Wednesday, 28 July 2010

63 wapigana vikumbo viti maalum wanawake

Na Mwanajuma Abdi
IDADI kubwa wanawake wamejitokeza katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi za wasomi, wafanyakazi, walemavu, ubunge, uwakilishi, kupitia viti vya wanawake katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Katibu wa Mkoa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Asia Juma Khamis aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili jana, katika mkutano mkuu wa UWT Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wa kuwapigia kura wagombea wa CCM wanawake watakaoingia katika vyombo vya kutunga sheria baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu utaofanyika Oktoba 31, ulifanyika Amani mjini hapa.

Alisema wanawake 63 wamejitokeza katika kuwania nafasi hizo ili kuweza kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT kwa kuongeza idadi ya washiriki katika vyombo vya maamuzi na kufikia asilimia 50 iliyoongezwa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Alieleza kwa upande wa viti maalum katika Baraza la Wawakilishi wamejitokeza wagombea 23 kati ya hao watano ndio watakaochaguliwa, Ubunge wamejitokeza 22 ambao nao pia wanatakiwa watano, wasomi watakaoingia katika Baraza la Wawakilishi wamejitokeza watano anahitajika mmoja na msomi mmoja amejitokeza kuingia katika Bunge hivyo hatakuwa ana mpinzani.

Aidha nafasi nyengine zilizojitokeza wagombea ni pamoja na viti vya ulemavu, nafasi za wafanyakazi na muakilishi wa Jumuia za kiraia (NGOs).

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Yussuf Mohammed alisema akinamama katika uchaguzi wa mwaka huu wamehamasika kuchukuwa fomu kwa wingi katika ngazi za udiwani, uwakilishi na ubunge ndani ya viti maalum na majimboni.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kuchagua viongozi wenye sifa ambao watawasaidia kuwatetea wanawake na sio wanaojali maslahi yao.

Mwenyekiti huyo, alitoa wito kwa wagombea watakaoshindwa wasinune wala wasijiweke makundi kwani kufanya hivyo ni athari kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi katika kipindi hiki cha kuelekea chaguzi mkuu.

Nae Makamo Mwenyekiti wa UWT Taifa, Asha Bakar akitoa shukurani kwa Mwenyekiti Yussuf, alimuahidi mkutano huo utafanyika kwa amani na utulivu, sambamba na kuwapata wagombe wake watakaoingia katika vyombo vya maamuzi.

Aidha aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo uchaguzi unapomalizika watu wote warudi wawe wamoja katika kudumisha mashirikiano yao katika kuhakikisha CCM inashinda katika uchaguzi mkuu.

No comments:

Post a Comment