Nahodha asisitiza umoja miongoni mwa Waislam
Na Abdulla Ali, Dar es Saalam
IMEELEZWA kuwa wakati umefika kwa Nchi za Kiislamu kuwekeza kwenye elimu ya Sayansi kwa lengo la kujiongezea uwezo na kukabiliana na ushindani wa mataifa Makubwa.
Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha alisema hayo alipokuwa akifungua semina ya Hijja na Umoja wa Kimataifa wa Umma wa Kiislamu iliyofanyika katika ukumbi wa Mayfair Plaza jijini Dar es Salaam.
Waziri Kiongozi alisema ukosefu wa elimu ya kutosha na umoja miongoni mwa waislamu ni miongoni mwa sababu zinazosababisha matatizo ya umasikini katika jamii hiyo.
Nahodha alisema kutokana na hali hiyo kuna haja ya kuimarisha umoja miongoni mwa waislamu, umoja ambao utapatikana kwa kueneza elimu na uhamasishaji wa dini.
Alisema Waislamu wakiungana wataweza kupambana na matatizo yao yakiwemo ya kiuchumi na kisiasa ,hivyo watajiongezea nguvu katika dunia.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Hijja na Kiongozi wa ujumbe wa Iran Sayyid Ali Qadhy Askary, alisema lengo lao ni kukutana na waislamu wenzao ili kubadilishana mawazo na kujifunza kutoka kwa waislamu wa kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Alisema ibada ya Hijja ina imarisha umoja wa waislamu wa Mataifa mbali mbali kwa kuwakutanisha sehemu moja na semina yao inazidi kuimarisha lengo hilo kwa kutoa fursa ya kuimarisha zaidi kutokana na mapendekezo yao.
Semina hiyo ya siku mbili imewajumuisha Mashekh,Maulama kutoka Iran,Tanzania, Kenya, Uganda na baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika, ambapo imefunguliwa na Rais Mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi na kufungwa na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha.
No comments:
Post a Comment