabu yake umeona ni vyema umpate kocha huyo ili kuliongezea nguvu benchi la ufundi, na kwa kuwa inaamini ana uwezo mkubwa wa kuisaidia ili iweze kufanya vizuri.

Hata hivyo, amefafanua kuwa kocha huyo raia wa Misri, atafanya kazi na kikosi chake kwa ajili ya mashindano hayo tu kwa kadiri itakavyoendelea, na baada ya hapo atarudi kushughulikia kazi iliyomleta nchini kuzinoa timu za taifa.

Aliongeza kuwa, Mmisri huyo ambaye tayari ameanza kibarua hicho tangu Jumatatu iliyopita, atashirikiana na makocha wa timu hiyo Said Omar Kwimbi pamoja na Saleh Ahmed ‘Machupa’, kuiandaa timu hiyo inayokabiliwa na kazi ngumu ya kuwatoa wawakilishi wa DRC AS Vita, kwenye kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza na gazeti hili jana asubuhi kwenye uwanja wa Mao Tsetung ambako kikosi hicho kinafanya mazoezi yake,

Abbas alisema amefurahishwa mno na uonozi wa timu hiyo kumuona anafaa kutoa mchango wake, na kuahidi kuwa atashirikiana vyema na wenzake kuhakikisha wanaleta mafanikio.

“Ingawa nimeletwa kufundisha vijana wa timu za taifa, lakini kwa kuwa niko Zanzibar najiona ni miongoni mwa raia wa nchi hii, hivyo niko tayari wakati wowote kuisaidia klabu yoyote itayonitaka hasa kwenye michuano ya kimataifa”, alifafanua Mmisri huyo.

Hiyo itakuwa mara ya tatu kwa kocha huyo kuzisaidia klabu za Zanzibar zinaposhiriki mashindano ya klabu barani Afrika, ambapo mwaka jana aliibeba Miembeni ilipoikabili Petro Jet ya Misri katika michuano ya Kombe la Shirikisho,

Aidha mwaka huohuo, alikwishaanza kuinoa Mafunzo iliyokuwa ikijiandaa kwa mashindano ya Kombe la Kagame, lakini akaiacha njiani kutokana na suitafahamu iliyoibuka kati yake na benchi la ufundi la timu hiyo.

Zanzibar Ocean View inaanza kutupa karata yake ya kwanza Jumapili Januari 30, kwenye uwanja wa Amaan, kwa kuikaribisha AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kabla kurudiana nayo wiki mbili baadae mjini Kinshasa.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifungua rasmi mafunzo kwa vitendo ya madaktari wachanga na upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo kutoka katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ulifanyika katika hoteli ya Sea Cliff jijini Dar tarehe 24.1.2011. John Lukuwi

WATAKAONYANYASA WAFANYAKAZI KUPIGWA 'STOP'

Watakaonyanyasa wafanyakazi kupigwa ‘stop’ Zanzibar

Na Mwanajuma Abdi

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema haiko tayari kuwavumilia wawekezaji watakaowanyanyasa wafanyakazi katika sekta ya utalii kwa kukiuka sheria za nchi.

Hotuba ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdallah Shaaban ilieleza.

Taarifa hiyo ilitolewa katika Mahafali ya Chuo cha The African Utalii College iliyowajumuisha wahitimu 69 wa Diploma na Cheti, yalifanyika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

Alisema serikali haitowavumilia wawekezaji wenye tabia hiyo, wakiwa wa nje ama wa ndani, ambao kwa kufanya hivyo watakuwa wanakiuka sheria zilizowekwa katika sekta hiyo ili kuweza kupata haki zao, sambamba na wale wanaofukuzwa kazi ovyo.

Kauli hiyo aliitoa kufuatia wanafunzi hao kusema kwamba kero kubwa inayoikabili sekta ya utalii ni kukatishwa kwa mikataba ghafla, kufukuzwa ovyo pamoja na kunyanyaswa.

Alisema serikali inatoa ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji kuja nchini kuwekeza ili uchumi uweze kuimarika lakini haipo tayari kuona watu wake wananyanyasika.

Aidha alifahamisha kuwa, mahafali hayo yawe kichocheo kwa kuimarika sekta utalii, ambayo inachukuwa nafasi kubwa katika kukuza uchumi na pato la taifa, hivyo aliwataka wahitimu hao kujituma zaidi ili kufikia malengo ya Zanzibar kuwa na wataalamu katika kada mbali mbali.

Maalim Seif alisema kuanzishwa kwa Chuo hicho Zanzibar ni ishara njema ya kukuzwa kwa viwango vya elimu katika sekta hiyo pamoja na kufikia malengo ya kuwa na utalii wenye mazingira bora ya utoaji wa huduma.

Alisema Zanzibar inasifika duniani kote kwa watu wake wanaheshimu mila na desturi zao na kutoa ushirikiano kwa wageni wanaofika nchini, jambo ambalo linasaidia kuongezeka idadi ya watalii mwaka hadi mwaka.

Hata hivyo, aliwashauri wahitimu hao kuvitumia vyeti hivyo wenyewe kwa vile ndio wataoweza kuvifanyia kazi na sio kuwapa watu wengine wasiohusika kunaweza kukasababisha mzigo kwa muajiri.

Mapema Mkuu wa Chuo hicho, Sostenes Mugeta Mafuru aliomba Serikali iendelee kuipa ushirikiano sekta binafsi na kupewa kazi wanazoweza kuzifanya wazalendo badala ya kupewa kipaombele wageni.

Risala ya wahitimu, iliyosomwa na Fatma Khamis iliiomba Serikali kuwaangalia wawekezaji katika sekta ya utalii, wanaowanyanyasa wafanyakazi wachukuliwe hatua.

Wahitimu 60 walitunukiwa vyeti vyao kwa kufaulu masomo ya kutembeza watalii, masomo ya lugha kama ya kihispania, kingereza, kitaliana na kiarabu, mafunzo ya mawasiliano ya kompyuta, mapischi na utoaji wa huduma za vinywaji na kutunza vyumba.

WAWAKILISHI WACHOSHWA UINGIZAJI BIDHAA MBOVU

Wawakilishi wachoshwa uingizaji bidhaa mbovu

Wataka wanaoingiza wasifumbiwe macho
Na Mwantanga Ame

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameitaka serikali kutowaonea haya wafanyabiashara wadanganyifu wanaoingiza nchini bidhaa zilizopitwa na wakati.

Wajumbe hao walieleza hayo jana walipokuwa wakichangia Mswada wa Sheria ya kuweka masharti ya uendelezaji, ukuzaji na uwekaji wa Viwango na Ubora wa Bidhaa, uliowasilishwa na Waziri wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui.

Wajumbe hao walisema wakati wa kufumbiwa macho waingiza bidhaa zisizo na viwango kwa kuangalia misingi ya udugu, ujamaa na urafiki umepitwa na wakati.

Walisema hatua ya serikali kuuwasilisha mswada huo wa sheria ni jambo la msingi kwani awali walishindwa kulifanyia kazi suala la bidhaa hizo, kutokana na baadhi yao kutishiwa maisha na kufukuzwa kazi na wanaowalinda wahusika hao.

Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, alisema kuliwahi kutishiwa maisha kwa watu watakaowachukulia hatua waingiza bidhaa mbovu nchini.

Alisema wakati serikali ikiwa katika hatua ya kuisubiri sheria kufanya kazi zake ingepaswa kuwabana wafanyabiashara wa soko la ndani kutengeneza biashara zao katika viwango, kwani inawezekana kabisa wafanyabiashara wasipowekewa masharti wakasababisha bidhaa za wengine zikashindwa kutumia masoko ya nje kama ilivyojitokeza katika biashara ya embe iliyozuiliwa Dubai kutokana na kupigwa moto.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni, Mahmoud Mussa alisema ni vyema serikali wakati ikipitisha sheria hiyo kuviangalia vipengele vilivyomo visiweze kumtia hasara mfanyabiashara wa Zanzibar, kutokana na uzembe wa baadhi ya mawakala.

Akifafanua kauli hiyo alisema baadhi ya mawakala wamekuwa wakiingiza mizigo ya watu bila ya kuzingatia nchi inakokwenda, jambo ambalo linaweza kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wa Zanzibar itapobainika kuwa bidhaa alizobeba si zake na hazina kiwango.

Kwa upande wake Mwakilishi Abdalla Juma, alisema ni vyema kwa serikali baada ya kupitishwa sheria hiyo ibadilike katika kulisimamia tatizo hilo, kwani Zanzibar imegeuzwa jaa la utupaji wa vyakula vibovu pamoja na vifaa visivyofaa kutumiwa vikiwemo vya ujenzi.

Alisema hivi sasa kuna bidhaa za asilimia 80 katika maduka ya Zanzibar zimeonekana hazina viwango hasa mchele jambo ambalo tayari limewasababishia baadhi ya watu kuuguwa ugonjwa wa magoti na kushindwa kutembea.

Nae Mwakilishi Suleiman Hamad, alisema kuna tatizo kubwa la baadhi ya watendaji wanaopewa majukumu katika kusimamia vitengo vya biashara kutowajibika ipasavyo jambo ambalo litahitaji kuangaliwa.

Alisema Mkemia Mkuu baada ya kupitishwa sheria hiyo inatarajiwa kuona anatekeleza majukumu yake vyema bila ya kufanya uzembe ambao utasababisha matatizo hayo kuendelea kutokea nchini.

Mwakilishi wa Mfenesini, Ali Abdalla Ali, alisema usimamizi wa sheria hiyo ni moja ya jambo la msingi ambalo litahitaji kufanyiwa kazi ili kuweza kuondolewa shaka kwa Idara itayopewa jukumu kusimamia eneo hilo.

Mwakilishi wa Viti Maalum, Raya Hamad Suleiman, alisema licha ya serikali kuliangalia tatizo hilo pia italazimika kuviangalia vitu vinavyoingizwa nchini hasa mitumba ambayo inaingizwa ikiwa imechoka kimatumizi.

Mapema Waziri wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui, alisema sheria hiyo imebeba maeneo mengi yatayoweza kuleta mabadiliko ya msingi katika kuifanya Zanzibar kuwa yenye kuendesha vyema sekta ya biashara.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo, Salmin Awadh Salmin, alisema hali ya uingizwaji wa bidhaa Zanzibar bado sio nzuri kutokana na kutokuwa na uthibitisho rasmi wa kukaguliwa na zile zinazotoka nchini kwenda nje.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema inawezekana yaliojitokeza juu ya kusimamia shughuli hizo kunasababishwa na migongano ya sheria jambo ambalo sio zuri kuachiwa kuendelea kwa hivi sasa kwa vile inawezekana ndio chanzo cha kutokea yanayojitokeza sasa.

Mwenyekiti huyo alisema wakati serikali inaendelea kuandaa mazingira mazuri ya usimamizi wa viwango ni vyema ikaenda sambamba na kuandaa sheria itayokuwa inamhusu Mkemia Mkuu wa serikali ili kumuwezesha mfanyabiashara asieridhika na ukaguzi iwe anaweza kukata rufaa kwa Mkemia Mkuu.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi kitaendelea tena leo ambapo wajumbe hao watayapitia masuala na majibu ya Wajumbe hao na kuyapatia ufafanuzi kutoka kwa watendaji wakuu wa serikali.

MAREKANI KUIWEZESHA TANZANIA KATIKA KILIMO.

Marekani kuiwezesha Tanzania katika kilimo

Na Premi Kibanga, Dar es Salaam

Tanzania imeteuliwa kuwa moja ya nchi nne duniani itakayofaidika na mpango maalum wa serikali ya Marekani unaojulikana kama Feed The Future (FTF).

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso E. Lenhardt alimueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete jana kwenye mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam.

“Huu ni mpango maalum unaolenga katika kuendeleza na kukuza kilimo, kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza uhaba wa chakula”, Balozi Lenhardt alimueleza Rais Kikwete.

Balozi huyo alimuhakikishia Rais Kikwete kuwa Marekani imekusudia kushirikiana na Tanzania katika juhudi za kuinua kilimo.

Balozi Lenhardt, alisema mpango huu sio tu utaongeza upatikanaji wa chakula nchini, lakini pia utaongeza uwezo wa Tanzania katika kufanya mambo mengi zaidi katika sekta ya kilimo.

"Mpango huu utaipatia Tanzania vitendea kazi na kuiwezesha kujenga uwezo wa kuzalisha zaidi na kutengeneza fursa nyingi zaidi", aliongeza Balozi huyo.

Nchi zinazolengwa katika mpango huu ni Tanzania, Ghana, El Salvador na Ufilipino.

Balozi Lenhardt alisema Tanzania na nchi hizo zimechaguliwa kutokana na juhudi zake katika utawala bora, juhudi za kukuza kilimo, kuwa ardhi ya kutosha, na maji.

Balozi Lenhardt alisema

maeneo yatakayoanza kufaidika na mpango huu ni Zanzibar, Morogoro, Dodoma, Manyara, na maeneo ya kanda za juu Kaskazini na za Kusini mwa Tanzania.

Kwa upande wake Rais Kikwete, aliishukuru serikali ya Marekani na alimueleza Balozi Lenhardt kuwa msaada huu ni muhimu kwa Tanzania katika sekta ya kilimo ambayo inabeba asilimia 80 ya ajira yao.

"Tukiongeza uzalishaji katika kilimo tutaweza kuwafikia Watanzania kwa asilimia 80 ambao wanategemea kilimo, na huo ni msaada na juhudi kubwa sana”. Rais alisema.

HAJA BINAFSI YA TUNDU LISSU YAIVA

Hoja binafsi ya Tundu Lissu yaiva

Na Jumbe Ismailly, Singida

MBUNGE wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, amedhamiria kuwasilisha hoja binafsi katika kikao kijacho cha Bunge, ambayo ina madhumuni ya kutaka iundwe kamati ya Bunge kuchunguza matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI).

Mbunge ambaye ni mwanasheria maarufu, alitangaza azma hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hoteli ya Aque Vitae, iliyopo mjini Singida.

Alisema katika hotuba ya Waziri mkuu aliyoitoa katika kikao cha Bunge cha mwezi Juni, mwaka jana, serikali kupitia Bunge hilo ilitenga fedha nyingi kwa ajili ya Mkoa wa Singida kugharamia sekta ya elimu.

Alisema katika fedha hizo zilizoidhinishwa na Bunge hadi kufikia mwezi Machi mwaka jana ni shilingi 1,187,000 ndizo zilizokuwa zimetumika na kwamba 905,000,000 zilirudishwa hazina baada ya kukosa kazi ya kufanya.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili Mkoa wa Singida umerudisha Hazina zaidi ya shilingi 1,350,000,000 zilizokuwa zigharamie sekta ya elimu huku akihoji kwa nini wananchi wachangishwe wakati fedha zinarejeshwa hazina.

"Watanzania wangependa kujua hizi fedha zimerudi kweli hazina au zimetumika kwa mambo mengine tusiyoyajua, ndiyo sababu nyingine ya kupeleka hoja binafsi ya kutaka Bunge lichunguze hii ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, ili Bunge linalotoa fedha liridhike kwamba kweli hii fedha haijatumika visivyo”,alisema Lissu.

Mbunge huyo alihoji sababu zilizofanya zisitumike wakati Watanzania wanachangishwa fedha kwenye elimu kwa nguvu bila kuwepo sheria na utaratibu.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Dar-es-Salaam, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Singida,Yusufu Kipengele alikanusha habari hizo na kuongeza kwamba mpaka sasa ofisi yake inadaiwa na wazabuni wadogo wadogo shilingi milioni 16.

"Mimi mwenyewe nadaiwa na wazabuni wadogo wadogo shilingi milioni kumi na sita kwani mpaka sasa hupatiwa fedha kidogo tu za kuendeshea ofisi na ninavyofahamu mimi ni kwamba kila Halmashauri inadaiwa na wazabuni wa aina hiyo siyo chini ya shilingi milioni ishirini kila moja", alisema.

Monday 24 January 2011

WAFANYAKAZI wa Idara Utunzaji wa Barabara wakiziba kiraka baada ya kufanyika kazi bomba la mbaji safi lilokuwa limepasuka eneo la Mtoni likiwa limepita katika barabara hiyo likipeleka maji mjini.(Picha na Othman
Maulid)

WATOTO WA DK. SHEIN WANGA'ARA MAKUNDUCHI

Watoto wa Dk. Shein wang’ara Makunduchi

Na Mwajuma Juma

TIMU ya soka ya Ofisi ya Rais, Ikulu, juzi iliwatoa nishai wenyeji wao Jamhuri ya Makunduchi, kwa kuichakaza mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa huko Makunduchi.

Katika pambano hilo ambapo watoto wa Dk. Shein walitawala kwa muda wote, walipata mabao yao kupitia kwa wachezeji Makame aliyefunga magoli mawili pamoja na Omar Himid.

Katika mchezo mwengine wa kirafiki, timu ya soka ya Zanzibar Veterans, iliiadhibu bila huruma Baja Veterans kwa kuibanjua mabao 5-1, kipute kilichopigwa uwanja wa Amaan nje.

Mabao ya washindi katika mtanange huo, yalifungwa na Ali Abdallah, Hakim Mohammed, Nassor Mwinyi ‘Bwanga’ na Suluhu Hassan, wakati lile la kufutia machozi kwa Baja lilinasishwa kimiani na Abeid Jiwe.

Michezo yote hiyo ilichezwa kwa lengo la kudumisha urafiki kati ya timu

CULTURE YAPATA VIONGOZI WAPYA

 Culture yapata viongozi wapya

Na Salum Vuai

KLABU ya muziki ya taarab na maigizo Culture. Imepata viongozi watakaiongoza kwa kipibndi cha miaka mitatu ijayo.

Hatua hiyo imekuja kutokana na uchaguzi mkuu wa klabu hiyo kongwe nchini uliofanyika Januari 23, kwenye makao yake makuu yaliyopo Vuga m,mjini Zanzibar.

Katika uchaguzi huo uliotanguliwa na mkutano mkuu ambao ulipokea ripoti ya utendaji wa klabu hiyo kwa kipindi kilichopita, Khamis Mikidadi Ali alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti, huku nafasi ya Msaidizi Mwenyekiti ikienda kwa Said Mwinyi Chande.

Taimour Rukuni Taha, alifanikiwa kushika tena nafasi ya Katibu Mkuu, ambapo msaidizi wake anakuwa Hassan Suleiman ‘Chita’ ambaye pia anavaa kofia ya ukatibu mwenezi.

Wengine waliochaguliwa kuongoza kl;abu hiyo na nafasi zao zikiwa kwenye mabano ni pamoja na Chimbeni Kheri Chimbeni (Mshika Fedha), Masoud Mohammed Masoud (Msaidizi Mshika Fedha), Ali Hassan Ali (Mkurugenzi Muzeka) na msaidizi wake anakuwa Juma Abdallah Othman.

Katika safu hiyo ya uongozi pia wamo Makame Kombo (Mkuu wa Michezo), Haaji Nahoda (Mkuu wa Jumba), na wajumbe wawili wa Halmashauri Kuu ambao ni Ali Mrisho Mkanga pamoja na Mtumwa Mbarouk Mamboka.

Viongozi wote hao walitoa ahadi ya kusimamia vyema utekelezaji wa maazimio yaliyomo kwenye mpango kazi wa klabu hiyo kwa kipindi kijacho, na kurekebisha kasoro mbalimbali za kiutendaji zilizojitokeza kabla kwa lengo la kuiimarisha klabu hiyo iliyoasisiwa mwaka 1965.

UWANJA WA MAO TSETUNG KUFANYIWA MATENGENEZO.

 Mao Tsetung kufanyiwa matengenezo

Na Aboud Mahmoud

UONGOZI uliochaguliwa hivi karibuni kusimamia uwanja wa michezo wa Mao Tsetung, umesema unakusudia kuufanyia matengenezo uwanja huo katika sehemu zote muhimu.

Msaidizi Meneja wa uwanja huo Abdullah Thabit 'Dula Sunday', amesema kwa kushirikiana na Meneja wake Hassan Abdulnabi ‘Teso’, watahakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Maeneo aliyoyataja kuwa yatapewa kipaumbele, ni pamoja na ujenzi wa choo uwanjani hapo.

"Kuna sehemu nyingi zinazohitaji kufanyiwa matengenezo katika uwanja huu, kuna mambo mengi muhimu kuwemo katia uwanja wa michezo kwa mfano vyumba vya kubadilishia nguo kwa wanamichezo, waamuzi na kadhalika”, alisema.

Hata hivyo, hakueleza ni wapi wanatarajia kupata fedha kwa ajili ya kazi hiyo, wala kutoa muda wa kufanyika na kumalizika kwake.

Uwanja huo uliojengwa kwenye miaka ya mwishoni mwa 40 na mwanzoni mwa 50, una historia kubwa hapa nchini ambapo uliwahi kutumika kwa mashindano ya Gossage, na sasa unakabiliwa na hali mbaya kila eneo.

Licha ya uchakavu na kuporomoka kwa baadhi ya kuta zake, uwanja wa Mao Tsetung ndio unaotegemewa sana kwa michezo mbalimbali ikiwemo ligi kuu ya soka ya Zanzibar.

WAKAGUZI KUTUMWA KUCHAKACHUA HESABU ZFA.

 Wakaguzi kutumwa kuchakachua hesabu ZFA

 Wizara yakiri kuwepo ukiukwaji katiba, ubabaishaji
Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, imesema inakusudia kupeleka wakaguzi wa hesabu katika ofisi za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ili kupitia matumizi na taratibu zote za kifedha ndani ya chama hicho.

Waziri wa wizara hiyo Abdilahi Jihad Hassan, alisema hayo alipokuwa akijibu suala la nyongeza lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo Nassor Salum Ali 'Jazeera', kwenye kikao cha jana asubuhi.

Mwakilishi huyo alitaka kujua hatua zilizochukuliwa na wizara hiyo dhidi ya Katibu Mkuu wa ZFA ambaye alimtaja kuwa ndiye anayepaswa kubeba dhima juu ya mizengwe iliyofanyika katika chama hicho kufuatia uchaguzi wake mkuu.

Akizungumzia kadhia hiyo, Jihad alikiri kuwa kuna matatizo mengi katika uendeshaji wa kazi za ZFA, hasa mambo yahusuyo fedha, hivyo akasema wizara yake itapeleka wakaguzi wa hesabu katika ofisi zote za chama hicho Unguja na Pemba.

Aidha alibainisha kuwa wizara yake inafahamu kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa katiba katika utendaji wa chama hicho, pamoja na kuendesha vikao bila kufuata taratibu.

Hata hivyo, alisema baada ya Ofisi ya Mrajis kuingilia kati kadhia hiyo na kutumia uwezo iliopewa kisheria, iliamua kusimamisha mara moja uchaguzi mkuu wa marudio ambao ZFA ilipanga ufanyike Januari 19, huko Nungwi Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

"Kwa mamlaka aliyopewa katika kifungu cha sheria namba 19 (a,b,d), Mrajis ameamuru uongozi wa zamani urudi madarakani na kwamba shughuli zote zifanyike kwa maandishi na kuwasilishwa kwake, kwa sasa mambo yanakwenda, tusubiri uchaguzi ufanyike kati ya wiki ya mwisho ya Februari na mwanzoni mwa Machi", alieleza Waziri Jihad.

Alieleza katika hali ya sasa ambapo ZFA inaendelea na kazi zake kwa agizo la Mrajis kuwarudisha viongozi wa zamani, wizara yake imeona iendelee kuupitia kwa kina mgogoro huo ambao kwa kiasi kikubwa unamuhusu Katibu Mkuu kabla haijaamua kuchukua hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kumuondosha kama wengi wanavyopendekeza.

Chama cha Soka Zanzibar kilikumbwa na mtafaruku mkubwa tangu baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Pemba Januari 31, kufuatia Rais aliyeshinda Ali Ferej Tamim kukatiwa rufaa kwa madai ya kutowasilisha cheti cha elimu ya sekondari, hali iliyoibua pia matatizo mengine ambapo ilibainika baadhi ya wajumbe waliopiga kura hawakustahiki.

Saturday 22 January 2011

DK. SHEIN WAHITIMU VYUO VIKUU WASAIDIE MAENDELEO YA NCHI.

Dk.Shein: Wahitimu Vyuo vikuu wasaidie maendeleo ya nchi

 Ni katika kuelimisha sayansi, teknolojia mashambani, uvuvi
 Afungua milango zaidi kwa wawekezaji sekta ya elimu
Na Rajab Mkasaba

VYUO Vikuu duniani vimetakiwa kufungua matawi yao Zanzibar kutokana na kuwepo mazingira mazuri ya kuwekeza katika elimu, pamoja na soko kubwa la wanafunzi wa ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipohutubia katika mahafali ya tano ya Chuo Kikuu cha Elimu cha Zanzibar kilichopo Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Dk.Shein amevitaka Vyuo hivyo kutumia mafanikio makubwa yaliyopatikana na Chuo Kikuu cha Elimu cha Zanzibar, ambacho kiko chini ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika cha Khartoum kama kigezo cha mazingira bora yaliyopo Zanzibar.

Katika kufungua matawi hayo, Dk.Shein alisisitiza umuhimu wa matawi hayo kuwekwa katika visiwa vya Unguja na Pemba, ambamo pia mbali ya faida zitazopata vyuo hivyo, kuna usalama, utulivu na ushirikiano mkubwa.

‘Tayari Serikali yangu imeshafungua milango ya uwekezaji katika sekta ya elimu, napenda kurudia tena leo kusisitiza tena mje kuwekeza na kuahidi ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini’ alisema Dk.Shein.

Dk. Shein alikipongeza na kukishukuru Chuo Kikuu cha Elimu cha Zanzibar kwa kuweka gharama za mafunzo bei zenye kuzingatia watu masikini, pamoja na kutaka kuongezwa kwa unafuu ili wananchi wengi zaidi waweze kumudu kulipia masomo hayo, jambo ambalo amesema pia lifanywe na Vyuo Vikuu vingine hapa nchini.

Dk.Shein alikipongeza Chuo hicho cha kuzingatia uwiano wa kijinsia, ambapo alisema inafurahisha kuona katika mwaka wa tatu kina wanafunzi 152, ambapo wanawake ni 84, huku mwaka wa kwanza ukiwa na wanafunzi 307 ambapo 185 ni wanawake n 122 wanume.

Katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Zanzibar, Dk.Shein alisema kuna umuhimu mkubwa wa kupatikana walimu wa sayansi na teknolojia kama wanaotolewa na chuo hicho, ili waweze kusaidia kuelimisha wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaoendesha viwanda.

‘Kuna haja ya wahitimu wa sayansi na teknolojia, kutumia muda wenu wa ziada kuelimisha wakulima, wavuvii, wafugaji na wananchi wetu katika kutumia njia bora za kuimarisha shughuli hizo’ alisisitiza Dk.Shein.

Dk.Shein alisema chuo hicho ni mdau mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanikisha malengo ya Mapinduzi hasa katika kuimarisha elimu na kuwapatia elimu bora wananchi.

Alisema mahafali hayo yametokea wakati muafaka, ambapo Zanzibar inaadhimisha miaka 47 ya Mapinduzi yake matukufu, pamoja na kushukuru kupewa fursa kuwa mgeni rasmi akiwa katika muda mfupi wa uongozi wake Zanzibar.

Rais Shein alisisitiza umuhimu wa kupatikana walimu wengi katika kufanikisha malengo ya Serikali kuimarisha elimu katika ngazi mbali mbali ikiwemo maandalizi, msingi, sekondari na vyuo, ndio maana ikaweka sera ya kushirikiana na sekta binafsi ili kufanikisha mpango huo.

Aliipongeza na kuishukuru sekta binafsi ikiwemo Jumuiya ya African Muslim Agency kwa kuiunga mkono serikali kuitikia wito wa kusaidia katika kuinua elimu nchini.

Pia, Dk.Shein alikipongeza chuo hicho, pamoja na vyuo vikuu vingine viwili vilivyopo Zanzibar kwa kutoa Digrii za sayansi, ambazo amesema ni tegemeo kubwa kwa maendeleo ya Zanzibar katika kipindi hichi ambapo ulimwengu unaendeshwa kwa sayansi na teknolojia.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alikipongeza chuo hicho kwa kuanzisha mipango yake ya kuwa Chuo Kikuu Kamili katika kipindi kifupi kijacho.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Chuo hicho, Dk. Abdulrahman Al Muhala akitoa taarifa fupi ya chuo hicho alisema malengo ya wananchi wa Quwait kuwasaidia ndugu zao wa Zanzibar kupata maendeleo katika utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) na Dira ya Maendeleo 2020 yanafanikiwa kila uchao kwani tayari chuo hicho kimezalisha walimu wengi katika fani ya sayansi, jamii na kiarabu ambao wanatumika katika sekta mbali mbali.

Alisema wananchi wa Quwait wanaisaidia Zanzibar ili kuimarisha urafiki na udugu baina ya nchi hizo mbili, pamoja na kulipa fadhila ambazo wananchi wa Quwait walifanyiwa Zanzibar siku za nyuma wakati walipokuwa wakifika Zanzibar kwa shughuli mbali mbali ikiwemo usafiri wa baharini na biashara.

Akizungumzia mafanikio ya Chuo hicho, Dk. Abdulrahman alisema kwamba chuo hicho kimepiga hatua kubwa ikizingatiwa kuwa kimeanza kwa kuwa na wanafunzi 25 miaka 12 iliyopita na kufikia 1054 hivi sasa.

Aidha, alitaja maendeleo mengine kuwa ni kuongezeka kwa fani zinazosomeshwa hapo, pamoja na walimu wa kufundisha masomo mbali mbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti huyo aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar na Serikali yao kwamba kiwango cha elimu kinachotolewa chuoni hapo kitaongezeka kila muda ukienda, kwani tayari kumeshatekelezwa Mpango Mkakati wa kuhakikisha hilo.

Alisema mpango huo utaongeza uzalishaji wa walimu bora, ambapo pia alikaribisha walimu wanaotaka kujiendeleza kujiunga na chuo hicho, katika masomo ya Jografia, Historia, Physics, Hesabu, Baolojia na Chemistry, pamoja na kiarabu na masomo ya dini ya kiislamu.

Jumla ya wanafunzi 177 wamehitimu na kutunukiwa Digrii zao kwenye mahafali hiyo ya tano, wakitoka katika fani za sayansi, sayansi jamii na kiarabu.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo cha Kimataifa cha Afrika kutoka Sudan, Profesa Mahd Satti, aliahidi kutoa nafasi zaidi za masomo kwa Zanzibar kama hali itavyoruhusu na akakipongeza Chuo cha Elimu Chukwani kwa kuwa balozi bora wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, aliwataka wahitimu wa mahafali hiyo kuwa wazalendo na kubakia kufanya kazi nyumbani kwao, ambako mchango wao unahitajika sana.

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mabalozi wadogo wa nchi mbali mbali wanaofanya kazi zao Zanzibar na viongozi wa taasisi mbali mbali za kitaifa na kimataifa.

VISHOKA WA ARDHI WAMUUMIZA KICHWA SHAMUHUNA.

‘Vishoka’ wa ardhi wamuumiza kichwa Shamuhuna

 Sasa wauza kiwanja cha Ikulu
Na Mwanajuma Abdi

WAZIRI wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna amesema lipo tatizo la baadhi ya watu kujibebesha mamlaka ya kuuza ardhi hata ikiwa serikali imeyatenga kwa kazi maalum.

Shamuhuna alieleza hayo mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, alipokuwa akitoa ufafanuzi kufuatia wajumbe wa Baraza hilo kujadili hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyoitoa wakati alipolizindua Baraza hilo mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema tatizo la kuuza ardhi Zanzibar limekuwepo ambapo baadhi ya watu kwa makusudi wamekuwa wakiyauza maeneo ya ardhi yaliyotengwa kwa shughuli mbali mbali bila ya kuogopa.

Alikitoa mfano alisema hivi karibuni wapo watu wameuza ardhi ya kujengewa Ikulu, katika eneo la Chuini na kujichukulia fedha za uuzaji huo.

Waziri Shamuhuna alifahamisha kuwa, alipata 'vinoti' vya kumchokoza kwamba suala la ardhi haliwezi, jambo ambalo usiku wake watu wameuza eneo la Chuini lililotengwa na Serikali kwa kujengea Ikulu siku zijazo na tayari wamegawana fedha.

Waziri huyo alivipongeza vyombo vya habari kwa kufuatilia na kuandika matatizo ya ardhi, jambo ambalo linamsaidia katika ufuatiliaji wa tatizo hilo.

Akizungumzia suala la maji safi na salama, alikiri kuwepo kwa tatizo katika huduma hiyo na kueleza kuwa hakuna Jimbo lolote lililokamilika kwa wananchi wake kupata maji ya uhakika.

Waziri Shamuhuna alisema mradi wa Japan umekamilika, lakini bado tatizo la maji lipo hivyo jitihada zinaendelea kuchukuliwa ili wananchi wapate huduma hiyo.

Aidha alisema serikali inaendelea na mchakato wa kufanyika kwa utafiti wa uwezekano wa kuchimbwa mafuta Zanzibar, ili yaweze kukuza uchumi wa nchi.

Alisisitiza kwamba, mafuta yakipatikana yatabakia ya Zanzibar na sio ya Muungano katika kuendeleza uchumi na ustawi wa jamii, sambamba na kudumishwa kwa utulivu na amani nchini, ambayo ndio shabaha kubwa ya kupatikana kwa maendeleo ya haraka.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema Zanzibar ni nchi ya visiwa, hivyo uchumi wake unategemea kukuzwa kwa huduma katika bandari, utalii na uwanja wa ndege ili iondokane na utegemezi wa wahisani kutoka nje.

Alieleza katika bajeti ya serikali shilingi bilioni 171 ni mapato ya ndani ukilinganisha na bajeti yenyewe ni shilingi bilioni 424, ambapo asilimia 60 ya bajeti ni utegemezi kutoka kwa wahisani.

Waziri huyo, aliongeza kusema kwamba, ili kuondokana na masuala hayo Zanzibar inahitaji kujiimarisha ili iweze kuuza mafuta ya ndege na meli katika kutimiza malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilahi Jihad Hassan alisema kuingizwa sekta ya utalii katika wizara hiyo itaendelea kuimarika kwa vile vyombo vya habari vina msukumo tosha wa kuelimisha jamii hususani vijijini ili nao waweze kufaidika na mapato ya nchi.

Akifanya majumuisho ya hotuba hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame alisema Serikali itaendelea kuimarisha rasilimali muhimu ikiwemo uvuvi, kilimo na kukuza elimu nchini.

Sambamba na kushughulikiwa upya muundo wa utumishi wa Serikali, ambapo Wizara maalum imeundwa kwa lengo la kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.

HAKUNA UFUKWE ULIOUZWA

Hakuna ufukwe uliouzwa - SMZ

Na Mwandishi wetu

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema hakuna ufukwe uliouzwa kwa Wawekezaji Visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, Issa Sarboko Makarani, alisema kimsingi sheria ya ardhi inaeleza bayana kuwa ardhi yote ni mali ya Serikali ikiwemo fukwe.

“Nimeshangazwa sana na hawa watu wanaoeneza uzushi kuwa SMZ imeuza ufukwe …huu ni uongo usiokuwa na chembe ya ukweli” alisema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Alisema sheria nambari 12 ya ardhi ya mwaka 1992, inatamka bayana kuwa Mwekezaji haruhusiwi kuuziwa ardhi bali anakodishwa tu.

Kauli ya Serikali imekuja siku chache baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa Kampuni ya Kempinski kuuziwa ufukwe katika eneo la Ras Shangani Mjini Unguja kwa ajili ya ujenzi wa hoteli ya kitalii.

“Serikali haijauza, kilichopo ni kuwa mwekezaji Kempinski amepewa Lease (amekodishwa) tena baada ya kufuata taratibu zote na wala hakuna mizengwe yoyote” alisema Makarani.

Makarani amesisitiza kwamba Zanzibar haijauza ufukwe, bali imetoa ruhusa ya ujenzi wa hoteli ya kisasa yenye hadhi ya juu katika eneo baina ya nyumba ya kihistoria ya Mambo Msiige na Starehe Club.

Akizungumzia ujenzi unaokusudiwa kufanywa na Mwekezaji Kampuni ya Kempinski, Makarani alisema ujenzi huo kwa mujibu wa mkataba wa ukodishwaji wa eneo hilo ni wenye kuzingatia sheria na masharti ya uhifadhi na uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao unatambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi Elimu na Utamaduni(UNESCO) kuwa ni urithi wa ulimwengu.

“Taratibu zinaendelea za matayarisho ya ramani itakayokidhi haja ya SMZ na matakwa ya urithi wa ulimwengu…Mamlaka itathibitisha ramani ya ujenzi baada ya kufikiwa viwango vinavyokubalika vya uhifadhi wa Mji Mkongwe, sasa nashangaa hao wanaosema maneno ya ajabu ajabu kawaambie ufukwe haujauzwa” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo.

Makarani alisema kwa sasa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wa Zanzibar ipo katika mchakato wa kupitia ramani ya Kempinski kwa ajili ya kutazama vigezo vya Kitaifa na Kimataifa.

Aidha, amewahakikishia wananchi kwamba Zanzibar haimo katika orodha ya hatari ya kufutwa katika urithi wa Ulimwengu kwa kuwa tangu ilipotambuliwa rasmi mwaka 2000, Mji Mkongwe umeendelea kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Serikali vinaeleza kuwa Kampuni ya Kempinski imelipa bilioni 2 milioni 880 kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na fedha hizo kuwekwa katika hazina ya Serikali.

Kwa mujibu wa utaratibu, ukodishwaji wa ardhi kwa mgeni hekta moja ikiwa sawa na eka 2.4 inakodishwa kwa Dola za marekani 5000 kwa mwaka ambapo Kempinski eneo alilokodishwa halijafikia hata eka moja wamekodishwa kwa Dola 10,000 kwa mwaka.

Habari kutoka Mamlaka zinazohusika zinasema kikawaida kodi ya ardhi huongezeka kati ya asilimia 10 hadi 15 ikiwa ni kodi ardhi ya ukodishwaji kwa mwaka ikiwa ni ongezeko la thamani,lakini kampuni ya Kempinski italazimika kulipa asilimia 25 kila mwaka.

Chini ya mradi huo, Kampuni ya Kempinski inatarajia kuwekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 30 ambazo zitahusisha ukarabati wa jengo la kihistoria la Mambo Msiige, ujenzi wa bustani ya kisasa na hoteli yenye hadhi ya nyota tano itakayojengwa ilipokuwa starehe klabu.

Nchini Tanzania kampuni ya Kempinski imewekeza katika miradi mikubwa ya hoteli za kitalii zenye hadhi ya nyota tano ikiwemo Zamani Zanzibar Kempinksi,Bilila Lodge Kempinski Serengeti,Hotel Ngorongoro Kempinski na Kilimanjaro Hotel Kempinski Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Mji Mkongwe alisema Mwekezaji Kempinski ametakiwa kulifanyia ukarabati jengo la Mambo Msiige kuliweka katika haiba yake kulingana na maelekezo ya UNESCO ambayo tayari Mwekezaji huyo ameyazingatia.

Katika michango yao mbalimbali Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika vikao tofauti waliitaka Serikali kuchukua hatua ya kulihifadhi eneo la kuanzia jengo la Mambo Msiige hadi starehe klabu kwa kuwa lilikuwa ni maficho ya magenge ya kihuni.

Kuhusu kukodishwa kwa majengo ya Serikali, Sarboko amesema suala hilo limeelezwa kwa kina katika sera ya Taifa ya nyumba kama tamko la sera namba 6 linavyoeleza kuhusu azma ya Serikali kujiondoa katika umiliki na ukodishaji wa nyumba zake.

“Serikali itajiondoa kwenye umiliki na ukodishaji wa baadhi ya nyumba za Maendeleo za mjini na vijijini, baadhi ya nyumba za Mji Mkongwe,nyumba za vijijini na nyumba kongwe kwa awamu kwa kuziuza baadhi yake.

Hadi sasa jumla ya nyumba 938 za Serikali zimeuzwa kwa wananchi waliokuwa wakiishi ndani ya nyumba hizo ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya nyumba ya mwaka 2009 iliyopitishwa Baraza la Wawakilishi.

Mwekezaji mwingine S.S. Bakhressa kwa ushauri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, amekodishwa jengo lililokuwa likitumiwa na wizara hiyo, kwa ajili ya mradi wa hoteli ya kitalii ambapo ameshalipa dola milioni 1.5.

PINDA AWATAKA WABUNGE CCM KUSHIKAMANA

Pinda awataka Wabunge CCM kushikamana

Na Mwandishi Maalum

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa CCM amewataka wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa na umoja na kuacha malumbano kwani kwa kufanya hivyo wataiyumbisha nchi.

Pinda ametoa rai hiyo jana asubuhi (Jumamosi, 21 Januari 2011), alipofungua semina ya siku tatu ya wabunge wa CCM iliyoanza jana hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema lengo la semina hiyo ni kuwasaidia wabunge watambue wajibu wao wakiwa Bungeni. “Mada kuu ya jana ni Kanuni za Kamati ya Wabunge wa CCM na kesho tutajadili wajibu wa Wabunge wa CCM katika Bunge la Vyama Vingi, na hii itaendelea hadi Jumatatu,” alisema.

Akihimiza kuhusu ushiriki wao Bungeni, Waziri Mkuu alisema: “Kila mbunge anapaswa kusoma vizuri Kanuni za Bunge na kuzielewa ili waweze kuchangia kwa umakini mijadala ya bungeni. Kila mbunge ana wajibu wa kuhudhuria vikao vyote vya Bunge na kipimo kizuri cha Mbunge ni jinsi anavyoweza kuchangia mijadala katika Bunge…”.

Aliwataka wabunge hao wawe wepesi kusoma machapisho na kufanya tafiti ili waweze kuwa na hoja nzito wakati wanapotoa michango yao Bungeni.



Alitumia fursa hiyo kuwahimiza mawaziri wote wa Serikali ya Muungano wa Tanzania kuwa makini na ratiba za vikao vya Bunge ili wahakikishe wanakuwepo bungeni katika kipindi chote cha Bunge.

Pia alimshukuru Spika wa Bunge, Anna Makinda kukubali ofisi ya Bunge igharimie semina hiyo pamoja na semina nyingine ambazo zitafanyika kwa wabunge wa vyama vingine.

Alisema leo Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete atahudhuria semina hiyo na kwamba anatarajiwa kuifunga Jumatatu mchana.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Pinda ameahidi kutoa shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuchangia ununuzi wa kompyuta 24 zinazohitajiwa na kituo cha kulea watoto yatima cha SOS kilichopo barabaraya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam.

Pinda alitoa ahadi hiyo alipotembelea kituo hicho na kukagua miundombinu ya kituo hicho ikiwemo pia madarasa ya shule ya awali pamoja na nyumba wanazoishi watoto hao.

Waziri Mkuu alitoa mchango huo baada ya kuelezwa kuwa kituo hicho kina mpango wa kuanzisha darasa maalum la kompyuta (computer lab) ili watoto hao waweze kupata mafunzo ya teknolojia ya habari (IT) na kwamba kituo kinahitaji kompyuta 24.



Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu katika kituo hicho. Mkurugenzi wa Taifa wa SOS Children Villages, Rita Kahurananga, alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika hilo lina vituo vingine kama hivyo huko Zanzibar na Arusha na kwamba wana mpango kuanzisha vituo vingine Iringa, Bagamoyo na Mtwara ifikapo mwka 2016.

Naye Mkurugenzi wa Kijiji hicho, Dk. Alex Lengeju alimweleza Waziri Mkuu kwamba kijiji hicho ni miongoni mwa vijiji 500 vya SOS vya kulea watoto yatima vilivyopo katika nchi mbalimbali duniani ambavyo vinatumia mfumo wa familia mbadala.

“Inaumiza kuona watoto wakiishia mitaani, tunachofanya ni kuwachukua watoto ambao hawana ndugu kabisa, tukiwaleta hapa wanaishi watoto 10 katika nyumba moja chini ya uangalizi wa mlezi ambaye ndiye mama wa familia hiyo, wanakuwa na kaka na dada wa familia miongoni mwao… tunawalea wakitambua mfumo wa kuishi kama familia na kuishi kama wanakijiji wakitambua uwepo wa majirani zao,” alisema.

Alisema kijiji hicho kina nyumba 13 zenye uwezo wa kuchukua watoto 130 lakini hadi sasa wana watoto 123 ambao wanasoma shule mbalimbali za jijini lakini wengi wao wako shule ya awali iliyopo ndani ya kijiji hicho. “Shule ya awali ina watoto 83 wenye miaka kati ya mitatu na sita ambao 55 kati yao wanatoka familia za jirani hapa Mwenge na Sinza.”

Alisema Kijiji cha SOS kimeanzisha pia Mpango wa Kuimarisha Familia (Family Strengthening Programme) kwa kutoa huduma kwa walengwa wanaoishi nje ya kituo hicho kwa kuwalisha, kuwaelimisha na kuwaandaa wajitegemee kimaisha na kwamba hadi sasa wanahudumia watoto 200 na watoa huduma 53.

Alisema kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo kwenye jamii, wana mpango wa kuhudumia watoto 1,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Alisema kutokana na majukumu hayo, kama watapata eneo la kutosha, kituo kina mpango wa kujenga shule ya msingi, shule ya sekondari, shule ya ufundi na hospitali ambavyo alisema vitatoa huduma kwa jamii inayowazunguka.

Friday 21 January 2011

WATU WENYE ULEMAVU WAWEZESHWE KUKABILI SOKO LA AJIRA

Watu wenye ulemavu wawezeshwe kukabili soko la ajira

Achukizwa na ubaguzi wanaofanyiwa
Na Abdi Shamnah

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, amesema watu wenye ulemavu wawezeshwe kielimu ili waweze kutumia fursa za ajira zilizopo badala kukumbukwa kwenye upendeleo.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo huko Migombani alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar, ikiwa ni mfululizo wa ziara zake za kuzitembelea Idara zilizoko chini ya Ofisi yake.

Makamu huyo alisema tatizo la ajira ni kilio cha vijana nchini kote, hata hivyo serikali ina wajibu mkubwa kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata elimu ya kutosha ili waweze kutumia vyema fursa za ajira zilizopo.

Maalim Seif alisema lazima walemavu wawezeshwe katika kupewa haki na fursa za kielimu ili waweze kushindana kwenye soko la ajira kwa sifa walizonazo na si nafasi za kupendelewa.

Alisema lengo la serikali kuiona jamii ya Wazanzibari inapata haki na fursa sawa na wengine bila ubaguzi wa aina yeyote, iwe kwa misingi ya kimaumbile, jinsia au ukamilifu wa viungo.

Maalim Seif alisema elimu kwa jamii ya watu wenye ulemavu inawezekana, mbali na vifaa wanavyotumia kugharimu fedha nyingi.

Katika hatua nyingine Malim Seif, aliwapongeza walimu wa skuli ya msingi mjumuisho Kisiwandui, kwa kazi ngumu ya kuwaendeleza kielimu wanafunzi wenye mahitaji maalum, wakiwemo wasioona,viziwi pamoja na walemavu wa akili.

Wakati huo huo Maalim Seif alifanya mazungumzo na watendaji wa Jumuiya za Watu wenye Ulemavu, ambapo moja ya changamoto kubwa waliyonayo ni tatizo sugu la unyanyaswaji wa kijinsia dhidi yao.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya watu wenye Ulemavu wa Akili, Faudhia Haji Mwita, alisema sheria iliopo haitoi mwanga mzuri, kukiwa na kesi nyingi za vijana wenye ulemavu wa akili kubakwa.

Alifafanua nyingi ya kesi hizo zinapofikishwa Mahakamani , mapungufu ya kisheria hujitokeza na washitakiwa kuachiwa kwa kile kinachodaiwa ‘mdhuriwa kushindwa kujieleza’.

Aidha alisema vijana wenye ulemavu wa akili wanakabiliwa na changamoto kubwa paler wamalizapo skuli, kwa vile huwa hawana shughuli maalum za kufanya.

Makamu huyo pia alipata fursa ya kuzitembelea Jumuiya mbali mbali za watu wenye ulemavu, ikiwemo UWZ, Jumuiya ya wasioona, Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu na Kituo cha watu wenye Ulemavu na Maendeleo.

SERIKALI IZIBE MIANYA UVUJAJI MAPATO.

serikali izibe mianya uvujaji mapato



Mwanajuma Abdi


SERIKALI imeshauriwa kuchukua kila jitihada zitakazo hakikisha inaziba mianya yote ya uvujaji wa mapato.

Mwakilishi huyo alieleza hayo jana katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akichangia hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliyoitoa katika uzinduzi wa Baraza la nane la Wawakilishi Zanzibar Novemba 11 mwaka jana.

Alisema mipango ya serikali kuawezesha wananchi kuondokana na umasikini itaweza kukamilika endapo serikali itakuwa na fedha za kutosha ambazo zitapatikana kwa kuzibwa mianya inayovujisha mapato hayo.

“Wananchi bado masikini wa kawaida wanamiliki kipato cha shilingi 60,000, hivyo miwanya ya uvujaji wa mapato ya serikali izidhibitiwe kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi”,alisema Mwakilishi huyo.

Aidha Hamza alishauri vyema ingefikiriwa kuundwa kwa baraza dogo la mawaziri ambalo lingeweza kufanya kazi katika kuwakomboa wananchi kutokana na umasikini.

Alifahamisha kuwa nchi ndogo na changa kama Zanzibar hakikupaswa kuwa na baraza kubwa liliopo hivi sasa ambalo limekuwa likitumia fedha nyingi.

Alisema Zanzibar ni nchi ndogo ambayo ina mawaziri wengi karibu 24 ukilinganisha na nchi nyengine duniani, jambo ambalo husababisha matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kuwahudumia.

Alisema pamoja na serikali iliyokuwepo madarakani kujikita zaidi katika maridhiano, lakini pia mkazo uwekwe katika kuangalia umasikini ambao umekuwa ukiwakabili wananchi wengi.

Akizungumzia uharibifu wa mazingira uweze kudhibitiwa ni lazima matumizi ya misumeno ya moto ipigwe marufuku na itumike kwa watu wenye vibali maalumu.

Nae Mwakilishi Mbarouk Jimbo la Mkwajuni, Mbarouk Wadi Mussa alisema mahoteli yaliyopo nchini yaangaliwe upya juu ya utoaji wa ajira kwa kwani yamekuwa yakikwepa kuajiri vijana wazalendo pamoja na kuwa na sifa na uwezo.

Akizungumzia kiwanda cha Mahonda kilichokuwa kinazalisha sukari, ambapo ajira ya watu wengi katika Mkoa wa Kaskazini, alisema kiwanda hicho kimeshindwa kufanyakazi pamoja na kupata muwekezaji.

Naye Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansour Yussuf Himid alisema Korea Kusini imesaidia Dola za Marekani milioni 53 za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji maji.

Aliongeza kusema kwamba, Serikali imetenga ekari 8,521 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji maji, ambapo hadi sasa ni hekta 700 ndio zimetumika Unguja na Pemba na huku nyengine zikitumika kwa kilimo cha kutegemea mvua.

Sambamba na hilo alieleza Kitengo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbani kitaimarishwa zaidi ili kufanyika kwa tafiti mbali mbali zinazohusiana na kilimo pamoja na kuongeza hadhi ya Chuo cha Kizimbani kwa kutoa kiwango cha Diploma, ambapo mkupuo wa kwanza utatoka mwaka 2013.

HUDUMA YA SHERIA WASAMBAZA DOZI YA KATIBA

Huduma za sheria wasambaza dozi ya katiba

Na Asya Hassan

HUKU wanaharakati wakipaza sauti kulilia mabadilisho ya katiba mpya nchini Tanzania, kituo cha huduma za sheria cha Zanzibar, kimeanza kutowa elimu ya katiba.

Mkurugenzi wa kituo hicho Is-haka Sharifu alisema kituo chake kimekuwa kikikusanya makundi mbalimbali katika jamii kuyapatia elimu hiyo.

Alifahamisha hali hiyo inatokana na ukweli kwamba wananchi wengi pamoja na kulilia katiba mpya, lakini hawaielewi hiyo katiba ni kitu gani na nini kisichokubalika kwenye katiba hiyo.

Mkurugenzi huyo huyo alisema wananchi watakapo juwa umuhimu wa katiba ndipo watakapotoa mawazo sahihi na yenye mustakbali mwema kwa nchi wakati wa ukusanyaji wa maoni ya katiba utakapo wadia.

Aidha Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kwa kuwataka wananchi wa Zanzibar wajitokeze kikamilifu kutoa maoni yao wakati muida wa kamati ya kukusanya maoni utakapofika rasmi.

Alisema kituo chake mbali ya kufundisha katiba, pia kimekuwa kikijishughulisha na utoaji wa mafunzo mbali mbali yanayohusu sheria katika jamii.

Aliyataja miongoni mwa mafunzo yanayotolewa ni miongoni mwa taaluma ya sheria pamoja na huduma ya kwanza na mafunzo hayo yakiwafikia watu mbalimbali kama vile polisi, walimu na wananchi wa kawaida.

Hata hivyo alisema kwa mwaka 2010 wananchi waliopatiwa taaluma hiyo kwa upande wa Unguja walikuwa 1,549 na kwa upande wa Pemba walikuwa 2,671.

Aidha alisema katika mwaka huu watu mbalimbali hufika kituoni hapo kupatiwa ushauri wa mambo mbalimbali yanayohusu sheria.

TANZANIA KUIANDALIA SERA YA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA

Tanzania kuiandalia sera Teknolojia ya Nyuklia

Na Mwantanga Ame

SERIKALI ya Tanzania inajiandaa kutayarisha sera ya Teknologia ya Nyuklia ambayo itaiwezesha nchi kutumia nishati hiyo kwa shughuli za kimaendeleo.

Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknologia Tanzania, Dk. Raphael Chibuuda alieleza hayo alipokuwa akizungumza na uongozi Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Alisema dhamira ya serikali ya kutayarisha sera hiyo itahakikisha kuona nishati hiyo inasaidia katika shughuli za kimaendeleo ikiwemo kilimo, nishati, elimu na hospitali ambapo hivi sasa wamekuwa wakitumia nishati hiyo katika mionzi.

Naibu huyo alisema Tanzania imekuwa ikitumia nishati hiyo ya nyuklia kwa kiasi kidogo kutokana na kutokuwa na sera mahususi ambayo inasimamia matumizi salama ya nyuklia kwa maendeleo ya jamii.

Aliwatoa hofu wenye hofu ya kutumika vibaya kwa teknolojia hiyo na kueleza kuwa lengo ni kusukuma mbele maendeleo ya taifa.

Alisema ghofu ambayo ilijitokeza nchini Irani baada ya kuamua kutumia nishati hiyo haina haja ya kulinganishwa na dhamira ya Tanzania katika matumizi ya nishati hiyo kwani hivi sasa tayari inatumia nishati hiyo katika shughuli za utibabu.

Aidha, Dk. Raphael alisema, taasisi yake imeamua kuchukua hatua hiyo ikiwa ni moja ya mipango itayoweesha kukuza shughuli za kisanyasi ambapo mbali ya sera hiyo pia inajiandaa na sera ya Mawasiliano ya simu (ICT).

Alisema sera hiyo lengo lake ni kuona mawasiliano ya simu yanawekewa mazingira mazuri kutokana na hivi sasa kuimarika huku makampuni ya simu yakionekana kutokuwa na muongozo imara.

Kutokana na mipango hiyo Dk. Raphael, alisema ipo haja kwa kitengo cha utafiti katika Chuo Kikuu cha Taifa SUZA kikajiimarisha zaidi kwa vile kinachoonekana hivi sasa kutokuwa tayari kwa watu kujituma kufanya tafiti kwa visingizo vya ukosefu wa fedha.

Alisema ni kweli sababu hiyo ipo lakini haina haja ya kuwafanya kuacha kutayarisha tafiti kwa vile tafiti zenyewe zikifanyia zinauwezo mkubwa wa kuwaingizia fedha kutokana na kila tafiti itayofanywa inakiwango cha asilimia nane kwa fedha zitazotengwa kwa utafiti mzima.

Dk. Raphael, aliwataka wasimamizi wa Chuo hicho kuona wanakuza utafiti wa sayansi kwani Zanzibar ipo chini katika kufanya tafiti za aina hiyo, huku watafiti wake kushindwa kutumia masoko ya nje na badala yake kubakia wakisubiri tafiti za hapa nchini pekee.

Nae Mkurugenzi wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknologia Tanzania Hassan Mahmoud Mshunda alisema Chuo Kikuu cha Taifa SUZA kitapewa nafasi ya kipekee kuona inawasomesha zaidi walimu wake na wanafunzi wataotaka kujiunga na fani ya utafiti ambapo hivi sasa tayari wizara hiyo imewasomesha Wazanzibari watano.

Mkurugenzi huyo alisema matatizo yaliowahi kujitokeza ya kuwapo kwa malalamiko ya kutopewa nafasi za masomo kwa Wazanzibari waliowahi kuomba Wizara yake itayashughulikia kuona hayatatokea tena.

“Kwa hili nduguzanguni ninawaombeni radhi kwani aliefanya hivi naamini hakufahamu nini majukumu yetu sasa ninachokuombeni leteni maombi yenu na tutayafanyia kazi kwani tayari tuna Wazanzibari watano tumeshawapa nafasi hizo”, alisema Mkurugenzi huyo.

Kauli ya Mkurugenzi huyo imekuja baada ya mmoja Mkurugezi wa Utafiti katika Chuo Kikuu cha SUZA, Dk. Mohammed Ali Sheikh, kuueleza uongozi wa wizara hiyo wa kuwapo kwa matatizo yaliowahi kumkuta ya kukataliwa ruhusa ya fedha za kufanya utafiti ambao aliomba kwa Wizara hiyo.

Thursday 20 January 2011

ADB KUIPIGA TAFU SEKTA BINAFSI.

ADB kuipiga tafu sekta binafsi

Na Mwantanga Ame

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (ADB), imeahidi kuendeleza kutoa misaada yake kwa sekta binafsi, kutokana na kuridhishwa na hatua za kimaendeleo zilizofikiwa.

Mwakilishi wa Benki hiyo nchini Tanzania, Mary Muduuli, alieleza hayo kwenye mazungumzo yake na uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi, Mipango na Maendeleo, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu.

Mwakilishi huyo alisema Benki yake imeridhishwa na utekelezwaji wa miradi ya kimaendeleo hapa Zanzibar inayofadhiliwa na benki hiyo.

Alisema kutokana na kuridhishwa na hatua hizo ADB, iko tayari kuendeleza kutoa michango yake kwa Zanzibar kwa kuiangalia zaidi maeneo ya sekta binafsi kwani ndio yenye kutoa mchango mkubwa kwa taifa.

Alisema Benki yake itaiangalia sekta hiyo ikiwa ni moja ya mikakati ya kutekeleza mpango wa kupambana na umasikini MKUZA, ambao una mahitaji mengi katika kuleta maendeleo ya nchi na kuinua hali za wananchi.

Aidha Marry alisema, inafurahisha kuona serikali ya Zanzibar, imekuwa ikifanya jitihada mbali mbali za kutekeleza mpango huo, ambao ni muhimu katika kukuza maisha ya wananchi.

Alisema Benki hiyo hivi sasa inaangalia maeneo muhimu yatakayoweza kusaidiwa chini ya mpango huo sambamba na kujua mahitaji.

Akiyataja maeneo ambayo benki yake itayapa kipaumbele katika kusaidia ni pamoja na mafunzo ya amali ambayo ndiyo yatayoweza kufungua milango ya kuondoa matatizo katika kupambana na umasikini.

Alisema Zanzibar imekuwa ikipiga hatua vyema kwenye miradi ya utoaji wa huduma kama vile maji barabara na mawasiliano.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Khamis Mussa Omar, aliishukuru Benki hiyo kutokana na michango yake inayoitoa kwa Zanzibar, kwani imewezesha nchi kupiga hatua za kimaendeleo.

Aliitaja miradi hiyo ni pamoja na msaada wa miradi ya maji, sekta ya Afya ikiwa pamoja na kujenga jengo la maabara katika Chuo cha Afya, ujenzi wa nyumba za madaktari na maeneo mengine ya huduma za kijamii.

Alisema Changamoto ambayo serikali hivi sasa inakabiliana nayo ni ukuzaji wa sekta binafsi kutokana na hivi sasa ndio yenye mahitaji mengi kutokana na kukosa miundo mbinu ya kufanyia shughuli zao, mitaji masoko na ukosefu wa teknologia.

MFUNGWA WA RUSSIA AFARIKI ZANZIBAR.

 Mfungwa wa Russia afariki Zanzibar


Na Khamis Amani

RAIA mmoja wa Russia, aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar amefariki dunia.

Inarserger Othirov, amefariki dunia Januari 9, mwaka huu katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja ambapo alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa za Daktari kutoka Hospitali hiyo ya Mnazimmoja, marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya homa, kifua kikuu (TB), pamoja na uvimbe uliojaa maji katika pafu lake la upande wa kulia.

Staff Ofisa wa Vyuo vya Mafunzo, Makao Makuu Kilimani wilaya ya Mjini Unguja, Makame Kombo Ame, alithibitisha kutokea kifo cha mwanafunzi huyo wa Chuo cha Mafunzo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake, Staff Ofisa huyo, huyo alisema kuwa, marehemu amefariki siku tisa mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo kwa matibabu.

Alisema kuwa, kabla ya kifo chake Ivan Ochirov kama jina lake la umaarufu alilokuwa akijulikana nalo Chuoni humo, alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Chuoni humo, lakini baadae alilazimika kupelekwa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja baada ya hali yake kuwa mbaya.

Akiwa hospitalini hapo kwa matibabu, Januari 9 mwaka huu majira ya saa 12:15 za asubuhi Ivan alifariki dunia, kwa mujibu wa Staff Ofisa huyo.

Alifahamisha kuwa, mara baada ya kifo hicho mwili wake ulikabidhiwa wazee wake wote wawili waliokuwepo hapa nchini, chini ya usimamizi wa Balozi wa Russia nchini Tanzania kwa taratibu za mazishi.

Kwa mujibu wa Staff Ofisa huyo, mazishi ya marehemu huyo yalifanyika Zanzibar saa nane mchana, katika ufukwe wa pwani ya Migombani ngazi mia, kwa kuuchoma moto mwili wa marehemu huyo.

Ivan alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi wawili wanaotumikia kifungo cha maisha Chuo hicho cha Mafunzo, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi kijana mwenzao raia wa Russia kwa kumchoma moto, tukio ambalo lilitokea Zanzibar mwaka 1998.

Kabla ya adhabu hiyo, Ivan na mwenzake huyo (jina halikupatikana), ambaye naye pia ni raia wa Russia, Mei 31, 2001 walihukumiwa kutumikia Chuo hicho kwa muda wa miaka 15, baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila ya kukusudia katika kesi ya jinai namba 14/1998 iliyokuwa ikiwakabili Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Lakini hata hivyo, Aprili 23, 2004 jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, ilitengua adhabu hiyo na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa, baada ya kuonekana kuwa wameua kwa makusudi.

Adhabu hiyo imetolewa baada ya kushindwa kwa rufaa yao waliyoiwasilisha mahakamani hapo, kwa kupinga adhabu hiyo ya miaka 15 Chuo cha Mafunzo iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Hata hivyo, aliyekuwa Rais wa Zanzibar kwa wakati huo Dk. Amani Abeid Karume, Novemba 12, 2002 aliwapatia msamaha kutoka adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kifungo cha maisha.

Kwa mujibu wa Staff Ofisa huyo, pamoja na kutumikia kifungo cha maisha Chuoni hapo, hali ya mwanafunzi mwenzake bado inaendelea vizuri.

OPERESHENI YAANGAMIZA KUNGURU 200,000

Operesheni yaangaamiza kunguru 200,000

Na Mwantanga Ame

KUNGURU 200,000 wameuwawa baada ya Idara ya Mazao ya Biashara, Matunda na Misitu kuendesha operesheni maalum ya kuwaangamiza ndege hao, ambao wamekuwa wakisababisha uharibifu mkubwa.

Kunguru weusi ni ndege ambao mbali ya kusababisha hasara ya mamilioni kwa makampuni na watu binafsi, pia wamekuwa ni ndege wenye kuharibu mazingira.

Idara hiyo imechukuliwa hatua ya kuwaangamiza ndege hao, baada ya kubainika kuwepo kwa ongezeko kubwa la ndege hao kiasi ambacho wanashindwa kujitosheleza haja ya kimaumbile na kuwafanya kuwa wezi kwa kiasi kikubwa huku wakiisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na wizi wanaoufanya.

Akizungumza na Zanzibar Leo Mkuu wa operesheni hiyo Yussuf Kombo, alisema operesheni hiyo ilianza Januari 2010 tayari wameweza kuwaangamiza kunguru 200,000 hadi kufikia mwezi Disemba mwaka jana katika maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema hivi sasa kunguru hao wamekuwa wakionekana katika maeneo mbali mbali wakizagaa nyakati za asubuhi ambapo hufa baada kuwekewa dawa kwenye nyama maalum ambazo huwekwa sumu na kutupwa katika mapaa ya nyumba.

Alisema wameamua kutumia mapaa ya nyumba kuweka nyama hizo kutokana na kulinda mazingira ardhi pamoja na viumbe vyengine visiweze kufikia vyakula hivyo ambapo kunguru wanapojaribu kula huwachukua masaa 13 kuweza kufariki na ndio maana hufa wakati wa usiku wanapolala.

Akifafanua kauli hiyo alisema wizi mkubwa ambao wamekuwa wakiufanya ni kuiba mapapai, mahindi pamoja na wakiiba macho ya ndama wa ng’ombe kwa kuwatofoa na kuwasababishia vidonda.

Wizi mwengine ambao wamebainika kuufanya ni wa mabendeji ya wagonjwa yanayotupwa katika Mahospitali ambapo baadae wanapogundua kuwa hayaliki huyatupa mitaani jambo ambalo husababisha uchafuzi wa mazingira.

Aidha aliutaja wizi mkubwa ambao huufanya kunguru hao Afisa huyo alisema ni katika makampuni ya simu ambapo huiba moja ya kifaa muhimu cha mawasiliano ambavyo huwa ndani ya minara ya simu.

Alisema tayari kampuni ya simu ya Zantel imekuwa inapoteza milioni 30 kwa nusu saa inapotokezea kuibiwa kwa kifaa hicho na kunguru hao ambapo husababisha kukosekana kwa mawasiliano nchi nzima.

Akiendelea Afisa huyo alisema hivi sasa baada ya kuwepo kwa operesheni hiyo baadhi ya kunguru wameanza kuitambua na kuamua kuukimbia Mji na kuhamia Kiwengwa na Nungwi jambo ambalo limekuwa likiwafanya kulazimika kufukuzana nao.

Alisema hali hiyo imekuwa ikiwapa wakati mgumu wa kutekeleza zoezi hilo kwa vile hulazimika kutumia gharama kubwa ya kukimbizana nao kutokana na watendaji kutokuwa na chochote vikiwemo usafiri wa kutosha na baadhi ya vifaa muhimu vya kufanyia kazi hiyo ikiwemo ya ununuzi wa nyama inayotumika kuwategeshea ndege hao.

Alisema mradi huo fedha ambazo umetengewa kutumia ni shilingi milioni 12 kutoka katika mfuko wa mradi wa usimamizi wa Mazingira wa ukanda wa Pwani (MACEMP).

Alisema kwa mwaka huu mradi hautaweza kuwashirikisha watoto kwa kukamata makinda ya ndege hao ama mayai kutokana na kujitokeza watoto wengu kuanguka katika miti na kuwasababishia kupata athari katika viungo vyao.

Kutokana na kuwepo kwa kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kuendesha kampeni hiyo Afisa huyo aliwataka wananchi, wafanyabiashara na makampuni ya simu kuona haja ya kutoa michango yao itayoweza kufanikisha kazi hiyo.

“Kama mfanyabiashara mwenye kujali biashara yake anapata hasara ya shilingi milioni 30 kwa nusu saa kwa nini asishirikiane nasi kusaidia japo milioni 2 au 3 ama kutoa ng’ombe mmoja tukapata nyama ya kutegeshea tungekuwa mbali tunaomba wenye uwezo wasaidie hili kwani kunguru watatumaliza” Alisema Afisa huyo.

Alisema wengi wa wakulima hivi sasa wameanza kukata tamaa kutokana na uharibifu wa ndege hao kiasi cha kuwafanya kushinda mashambani muda mwingi kuwainga baada kukimbia mjini na kuhamia mashambani kwa hofu ya kuuliwa.

Afisa huyo aliwataka wananchi kutokuwa na hofu ya zoezi hilo kutokana na kuwabaini kunguru hao nyakati za asubuhi kwa vile dawa wanayoitumia sio ya kunyunyiza katika anga hutupwa katika nyama na ndege hao hula asubuhi.

Kunguru ni moja ya ndege walioapizwa na Nabii Nuhu, baada kushindwa kurudi kutoa majibu sehemu aliyotumwa kutokana na kukuta mizoga ya vyakula mbalimbali ambapo Nabii huyo, alimuapiza kuhangaika maisha yake.

Historia kunguru hao kuja Zanzibar inaelezwa ni zawadi iliyoletwa kwa watawala wa zama hizo.

WAWAKILISHI KUJADILI HUTUBA YA DK. SHEIN KUBADILISHA KANUNI.

Wawakilishi kujadili hotuba ya Dk. Shein, kubadilisha kanuni

Na Mwantanga Ame

BARAZA la Wawakilishi la Zanzibar linatarajiwa kuanza kikao chake leo ambapo kitajadili hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyoitoa katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Baraza la Nane.

Wajumbe hao watajadili hotuba hiyo baada ya kuitafakari kwa muda sasa kutokana na hotuba hiyo kuzungumzia masuala mbali mbali ya kimsingi na maelekezo ya kutosha kuhusu dira na mwelekeo wa serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Sehemu kubwa ya hotuba hiyo inaelekeza jinsi gani serikali itatekeleza ahadi ya kuimarisha utoaji wa huduma bora za jamii, kukuza elimu hasa ya sayansi, utekelezaji mpango wa mapinduzi ya kilimo na uvuvi.

Aidha katika hotuba hiyo, Wawakilishi watajadili masuala ya muungano na nia ya kuimarisha kwa manufaa ya pande hizo mbili, kushughulikia uanzishwaji wa viwanda pamoja na kujadili matatizo ya kibiashara.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee, alisema moja ya ajenda itakayowasilishwa katika kikao hicho kitachodumu takriban wiki mbili kitaijadili hotuba hiyo.

Alisema baraza limeamua kuweka ajenda hiyo kwa vile Rais baada ya kuisoma haikupata kujadiliwa kwa sababu kikao hicho kilikuwa cha muda mfupi na kuamuliwa kujadiliwa katika kikao cha pili.

Aidha kikao hicho kimepokea maswali 145 ambapo watendaji wakuu wa serikali watayajibu na kuyatolea ufafanuzi.

Mbali na kazi hiyo pia, baraza hilo litazipitia kanuni za Baraza hilo ikiwa ni hatua ya kuzifanyia mabadiliko ili ziende sambamba na mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa ambapo maeneo kadhaa yatalazimika kufanyiwa mabadiliko.

Mabadiliko ambayo yanahusisha kuondolewa nafasi za wakuu wa Mikoa ndani ya kanuni hiyo, kuondoa nafasi ya Waziri Kiongozi na kuingiza Makamu wa Pili wa Rais kuwa ndie Mkuu wa shughuli za serikali na kanuni ambazo zitakuwa zinaelekeza namna ya uwakilishi kupitia kamati za Baraza badala ya mfumo wa sasa kutumia Mawaziri Kivuli pamoja na kuweka Mnadhimu Mkuu wa serikali badala ya wanadhimu wa Vyama.

Baraza hilo litakuwa ni la kwanza katika muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa kuanza mjadala wake ambapo wajumbe wake hawatakaa kwa utaratibu uliozoeleka hapo awali wa Chama tawala kukaa upande wa kulia na upinzani kushoto na badala yake watachanganyika huku Mawaziri na Manaibu wake watakuwa katika safu za mbele.

WAZIRI ABOUD ATAKA WATOTO WAFUNZWE HISTORIA.

Waziri Aboud ataka watoto wafunzwe historia

Na Yunus Sose, STZ

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, amewataka wazee wa kijiji cha Kizimkazi Mkunguni, kutafuta mbinu za kuwafundisha watoto wao umuhimu wa kuielewa na kuitunza historia ya skuli yao.

Aboud alisema kueleweka hitoria hiyo kutakuwa kivutio kwa watalii na kuwa kielelezo cha historia kwa vizazi vijavyo.

Alisema Zanzibar ni moja ya visiwa vyenye rasilimali nyingi za kihistoria hivyo, wananchi wa sehemu hizo wanapaswa kuziendeleza rasilimali hizo kwa kuzitunza na kuzijengea mazingira ambayo wageni wanaweza kuvutika.

Waziri Aboud aliyaeleza hayo alipozungumza na wajumbe wa kamati ya maendeleo ya kijiji cha Kizimkazi Mkunguni, kamati ya Shehia, kamati ya skuli baada ya kukabidhi shilingi milioni 1.5.

Fedha hizo alikabidhi kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alizoahidi kusaidia ujenzi wa jengo jipya la skuli ya Kizimkazi katika sherehe za kutimia miaka mia moja kwa skuli hiyo zilizofanyika mwishoni mwa Disemba alipohudhuria akiwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo.

Alisema serikali kwa upande wake itaendelea kuwaunga mkono wananchi wanapoanzisha miradi ya maendeleo, kuhakikisha inamalizika kwa wakati.

Alizipongeza kamati za kijiji cha Kizimkazi kwa kuwa na nguvu moja na kuonesha mshikamano, hali ambayo wananchi wa kijiji hicho wamekuwa mfano katika harakati za kujiletea maendeleo

"Serikali inatambua mchango wenu wa kuendeleza miradi ya maendeleo lakini hili la kuendeleza historia ya skuli yenu msije mkalifanyia mzaha na ni vyema mkaliandalia utaratibu wa kufanyika sherehe za aina hiyo kila mwaka," alisema waziri Aboud.

Aliwafahamisha wananchi wa kijiji hicho ambapo ujumbe wake uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mustapha Mohamed Ibrahim kuielezea historia halisi ya wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo ili nao wawe na upeo wa historia yao wasijekupotoshwa na watu wengine ambao wanatoka nje ya kijiji hicho.

Akitoa salamu za wanakamati za kijiji hicho, Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kijiji hicho, Hassan Mkadam Khamis ameipongeza ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kutochelewesha ahadi wanazozitoa jambo ambalo limekuwa likiwapa moyo mkubwa wananchi hasa wa vijijini.

MARUBANI KUJIANDA KUGOMA

. Marubani wajiandaa kugoma

 TATP yadai kuchoshwa kudai maslahi bora kwao
 Wadai rushwa yatumika kusajili marubani wageni
Na Kunze Mswanyama,Dar es salaam

HUKU migomo ikiendelea kurindima kwenye Vyuo Vikuu, Taifa linaweza kusimamisha shughuli za usafiri wa anga, kutokana na Marubani nao kujiandaa kuingia kwenye mkumbo huo.

Marubani hao wanajiandaa kuingia kwenye mgomo wa kususia kuzipaisha ndege angani, wakiishinikiza serikali kuwaboreshea maslahi yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Marubani (TATP), Kepteni Khalal Iqbar, alibainisha kuwepo kwa mgomo huo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema dhamira kubwa ya kutaka kuingia kwenye mgomo wa kutozirusha ndege hizo angani ni kutokana na kuitaka serikali kujali maslahi yao badala ya kuwapendelea marubani wa kigeni.

Kepteni Khalal, alisema marubani wazalendo wamekuwa wakinyanyaswa hasa pale wanapofuatilia madai yao, akisema tayari wamefungua kesi mahakamani na hivyo wanasubiri kuarifiwa siku ya kuanza kesi hiyo.

TATP, ilisajiliwa mwaka jana, ambapo kilianzishwa rasmi mwaka 1961 na kwamba mwaka 1984 kilianza kupoteza mwelekeo na kilikuwa kikifanya kazi pasipokuwa na usajili wa kisheria jambo ambalo ni kinyume na sheria ya Tanzania.

"Mnajua kila wanataaluma wanakuwa na chama chao cha kutetea maslahi yao, walimu wana CWT tena ni walimu wazawa tu, Madaktari wana chama chao, walinzi na kila taaluma, na sisi tumesajili cha kwetu, lakini tunalazimishwa kuwaingiza wageni ili kuwa na kauli, katika chama hicho, hatutaki", alisema katibu huyo.

Alisema Wizara zinazohusika na maslahi yao, zimekuwa zikiwadharau na hata kuwaandikia barua zinazoonesha dharau jambo linalowaweka katika wakati mgumu, ilhali wao walikuwa wakifanya kazi katika Shirika la ndege la serikali la ATC lililokosa uwezo wa kuwaajiri.

"Nawaambia kuna mashirika ya ndege hayana rubani Mtanzania hata mmoja na mengine yanatumia marubani wasiokuwa na uzoefu tena hawana hata leseni, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kanuni za kitaifa na kimataifa za urushaji ndege", alisema.

Khalal alisema yapo mashirika ya ndege ambayo pia yanatumia rushwa kupata leseni za marubani wa ndege zao, ambao pia wanashirikiana na Maofisa wa wizara katika kupatikana kwa leseni hizo.

Alisema wao walisomeshwa kwa pesa za walipa kodi wa Tanzania lakini hawatumiki kwa maslahi ya taifa kwa kuwa tu kuna urasimu katika mamlaka ya ndege na hata kwa baadhi ya maofisa wa wizara wanaotumika kutoa vibali vya kufanya kazi kwa kulaghaiwa kwa pesa na wageni hao wasiojali maslahi ya taifa.

Chama hicho kina majina ya Marubani wasaidizi wanaofanya kazi pasipokuwa na vibali na hawajatimiza masaa 360 ya kurusha ndege ili kupata ajira sehemu yoyote jambo linalofanya kuwa na hatari zaidi ya kupata ajali nyingi za ndege na hivyo wao wanajiandaa kupinga hali hiyo kwa kutumia mbinu zozote.

Naye Kepteni William Silaa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama hicho, alisema kuna vijana wengi tu wa Tanzania ambao hawana kazi lakini wamesoma na kufaulu elimu ya urubani na nafasi zao kuchukuliwa na wageni ilihali wote wana elimu sawasawa.

Silaa alisema,"Najisikia uchungu sana kuona kuwa nchi inataka kuingia kwenye hali mbaya watakapotangaza, serikali inawajali wageni wakati watoto wa hapa tunatumika kwa mashirika ya nje tena yanayotunyanyasa na serikali ikifahamu hilo hata haichukui hatua zozote",alisema Ofisa huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi.

"Wanasema eti sisi hatuna elimu ya kutosha na umakini wetu ni mdogo. Pia wanadai eti sisi ni walevi, wao wanaendesha ndege wakiwa na vileo vyao pembeni na wakitua tu wanakimbilia baa, sasa nani mlevi kati yetu na wao?” alihoji Silaa ambaye ni baba wa Meya wa Ilala.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mgogoro wa chini kwa chini baina ya serikali na marubani hao jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa taifa na hata kuzorotesha usafiri wa anga ambao pia hutumika kuwasafirisha watalii na hivyo kuongeza mapato ya taifa.

SEKTA YA USAFIRI DUNIANI KUKUTANA ZANZIBAR.

Sekta ya usafiri duniani kukutana Zanzibar

Na Mwanajuma Abdi

ZANZIBAR kwa mara ya kwanza itaandaa mkutano wa kimataifa utaowashirikisha wadau wa usafirishaji, uchukuzi na usambazaji kutoka nchi mbali mbali duniani, ambao utaanza kufanyika mwezi Machi mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya mkutano huo, ambae pia ni Meneja Mkuu wa Bandari Kavu kupitia kampuni ya Azam jijini Dar es Salaam, Ashraf Khan, alisema hayo katika Ofisi ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Malindi mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Khan alisema mkutano huo wa kimataifa utakuwa wa siku mbili ambapo utaanza Machi 8 na ambapo wadau wa sekta ya usafirishaji wa ndani na nje watajadili uendeshaji wa majukumu yao.

Alisema mkutano huo ni wa kwanza kufanyika Zanzibar na utafanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, itawashirikisha washikiri kutoka katika Bara la Afrika, Ulaya, Asia na Tanzania ambao utatoa fursa kwa wadau kubadilishana mawazo na kupata taaluma inayohusiana na kazi zao.

Alieleza mkutano huo utatoa nafasi ya wadau kujifunza jinsi ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa, ambapo mada mbali mbali zitajadiliwa ikiwemo ya usalama wa anga, usalama wa usafirishaji wa majini.

Hata hivyo, alisema mada nyengine zitakuwa ni usalama wa barabarani, ambao ni muhimu katika kupunguza ajali, taaluma ya usafirishaji na uchukuzi na uendeshaji na usalama wa reli.

Nae Katibu Mkuu wa The Chartered Insitute of Logistics and Transport (CILT), Tanzania, Ramadhani Sawaka alisema mkutano huo umeandaliwa na Taasisi hiyo ya Kimataifa yenye makao makuu yake Uingereza.

Alifahamisha kuwa, kufanyika kwa mkutano huo Zanzibar pia itasaidia katika kuitangaza kiutalii katika kukuza uchumi wa nchi, sambamba na kutanuka kwa huduma za usafirishaji.

Alisema wadau hao watakapokuwepo nchini watazungumzia kwa undani masuala mazima ya usalama katika usafirishaji, uchukuzi na usambazaji

Wednesday 19 January 2011

MTAALAM ATAJA CHANGAMOTO ZA KUPAMBANA NA KICHOCHO ZANZIBAR

Mtaalamu ataja changamoto za kupambana na kichocho Z’bar


Na Mwanajuma Abdi

JAMII imeshauriwa kuepukana na utamaduni wa kujisaidia haja ndogo na kubwa katika mito, mabwawa na madimbwi ya maji ili kuepukana na vijidudu vinavyoeneza maradhi ya kichocho nchini, maradhi ambayo bado tatizo nchini.

Ushauri huo umetolewa na Meneja wa Mpango wa kupambana na maradhi Dk. Khalfan A. Mohammed wakati akizungumza na gazeti hili Mianzini Lumumba mjini hapa.

Alisema maradhi ya kichocho bado yanaisumbua jamii na hasa watoto Unguja na Pemba, ambapo maambukizi yake kwa mujibu wa mtaalamu huyo yanapatikana zaidi kwenye mito na maji yaliotuama.

“Maradhi haya husababishwa na vijijidudu vinavyoitwa “Schistosome haematobium, ambavyo hutokana na konokono wanaoishi katika sehemu hizo ambapo kupitia katika haja ndogo (Urinary Schistosomicesis),” alieleza Dk. Khalfan.

Aidha, alieleza maradhi hayo licha ya kupungua kutoka asilimia 60 hadi 40 katika miaka ya 90 lakini kwa sasa ugonjwa huo umefikia asilimia 10 hadi 15, yakiwa bado yanaendelea kuisumbua jamii.

Aliyataja maeneo yaliyokithiri kwa maradhi hayo, ambapo kwa upande wa Pemba yanapatikana takriban sehemu zote nakwa Unguja baadhi ya maeneo kama Kinyasini, Fuoni, Mwera na Chaani, ambapo Wilaya ya Kusini ndio pekee iliyokuwa haina ugonjwa huo.

Hata hivyo, alisema mradi wa miaka minne hadi mitano unaofadhiliwa na Mfuko wa Bill na Melinda wa Marekani unatarajiwa kuanza mwaka huu, ambapo mkutano wa kujadili hatua zitazochukuliwa katika kupambana na maradhi hayo unatarajiwa kufanyika Februari nane na tisa mwaka huu, huko Pemba.

Alifahamisha kuwa, mkutano huo utajadili jinsi ya utoaji wa elimu ya afya kwa jamii, kugawa dawa maskulini na kuwatokomeza konokono kwa kupiga dawa katika maeneo yaliyokithiri ugonjwa huo.