Jamii yatakiwa kuuheshimu mwezi wa Ramadhani
Na Mwantanga Ame
OFISI ya Mufti Zanzibar, imeitaka jamii kuacha vitendo viovu ikiwemo kuvaa mavazi yasiostahili ili kuuheshimu mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Taarifa iliyosambazwa jana kwa vyombo vya habari hapa nchini na Katibu wa Afisi hiyo Sheikh Fadhil Soraga, ilieleza kuwa ni vyema kwa jamii kuupa heshima mwezi huo kwa kuacha vitendo viovu wakati funga hiyo ikiwa inaendelea.
Waumini wa dini ya kiislamu wameanza kufunga mwezi wa Ramadhan jana ikiwa ni utekelezaji wa nguzo ya nne katika dini hiyo ambapo Zanzibar ni asilimia kubwa ya waumini hao.
Sheikh Soraga, alisema suala la kuupa heshima mwezi huo ni jambo la msingi kwa wananchi wote wa Zanzibar kujizuia na vitendo viovu ambavyo vitaweza kubatilisha saumu za wengine ikiwa ni hatua itayosaidia funga hiyo kufanyika kwa utulivu.
Alisema si jambo la busara kwa watu wenye tabia ya kupenda kufanya mambo maovu ama kuvaa mavazi yasiyokuwa na heshima katika mwezi huu.
Hata hivyo, Sheikh Soraga, amewapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano wao kwa Afisi hiyo kwa kuipatia taarifa za kuandama kwa mwezi baada ya kuuona katika maeneo yao.
Alisema wananchi hao waliweza kuuona mwezi huo katika maeneo ya Taveta, Nyerere, Jambiani na Mombasa ingawa katika ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki ulishindwa kuonekana kutokana na kuwepo kwa mawingu mazito baada ya kuzama kwa jua.
Tuesday, 2 August 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment