Na Ramadhan Makame
MELI inayomilikiwa na Emirates Shipping Lines, Mv Viona jana ilitia nanga katika bandari ya Malindi na kushusha makontena 250 yenye bidhaa zilizoagiziwa na wafanyabiashara wa Zanzibar.
Mkurugenzi wa Operesheni katika shirika la Bandari, Mohammed Salum 'Shilton', alisema meli hiyo imetokea Dubai na ilitarajiwa kushusha makontena hayo yote kwa siku moja.
Shilton alisema hii ni mara ya kwanza meli ya kampuni ya Emirates Shipping Lines, meli yake kufunga gati katika banadari hiyo, huku akiieleza kuwa meli hiyo ina urefu wa mita 178.
Mkurugenzi huyo alisema meli hiyo imesajiliwa Monrovia nchini Liberia na imekuwa na kawaida ya kuchukua makontena kwenye bandari za Mashariki ya Kati na barani Asia.
Aidha alifahamisha kuwa kabla ya meli hiyo kufunga nanga muwakilishi wa Emirates Shipping Lines, alifika kuonana na uongozi wa shirika hilo na kulipongeza kutokana na kuimarisha huduma zake hasa za upakuzi wa makontena.
"Muwakilishi wa kampuni hiyo ameridhika na huduma zetu za kushusha makontena zilivyoimarika na kuahidi kuleta meli zaidi kwenye bandari yetu",alisema Shilton.
Alisema upakuaji wa haraka wa makontena uliopo katika Bandari ya Malindi , unatokana na shirika hilo kuwa na vifaa vya kisasa hali inayochangia kuziondoshea meli adha ya kupiga foleni ya kusubiri kufunga gati.
No comments:
Post a Comment