29/9/2010
Zitto Kabwe: Mafuta si suala la Muungano
Ahoji Zanzibar kutofaidika na madini ya Bara
Na Salum Vuai, Maelezo
MGOMBEA ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe, amesema iwapo atarudi tena bungeni, atasimamia kwa nguvu zake zote ili suala la mafuta na gesi liondoshwe katika orodha ya mambo ya Muungano.
Kabwe alikuwa akijibu suala kuhusu Muungano katika mdahalo uliowakutanisha wagombea wa kundi la vijana uliofanyika katika hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam na kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV juzi usiku.
Katika mdahalo huo ulioshirikisha wagombea wa vyama vya CUF na CHADEMA kutoka majimbo ya mikoa mbalimbali chini ya uenyekiti wa Jenerali Ulimwengu, Kabwe alisema kimsingi anakubaliana na hoja kuwa iwapo Zanzibar kuna mafuta, basi hiyo ni mali yake na haijuzu kutiwa mkono na Serikali ya Muungano.
Alifahamisha kuwa, kwa vile Zanzibar haifaidiki na rasilimali za madini zinazopatikana Tanzania Bara, ni haki ya wananchi wa huko kudai mafuta yanayoaminika kuwepo visiwani yasiingizwe katika mambo ya Muungano.
"Suala la mafuta yanayokisiwa kuwepo Zanzibar, limezua mjadala mkubwa bungeni, mimi sioni mantiki ya kuwanyima Wazanzibari haki yao, kwani nao pia hawafaidiki na rasilimali za madini zilizoko Bara, nitajitahidi kuona mafuta yanaondoshwa kwenye mambo ya Muungano", alieleza msimamo wake.
Aidha alieleza kuwa mbali na suala hilo, zipo Wizara nyingi zilizo chini ya mwamvuli wa muungano wa Tanzania lakini haziihusu Zanzibar ingawa ina wabunge.
Hata hivyo, mgombea huyo alisema muungano wa Tanzania ni kitu cha thamani kubwa ambacho nchi nyingi duniani zinatamani kuwa na umoja kama huo lakini zimeshindwa.
Aliwasifia waasisi wa muungano huo hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na marehemu Abeid Amani Karume, akisema wameweka misingi imara ya udugu kati ya watu wa pande mbili hizo, ambayo inahitaji kuimarishwa kwa kutoruhusu mgawanyiko.
Ili kufikia azma hiyo, alishauri kuweko na haki sawa kwa wananchi wa nchi hizo kwa kutozusha mifarakano katika mambo yanayoweza kupatiwa ufumbuzi bila kusuguana.
Alifahamisha kuwa, muungano wa Tanzania uliasisiwa kama njia ya kuelekea umoja wa Afrika nzima ambao waasisi wake na viongozi wa zamani wa nchi mbalimbali wakiwemo Kwame Nkrumah wa Ghana na Gamal Abdelnasser wa Misri walikusudia kuunda.
"Pamoja na kasoro zinazojitokeza, lakini muungano wetu ni urithi mzuri tulioachiwa na waasisi wa taifa letu, hivyo changamoto zilizopo zitufunze namna bora ya kuuimarisha na kuuenzi na kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunawaenzi waanzilishi wake", alifahamisha.
Nao wagombea wa CUF kutoka baadhi ya majimbo ya Morogoro na Dar es Salaam, walisisitiza msimamo wa chama chao kuunda serikali tatu iwapo watashinda katika nafasi ya uraisi wa Tanzania.
Walisema chama chao hakioni sababu ya kuendelea na mfumo wa serikali mbili, na kuelezea jambo hilo linaridhiwa na wananchi wengi wa Tanzania Bara, ambao wanaona njia hiyo tu ndiyo itakayosaidia kuondosha baadhi ya kero za muungano huo.
Mwenyekiti mwenza wa mjadala huo Jenerali Ulimwengu, alisema utaratibu huo utaendelea katika maeneo mbalimbali ili kuwapa wananchi fursa ya kufahamu kwa undani mwelekeo wa wagombea wao kabla kuingia katika uchaguzi mkuu Oktoba 31, mwaka huu.
Aliwapongeza wagombea walioshiriki kikao hicho kwa kusema hiyo ni miongoni mwa dalili za kukua kwa demokrasia nchini.
Wednesday, 29 September 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment