Wednesday 29 September 2010

REDEA YAIBUA KAULIMBIU NZITO.

RADEA yaibua kaulimbiu nzito




WAKATI Watanzania wakijiandaa kuingia katika uchaguzi mkuu Oktoba 31, mwaka huu, wananchi wa jimbo la Rahaleo wametakiwa kutumia fursa hiyo kuchagua viongozi wenye dira na dhamira ya kweli kuwaletea maendeleo bila kujali vyama wanavyotoka.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Rahaleo jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo jimbo hilo (RADEA) Nabahani Said Washoto, alisema jimbo hilo linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo viongozi waliopita wameshindwa kuzipatia ufumbuzi licha ya kutoa ahadi tamu kila wakati wa uchaguzi unapofika.

Washoto aliyataja baadhi ya matatizo makubwa waliyonayo wananchi wa jimbo hilo, kuwa ni pamoja na kero ya dawa za kulevya, ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na kutokufika mbali kielimu, uhaba wa maji safi na salama na nyengine ambazo alisema zimekuwa zikiwasumbua wananchi bila hatua za kuzimaliza kuchukuliwa.

Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa, uzoefu unaonesha wagombea wengi wanakuwa na kauli tamu za kuvutia wapiga kura, lakini wanapofanikiwa kuvipata viti vya mabaraza ya kutunga sheria, wanajisahau na kutumikia nafsi zao badala ya wananchi waliowapa ridhaa.

Kutokana na hali hiyo, Washoto alisema jumuiya yake inakusudia kufanya kongamano litakalowakutanisha wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani wa vyama vyote jimboni humo na wananchi ili kuwe na mjadala wa wazi utakaowawezesha wapiga kura kuwauliza masuala juu ya watakavyotumia nafasi zao kwa maslahi ya wananchi hao.

Alisema kongamano hilo limepangwa kufanyika wakati wowote kuanzia mwisho wa mwezi huu, likilenga kuwapima wagombea hao ili wananchi wajue ni wepi kati yao wenye uwezo na nia thabiti ya kumaliza matatizo yao na kuliletea maendeleo jimbo la Rahaleo.

Alifahamisha kuwa tayari walishakutana na wagombea wa vyama vyote katika nafasi hizo, na kuwaeleza dhamira ya kufanya kongamano hilo ambapo waliafiki na kupongeza hatua hiyo kwa kusema inafaa kuigwa na majimbo mengine.



“Sisi ni jumuiya isiyo ya kiserikali yenye madhumuni ya kuhamasisha maendeleo, tunataka wananchi wazinduke ili watakapochagua wasifanye makosa kama ya nyuma, kwani Rahaleo imekosa msukumo wa maendeleo, tunakusudia kubadilisha hali hiyo” alifafanua.

Washoto alieleza kuwa huu si wakati tena wa kukubali kulishwa maneno ya ‘halua’ ambayo lengo lake ni kuwanasa wapiga kura kwa maslahi ya wachache.

Alisisitiza kauli mbiu ya jumuiya hiyo isemayo ‘Mtu kwanza chama baadae’, akisema wapiga kura wanapaswa kuondokana na dhana ya kubeba vyama vyao hata kama wagombea wao hawana mwelekeo wa kuwasaidia.

Naye Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Kidawa Abdi Khatib, alizitaja baadhi ya sifa ya kiongozi bora kwa mujibu wa katiba ya RADEA, ambazo ni awe na ushirikiano na wanajimbo bila kujali tafauti zao.

Nyengine nia aweze kupima na kupambanua mambo yanayohusiana na maendeleo ya wanajimbo, pia awe na sifa ya utumishi zaidi na sio utashi wa ukubwa na madaraka, anaejalai utu na sio ubinafsi pamoja na kuwa muwajibikaji.

No comments:

Post a Comment