Saturday, 17 July 2010

Rais Karume awanadi Dk.Shein, Dk. Bilan

Na Bakari Mussa, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya kufanikisha zoezi la upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Alisema mazingira hayo ni pamoja na kutengeneza kadi za kupigia kura za kisasa pamoja na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, ambavyo vina hadhi bora kuliko vya nchi yeyote katika ukanda wa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Dk. Karume aliwataka wananchi wa Zanzibar, kuvitumia vitumbulisho hivyo pale vitakapohitajika ikiwa ni pamoja na Julai 31 mwaka huu, kwenye zoezi la upigaji wa kura ya maoni kuamua juu ya muelekeo mpya wa serikali baada ya uchaguzi mkuu.

Rais Karume aliyasema hayo jana katika Kiwanja cha Gombani Kongwe Chake Chake Pemba, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba, katika hafla ya kumtambulisha mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Ali Mohammed Shein na mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal.

Dk. Karume alifahamisha kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta zote muhimu za kijamii ambapo hilo limewezeshwa kutokana na kuwepo umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari wote.

Aliwataka wananchi kuendeleza kasi hiyo ya mshikamano miongoni mwao iliyooneshwa kwenye awamu ya sita na kwamba maendeleo zaidi yatapatikana kwa kuendelezwa yale yaliyoasisiwa na awamu hiyo.

Dk. Karume aliwataka wananchi wa mikoa miwili ya Pemba na Zanzibar kwa ujumla kuwaunga mkono wagombea CCM, kwani Dk. Shein na Dk. Bilal ni watu mahiri na wenye uwezo wa kuongoza Taifa.



Alisema Uamuzi wa CCM kuwateuwa Wagombea hao ni wa busara, hekima na demokrasia, kwani wote walikuwa wanafaa nafasi walioomba lakini mtu mmoja tu, ndie anaetakiwa, hivyo kila mgombea aliyekuwa na kundi ni vyema na ni lazima kuvunjwa na hatimae kumuunga mkono Dk. Shein kwa lengo la kukipatia Ushindi CCM.

Aidha, Mgombea Urais Zanzibar, kupitia tiketi ya CCM ambae pia ni Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Shein, aliwashukuru wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba,kwa mapokezi yao makubwa waliyoyaonesha kwake na kwa Dk. Bilal kwamba mapokezi hayo yameonesha Ishara ya Upendo kwao na Chama cha Mapinduzi kwa ujumla.

Aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano, miongoni mwao ili kujenga historia yao ya upendo.

Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekitiwa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amefanya mambo mengi makubwa ya maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar, pamoja na changamoto mbali mbali alizokuwa nazo lakini Umoja waliokuwa nao wananchi kwake na Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar inajivunia maendeleo hayo.

“Mafanikio ya maendeleo yalioletwa na Rais Karume, yanaonekana na yanaendelea na yataendelezwa hatua kwa hatua wakati utakapowadia wa kunadi Sera za CCM,” alisema Dk. Shein.

“Rais Amani, amefanya kazi kubwa na isiyo kifani kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar jambo ambalo kila mmoja anafurahia”alieleza mgombea huyo.

Dk. Shein, alimpongeza Rais Karume, kwa kufanya mazungumzo ya maridhiano na Katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, yenye lengo la kuleta umoja na mshikamano ndani ya nchi hii, hivyo alisema mazungumzo hayo yatakuwa endelevu iwapo wananchi watapiga kura ya ndio katika kura ya maoni ifikapo tarehe 31 .7 mwaka huu.

Nae Mgombea mwenza wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alikipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kumlea na kumtunza na kumpa heshima kubwa ya kuwa mgombea mwenza wa Jamhuri ya Muungano jambo ambalo hatalisahau katika maisha yake yote.

Aliendelea kusema kuwa katika mbio za kuwania Urais wa Zanzibar walikuwa wengi na ndio Demokrasia ndani ya CCM, lakini yule alieshinda amechaguliwa na WanaCCM, wenyewe hivyo kama kulikuwa na makundi ndani ya Chama sasa yamekwisha ni kuungana na Dk. Shein, lengo likiwa ni Ushindi ndani ya CCM.

“Bila ya CCM, hakuna maendeleo, hakuna Demokrasia, wala maelewano wala sheria, na yote yaliojitokeza Dodoma ni ya Kisheria na Kidemokrasia” alieleza Dk. Bilal.

Alieleza kuwa uongozi wa Dk. Karume, umefanya mengi mazuri kwa wananchi wa Zanzibar, hivyo Wazanzibari hawana budi kuungana pamoja na kuyaendeleza yale yote ambayo Rais Karume aliyafanya katika uongozi wake huo.

Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kupata kura 99.16% na kuwa Mgombea pekee kwa Chama cha Mapinduzi ili aweze kuendelea kuipeperusha Bendera ya CCM, kwa mara nyengine tena na kuiongoza Tanzania.

Nao WanaCCM na wananchi wa mikoa miwili ya Pemba, katika risala yao wameeleza kuridhishwa na maendeleo makubwa yaliofikiwa Zanzibar chini ya Uongozi wa Rais Karume, na kueleza imani yao kwa Mgombea alieteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar Dk. Shein kuwa na uwezo wa kuyaendeleza maendeleo yaliofikiwa nchini.

Walieleza kuwa hawatasahau maendeleo yaliopatikana katika Uongozi wa awamu ya sita na wataendelea kuyathamini maendeleo hayo ili yawe endelevu kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Maelfu ya wananchi na WanaCCM wa mikoa miwili ya Pemba walihudhuria kwa furaha kubwa katika kuwapokea na kuwaona wagombea wao kuanzia kiwanja cha Ndege cha Karume Pemba, hadi kiwanja cha Gombani ya kale ambapo palifanyika hafla hiyo iliyoambatana na burdani mbali mbali.

No comments:

Post a Comment