Sunday 19 December 2010

UINGEREZA YARIDHIASHWA NA MAELEWANO ZANZIBAR.

Uingereza yaridhishwa na maelewano Zanzibar

Na Ali Mohamed, Maelezo
Jumatatu 20 Disemba 2010
UINGEREZA imeelezea kuridhishwa na hali ya maelewano, mashirikiano na maendeleo ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa iliyoundwa na Dk. Ali Mohamed Shein.

Uingereza imewekwa bayana hali hiyo kupitia Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Deane Coner baada ya chakula cha mchana huko Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema hatua iliyofikiwa na Zanzibar inaonesha ishara njema kwa wananchi wa Zanzibar ya kushirikiana na kulisukuma gurudumu la maendeleo ya nchi kwa maslahi ya wananchi wote.

Kwa niaba ya nchi yake Balozi huyo alisema Uingereza itazidisha mashirikiano na Zanzibar na kuisadia katika miradi mbali mbali ya maendeleo.

Aidha aliitakia Zanzibar mafanikio mema katika maelewano na mashirikino na kutoa wito kwa viongozi na wananchi kudumisha zaidi hali hiyo kwa maslahi ya nchi yao.

Deane Coner, alifika katika kijiji hicho cha Makunduchi kwa ajili ya kufungua wodi ya wazazi katika hospitali ya Makunduchi iliyojengwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Uingereza (HIPZ).

Akimfahamisha mchakato uliopitiwa na Zanzibar hadi kufika hatua hiyo ya kuundwa kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Ali Mzee alimwambia Kamishna huyo kuwa uamuzi huo ulikuwa ni wa Wazanzibari wote bila kujali itikadi za kisiasa.

Nae Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Haroun Ali Suleiman, ambae ndie aliyekuwa mwenyeji wa Kamishna huyo katika chakula hicho cha mchana alisema anaamini kuwa serikali iliyoundwa ya Umoja wa Kitaifa itaivusha Zanzibar kuelekea katika maendeleo makubwa.

UINGEREZA KUENDELEA KUISAIDIA ZANZIBAR

Uingereza kuendelea kuisaidia Zanzibar

Na Ameir Khalid
Jumatatu 20 Disemba 2010

SERIKALI ya Uingereza imeahidi kushirikiana na Serikali ya Mapinguzi ya Zanzibar, katika kuendeleza maendeleo yaliyopo nchini ikiwemo kusaidia sekta ya afya ili wananchi waweze kuondokana na matatizo yanayowakabili.

Hayo yameelezwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diane Corner alipokuwa akifungua wodi ya wazazi ya hospitali ya Cottege Makunguchi Wilaya ya Kusini Unguja.

Alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya, Serikali ya Uingereza itaendeleza mafanikio zaidi kama yalivyofanywa katika kulifanyia matengenezo jengo hilo la wazazi ambalo litakuwa la kisasa na lenye vifaa vya kisasa.

Nae Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Juma Duni Haji, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajali shida zinazowakabili wananchi wake katika kupata huduma ya afya pamoja na matatizo mengine yanayowakabili wafanyakazi wa sekta hiyo.

Alisema kutokana na matatizo hayo Serikali inaelewa na ipo katika hatua ya kuyafanyia kazi ili matatizo hayo yaweze kuondoka na kusema kuwa ni vyema kwa wananchi pamoja na wafanyakazi hao kuwa na subira kwani matatizo hayo hayawezi kuondoka mara moja.

Waziri huyo alifahamisha kuwa kampeni ya kuwahamasisha kinamama juu ya kufika hospitali wanapojihisi wakiwa wajawazito imefanikiwa kwa kiasi fulani na hivyo ufunguzi wa jengo hilo utawawezesha wananchi wa Wilaya ya Kusini kuweza kunufaika zaidi na huduma hiyo.

Aidha aliishukuru Jumuiya ya HIPZ kwa msaada huo wa ujenzi wa jengo hilo ambalo alisema litapunguza baadhi ya matatizo yaliyokuwa yanaikabili hospitali hiyo.
WACHUKUZI wa mizigo kwa kutumia gari ya inayokokotwa na Ngombe wakiwa wamembebesha mizigo kupita kiasi na wenyewe wakiwa wamempanda juu bila ya kujali haki za Wanyama wakiwa katika barabara ya Kwaalamsha.(Picha na Othman Maulid)

UNICEF YAPONGEZA MIKAKATI YA KUPAMBANA NA UDHALILISHAJI

UNICEF yapongeza mikakati ya kupambana na udhalilishaji

Na Sharifa Maulid
Jumatatu 20 Disemba 2010
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), limesema litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika utekelezaji wa programu zake mbali mbali kwa lengo la kumuhifadhi mtoto.

Mwakilishi mkaazi wa UNICEF Zanzibar, Ruth Leano alieleza hayo alipokuwa akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Rahma Mohammed Mshangama huko afisini kwake Mwanakwerekwe mjini Zanzibar.

Mwakilishi huyo alisema Shirika hilo kupitia programu zake litafanya kila iwezekanavyo kusaidia watoto wa Zanzibar.

Alisema hivi sasa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika uhifadhi wa mtoto hasa kwa kuundwa kwa kamati za kupambana na udhalilishaji wa kijinsia kuanzia ngazi ya chini hadi taifa pamoja na utayarishaji wa sheria ya mtoto Zanzibar.

Ruth alisema watendaji wa kitengo cha uhifadhi wa mtoto kutoka shirika lake wameshauri kuingizwa masuala ya watoto katika programu mbali mbali nchini ikwemo Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA).

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Rahma Mshangama alisema kuunganiswa kwa Wizara yake na Idara ya Ustawi wa Jamii iliyokuwa wizara ya Afya ni hatua nzuri ya kuleta ufanisi wa kumlinda na kumuhifadhi mtoto nchini.

Kuhusu rasimu ya sheria ya mtoto Zanzibar alisema mwamko zaidi unahitajika kwa wadau mbali mbali wakiwemo viongozi wa dini na wajumbe wa baraza la Wawakilishi, hivyo ameliomba shirika la UNICEF kutoa ushirikiano wake ili kuweza kutekeleza hatua iliyofikiwa.

Katibu huyo ameliomba Shirika hilo na wadau wengine kuwawezesha wazazi kiuchumi katika kubuni na kuendesha miradi ili kunyanyua vipato vyao jambo ambalo litasaidia kupunguza ajira za watoto nchini.

“Katika kupambana na udhalilishaji wa kijinsia ujumbe kutoka Zanzibar ulioshirikisha watendaji wa Wizara yangu, Polisi, Mkurugenzi wa mashtaka, Mahakama, watendaji wa ustawi wa jamii pamoja na wadau wengine walikwenda nchini Zambia kuangalia wenzetu wamefanya nini katika kupambana na tatizo hilo, hivyo ripoti ya ziara hiyo itasaidia sana Zanzibar kwenye utekelezaji wa kuondosha tatizo hilo”,alisema.

VITONGOJI WAAHIDIWA UFUMBUZI WA MGOGORO WA ARDHI.

Vitongoji waahidiwa ufumbuzi mgogoro wa ardhi

Na Suleiman Rashid Omar Pemba
Jumatatu 20 Disemba 2010.

WAZIRI wa Nchi Afisi ya Makamu wa pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed amewataka wananchi wa Vitongoji, kisiwani Pemba kuendeklea kuvumilia wakati Serikali inalitafutia ufuimbuzi tatizo la kuchukuliwa ardhi yao.

Waziri Aboud ameyasema hayo nyakati tofauti alipozumgumza na wananchi wa eneo hilo, alipoyakagua maeneo yanayolalamikiwa na wananchi hao.

Alimesema Serikali ipo pamoja na wananchi hao na ameahidi kulifuatilia suala hilo kwa kina hadi pale suluhisho la kweli litakapopatikana na kusisitiza kwamba Serikali inalisimamia ili kila mmoja apatiwe haki yake bila kudhulumiwa.

Aidha, aliwataka wananchi hao kupanga mipango mizuri ya kutumia ardhi kwa vile ardhi katika visiwa hivi ni chache na idadi ya wakaazi inaongezeka siku hadi siku, hivyo ni vyema ikatumika kwa njia bora ili kila mwananchi afaidike nayo.

Kwa upande mwengine, Waziri Aboud amewataka viongozi wa Wilaya ya Chake Chake kusimamia maeneo yote yanayolalamikiwa na kuhakikisha kuwa hayajengwi hadi pale taratibu zitakapokamilika ikiwa pamoja na wadai kulipwa fidia.

Naye, Mwakilishi wa jimbo la Wawi, Maalim Nassor Juma amewataka wananchi hao kuwa wavumilivu na yeye akiwa ni kiongozi wao atalifuatilia suala hilo katika ngazi zote hadi pale ufumbuzi utakapofikiwa.

MFUKO WA BARABARA KUTUMIA 4.609BN /- MATENGENEZO BARABARA KADHA.

Mfuko wa barabara kutumia 4.609bn/- matengenezo barabara kadha
Jumatatu, 20 Disemba 2010

FUKO wa Barabara nchini unakusudia kutumia shilingi bilioini 4.609 kuzifanyia matengenezo bara bara kadhaa Unguja na Pemba.

Fedha hizo ni sehemu ya michango ya wananchi inayotokana na kodi ya mfuko wa barabara inayokuswanya kutokana na huduma ya barabara ambapo mwaka 2010/2011 mfuko huo umekusanya shilingi bilioni 0.842 sawa na asilimia 15 ya makusanyo yote.

Mkurugenzi wa Mfuko huo, Abdi Khamis alimwambia Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango, Omar Yussuf Mzee kwamba fedha zitazotumika kwa ujenzi wa barabara hizo ni sawa na asilimia 85 ya makusanyo yote ambayo yalifikia shilingi bilioni 5.451 mwaka 2010/2011.

Barabara zitakazohusika na mpango huo, ni ya mzunguko Mwanakwerekwe na kuendelea hadi eneo la nyumba mbili.

Barabara nyengine alioitaja ni ya Bungi Miembe Mingi kutokana na kuwepo kasoro ya kiwango cha barabara hiyo na kuweza kusababisha ajali za mara kwa mara.

Bara bara nyengine inayoingiakwenye mpango huo ni ya Mwembe njugu kuelekea Kibanda Hatari, Sokoni kwa Mchina hadi Mwanakwerekwe, Mpendae hadi Nyumba mbili, Kidongechekundu hadi Jang’ombe, Mwembemadema hadi Kikwajuni na Koba hadi Kajengwa.

Kwa upande wa Pemba, Mkurugenzi huyo alizitaja barabara zitakazojengwa ni ya Wete Weni, Ole hadi Konde, Chakechake hadi Wesha, Mbuguani hadi Tironi na Wesha hadi Mkumbuu.

Nyengine Kipapo hadi Mgelema, Chake Chake hadi Mjini na mitaa mbali mbali, kwa maelezo yake, maandalizi ya barabara za Mji wa Zanzibar, alisema yamefikia hatua nzuri baada ya kutumiwa kampuni mbali mbali kufanya kazi bhizo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, hadi Novemba mfuko huo unaidai serikali shilingi 757,870,674.60 .

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alikosoa mfumo unaotumika kuendeshea mfuko kwa kuendelea kuwekwa chini ya Wizara ya Miundo mbinu.

Saturday 11 December 2010

DK. SHEIN : AHADI ZOTE ZILIZOTOLEWA KWENYE KAMPENI ZITATEKELEZEKA.

Dk. Shein: Ahadi zote zilizotolewa kwenye kampeni zitatekelezwa

• Asema Zanzibar imegeuka chuo cha demokrasia


• Ashukuru na kuwataka WanaCCM kuimarisha chama


• Awatoa hofu kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Jumapili 12 Disemba 2010
Na Rajab Mkasaba

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewashukuru WanaCCM na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa kumchagua yeye na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuiongoza Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Aidha, Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi wa haki, amani na utulivu mkubwa ulioonesha kupevuka kwao kidemokrasia ambao umeipa heshima kubwa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa.

Dk. Shein ambaye katika ziara hiyo alifuatana na mkewe Mama Mwanamwema Shein, aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na Viongozi wa CCM, Jumuiya za CCM na Wazee wa CCM wa ngazi ya Tawi, Wadi na Jimbo.

Ikiwa ni siku yake ya awali ya kufanya ziara katika Wilaya zote kumi za Zanzibar Dk. Shein alianza Makunduchi Wilaya ya Kusini na hatimae alizungumza huko Dunga Wilaya ya Kati na kueleza madhumuni ya ziara hiyo ikiwa ni kutoa shukurani kwa wananchi na wanaCCM kwa kufanya uchaguzi kwa salama na amani sambamba na amani na utulivu.

Alitoa pongezi kwa Mkoa huo wa Kusini kufanya vizuri katika uchaguzi Mkuu uliopita kwa kuendeleza historia ya ushindi na kuwapongeza kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi yao ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliopita.

Dk. Shein aliwapongeza Wazanzibari wote kwa kushiriki katika uchaguzi kwa amani na utulivu na kueleza kuwa kazi kubwa iliyopo hivi sasa ni kutekeleza ahadi na kuimarisha maendeleo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba anayoiongoza yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa itafanya kazi vizuri na ataisimamia vyema bila ya hofu katika kutekeleza majukumu yake na atatenda haki kwa Wazanzibari wote bila ya kujali tofauti ya itikadi za kisiasa.

Alieleza kuwa asilimia ya ushindi iliyopatikana katika Mkoa wa Kusini Unguja ni kubwa na imeweza kuthibitisha wazi kuwa Mkoa huo ndio ngome ya CCM.”Hiyo ndio sifa ya CCM ya kuahidi na kufanya” alisema Dk.Shein.

Dk. Shein alieleza kuwa nia ni kuona ahadi zote alizozitoa wakati wa Kampeni za uchaguzi uliopita zinafanikiwa ikiwa ni pamoja na kupata maendeleo na kuahidi kuwawezesha akina mama kama alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi na kusema kuwa lengo lipo vile vile la kuanzisha Benki ya Wanawake.

Alieleza kuwa aliahidi kutekeleza kampeni kwa ustaarabu yeye na viongozi wenziwe na ndivyo ilivyofanyika hatua ambayo imeipelekea Zanzibar kupata sifa ndani na nje ambayo ilipelekea uchaguzi uwe wa amani na utulivu. Pia Dk. Shein aliwashukuru wananchi wote walioshiriki kwa njia zote katika kufanya kampeni zilizoipa ushindi CCM.

Alisema kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yanabeba umuhimu mkubwa kwa wananchi kwa kuwawezesha kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuweza kuimarisha maendeleo katika sekta zote zikiwemo elimu, afya, huduma muhimu ikiwemo maji safi na salama na nyenginezo kazi ambayo itaendelea kuimarishwa.

Dk. Shein alieleza kuwa ahadi yake ya kuimarisha sekta ya michezo na kuwajengea mazingira mazuri wasanii wa vikundi vyote kwa kuwajengea studio ya kisasa lipo pale pale.

Pia, Dk. Shein alitoa wito kwa wanaCCM kushirikiana na kuwa kitu kimoja ili kuweza kukiimarisha Chama na kueleza kuwa ana imani kuwa kundi lililopo hivi sasa ni kundi la CCM.

Alieleza kuwa chama chake kitaendelea kufuata Katiba na Sheria za nchi katika mfumo mzima wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambayo itaendelea kuwepo sambamba na nafasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Dk. Shein alitawaka wanaCCM kutoa kuwa na hofu na kuwaelezwa kuwa ipo kikatiba kwa kutekelezwa matakwa ya wananchi wa Zanzibar na si maslahi ya mtu binafsi au kiongozi fulani.

Alisema akiwa Rais aliyechaguliwa na wananchi atatekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha maslahi ya wananchi yanalindwa na kutekelezwa na si vinginevyo na kiongozi yoyote aliyepewa madaraka akayatumia kinyume hatokuwa pamoja nae.

Nae Mama Mwanamwema alitoa salamu zake za pongezi na shukurani kwa WanaCCM wa Mkoa wa Kusini kwa kuweza kumuunga mkono Dk Shein na kuwashukuru kwa kutimiza ahadi zao kwa vitendo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Ferouz, nae alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kufanya kampeni ambazo hatimae CCM imepata ushindi mkubwa sana katika ushindi wa Majimbo kwa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.

Alisifu juhudi za Dk. Shein alizochukua mchana na usiku, ambazo zimeweza kuleta ushindi mkubwa, na kumpongeza kwa niaba ya wanaCCM kwa umakini na busara kubwa aliyofanya ya kuunda Baraza la Mawaziri.

Nao wanaCCM wa Wilaya ya Kusini Unguja walieleza kutekeleza ahadi yao ya Wadi zote 11 na Majimbo mawili kuwa yatachukuliwa na CCM ahadi ambayo waliitoa wakati Dk. Shein alipofika Wilayani humo wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita na kueleza kuwa Mkoa wa Kusini ni Ngome ya CCM.

Wametoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuunda Baraza zuri la Mawaziri na kueleza kufarajika kwao na Baraza hil la Mawaziri na kujenga matumaini makubwa ya kuweza kupata maendeleo zaidi.

Mapema Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mashirikiano makubwa waliompa na hatimae CCM kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliopita.

Dk.Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar katika ukumbi wa ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui mjini Unguja.

Alisema kuwa kuzungumza na wazee ni utamaduni na heshima ya CCM kwa kutambua umuhimu wa wazee ikiwa ni pamoja na kupata busara zao.

Dk. Shein alitoa shukurani kwa wazee hao na kueleza kuwa juhudi zao zimeweza kuzaa matunda na hatimae chama cha CCM kuweza kupata ushindi pamoja na kuendeleza amani na utulivu iliyopo nchini.

Aidha, Dk. Shein aliwahakikishia wazee hao kuwa ataendelea kufanya kazi nao ikiwa ni pamoja na kupokea busara, hekima na ushauri wao ili kuweza kuimarisha chama pamoja na kuleta maendeleo endelevu hapa nchini.

Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa wito kwa wazee hao kuendelea kufanya kazi kwa pamoja, kuendeleza mashirikiano kwa lengo la kufuata nyayo za chama cha ASP za umoja na mashirikiano.

Alieleza imani yake kuwa wazee hao wataendelea kushirikiana kwa pamoja ili kukiimarisha chama na kuweza kuwasaidia viongozi wao pamoja na kuweza kuwapa nguvu vijana kufanya kazi zao vizuri.

Nao wazee walieleza matumaini yao kwa Dk. Shein kuwa atakuwa mtendaji bora zaidi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuwa muumini mzuri wa kuendeleza Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.

Wazee hao walimpongeza Dk. Shein kwa ushindi alioupata katika uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

WATAKA UBAGUZI WA KIUCHUMI UONDOSHWE.

Wataka ubaguzi wa kiuchumi uondoshwe

Na Mwantanga Ame
Jumapili 12 Disemba 2010

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeshauriwa kuzifuta sheria zinazoonekana kuleta ubaguzi kwenye nyaja ya uchumi, ili kukuza pato la taifa pamoja na maisha katika jamii.

Mwanasheria wa kujitegemea Awadh Said, alieleza hayo alipokuwa akichangia kwenye kongamano la siku moja la kuadhimisha siku ya haki za Binadamu, lililofanyika Ukumbi wa EACROTANAL Mjini Zanzibar.

Alisema kama serikali imekubali kufuata haki za binadamu lazima iondoshe ubaguzi kwenye eneo la kiuchumi hasa katika kilimo, masoko na masuala ya kijamii.

Mwanasheria huyo alitoa mfano wa zao la karafuu ambalo alisema liko chini ya usimamizi wa serikali huku wakulima wakiwa wanapangiwa bei, sehemu ya kuuzia ambapo wakulima wengine wakiwa wako huru kuuza kwa bei na mahali wanapotaka.

Alisema huo ni aina ya ubaguzi wa kiuchumi kwa vile umekuwa ukiwapa haki wakulima wa mazao mengine kufanya watakavyo huku wakulima wa zao la karafuu wakibanwa.

Alisema kama serikali imefikia hatua ya kupinga ubaguzi lazima suala la wakulima wa karafuu nalo liwekwe wazi kusiwe na ubaguzi.

“Inashangaza mazao yote ya wakulima wamekuwa wakiachiwa kijipangia na kuuza kwa bei wazitakazo, lakini zao la karafuu bado linaendelea kubanwa kwa kufanywa na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) pekee”, alisema Awadh.

Alisema kuendelea kuweka zao hilo kufanywa na ZSTC, ni sawa na ubaguzi unaonyima utoaji wa Haki za binadamu kiuchumi na ni lazima serikali iliangalie.

"Sheria ya karafuu inambagua mkulima kwani imewekewa mipaka huku wakulima wengine wanaachiwa kuuza bidhaa zao watakavyo" alisisitiza.

Aidha, Mwanasheria huyo alisema ili kilimo hicho kiweze kuwa na tija ni vyema kwa serikali ikauangalia upya uamuzi wa kuendelea kulisimamia zao hilo kwani ubaguzi wa kilimo hautaweza kuleta maendeleo katika kukuza pato la taifa.

Nao washiriki wengine kwenye kongamano hilo, walisema ipo haja ya usimamizi wa sheria za kazi, usalama barabarani na maslahi ya wafanyakazi ni mambo ya msingi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi Zanzibar.

Mmoja wa wachangiaji hao Mohammed Yussuf ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Utafiti (ZIPPOR), alisema, Zanzibar inapaswa kujivunia kutokana na kuongezeka kwa utawala bora ikilinganishwa na miaka ya nyuma, lakini ipo haja serikali ikalisimamia tatizo la rushwa na wizi wa fedha za serikali.

Alisema baadhi ya watumishi wamekuwa kero kwa jamii kutokana na kuiibia serikali kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo linadhoofisha uchumi wa nchi.

Nae Amrani Umbaya Vuai, alisema kuwepo kwa ongezeko la usafiri wa magari serikali inapaswa kuanza kufikiria mkakati utaoutumika kupunguza ajali kwani tayari kumekuwa na madereva wanaogonga watu ovyo na kisha kukimbia huku wakiacha familia nyingi kuwa mayatima.

Nae Profesa Chris Peter Maina, alisema ipo haja ya kuangaliwa kwa sheria ya ukaazi kwani wanawake wanaoolewa huzuiliwa kupiga kura eneo ambalo mume wake anaishi huku mume huyo akiachwa huru kuchagua kupiga kura kwenye nyumba yeyote anayoamkia ikiwa ana zaidi ya mke mmoja.

Alisema hali hiyo inamnyima uhuru mwanamke hilo ni lazima liangaliwe kwa vile bado limekuwa halimpi haki mwanamke huku likimuacha mwanamme huyo kupiga kura apatakapo haki ambayo ilitakiwa iwe kwa wote.

JINA LA MGOMBEA UMEYA WA ZANZUBAR CCM LEO.

Jina la mgombea Umeya wa Z'bar CCM leo
Na Mwantanga Ame
Jumapili 12 Disemba 2010

BAADA ya Kamati Kuu CCM, kuyarejesha majina mawili ya wanaowania nafasi ya Umeya wa Mji wa Zanzibar, ngoma nzito kwa Meya aliyemaliza muda wake Mahboub Juma Issa, kwani kazi ya ziada itamlazimu kuchukua kuvuka kigingi cha kuitetea nafasi hiyo.

Kazi hiyo itamkumba Meya huyo kwenye kikao kinachotarajiwa kutoa maamuzi ya nani atakuwa Meya wa Mji wa Zanzibar, baada ya jina la mpinzani atakaechuana nae nalo kurejeshwa na Kamati hiyo.

Kikao kitachotoa jina la mgombea wa Umeya wa Zanzibar kinatarajiwa kufanyika leo katika Afisi ya Chama Mkoa wa Mjini huko Amani Mjini Zanzibar, ambapo pia kitachagua mgombea Naibu Meya kati ya wagombea watatu.

Hapo awali Kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, kilichofanyika juzi Mjini Dar es Salaam kwa ajili ya kupitisha majina ya wagombea, ambapo kiliyarejesha majina yote mawili likiwemo la mpinzani wake Khatib Abrahman Diwani wa Miembeni.

Kurudi kwa majina hayo mawili tayari baadhi ya watabiri wanadai kuwa kazi kubwa itamkuta Meya, Mahboub leo hii ili kuona anafanikiwa kubakia katika kiti hicho kwa miaka mitano ijayo.

Mahboub, tayari ameshakaa katika kiti cha Umeya wa Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano iliyopita akiwa ni Diwani wa wadi ya Kisimamajongoo aliyetokea Jimbo la Kikwajuni.

Abrahman ni Diwani mpya wadi ya Miembeni anaewania nafasi hiyo kwa mara ya kwanza ambaye alishika nafasi hiyo baada ya kushinda uchaguzi wa marudio katika Waji hiyo kwa Jimbo la Kikwajuni.

Kutokana na upya wa Diwani huyo tayari baadhi ya watabiri wa mambo ya kisiasa waliliambia gazeti hili kuwa Meya huyo aliemaliza muda wake atakuwa na kazi kubwa kutokana na changamoto iliyojitokeza kuona wagombea hao kutoka katika Jimbo moja.

Walisema bila ya kutaka kutajwa majina yao kutokana na ukaribu wa Mgombea huyo wanasiasa hao walisema hawafahamu ni kwanini iwe wagombea hao kutoka Jimbo moja kutaka kuwania nafasi hiyo ingawa ni Demokrasia.

Walifahamisha kuwa wasingemuona Meya huyo kuwa na kibarua kikubwa pale ingetokezea kwa CCM kuweka jina moja ama Wagombea hao kutokea katika Majimbo tofauti kati ya manane yalioshikwa na Chama hicho.

Sababu nyengine ambayo waliieleza ushindani wanautarajiwa kuwa mkali kwa wagombea hao kutokana na kuwapo kwa sura nyingi mpya, ndani ya Baraza hilo na sio zile ambazo alizofanya nazo kazi katika Baraza lililopita hapo awali.

Kutokana na hali hiyo wafuatiliaji hao wa mambo ya siasa walifahamisha kuwa wanachokitabiri kuwapo kwa ushindani mkali kwa wagombea hao baada ya majina yao kufikishwa katika Baraza la Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi.

Tayari wagombea hao ili wameanza kufanya kampeni zao kwa wajumbe wa baraza hilo pamoja na viongozi wa Chama ili kuona kila mmoja anafanikiwa katika uchaguzi huo.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Mahboub alisema ana imani kubwa ya kuweza kubakia katika nfasi yake hiyo kwa vile wagombea wote ni kuwa wanatoka katika Jimbo moja.

Alisema amepokea uteuzi wa jina lake kurudi na mpinzani wake kwani kitachoenda katika kikao hicho ni mchuano wa wagombea wanaotoka katika Jimbo moja na atakuwa tayari kupokea matokeo ya aina yoyote.

Alisema lengo lake bado kuwa aina yoyote ya matokeo yatabakia kuwa na mgombea wa CCM katika Baraza la Madiwani ili kuweza kushirikiana na wanachama wa CCM waliomo katika Baraza hilo waweze kufanya kazi zao vizuri na kwa ushirikiano.

DAWA YA UNYANYASAJI MAKAZINI YAJA.

Dawa ya unyanyasaji makazini yaja

Na Halima Abdalla
Jumapili 12 Disemba 2010

KAMISHNA wa Kazi kutoka Wizara ya Kazi na Uwezeshaji Kiuchumi, Iddi Ramadhan Mapuri, amesema wanaandaa ziara ya kufanya ukaguzi kwenye sehemu za kazi ili kuangalia matatizo yanayowakabili wafanyakazi.

Alisema ukaguzi huo utakaofanywa utasaidia kuweza kutatua migogoro ya kikazi watakayoibaini kwa wafanyakazi na waajiri.

Aidha Mapuri alisema, katika ukaguzi huo pia wataangalia mahusiano ya waajiri na wafanyakazi kwa kuangalia mikataba ya kazi, mazingira ya kazi, pamoja na masuala nyeti kama mishahara, haki na wajibu.

Sambamba na hayo alisema wanataka kujiimarisha ili kuweza kutoa takwimu zinazohusiana na ajira kwa wakati muafaka pamoja na kutelekeza sera ya ajira iliyopitishwa mwaka 2009.

“Lengo tunataka kamisheni ya kazi iwe na uwezo wa kufanya kazi kwa kujiimarisha zaidi na kwa nguvu zaidi ikiwemo kukamilisha kanuni za sheria za kazi ambazo hazijatayarishwa,’’alisema Mapuri.

Hata hivyo alisema katika kufanikisha hayo bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wataalamu ambao watakaofanikisha kufanya ukaguzi wa utatuzi wa migogoro hiyo ya wafanyakazi kwa kiwango cha ufanisi zaidi.

Sambamba na hayo alisema pamoja na changamoto zote zinazoikabili Idara yao karibu ya asilimia 75 ya migogoro wanayoipokea ya wafanya kazi wameweza kuitatua na kubwa wametayarisha mpango mkakati wa miaka mitano.

UNYANYASAJI WAFANYAKAZI MAJUMBANI WALAANIWA.

Unyanyasaji wafanyakazi majumbani walaaniwa

Na Sharifa Maulid
Jumapili 12 Disemba 2010


SERIKALI inatambua uwepo wa wafanyakazi wa majumbani ndio maana imetoa toleo maalum linalozingatia kiwango cha kima chao cha mishahara yao.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Ali Khamis Juma, alisema hayo alipokuwa akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya wafanyakazi wa majumbani Duniani.

Alisema kutokana na hali hiyo jambo linalotakiwa kuzingatiwa ni ufuatiliaji wa kazi zao ikiwemo masharti muhimu ya utendaji kazi.

Juma alisema mbali na watu kufanyakazi majumbani lakini bado kuna baadhi ya waajiri hawathamini, hawawapatii haki zao kwa kuwapa mikataba badala yake hutumia uwezo wao kuwadhalilisha.

Naibu huyo aliwataka waajiri nchini kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kutoa haki anazostahili mfanyakazi sambamba na wafanyakazi wenyewe kujenga msingi mzuri wa kazi za staha.

"Serikali inaungana na shirika la Kazi Duniani (ILO) na kuona umuhimu wa kuandaa mikataba wa kuweko kazi za staha kwa wafanyakazi majumbani", alieleza Naibu Katibu Mkuu huyo.

Alifahamisha kuwa, katika mkataba huo mambo mbali mbali yamezingatiwa ikiwemo kupata mishahara, likizo, mapumziko, mikataba ya kazi na faragha.

Aidha aliwataka wafanyakazi majumbani kujiunga katika jumuiya yao ili kuwa na sauti moja na kueleza yale yote ambayo watafanyiwa kinyume na maadili ya kazi.

Mapema akitoa salamu za shirikisho la Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Suleiman Omar, alisema wafanyakazi wa majumbani wanachangia maendeleo kwa waajiri na familia zao, hivyo ni vizuri waajiri kujitahidi kuwapatia haki zao na kuwathamini kama binaadamu.

Alisema wafanyakazi hao wanapewa majukumu makubwa katika nyumba na kuyatekeleza bila kujali saa anazofanyakazi na aina ya kazi anazozifanya.

Kongamano hilo limezungumzia juu ya Mkataba wa ILO ya wafanyakazi wa majumbani pamoja na umuhimu wa wafanyakazi majumbani kujiunga na jumuiya yao ya ZATHOCODAWU.

Wakati huo huo akilifunga kongamano hilo Katibu Mkuu wa ZATHOCODAWU, Ali Salum Ali alisema utekelezaji wa sheria za kazi umekuwa mgumu hivi sasa kutokana na sheria za kazi ambazo zimefanyiwa marekebisho 2005 kutokuwa na kanuni zake.

Alisema kesi nyingi zinazuhusu wafanyakazi na waajiri zinashindwa kufunguliwa na kuendeshwa vilivyo kutokana na kasoro hizo pamoja na Bodi ya kiwango cha mishahara kutokutana miaka minne sasa, jambo ambalo linasikitisha wafanyakazi wa majumbani.

Ujumbe wa mwaka huu 'Tufanyekazi za majumbani kuwa ni kazi ya Staha', kongamano hilo limefanyika katika ukumbi wa Eacrotanal mjini hapa.

WENGI WAMZIKA, WAELEZA WALIVYOGUSWA.

Wengi wamzika, waeleza walivyoguswa

Salum Vuai
Jumapili 12 Disemba 2010
MAMIA ya wananchi wa Zanzibar na vitongoji vyake wakiwemo wasanii wakongwe na chipukizi, walijitokeza katika mazishi ya marehemu Bakari Abeid Ali aliyefariki dunia jana.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa serikali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mwinyihaji Makame Mwadini, Rais mstafu wa awamu ya sita Dk Amani Abeid Karume, makatibu wakuu na watendaji kadhaa wa wizara mbalimbali.

Akielezea namna alivyoguswa na kifo cha marehemu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi, alimsifia kwa kipaji cha lugha fasaha alichokuwa nacho, akisema daima alijua ni maneno gani ya kuzungumza kwa wakati na pahala maalumu.

Aidha alisema marehemu Abeid alifahamu namna ya kuzifurahisha nyoyo zilizojaa majonzi katika namna ambayo mlengwa alifarajika na kurudi matao ya chini hata kama alikuwa amefura kwa hasira.

Mkuu huyo wa Mkoa alikuwa mshirika wa karibu na marehemu wakifanya kwa pamoja vipindi vya 'Ndivyo tulivyo' na 'Usilolijua' vilivyokuwa vikirushwa na Sauti ya Tanzania Zanzibar na Televisheni Zanzibar miaka kadhaa iliyopita.

Naye msanii mkongwe wa fani za ushairi Haji Gora, alisema marehemu alikuwa kama maktaba kwake kwani aliweza kuchota mengi katika kazi zake za usanii, na kwamba kifo chake ni sawa na maktaba hiyo kufungwa kufuli na ufunguo wake kutupwa katika bahari ya kina kirefu.

Msanii wa maigizo Hassan Suleiman 'Chita', alimtaja marehemu kuwa ni mwalimu aliyebobea na ambaye hakuwa na hiyana katika kutoa ujuzi wake kwa wasanii waliokuwa wakijifunza sanaa.

"Unavyoniona nikiigiza, ni sehemu ya faida nilizopata kutoka kwake, kwani alikuwa akinihimiza kwa kuniambia niwahi kuchota mapema kwani hakuna ajuaye lini ataondoka duniani.

GWIJI WA SANAA ZANZIBAR BAKARI ABEID AFARIKI DUNIA.

 Gwiji wa sanaa Bakari Abeid afariki dunia

Na Salum Vuai
Jumapili 12 Disemba 2010.

KAMBI ya wasanii wa fani za taarab na maigizo nchini, imegubikwa na msiba kwa kuondokewa na msanii gwiji na mkongwe Bakari Abeid Ali aliyefariki jana alfajiri nyumbani kwake Mombasa mbuyu mnene.

Marehemu huyo (77) amekutwa na mauti baada ya kukumbwa na maradhi ya kiharusi yaliyomsumbua kwa muda mrefu.

Msanii huyo aliyezaliwa Agosti 25, 1933 katika kijiji cha Ole kisiwani Pemba, atakumbukwa kwa umahiri wake katika sanaa za utunzi, uimbaji taarab na maigizo, ambapo aliweza kuwavutia mashabiki wengi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Wakati wa uhai wake katika enzi alizojikita kikamilifu katika usanii, Abeid alikuwa hodari wa kuwatuliza watazamaji alipokuwa jukwaani kwa namna alivyomudu kuiteka hadhira kwa umahiri wake wa kuigiza na kuimba.

Baada ya kudhihirisha kipaji chake, marehemu aliwahi kuwa mwanachama wa vyama tafauti vya taarab ikiwemo Michenzani alichoshiriki kukiasisi mwaka 1952, Nadi Ikhwan Safaa (1956) na Culture (1964).

Akiwa msanii mashuhuri, marehemu alishiriki kutunga na kuimba au kutia muziki nyimbo mbalimbali katika vikundi hivyo na miongoni mwa hizo ni 'Mazowea yana tabu', 'Njiwa peleka salamu', 'Tini tunda la tamasha', 'Pendo halijui siri', 'Bahati', 'Kisebusebu', 'Wagombanao hupatana', 'Nnapenda kwa ishara' na nyengine nyingi.

Mbali na shughuli za kisanii, marehemu Bakari Abeid alifanya kazi serikalini na kushika nyadhifa kadhaa kwa vipindi tafauti kama vile Afisa wa Sanaa katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii (1985), Mjumbe wa Baraza la Sanaa Tanzania (1986), Mjumbe Baraza la Sanaa Zanzibar (BASAZA) mwaka 1989.

Aidha aliwahi kuwa Mkuu wa Habari, na baadae wa utangazaji katika Idara ya Habari na Utangazaji Zanzibar, Mkuu wa Vipindi Televisheni Zanzibar na Mshauri wa Rais mambo ya utamaduni na pia mshereheshaji mkuu katika sherehe mbalimbali za kitaifa.

Wananchi wengi watamkumbuka kwa kipindi kilichompatia umaarufu mkubwa katikaSauti ya Tanzania Zanzibar cha 'Ndivyo tulivyo, akishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis ambacho baadae kilihamia Televisheni Zanzibar.

Marehemu aliyezikwa jana katika makaburi ya Mwanakwerekwe ambapo mazishi yake yalihudhuriwa na mamia ya wananchi wakiwemo wasanii wa fani mbalimbali, ameacha mtoto mmoja wa kiume.

BOMBOM YASHINDWA KUIRIPIA MIGOMBANI.

Bombom yashindwa kuiripua Migombani

Na Aboud Mahmoud
Jumapili 12 Disemba 2010

TIMU ya soka ya Migombani ya Zanzibar, imetoka kidedea kwa kuifunga timu ya Bombom ya mjini Dar es Salaam goli 1-0 katika mashindano ya muungano kwa timu za vijana wa daraja la central.

Katika mtanange huo uliochezwa kwenye uwanja wa Mao Tsetung bao la washindi lilipachikwa nyavuni na Omar Juma mnamo dakika ya 50.

Vijana wa Bombom walijaribu kwa kila hali kutafuta bao la kusawazisha na pengine la ushindi, lakini mabomu yao yalishindwa kufyatuka.

Aidha katika kiputehicho, Migombani ilipata pigo bada ya mchezaji wake Ali Salum kufurushwa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 76 kutokana na mchezo wa rafu.

Michuano hiyo inashirikisha timu za vijana kutoka Tanzania Bara na wale wa Zanzibar.

KILI STARS, IVORY COST ZAWANIA DOLA 30,000

 Kili Stars, Ivory Coast zawania dola 30,000

Na Mwandishi Wetu
Jumapili 12 Disemba 2010

BAADA ya kuzifunga timu za Ethiopia na Uganda katika michezo ya robo fainali juzi, timu za taifa za Tanzania Bara na Ivory Coast, leo zinajitupa katika uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam, kuwania taji la ubingwa wa michuano ya Chalenji.

Kabla kutinga hatua hiyo, Ivory Coast iliichapa Ethiopia mabao 2-1 katika nusu fainali, huku Kilimanjaro Stars ikiitoa jasho Uganda kwa dakika 120 kabla kuibuka na ushindi wa mabao 5-4 kwa changamoto ya mikwaju ya penelti.

Uganda ndio iliyokuwa ikiushikilia ubingwa huo kwa miaka mitatu na hivyo kubakisha kikombe cha zamani katika himaya yake.

Licha ya kupambana na moja kati ya timu vigogo barani Afrika, Kilimanjaro Stars inapewa nafasi kubwa kushinda leo, hasa kutokana na uwezo ilioonesha katika michezo iliyopita ambapo ngome yake imeruhusu kufungwa bao moja tu muda wa dakika 90 za michezo minne iliyocheza.

Ingawa Stars ilianza kwa kipigo cha bao 1-0 mbele ya Zambia katika mchezo wake wa kwanza, lakini ilionesha kuimarika hatua kwa hatua, hali inayowapa matumaini Watanzania kushuhudia ikifuta aibu ya kukosa mataji kwa miaka mingi sasa.

Kocha Jan Poulsen anatarajiwa kuwapanga nyota wake wote muhimu kuanza kusaka ushindi mapema akiwemo Mrisho Ngassa, John Boko, Nurdin Bakari, Shadrack Nsajigwa, Juma Nyoso, huku mlangoni kama kawaida akiwekwa Juma Kaseja ambaye alipangua penelti moja na kuipeleka timu hiyo katika fainali kwenye mchezo dhidi ya Uganda.

Hata hivyo, pamoja na kucheza kwenye uwanja wa nyumbani wakishajiishwa na maelfu ya mashabiki wake, lakini Stars itakuwa ikikabiliana na upinzani mkali kwani Ivory Coast si timu ya kubeza kwani ina uwezo wa kufuta ndoto za Watanzania kubakisha taji hilo kama haitakuwa makini.

Kimsingi Tanzania imeshatwaa kombe la Chalenji kwa kuwa inacheza na timu mwalikwa, ambayo hata kama itashinda, itakabidhiwa zawadi ya fedha bila kikombe, lakini kuibuka na ushindi ni kitu muhimu kitakachowapa faraja Watanzania.

Pambano hilo litatanguliwa na lile la kutafuta mshindi watatu ambalo litazikutanisha timu za Ethiopia na Uganda zilizopoteza michezo ya nusu fainali.

Friday 10 December 2010

JAMII YAKITHIRI KUVUNJA HAKI ZA BINAADAMU --WANASHERIA.

Jamii yakithiri kivunja haki za binaadamu - Mwanasheria

Chanzo kutokuwa na elimu, jinsi ya kuzidai
Na Mwantanga Ame
Jumamosi 11 Disemba 2010

VITENDO vya uvunjaji wa Haki za Binaadam vimeshamiri zaidi ndani ya jamii ikilinganishwa na serikali inavyovunja haki hizo.

Mwanasheria kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, Ali Uki alieleza hayo alipokuwa akitoa mchango kwenye kongamano la kuadhimisha siku ya kimataifa ya Haki za Binaadam lililofanyika katika ukumbi wa EACROTANAL Mjini Zanzibar.

Alisema uchunguzi uliofanywa na kituo cha Huduma za Sheria, umebaini vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu kufanywa zaidi na wanajamii kuliko serikali.

Kongamano hilo lilitayarishwa na Kituo Cha Huduma za Sheria kwa ajili ya kuadhimisha miaka 62 ya siku ya haki za binadamu ambapo liliwashirikisha wadau mbali mbali wakiwemo vyama vya siasa, Wanasheria, Asasi za kiraia,Taasisi Binafsi, na vyombo vya habari.

Mwanasheria huyo alisema, ushahidi unaonyesha kuwepo vitendo vingi vya uvunjifu wa Haki za Binaadam kwenye nyumba nyingi wanazoishi wananchi, hali inayotokana na wanajamii wengi kutojua njia za kupata haki pale zinapokiukwa haki hizo.

"Sehemu kubwa ya haki za binadamu zimekuwa zikivunjwa na watu binafsi na sio serikali inawezekana hili likawa linachangiwa watu hawajui namna ya kudai haki zao",alisema Uki.

Alifahamisha kuwa suala la ubaguzi kwenye nchi nyingi za Kiafrika ikiwemo Tanzania, linaendelea kwenye nyanja mbali mbali ikiwemo ajira ambapo mtu huangaliwa sehemu anayotoka, dini huku waliosoma kuachwa mitaani na kuajiriwa ambao hawana elimu.

Alisema uwepo wa baadhi ya vitengo kwa ajili ya kupima vigezo muhimu vya kuajiriwa kazini kama GSO, ni moja ya vitengo ambavyo vinaweza kutumika kufanya ajira za kibaguzi kwani huweza kupima mwananchi huyu ni wa dini gani ama mzaliwa wa wapi.

Aidha Mawanasheria huyo alilalamikikia baadhi ya vipengele vya Mabadiliko 10 ya Katiba ya Zanzibar, juu ya kipengele kinachozungumzia masuala ya haki za binadamu kesi zake kukomea katika Mahakama za Zanzibar na kutotoa haki kufikishwa katika Mahakama ya Rufaa kama pindipo ikijitokeza kufanya hivyo.

Mapema Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, akifungua kongamano hilo alisema ipo haja ya kufanyika kwa tathimini ambayo itabainisha kama Katiba ya Zanzibar na sheria zake zinakubaliana na misingi ya utoaji wa haki za binadamu.

Waziri Bakary, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepania kuheshimu haki za binadamu, lakini jitihada hizo zinaonekana bado hazijafika pale panapotakiwa na ni vyema kwa Wazanzibari kujitahidi kufanikiwa kwenye utekelezaji wa haki hizo.

Waziri huyo alibainisha jitihada kadhaa zilizochukuliwa na serikali katika kuhakikisha inaboresha misingi ya haki za binaadam, ikiwemo kuheshimu mikataba ya kimataifa 'Beijing Platform for Action', kuweka sheria ya kuwalinda wari na wajane,kuongeza idadi ya wanawake katika Baraza la Wawakilishi kufikia asilimia 40 na kuweka sheria za kumlinda mtoto.

Alisema jambo la msingi ambalo linahitajika kuangaliwa ni kuona vipi mwananchi anajengwa namna ya kutambua haki binaadamu kuwa ni haki zao za msingi na sio kufanywa kama ni fadhila.

Nae Mtoa mada katika kongamano hilo, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu, Joaquine De Mello, alisema kuna changamoto kubwa Tanzania kupambana na tatizo la ubaguzi kwani bado yapo mengi yanayotendeka ndani ya familia tofauti ya za rangi, ngozi urefu na ufupi, jinsia, ujana, uzee, mtoto wa kike na wakiume na wanaume kukabiliana na wanawake.

Kamishna huyo akiyataja changamoto nyengine alisema ni ya utajiri na raslimali, tajiri na maskini, viwango vya elimu, Mamlaka na uwezo, hali za afya na fedheha za kukosa afya kwa wagonjwa wa UKIMWI, ukoma na ugumba au utasa.

WAZIRI WA MIUNDOMBINU AZUIA SAFARI ZA MELI YA MV MAENDELEO.

Waziri wa Miundombinu aizuia safari za MV Maendeleo

Na Raya Ahmada, Pemba
Jumamosi 11  Disemba 2010

WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Massoud ameizuia meli ya M.V Maendeleo kuendelea na safari zake za kawaida za kubeba mizigo na abiria.

Waziri huyo amelazimika kuzuia safari za meli hiyo, kutokana na kuharibika mashine yake moja ikiwa kwenye safari zake hali iliyosababisha kufungwa tagi na kukokotwa hadi bandarini Mkoani.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masuod Hamad alitoa agizo hilo mbele ya manahodha na mafundi wa meli hiyo huko bandarini Mkoani, akiwa katika ziara zake za kuyatembelea Mashirika na Idara zilizomo katika wizara hiyo kisiwani Pemba.

Waziri huyo alisema hatua ya kuzuiliwa safari za meli hiyo inatokana na kuharibika mara mbili wakati ilikiwa kwenye safari zake za Unguja na kuifanya meli hiyo itembee ikiwa na mashine moja.

Alisema serikali inajali na kuthamini maisha ya wananchi wake na wala haitakubali kuona meli hiyo inasafirisha abiria ikiwa inatembea na injini moja kama ilivyokuwa ikifanya.

“Meli ipelekwe Mombasa ikatengenezwe injini zote mbili ndio ifanye kazi za kupakia abiria”, alieleza.

Akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo kwa wakati tofauti, aliwataka wakuu wa vitengo kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini na sio kujenga woga kwa kuwaogopa wakubwa wao au kufata matakwa yao.

Nae Naibu waziri wa wizara hiyo Issa Haji Usi, alisema lengo walilojipangia ni kufanya mabadiliko kwa kuifanya wizara hiyo kuwa ya mfano katika utoaji wa huduma za uhakika kwa jamii.

Nae fundi mkuu wa meli ya M.V. Maendeleo alikiri kuharibia meli yao wakati wameshaingia katika maeneo ya kisiwa cha Pemba na kusaidiwa na tagi ya mpaka kwenye gati ya Mkoani.

Hiyo ni ziara ya kwanza kwa waziri wa Miundombinu na Mawasiliano na Naibu wake kutembelea Mashirika na Idara za wizara hiyo.

KUPOROMOKA KWA MAADILI KWACHANGIA UDHALILISHAJI WA WATOTO.

Kuporomoka maadili kwachangia udhalilishwaji watoto

Na Mwanajuma Abdi
Jumamosi 11Disemba 2010

HUKU wimbi la udhalilishaji watoto likiendelea katika jamii, baadhi ya wazazi na walezi wanadaiwa kuwa na mchango mkubwa unaosababisha watoto wao wadhalilishwe na kubakwa.

Washiriki wa mkutano wa mwaka uliwakutanisha wadau mbali mbali, kupitia Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Zanzibar (WEZA) unaoendeshwa na shirika la CARE Tanzania na Jumuiya ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA),walieleza hayo katika Ukumbi wa Elimu Mbadala Rahaleo mjini hapa.

Walisema baadhi ya wazazi wa kike na wa kiume wanahusika kwa njia moja ama nyengine katika kuharibiwa watoto, kutokana na kuwavisha nguo fupi na za kubana, sambamba na akinababa kuwageuza watoto wao kama ni sehemu ya wake zao kwa kufanyanao mapenzi.

Akichangia katika mjadala, Mwakilishi kutoka Umoja wa Watu wenye Ulemavu, Salma Haji Sadaat, alisema wakati wa Sikukuu wazazi huwapaka watoto hina na piko kama watu wazima pamoja na kuwasuka rasta, jambo ambalo huwa vichocheo kwa wabakaji.

Alisema mbali ya watoto hao kurebwa kwa piko na hina pia huvishwa nguo vifupi zenye kubana huku miili yao ikionekana wazi.

"Starehe zimeongezeka, tunawarembea watoto wetu sana ndio sababu ya kudhalilishwa watoto pamoja na kuongezeka mimba za utotoni",alisema.

Salma alipongeza hatua ya Serikali za Mkoa kuzuia madisco katika viwanja vya sikukuu na kueleza kuwa makakati huo uendelee ili kuwaepusha watoto na vishawishi.

Nae Asha Aboud kutoka Jumuiya ya Kuwawezesha Wanawake, aliwatupia lawama wanaume na kuwataka wasifanye kisingizio cha mavazi kwani kuna watoto wa kiume wengi wanaharibiwa ikiwa hata hawavai nguo fupi.

Alisema wakati umefika kwa jamii kubadilika na kuungana pamoja katika kupiga vita masuala mazima ya udhalilishaji wa watoto.

Nae Siajabu Suleiman kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, aliwashauri akina mama wawe macho na waume zao kwani baadhi yao wanajihusisha na uharibifu wa watoto wao kwa kuwabaka na kuwalawiti.

Akitoa majumuisho katika mkutano huo wa siku moja, Meneja wa Mradi wa WEZA, Rase Matovu alisema mradi huo wa miaka minne umeanza mwaka 2008 na unamalizika Disemba mwakani, hivyo alitoa wito kwa waliowezeshwa watumie mafunzo hayo kuiendeleza jamii.

Mapema akiwasilisha maelezo ya mradi huo, Afisa Muwezeshaji, Ismail Salum alisema lengo lake ni kuchangia kupunguza umasikini kwa wanawake wa Zanzibar katika kuinua kipato chao na kuwaondoshea vikwazo.

Alisema kesi 36 zimeripotowa za ndoa na mimba za mapema, sambamba unyanyasaji wa kijinsia kwa kutekelezwa na waume zao kesi 22 kati ya hizo 15 zilipatiwa ufumbuzi.

Mkutano huo ulifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Haji Makungu Mgongo, aliupongeza mradi huo kwa kufanya kazi vizuri katika kuwashirikiana na wanavikundi vinavyowashirikisha wanawake na wanaume katika Wilaya zote nne katika kuwajengea uwezo katika suala zima la kukuza uchumi na kuondokana na umasikini nchini.

Dk. SHEIN KUFANYA ZIARA YA KUWASHUKURU WANA CCM.

Dk. Shein kufanya ziara ya kuwashukuru wanaCCM



Na Mwandishi Wetu
Ijumaa 11 Disemba 2010
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Muhamed Shein, anatarajia kuanza ziara ya kichama katika Wilaya za Mikoa Mitano ya Zanzibar.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Itikadi na Uenezi, Vuai Ali Vuai imeeleza kuwa kwenye ziara hiyo Dk. Shein atazungumza na viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali.

Alisema lengo la ziara hiyo pamoja na mambo mengine, ni kutoa shukurani na kwa wanaCCM kwa kikiwezesha Chama hicho kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema Dk. Shein ataanza rasmi ziara hiyo Disemba 11 mwaka huu katika Mkoa wa Kusuni Unguja, ambapo majira ya asubuhi ataanza ziara hiyo Wilaya ya Kusini na baade kutembelea Wilaya ya Kati.

Katibu Vuai alisema Disemba 12, Dk. Shein ataendelea na ziara yake Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo taanzia Wilaya ya Kaskazini ‘B’ asubuhi na jioni kumaliza Wilaya ya Kaskazini ‘A’.

Ziara hiyo kwa kisiwa cha Unguja itamalizika Disemba 13, kwa kuzitembelea Wilaya za Magharibi na Wilaya ya Mjini.

Baada ya kuzimaliza wilaya za Unguja, Dk. Shein atakuwa atawasili kisiwani Pemba Disemba 14, ambapo Disemba 15 ataanza ziara katika wilaya ya Micheweni na Wete na kumaliza ziara hiyo Disemba 16 kwa Wilaya za Mkoani na Chake-Chake katika Mkoa wa Kusuni Pemba.

MAADHIMISHO YA UHURU TANZANIA BARA YAFANA.

Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania bara yafana




Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Alhamisi 9 Disemba 2010

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, jana aliongoza Watanzania kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanzania bara.

Tanzania bara, iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika kabla ya Muungano wa mwaka 1964, ilijipatia Uhuru wake Disemba 9 mwaka 1961, ambapo hadi jana imetimia miaka 49.

Sherehe hizo zilizofanyika katika kiwanja cha Uhuru jijini Dar es Salaam, pia zilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Aidha pia zilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda, Spika wa Bunge Anne Makinda, Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, Mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar, Mabalozi pamoja na viongozi waandamizi wa serikali za Tanzania.

Katika maadhimisho hayo ya siku ya Uhuru, Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama alikagua gwarige maalum lililoandaliwa na vikosi hivyo.

Aidha vikosi hivyo, vilipata nafasi ya kucheza gwaride huku vikipita mbele ya jukwaa kuu vikitoa salamu ya heshima na utii kwa mwendo wa pole na mwendo wa haraka.

Katika sherehe za jana pia zilinogeshwa na ndege za kivita za Jeshi la Wananchi wa Watanzania zilizokuwa kipita juu ya anga la uwanja wa Uhuru, pamoja na vikisoi vya jeshi hilo kupiga mizinga 21.

Mbali ya burudani hizo, sherehe za miaka 61, zilipambwa na vijana wa sarakasi ambao walionyesha sanaa za aina mbali mbali katikati ya kiwanja hicho, huku wanafunzi wa skuli ya kimatifa ya Hazina, wakionyesha ufundi wa sarakasi.

Maadhimisho hayo yalitumbuizwa na ngoma za aina tatu ikitangulia ile ya gonga kutoka Zanzibar, ngoma ya Sangula kutoka Ulanga, Morogoro na ngoma ya Lirandi kutoka Musoma, Mara.

Tanganyika ilijipatia uhuru wake mwaka 1961 kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza, kufuatia harakati za kudai uhuru zilizofanywa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

TUME YA HAKI ZA BINAADAMU YAIZINDUA SERIKALI.

Tume ya Haki za Binaadamu yaizindua serikali


 Yaitaka iwashughulikie wanaopindisha sheria


Na Mwanajuma Abdi
Alhamisi 9 Disemba 2010

TUME ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora imesema wakati umefika kwa Serikali kuchukua hatua kali dhidi yawanaopindisha sheria kwa makusudi, wala rushwa na wavivu wasiowajibika katika kesi za udhalilishaji wanawake na watoto.

Kamishna wa Tume hiyo, Zahor Khamis, alieleza hayo kwenye taarifa aliyoitoa kupitia vyombo vya habari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Haki za Binaadamu duniania, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Kemea, Komesha Ubaguzi'.

Alisema Zanzibar ikiwa inaadhimisha siku hiyo kwa kuweka kipau mbele mambo ya msingi kwa kuishauri Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaopindisha sheria kwa makusudi na wanaokula rushwa katika kuharibu ushahidi wa kesi za udhalilishaji wanawake na watoto.

Alieleza hali ya udhalilishaji wanawake na watoto imekuwa ikiongezeka ndani ya jamii na kuonekana kama ni hali ya kawaida au kufikiwa ufumbuzi kwa njia za mkato ikiwemo kuzisuluhisha kesi hizo.

Aidha aliwatupia lawama Polisi na Hospitali kwa kutoshughulikia matatizo hayo kwa wakati, sambamba na mlalamikiwa kutofikishwa katika vyombo vya sheria.

Alieleza na iwapo mlalamikiwa anapofikishwa katika vyombo vya sheria mahakama huchelewesha kesi, kuharibu ushahidi na kuwepo mazingira ya rushwa.

Kamishna Zahour alifahamisha kuwa, tatizo hilo ni pana, ambapo mbali ya uwajibikaji wa vyombo ya umma pia kumejitokeza kwa tatizo la wananchi kutojua haki zao katika masuala ya udhalilishaji na kutoa wito kwa Taasisi za Serikali na Jumuiya za kiraia kuendelea na juhudi za kuwaelimisha wananchi ili wazijue haki zao.

Kwa upande mwengine alisema wimbi la migogoro ya ardhi nalo limekuwa likiongezeka, ambapo hivi sasa limekuwa ni tatizo la jamii na kushauri kufanyiwa kazi kwa kufanyika utafiti wa kina na hatimae kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

"Tusiridhike kusema kuwa migogoro ya ardhi itatatuliwa na mahakama au kudhani kuwa sheria ya ardhi ni nzuri sana na hivyo migogoro inatokana na ukorofi wa baadhi ya watu, kwa sasa hili ni tatizo la jamii hivyo halina budi kufanyiwa kazi ya utafiti", alifafanua Zahour.

Akigusia maridhiano ya kisiasa, Kamishna huyo alisema hatua iliyofikiwa Zanzibar imesaidia kuweka nchi katika amani na utulivu na kudumisha mshikamano uliondosha siasa za chuki na za kubaguana.

Aliongeza kusema kwamba, hali hiyo haina budi kutunza na kukuzwa ili wananchi wasirudi walikotoka, hivyo vyama vya siasa vinawajibu wa kuwaelimisha wanachama wao katika kuyaenzi maridhiano hayo na kuachana na maneno na mambo ambayo yanaweza kuathiri.

Maadhimisho ya siku ya Haki za Binaadamu Duniani inatokana na madhila na madhara yaliyotokana na vita vikuu vya pili vya Dunia mwaka 1946, sambamba na kukumbushana kutekeleza mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binaadamu, ambapo Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kuridhia mkataba huo.

WENYE VVU SINGIDA WAHAMASISHANA KUACHA UTEGEMEZI.

Wenye VVU Singida wahamasishana kuacha utegemezi



Na Jumbe Ismailly, Singida
Alhamisi 9 Disemba 2010

CHAMA cha watu wanaoishi na virus vya UKIMWI (SIPHA) Mkoani Singida kimewataka wanachama wake kujenga utamaduni wa kutokuwa tegemezi kwa wafadhili kwa kubuni na kuanzisha miradi ya kujiongezea vipato.

Mjumbe wa kamati ya tendaji wa chama hicho, Juliana Samweli, alisema hayo kwenye semina ya siku tano ya kuwajengea uwezo wanachama wa chama hicho, kutambua wajibu wao.

Alisema kwamba idadi kubwa ya wanachama wa SIPHA, bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutokuwa na miradi yenye uhakika inayoweza kukidhi mahitaji yao ya kila siku na hivyo kuwafanya wawe tegemezi.

Alifahamisha kuwa kutokana na hali hiyo kumechangia pia wanachama hao kuanza kujinyanyapaa wenyewe, jambo linalochangia watu wengine pia kuwatenga katika shughuli mbali mbali za kijamii

“Changamoto tunazokumbana nazo katika asasi yetu ni kutokuwa na miradi yenye uhakika ya kuweza kukidhi mahitaji yetu ya kila siku, sisi wenyewe kama wadau tumekuwa na unyanyapaa watu wamekuwa hawatuelewi”, alisema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa SIPHA, Selemani Athumani alisema malengo ya mafunzo hayo kuwa ni kuwajengea uwezo wanachama wake ili waweze kufahamu wajibu wao na wapo katika chama hicho kwa malengo gani.

Mwenyekiti huyo alizitaja changamoto zinazoikabili asasi hiyo kuwa ni pamoja na wanachama kutojua wajibu wao katika shirika, uhaba wa raslimali fedha kutokana na shirika kuwa si la kibiashara.

CHAMA cha watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI (SIPHA) Mkoani Singida kina wanachama 52, kiliomba shilingi milioni 5 kutoka The Foundation for Civil Society kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanachama wake.

KAMATI KUU KUUKATA MZIZI WA FITINA WA UMEYA ZANZIBAR.I

Kamati Kuu kuukata mzizi wa fitna wa Umeya Z'bar


Na Mwantanga Ame
Alhamisi 9 Disemba 2010

HATIMA ya nani atabebeshwa jukumu la kuwania kiti cha Umeya wa mji wa Zanzibar na Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya, itajulikana leo baada ya Kamati Kuu ya CCM kupitisha baraka zake.

Kwa mujibu wa taarifakutoka ndani ya CCM zinaeleza kuwa Kamati hiyo itakuwa na kikao chake leo jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine itayapitia majina ya wanaCCM waliojitokeza kuwania nafasi ya kwa miji mbali mbali Ukiwemo wa Zanzibar.

Kikao cha Kamati Maalum ya Zanzibar, ilikaa wiki iliyopita ambapo ilipitisha majina ya wanaCCM wawili waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kwa Mji wa Zanzibar, huku pia majina ya waliojitokeza kuwania nafasi za Uenyekiti wa Halmshauri za Wilaya.

Majina yaliopitishwa na kikao hicho kuwania Umeya wa Zanzibar ni pamoja na Meya aliyemaliza muda wake, Mahboub Juma Issa ambaye atakabiliwa na kibarua kizito cha kutetea kiti hicho, baada ya kujitokeza kada mwenzake anayekinyatia kiti hicho kutoka katika Jimbo moja.

Mpinzani wa Mahboub ambaye ni Diwani wa Kikwajuni, ni Diwani wa Miembeni Abdurahman Khatib, ambao wote wanatoka jimbo moja la Kikwajuni.

Katibu wa Idara ya Uenezi Siasa na Itikadi Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alithibitisha kuwapo kwa kikao cha Kamati Kuuu leo ambacho kitajadili majina ya wanaCCM hao.

Hata huvyo Vuai alisema taarifa zaidi za kikao hicho anayezifahamu Naibu Katibu Mkuu Visiwani Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz ambaye nae alipozungumza na Zanzibar Leo, alithibitisha kuwapo kwa kikao hicho.

Hata hivyo Ferouz alisema taarifa zaidi za kikao cha leo anazo msemaji wa kikao hicho ambaye ni katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba.

Meya huyo aliyemaliza muda wake anaonekana kuzunguka huku na kule huku taarifa za wapambe zikieleza kuwa yuko katika kampeni kali kwa Wajumbe wa NEC, huku Mgombea mwenzake naye akikanyaga maeneo hayo hayo ya kuomba ridhaa kwa wajumbe hao kupitisha jina lake.

Hapo awali Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharib, kupitia msemaji wake Maulid Issa, kilieleza kuwa kwa upande wa Naibu Meya, nafasi hizo tayari zimepata wagombea watano waliojitokeza.

Majina ambayo yanayosubiri baraka hizo Katibu huyo alisema ni la Diwani wa Wadi ya Mlandege, Khamis Mbarouk Khamis, Mussa Haji Idrisa wa Wadi ya Mwembemakumbi na Shara Ame Ahmeid wa viti Maalum Wanawake.

Hadi sasa ni Chama cha CUF, kimekuwa kimpya huku kikiwa na Madiwani katika Majimbo ya Mjini likiwemo wa Wadi za Jimbo la Mji Mkongwe, ikiwemo ya mchangani na Mtoni,

Aidha, uchaguzi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi, nao umeshafanyika na aliyepishwa nafas ya Mwenyekiti ni Masoud Abrahman alieshika nafasi ya kwanza na kumshinda Shaka Hamdu amekuwa wa pilina Omar Ali Khamis ni watatu.

Nafasi za Umakamu, watasubiri matokeo ya vikao hivyo ni pamoja na Amina Ali Mohammed, Aziza Abdalla na Msimu Seif.

DEREVA KIZIMBANI KWA KUTOFUNGA MKANDA

Dereva kizimbani kwa kutofunga ukanda




Na Khamis Amani
Alhamisi 9 Disemba 2010

MKAAZI mmoja wa Amani wilaya ya Mjini Unguja, ambaye ni dereva wa gari ya abiria iyendayo njia namba 501 yenye nambari za usajili Z 584 CG, amefikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kwa kosa la kushindwa kufunga ukanda wa usalama.

Mshitakiwa huyo Yussuf Mohammed Juma (27), amekubali kosa hilo mahakamani hapo, na kuhukumiwa kulipa faini ya shilingi 20,000 au kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi mitatu.

Adhabu hiyo dhidi yake imetolewa na hakimu Janet Nora Sekihola, mara baada ya kukubali kosa hilo alilosomewa na Mwendesha Mashitaka Khamis Jaffar Mfaume, Mwanasheria wa serikali kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakati Mwanasheria huyo wa serikali kuomba itolewe adhabu kwa mujibu wa sheria kwa madai hawana kumbukumbu za makosa ya zamani dhidi yake, kwa upande wake mshitakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo imsamehe.

Hakimu Janet Sekihola baada ya kupitia hoja za pande mbili hizo, alimtaka mshitakiwa huyo kulipa faini ya shilingi 20,000 au kutumikia Chuo hicho kwa muda wa miezi mitatu, faini ambayo aliilipa mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa huyo alidaiwa kushindwa kufunga ukanda wa usalama, wakati akiendesha gari hiyo alipokuwa akitokea upande wa Kwabiziredi kuelekea upande wa Michenzani.

Kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu cha 130 (2) (4) cha sheria namba 7/2003 sheria za Zanzibar, lilidaiwa kutokea Kariakoo wilaya ya Mjini Unguja, saa 2:45 za asubuhi ya Disemba 5 mwaka huu.

DEREVA ALIPA FAINI KUKWEPA CHUO CHA MAFUNZO

Dereva alipa faini kukwepa Chuo cha Mafunzo



Na Khamis Amani
Alhamisi 9 Disemba 2010


DEREVA wa gari ya abiria yenye nambari za usajili Z 745 AY, amenusurika kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita, baada ya kulipa faini ya shilingi 70,000.

Faini hiyo ameilipa baada ya kutiwa hatiani na mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, dhidi ya kesi ya kuendesha gari ya abiria ikiwa leseni ya udereva haimruhusu.

Abdallah Kweli Juma (26) mkaazi wa Amani wilaya ya Mjini Unguja, amepatikana na hatia hiyo, baada ya kukubali kosa hilo mbele ya hakimu Janet Nora Sekihola alikofikishwa kujibu shitaka hilo.

Mara baada ya kukubali kosa hilo lililowasilishwa na Mwanasheria wa serikali Khamis Jaffar Mfaume, kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), mahakama hiyo ilimtaka kulipa faini ya shilingi 70,000 au kutumikia Chuo hicho cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, huku mshitakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo imsamehe, upande wa mashitaka kwa upande wake uliomba itolewe adhabu kwa mujibu wa maelekezo na kudai kuwa hawana kumbukumbu za makosa ya zamani juu yake.

Awali akiwa mahakamani hapo ilidaiwa kuwa, kinyume na kifungu cha 102 (a) (b) cha sheria namba 7/2003 sheria za Zanzibar, mshitakiwa huyo alipatikana akiendesha gari ya abiria iendayo njia namba 505 ikiwa leseni yake ya udereva haimruhusu.

Mahakama ilifahamishwa kuwa, kisheria alitakiwa kuwa na leseni ya class D, badala ya class DI aliyokuwa akiitumia shitaka ambalo alilikubali mahakamani hapo.

KETE MBILI ZA DAWA ZA KULEVYA ZAMFIKISHA MAHAKAMANI.

Kete mbili za dawa za kulevya zamfikisha mahakamani



Na Said Abdu-rahman, Pemba
Alhamisi 9 Disemba 2010

MAHAKAMA ya Wilaya Wete imempeleka rumande wiki mbili kijana mmoja mkaazi wa Chasasa anayekabiliwa na mashitaka ya kupatikana na dawa za kulevya kinyume na sheria.

Mshitakiwa huyo Juma Khamis Juma (19), ambae alifikishwa Mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa shitaka lake hilo.

Akiwa Mahakamani hapo mbele ya Hakimu Nyange Makame, Mwendesha Mashitaka kutoka Jeshi la Polisi Msaidizi Mkaguzi wa Polisi, Massoud alimsomea mshitakiwa hiyo kosa linalomkabili.

Alidai kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 16(1)(a) sheria No, 9 ya mwaka 2009, sheria ya Uingizaji na Matumizi ya Dawa haramu, sheria za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa hati ya maelezo ya mashitaka iliyowasilishwa Mahakamani hapo na kusomwa na Mwendesha Mashitaka huyo, ilidai kuwa shitakiwa huyo alipatikana na dawa za kulevya aina ya heroine kete mbili ndani ya kibiriti zenye uzito wa gramu.

Alifahamisha kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 6 mwaka huu majira ya saa 5:00 za asubuhi huko Bopwe Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu lolote Mahakamani hapo kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo.

Baada ya Maelezo hayo Mwendesha mashitaka Msaidizi Mkaguzi wa Polisi, alimuomba Hakimu Nyange kuliahirisha shauri hilo na kulipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusomwa Mahakama inayohusika.

Hakimu Nyange alikubaliana na ombi la Mwendesha Mashitaka na hivyo kuiahirisha kesi hiyo hadi Disemba 20 mwaka huu ambapo kesi hiyo itasikilizwa katika Mahakama ya Mkoa .

MSHITAKIWA WIZI WA BASKELI ANYIMWA DHAMANA.

Mshitakiwa wizi baiskeli anyimwa dhamana



Na Khamis Amani
Jumatano 8 Disemba 2010

MAHAKAMA ya Mwanzo Mwanakwerekwe, imemnyima dhamana na kumpeleka rumande kwa muda wa siku 14, kijana mmoja anayeshitakiwa kwa wizi wa baiskeli yenye makisio ya thamani ya shilingi 65,000.

Mahakama hiyo iliyo chini ya hakimu Ndame Ali Mkanga, imechukuwa uwamuzi huo baada ya mshitakiwa huyo kushindwa kuwasilisha wadhamini mahakamani hapo.

Mtuhumiwa huyo ni Hassan Bakari Mohammed (22) mkaazi wa Nyerere wilaya ya Mjini Unguja, ambaye pamoja na kushindwa kuwasilisha wadhamini hao, lakini aliiomba mahakama hiyo impatie dhamana.

Kabla ya maamuzi hayo ya mahakama, Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Koplo wa Polisi Hassan Mussa Mshamba, alimsomea mshitakiwa huyo shitaka hilo la wizi chini ya kifungu cha 267 (1) na 274 (1) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, ambalo alilikana.

Katika madai yake, Mwendesha Mashitaka huyo alidai kuwa Disemba Mosi mwaka huu, majira ya saa 8:30 za mchana huko Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi Unguja, aliiba baiskeli moja aina ya Sport Sehewa.

Alifahamisha kuwa, baiskeli hiyo yenye rangi nyeusi ina thamani ya shilingi 65,000 kwa kukisia, mali ya Suleiman Mohammed Salum.

Pamoja na kukana shitaka hilo, upande wa mashitaka ulidai upo tayari kuthibitisha kosa hilo, kwa madai upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba ipangiwe tarehe ya kusikilizwa pamoja na kutolewa kwa hati za wito kwa mashahidi.

Hakimu Ndame Ali Mkanga, alikubaliana na hoja hizo aliliahirisha shauri hilo hadi Disemba 22 mwaka huu kwa kusikilizwa, na kuuamuru upande huo wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Tuesday 7 December 2010

DK. SHEIN SERIKALI KUIIMARISHA SEKTA YA AFYA

Dk. Shein: Serikali kuiimarisha sekta ya afya



Rajab Mkasaba


Jumanne 7 Disemba 2010


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imepania kuimarisha sekta ya afya visiwani hapa.

Dk. Shein alisema mbali ya mipango iliyopo pia Serikali imedhamiria kuipa hdahi kamili hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya Rufaa.

Rais Shein, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na viongozi pamoja na watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ikiwa ni hatua yake ya kuzitembelea Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kikao hicho kilichofanyika Ikulu mjini Zanzibar, kilihudhuriwa na Makamo wa Kwanza na Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.

Aidha Rais Shein, alisema kuwa pia Serikali itazipandisha daraja baadhi ya hospitali za Wilaya na Mikoa.

Rais Shein, alisema Serikali yake itahakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto zote zinazoikabili sekta hiyo ikiwa ni pamoja na maslahi kwa wafanyakazi wake, vifaa na majengo ya hospitali na taasisi za Wizara hiyo.

Aidha, Dk. Shein aliwaeleza watendaji hao kuwa mashirikiano baina yao yanahitajika ili ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi uweze kupatikana.

Nao viongozi na watendaji wa Wizara ya Afya walimueleza mafanikio yaliofikiwa katika sekta hiyo pamoja na changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kueleza mikakati waliyoiweka katika kupambana na changamoto hizo.

Pamoja na hayo, watendaji hao wamemuahidi Dk. Shein kuwa wataendeleza mashirikiano ya pamoja katika kuimarisha sekta hiyo ya afya.

SHEKH SORAGA ATAKA WAISLAMU WAWAJIBIKE.

Sheikh Soraga ataka waislamu wawajibike



Na Mwantanga Ame


Jumanne 7 Disemba 2010

WAISLAMU na wametakiwa kusherehekea mwaka mpya wa kiislamu huku wakitambua wanajukumu la kutoa mchango wa kuwajibika katika serikali mpya ya Zanzibar, ili kuifanya kuwa ni yenye neema katika mwaka ujao.

Katibu wa Afisi wa Mufti ya Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga aliyasema hayo jana katika salamu zake kwa waumini wa dini ya kiislamu na Wazanzibari wote katika kuadhimisha mwaka mpya wa Kiislamu.

Mwaka mpya wa kiislamu kwa mujibu wa kalenda ya kiislamu unatarajiwa kuanza leo ambapo ni mwaka 1432 (HIJRIA).

Katibu huyo alisema kutokana na Zanzibar kuwa ipo katika hali ya amani na utulivu baada ya kumalizika kwa zoezi la uchaguzi Mkuu, ni vyema waumini wa dini ya kislamu na wakaelewa kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kushiriki kufanya kazi kwa bidii.

Katibu huyo alisema kuwa kila Mzanzibari aliyepata nafasi ya kuwaongoza wenzewe ahakikishe kuwa anatumiwa nafasi aliyopewa kwa uadilifu na kutimiza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi.

Alisema suala la kuipembejea kazi yake, kuwa muaminifu na kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi ni moja ya mambo ya msingi yanayohimizwa katika dini na ni haramu kwa mtu kupokea mshahara ambao hakuufanyia kazi.

Sheikh Soraga alisema jambo la msingi ambalo waislamu wanatakiwa kuzingatia ni kuhakikisha mwaka mpya ulioingia unawajengea mapenzi na mshikamano na viongozi waliopo madarakani bila ya kujali itikadi zao za kisiasa.

Aidha katibu huyo aliiomba jamii kuimarisha maadili kwa vijana wa Zanzibar kwa maslahi ya nchi na vizazi vijavyo kwani ndio wanaotegemewa kulijenga taifa hili hapo baadae.

Alisema Zanzibar yenye mabadiliko mapya ya uongozi itawezekana kuwa bora zaidi iwapo watu wote watakubali kushirikiana katika kuwaongoza vijana katika maadili yaliyo sahihi.

"Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu Subhana Wataala, aibariki nchi yetu na awawafikishe viongozi wetu hasa Rais wetu na Makamu wake wa rais, Mawaziri, Manaibu na wote walioteuliwa katika nchi yetu wawe na ikhlas na uadilifu", alisema Katibu huyo.

Aidha alisema huu ni wakati muafaka wa kutubia dhambi kwa kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kuomba maghafira na kumtaka msamaha.

Waislamu wa Zanzibar wataungana na waislamu kote duniani ambao wanaadhimisha kuingia kwa mwaka mpya wa kiislamu ambapo Zanzibar wanakusudia kufanya maandamano ya amani Kumshukuru Mwenyezi Mungu.

MTAMBO WA KISASA WAKUWASHIA TAA UWANJA WA NDEGE WAFUNGWA.

Mtambo wa kisasa wakuwashia taa uwanja wa ndege wafungwa


Na Mwanajuma Abdi
Jumanne 7 Disemba 2010

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imefunga mtambo wa kisasa uitwao SCADA wa kuwashia taa unaotumia mtandao wa komputa katika barabara ya kurukia na kutulia ndege ya kiwanja cha Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Idara ya Anga, Malik Mohamed Hanif, alisema mtambo wa SCADA ni wa kwanza kufungwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Alisema mtambo wa SCADA unatumiwa katika kuwasha taa katika barabara ya kurukia ndege na kutulia kwa nyakati za usiku na mchama ili kusaidia kuongoza vizuri ndege wakati inapofika katika Uwanja huo ikiwa angani.

Alieleza mtambo huo unaendeshwa kwa mtandao wa komputa unasaidia kurahisisha kazi iwapo taa zikiwa haziwaki katika eneo lolote linalozunguka katika barabara hiyo.

Aidha alisema awali uwanja huo ulikuwa unatumia mtambo wa MIMIC ambao ulikuwa unatumia 'swich' za kuwacha kwa kawaida, ambapo hata kama taa zitakuwa zinamatatizo sio rahisi kuonyesha kama hazikwenda kuangaliwa.

Alifahamisha kuwa, lakini tokea kufungwa kwa mtambo wa SCADA kila kitu kinajionesha katika kompyuta iwapo kutatokea hitalafu au kutowaka kwa taa katika kiwanja hicho.

Mkurugenzi huyo, alisema Uwanja huo unaendelea kuimarishwa baada ya kukamilika matengenezo upanuzi wa njia ya kurukia na kutulia ndege, ili kwenda sambamba na hadhi ya kimataifa na kuweza kuyavutia mashirika mbali mbali ya kimataifa.

Alifahamisha kuwa, hivi sasa ujenzi wa ukuta wenye urefu wa kilomita 12 unandelea, ambao utatumia jumla ya shilingi bilioni tano hadi kukamilika kwake.

Kuimarishwa kwa Uwanja huo utasaidia kuongeza mapato ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia safari za anga kwa kuongeza idadi ya ndege na watalii wengi kuja kutembelea nchini na wenyeji nao kutumia huduma hizo zilizokuwa bora kwa ajili ya kusafiri na kufanya biashara.

DK. BILAL AITOA HOFU MAHAKAMA MATUMIZI IT

Dk. Bilal aitoa hofu Mahakama matumizi IT



Said Ameir Dar es Salaam
Jumanne 7 Disemba 2010

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal amesema kuwa Idara ya Mahakama inakabiliwa na changamoto ya kuongeza na kuimarisha matumizi ya tekinolojia ya habari.

Alisema katika kipindi hicho ambacho matumizi ya tekinolojia ya habari yameingia katika kila sehemu ya maisha ya kikazi na binafsi, Idara hiyo nayo inapaswa kujipanga ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yake na kufikia malengo.

Makamu wa Rais, alisema hayo jana jijini Dar es Saalam, wakati alipokuwa akizindua rasmi Mfumo wa kurekodi mashauri Mahakamani kwa njia ya Kompyuta pamoja na kuzindua tovuti ya mahakama.

Dk. Bilal alisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya habari katika shughuli za mahakama na kueleza kuwa matumizi hayo hurahisisha uendeshaji wa kesi.

Dk. Bilal aliutaka uongozi wa Idara ya mahakama nchini, kufanya jitihada za kusambaza matumizi hayo ya tekinolojia ya habari katika Ofisi za mahakama nchini kote badala ya kuishia katika Ofisi za Mahakama Kuu Dar es salaam na vitengo vyake.

Mradi wa kuweka mfumo wa kurekodi mashauri mahakamani kwa kompyuta pamoja na uanzishwaji wa tovuti ya mahakama unafadhiliwa na Taasisi ya uendelezaji wa mazingira mazuri kwa uwekezaji Afrika-Investment Climate Facility for Africa-ICF.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya tovuti aliyoizindua Makamu wa Rais, alisema itakuwa vyema kuwa Idara ya Mahakama itafikiria kuondoa tovuti hiyo kutoka kuwa sehemu ya kupata habari(informative website) hadi kuwa tovuti ya upashaji habari (interactive website) ambapo wadau watapata fursa ya kuwasiliana na mahakama bila ya kuathiri Uhuru wa chombo(judiciary independence).

Kwa upande wake Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, alisema mbali ya kueleza furaha yake ya kuona kuwa hatimae mradi huo umeanza, alieleza changamoto mbali mbali zinazoukabili madi huo

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na namna ya kuwafanya majaji wauamini mfumo huo na kuukubali,kusambaza mfumo huo katika Ofisi za mahakama nyingine kote nchini, kuandaa kada mpya ya watumishi mahiri katika kurekodi mashauri na utoaji habari za mahakama.

Changamoto nyingine ni Ofisi za kuwekea miundombinu ya mfumo huo ambapo alibainisha kuwa Ofisi nyingi za mahakama hazikujengwa kurahisisha uwekaji wa miundombinu ya mfumo wa tekinolojia ya habari.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Katiba na Sheria Celina Kombani, Jaji Kiongozi Fakih Jundu, majaji wa mahakama ya Rufaa na wa Mahakama Kuu, Msajili wa Mahakama ya Rufaa Francis Mutungi,Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Oliver Mhaiki na watumishi wengine wa mahakama kuu, Mtendaji Mkuu wa ICF Bwana Omari Issa.

NEC ZANZIBAR YAJADILI WANAOWANIA UMEYA

NEC Zanzibar yajadili wanaowania Umeya



Na Mwandishi wetu
Jumanne 7, Disemba 2010
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Amani Abeid Karume jana alikiongoza kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar, kilichofanyika afisi kuu Kisiwandui.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, kikao hicho pamoja na mambo mengine kilipokea na kujadili majina ya wana CCM waliojitokeza kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Meya wa Manispaa ya Zanzibar kwa mwaka 2010-2015.

Katika kinyang’anyiro hicho, ni wanachama wawili tu ndio waliojitokeza kuomba kuwania nafasi hiyo, ambao ni Mahbubu Juma Issa na Khatib Abdulrahman Khatib.

Kikao hicho kimetoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya CCM juu ya wana CCM hao waliojitokeza kugombra nafasi hiyo kwa hatua zinazoendelea.

Monday 6 December 2010

JENGO LA UWANJA WA NDEGE KUAZA JANUARI.

Jengo la abiria uwanja wa ndege kuanza Januari


Na Mwanajuma Abdi


Jumatatu 6 Disemba 2010


JENGO la kisasa la abiria katika Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, utaanza Januari mwakani ambao utagharimu dola za Marekani milioni 70.4 hadi kukamilika kwake.

Mkurugenzi wa Anga, Malik Mohamed Hanif, alisema hayo alipokuwa akizungumza na gazeti hili, mjini hapa amesema ujenzi huo utaanza mapema mwezi ujao na utachukuwa miaka mitatu hadi kukamilika kwake, ambao utagharimu Dola za Marekani milioni 70.4.

Alisema jengo hilo litajengwa na kampuni ya Beijing Enginering Construction Group (BECG) ya China ambayo imeshinda zabuni ya ujenzi huo.

Alieleza hatua za awali za matayarisho zimeshafanyika za kupima udongo na hivi sasa kazi inayoendelea ni kuingiza vifaa vya ujenzi nchini ili kazi hiyo iweze kuanza mwezi ujao.

Aidha alifahamisha kuwa, ujenzi huo pia utahusisha barabara katika eneo la jengo hilo sambamba na kuweka maeneo maalum ya maegesho ya vyombo vya moto, ili kuweka haiba nzuri ya muonekano wake.

Ujenzi wa jengo jipya la kisasa la abiria linajengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar baada ya kupata fedha za mkopo nafuu kutoka China.

Hata hivyo kujengwa kwa jengo hilo litasaidia kuondoshea kero abiria wanaosafiri na wananchi mbali mbali wanakwenda kuwapokea wageni wao au kuwasindikiza katika uwanja huo.

UJENZI UKUTA WA UWANJA WA NDEGE WAANZA.

Ujenzi ukuta wa uwanja wa ndege waanza



Na Eva Msafiri, TSJ


Jumatatu 6 Disemba 2010

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeanza ujenzi wa ukuta utaozunguka Uwanja wa Kimataifa Abeid Amani Karume wenye urefu wa kilomita 12.

Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa Idara ya Anga, Malik Mohamed Hanif, alisema ujenzi huo unafanyika chini ya Kampuni ya Sagea Satom ya Ufaransa, ambayo ndio iliyohusika katika upanuzi wa Njia ya kurukia ndege na kutulia hivi karibuni, ambapo tayari kazi hiyo imekamilika na kuruhusu ndege kubwa kutua nchini.

Alisema ujenzi wa ukuta utahusisha kilomita 10 utakuwa kwa kiwango cha zega na kilomita mbili utawekwa waya (senyenge) ili kuruhusu kuonekana vizuri kwa kiwanja hicho.

Alifahamisha kuwa, ujenzi huo unafadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni tano na kazi ya ujenzi wa zege imeshaanza na kufikia kilomita tatu katika maeneo ya Mombasa na Kisauni.

Aidha alisema maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa ya upanuzi wa njia ya kurukia ndege na kutulia, Zanzibar imepata sifa kubwa kutoka kwa kampuni mbali mbali zinazotoa usafiri ndani na nje ya nchi.

Malik alieleza upanuzi wa njia ya kurukia ndege na kutilia imefikia kwa urefu kilomita 3022 kutoka kilomita 2462 za zamani na kufikia upana wa kilomita 45 kwa sasa, jambo ambalo limeongeza uwanja huo kuwa na hadhi ya kimataifa.

Hata hivyo, alisema sambamba na upanuzi huo lakini barabara yake (njia ya kurukia ndege na kutulia), iko imara zaidi katika viwango vya kimataifa hadi kufikia PCN 61, ambayo inauwezo wa kuhimili vishindo vya ndege za aina mbali mbali.

Mkurugenzi huyo, alisema hivi sasa kuna maombi ya kampuni tatu za mashirika ya ndege, ambazo zimepeleka maombi ya kuja kuangalia uwanja huo ili kuweza kuleta ndege zao Zanzibar, ambapo miongoni mwa kampuni hizo ni Shirika la Oman Air na Kampuni Emirate.

UN YAOMBWA KUENDELEA KUISAIDIA ZANZIBAR,

UN Yaombwa kuendelea kuisaidia Zanzibar



Na Abdi Shamnah


Jumatatu 6 Disemba 2010

MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ameuomba Umoija wa Mataifa kuendelea kutoa misaada yake kwa Zanzibar ili iweze kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Maalim Seif alitoa ombi hilo jana ofisini kwake Migombani wakati alipozungumza na Mwakilishi mkaazi wa Umoja wa Mataifa aliopo Zanzibar,Kana Sorro.

Amesema Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Global Funds limekuwa likitoa misaada mbali mbali kwa Zanzibar, ikiwemo ya kifedha kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi pamoja na Malaria.

Hata hivyo, alisema 2007 katika awamu ya kwanza ya misaada hiyo ya kipindi cha miaka miwili, Shirika hilo lilisititisha misaada yake kwa Zanzibar, na badala yake kutoa Dola 135,000 ikiwa ni msaada wa mwaka mmoja pekee (2007/08).

Kufuatia hali hiyo Maalim Seif alimuomba Mwakilishi huyo kuangalia uwezekano wa kuwepo misaada endelevu kwa Zanzibar, kwa kuzingatia kuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti ongezeko la ugonjwa huo kwa wastani wa asilimia 0.6.

Alimweleza Mwakilishi huyo kuwa uwepo wa makundi hatarishi yanayoishirikisha zaidi nguvu kazi ya Taifa, kunatishia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Alisema Serikali kupitia ofisi yake imejizatiti kiikamilifu kukabiliana na maambukizi na ugonjwa wa ukimwi sambamba na matumizi ya madawa ya kulevya.

Aidha Maalim Seif alimuomba Mwakilishi huyo kuangalia uwezekano wa kusaidia Zanzibar katika njia za kukabiliana na athari za kiimazingira zinazozikabili fukwe hapa nchini.

Alisema hali ya kimazingira katika fukwe, hususan zile ziliopo katika ukanda wa Kusini Mashariki ya Bahari ya Hindi ni mbaya, ambapo maji ya chumvi yamekuwa yakimega ardhi ya kisiwa hiki kila kukicha.

Katika hatua nyuingine Maalim Seif aliiomba UN kuangalia njia za kuweza kuisaidia Zanzibar kuimarisha Daftari lake kiutawala, akianisha kuwepo kwa kasoro kubwa katika daftari hilo, ambapo baadhi ya Wazanzibari wenye sifa wamekosa kuandikishwa, hali iliopelekea kukosa kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Nae Mwakilishi wa UN nchini, Kana Sorro, alimhakikishia Makamu wa kwanza wa Rais kuwa mapendekezo hayo ameyachukua kwa ajili ya kuyafanyia kazi.

NCHI ZINAZOENDELEA ZIZUIE UHARIBIFU WA MAZINGIRA.

Nchi zinazoendelea zizuie uharibu wa mazingira


Na Khatib Juma Mjaja, Denmark


Jumatatu 6 Disemba 2010


NCHI zinazoendelea zimetakiwa kutilia maanani utekelezaji wa mikakati ya kuzuia uharibifu wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya kupunguza athari za kimazingira zinazotokea.

Akizungumza na ujumbe wa wafanyakazi wa taasisi za nchi mbali mbali,huko Makao Makuu ya Taasisi ya Mazingira kwa nchi za Ulaya, mjini Copenhagen Denmark,Meneja wa miradi ya mabadiliko ya tabia nchi kwa nchi za Ulaya na mtaalamu wa utafiti wa mazingira Dk. Hans Martin Fussel, alisema athari za kimazingira zinazojitokeza zitaongezeka endapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa.

Alisema miongoni mwa mikakati iliyowekwa na mkutano wa kujadili mabadiliko ya tabia nchi, jijini Copenhagen mwaka 2009, ni pamoja na nchi za Ulaya kupunguza matumizi ya gesi za kemikali zinazoathiri hali ya hewa kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020.

Aidha katika mkutano huo wa mwaka jana nchi zinazoendelea zimetakiwa kupunguza uharibifu huo kwa asilimia kati ya 20 hadi 30 ifikapo mwaka 2015.

Alisema hali ya sasa ya uharibifu wa mazingira ya anga imefikia nyuzi joto 2 huku kiwango cha kawaida kinachohitajika kuwa na uwiano wa hali ya hewa ni asilimia 0.8.

Alisema kiwango hicho cha asilimia 2 kilichopo sasa ni miongoni mwa sababu zinazopelekea majanga ya kimazingira yanayotokea kama vile, mafuriko kutokana na kuyeyuka kwa theluji milimani, vimbunga na mtandao wa barafu katika visiwa vya kijani ” Green land”.

Aidha Dk. Fussel alisema ongezeko la joto, linalosababishwa na uharibifu wa mazingira,linasababisha uzalishaji mdogo wa vyakula kwenye nchi nyingi za dunia ya tatu kukumbwa na majanga ya njaa mara kwa mara.

Dk. Fussel, alisema suala la uharibifu wa mazingira lazima lichukuliwe kwa tahadhari ya kipekee la si hivyo athari zake zitaendelea kuiathiri dunia.

WAISLAMU KUADHIMISHA MWAKA WAO MPYA KWA MAANDAMANO

Waislamu kuadhimisha mwaka wao mpya kwa maandamano



Na Issa Mohammed


Jumatatu 6 Disemba 2010

WAUMINI wa dini ya kiislamu wa Zanzibar wanatarajia kufanya matembezi maalum ya kusherehekea kuingia kwa mwaka mpya wa kiislamu 1432, unaotarajiwa kuanza Jumanne ijayo.

Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, alisema waislamu hao wakiwemo wanaume na wanawake watafanya matembezi hayo katika barabara mbali mbali za mjini Zanzibar.

Akizungumza na waislamu katika msikiti Mkuu wa Mushawwar uliopo Mwembeshauri, Soraga alisema matembezi hayo yataanza katika viwanja vya Kisonge Michenzani, yatapita katika barabara mbali mbali za mji wa Zanzibar.

Sheikh Soraga alifahamisha kuwa matembezi hayo yatakayokuwa ya aina yake kufanywa visiwani Zanzibar na kwamba yatapambwa kwa kasda kutoka vyuo mbali mbali vya kiislamu viliopo mjini hapa.

Alisema matembezi hayo yatafuatiwa na mhadhara utakaofanywa katika viwanja hivyo ukiwa na lengo la kuwakumbusha waislamu mambo mbali mbali wanayopaswa kuyafanya wakiwa hapa duniani.

Katibu wa Mufti aliwataka waumini wa dini ya kiislamu kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha matembezi hayo muhimu hasa katika wakati huu ambao Zanzibar inakusudia kurejesha hadhi yake ya kuwa kitovu cha Uislamu katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na kati.

Hata hivyo sheikh Soraga hakusema mgeni rasmi katika matembezi hayo atakuwa ni kiongozi gani.

WAZIRI ABOUD ASISITIZA NIDHAMU, UPENDO KWA WAFANYAKAZI.

Waziri Aboud asisitiza nidhamu, upendo kwa wafanyakazi



Na Luluwa Salum, TSJ


Jumatatu 6 Disemba 2010

NIDHAMU, upendo na ushirikiano ndio muhimili ndivyo vitakavyowezesha kupatikana kwa ufanisi kwenye sehemu za kazi.

Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, alisema hayo wakati alipotembelea Afisi za Wizara hiyo zilizopo Pemba na kuzungumza kwa mara ya kwanza na wafanyakazi wa Wizara hiyo tangu kushika wadhifa huo.

Aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa jukumu kubwa la Wizara ya Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, ni kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kuwatatulia shida zao zinazowakabili.

Alisema watakapofanya kazi zao kwa uadilifu kutawafanya wananchi wawe na imani na serikali yao na kuwataka kuwa makini katika matumizi ya fedha za umma, pamoja na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Aidha aliwataka watendaji wa juu kutokuwa na upendeleo katika suala la ajira pamoja na nafasi za masomo zinapopatikana kwani wafanyakazi wote wana haki sawa, na kusema kufanya hivyo kutawajengea mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Kwa wake Afisa Mdhamini wa Wizara hio Pemba, Amran Massoud, alimpongeza Waziri Aboud kwa kuona umuhimu wa kukutana nao na kuahidi kushirikiana nae ,na kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata sheria.

WANANCHI WATAKA MFANO WA ZANZIBAR EXPLORE UIGWE.

Wananchi wataka mfano wa Zanzibar Explore uigwe



Na Aboud Mahmoud


Jumatatu 6 Disemba 2010

KAMPUNI mbali mbali nchini zimetakiwa kuiga mfano wa Kampuni ya Zanzibar Explore kutokana na jitihada zake inazozichukua katika kuwaunganisha wanajamii na kutoa misada mbali mbali.

Ushauri huo umetolewa na wananchi mbali mbali wakati walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kumalizika kwa kongamano la siku ya UKIMWI duniani lililofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Serena Inn.

Wananchi hao walisema kuwa kampuni hiyo inayoongozwa na Maryam Olsen imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia nyanja mbali mbali kwa wanajamii wa Kizanzibari.

"Naipongeza sana kampuni ya Zanzibar Explore imekuwa mstari wa mbele kusaidia huduma mbali mbali za kijamii,hii ni dalili nzuri kwa sisi wananchi wa Zanzibar,"alisema Suleiman Mauly kutoka Drug Free Zanzibar

Aidha wananchi hao walioshiriki katika kongamano hilo walisema kuwa kuna haja kubwa ya kampuni mbali mbali binafsi kufuata nyayo za kampuni hiyo kuwa kuwa bega kwa bega na jamii.

"Ningependa kutoa ushauri wangu kwa kampuni nyengine kujitokeza na kuiga mfano wa Zanzibar Explore kutokana na kuisaidia jamii katika mambo mbali mbali,"alisema Fatma Thomas kutoka ZAPHA+ .

Nae Salim Ahmed alisema kuwa Zanzibar Explore imekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada wa huduma za kijamii ikiwemo katika watu wanaoumwa na ugonjwa wa akili,wanaoishi na virusi vya ukimwi pamoja na watu wanaoacha kutumia madawa ya kulevya.

Zanzibar Explore ni moja ya taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ambayo imejikita zaidi katika utoaji wa huduma za jamii katika nyanja mbali mbali katika visiwa vua Unguja.

SHEKH SHARIF ATAKA WAKATWE WANAOJINUFAISHA KWA JINA LAKE.

Sheikh Sharif ataka wakamatwe wanaojinufaisha kwa jina lake


Na Kunze Mswanyama, Dar


Jumatatu 6 Disemba 2010

WAKAAZI wa Jiji la Dar es Salaam, wameaswa kutowasikiliza watu wanatumia jina na nembo ya Sheikh Sharif Zaharani Foundation, ili kuwahadaa wananchi.

Sheikh Sharrif alitoa tahadhari hiyo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari huko afisi kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema tayari kuna taarifa za kubakwa wasichana wawili na mtu ambaye alitumia jina na nembo yake Sheikh Sharrif Foundation na sambamba na kuwepo kwa taarifa za utapeli.

Alisema wapo watu wanaotumia nembo na jina lake kwa maslahi binafsi wakidai kuwa nao wanaouwezo wa kuwahudumia watu kiroho.

Sheikh huyo ambaye ana umri wa miaka tisa, alisema watu hao pia wanajitambulisha kuwa wao ni masharifu kumbe siyo bali ni matapeli wa mjini wanaotumia uongo wa dini ili kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Sheikh Sharrif aliwataka wananchi kutosita kuwachukulia hatua za kisheria matepeli hao kwa kuwafikisha katika vituo vya polisi kwani wapo kwa ajili ya kuwaibia watu.

“Wale wote waliokwisha fanyiwa matendo hayo watoe taarifa katika kituo chochote cha polisi kilicho karibu nao, ili kurahisisha kukamatwa kwao na sheria kuchukua mkondo wake”, alisema.

Wakati huo huo, serikali ipongezwa kwa hatua yake ya kuruhusu matumizi na usajili wa waganga wa tiba mbadala baada ya waganga hao kufungiwa kufuatia wimbi la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Akitia pongezi hizo, mgunduzi wa dawa ya figo, Danny Kyauka, alisema wakati wote walipokuwa wamefungiwa leseni zao, walikuwa wakitoa huduma kwa kujifichaficha.

Dokta Danny, alisema kuruhusiwa kwa leseni zao kutawafanya kuendelea kutoa huduma hizo bila ya kificho, sambamba na kuwapatia huma za matibau wnaanchi wenye watatizo mbali mbali.

MAABARA YA JAMII KUPUNGUZA VIFO VYA WATOTO.

Maabara ya jamii kupunguza vifo vya watoto


Na Masanja Mabula, Pemba


Jumatatu 6Disemba 2010

MRADI wenye lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga walio na umri wa siku moja hadi siku 28 unatarajiwa kuendeshwa na maabara ya Afya ya Jamii Kisiwani Pemba ikishirikiana na Chuo Kukuu cha John Hopkins cha Marekani.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika Wesha ukumbi wa Pemba Bahari, na kuwajumuisha viongozi wa maabara hiyo, viongozi wa Chuo Cha JHU na wataalamu wengine kutoka Zambia, Mkurungenzi wa Maabara ya Afya ya Jamii kisiwani Pemba Dk. Said Mohammed Ali alisema mradi huo utakuwa ni muda wa miaka 5.

Alisema katika utekelezaji wa mradi huo watendaji wa maabara ya afya ya jamii watakuwa wanafuatilia akinamama wanaobeba mimba hadi kufikia siku 28 tokea kujifungua kwa kuwapatia dawa kwa ajili ya kuwapaka watoto wao katika sehemu ya kitovu.

Alisema chini ya mradi huo ambao utawashirikisha wakunga wa jadi, watawapatia vitendea kazi ikiwemo dawa na simu za mikononi ambapo pia watatakiwa kuwahamiza mama wajawazito kujifungulia katika haspitali na vituo vya afya.

Mkurugenzi huyo alisema mama akijifungua katika hospitali au kituo cha afya, ataweza kupatiwa huduma za kitaalamu pale yatakapojitokeza.

Dk.Said alisema katika utafiti wa awali uliofanywa hivi karibuni na maabara hiyo, umebaini kuwepo na mwitikio mzuri kutoka kwa jamii na kwamba ana imani kuwa mradi huo utapata mafanikio makumbwa.

Mbali na kufanyika hapa kisiwani Pemba, mradi huo ambaao umefadhiliwa na kituo cha Afya na Maendeleo cha Boston University cha Marekani pia unatarajia kufanyika katika nchi ya Zambia

Katika mkutano huo pia alihudhuria Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mwamboya pamoja na Mkurungezi wa Wizara hiyo Dk. Malick Juma