Monday 4 October 2010

REDIO JAMII TANZANIA KUKUTANA LEO.

Redio jamii Tanzania kukutana Micheweni leo

Na Mwandishi wetu
4 OCTOBER 2010

REDIO jamii kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania, zinakutana Micheweni kisiwani Pemba leo kwa mafunzo ya kuimarisha utendaji wa vituo hivyo nchini.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Said Shaaban, imesema kuwa mafunzo hayo yametayarishwa kwa ushirikiano baina ya Wizara hiyo na Shirika la UNESCO.

Said Shaaban ameeleza kuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo atakuwa Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna.

Katibu huyo ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutekeleza mpango wa kuimarisha vituo vya redio jamii nchini, ambazo zina mchango mkubwa wa kuwaletea maendeleo wananchi wa jamii husika.

Zanzibar hadi sasa ina redio jamii moja iliyo Micheweni, ambayo imewekwa makusudi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wa kijiji hicho, ikiwa ni hatua za utekelezaji Mkakati wa Kukuza uchumi na kuondosha umasikini Zanzibar (MKUZA).

Micheweni ni eneo ambalo lilikuwa katika hali mbaya zaidi kiuchumi Zanzibar, ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa na SMZ kuondosha hali hiyo, ambapo sasa ugumu wa maisha umeanza kupungua kwa kuweko miundombinu muhimu kwa wananchi kufanya kazi na kujikomboa.

Wakati wa ufunguzi wa Redio Jamii ya Micheweni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, aliahidi maeneo mengine ya Zanzibar yatakuwa na redio kama hizo ili kuharakisha maendeleo yao.

No comments:

Post a Comment