Tuesday, 1 March 2011

Rais Kikwete ziarani Ufaransa

Rais Kikwete ziarani UfaransaNa Mwandishi maalum, Dar

RAIS wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini jana kuelekea Paris, Ufaransa kushiriki mkutano wa Kimataifa wa Tasnia ya Uziduaji yaani Global Extractive Industries Transparency Initiative –EITI.

Katika mkutano huo Rais Kikwete atatoa mada juu ya umuhimu wa shughuli za uziduaji na uwazi katika mapato ya madini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kurugenzi ya mawasiliano Ikulu,mkutano huo wa siku mbili unaonza leo una malengo ya kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mapato yatokanayo na uchimbaji madini, mafuta na gesi asilia.

Tanzania iliomba na kupewa uanachama wa muda wa EITI tangu mwaka 2009.

Hata hivyo, itaweza kupata uanachama kamili baada ya kuwa imekamilisha na kutimiza vigezo vya kuwa mwanachama kamili na kuweka misingi ya utoaji taarifa hizo muhimu kwa umma juu ya malipo ya kodi kutoka makampuni mbalimbali yaliyopo nchini.

Lengo kuu la kujiunga na EITI ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia kwa kutangaza hadharani malipo yanayotokana na rasilimali zake kwa manufaa ya wananchi.

Utaratibu huo utaweka uwazi na kuondoa usiri ambao unaweza kuwa mwanya wa kuficha mapato halisi ya makampuni husika.

Baada ya kumaliza mkutano huo, Rais Kikwete ataelekea Nouakchott, Mauritania kwa ajili ya kikao cha Marais wa Afrika wanaotafuta suluhisho la mgogoro wa kisiasa wa Ivory Coast.

Akiwa Mauritania, Rais Kikwete atajiunga na marais wa Mauritania, Afrika Kusini, Burkina Faso, Chad, Nigeria na Equatorial Guinea pamoja na wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Balozi Jean Ping na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN).

Katika kikao hicho, viongozi hao watafikia uamuzi wa AU kuhusu mzozo huo na kupendekeza namna gani ya kuutatua mzozo huo ulioripuka baada uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba mwaka uliopita.

Matokeo yake, nchi hiyo imegawanyika katika sehemu mbili, moja ikimuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Alassane Quattara na nyingine ikimuunga mkono Rais aliyekomadarakani Laurent Gbagbo.

Kila mmoja kati ya wanasiasa hao amejitangaza kuwa rais na kila mmoja ameunda na kutangaza serikali katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Wiki iliyopita, viongozi hao wa Afrika walikutana mjini Nouakchott na baadaye wakaenda Abidjan, Ivory Coast ambako walikutana na viongozi hao wawili nchini humo katika jaribio la kutafuta suluhisho la mzozo huo.

No comments:

Post a Comment