Tuesday, 1 March 2011

NGOs nyingi hazijasajiliwa

NGOs nyingi hazijasajiliwa

Na Kauthar Abdalla


UCHUNGUZI unaonesha Jumuiya nyingi za vijana (NGOs) ama hazijasajiliwa au hazina hesabu za benki hali ambayo inazifanya zishindwe kuendesha shughuli zao na kufaidika na miradi inayotolewa na taasisi mbali mbali.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, katika ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani, vijana wengi wamesema Jumuiya zao hazijasajiliwa kutokana na kile walichokieleza kuwepo kwa urasimu katika taasisi zinazohusika na masuala ya usajili wa NGOs.

Amesema hali hiyo inazifanya NGOs kufanya kazi bila ya kuwa na miradi mikubwa kwa kuwa masharti ya kupata fedha pamoja na mambo mengine yanazitaka Jumuiya kuwa na cheti cha usajili na hesabu ya benki.

Aidha tatizo jengine ambalo linazikabili NGOs nyingi ni kutokuwa na ripoti za fedha za mwaka zilizofanyiwa ukaguzi, lakini pia matumizi mengi yamekuwa yakifanywa bila ya kuwepo stakabadhi halali.

Akizungumza na vijana katika mkutano maalum wa kuwafahamisha jinsi ya kuandika michanganuo ya kuomba fedha, Katibu Mkuu Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Rahma Mshangama, amewataka vijana kuandika miradi itakayokidhi vigenzo vinavyotakiwa na wafadhili ili waweze kuingiziwa fedha.

Alisema vijana wafanye upembuzi yakinifu wa kuandika miradi bora ambayo itajikita katika kulikomboa kundi la vijana na ambayo itakuwa na ushawishi wakati itakapopitiwa na wafadhili.

Alisema lengo la mfuko wa vijana ambao umeanzishwa hivi karibuni ni kulikomboa kundi kubwa la vijana, ambalo limekuwa likikabiliwa na umaskini, ukosefu wa ajira, utumiaji wa dawa za kulevya na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Alisema vijana wanapaswa kufahamu kwamba michanganuo itakayokidhi vigenzo ikiwa ni pamoja na akaunti za benki, cheti cha usajili na ripoti ya matumizi ya fedha iliyofanyiwa ukaguzi ndiyo itakayopatiwa msaada wa fedha hizo.

Mkutano huo uliwashirikisha mamia ya vijana kutoka maeneo yote ya Unguja na mwengine kama huo utafanyika kisiwani Pemba.

Februari 20, serikali ya Norway ilitangaza kuupatia mfuko wa vijana Zanzibar msaada wa dola za Marekani 100,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 144 ili kusaidia ukombozi wa kundi hilo.

Fedha hizo zitatolewa kwa zile NGOs za vijana zitakazowasilisha miradi itakayokidhi vigenzo chini ya usimamizi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa, UN-HABITAT.

Kiwango cha chini cha ufadhili kwa Jumuiya hizo ni dola za Marekani 5,000 na kiwango cha juu ni dola 30,000 ambazo zitatolewa mara moja kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment