Tuesday, 2 August 2011

WAZANZIBAR WATAKA TAASISI YA KUPAMBANA NA RUSHWA.

Wazanzibari wataka taasisi ya kupambana na rushwa

Na Kassim Kassim, TUDARCO
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya muundo wa Umoja wa Kitaifa, imeshauriwa kuwa umefika wakati wa kuwa na taasisi yake itakayodhibiti rushwa na mambo ya kifisadi.
Ushauri huo umetolewa na baadhi ya washiriki wa kongamano la siku moja lililoandaliwa na Jumuia ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), lililofanyika ukumbi wa Beyet el Yamin Malindi mjini hapa.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Mohammed Yussuf alisema Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na tatizo la rushwa na vitendo vya kifisadi kwa baadhi ya watendaji serikalini, hivyo wakati umefika kwa serikali kuvikomesha vitendo hivyo kwa kuwa na taasisi maalum itakayokabiliana navyo.
"Serikali ya Umoja wa kitaifa ni vyema ikaangalia uwezekano wa kuunda ‘Anti Corruption Commission’ maana rushwa kwa baadhi ya watendaji wa serikali imetawala na kila siku wanajijengea majumba na miradi ya gharama ambayo hayaendani na kipato chao", alisema Yussuf.
Aidha mdau huyo wa kongamano alisema serikali na hasa mawaziri kupunguza matumizi ya ununuzi wa gari za kifahari ambazo zina gharama kubwa zaidi ikilinganishwa na gari anayotumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa au waziri Mkuu wa Sweden.
Alisema vigogo wa serikali wakiwemo mawaziri, manaibu na baadhi ya maofisa wakuu wanatumia gari aina ya ‘Prado’ ambazo ni ghali zaidi ikilinganishwa na gari aina ya Volvo inayotumiwa na Ban Ki-moon katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na waziri Mkuu wa Sweden.
Kwa upande mwengine aliipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake za kuleta umoja miongoni mwa wananchi wa Zanzibar hasa baada ya kukubali kuundwa serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi mkuu iliyotokana na zoezi la kura ya maoni lililofanyika mwaka mmoja uliopita.
Na Mwandishi wa Habari mkongwe visiwani hapa, Said Salim Said, akitoa mada alisema ni vyema serikali ikabuni utaratibu wa kuwa na mafunzo ya ndani kwa watendaji wa serikali, ambayo yatakuza uwajibikaji na kuwa wepesi wa kuwahudumia wananchi.
"Serikali ya Zanzibar ni vyema ikawa na ‘in house training’, kwa ajili ya kuinua uwajibikaji wa watendaji wake, maana sasa unaweza kwenda katika ofisi fulani ukapata majibu yasiyoridhisha, hivyo ni vyema serikali ikaandaa mafunzo ya ndani kuinua uwajibikaji wa watendaji hao", alisema mkongwe huyo.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Ali Vuai aliiomba serikali kupitia upya mpango wa maendeleo wa Zanzibar ujulikanao kama MKUZA ili uweze kuendana na azma yake ya kuinua hali za wananchi wa kawaida.
Alisema serikali ni vyema ikapeleka mpango huo kwa wananchi ili waujadili na kuutolea ufafanuzi wa namna ya kuweza kuutekeleza na sio kuambiwa tu utainua vipi hali za wananchi ambao wengi wao ni masikini.
"Serikali ni muhimu ikapitia upya mpango wake wa maendeleo ili uweze kutekelezeka kama ulivyokusudiwa kwa kuwatoa wananchi kwenye umasikini, serikali ipeleke mpango huo kwa wananchi waweze kuujadili na kuutolea mapendekezo yao."
Aidha alipendekeza kwa serikali kuachana na mfumo wa kutegemea mapato kutoka kwenye kodi ya ongezeko la thamani (VAT) bali iangalie uwezekano wa kutoza kodi kwa makampuni (corporate tax) ambayo mengi yao hukwepa kulipa kodi kwa kubadilisha majina kila baada ya muda na kupelekea kwa serikali kukosa mapato yanayoweza kuondoa umasikini kwa wananchi.
Kongamano hilo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

No comments:

Post a Comment