Umeme wapeleka neema ya uwekezaji Pemba
Na Ali Haji Mwadini, Pemba
IKIWA ni mwaka mmoja sasa tokea kuzinduliwa kwa umeme wa uhakika kutoka Tanga, tayari jumla ya makampuni kumi (10) ya uwekezaji yameshapeleka maombi yao kwa Mamlaka ya Ukuzaji vitega Uchumi (ZIPA), ili waweze kuruhusiwa kuwekeza katika sekta mbali mbali kisiwani Pemba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Afisini kwake Chake Chake Pemba, Mkurugenzi Mkaazi wa Mamlaka hiyo Pemba, Fadhila Hassan Abdallah, alisema kuwa wawekezaji hao wameonesha nia hiyo kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika kisiwani humo.
Alisema kuwepo kwa umeme wa uhakika kisiwani Pemba, ndiko kulikotoa hamu kwa wawekazaji mbali mbali na kutuma maombi yao, ambapo hapo awali kasi ya wawekezaji ilikuwa ndogo.
“Kwa sasa wawekezaji wanaongezeka, tayari jumla ya wawekezaji 10 kutoka sehemu mbali mbali, wameshatuma maombi yao kwetu na tunayafanyika kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, hii imetokana na kupatikana kwa umeme wa uhakika” alielezea Fadhila.
Aliyataja makampuni hayo kuwa ni Barrick International, GS limited, MS Company, Medical Tourism, Pemba Bottlers Company, Holding Company, Kigomasha Ecology, AQUA farms, Fundu Lagon na Manta reef, ambayo yanatoka nchi za Kenya, Marekani, Sweden, Ujerumani na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Alifafanua kuwa pamoja na kuwepo kwa umeme wa uhakika, chengine kilichowavuti wawekezaji hao ni suala zima la amani na utulivu uliotawala hapa Zanzibar na hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka jana.
Akizungumzia juhudi zinazofanywa na ZIPA katika kuwavutia wawekezaji, Fadhila alibainisha kuwa, wameanzisha kituo kimoja cha ushirikiano (One stop centre) ambacho kinawajumuisha wataalamu kutoka Idara za Uhamiaji, Ardhi kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ambayo yatawavutia wawekezaji kutoka mataifa mbali mbali.
“Wawekezaji hawa wanataka kuwekeza katika kutayarisha maji ya Chupa, Mwani, kujenga Skuli, kusindika matunda na kuimarisha utalii kwa kuweka mazingira mazuri katika mahoteli yao” alisema Mkurugenzi Mkaazi.
Akitolea mfano kijiji ya Kiuyu Mbuyuni Micheweni Pemba, kilichokataa utalii, alisema kuwa mamlaka inakabiliana na changamoto kubwa kutoka kwa wanajamii kwa kukataa kuwekezwa katika vijiji vyao, hivyo mamlaka inajipanga vizuri ili kuendeleza kasi yake ya utowaji taaluma kwa jamii kisiwani Pemba.
Hivyo alitoa wito kwa jamii, kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutoa mashirikiano mazuri kwa wawekezaji wakati wote na kusisitiza kuwa kuwepo kwa wawekezaji kunapelekea wananchi kupata fursa ya kuuza mazao yao mbali mbali na kupata misaada ya kimaendeleo kutoka kwa wawekezaji kama wanavyofaidika watu wa Wambaa, ambapo Fundu lagon wameanzisha shamba darasa kwa lengo la kufundisha wanajamii juu ya kutayarisha mboga mboga.
Tuesday, 2 August 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment