Tuesday 1 March 2011

Zanzibar yaikuna Uswissi

Zanzibar yaikuna Uswissi


Rajab Mkasaba, Ikulu

USWISSI imesema kufanikiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa kunatokana na juhudi zilizochukuliwa na serikali kwa kuwaelimisha mapema wananchi wake juu ya mfumo huo.

Balozi wa Uswissi nchini Tanzania, Adrian Schlapfer alisema hayo jana alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Balozi Schlapfer alitoa pongezi kwa Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kufanikisha uchaguzi kwa amani na utulivu na hatimae kuundwa kwa Serikali ambayo imepata mafanikio kwa kuanza kazi vizuri.

Alisema hatua iliyofikiwa na Zanzibar kufanikisha Serikali hiyo na kuanza kuleta maendeleo inatokana na elimu ya kutosha iliyotolewa kwa wananchi juu ya serikali yao kabla na baada ya uchaguzi mkuu uliopita.

Balozi huyo alisema Zanzibar imejijengea heshima na sifa kubwa kitaifa na kimataifa kutokana na kufanya uchaguzi uliokuwa huru na haki.

Alisema miongoni mwa mambo yaliyochangia kufanikiwa kwa serikali ni pamoja na kuwepo kwa suala zima la utawala bora.

Katika maelezo yake hayo, Balozi Schlapfer alisema Uswissi inathamini uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo kati ya nchi hiyo na Zanzibar na kuahidi kuimarisha zaidi uhusiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Alisema Uswissi itaendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo Zanzibar na kueleza lengo la serikali yake la kuanzisha mradi maalum wa afya.

Balozi huyo alisema azma ya kuanzisha mradi huo ni kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya.

Akieleza juu ya sifa na haiba ya Zanzibar katika sekta ya utalii, Balozi huyo alieleza kuwa visiwa vya Zanzibar vimejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii pamoja na ukarimu wa wananchi wake kwa wageni.

Alisema kutambulika na kukua kwa sekta ya utalii kumeweza kupanua soko la ajira ambapo baadhi ya wataalamu wa huduma za utalii kutoka nchini mwake wapo Zanzibar wakifafanya kazi katika hoteli za kitalii.

Kwa misingi hiyo alisema nchi yake ina nafasi nzuri ya kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo na kuahidi kuitangaza Zanzibar kiutalii nchini mwake.

Nae Dk. Shein kwa upande wake alimueleza Balozi huyo kuwa ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Uswissi umeweza kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo nchini.

Dk. Shein alimueleza Balozi Schlapfer kuwa Uswissi imekuwa mdau mzuri wa maendeleo ya Zanzibar kwa kuweza kuunga mkono sekta mbali mbali zikiwemo elimu, kwa kutoa nafasi za masomo pamoja na sekta nyenginezo.

Alisema azma ya Uswissi ya kuanzisha mradi maalum wa sekta ya afya utaweza kusaidia juhudi za serikali katika kuimarisha sekta hiyo ambayo ni muhimu katika maendeleo ya wananachi na kufikia malengo ya Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA).

Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itahakikisha inatoa mashirikiano ya karibu zaidi kwa lengo la kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

Akizungumza juu ya mafanikio ya kisiasa yaliopatikana, Dk. Shein alisema amani, utulivu, mshikamano na umoja wa Wazanzibari ndio uliopelekea kufanyika uchaguzi ulio huru na haki.

Alieleza kikubwa kinachohitajiwa na Wazanzibari hivi sasa ni maendeleo, hivyo juhudi za pamoja zitaendelea kuchukuliwa kwa kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo zaidi.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa nchi kwa mashirikiano yake pamoja na misaada inayotoa kwa Zanzibar pamoja na kutoa shukurani zake kwa nchi hiyo kwa kushiriki vyema katika uangalizi wa uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema hatua hiyo imeitia moyo Zanzibar na kuweza kujitambua kuwa ina nafasi katika kujiletea maedneleo endelevu na kuendeleza amani na utulivu uliopo.

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo Zanzibar ni sehemu moja wapo ya uwekezaji hivyo inawakaribisha waekezaji kutoka nchini humo kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii, uvuvi na sekta nyengine muhimu

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuimarisha uhusiano wa kielimu kwa vyuo vikuu vya nchini humo na vile vya Zanzibar kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

No comments:

Post a Comment