Thursday, 30 September 2010

DK. SHEIN : MSIDANGANYIKE.

Dk. Shein: Msidanganyike



Chagueni CCM kwa maendeleo


Aahidi maendeleo zaidi Kaskazini Unguja

Na Mwanajuma Abdi

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema chama hicho ndicho chenye uwezo mkubwa wa kuwaletea maendeleo wasidanganyike na vyama vingine vinavyotoa ahadi zisizotekelezeka.

Alisema Serikali ya CCM imesambaza huduma za afya, elimu, maji na imetandika miuondombinu ya barabara na nishati ya umeme kwa wananchi wake, katika kuwafikishia maendeleo ya kweli.

Kauli hiyo ameitoa jana, Bumbwini Makoba Wilaya ya Kaskazini 'B', Unguja, katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu utaofanyika Oktoba 31 mwaka huu, ambapo aliwanadi wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani wa majimbo matatu ya Kitope, Bumbwini na Donge.

Aliwataka wananchi wasidanganyike na ahadi za vyama vyengine, hivyo aliwasihi wasikilize sera za kila vyama ili wajuwe nani anatoa hadi za ukweli na zinazotekelezeka kama za CCM, ambapo aliwaomba kura zao wawapigie wagombea wa Chama hicho kuanzia Urais wa Zanzibar, Tanzania, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

Dk. Shein, ambae ni Makamu wa Rais wa Tanzania, alieleza CCM ni nambari 'one' na ndio chama makini katika kutekeleza ilani na sera zake zinazoahidiwa wakati wa kampeni, ambazo ni muongozo wa katika Serikali kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi bila ya ubaguzi.

Alieleza CCM ni chama pekee chenye historia kubwa ya nchi kutokana kuunganisha vyama vya ASP na TANU, ambapo mwaka 1963 ilani ya Chama cha Afro Shirazi Party ilinadiwa na jambo hilo linaendelea kunadi sera na ilani za Chama Cha Mapinduzi kwa sasa baada ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi.

Aliongeza kusema kwamba, Chama hicho ndicho pekee chenye uwezo wa kulinda na kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar Januari 1964 na pia kina uwezo na jukumu la kudumisha amani na utulivu kwa kuleta umoja na mshikamano nchini.

Aliwahakikishia wananchi wa majimbo ya Kitope, Bumbwini na Donge kwamba maendeleo makubwa yatafanywa huko pindi akipata ridhaa ya kuongoza Zanzibar katika huduma za maji safi na salama kwa kupitia mradi mkubwa wa ACRA unaofadhiliwa na jumuiya mbali mbali katika ambapo shehia 18 watafaidika na huduma hiyo utaotumia zaidi ya shilingi bilioni 1.8.

Alisema mradi huo pia utakwenda sambamba na ujenzi wa vyoo vya kisasa kwa nyumba 533, ambapo katika kijiji cha Bumbwini nyumba 200 zitafaidika pamoja na hupatiwa huduma bora kwa wafugaji, kilimo cha mboga mboga na hivi sasa wananchi 100 wameshapatiwa mafunzo ya kilimo hicho na mpunga wa umwagiliaji maji kwa kulima ekari moja na kuweza kupata mavuno ya magunia 30.

Alifahamisha kuwa, mapinduzi ya kilimo yatafanyika katika kuwakomboa wakulima kwa kuwapatia nyenzo na kuwajengea uwezo katika kuzalisha mazao ya matunda na minazi kutokana na mengi yao kuparama na kusababisha kutozaa tena kutokana na kukatwa kwa makuti na mengine kuzeeka kwa kufikisha miaka 100.

Alieleza pia kutajengwa barabara ya Bumbwini Makoba hadi Kiongwe mpaka pwani, Bumbwini hadi Mwangapwani kutokana hiyo ni miji ya kihistoria lazima watu waje kujifunza na waone maendeleo.

Alizitaja barabara nyengine atazojenga ni Kitope - Kichwele - Pangani itakuwa na urefu wa kilomita nne, barabara ya Donge Mtambile hadi Muwanda kilomita tatu pamoja na daraja ya Zingwezingwe litajenga kwa kisasa, ambapo umeme pia vijiji vyote vilivyokuwa haujawahi kufika katika Jimbo la Kitope kama Mchungwani na Mbaleni.

Dk. Shein alisema ataimarisha huduma ya afya katika majimbo hayo na kuwapeleka madaktari bingwa wa kuchunguza maradhi mbali mbali pamoja na kuwapatia gari la wagonjwa 'Ambulance' kituo cha Afya cha Misufini ili kukuza huduma za mama na mtoto.

Mgombea huyo aliyekuwa na mkewe Mama Mwanamwema Shein, aliahidi kukuza elimu kuanzia msingi hadi vyuo vikuu, ambapo katika kijiji cha Muwanda kutajenga skuli ya sekondari ya kisasa pamoja na nyumba za walimu tatu, ambapo alitoa wito kwa wazazi kuwahimiza vijana kusoma ili waweze kupata nafasi ya kusoma elimu ya juu katika vyuo vikuu vya Zanzibar.

Alifafanua kuwa, wataanzisha Diploma ya sayansi ili walimu kuweza kusomesha pamoja na watu wengine wataohitaji kupata masomo ya uongozi bora, ili nchi ipige hatua za maendeleo kwa haraka kwani bila ya kuwa na vijana wasomi hatuwezi kupiga hatua kwa kasi kubwa.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz alisema mafanikio makubwa yamefanywa wilaya ya Kaskazini 'B', Unguja pamoja na kusambazwa matrekta kwa ajili ya kuimarisha kilimo chini ya Utawala wa Rais wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, hivyo aliwaomba wananchi wakipigie kura ili maendeleo zaidi yapelekwe huko.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini, Haji Juma Haji, aliwakumbusha wananchi kuwa wasiharibu kura zao kwa vyama vyengine visivyoweza kushinda kwa vile kura zao hazitotosha ni bora wakawapigia wagombea wa CCM wanaowania nafasi mbali mbali za Urais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, Rais wa Tanzania, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

No comments:

Post a Comment