JK: Umasikini kwa wavuvi kuwa historia
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete na Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu amesema kuwa endapo atachaguliwa tena ataanzisha mpango maalum wa kuwakopesha zana wavuvi katika maziwa ya Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete amewatangazia majambazi wanaofanya uhalifu, kushambulia na hata kuua wavuvi katika maziwa ya Tanzania kuwa sasa kiama chao kimefika.
Rais Kikwete ameyatangaza hayo, alipofanya mikutano ya Kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu katika maeneo ya Busekera, wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara na Ukara, wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza na wananchi katika eneo la Busekera, Kata ya Bukumi, Jimbo la Uchaguzi la Musoma Vijijini Mkoani Mara, jioni ya jana, Rais Kikwete alitangaza ama ya Serikali yake kuwainua wavuvi kutoka kwenye umasikini.
Amesema kuwa katika kuinua hali hiyo ya wavuvi, Serikali yake, kama itachaguliwa tena, itaanzisha mpango maalum wa kuwakopesha zana wavuvi katika maziwa ya Tanzania kama ule wa MACEMP ambao unatumika kuwakopesha wavuvi wanaovua katika Bahari ya Hindi katika maeneo ya Pwani ya Tanzania.
“Endapo tutachaguliwa, tutaanzisha mpango wa kuwakopesha zana wavuvi katika maziwa ya Tanzania kwa kuwapokesha boti, injini, nyavu na zana zote muhimu ili kuinua kipato chao kwa kuvua samaki wengi zaidi,” amesema Rais Kikwete katika eneo hilo lililoko pwani ya Ziwa Victoria.
Akizungumza katika eneo la Bwisya la Kisiwa cha Ukara, kilichopo wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, Rais Kikwete ametangaza kiama kwa majambazi ambao wamekuwa wanawashambulia wavuvi na wasafiri katika Ziwa Victoria kwa kusema kuwa sasa mwisho wao umefika.
“Nataka kuwahakikishieni ndugu zangu kuwa najua kuwa mmekuwa mnasumbuliwa na majambazi katika Ziwa Victoria. Tatizo hilo tumelipatia ufumbuzi na napenda kutangaza kiana cha majambazi, mwisho wao umefika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tutaanzisha kikosi maalum cha kutoa ulinzi katika Ziwa Victoria katika maziwa yetu mengine. Vijana wako kwenye mafunzo na tutanunua boti za kisasa za ulinzi kukiwezesha kikosi hicho kufanya kazi vizuri. Mtalala, mtavua, mtaisha bila wasiwasi kutoka kwa majambazi na ujambazi.”
Rais Kikwete pia amesema kuwa endapo atachaguliwa tena kurudi madarakani, atahakikisha kuwa wananchi wanapata usafiri wa uhakika zaidi kwa kununua kivuko kipya kuchukua nafasi ya MV Nyerere ambacho kimechoka.
Rais Kikwete jana ameendelea na Kampeni katika maeneo ya Ukara na Nansio katika Wilaya ya Ukerewe, Kisesa na Nyanguge katika Wilaya ya Magu, na Lamadi na Bariadi katika Mkoa wa Shinyanga.
Wednesday, 29 September 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment