Monday, 31 May 2010

Hakuna maendeleo bila mageuzi ya kifedha kimataifa- Dk. Karume



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume ametoa wito wa kuwepo mabadiliko katika taasisi za kifedha za Kimataifa ili kutoa nafasi sawa katika mataifa yote makubwa na madogo ulimwenguni.
Wito huo ametoa wito huo katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi Duniani (WEF) uliomalizika jana mjini Doha, Qatar.

Katika mkutano huo Rais Karume alisisitiza kuwa maendeleo ya uhakika hayawezi kupatikana bila ya kuwepo mageuzi ya kifedha ya kimataifa hasa kwa kuzingatia kuwa taasisi hizo ziliundwa wakati ambao kulikuwa na nchi chache zenye uwezo wa kiuchumi na kiutawala duniani.


Alieleza kuwa wakati huo taasisi hizo ziliundwa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya nchi hizo chache.

“Taasisi hizo ziliundwa ili kukidhi mahitaji hayo lakini sasa wadau ambao ni sisi sote tuko wengi na ni lazima kupatikana usawa wa fursa ili kuweza kushiriki kikamilifu”, alisema Dk. Karume.


Aidha, Rais Karume alizungumzia umuhimu wa elimu katika kuleta maendeleo ya binaadamu na kusisitiza haja ya kuiimarisha sekta hiyo.

“Elimu ndio ufunguo wa maisha katika maendeleo ya binaadamu”, alieleza Rais Karume.

Rais Karume alisisitiza umuhimu wa kuwepo ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya elimu.

Katika mkutano huo, Rais Karume alikuwa ni miongoni mwa wazungumzaji wakuu katika ufunguzi wa mkutano huo.

Wazungumzaji wengine katika mkutano huo uliofunguliwa na Amir wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani, aliyekuwa mrithi wa Mfalme wa Norway Prince Haakon, Mke wa Mfalme wa Jordan Malkia  Rania, Waziri wa Maendeleo wa Singapore na wengineo.


Katika mazungumzo hayo walisisitiza haja ya kuimarisha sekta ya elimu kwani ndio mkombozi katika kuimarisha sekta zote za maendeleo na ukuzaji wa uchumi.


Akifungua mkutano huo mkubwa wa kiuchumi duniani, Amir wa Qatar alisisitiza ushirikiano wa kimataifa na kubuni mikakati itakayosaidia katika kupambana kwa pamoja na matatizo ya kiuchumi duniani.

Nae mke wa Mfalme wa Jordan, Malkia Rania alizungumzia umuhimu wa maendeleo ya vijana hasa katika elimu.


Malkia Rania alieleza kuwa kukosekana kwa elmu kunasababisha ukandamizaji wa vijana na watoto sambamba na kukosa fursa za kujiimarisha kimaendeleo.

Ufunguzi wa mkutano huo uliendeshwa na Profesa Claus Schwab ambaye ndie Mwenyekiti Mtendaji wa WEF.

Mkutano huo ulitanguliwa na mikutao midogo midogo ya majadiliano juu ya mada mbali mbali zikiwemo elimu, afya, maendeleo ya ushirikiano wa kimataifa, uimarishaji wa uchumi na fedha, mazingira, usalama na nyenginezo ambayo iliwashirikisha viongozi mbali mbali kutoka sekta tafauti za serikali na zile za kibinafsi wakiwemo mawaziri,wataalamu na wakuu wa taasisi mbali mbali ambapo Tanzania pia imewakilishwa na baadhi ya Mawaziri waliomo katika nyanja hizo.

No comments:

Post a Comment