Tuesday 1 March 2011

Dk. Bilal akutana na ujumbe kamati ya Bunge la Afrika Mashariki

Dk. Bilal akutana na ujumbe kamati ya Bunge la Afrika Mashariki



Mwandishi Maalum, Dar


MAKAMU wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amesema Bunge la Afrika Mashariki lina wajibu wa kuhakikisha kuwa ndoto ya wananchi wa ukanda huo ya kutaka kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki inatimizwa.

Dk. Bilal ameyasema hayo jana alipokutana na mazungumzo Kamati ya Uongozi ya Bunge la Afrika Mashariki ikiongozwa na Spika wa Bunge hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati Abdirahin Abdi ilipomtembelea Ikulu, Jijini Dar es salaam.

Dk. Bilal aliuambia ujumbe wa kamati hiyo kuwa shirikisho litakapoundwa wananchi watakuwa na uhuru zaidi wa kuwekeza popote pale katika nchi hizo kutokana na ukweli kwamba bado watakuwa wamewekeza ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.

“Kama utawekeza Rwanda, Tanzania, Burundi utakuwa umewekeza kwenye ukanda wa Afrika Mashariki. Hivyo hivyo kwa Kenya na Uganda,” alisema na kuongeza “lazima mjenge matumaini kuwa mtafanikiwa. EU ilichukua miaka mingi lakini mwishowe shirikisho limeundwa.”

Akizungumza kwa niaba ya kamati, Spika Abdi alielezea umuhimu wa kuwa na mfumo unaolingana wa elimu ya juu kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hali ambayo itasaidia kuwawezesha wahitimu kuwa na elimu yenye ubora na viwango vinavyofanana na hivyo kuwa rahisi kwao kupata ajira.

Akizungumzia hoja hiyo Makamu wa Rais alisema iwapo kutakuwa na muundo unaokubalika kikanuni ni jambo jema kwa vile kuwa na mfumo unaolingana utawawezesha wanafunzi wanapohama kutoka nchi moja kwenda nyingine kuendelea na masomo yao kama kawaida chini ya kanuni na taratibu zilizopo.

“Tukiwa na muundo unaokubalika kikanuni, haitaleta shida kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanapohama kutoka nchi moja kwenda nyingine. Kwa mfano mwanafunzi anaweza kusoma mwaka wa kwanza Dar es salaam, mwaka wa pili akaendelea Nairobi na mwaka wa tatu labda Rwanda. Inakubalika na hakuna atakayelaumu kiwango cha elimu,” alidokeza Dk. Bilal

Kamati hiyo ilifika Ikulu kwa lengo la kumwelezea Makamu wa Rais jinsi inavyoendesha shughuli zake katika kuhakikisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinapiga hatua zaidi ya kimaendeleo.

Spika wa Bunge hilo alitumia fursa hiyo pia kuipongeza serikali na wananchi wa Tanzania kwa kufanya uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwa amani na utulivu na pia kutoa pole kufuatia janga la miripuko ya mabomu ya hivi karibuni iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) 511 KJ Gombo la Mboto, Dar es salaam.

1 comment:

  1. Dr.Bilal acha pumba, mimi ni mzanzibari wala sioni tija yoyote ya kiuchumi kwa Zanzibar kuwemo ndani ya shirikisho hilo.

    Hao EU wameunda shirikisho wakati wakiwa hatua nyingi mbele za kimaendeleo.Sio kukurupuka na kuunda shirikisho, wakati matatizo muhimu ya wananchi wa Zanzibar hayapatiwa ufumbuzi.

    Tuna jinamizi la muungano limebakia kiporo, sasa hao tunakwenda kutafuta miungano mengine ya EA.Hayo ndio maoni yangu kwenye mchakato wa shirikisho, Zanzibar iachwe hadi muungano na Tanganyika utapopata ufumbuzi!!

    ReplyDelete