Thursday, 30 September 2010

KAMPENI ZA KISTAARABU ZAENDELEA KILA KONA ZANZIBAR.

Kampeni za kistaarabu zaendelea kila kona Zanzibar



 Polisi wataka kudumishwa amani, utulivu


Na Mwantanga Ame

HUKU kampeni za kuwania madaraka kwa vyama za siasa zikiwa zimeshika kasi, Makamanda wa jeshi la Polisi wameeleza kuwa zinaendelea vyema bila kuripotiwa uvunjifu wa amani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Muandishi wa habari hizi, Makamanda wa Mikoa Mitano ya Unguja na Pemba, walieleza kuwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu vimekuwa vikiendesha kampeni hizo kwa ustaarabu mkubwa.

Kamanda wa Polis Mkoa wa Kaskazini Unguja Masoud Mselem Mtulia, alisema hali katika Mkoa huo shuari baada ya wagombea wa vyama kwa ngazi ya kitaifa na majimbo kuendesha kampeni zao bila ya kutokea kwa vitendo vya kuhatarisha amani.

Alisema matatizo yalijitokeza baada ya kuanza kwa kampeni katika Mkoa huo ni kuwapo kwa baadhi ya wahuni wasiofahamika kuchana picha za wagombea.

Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma, alisema hadi sasa kampeni za vyama katika wilaya zake zinaendelea vyema na hakuna matatizo yliowahi kuripotiwa ya uvunjifu wa amani.

Huku kukiwepo tuhuma za misafara ya wafuasi wa CCM na CUF kurushiwa mawe katika eneo la Bububu wiki iliyopita, wairudi kwenye mikutano ya kampeni huko Kaskazini Unguja.

Kamanda wa Mkoa wa kaskazini Pemba Yahya Bugi, alisema kampeni za Mkoa huo zimeenda kwa amani pamoja na kujitokeza kwa matatizo madogo madogo yakiwemo ya baadhi ya watu wasiojulikana kuchaniana picha za wagombea.

Alisema asilimia kubwa ya picha ambazo zimekuwa zikichanwa zimekuwa zikihusishwa wagombea wa nafasi ya Urais kwa chama cha CCM na CUF.

Alisema jeshi hilo limekuwa likikabiliwa na tatizo la kukosa ushahidi wa kutosha jambo ambalo linasababisha kutowatambua wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Huko Mkoa wa Kusini Pemba, Kamanda wa Mkoa huo, Hassan Nassir, alisema hakuna matukio maovu yaliyoripotiwa kwenye kampeni za siasa zinazoendelea katika mkoa huo.

Naye Kamanda wa Mkoa wa Kusini Unguja, Agustino Ollomo, alisema hali ya kampeni katika mkoa wake sio mbaya inaendelea vyema na wanachama wa vyama wamekuwa wakitumia viwanja mbali mbali bila ya bughudha kufanya kampeni zao.

Hata hivyo, Makamanda hao wamewataka wananchi kuhakikisha wanaendeleza amani ya nchi wakati wakisubiri kushiriki katika uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.

Wakati huo huo Kamishna Msaidizi wa Opereshini katika Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame, amevitaka vyama vya siasa kuchukua tahadhari ya kujizuia kuanzisha kwa vurugu baada ya kujionesha kuwapo kwa viashiria vya aina hiyo.

Tahadhari hiyo ameitoa huku kukiwa baadhi ya watu wameashaanza kuanzisha mtindo wa kurushiana mawe wanaporudi katika mikutano ya kampeni.

No comments:

Post a Comment