Thursday, 30 September 2010

MAWASILIANO HUHARAKISHA MAENDELEO --- MWAKILISHI UNIFEM

Mawasiliano huharakisha maendeleo - Mwakilishi UNIFEM



Na Sheikha Haji

MWAKILISHI wa mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kuwasaidia wanawake UNIFEM, Mohammed Buba amesema, ili wanawake waweze kupata maendeleo ya haraka, mawasiliano ya redio ni muhimu katika maisha yao ya kila siku.

Buba alisema mara nyingi wanawake wamekuwa wakikosa fursa ya kusikiliza taarifa mbalimbali zinazojiri ulimwenguni kote kutokana na mzigo wa kazi unaowakabili.

" Wanawake wakipatiwa nafasi ya kupata habari na kushiriki katika maendeleo wanaweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo", alisema mwakilishi huyo.

Akitoa msaada wa redio 200 zinazotumia nguvu za jua kwa vikundi vya wanawake walio katika mradi wa kuwanyanyua wanawake kiuchumi WEZA, alisema iwapo watazitumia katika shughuli zao zitawasaidia kupata taarifa mbali mbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Mradi wa redio jamii unalengo la kuviwezesha vikundi 60 vya mradi wa WEZA, vikiwemo 30 kwa Unguja na 30 kwa Pemba, kuandaa vipindi mbalimbali vinavyolenga kuwapatia elimu ya uchaguzi, haki na masuala ya kimaendeleo ambavyo vitarushwa hewani na kituo cha redio cha Zenj FM.

Wakitoa maoni yao juu ya mpango huo wanawake hao walisema, redio hizo zitawasaidia katika kuwaelimisha na kwamba kutokana na kujua umuhimu huo wataweza kuzitumia ipasavyo ili kuleta mabadiliko.

Walisema mara nyingi wamekuwa wakikosa fursa ya kusikiliza habari hususan wakati wa asubuhi na mchana kutokana na kuzongwa na mzigo wa kazi za mashambani na hivyo wanaporudi huharakia shughuli za nyumbani.

"Shughuli za nyumbani ni kikwazo kazi ni nyingi hivyo unasahau kabisa kushughulikia taarifa na vipindi muhimu", alisema mmoja wa waratibu wa vikundi hivyo.

Wakati huohuo, Afisa wa WEZA, Asha Abdi aliwataka wanawake hao kuitumia fursa hiyo kwa kubuni mbinu mbalimbali zikiwemo kutengeneza vipindi vitakavyokuwa na nguvu ya kuwaletea maendeleo.

Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa kupitia vipindi hivyo kuelekea uchaguzi ni pamoja na sifa za kiongozi bora, sheria na haki za kupiga kura, sera za vyama na umuhimu wa wanawake kupiga kura.

No comments:

Post a Comment