Friday, 8 April 2011

WALEMAVU NA BONAZA LA MICHEZO

Walemavu kuandaa Bonaza la michezoNa Mwajuma Juma

CHAMA cha Michezo cha Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SADZ), kinatarajia kuandaa Bonanza maalumu la michezo kwa ajili ya kubaini vipaji vipya vya wanamichezo wake.

Bonanza hilo lililopangwa kuwa la wazi, linatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Amaan, kwa kuwajumuisha walemavu wa aina tafauti.

Mwenyekiti wa chama hicho Bakari Haidar Madoweya, ameliambia gazeti hili kuwa bonanza hilo linapangwa kuendeshwa mara baada ya kumalizika kwa sherehe za tamasha la Pasaka.

Hata hivyo, Madoweya alisema bado chama chake hakijapanga tarehe ya kufanyika Bonanza hilo zaidi ya kusema kuwa linasubiri kumalizika kwa tamasha la Pasaka.

Alisema mbali na kutaka kuvitambua vipaji vya wanamichezo, lakini pia Bonanza hilo ni kuwatanabahisha watu wenye ulemavu kujifahamu kuwa nao wana nafasi kama watu wengine, kushiriki katika michezo ndani na nje ya nchi.

Aidha alieleza Bonanza hilo litasaidia kujua uwezo wa wanamichezo hao pamoja na nini kifanyike ili kufikia kiwango cha kuweza kushiriki michezo ya walemavu ya dunia (Paralympic) ambayo wamekuwa wakishiriki kila yanapofanyika.

Sambamba na hilo, alisema katika mwezi huu wa Aprili, wanatarajia kukutana na wanamichezo wenzao kutoka Tanzania Bara, kwa ajili ya kucheza michezo mbalimbali kati ya timu za vyama vyao vya watu wenye ulemavu.Chama cha michezo cha watu wenye ulemavu Zanzibar kina wanachama kati ya 30 na 50, ambao ni walemavu wa jinsia tafauti.

No comments:

Post a Comment