Thursday 4 August 2011

KARAFUU ZAPANDA BEI TENA

Karafuu zapanda bei tena

Na Mwandishi Wetu
IKIWA siku chache kupita tangu serikali kutangaza bei mpya ya karafuu, bei imepandishwa tena ambapo katika bei hiyo mpya kilo moja ya daraja la kwanza itauzwa kwa bei ya shilingi 15,000 huku pishi ikiuzwa kwa shilingi 22,000.
Bei hiyo mpya, kwa kiasi kikubwa itawanufaisha wakulima na kuacha kuzisafisrisha kwa njia ya magengo kuzipeleka nchi jirani.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bishara ya Taifa Zanzibar (ZSTC), Suleiman Juma Jongo amesema bei mpya ya kilo moja ya daraja la kwanza itapanda kutoka shilingi 10,000 hadi 15, huku pishi moja ikiuzwa shilingi 22,000 badala ya shilingi 15,000 za awali.
Alisema kuwa daraja la pili la karafuu kilo moja itauzwa shilingi 14,500 badala ya 9,500, huku pishi moja ya daraja hilo ikipanda kutoka kutoka shilingi 14,250 hadi 21,500.
Aidha Jongo alisema kilo moja ya karafuu daraja la tatu itauzwa shilingi 14,000 kutoka shilingi 9,000 na pishi moja ya daraja hilo itauzwa shilingi 21,000 kutoka shilingi 13,500.
Katika tangazo hilo jipya, bei ya makonyo itauzwa kilo moja shilingi 1,500 huku kila mwenye shamba la karafuu akitakiwa kumlipa shilingi 2,000 mchumaji kwa kila pishi moja.
Mkurugenzi huyo alisema kupandishwa kwa bei hiyo mpya kunafuatia ahadi iliyowekwa na Rais wa Zanzibar kupandisha bei ya zao hilo ili liweze kuleta tija kwa wakulima.
"Katika kutekeleza ahadi ya Rais, serikali inatangaza mabadiliko ya bei ya karafuu itakayotumika hivi sasa badala ya zile zilizotangazwa hapo awali”, ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema kupandishwa huko sio mwisho wa safari kwani, serikali itapandisha bei ya zao hilo kulingana na kupanda bei katika soko la dunia.
Mkurugenzi huyo aliwaomba wananchi watoe ushirikiano kwa kuhakikisha kuwa karafuu zao zote wanaziuza kupitia shirika la ZSTC na kuacha kabisa kuzisafirisha kwa njia ya magendo ambayo yanaangusha uchumi wa Zanzibar.
Kenya inatajwa kuwa imekuwa ikipokea karafuu za Zanzibar kwa njia ya magendo na kuziuza katika soko la dunia pamoja na kwamba nchi hiyo haizalishi karafuu.
Nchi nyengine maarufu zinazozalisha karafuu ukiachilia Zanzibar ni pamoja na Indonesia, India, Madagascar, Brazil, Comoro na Sri Lanka.

1 comment:

  1. A.ALAYKUM NAOMBA MUJITAHIDI KUWEKA HABARI ZOTE MUHIMU NA PICHA ZAKE KWENYE UKURASA WA MWANZO HUSUSAN HABARI ZA MICHEZO AMBAZO ZITAWAVUTIA VIJANA WENGI AMBAO KIU YAO NI MICHEZO YA NJE ILI YATOKE MAGAZEII,PIA KWENYE MAKALA ZENU MUWEKE MAKALA ZA KIDINI ILI KUTOA ELIMU KWA JAMII MFANO ,NDOA,FUNGA,SWALA,ZAKA,HIJJA NANYENGINEZO ILI KUIELEWESHA JAMII YA WAZANZIBARI NA NYENGINE.

    ReplyDelete