Maofisa, wakulima kushiriki maonesho Dodoma
Na Shauri Makame
WAKULIMA 53 na maofisa 12 kutoka wizara ya Kilimo na Maliasili, wanatarajiwa kuondoka Zanzibar kuelekea mkoani Dodoma kwenye maonesho ya wakulima (nane nane).
Maonesha hayo ambayo yanayofanyika katika ngazi ya kitaifa mkoani humo kwa mwaka wa nne mfululizo yaliyofunguliwa rasmin juzi na rais wa Jamhuri ya Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, yanatarajiwa kumalizika Agosti 8 mwaka huu.
Msafara huo wa Zanzibar utaongozwa na ofisa Ufatiliaji na Tathmini (AM&E) wa Programu za Kuimarisha Huduma za Kilimo na Sekta ya Kuendeleza Mifugo (ASSP na ASDP-L), program ndogo ya Zanzibar, Mtingwa Ramadhan Mapuri.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kabla ya kuondoka mkuu huyo wa msafara aliwataka wakulima kuithamini ziara hiyo ya mafunzo ambayo inalengo la kubadilishana mawazo na uzowefu miongoni mwa wakulima wa Tanzania.
Alisema uzowefu wa ziara kama hizo zilizopita umeonesha kwamba wakulima na wafugaji wengi wa Zanzibar hupiga hatua kubwa ya uzalishaji kwa kuiga taaluma mbali mbali kutoka kwa wakulima wenzao wa Tanzania Bara.
Maonesho ya wakulima nane nane ambayo hufanyika kila mwaka katika mwezi wa Agosti ambapo wakulima na wafugaji hupata fursa ya kuonesha bidhaa mbali mbali wanazozalisha sambamba na kubadilishana mawazo miongoni mwao.
Ziara hiyo ambayo imefadhiliwa na progamu za ASSP na ASDP-L, progamu ndogo ya Zanzibar, imegharimu jumla ya shilingi milioni 23,220,000.
Programu za ASSP na ASDP-L ambapo lengo lake ni kumpunguzia umasikini mkulima na kumwezesha kuwa na uhakika wa chakula, zimekuwa zikiwapeleka wakulima kwenye maonesho kama hayo tangu mwaka 2008 kwa lengo la kupata mbinu mbadala za uzalishaji wenye tija zaidi.
Thursday, 4 August 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment