Monday, 4 October 2010

VYOMBO VYA HABARI VIMEVICHA SAUTI ZA WANAWAKE KWENYE KAMPENI.

Vyombo vya habari vimeficha sauti za wanawake kwenye kampeni



Na Ramadhan Makame
3 OCTOBER 2010., JUMAPILI.
UTAFITI uliofanywa na taasisi ya Synovate ya kuvitathmini jinsi vyombo vya habari vinavyoripoti harakati za uchaguzi, umebainisha kuwa vyombo hivyo viko mbali na haviwapi nafasi wagombea wa kike.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa vyombo vya habari vya Zanzibar, Meneja wa taasisi hiyo Aggrey Oriwo alisema vyombo hivyo vimeziweka mbali sauti za wagombea wa kike ilinganishwa na wale wa kiume.

Alisema mara nyingi vyombo hivyo vimekuwa vikiwaripoti kwa kuwatambulisha wanawake kama wake wa wagombea.

"Sauti za wanawake hazipo kwenye kampeni, zinasikika wakitambulishwa kama wake wa wagombea",alisema meneja huyo.

Alisema wagombea wa kile waliosimama kwenye majimbo kuomba nafasi mbali mbali kupitia vyama tofauti hawapewi nafasi ya kujieleza wenyewe ikilinganishwa na wanaume jambo ambalo si haki.

Aidha utafiti huo wa Synovate, ulibainisha kuwa vyombo vya habari za Zanzibar kwa kiasi kikubwa vinakipendelea zaidi chama cha Mapindizi kwa kuripoti habari zake ilinganishwa na vyama vyengine.

Meneja huyo alisema chama hicho tawala kimejizolea asilimia 40 pekee huku vyama vilivyobaki vikigawana asilimia 60 ilioyobakia.

Utafiti huo pia ulibainisha mada zilizopewa umuhimu kwenye kampeni hizo ambapo vyombo vingi vimekuwa vikiandika habari zenye kusisitiza amani katika visiwa hivi.

Mada nyengine zilizoripotiwa kwa wingi ni pamoja na suala la elimu,afya kilimo, ajira na haki za binaadamu huku mada ya ufisadi ikiwa haijapewa umuhimu na vyombo vya Zanzibar ikilinganishwa na bara.

Matokeo ya utafiti huo yalitolewa kwenye semina ya siku moja iliyofanyia Zanzibar Beach Resort, ambapo waandishi waliuponda utafiti huo wakisema haki haikutendeka.

Waandishi hao walihoji njia zilizotumika kupatikana matokeo hayo hasa madai ya kukibeba chama cha Mapinduzi, huku vyama vya upinzani vikishindwa kutumia nafasi ya bure iliyowekwa katika vyombo vya uma.

No comments:

Post a Comment