Na Mwanajuma Abdi
KAMATI ya watu sita ya kusimamia utekelezaji wa azimio la Baraza la Wawakilishi kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeanza kazi ya kuwaelimisha wananchi wa Unguja na Pemba juu ya upigaji wa kura ya maoni itayofanyika Julai 31 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ali Mzee Ali, alisema kamati hiyo inawajumuisha watu sita imeanza kazi rasmi kwa kuwaelimisha wananchi kwa kupitia njia mbali mbali ikiwemo kuvitumia ipasavyo vyombo vya habari.
"Kamati imeundwa kwa mujibu wa kifungu namba 11 cha maazimio ya Baraza kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya hoja ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo inawajumuisha wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na CUF akiwemo Makamo Mwenyekiti Abubakar Khamis Bakary (CUF), wajumbe ni Ali Abdalla Ali (CCM), Haji Omar Kheir (CCM), Nasso Ahmed Mazrui (CUF), Zakiya Omar Juma (CUF) na yeye ni Mwenyekiti", alisema Ali Mzee.
Alieleza licha ya kubakia kwa muda mchache wa wiki mbili, lakini kamati hiyo itafanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa umma kuhusiana na suala la kura ya maoni, ambapo alisisitiza kwamba waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuifikisha sauti ya kamati hiyo kwa wananchi.
Alifahamisha kuwa, wananchi walio wengi wakiunga mkono juu ya uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kikao cha Baraza la Wawakilishi kitaitishwa mwezi ujao kwa ajili ya mabadiliko ya katiba ya Zanzibar.
"Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinatarajiwa kufikia tamati yake Ijumaa, lakini bado wajumbe wake wataendelea kuwa wawakilishi hadi Oktoba 31 siku ya uchaguzi mkuu ndio watapoteza sifa hiyo, hivyo watakuwa na uwezo wa kuitisha kikao cha dharura baada ya kumaliza mkutano wa 20 wa Baraza hilo.
Mwenyekiti huyo, alifahamisha kuwa, katika chaguzi mbali mbali zilizofanyika ya vyama vingi vya siasa Zanzibar kuanzia mwaka 1995, mwaka 2000 na mwaka 2005 zilikuwa zikifanyika kwa mazingira ya chuki na uhasama mkubwa ulijengeka wa kisiasa na Chama cha Wananchi (CUF) kilikataa matokeo, sambamba na kuvunjika kwa muafaka.
Alisema muafaka wa kwanza ulikuwa mwaka 1999 chini ya uongozi wa Dk. Salmin Amour haukutekelezwa hata kidogo, muafaka wa pili ulikuwa 2001 chini Dk. Amani Abeid Karume ulitekelezwa kidogo kwa kufanywa marekebisho a katiba ya Zanzibar mwaka 1984 (marekebisho ya nane 2002 na marekebisho ya tisa 2003).
Hata hivyo alifafanua kuwa, siasa za chuki na hasama ziliejea na kujitokeza tena katika uchaguzi mkuu wa 2005 na muafaka wa tatu ulifuuka Navemba 2009 baada ya mazungumzo ya Navombe 5, mwaka jana baina ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shaif Hamad.
Akimnukuu Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake aliyoitoa Disemba 30, 2005 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alionyesha nia ya dhati ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar unaojitokeza kila mara baada ya uchaguzi mkuu katika kutekeleza azma ake hiyo, kamati ya pamoja ya CCM na CUF iliundwa.
No comments:
Post a Comment