Na Mwanajuma Abdi
MWENYEKITI wa Jumuia ya ZAYEDESA, ambae pia ni Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Shadya Karume amesema kujengwa nyumba ya watoto yatima Mazizini inalenga kuwaekea mazingira mazuri ya makaazi, kutokana na nyumba ya Forodhani kuwa finyu.
Hayo aliyasema jana, wakati akizungumza na Rais wa Jumuiya ya Maendeleo ya Elimu na Upasuaji wa Mishipa ya Kichwa na Mgongo ya Spain, Dk. Jose Piguer, huko Ikulu ya Migombani mjini hapa.
Alisema nyumba ya watoto yatima Forodhani ilianza kutumika baada ya Mapinduzi, 1964, ambapo kutokana kuongezeka kwa watoto na kukua kwa shughuli mbali mbali katika Mji Mkongwe wa Zanzibar kumekuwa na ufinyu wa nafasi katika nyumba hiyo, hali iliosababisha ZAYEDESA kujenga nyumba mpya ya kisasa katika eneo la Mazizini.
Mama Shadya Karume alimshukuru Dk. Jose kwa kuamua kusaidia vifaa mbali mbali kwa ajili ya nyumba ya watoto yatima ya Mazizini, ambayo ipo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha mambo madogo madogo kwa ajili ya kuhamia watoto wanaoishi katika nyumba ya kulelea watoto Forodhan, ambao wapo chini ya hifadhi ya Serikali.
Alifahamisha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuwatunza watoto hao kwa kuwapatia huduma mbali mbali pamoja na elimu, ambapo misaada kama hiyo inasaidia kuongezea nguvu katika kuwapatia makaazi bora watoto yatima wajione kama wanawazazi kamili.
Nae, Dk. Jose Piguer alisema jumuia hiyo licha ya kuwa ya Hispania lakini inafanyakazi zake zaidi Bara la Afrika.
Alisema mbali ya kusaidia huduma za afya lakini hivi sasa imeguswa katika kusaidia watoto yatima wa Zanzibar.
Aidha alimpongeza Mama Shadya Karume kwa kusimamia vizuri Jumuia anayoingoza ya ZAYEDESA, katika kuwasaidia vijana, wanawake katika kuwakomboa na umasikini, sambamba na uhifadhi wa mazingira na kuwajengea nyumba ya kisasa watoto yatima katika kuwapatia makaazi bora.
No comments:
Post a Comment