Tuesday 27 July 2010

Moto wasababisha kizaa zaa Darajani, vifaa vya mamilioni vyaangamia

Na Ramadhan Makame
MOTO uliozuka jana majira ya saa 4:30 asubuhi katika eneo la Darajani mjini hapa umeteketeza maduka matatu yaliyosheni bidhaa mbali mbali.

Moto huo uliosababisha msongamano wa watu kwenye eneo hilo la kibiashra hakuathiri maisha ya mtu yeyote mbali ya kuteketeza mali za wafanyabishara zilizokuwemo ndani ya maduka.

Mmoja wa wafanyabiasha ambaye duka lake limeathirika kwenye tukio hilo Mahir Mohammed, alidai chanzo cha mto huo inawezekana kinatokana na mafundi waliokuwa wakifanya matengenezo ya kuchoma 'walding'.
 
Mahir ambaye ni mfanyabishara wa rangi na vifaa vya ujenzi alisema pembeni ya duka lake kulikuwa kukifanywa matengenezo ya kuchoma kwa 'walding' hali iliyosababisha kuzuka kwa moshi mwingi na baadae moto kusambaa kwenye duka hilo na maduka ya jirani.
 
"Sisi tulikuwa dukani kama kawaida yetu ghafla tunauona moshi mwingi na baadae kufuatia moto, walijaribu kuuzima kwa udongo lakini ulishindikana na kusababisha maafa haya",alisema Mahir.

Naye mfanyabishara mwengine katika eneo hilo, Juma Abdulla Hassan alisema chanzo cha moto huo inawezekana matengenenzo ya "welding" yaliyokuwa yakiendelea kwenye duka la jirani.
 
"Tumekaa mara tukasikia mdato mkubwa moshi mwingi na baadae kufuatiwa na moto, tulichofanya ni kujaribu kuokoa mali zilizomoko madukani",alisema mfanyabishara huyo.
 
Naibu Kamishna wa Kikosi za Zimamoto na Uokozi Gora Haji Gora, alisema kikosi chake kiliarifiwa kuzuka kwa moto huo na kilichukua muda mfupi kuwasilisi kwenye eneo hilo.

Alisema kikosi hicho kilifika kwenye eneo hilo huku moto huo ukiwa umeshika kasi kabla ya kuanza kuudhibiti.
 
"Tulijipanga vizuri baada ya kupokea taarifa na ndio maana vijana wangu wamefanikiwa kuudhibiti",alisema Gora.
 
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Abdulla Mwinyi Khamis ambaye alifika kwenye eneo hilo alisisitiza kazi za ufundi wa umeme wapewe mafundi wafanyakazi wa shirika la Umeme (ZECO) na wafanyabishara waweke vifaa maalum vya kuzimia umeme kwenye maeneo yao ya biashara.
 
"Umeme usiungwe kiholela kazi hiyo wapewe mafundi na wafanyabishara wanamali za mamilioni kwenye maduka kwanini hawanunui vifaa vya kuzimia umeme?".
 
Mkuu wa Operesheni kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Hamdan Omar Makame alisema jeshi lake lililazimika kufanya kazi ya ziada kuzuia wale waliokuwa na tamaa ya kukwapua vitu wakati uokozi ukiwendelea.

"Tumechukua nafasi yetu, kwa mazingira kama haya unapaswa uwadhibiti wale wanaowania ngawira badala ya kutoa msaada",alisema Kamishna Hamdan.
 
Kamanada wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Aziz Juma alisema ni mapema mno kutahmini hasara iliyopatikana pamoja na chanzo cha moto huo.
 
"Ndio kwanza tupo kwenye eneo hili siwezi kuwaambia nini chanzo na harasa ipo imepatikana hadi hapo tutakapopitisha uchunguzi",alisema Kamanda Aziz.
 
Katika harakati za uokoza wa mali kwenye maduka hayo pamoja na ulinzi mkali imeripotiwa vibaka nao kuchukua nafasi yao kwa kupora baadhi ya vitu vikiwemo vitambaa.
 
Maduka yaliyoathirika kwenye tukio hilo yanauza bidhaa za vyakula, vitambaa, vifaa vya ujenzi na mapambo.

No comments:

Post a Comment