Monday 4 October 2010

JOTO LA UCHAGUZI OCTOBER 31.

JOTO LA UCHAGUZI OKTOBA 31



Maziko yageuzwa mitaji ya siasa Z'bar


 Vigogo watoa mikono zaidi ya mara mbili kwa watarajiwa


 Wengine wajipitisha pitisha waonekanwe na wapiga kura

Na Khamis Haji
3 OCTOBER 2010
KATIKA hali inayoonekana ni kinyume na mila na taratibu za misiba kwa wananchi wa visiwa vyetu, baadhi ya watu wenye malengo ya kisiasa wameonekana wakiitumia mikusanyiko ya misiba kujinufaisha na kufikia malengo yao kisiasa.

Hali hiyo imebainika kushika kasi zaidi wakati huu wa harakati za uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu ambao unaonekana kuwa na ushindani mkubwa miongoni mwa wagombea.

Hivi sasa kampeni za uchaguzi huo zimepamba moto ambapo wagombea pamoja na watu wanaosaka nafasi za uteuzi kutoka kwa viongozi wanaotarajiwa kushika nyadhifa za juu katika serikali ijayo wamekuwa wakitumia kila mbinu kufanikiwa.

Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa kufuatia misiba mbali mbali iliyotokea wakati huu wa harakati za uchaguzi umebaini kwamba wanasiasa wamekuwa makini kufuatilia mikusanyiko hiyo ambayo hujumuisha watu mashuhuri pamoja na wapiga kura wengi.

Uchunguzi huo umegundua baadhi ya wanasiasa hao huwa na harakati kubwa zisizo za kawaida wakati wa mikusanyiko ya misiba hiyo kwa kujipitisha mbele ya viongozi watarajiwa na wapiga kura, kiasi baadhi ya wakati kuonekana kama 'vituko'.

Miongoni mwa misiba hiyo ni ile ya viongozi mashuhuri wa kisiasa, viongozi wa dini, viongozi wa michezo na watu maarufu, waliokwenda mbele ya haki katika siku za hivi karibuni, ambapo wananchi wengi waliweza kuhudhuria kwenye misiba hiyo, wakiwemo viongozi wakuu wa nchi.

Kwa mfano katika misiba hiyo ya wanasiasa na viongozi wa dini pamoja na misiba miwili iliyofanyika katika mtaa wa Mchangani mjini Zanzibar katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, baadhi ya watu waliohudhuria walipigwa na mshangao kutokana na tabia waliyoiona kwa baadhi ya wanasiasa hao.

Wanasiasa hao wengi wao ni wale wanaosaka nafasi za uteuzi na wagombea wanaowania nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, na wamekuwa karibu na kila mtu ambaye wanahisi anaweza kuwa na mchango katika kuwawezsha kufikia malnego hayo.

Kwa upande wengine baadhi ya watu wenye matumaini ya uteuzi kutoka kwa viongozi watarajiwa wamebainika pia kuitumia kikusanyiko hiyo kwa malengo hayo, ambapo wamekuwa mstari wa mbele kusalia viongozi wakuu wa nchi na wagombea hasa wa nafasi ya Urais.

Katika msiba mmoja miongoni mwa iliyotokea katika kipindi hichi cha harakati za uchaguzi, kiongozi mmoja (jina limehifadhiwa) alionekana akiwapiga vikumbo wananchi waliohudhuria katika mkusanyiko, ili kumfikia mgombea mmoja wa Urais kumpa mkono.

Hata hivyo, mara baada ya kiongozi huyo kufanikiwa kumpa mkono mgombea huyo, hakutosheka na kutafuta nafasi nyengine, ili awe kumpa tena mkono, tukio ambalo ilizua udadisi mkubwa miongoni mwa wananchi wengi waliokuwa wakishuhudia hali hiyo ikitokea.

Baadhi ya wazee na watu mashuhuri waliohijiwa na Zanzibar Leo kuhusiana na tabia hiyo walionesha kusikitishwa na hali hiyo na kuielezea kuwa inakwenda kinyume na mila, utamaduni na taratibu za misiba hapa Zanzibar.

Walisema kwamba maziko ni kitu cha kipekee, lakini pia ni sehemu ya ibada, hivyo si vyema kuhusishwa na tamaa za madaraka ya siasa.



"Ni kweli kwenye misiba sasa tunashuhudia wanasiasa wengi, hata wale ambao katika siku zisizokuwa na uchaguzi usingewaona, lakini si katika taratibu zetu kuingiza siasa kwenye masuala ya maziko", alisema mzee Ali Abdallah wa mtaa wa Mlandege.

Baadhi ya wananchi waliozungumzia tabia hiyo walisema kwamba tabia ya kutumia mikusanyiko hiyo kwa tamaa za kisiasa ni kujisumbua bure, kwa vile wapiga kura wanaelewa vigezo vya kuchagua wagombea na sio kujipitisha mbele yao siku za uchaguzi.

Walisema kwamba hata hao viongozi wanaotarajiwa kushika nyadhifa za juu serikalini, pia wanakuwa na vigezo vyao vya uteuzi na sio tu kwasababu mtu anahudhuria sana kwenye misiba na sherehe.

Kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu hivi sasa zinaendelea kwa kasi tokea zilipoanza Septemba 10, baada ya kukamilika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) sehemu kubwa ya maandalizi ya uchaguzi huo tayari yamekamilika na kwamba vifaa kama vile karatasi za kura zinazochapishwa nchini Afrika Kusini zinaratajiwa kuwasili nchini Oktoba 26.

No comments:

Post a Comment