Na Mwantanga Ame
IKIWA zimebakia siku chache kabla ya kuanza zoezi la uchukuaji wa fomu kuwania nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani ndani Chama cha Mapinduzi (CCM), Mawaziri kadhaa wametangaza nia ya kujitosa tena majimboni.
Vigogo hao, wameelezea nia zao katika mahojiano na gazeti hili kwa wakati tafauti na kuthibitisha kuwa watajitosa kwa mara ya kwanza kuwania majimboni katika uchaguzi Mkuu ujao huku wengine wakiwa ni wakongwe wanaoendelea kuyashika majimbo hayo.
Wa kwanza kuthibitisha kuingia kwenye mchakato huo ni Waziri wa Nchi Afisi ya Rais anayeshughulikia Fedha na Uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame ambaye alieleza wazi kuwa anajitayarisha kutetea Jimbo analoliongoza hivi sasa la Dimani.
Waziri Mwinyihaji, ameliambia gazeti hili kwamba atahakikisha anachukua fomu kwa ajili ya kuomba tena ridhaa za wananchi wa Jimbo hilo bila ya wasiwasi.
Alisema anafanya hivyo akiamini kuwa wapo wanachama wengine wa CCM pia wameweka nia kama hiyo lakini bado kwake haijawa kikwazo kwa sababu kila mtu ana haki hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, ambaye ni Mwakilishi wa Kwamtipura, alieleza kuwa nia ya kutaka kuwania nafasi ya Uwakilishi katika Jimbo hilo bado anayo kwa vile umri unamruhusu kufanya hivyo.
Alisema bado ana ushirikiano mkubwa na wananchi wa Jimbo hilo huku kukiwa na mambo ambayo yanamhitaji kuyafanyia kazi hapo baadae.
Alisema kujitokeza kwa idadi yoyote ya wananchi watakaoingia kwenye Jimbo hilo, hakumpi ugumu kwa vile hakuna mwenye hatimiliki ya Jimbo na hilo ni jambo wazi katika kucheza na demokrasia, akiamini kuwa kipindi chake amekitumia vizuri.
Kuhusu mchakato wa upigaji kura za maoni, ambao utafanyika wakati yeye akiwa bado na majukumu mengi serikalini, Waziri Hamza alisema hilo ni linaweza kumpa uzito kwa vile muda uliotangazwa na Chama chake kuanza kwa mchakato huo utaingiliana na shughuli za Bajeti ya Zanzibar.
“Nimo katika kujipanga kwani katika kipindi hichi kutakuwa na mambo mengi ambayo yatanihitaji niyafanye likiwemo la kupiga kura ya maoni ya CCM, kufanya kampeni zangu, kushiriki mikutano ya bajeti, na kura ya maoni ya Tume ya Uchaguzi” alisema Waziri huyo.
Katika hatua nyengine, Waziri wa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Abdalla Juma, akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema yeye bado anatafakari kama ajitokeze kuwania nafasi katika Jimbo alilozaliwa la Dimani au la.
Waziri Asha alisema ameamua kuchukua hatua hiyo kwa kile alichosema wasiwasi wa kuwepo uwezekano wa kupatikana kwa asilimia ndogo ya wagombea wanawake kwa vile bado anaona nguvu ya wanaume katika uchaguzi ujao ipo juu.
Alisema licha ya CCM kutoa ofa ya kuwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi katika majimbo, bado huenda wanawake wasipewe.
Waziri huyo alifahamisha kwa vile tayari kuna wanawake wengi ambao wameanza kuonesha nia ya kutaka kuwania katika majimbo ni vyema Chama kikahakikisha kinatimiza ahadi yake.
Hata hivyo, Waziri huyo aliwataka wanawake kutovunjika moyo na badala yake wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu katika majimbo yao.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Mazingira, Burhani Sadat Haji, alishatangaza mapema nia yake ya kuwania Jimbo la Kikwajuni akisema bado uwezo wa kulitumikia anao.
Kiongozi mwengine ambaye alishawahi kuelezea nia ya kutaka kuwania Jimbo ni Naibu Waziri Kiongozi na waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna kwa kuetetea Jimbo lake la Donge baada ya kuelezea nia hiyo mbele ya wananchi wa Jimbo hilo.
Licha ya baadhi ya viongozi kuelezea nia hizo hadharani, bado wapo ambao hawajajitokeza kutoa kauli hizo kwa maelezo mbali mbali na huenda idadi ya wanachama wenye nia kama hiyo ikaongezeka kadri muda unavyokwenda mbele.
Wanaotajwa ni pamoja na Waziri wa Maji, Ujenzi Nishati na Ardhi, Mansoor Yussuf Himid, anaelishikilia Jimbo la Kiembe Samaki, Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji, Samia Suluhu Hassan kwa tiketi za Wanawake Wilaya ya Kusini.
Wakati kundi hilo la Mawaziri likijitayarisha tayari pia kuna kundi la Makatibu Wakuu na Wakurugenzi ndani ya serikali ya SMZ nao huenda wakajitokeza kuwania baadhi ya majimbo katika uchaguzi Mkuu ujao.
Mkurugenzi wa Idara ya Maafa Zanzibar, Waride Bakari Jabu, amelihakikishia gazeti hili katika mahojiano maalum kuwa nia ya kuwania nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Kiembe Samaki katika uchaguzi Mkuu ujao anayo na wakati wowote atatangaza rasmi.
Waride alisema ameamua kuchukua uamuzi huo ikiwa ni sehemu ya demokrasia yake huku Chama cha Mapinduzi kikiwa kimesisitiza wanawake wajitokeze kuwania nafasi za uongozi katika Majimbo.
Licha ya Mkurugenzi huyo pia wapo Makatibu Wakuu kadhaa ambao watajitokeza katika kuwania nafasi za kuomba kuteuliwa majimboni.
Makatibu Wakuu hao wengi wao wanatajwa wana nia ya kuomba kuteuliwa katika Majimbo ya Vijijini kwa Unguja na Pemba.
Watachukua hatua hio baada kutekeleza sheria ya uchaguzi, ya mwaka 1984 kifungu cha 45(1) (a) kinachoeleza kuwa endapo uchaguzi Mkuu umepangwa kufanyika siku ya uteuzi kwa Jimbo lolote haitakuwa chini ya siku tano au zaidi ya siku ishirini na tano baada ya kuvunjwa Baraza la Wawakilishi.
Kutokana na kifungu hicho cha sheria tayari Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza ratiba ya uteuzi wa kwa nafasi za wagombea wa Urais, Uwakilishi na Udiwani kazi ambayo inatarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 3, 2010 na uchaguzi kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.
Tume hiyo imefahamisha zoezi la uchukuaji wa fomu kwa nafasi ya urais wa Zanzibar litaanza Septemba 10, 2010 na Septemba 15 ni kwa ajili ya wagombea nafasi za Uwakilishi na Udiwani.
No comments:
Post a Comment