Saturday, 2 October 2010

WANAHABARI KUWENI MAKINI KUFANIKISHAUCHAGUZI -- JAJI MSHIBE

Wanahabari kuweni makini kufanikisha uchaguzi – Jaji Mshibe

Na Ramadhan Makame, 1 Oktoba 2010

HUKU Taifa likikaribia kuingia katika uchaguzi mkuu, waandishi wa habari wametakiwa kuwa makini kuiepusha nchi kuingia kwenye machafuko.

Jaji wa Mahakama Kuu wa Zanzibar, Mshibe Ali Bakari alieleza hayo katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort alipokuwa akifungua kongamano la siku moja lililoelezea dhima ya vyombo hivyo katika uchaguzi.

Jaji Mshibe alisema endapo vyombo vya habari na waandishi wa habari watateleza na kuruhusu kufanya makosa vinaweza kuiweka nchi katika hali mbaya ya mifarakano na ghasia.

Mshibe alisema kalamu za waandishi zikitumika vyema zitaweza kufanikisha kuiepusha nchi kuingia kwenye machafuko ambapo yakitokea yataweza kumuathiri kila mtu.

“Machafuko yanapotokea hayachagui kila mtu ataathirika hata wewe mwenyewe uliyeandika habari hiyo nawe utakwenda na mafuriko”,alisema Jaji Mshibe.

Aidha alisema kinachohitajika kwa waandishi na vyombo vyao katika kipindi hichi kuacha kuripoti mambo yenye maslahi yao binafsi sambamba na kulipendelea kundi fulani.

“Nchi imepita katika kipindi kigumu, jamani andikeni mambo yanayohusu watu sio mambo yenu binafsi ambayo yanaweza kuiweka nchi katika pahali pabaya”.

Akitoa mada katika semina hiyo, Mhadhiri wa Chuo cha Uandishi wa Habari IJMC, Ayoub Rioba alisema vyombo vya habari vina wajibu wa kuandika habari za usawa, kutompendelea mtu sambamba na kuzichambua habari mbali mbali ambazo zitasaidia uelewa kwa wananchi.

Naye Mwandishi wa habari kutoka nchini Afrika Kusini Wellington Radu, akielezea uzoefu wa kuripoti habari za uchaguzi, alisema vyombo vya habari nchini humo wakati wa uchafuzi hutoa taaluma ambayo huwawezesha wananchi kufahamu mambo mbali mbali juu ya uchaguzi.

Wakichangia kwenye semina hiyo waandishi wa habari Zanzibar, walitaja vikwazo kadhaa wanavyokabiliana navyo wakati wa kuripoti masuala ya uchaguzi.

Semina hiyo ya siku moja imeandaliwa na MISA-Tan na kufadhiliwa na shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Washiriki katika mkutano huo walikuwa ni pamoja na waandishi wa habari waandamaizi, wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari, viongozi wa vyama vya siasa na taasisi zisizo za kiserikali.

No comments:

Post a Comment