Tuesday, 2 August 2011

MAALIM SEIF KUKOSEKANA UMOJA KUMEREJESHA NYUMA ZANZIBAR.

Maalim Seif: Kukosekana umoja kumeirejesha nyuma Zanzibar
Na Mwanajuma Abdi
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kukosekana kwa umoja kulipelekea kujengeka uadui wa kutoaminiana, na kuheshimia miongoni mwa wananchi na kusababisha hali kuwa mbaya iliyorejesha nyuma maendeleo ya kiuchumi nchini.
Maalim Seif alieleza hayo jana wakati akifungua kongamano la siku ya Umoja wa Kitaifa, iliyotimia mwaka mmoja tokea wazanzibari kuamua mfumo huo, lililoandaliwa na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) lililofanyika ukumbi wa Beyt El Yamin, mjini hapa, ambapo kauli mbiu ni ‘Zanzibar Haitarudi tena Nyuma’.
Alisema kukosekana kwa umoja huo kulisababisha imani kudhoofika, kununiana, kutukanana, kutengana, kuhujumiana na kuuana ilimradi ubinaadamu uliondoka kabisa, jambo ambalo kwa sasa mambo hayo yameondoka.
“Wenye busara wamekuwa wakisema ‘ikiondoka imani, hakuna amani’, hakuna aliyeishi kwa amani, hata kama akilindwa nje ya maridhiano na umoja wa kitaifa”, alisisitiza maalim Seif.
Alieleza wengi wao ni mashahidi kuwa Zanzibar haijawahi kuwa na utulivu na kisiasa takriban nusu karne nzima, uanzishwaji wa mfumo wa kisiasa wa vyama vingi wakati wa ukoloni katika miaka ya 1950, ulisababisha mpasuko mkubwa wa kisiasa, ambapo kuanzia enzi hizo jamii ya kizanzibari iligawika karibu katikati katika mapande mawili na kila pande lilijitambulisha na chama kimoja au muungano wa zaidi chama kimoja.
“Kipindi cha 1957-1964 Zanzibar ilishuhudia msuguano mkali baina ya wafuasi wa Chama cha Afro Shirazi (ASP) kwa upande mmoja na muungano wa vyama vya Zanzibar Nationalist Party – Hizb al Wattan (ZNP) na Zanzibar Pemba Peoples Party (ZPPP), msuguano huo ulipelekea wazanzibari kuukaribisha uhuru wake Disemba 10, 1963 kwa mitazamo tofauti”, alisema.
Alisema masikitiko makubwa walioyashuhudia wananchi baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa ni kurejea kwa ule mpasuko wa jamii ya kizanzibari, ambapo nchi iligawika nusu ya watu wakaunga mkono chama mrithi wa ASP yaani CCM na nusu wakaunga mkono chama kipya cha CUF.
Alieleza mfumo wa utawala uliokuwepo wa mshindi kuchua kila kitu na alieshindwa kupoteza kila kitu ulichochea msuguano uliowepo.
Aidha alifahamisha kuwa, sasa ni miezi tisa tangu kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa, ambapo alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuiongoza serikali hiyo kwa hekima na busara kubwa kiasi kwamba viongozi wanashirikiana katika kazi kwa ajili ya kuwaletea maslahi wananchi wa visiwa hivi.
Aliongeza kusema kwamba, Umoja wa Kitaifa ni hazina ya wazanzibari kwa zama na zama huko nyuma, hazina hiyo ilikuwa imepotea kwa zaidi kidogo ya nusu karne sasa imepatikana kwa watu kuishi kwa kuvumiliana, kuheshimiana, kusaidiana na kutakiana kila la kheri kwa hakika na kufikia ukombozi wa kweli wa nchi na maisha kwa ujumla.
Nae Katibu wa WAHAMAZA, Mwandishi Mwandamizi, Salma Said alisema ni mwaka mmoja uliopita nchi kuripuka kwa furaha baada ya matokeo ya kura ya maoni ya kudhihirisha kuwa karibu thuluthi mbili ya wazanzibari walichagua kupiga NDIO katika kura hiyo na hivyo kufungua ukurasa mpya wa kisiasa.
Aliomba Serikali siku hiyo ifanywe iwe kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Nao watoa mada katika kongamano hilo, walishauri Serikali kuangalia changamoto mbali mbali zinazoikabili Serikali hiyo ikiwemo ufisadi na rushwa iliyotawala nchini, matumizi ya magari ya fahari ya Mawaziri na muundo mkubwa wa Baraza la Mawaziri, ambapo wengine hata Wizara hawana, jambo ambalo kwa nchi kama hii changa linaongeza umasikini.
Makamu wa Kwanza wa Rais, maalim Seif Sharif Hamad alitoa ufafanuzi juu ya maswali hayo kwa kusema si vyema wananchi wakalalamika kwani bado ni mapema kwa Serikali hiyo, ambapo aliahidi kufanyiwa kazi kasoro hizo.
Alisema suala la rushwa, mswada unatarajiwa kufikishwa katika Baraza la wawakilishi katika kikao kijacho, sambamba na kuvipongeza vyombo vya habari hasa vya Serikali kwa kupiga hatua kubwa katika utoaji wao wa taarifa.
Nao wananchi mbali mbali wakichangia katika kongamano hilo, waliomba iendelezwe na watu wasirudi kamwe walikotoka na kinachotakiwa wazanzibari wawe wamoja katika kudai mambo yanayohusu nchi yao.

No comments:

Post a Comment