Wednesday 29 September 2010

MUZADALIFA YAHIMIZA MATUZO KWA WATOTO YATIMA

Muzdalifa yahimiza matunzo kwa watoto yatima


JUMUIA ya Muzdalifa, kwa kushirikiana na Taasisi ya kiislamu ya Insani Yrdim Vakfi (IHH) ya Uturuki imetoa shilingi 13,000,000 kusaidia watoto yatima katika mradi wa pamoja wa kuwajengea uwezo wa kimaisha watoto katika masuala ya elimu na uchumi.

Akikabidhi fedha hizo, Mwenyekeiti wa Jumuia hiyo Abdalla Khadhar amesema kuwa msaada huo ni muhimu kwa watoto mayatima katika kuendeleza maisha yao ya kila siku na kuwataka wazazi kuitumia vyema misaada inayotolewa kwa watoto wao.

Alisema misaada mbali mbali inayotolewa na wafadhili kwa ajili ya watoto mayatima inapaswa kuwafikia walengwa na wala isiwe miradi kuwaendeleza wazazi nazaidi ifikirie kutatua matatizo yanayowakabili watoto hao.

“Tunajuwa nyinyi walezi na wazazi wa watoto mayatima ndiyo mnaodhibiti fedha hizi kwa ajili ya watoto wenu lakini lazima matumizi yake yalenge kuwaondolea matatizo wanayokabili badala ya kuelekeza matumaini kwa mambo mengine,” alisema Maalim Abdalla.

Aidha aliwataka wazazi kuwa karibu na viongozi wa jumuia hiyo mara kwa mara ili kuwa na mikakati ya pamoja kuhusu mambo muhimu yanayowakuta watoto.

Nae Katibu Mtendaji wa Jumuia hiyo, Farouk Hamad amewahimiza wazazi na walezi wa watoto yatima waache tabia ya kuwatekeleza watoto wao na kuwapatia huduma bora za malazi, chakula na kuwatengenezea maisha mazuri ya baadae.

Alisema jumuia yake itaendelea kutafuta wafadhili zaidi wa nje na ndani ili kuhakikisha weartoto wanapata manufaa zaidi kutokana na misaada inayotolewa hivyo kuongeza kasi ya kutafuta wafadhili zaidi wa ndani na nje ya nchi.

Mapema Mkuu wa kitengo cha watoto yatima katika Jumuia hiyo, Amir Seif alisema kila mtoto aliweza kukabidhiwa shilingi laki moja 35 elfu kwa ajili ya kusaidia huduma mbali mbali.

No comments:

Post a Comment