Wednesday 29 September 2010

WANAWAKE ZANZIBAR WASIFANYE MAKOSA -- MAMA SHEIN

Wanawake Zanzibar wasifanye makosa - Mama Shein



Mwandishi Maalum – Zanzibar

MKE wa mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi Mama Mwanamwema Shein amewataka wanawake visiwani Zanzibar wasifanye makosa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu kwa kuchagua upinzani.

Mama Shein aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na akina mama wa vikundi mbalimbali vya kilimo cha mwani kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja na Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani.

Alisema wanawake wanapaswa kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo, kwani chama hicho tayari kimepanga mipango madhubuti ya kuendeleza akina mama katika Ilani yake ya Uchaguzi ya 2010-2015.

Alisema miongoni mwa mipango hiyo ni uanzishwaji wa Benki ya Wanawake Zanzibar ambayo itawawezesha wanawake kuweka na kukopa ili kuimarisha shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

“Mikopo hiyo itatusaidia akina mama kuendeleza miradi yetu iwe ya kilimo cha mwani, migomba, kusomesha watoto, kujenga nyumba na miradi mingine mtakayoibuni,” alisema Mama Shein na kusisitiza wasisahau kulipa ili wengine wanufaike.

“Hivyo, mwaka huu tusikosee, tukikosea tutakuja kujuta. Tujipange tutafute kura nyingi kwa CCM ili mambo yetu haya akina mama yaweze kufanikiwa,” alisema Mama Shein.

Mama Mwanamwema alitumia fursa hiyo kuwahimiza akina mama visiwani hupa kutilia mkazo suala la kusomesha watoto wote wakiwemo wa kike na wa kiume kwa kuwa ndio wanaotegemewa kuwa viongozi wa baadae.

Alisititiza suala la akina mama kuimarisha mshikamano, amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwani mara nyingi kupotea kwa amani waathirika wakubwa wanakuwa ni wanawake na watoto.

No comments:

Post a Comment