Wednesday, 29 September 2010

WATOTO VIJIJINI KUUNDIWA "JAMUHURI GARDEN " ZAO.

28/9/2010


Watoto vijijini kuundiwa ‘Jamhuri Garden’ zao



MENEJA wa uendeshaji wa bustani ya Jamhuri Ali Abdallah Ali, amesema wanakusudia kuwapelekea wananchi wa vijiji mbalimbali vya Unguja pembea kwa ajili ya kuwafurahisha watoto walioko huko.

Alisema hatua hiyo inalenga kuwapa fursa watoto wa vijijini ambao hawawezi kufika mjini kwa kufuata pembea zilizoko ‘Jamhuri Garden’, Forodhani au Kariakoo, ili nao wafurahi kama wenzao wa mjini.

Aidha alieleza kuwa kiingilio katika viwanja vitakavyowekwa pembea hizo huko vijijini, kitakuwa kidogo kulinganisha na shilingi 500 zinazotozwa kwa bustani ya Jamhuri.

“Kwa kuwa watoto wote wanahitaji muda na maeneo mazuri ya kupumzika na kucheza, tunaandaa mpango wa kuwasiliana na halmashauri za wilaya mbalimbali kuona namna ya kufanikisha upatikanaji wa viwanja ili tupeleke pembea kwa ajili ya watoto wetu”, alifafanua.

Hata hivyo, hakuweza kusema mpango huo utaanza lini na katika kiijiji gani.

Akizungumzia maendeleo ya bustani ya Jamhuri, Meneja huyo alisema tangu kuwekwa pembea, zaidi ya watu 1000 wengi wao wakiwa watoto, hufika bustanini hapo kila siku ya mwisho wa wiki kwa ajili ya kupanda pembea.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Zanzibar Mahboob Juma Issa, alisema kuimarishwa kwa bustani hiyo kumesaidia kuwapa watoto faraja na kuwa na pahala salama pa kuchezea badala ya kuzurura barabarani na kucheza michezo ya hatari.

Aidha alisema upoteaji wa watoto umepungua sana katika siku za hivi karibuni, kwani wengi wao wakitafutwa huonekana wakicheza katika bustani hiyo jambo alilosema linapunguza wasiwasi wa wazazi na walezi.

No comments:

Post a Comment