Monday 4 October 2010

NDEGE YATUWA KWA DHARURA KIJIJI CHA MTENDE.

Na ISSA MOHAMMED. 
3 OCTOBER 2010 JUMAPILI

NDEGE ndogo imetua barabarani kwa dharura baada ya kupata hitilafu ya mashine yake eneo la Chau nje kidogo ya kijiji cha Mtende wilaya ya kusini Unguja jana.

Akizungumza na Zanzibar leo huko Mtende Meneja Mawasiliano ya Anga Zanzibar, Said Sumry, amesema ndege hiyo ilikuwa ikitumika kwa mafunzo ya urubani.

Alifahamisha kuwa ndege hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Tropical Air ilikuwa ikiendeshwa na rubani Keyvan Cazdat, raia wa Iran, aliyekuwa akimfundisha urubani, Abrahman Mohammed, raia wa Tanzania.

Hata hivyo, alisema rubani huyo pamoja na mwanafunzi wake wako salama, ingawa ndege imepata athari kidogo kutokana na kuingia kwenye msingi wenye mawe.

Alisema ndege hiyo iliruka katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, Kiembesamaki nje kidogo ya mji wa Zanzibar, saa 3.44 asubuhi, na ilipofika eneo hilo saa 3.55, ilipata hitilafu ikiwa angani, ndipo rubani akaamua kutua barabarani.

Sumry alieleza ndege hiyo yenye namba 5H-TFS aina ya Piper 28-140, kwa kawaida hutumika kuwapa mazoezi marubani wanafunzi katika eneo hilo, kutokana na kutotumiwa na ndege nyingine zinapofanya safari zake za kawaida.

Tukio la ndege kutua barabarani kwa dharura ni la pili katika kipindi cha mwaka huu, ambapo mapema mwaka huu ndege ndogo kama hiyo ilitua katika barabara ya Kiwengwa mkoa wa Kaskazini Unguja.

Pia ndege ndogo ya kampuni hiyo ya Tropical Air iliwahi kuanguka baharini miaka kadhaa iliyopita karibu na kisiwa cha Chumbe, wilaya ya Kusini Unguja, ikiwa na abiria wawili ambao ni mtu na mkewe.

Katika tukio hilo, abiria hao pamoja na rubani walinusurika kifo baada ya rubani kuwavisha abiria wake vifaa maalum vya kuokoa maisha vilivyowawezesha kuelea baharini, kabla ya ndege hiyo kuanguka.

Rubani na abiria hao waliokolewa baada ya kuelea baharini kwa zaidi ya saa 12.

No comments:

Post a Comment