Saturday, 17 July 2010

Viongozi wa dini waelimishe Serikali ya umoja wa kitaifa

Na Ramadhan Makame
ENDAPO wananchi wataridhia kura ya maoni itakayopigwa mwishoni mwa mwezi huu, serikali ya umoja wa kitaifa itakayoundwa itazingatia sera za pamoja zinazojali kuindeleza Zanzibar.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya watu sita ya Baraza la Wawakilishi yenye madhumuni ya kusimamia hoja ya baraza hilo ya kufanyika kwa kura ya maoni, Abubakar Khamis Bakary, aliwaeleza viongozi wa dini kwenye mkutano maalum uliofanyika katika ukumbi wa baraza hilo.

Abubakar ambaye pia ni mkuu wa kambi ya upinzani katika baraza hilo, alisema vyama vya siasa vilivyopo Zanzibar, havitofautiani kwenye sera zao, tofauti yao ni namna ya utekelezaji wa sera hizo kwa maendeleo ya wananchi.

"Sera za CCM na CUF zinafanana na zina lengo moja, nalo ni kuwaletea maendeleo wananchi, kuwapatia amani, ustawi wa maisha yao", alisema Makamo huyo.

Alifahamisha kuwa msingi wa kutekelezwa sera ya pamoja (minimum policy) katika serikali ijayo unatokana na utekelezwaji wa malengo ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.

"Hakuna baya hata moja kwenye malengo ya Mapinduzi, hayo ndiyo yatakayotekelezwa kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoundwa kwa maslahi ya wananchi wetu wote",Makamo huyo aliwaeleza viongozi hao wa dini.

Abubakar, aliwataka viongozi hao kuchukua nafasi yao kwa kuwaelimisha wafuasi wao, juu ya umuhimu wa zoezi hilo na hatima nzuri ya baadae ya Zanzibar na Wazanzibari.

Alisema wajumbe wa baraza hilo, wameridhia kupelekwa suala la kura ya maoni likaamuliwe na wananchi kutokana na uzito wake na umuhimu kushirikishwa wananchi katika maamuzi yanayohusu mustakbali wa taifa lao.

"Sisi wawakilishi tumepitisha azimio kutokana na kuweka maslahi ya taifa mbele, kuondosha mifarakano na migogoro inayojitokeza kila baada ya uhchaguzi".

Aidha alisema serikali itaheshimu matokeo yeyote yatakayotoka kwa wananchi kwenye upigaji wa kura hiyo.

Kwa upande wao viongozi hao wa dini, waliahidi kulifikisha suala hilo kwa waumini wao huku wakitahadharisha juu ya vyombo vya dola kuja kuwatimua kwenye viriri kwa hisia za kuchanganya dini na siasa.

"Ni vyema kwanza mkazungumza na vyombo vya dola, kwa sababu itaonekana haramu kuzungumza dini na siasa na hivyo viongozi wa dini tutaingia kwenye hatia",alisema mmoja wa mashekh aliyehudhuria mkutano huo.

Naye mchungaji wa KKKT, Maloda Shukuru alisema uwepo umakini kwenye uundwaji wa serikali kwani uzoefu unaonyesha kuwa matatizo hujitokeza wakati wa kugawana zile zinazoitwa wizara nyeti.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, sheikh Khalid Mohammed Mrisho aliwataka viongozi wa dini walifikishe jukumu hilo kwa kuwafikishia waumini wao kwani viongozi wa siasa wamelifikisha kwa kuogopa kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

No comments:

Post a Comment